Tunaendelea na sura hii kwa kutazama mafundisho mengine yanayopendwa sana, lakini ya makosa, kuhusu Shetani na vita ya kiroho. Hatimaye tutatazama kinachosemwa na Maandiko kuhusu vita ya kiroho inayotakiwa kutendwa na kila mwamini.
Hekaya Ya Tano: “Tunaweza Kuangusha Ngome Za Mapepo Katika Anga Kwa Vita Ya Kiroho.”
Kulingana na Maandiko, hakuna shaka kwamba Shetani anatawala juu ya majeshi ya pepo wabaya ambao wanakaa katika anga la dunia, na wanaomsaidia kutawala ufalme wa giza. Biblia pia inaonyesha kwamba katika hao pepo, wapo wenye kutawala eneo fulani kijiografia (ona Danieli 10:13, 20, 21; Marko 5:9, 10). Maandiko pia yanaonyesha kwamba Wakristo wana mamlaka ya kutoa pepo katika watu wengine, na wana wajibu wa kumpinga Shetani (ona Marko 16:17; Yakobo 4:7; 1Petro 5:8, 9). Lakini je, Wakristo wanaweza kuangusha mapepo walioko juu ya miji? Jibu ni kwamba, hawawezi, na kujaribu kufanya hivyo ni kupoteza muda wao.
Kwa kuwa tunaweza kutoa pepo katika watu si sababu ya kudhani kwamba tunaweza kuangusha pepo wanaotawala juu ya miji yetu. Ipo mifano mingi sana ya watu kutolewa pepo katika Injili na kitabu cha Matendo, lakini, unaweza kukumbuka mfano hata mmoja wa mtu kuangusha pepo aliyekuwa anatawala mji au eneo la kijiografia katika Injili au Matendo ya Mitume? Huwezi kwa sababu mifano hiyo haipo. Je, unakumbuka fundisho au ushauri hata mmoja katika nyaraka, kuhusu wajibu wetu kuangusha mapepo wabaya kutoka angani? Hakuna. Basi, hatuna msingi wa KiBiblia kuamini kwamba tunaweza au tunapaswa kupambana katika “vita ya kiroho” dhidi ya mapepo wabaya katika anga.
Kulazimisha Mifano Izidi Maana Yake
Mara nyingi Wakristo hufanya kosa la kupata maana nyingine zaidi ya iliyokusudiwa na Mungu katika vifungu vya Maandiko vinavyotumia lugha ya mfano. Mfano mzuri ni jinsi wengi wanavyoelewa vibaya maneno ya Paulo kuhusu “kuangusha ngome” yafuatayo.
Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili. (Maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangushya ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia (2 Wakor. 10:3-6).
Kutokana na maneno hayo – “kuangusha ngome” – ambayo ni lugha ya mfano, fundisho zima limejengwa ili kutetea wazo la kufanya “vita ya kiroho” kwa ajili ya “kuangusha ngome” za mapepo katika anga. Lakini ni vizuri tuelewe kwamba Paulo hapo hasemi juu ya mapepo katika anga, bali ngome za imani za uongo ambazo zimo katika mawazo na akili za watu. Paulo anaharibu fikra, si mapepo wabaya katika ulimwengu wa roho!
Hili linakuwa wazi zaidi tunaposoma maandiko hayo kulingana na mantiki yake. Paulo alisema hivi: “tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikra ipate kumtii Kristo” (maneno mepesi yameongezwa ili kukazia). Vita ambayo Paulo anaizungumzia kwa lugha ya mfano ni vita dhidi ya mawazo au fikra ambazo ziko kinyume na maarifa ya kweli ya Mungu.
Kwa kutumia mifano ya kijeshi, Paulo anaeleza kwamba tuko vitani, vita ili kupata mawazo ya watu walioamini kweli za Shetani. Silaha yetu kubwa katika vita hii ni ukweli, na ndiyo sababu tumeagizwa kwenda duniani kote na kuhubiri Injili, tukivamia eneo la adui kwa ujumbe unaoweza kuwaweka mateka huru. Ngome tunazoharibu zimejengwa kwa matofali ya uongo, na kuunganishwa na sementi ya udanganyifu.
Silaha Kamili Za Mungu
Fungu lingine katika maandiko ya Paulo linalotafsiriwa vibaya mara kw amara ni Waefeso 6:10-17, mahali ambapo aliandika juu ya wajibu wetu kuvaa silaha kamili za Mungu. Ingawa fungu hili linahusu mapambano ya Mkristo dhidi ya Shetani na mapepo wabaya, hakuna popote panaposema kuhusu kuangusha mapepo wanaotawala miji. Tunapojifunza fungu hilo vizuri sana, inakuwa wazi kwamba Paulo alikuwa anaandika kuhusu wajibu wa kila aaminiye binafsi kupingana na mipango ya Shetani katika maisha yake mwenyewe, kwa kutumia ukweli wa Neno la Mungu.
Tunaposoma fungu hilo, ona pia kwamba kuna lugha ya mifano. Ni wazi kwamba Paulo hakuwa anazungumza juu ya silaha halisi zinazoshikika ambazo Wakristo wanapaswa kuvaa kwenye miili yao. Badala yake, anazungumza juu ya silaha kwa lugha ya mfano. Kila sehemu moja ya silaha inayotajwa ni mfano wa kweli mbalimbali za kiroho ambazo Wakristo wanapaswa kutumia kwa ajili ya ulinzi dhidi ya Shetani na pepo wabaya. Kwa kujua, kuamini na kutenda Neno la Mungu, Wakristo, kwa lugha ya mfano, wanakuwa wamevaa silaha za Mungu zinazowalinda.
Basi, tutazame fungu hilo katika Waefeso mstari kwa mstari, huku tukijiuliza hivi: Je, Paulo alikuwa anajaribu kutuambia nini hasa?
Asili Ya Nguvu Zetu Kiroho
Kwanza: Tunaambiwa tuwe “hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake” (Waefeso 6:10). Mkazo ni kwamba tusipate nguvu zetu kutoka kwetu wenyewe, bali kutoka kwa Mungu. Hili linatokea zaidi katika tamko la pili, kwamba, “Vaeni silaha zote za Mungu” (Waefeso 6:11a). Hizo ni silaha za Mungu, si zetu. Paulo hasemi kwamba Mungu naye huvaa silaha, bali kwamba tunahitaji silaha ambazo Mungu ameandaa kwa ajili yetu.
Mbona tunahitaji silaha ambazo Mungu ametupa? Jibu ni hili: “Mpate kuzipinga hila za Shetani” (Waefeso 6:11b). Silaha hizi ni kwa ajili ya kujilinda, si za kushambulia. Kusudi lake si kutufanya tutoke na kuangusha mapepo wabaya juu ya miji. Ni ili tuweze kuzipinga hila za Shetani.
Tunajifunza kwamba Shetani ana mipango miovu ya kutushambulia, na kama hatutakuwa tumevaa silaha ambazo Mungu anatoa, tutawezwa. Vile vile, ona kwamba ni wajibu wetu kuvaa silaha hizo, si wa Mungu.
Tuendelee.
Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).
Hapa mambo yanakuwa wazi kabisa kwamba Paulo hasemi juu ya vita ya kimwili, dhidi ya vitu vinavyoweza kuonekana na kushikika, bali ya kiroho. Tunapambana dhidi ya mbinu na mipango ya pepo waovu wa ngazi mbalimbali, kama zinavyotajwa na Paulo. Wasomaji wengi hudhani kwamba Paulo aliorodhesha hao pepo kulingana na udogo wao hadi ukubwa wao, “falme na mamlaka” wakiwa ndiyo cheo cha chini, na “majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” wakiwa ndiyo wa cheo cha juu kabisa.
Swali: Tunawezaje kupambana na viumbe wa kiroho? Tunaweza kulijibu hivi: Viumbe wa kiroho wanawezaje kutushambulia? Rahisi kabisa! Wanatushambulia kwa majaribu, mawazo, mapendekezo na fikra zenye kupingana na na Neno la Mungu na mapenzi ya Mungu. Basi, silaha yetu au ulinzi wetu ni kulijua, kuliamini na kulitii Neno la Mungu.
Kwa sababu hiyo, twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama (Waefeso 6:13).
Hapa tena, ona kwamba kusudi la Paulo ni kutuwezesha sisi kupingana na kusimama dhidi ya mashambulizi ya Shetani. Kusudi lake si kutuwezesha tutoke na kwenda kumshambulia Shetani na kuangusha pepo kutoka angani. Katika fungu hili, Paulo anatuambia tusimame imara mara tatu. Nafasi yetu sisi ni kujitetea, si kupambana.
Silaha Yetu Kubwa – Ukweli
Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni (Waefeso 6:14a).
Kinachoshikilia silaha zetu ni hiki: ukweli. Kweli ni kitu gani? Yesu alimwambia Baba Yake hivi: “Neno lako ni kweli (Yohana 17:17). Hatuwezi kufanikiwa kusimama dhidi ya Shetani mpaka tujue ukweli ambao tunaweza kuutumia kukabiliana na uongo wake. Yesu alionyesha jambo hilo vizuri kabisa wakati alipojaribiwa huko nyikani. Alijibu kila wazo la Shetani hivi: “Imeandikwa.”
Paulo anaendelea hivi:
Na kuvaa dirii ya haki kifuani (Waefeso 6:14b).
Tunapaswa kujua kuhusu aina mbili za haki, kama Wakristo. Kwanza: Tumepewa haki ya Kristo kama zawadi (ona 2Wakor. 5:21). Wale wanaomwamini Yesu wamehesabiwa haki Yake, Yeye aliyechukua dhambi zao msalabani. Msimamo huo wa kuwa na haki umetukomboa kutoka utawala na kifungo cha Shetani.
Pili: Tunapaswa kuishi katika haki, tukitii amri za Yesu. Pengine hicho ndicho Paulo analenga anaposema juu ya dirii ya haki. Kwa kumtii Kristo, hatumpi Shetani nafasi ya aina yoyote (ona Waefeso 4:26, 27).
Msimamo Thabiti Katika Viatu Vya Injili
Na kufungiwa miguu utayari tuupatao kwa Injili ya amani (Waefeso 6:15).
Kujua, kuamini na kutendea kazi kweli ya Injili hutupa sisi msimamo thabiti dhidi ya mashambulizi ya Shetani. Viatu vilivyovaliwa na askari wa Kirumi vilikuwa na vyuma upande wa chini, vilivyowafanya wasimame imara katika uwanja wa mapambano. Yesu anapokuwa Bwana wetu, tunao msimamo thabiti dhidi ya uongo wa Shetani.
Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu (Waefeso 6:16).
Hapa tena, ona mkazo wa Paulo: Ni sisi kujilinda. Hazungumzi juu ya kuangusha mapepo walioko juu ya miji. Anasema kuhusu kutumia imani yetu katika Neno la Mungu ili kupingana na uongo wa Shetani. Tunapoamini na kufanyia kazi kile ambacho Mungu amesema, inakuwa sawa na kuwa na ngao yenye kutulinda na uongo wa Shetani, ambao kimfano unawakilishwa na “mishale yote yenye moto, ya yule mwovu.”
Neno La Mungu – Upanga Wetu Wa Roho
Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu (Waefeso 6:17).
Biblia inasema kuhusu wokovu kwamba ni pamoja na ukombozi wetu kutoka utumwa wa Shetani. Mungu “ametukomboa kutoka ufalme wa giza, na kutuhamisha kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo Lake (Wakolosai 1:13). Kujua hilo ni sawa na kuwa na kofia yenye kulinda akili zetu zisiamini uongo wa Shetani kwamba bado tuko chini ya utawala wake. Shetani si bwana wetu tena – Yesu ndiye Bwana wetu.
Tena, tunapaswa kuchukua “upanga wa Roho” ambao, kulingana na maelezo ya Paulo, ni mfano wa Neno la Mungu. Kama tulivyokwisha ona, Yesu ndiye mfano bora wa askari wa kiroho ambaye alitumia kwa ustadi mkubwa upanga Wake wa kiroho. Wakati wa kujaribiwa Kwake huko nyikani, kila mara alimjibu Shetani kwa kumtajia Neno la Mungu moja kwa moja. Vivyo hivyo na sisi, kama tunataka kumshinda Shetani katika mapambano ya kiroho, tunapaswa kujua na kuamini kile ambacho Mungu kasema, tusije tukadanganyika na uongo wa Shetani.
Ona pia kwamba Yesu alitumia “upanga wa Roho” katika kujilinda. Kuna wanaopenda kuonyesha kwamba, sisi tunaodai kwamba silaha zinazotajwa na Paulo ni za kujilinda, lakini upanga ni silaha ya kushambulia. Basi, wanajaribu kujenga hoja na dhana – japo dhaifu – kwamba, fungu hili katika Waefeso 6:10-12 linafaa kutumiwa kutuonyesha wajibu wetu wa kushambulia na “kuangusha ngome” za pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Ni wazi kwamba kutokana na kusoma sababu ya Paulo mwenyewe kwa nini Wakristo wavae silaha za Mungu (ili wapate “kuzishinda hila za Shetani”), tunajua hapo anazungumzia matumizi ya kujilinda ya silaha hizo. Tena, japo upanga unaweza kudhaniwa kuwa silaha ya kushambulia, unaweza vile vile kutumika kama silaha ya kujilinda, maana unaweza kutumika kuzuia na kulinda shambulizi la upanga wa adui.
Tena, inabidi tuwe makini sana tusiharibu maana ya mfano mzima, katika juhudi zetu za kutafuta maana ya kila sehemu ya hiyo silaha, ambayo hata haipo wakati mwingine. Tukianza kubishana kuhusu kazi ya upanga, kwamba ni ya kujilinda au kushambulia, “tunakwenda mbali” kuliko maana ya mfano wenyewe, katika kukata-kata mfano rahisi tu ambao haukukusudiwa kugawanywa vipande vipande kiasi hicho.
Je, Yesu Hakutuagiza “Kumfunga Mwenye Nguvu”?
Katika Injili, tunasoma mara tatu Yesu akitaja kuhusu “kumfunga mwenye nguvu.” Lakini, hakuwaambia wanafunzi Wake kwamba “kumfunga mwenye nguvu” ni kitu wanachotakiwa kufanya. Hebu tutazame maneno halisi ya Yesu katika mantiki yake.
Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele, kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu (Marko 3:23-30. Maneno mepesi kukazia).
Ona hapo kwamba Yesu hakuwa anawafundisha wafuasi Wake jinsi ya kufunga wenye nguvu. Alikuwa anajibu lawama za waandishi wa Yerusalemu kwa hoja nzito na mfano dhahiri kabisa.
Wao walimshtaki kwa kutoa pepo akitumia nguvu za kipepo. Akawajibu kwa kusema kwamba Shetani angekuwa kichaa kujipinga. Hakuna mtu awezaje kujibu hoja hiyo kwa namna yoyote!
Sasa – Kama Yesu hakutumia nguvu za Shetani kutoa pepo, alikuwa anatumia nguvu za nani? Lazima ilikuwa nguvu kuliko ya Shetani. Ilibidi iwe nguvu ya Mungu, nguvu ya Roho Mtakatifu. Basi, Yesu akazungumza kimfano kuhusu Shetani, akimlinganisha na mtu mwenye nguvu anayelinda vitu vyake. Anayeweza kuchukua mali za huyo mwenye nguvu lazima awe mwenye nguvu kuliko yeye – ambaye ni Yesu Mwenyewe. Hayo ndiyo maelezo ya kweli kuhusu jinsi alivyotoa pepo.
Hili fungu lenye kumtaja mtu mwenye nguvu, pamoja na yale mengine yanayopatikana katika Mathayo na Luka, hayawezi kutumiwa kuruhusu “kufungwa kwa wenye nguvu katika miji”. Tena, tunapotazama Agano Jipya lote, hatupati mifano yoyote ya mtu awaye yote akifanya kazi ya “kuwafunga wenye nguvu” katika miji, wala hatuoni maelekezo yoyote kwa mtu yeyote kufanya hivyo. Basi, kwa usalama kabisa tunasema, kujaribu kufunga na kukosesha nguvu “pepo mwenye nguvu” katika eneo lolote kijiografia au mji, si kitu kinachoruhusiwa kwa Mkristo KiBiblia.
Vipi Kuhusu “Kufunga Duniani Na Mbinguni”?
Tunasoma mara mbili katika Injili, maneno ya Yesu yafuatayo: “Lolote mtakalolifunga duniani litafungwa mbinguni, na lolote mtakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa na mbinguni.” Maneno hayo yameandikwa katika Injili ya Mathayo, mara zote mbili.
Je, Yesu alikuwa anatufundisha kwamba tunaweza, na tunapaswa “kufunga” mapepo yaliyoko angani?
Kwanza – Tutafakari maneno kufunga na kufungua. Yesu anapotumia maneno hayo ni kwa lugha ya mfano, maana hakumaanisha kwamba wafuasi Wake wachukue kamba au nyuzi na kufunga chochote au kufungua chochote kilichofungwa na kamba au nyuzi za kimwili. Basi, alimaanisha nini?
Ili tupate jibu, tunapaswa kutazama matumizi Yake ya maneno kufunga na kufungua katika mantiki husika wakati aliposema maneno yenyewe. Je, alikuwa anazungumzia swala la pepo wachafu? Kama ndivyo, tunaweza kusema maneno Yake kuhusu kufunga yanahusiana na kuwafunga pepo wachafu.
Basi, tutazame fungu la kwanza, ambapo Yesu alitaja kuhusu kufunga na kufungua.
[Yesu] Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-Yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakwambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni (Mathayo 16:15-19. Maneno mepesi kukazia).
Sababu ya fungu hili kufasiriwa kwa njia nyingi sana ni kutokana na kuwa na aina tano za mifano, kama ifuatavyo: (1) “damu na nyama”, (2) “mwamba”, (3) “milango ya kuzimu”, (4) “funguo za ufalme wa mbinguni,” na (5) “kufunga na kufungua.” Yote hayo ni maneno ya mfano, yanayozungumza kuhusu kitu kingine.
Milango Ya Kuzimu
Pamoja na maana hasa ya mifano hiyo, unaweza kuona kwamba katika fungu hili, Yesu hakutaja pepo waovu. Kitu alichosema ni “milango ya kuzimu,” ambayo ni lugha ya mfano tu, maana hakuna chochote kinachoweza kufanywa na milango halisi ya kuzimu ili kulizuia kanisa.
Je, “milango ya kuzimu” maana yake nini? Pengine inawakilisha nguvu za Shetani, na Yesu alimaanisha kwamba nguvu za Shetani zisingezuia kanisa Lake kujengwa. Au pengine alimaanisha kwamba kanisa ambalo angejenga, lingewaokoa watu kutokana na maisha ya kufungiwa na milango ya kuzimu.
Ona kwamba Yesu alitaja milango ya aina mbili – milango ya kuzimu na milango ya mbinguni – anapomwambia Petro kwamba atampa “funguo za mbinguni.” Mlinganisho huo unaunga mkono hoja kwamba maneno ya Yesu juu ya milango ya kuzimu ni mfano wa kazi ya kanisa kuwaokoa watu wasiende kuzimu.
Hata kama Yesu alimaanisha kwamba “nguvu zote za Shetani zisingezuia kanisa Lake,” hatuwezi kuamua kwamba maneno aliyosema juu ya kufunga na kufungua ni maagizo Yake kuhusu tunachopaswa kufanya na pepo wabaya walio juu ya miji. Hii ni kwa sababu hatupati mifano yoyote katika Injili au Matendo, ya mtu yeyote akifunga pepo waovu juu ya miji, wala hatupati maagizo ya aina hiyo katika nyaraka. Vyovyote tutakavyotafsiri maneno ya Kristo juu ya kufunga na kufungua, tafsiri yetu lazima ikubaliane na sehemu zingine za Agano Jipya.
Kwa kuwa hakuna mfano wowote kimaandiko kuhusu jambo hilo, inashangaza jinsi ambavyo mara nyingi Wakristo wanasema, “Ninamfunga Shetani katika jina la Yesu,” au “Ninafungua malaika wawe juu ya mtu huyo” na kadhalika. Humkuti mtu yeyote akisema hivyo mahali popote katika Agano Jipya. Mkazo katika Matendo na nyaraka si kuzungumza na Shetani au kufunga na kufungua pepo waovu, bali mkazo ni kuhubiri Injili na kumwomba Mungu. Kwa mfano: Wakati Paulo alipokuwa anateswa mara zote na mjumbe (au malaika) wa Shetani, hakujaribu “kumfunga”. Alimwomba Mungu kuhusu jambo hilo (ona 2Wakor. 12:7-10).
Funguo Za Mbinguni
Hebu tutazame zaidi mantiki husika ya maneno ya Yesu juu ya kufunga na kufungua. Ona kwamba, kabla ya kutaja kufunga na kufungua, Yesu alisema angempa Petro “funguo za ufalme wa mbinguni.” Petro hakupewa funguo yoyote halisi ya lango la mbinguni, hivyo, maneno ya Yesu lazima yawe ya mfano. Je, “funguo” zinawakilisha nini? Funguo zinawakilisha njia ya kufikia kitu ambacho kimefungwa. Mtu mwenye funguo ana jinsi au njia ya kufungua milango fulani, ambayo wasiokuwa na funguo hawana.
Sasa – tunapotazama huduma ya Petro kama inavyoelezwa katika kitabu cha Matendo, ni kitu gani tunachomwona akifanya, kinachoweza kuhesabika kuwa ni kufungua milango ambayo imefungwa kwa wengine?
Kimsingi, tunamwona akitangza Injili – ile yenye kufungua milango ya mbinguni kwa wote watakaoamini (ambayo pia hufunga milango ya kuzimu). Kwa hali hiyo, sisi sote tumepewa funguo za ufalme wa mbinguni, maana sote ni mabalizi wa Kristo. Basi, funguo za ufalme wa mbinguni ni Injili tu ya Yesu Kristo, ambayo ni ujumbe unaoweza kufungua malango ya kuingia mbinguni.
Kufunga Na Kufungua
Mwisho – baada ya kuahidi kumpa Petro funguo za ufalme wa mbinguni, Yesu alitoa tamko Lake kuhusu kufunga na kufungua – la tano katika fungu tunalotazama sasa.
Kulingana na mantiki ya matamko tuliyokwisha tazama, Yesu alimaanisha nini? Kufunga na kufungua kwa Petro kunahusikaje na Yesu kulijenga Kanisa Lake – kuwaokoa watu kutoka Kuzimu, na kutangaza Injili?
Uwezekano ni mmoja tu kwa kweli. Maana ya Yesu ilikuwa hii: “Ninakuruhusu wewe kuwa mwakilishi wa mbinguni. Timiza wajibu wako duniani, na mbingu itakuunga mkono.”
Kama mwajiri atamwambia mfanya kazi wake muuzaji hivi: “Chochote utakachofanya Arusha kitakuwa kimefanyika ofisi kuu”, anapaswa kuelewaje maneno ya mkuu wake? Bila shaka angechukulia kwamba ameruhusiwa kuwakilisha kampuni yake huko Arusha. Maana ya Yesu ni kwamba, Petro alikuwa ameruhusiwa kumwakilisha Mungu wa mbinguni hapa duniani. Ahadi hiyo kwa Petro ingetia nguvu imani yake, wakati wa kuanza kutangaza ujumbe wa Mungu huko Yerusalemu, mbele ya macho makali ya waandishi na Mafarisayo – watu ambao walidhani wao ndiyo wawakilishi walioruhusiwa na Mungu, na watu ambao zamani Petro aliwaheshimu hivyo.
Hii tafsiri ya maneno ya Yesu inakubaliana vizuri na sehemu ya pili ya tamko Lake, inayopatikana sura mbili baada ya hii, katika Injili ya Mathayo.
Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusiia, umempata nduguyo. La kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru. Amin nawaambieni, yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia ya kwamba, wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaoliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao (Mathayo 18:15-20. Maneno mepesi kukazia).
Katika fungu hili la pili lenye kutaja kufunga na kufungua, hakuna chochote katika mantiki chenye kutusababisha tuamini kwamba Yesu alikuwa anazungumzia kufunga pepo wabaya. Hapa, Kristo alitaja juu ya kufunga na kufungua moja kwa moja baada ya kusema swala la nidhamu kanisani.
Hii inaonyesha kwamba, kwa habari ya kufunga na kufungua katika fungu hii, Yesu alimaanisha hivi: “Ninakuwa wewe wajibu wa kuamua nani awe kanisani, na nani asiwe. Ni kazi yako. Utakapotimiza wajibu wako, mbingu itakuunga mkono.”
Kwa maana pana zaidi ni kwamba, Yesu alikuwa anasema hivi: “Mmeruhusiwa kuwa wawakilishi wa mbinguni duniani. Mna wajibu, na mtakapokuwa mnazitimiza duniani, mbinguni mtaungwa mkono kila mara.”
Mantiki Ya Kufunga Na Kufungua
Tafsiri hii inakubaliana na mantiki iliyopita na mantiki kubwa ya Agano Jipya kwa ujumla.
Kwa habari ya mantiki iliyoko, tunaona kwamba mara tu baada ya tamko Lake kuhusu kufunga na kufungua, Yesu alisema hivi: “Tena nawaambia ya kwamba, wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 18:19. Maneno mepesi kukazia).
Hapo tena ile mada ya “mtakachofanya duniani kitaungwa mkono mbinguni” inaonekana. Sisi hapa duniani tumeruhusiwa na tuna wajibu wa kuomba. Tunapofanya hivyo, mbingu itajibu. Maneno ya Yesu, “Tena nawaambia …” yanaonyesha kwamba ni kama anatoa ufafanuzi zaidi kuhusu tamko Lake la kwanza juu ya kufunga na kufungua.
Tamko la mwisho la Yesu katika fungu hili – “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” – linaunga mkono pia ile mada ya “mbinguni mtaungwa mkono”. Waamini wanapokusanyika katika jina Lake, Yeye akaaye mbinguni hutokea.
Hata kama hukubaliani kabisa na tafsiri yangu ya fungu tunalotazama, utapata kazi kubwa kutoa hoja inayoungwa mkono na Maandiko kwamba Yesu alikuwa anazungumzia juu ya kuwafunga pepo wachafu wanaotawala na kuwa juu ya miji!
Mpango Wa Mungu Unamhusisha Shetani
Shetani na malaika zake ni jeshi lililoasi, lakini haimaanishi haliko chini ya mamlaka ya Mungu. Liliumbwa na Mungu, (japo hawakuwa waasi walipoumbwa mara ya kwanza). Paulo aliandika hivi:
Kwa kuwa katika Yeye [Kristo] vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na viliyvo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana – ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka – vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake (Wakolosai 1:16. Maneno mepesi kukazia).
Yesu aliumba kila roho ya kimalaika ya kila ngazi, na Shetani pia. Je, alijua kwamba wengine wangeasi? Bila shaka. Basi, mbona akawaumba? Kwa sababu, angetumia hizo roho zilizoasi kusaidia kutimiza mpango Wake. Kama hakuwa na mpango wowote kwa ajili yao, angewafunga tu, kama tunavyoambiwa kwamba tayari amefanya hivyo na wengine (ona 2Petro 2:4), na kama atakavyofanya hivyo na Shetani siku moja (ona Ufunuo 20:2).
Mungu ana sababu za kumwacha Shetani na pepo wote wabaya kufanya kazi duniani. Angekuwa hana, wasingefanya kitu. Je, sababu za Mungu kumruhusu Shetani kufanya kazi duniani ni zipi? Sidhani kama kuna yeyote anaye-elewa sababu zote, lakini Mungu amefunua baadhi yake katika Neno Lake.
Kwanza – Mungu anamruhusu Shetani kufanya kazi kwa mipaka duniani ili kutimiza mpango Wake wa kuwapima binadamu. Shetani anakuwa chaguo lingine kwa wanadamu. Watambue wasitambue, binadamu ni watumishi, aidha wa Mungu au wa Shetani. Sasa, Mungu alimruhusu Shetani kumjaribu Adamu na Hawa – watu wawili waliokuwa na hiari ya kuamua ambayo walipewa na Mungu – ili kuwajaribu. Wote wenye hiari lazima wajaribiwe ili kudhihirisha kilicho mioyoni mwao – ama utii, au kutokutii.
Pili – Mungu humruhusu Shetani kufanya kazi kwa mipaka hapa duniani, kama wakala wa ghadhabu Yake juu ya watenda maovu. Tumekwisha thibitisha jambo hili mapema kwa kuonyesha matukio halisi katika Maandiko ambapo Mungu alileta hukumu juu ya wanaostahili kupitia pepo wabaya. Ukweli kwamba Mungu amemruhusu Shetani kutawala watu wasio-okoka wa dunia hii ni alama ya gadhabu Yake juu yao. Mungu huhukumu makundi ya watu waovu kwa kuwaruhusu binadamu waovu kuwatawala, na pia kwa kuruhusu viumbe waovu wa kiroho kuwatawala. Hilo linafanya maisha yao kuwa mabaya zaidi.
Tatu – Mungu anamruhusu Shetani kufanya kazi kwa mipaka hapa duniani ili kujitukuza Mwenyewe. “Kwa sababu, Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili aziharibu kazi za Ibilisi” (1Yohana 3:8). Kila mara Mungu anapoharibu kazi moja ya Shetani, tukio hilo hutukuza uwezo na hekima Yake.
Yesu Ni Mkuu Juu Ya Falme Na Mamlaka
Sisi kama Wakristo, wajibu wetu KiMaandiko ni kushungulika na Shetani na pepo wabaya kwa namna mbili: kuwapinga katika maisha yetu wenyewe (Yakobo 4:7), na kuwatoa katika wengine wanaotaka kufunguliwa na kuwekwa huru (Marko 16:17). Mkristo yeyote mwenye uzoefu wa kutoa pepo anajua kwamba, kwa kawaida, kama yule mwenye pepo hataki kuwekwa huru, haiwezekani kumtoa huyo pepo.[1] Mungu anaheshimu hiari ya kila mtu, na kama mtu anataka kujitolea kwa mapepo, Mungu hatamzuia!
Hii nayo ni sababu nyingine tena ya sisi kutoweza kuangusha pepo wanaotawala eneo la kijiografia. Hao pepo wanaowashikilia mateka watu wa hapo wanafanya hivyo kwa kibali chao. Tunapotangaza Injili kwao, tunawapa nafasi ya kuchagua. Wakichagua vizuri, watawekwa huru kutokana na Shetani na mapepo. Lakini wakichagua vibaya – yaani, wakiamua kutotubu – Mungu atamruhusu Shetani kuzidi kuwashikilia mateka.
Katika Maandiko, Yesu anatajwa kwamba ni “kichwa cha enzi yote na mamlaka” (Wakolosai 2:10). Ingawa maneno ya Kiyunani arche (kutawala) na exousia (mamlaka) hutumiwa wakati mwingine kusema juu ya viongozi wa kisiasa wa kibinadamu, yanatumika pia katika Agano Jipya kama majina kwa ajili ya viongozi pepo wa kiroho. Fungu maarufu kuhusu mapambano ya Mkristo dhidi ya wafalme (arche) na mamlaka (exousia) katika Waefeso 6:12 ni mfano mmoja.
Kimantiki, tukisoma kile ambacho Paulo aliandika kuhusu Yesu kuwa kichwa juu ya enzi yote na mamlaka katika Wakolosai 2:10, inaonekana wazi kabisa kwamba anasema juu ya nguvu za kiroho. Kwa mfano: Katika fungu hilo hilo, mistari minne baadaye, Paulo anaandika hivi juu ya Yesu: “Akiisha kuzivua enzi na mamlaka, alizifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo” (Wakolosai 2:15).
Kama Yesu ni kichwa juu ya watawala wa kiroho na mamlaka, basi ana enzi juu yao. Huu ni ufunuo mzuri sana kwa Wakristo wanaoishi katika tamaduni za kipagani, zenye kutawaliwa na ushirikina, waliokuwa wanaabudu sanamu zamani kwa sababu ya kuogopa uwezo wa mapepo waliojua kwamba wana mamlaka juu yao.
Njia Pekee Ya Kuepuka
Njia pekee ya kupona utumwa wa mapepo ni kutubu na kuiamini Injili. Hiyo ndiyo njia ya kupona ambayo Mungu ameipanga. Hakuna awezaye kuzifunga nguvu za mapepo juu ya mji na kukuweka huru, au hata uhuru kidogo. Bila mtu kutubu na kuiamini Injili, bado anakaa katika ghadhabu ya Mungu (ona Yohana 3:36), na hiyo ni pamoja na kushikwa mateka na nguvu za kipepo.
Ndiyo sababu hakuna mabadiliko yanayoweza kupimika katika miji ambayo mikutano mikubwa ya vita za kiroho imefanyika, maana hakuna chochote kilichotokea ambacho kimeathiri mamlaka ya kipepo yenye kutawala maeneo hayo. Wakristo wanaweza kupiga kelele kwa mamlaka na falme hizo mchana kutwa na usiku kucha. Wanaweza kujaribu kumtesa Shetani kwa vitu vinavyoitwa “lugha za mapambano”. Wanaweza kusema, “Tunafunga pepo wabaya juu ya mji huu” mara milioni na zaidi. Wanaweza hata kufanya mambo hayo yote wakiwa ndani ya ndege au wakiwa kwenye magorofa ya juu kabisa ya majengo marefu sana (kama wengine wanavyofanya); na kitu kipekee kitakachowaathiri pepo hao wabaya ni kwamba watapata nafasi ya kuwacheka hao Wakristo wajinga.
Basi, tufikie hekaya ya sita ya siku hizi, kuhusu vita ya kiroho.
Hekaya Ya Sita: “Vita Ya Kiroho Dhidi Ya Pepo Zinazotawala Eneo Hufungua Milango Ya Uinjilisti Wenye Matokeo.”
Kinachowasukuma Wakristo wengi wanaojihusisha sana katika vita ya kiroho dhidi ya pepo zinazotawala eneo, ni shauku yao kuona ufalme wa Mungu ukipanuka. Kwa hilo, wanastahili pongezi. Kila Mkristo anapaswa kutamani kuona watu wengi wakiokoka kutoka kwenye utumwa wa Shetani.
Lakini, ni muhimu pia kwamba tutumie mbinu za Mungu kujenga ufalme Wake. Mungu anajua kitakachofanya kazi, na kinachopoteza muda tu. Ametuambia wazi wazi wajibu zetu ni nini kuhusu kuongezeka kwa ufalme Wake. Kudhani kwamba tunaweza kufanya kitu kisichopatikana katika Maandiko, kitakachozidisha fanaka ya uinjilisti wetu – kitu ambacho Yesu, Petro wala Paulo hawakufanya katika huduma zao, ni upumbavu.
Kwa nini Wakristo wengi wanadhani kwamba vita ya kiroho inaweza kufungua mlango wa uinjilisti wenye mafanikio? Mara nyingi hoja zao ni kama ifuatavyo: “Shetani amepofusha akili za watu ambao hawajaokoka. Basi, lazima tupigane vita ya kiroho dhidi yake ili kumzuia asiwapofushe. Kile kinachowapofusha kikiondolewa, watu wengi zaidi wataiamini Injili.” Lakini je, huo ni ukweli?
Hakika Shetani amepofusha akili za watu ambao hawajaokoka. Paulo aliandika hivi:
Lakini, ikiwa Injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya Injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu (2Wakor. 4:3, 4).
Swali ni hili: Je, Paulo aliwapa Wakristo wa Korintho habari hizi kwa kusudi la kuwahamasisha wajihusishe na vita ya kiroho ili kuangusha mapepo wanaosimamia eneo, ili watu wasio-okoka wawe wasikivu zaidi?
Jibu ni Hapana, kwa sababu kadhaa zilizo wazi.
Kwanza: Paulo hakuendelea hivi: “Basi ndugu Wakorintho. Kwa kuwa Shetani ameipofusha akili ya wasioamini, ninataka mwingie katika vita ya kiroho na kuangusha pepo wote wanaosimamia maeneo, ili vinavyowapofusha wasioamini viondolewe.” Badala yake, kinachofuata ni kusema juu ya yeye kumhubiri Kristo, ambayo ndiyo njia pekee ya kuondoa upofu wa kiroho.
Pili – Hakuna popote katika barua zake ambapo Paulo aliwaagiza waamini wowote kuhusika na kuangusha ngome juu ya miji yao, ili matokeo ya uinjilisti yaongezeke.
Tatu – Tunajua kutokana na kusoma barua zote za Paulo, kwamba, hakuamini upofushwaji unaofanywa na Shetani ulikuwa sababu ya msingi ya wasioamini kudumu katika hali yao. Kweli, upofushwaji unaofanywa na Shetani unachangia kwa kiwango fulani, lakini si sababu pekee au iliyo kubwa. Sababu ya msingi yenye kuwafanya watu wasiokoke ni ugumu wa mioyo yao. Hili ni wazi kutokana na sababu rahisi tu kwamba Shetani hawezi kumfanya kila mtu kuwa kipofu. Watu wengine wanaposikia ukweli huamini, na hukataa uongo wote ambao waliamini hapo kwanza. Si kupofushwa na Shetani kunakosababisha kutokuamini kwao, bali ni kutokuamini kwao kunakosababisha Shetani kuwapofusha.
Mioyo Migumu
Katika barua yake kwa Waefeso, mtume Paulo alieleza vizuri kabisa sababu ya wasiokuwa Wakristo kubakia katika kutokuamini kwao.
Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao; akili zao zimetiwa giza [pengine ndiyo kupofushwa na Shetani], nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani (Waefeso 4:17-19. Maneno mepesi kukazia).
Paulo anasema, wasio-okoka wamefarakanishwa na uzima wa Mungu kwa sababu ya “ujinga uliomo ndani yao.” Mbona ni wajinga? “Kwa nini “akili zao zimetiwa giza”? Jibu ni, “kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao.” Wame”kufa ganzi”. Hiyo ndiyo sababu ya msingi ya watu kuendelea kutookoka.[2] Lawama wanabeba wao wenyewe. Shetani anachotoa ni ule uongo ambao wanataka kuuamini.
Mfano wa Yesu kuhusu mpanda mbegu na aina za udongo huonyesha hilo pia.
Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila… Na huo mfano, maana yake ni hii: Mbegu ni neno la Mungu. Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka (Luka 8:5, 11, 12).
Ona hapo kwamba ile mbegu, ambayo ni mfano wa Injili, ilianguka kando ya njia, na kukanyagwa. Haikuweza kupenya udongo mgumu ule ambao unakanyagwa na watu wanapotembea. Basi ikawa rahisi tu kwa ndege, ambao ni mfano wa Shetani, kuziiba zile mbegu.
Hoja kuu ya mfano huo mzima ni kulinganisha hali za mioyo ya watu (na jinsi wanavyopokea Neno la Mungu) na aina mbalimbali za udongo. Yesu alikuwa anaeleza kwa nini watu wengine huamini na wengine hawaamini – ni uamuzi wao.
Shetani anaingiaje hapo? Yeye ana uwezo wa kuiba Neno kutoka kwa wale wenye mioyo migumu tu. Ndege katika mfano huu ilikuwa sababu ya pili ya mbegu kutochipua. Sababu ya msingi ni udongo – yaani, ugumu wa udongo ndiyo ulifanya iwezekane ndege kuzipata mbegu.
Ndivyo ilivyo kwa habari ya Injili. Tatizo hasa ni mioyo migumu ya watu ambao wana hiari. Watu wanapokataa Injili, wanafanya uchaguzi wa kuendelea kuwa vipofu. Wangependa kuamini uongo badala ya ukweli. Yesu alisema hivi juu ya hilo: “Nuru imekuja ulimwengu, lakini watu wamependa giza kuliko nuru, maana matendo yao ni maovu” (Yohana 3:19. Maneno mepesi kukazia).
Biblia haitufanyi tuamini kwamba watu ni wazuri, wenye mioyo safi, ambao wataiamini Injili bila shida yoyote, mradi tu Shetani aache kuwapofusha. Kinyume chake ni kweli. Biblia inaonyesha picha mbaya sana juu ya tabia na hali ya mwanadamu, na Mungu atamwajibisha kila mtu kwa ajili ya uchaguzi wake wa dhambi. Akiwa kwenye kiti chake cha enzi cha hukumu, Mungu hatakubali kujitetea kwa mtu yeyote kwamba, “Shetani alinifanya nitende nilivyotenda.”
Jinsi Shetani Anavyopofusha Akili Za Watu
Shetani anapofushaje akili za watu? Je, ana nguvu fulani za ajabu za kiroho anazomimina ndani ya vichwa vya watu ili kuwazubaisha katika ufahamu wao? Je, pepo hutia makucha yake katika akili zao, na kwa njia hiyo kuwafanya washindwe kabisa kufikiri vilivyo? Hapana! Shetani hupofusha akili za watu kwa kuwapa uongo wa kuamini.
Ni hivi: Kama watu wangeamini kweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu aliyekufa kwa ajili ya dhambi zao, na kama kweli wangeamini kwamba siku moja watasimama mbele Zake na kutoa hesabu ya maisha yao, basi wangetubu na kuwa wafuasi Wake. Lakini hawaamini hayo yote. Ila, kuna kitu wanachokiamini. Wanaweza kuamini kwamba hakuna Mungu, au kwamba hakuna maisha mengine baada ya kufa. Wanaweza kuamini kwamba mtu akifa anarudi kuishi tena, au kwamba Mungu hawezi kumtupa yeyote jehanamu. Wanaweza kudhani kwamba matendo yao ya kidini yatawafikisha mbinguni. Lakini – chochote wanachoamini – kama si Injili, jina lake kwa kifupi ni: uongo. Hawaamini ukweli, hivyo, Shetani anawaweka katika hali ya upofu kwa njia ya uongo. Lakini, wakijinyenyekeza wenyewe na kuamini ukweli, Shetani hataweza kuwapofusha tena.
Uongo Wa Giza
Katika Maandiko, ufalme wa Shetani unaitwa “utawala wa giza” (Wakolosai 1:13). Giza ni mfano wa kutokuwepo na ukweli – kutokuwepo na nuru au kuangaziwa. Unapokuwa gizani, unakwenda kwa mawazo yako na mwishowe unaumia. Ndivyo ilivyo katika ufalme wa Shetani wa giza. Wale waliomo humo wanaishi maisha yao kwa kuwaza kwao, na mawazo yao yamejazwa uongo wa Shetani. Wako katika giza la kiroho.
Maelezo mazuri kuhusu ufalme wa Shetani ni kwamba, si ufalme wa kijiografia wenye mipaka dhahiri, bali ni ufalme wa imani – yaani, kuamini katika uongo. Ufalme wa giza uko mahali pamoja na ufalme wa nuru. Wale wenye kuiamini kweli wanaishi pamoja na wale wenye kuamini uongo.[3] Kazi yetu kubwa ni kutangaza kweli kwa watu ambao wanaamini uongo tayari. Wakati mtu anapoamini ukweli, Shetani anapoteza raia wake mmoja – hawezi kumdanganya tena!
Basi tunawaweka huru watu wasio-okoka, si kwa “kufunga” pepo waovu juu yao, bali kwa kutangaza kweli. Yesu alisema hivi: “Mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32. Maneno mepesi kukazia). Upofu wa kiroho huondolewa kwa ukweli.
Katika fungu hilo hilo la Maandiko katika Injili ya Yohana, Yesu aliwaambia watu ambao hawajaokoka hivi:
Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki (Yohana 8:44, 45. Maneno mepesi kukazia).
Ona tofauti ambayo Yesu anaonyesha kati Yake na Shetani. Yeye husema ukweli, Shetani ni mwongo wa mwisho.
Ona pia kwamba, ingawa Yesu aliwaambia wasikilizaji Wake kwamba baba yao ni Ibilisi, na ingawa alimweka Shetani wazi kama mwongo, bado aliweka wajibu wa kuamini kweli aliyowaambia juu yao. Halikuwa kosa la Shetani kwamba wao wamepofushwa – kosa lilikuwa lao. Yesu aliwawajibisha. Shetani huwasaidia watu “wanaopenda giza” kuendelea kukaa gizani kwa kuwapa uongo ambao wanaweza kuuamini. Lakini, Shetani hawezi kumdanganya yeyote atakayeamua kuiamini kweli.
Kwa kuwa mambo ndiyo hayo, njia ya msingi ya kusukuma nyuma ufalme wa giza ni kwa kueneza nuru – kweli ya Neno la Mungu. Nidyo maana Yesu hakutuambia, “Enendeni duniani kote na kumfunga Ibilisi.” Alituambia hivi: “Enendeni duniani kote na kuihubiri Injili.” Alimwambia Paulo kwamba kusudi la mahubiri yake lingekuwa kufungua “macho yao ili watoke katika giza na kuingia katika nuru, na watoke katika utawala wa Shetani na kumjia Mungu” (Matendo 26:18. Maneno mepesi kukazia). Ni kitu kilicho wazsi kabisa kwamba watu huepuka utumwa wa Shetani wanapojulishwa kweli ya Injili, kisha wafanye uamuzi wa kugeuka kutoka gizani na kuja nuruni, na kuamini ukweli badala ya uongo. Ngome pekee za “kuangushwa” ni ngome za uongo ambazo zimejengwa katika akili za watu.
Huu Ni Mpango Wa Mungu
Usisahau kwamba Mungu ndiye alimtupa Shetani kutoka mbinguni mpaka duniani. Angeweza kumweka popote pengine katika ulimwengu, au kumfunga milele. Lakini, hakufanya hivyo. Kwa nini? Kwa sababu alitaka kumtumia Shetani kutimiza lengo Lake hatimaye – lengo la kuwa na familia kubwa siku moja, ya watu wenye hiari, ambao wangempenda kwa uamuzi wao wenyewe na kumtumikia.
Kama Mungu alitaka familia ya watoto watakaompenda, vitu viwili vilitakiwa. Kwanza – Ilibidi aumbe watu wenye hiari, kwa sababu msingi wa upendo ni hiari. Mashine na mitambo haviwezi kupenda.
Pili – Ilikuwa lazima kuwajaribu katika mazingira ambayo wangekabiliwa na uchaguzi wa kutii au kutokutii – kumpenda au kumchukia. Watu wenye hiari lazima wajaribiwe. Na kama kutakuwepo na kipimo cha uaminifu, lazima kuwepo na jaribu la kutokuwa mwaminifu. Basi, tunaanza kuelewa sababu ya Mungu kumweka Shetani duniani. Shetani angekuwa chaguo mbadala kwa habari ya uaminifu wa binadamu. Angeruhusiwa (na mipaka fulani fulani) kumshawishi yeyote ambaye angetaka kusikiliza uongo wake. Kila mtu angekabiliwa na uchaguzi huu: Je, nimwamini Mungu au Shetani? Je, nimtumikie Mungu au Shetani? Watu watambue wasitambue, wote wamekwisha fanya uchaguzi tayari. Kazi yetu sisi ni kuwatia moyo watu ambao wamefanya uchaguzi wa makosa watubu na kuiamini Injili, na kufanya uchaguzi sahihi.
Je, hayo si ndiyo yaliyofanyika katika Bustani ya Edeni? Mungu aliweka mti wa ujuzi wa mema na mabaya pale, kisha akamkataza Adamu na Hawa wasile matunda yake. Kama Mungu hakutaka wasile, mbona aliuweka hapo? Jibu ni kwamba, ulikuwa kipimo.
Vile vile tunaona kwamba Shetani aliruhusiwa na Mungu kumjaribu Hawa. Hapo tena ni kwamba – ukitaka kupima uaminifu, lazima kuwepo na jaribu la kutokuwa mwaminifu. Shetani alimdanganya Hawa naye akamwamini, na wakati huo huo akaamua kutokuamini yale ambayo Mungu alikuwa amesema. Matokeo yake? Watu wa kwanza kuwa na hiari wakadhihirisha kutokuwa waaminifu kwao katika mioyo yao.
Vivyo hivyo, kila mtu mwenye uwezo wa kuamua hupimwa katika maisha yake yote. Mungu amejifunua kwa njia ya uumbaji Wake, hivyo, kila mtu anaweza kuona kwamba yupo Mungu mkuu (ona Warumi 1:19, 20). Mungu ametupa sote dhamiri, na ndani ya mioyo yetu tunajua kilicho sawa na kilicho kosa (ona Warumi 2:14-16). Shetani na mapepo yake wameruhusiwa, kwa kiwango fulani, kudanganya watu na kuwajaribu. Matokeo ni kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kuamua anapimwa.
Ukweli wa kusikitisha ni kwamba kila mwenye uwezo wa kuamua ameasi na “kuibadili kweli ya Mungu kwa uongo” (Warumi 1:25). Lakini, Mungu ashukuriwe kwa sababu ametoa malipo kwa ajili ya dhambi zetu, na njia ya sisi kuzaliwa katika familia Yake. Kifo cha Yesu cha kujitoa dhabihu ndiyo jibu la pekee lenye kutosheleza tatizo letu kabisa tatizo letu.
Uongo Wa Shetani Sasa, Na Baadaye
Sawa – Sasa tunaelewa angalau sababu moja kwa nini Shetani na jeshi lake la waasi wameruhusiwa kufanya kazi hapa duniani: Ni kwa kusudi la kuwadanganya wale wanaopenda giza.
Kweli hii inathibitishwa zaidi tunapogundua kwamba kulingana na kitabu cha Ufunuo, Shetani siku moja atafungwa na malaika mmoja na kukaa gerezani kwa miaka elfu moja. Sababu ya hilo ni nini? “Ili asiwadanganye mataifa tena” (Ufunuo 20:3). Wakati wa Miaka hiyo Elfu Moja, Yesu Mwenyewe atatawala dunia akiwa Yerusalemu.
Lakini baada ya hiyo miaka elfu, Shetani atafunguliwa kwa kitambo kidogo. Matokeo? “Atatoka ili kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za dunia” (Ufunuo 20:8).
Kama Mungu hataki Shetani awadanganye watu wakati huo, mbona atamwachilia? Tena ukizingatia kwamba kusudi la Mungu la kumfunga ni ili “asiwadanganye mataifa tena”?
Ni kweli kwamba Mungu asingependa Shetani adanganye mtu yeyote. Lakini anajua kwamba watu pekee wanaoweza kudanganywa na Shetani ni wale wasioamini maneno Yake Mungu. Shetani anaweza kuwadanganya wale tu ambao wanakataa ukweli, na ndiyo sababu Mungu anamruhusu kufanya kazi sasa, na atamruhusu kufanya kazi wakati huyo pia. Shetani anapowadanganya watu, hali za mioyo ya watu hudhihirika, na ndipo Mungu anapoweza kuchambua “ngano kutoka kwenye magugu” (ona Mathayo 13:24-30).
Hayo ndiyo yatakayofanyika mwishoni mwa Miaka Elfu wakati Shetani atakapofunguliwa. Atawadanganya wote wanaopenda giza, nao watakusanya majeshi yao kuzunguka Yerusalemu katika juhudi za kuangusha utawala wa Kristo. Mungu atajua anayempenda Yeye na anayemchukia Yeye. Basi, atatuma “moto kutoka mbinguni” mara moja, utakao”waangamiza” (Ufunuo 20:10). Shetani atatimiza makusudi ya Mungu wakati huo, kama tu anavyofanya wakati huu. Sababu hiyo miongoni mwa zingine inatosha kutufanya tuone kwamba ni ujinga kuwaza kwamba tunaweza “kuangusha pepo wanaotawala maeneo”. Mungu anawaruhusu wafanye kazi kwa sababu Zake Mwenyewe.
Uinjilisti KiBiblia
Ukweli halisi kabisa ni kwamba Yesu na mitume wa Agano Jipya hawakufanya vita hiyo ya kiroho ambayo wengine wanadai ndiyo kinachokosekana katika uinjilisti wenye mafanikio siku hizi. Hatumkuti Yesu, Petro, Yohana, Stefano, Filipo au Paulo “wakiangusha ngome” au “kuwafunga wenye nguvu” katika miji waliyohubiri. Badala yake tunaona kwamba walifuata uongozi wa Roho Mtakatifu kwa habari ya mahali alipowataka wakahubiri. Tunawaona wakitangaza Injili rahisi tu – kuwaita watu watubu na kumwamini Kristo – na tunaona wakifurahia matokeo ya ajabu sana. Na, katika nyakati ambapo waliwahubiria watu wasiotaka kusikia, waliokataa Injili, hatuwaoni wakiingia “kufanya vita ya kiroho ili Shetani asiendelee kupofusha akili za watu.” Badala yake tunawaona “wakikung’uta mavumbi ya miguu yao” kama Yesu alivyowaamuru, na kwenda mji mwingine (ona Mathayo 10:14; Matendo 13:5).
Ni ajabu kwamba mtu anaweza kudai kuwa “kuangusha ngome” na “kuwafunga wenye nguvu” ni sharti la kufanikiwa katika uinjilsti wakati ambapo kuna mifano maelfu ya uamsho mkubwa tu katika historia ya kanisa, ambapo “vita ya kiroho” aina hiyo haikutendwa.
Mtu atasema, “Sawa – lakini mbinu yetu inafanya kazi. Tangu tulipoanza kufanya aina hiyo ya vita ya kiroho, watu wameokoka kuliko wakati mwingine wowote.”
Kama huo ni ukweli, sababu ni hii. Yamekuwepo maombi zaidi kufuatana na Maandiko pamoja na kufanyika kwa uinjilisti, au ni kwa sababu ghafula, kundi la watu fulani limekuwa wasikivu kwa Injili.
Ungesemaje kama mwinjilisti mmoja angekwambia hivi: “Jioni hii kabla ya kuhubiri kwenye mkutano, nilikula ndizi tatu. Nilipohubiri, watu kumi na sita waliokoka! Hatimaye nimegundua siri ya uinjilisti wenye mafanikio! Tangu sasa, nitakuwa ninakula ndizi tatu kabla ya kuhubiri!”?
Bila shaka ungemwambia huyo mwinjilisti, “Kula kwako ndizi tatu hakuhusiani na hao watu kumi na sita kuokoka. Siri ya mafanikio yako ni kwamba, ulihubiri Injili, na watu hao kumi na sita waliokusikiliza walikuwa tayari kupokea.”
Mungu huliheshimu Neno Lake. Kama Mungu akitoa ahadi, na mtu atomize masharti ya hadi hiyo, Mungu atatunza ahadi Yake, hata kama huyo mtu anafanya mambo mengine ambayo si ya KiBiblia.
Ndiyo ukweli kuhusu matendo ya vita ya kiroho siku hizi. Ukianza kugawa vikaratasi vyenye ujumbe wa Injili na “kumfunga mwenye nguvu” juu ya mji wako wakati huo huo, kiasi fulani cha watu watakaokoka. Vivyo hivyo – ukianza kugawa vikaratasi vyenye ujumbe wa Injili bila ya kumfunga mwenye nguvu, kiasi kile kile cha watu wataokoka.
Jinsi Ya Kuombea Mavuno Ya Kiroho Kulingana Na Maandiko
Sasa basi – tuwaombeeje watu ambao hawajaokoka? Ni vizuri tutambue kwamba hakuna mafundisho katika Agano Jipya yenye kutuambia kwamba tuombe namna hii ili Mungu aokoe watu, wala hatuna taarifa zozote za watu katika Agano Jipya kuomba hivyo. Sababu ni kwamba, kwa mtazamo wa Mungu, Yeye amekwisha fanya kila kitu kinachohitajika kwa watu duniani kuokolewa. Yeye alitaka sana watu waokoke kiasi cha kumtoa Mwana Wake afe msalabani.
Lakini, mbona watu wote hawajaokoka mpaka sasa? Sababu ni kwamba si wote walioiamini Injili? Kwa nini hawakuamini? Kwa sababu mbili: (1) Ama hawajawahi kusikia Injili, au (2) Wameisikia, wakaikataa.
Ndiyo sababu, njia ya kuwaombea wasio-okoka kulingana na Maandiko ni kuomba wapate nafasi za kusikia Injili. Kwa mfano: Yesu alituambia “Mavuno ni mengi, bali watenda kazi ni wachache. Basi, mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno Yake” (Luka 10:2. Maneno mepesi kukazia). Ili watu waweze kuisikia Injili na kuokoka, lazima mtu awaambie. Ndiyo sababu tunapaswa kuomba ili Mungu atume watu kwenda kwao.
Kanisa la kwanza lilipo-omba juu ya mavuno kiroho, waliomba hivi: “Ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu, Yesu” (Matendo 4:29, 30. Maneno mepesi kukazia).
Aidha walikuwa wanaomba (1) nafasi za kutangaza Injili kwa ujasiri, au (2) ujasiri wa kuitangaza Injili katika nafasi ambazo walijua wangepata. Pia walitazamia Mungu athibitishe hiyo Injili kwa uponyaji, ishara na maajabu. Hayo ni maombi ya KiBiblia kabisa, na uone kwamba lengo lilikuwa kutoa nafasi kwa watu wasikie Injili. Mungu alijibu maombi yao, hivi: “Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri” (Matendo 4:31).
Paulo alishauri Wakristo waombeje kuhusu kupatikana kwa mavuno ya kiroho? Je, aliwashauri wamwombe Mungu aokoe watu zaidi? Hapana! Hebu tusome maneno yake.
Hatimaye ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee na kutukuzwa, vile vile kama ilivyo kwenu (2Wathes. 3:1. Maneno mepesi kukazia).
[Ombeni] Pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena (Waefeso 6:19, 20. Maneno mepesi kukazia).
Kama watu wataokoka au hapana kwa wakati huu ni swala lao, si swala la Mungu. Basi, maombi yetu yawe kwamba watu wasikie Injili na Mungu atusaidie kuitangaza. Mungu atajibu sala zetu, lakini hiyo bado si uhakikisho kwamba mtu ataokoka, maana Mungu anawapa watu haki ya kufanya maamuzi yao wenyewe. Wokovu wao unategemea jinsi watakavyoitikia Injili.
Hekaya Ya Saba: “Mkristo Anapotenda Dhambi, Anafungua Mlango Kwa Pepo Kuja Kukaa Ndani Yake.”
Ni kweli kwamba Mkristo anapotenda dhambi, yaweza kuwa ni kwa sababu amekubali jaribu la pepo. Kukubaliana na ushawishi wa pepo haumaanishi kwamba huyo pepo anaweza kumwingia mwamini. Tunapofanya dhambi kama Wakristo, tunavunja ushirika wetu na Mungu kwa sababu tumeacha kumtii (ona 1Yohana 1:5, 6). Tunajisikia hatia. Lakini si kwamba tumevunja uhusiano wetu Naye, maana sisi bado ni watoto Wake.
Tukiziungama dhambi zetu, “Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atusamehe dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9). Hapo, ushirika wetu Naye unarejeshwa. Ona kwamba Yohana hakusema tunahitaji kusafishwa pepo zozote zinazokaa ndani wakati tunapokuwa na hatia ya dhambi.
Kila Mkristo anakabiliwa kila siku na majaribu kutoka duniani, mwilini na kwa Shetani. Paulo aliandika kwamba kweli tunapambana na mapepo wa aina mbalimbali (ona Waefeso 6:12). Basi, kwa kiwango fulani, kila mwamini anasumbuliwa na mapepo. Hiyo ni kawaida , na ni wajibu wetu kumpinga Shetani na mapepo yake kwa imani katika Neno la Mungu (ona 1Petro 5:8, 9). Tunapoamini na kutenda kulingana na yale aliyosema Mungu, huko ndiko kumpinga Shetani.
Kwa mfano: Kama Shetani ataleta mawazo ya kuvunja moyo, tunapaswa kufikiria andiko lenye kupingana na hali hiyo, na kutii Neno la Mungu kwamba “furahini sikuzote” (1Wathes. 5:16) pamoja na “shukuruni kwa kila jambo” (1Wathes. 5:18). Ni wajibu wetu kutenda kulingana na Neno la Mungu na kubadili mawazo yaliyoletwa na Shetani kwa kutia mawazo ya Mungu.
Lazima tutambue kwamba, kama watu wenye hiari, tunaweza kufikiri kuhus chochote tunachotaka. Ikiwa mwamini ataendelea kuchagua kusikiliza na kukubaliana na mashauri ya pepo wabaya, anaweza kufungua mawazo yake yagandamizwe au kuonewa na pepo, ambayo ni hali ya kupokea na kutawaliwa zaidi na zaidi na mawazo mabaya. Akiamua kujitoa zaidi, atatawaliwa na aina fulani ya mawazo isiyo nzuri, kitu ambacho si rahisi kwa Mkristo, lakini huweza kutokea. Ila, hata na hapo, huyo Mkristo akitaka kuwa huru, anachohitaji kufanya ni kuamua kufikiri na kujitolea kwa Neno la Mungu, na kumpinga Shetani, naye anakuwa huru.
Lakini je, atafikia mahali pa kupagawa? Ndiyo, kama kwa hiari yake mwenyewe ataamua kutoka moyoni, bila kusukumwa, kumkana Kristo na kumwacha kabisa. Hapo hatakuwa Mkristo tena[4] na yawezekana akapagawa – akizidi kujitolea kwa huyo pepo aliyekuwa anamgandamiza au kumwonea. Lakini hilo liko mbali sana na wazo la kufungua mlango kwa ajili ya pepo ili aingie kwako kwa sababu ya dhambi moja tu.
Ni kweli kwamba hakuna mfano hata mmoja katika Agano Jipya wa Mkristo yeyote kupagawa na pepo. Wala hakuna onyo lolote litolewalo kwa Wakristo kuhusu uwezekano hatari huo wa wao kupagawa na pepo. Wala hakuna fundisho lolote litolewalo juu ya jinsi ya kutoa pepo kutoka kwa Wakristo wenzetu.
Ukweli ni kwamba, kama Wakristo, hatuhitaji pepo zitolewe kwetu – tunachohitaji ni akili zetu kufanywa upya kwa Neno la Mungu. Hiyo inakubalika na Maandiko. Paulo aliandika hivi:
Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu (Warumi 12:2).
Nia zetu zikiisha safishwa kutokana na taratibu za kizamani za kufikiri na kufanywa upya na kweli ya Neno la Mungu, tunapata ushindi juu ya tabia za kale na kuishi maisha ya kufanana na Kristo. Ukweli ndiyo hutuweka huru (Yohana 8:32). Tunabadilika tunapofanywa upya katika nia zetu, si kwa kutolewa pepo wote tulio nao!
Mbona basi kuna Wakristo wengi tu wenye kushuhudia kwamba wametolewa pepo (au mapepo)? Uwezekano mmoja ni kwamba, pengine walidhani tu kwamba wana pepo ambalo limetolewa. Wakristo wengi ni wepesi kudanganywa na hawajui sana Neno la Mungu. Basi, wanakuwa rahisi kutekwa na “watumishi wa ukombozi” ambao wanawashawishi watu kwa ujanja sana wanadhani kwamba wana pepo. Watu wakiisha shawishika kwamba wana pepo ndani yao, watashirikiana kirahisi tu na mtu yeyote anayeonyesha kujiamini kwa habari ya kutoa pepo ndani ya walio nazo.
Uwezekano mwingine ni kwamba watu kama hao ambao wametolewa pepo hawakuwa waamini halisi wa Kristo wakati wa kufunguliwa kwao, ingawa wao walidhani ni waamini. Injili ya kisasa ambayo iko tofauti kabisa na ile Injili ya Biblia, imewadanganya wengi sana kufikiri kwamba wao ni Wakristo, ingawa hawana tofauti yoyote na wasiokuwa Wakristo. Tena, Yesu si Bwana maishani mwao. Tunaona katika Maandiko kwamba, watu walipoamini Injili na kuzaliwa upya, pepo waliokaa ndani yao walitoka wenyewe (ona Matendo 8:5-7). Pepo hawawezi kumpagaa mtu mwenye Roho Mtakatifu ndani, na Roho Mtakatifu hukaa ndani ya watu wote walizaliwa mara ya pili.
Hekaya Ya Nane: “Kwa Kujifunza Historia Ya Mji, Tunaweza Kutambua Pepo Zinazotawala Hapo, Na Kufanikiwa Sana Katika Vita Ya Kiroho, Na Hatimaye Katika Uinjilisti.”
Hekaya hii imejengwa juu ya mawazo kadhaa, ambayo hayana msingi katika Maandiko. Wazo moja ni kwamba pepo wanaotawala eneo hukaa kwa muda mrefu sana. Yaani – waliokuwepo katika eneo kwa miaka mia kadhaa bado ndiyo wale wale. Hivyo, tukigundua kwamba mji ulianzishwa na watu wachoyo, tunaweza kuamua kwamba zipo roho au pepo za choyo juu ya mji huo hata leo. Kama mji ulikuwa kijiji cha Kihindi hapo kwanza, basi tuamue kwamba pepo za uchawi na uaguzi bado zinatawala mji huo mpaka leo. Na kadhalika na kadhalika.
Lakini je, ni kweli kwamba mamlaka zile zile ovu na falme zilizokuwa zinatawala eneo fulani kijiografia kwa miaka mia nyingi, bado zipo hata leo? Labda, lakini si lazima iwe hivyo.
Hebu tufikiri kisa tulichotazama mapema, kutoka sura ya kumi ya kitabu cha Danieli. Yule malaika asiyetajwa, aliyesaidiwa na Mikaeli kupigana na “mkuu wa Uajemi” alimwambia Danieli hivi: “Sasa nitarudi kupigana na mfalme wa Uajemi; na tazama, mkuu wa Uyunani naye atakuja” (Danieli 10:20. Maneno mepesi kukazia). Tunasoma katika historia kwamba Dola ya Uajemi ilishindwa na Wayunani kupitia mapigano na Iskanda Mkuu. Lakini, huyu malaika asiyetajwa jina alifahamu kuhusu mabadiliko yaliyokuwa yanakuja katika ulimwengu war oho – kwamba “mkuu wa Uyunani” alikuwa anakuja.
Je, mkuu wa Uyunani alipokuja, alitawala katika ulimwengu wa roho juu ya Dola ya Uyunani kama mkuu wa Uajemi alivyofanya katika ulimwengu wa roho juu ya Dola ya Uajemi? Pengine, na kama ndivyo, basi pepo kadhaa wa vyeo vya juu walibadilishana maeneo maana, Dola ya Uyunani ilitawala eneo lote lililokuwa Dola ya Uajemi. Wakati yanapotokea mabadiliko kisiasa hapa duniani, yawezekana kunakuwa na mabadiliko pia katika ufalme wa giza. Ila ukweli ni kwamba hatuwezi kujua, labda kama Mungu atatufunulia.
Vyovyote vile – haileti tofauti yoyote kwamba ni aina gani ya pepo wanaotawala juu ya eneo fulani kijiografia maana hakuna chochote tunachoweza kufanya juu yake kwa habari ya “vita ya kiroho”, kama tulivyokwisha ona mapema.
Kuwaweka Pepo Katika Makundi Kuliko Ilivyo
Tena, wakati mwingine, sisi hudhania tu kwamba wapo pepo wanaotawala aina fulani ya dhambi. Dhana nzima kwamba kuna “roho ya choyo,” “roho ya ashiki ya mwili,” “roho za dini,” “roho za ugomvi” na kadhalika, haina msingi katika Maandiko, licha ya wazo kwamba aina hizo mbalimbali za pepo hupatikana katika ngazi za juu za pepo wabaya wanaotawala katika ufalme wa giza.
Cha kushangaza kwa wale ambao hawajawahi kujifunza zile Injli nne kwa ukaribu, kuna aina tatu tu maalum za pepo ambazo Yesu alitoa. “Pepo bubu” anatajwa mara moja (Luka 11:14), na tunasoma mara moja juu ya “pepo bubu na kiziwi” (Marko 9:25), na zaidi ya mara moja tunasoma juu ya “pepo wachafu” ambao ni kama mchanganyiko wa pepo wote Yesu aliotoa, pamoja na yule “bubu na kiziwi” (ona Marko 9:25).
Je, haiwezekani kwamba huyo “pepo bubu na kiziwi” alikuwa na uwezo wa kumfanyia mtu kitu zaidi ya hayo? Bila shaka, maana yule mvulana katika Marko 9 alikuwa anapata kifafa pia. Basi, “pepo bubu na kiziwi” pengine si aina ya pepo, bali ni mtajo kuhusu jinsi pepo huyo alivyokuwa anamdhuru mtu fulani. Wengine wetu ni kama tunaehuka kwa habari ya “kupanga” mapepo mpaka tunakwenda hata zaidi ya mafunuo ya Biblia.
Pepo wanaotajwa katika Agano la Kale ni “pepo wa udanganyifu” (1Wafalme 22:22, 23), “pepo wa kupotosha” (Isaya 19:14), na “pepo wa ukahaba” (ktk Hosea 4:12; 5:4). Kwa habari ya aina ya kwanza na ya pili, hakika pepo wote wanaweza kuitwa “roho zidanganyazo” na “roho za kupotosha”. Kwa habari ya aina ya tatu, neno “pepo wa ukahaba” si lazima kuwa pepo mchafu maalum. Inaweza kuwa ni hali ya moyo iliyopo.[5]
Katika kitabu chote cha Matendo, wakati pekee ambapo pepo mchafu anatajwa ni katika Matendo 16:16, tunaposoma juu ya msichana aliyekuwa na “pepo wa utambuzi.” Na katika nyaraka zote, aina pekee ya pepo wanaotajwa hao ni “roho zidanganyazo” (ktk 1Timo. 4:1), ambazo zinaweza kuwa pepo aina yoyote ile.
Basi, kutokana na mitajo michache kuhusu aina fulani za pepo katika Biblia, inashangaza kusoma orodha za siku hizi za mapepo, zenye majina mia nyingi ya aina mbalimbali za pepo wanaoweza kuwapagaa watu au kutawala miji.
Hata hivyo, hatupaswi kudhani kwamba kuna mpangilio wowote, kwa dhambi maalum, wa pepo wa vyeo vya juu. Ni dhana tu kusema kwamba, “Kwa sababu kuna wingi wa kamari katika mji ule, lazima kuna pepo wa kamari juu yake.”
Kuna Pepo Wa Uvutaji?
Hebu fikiri jinsi ambavyo mtu angeonekana mjinga kama angesema hivi: “Kuna pepo wengi sana wa uvutaji katika mji huo, maana watu wengi humo wanavuta sigara.” Je, hao “pepo wa uvutaji” walikuwa wanafanya nini kabla ya miji hiyo kuwepo? Walikuwa wapi siku hizo? Walikuwa wanafanya nini kabla tumbaku haijajulikana na kutumiwa kwa ajili ya uvutaji? Je, sababu ya watu wavutao kupungua siku hizi ni kwa kuwa baadhi ya hao “pepo wa uvutaji” wa zamani wanakufa, au ni kwa sababu wanahamia katika maeneo mapya?
Unaona ujinga wenyewe tunaposema vitu kama, “Mji huo unatawaliwa na pepo za ashiki ya mwili, maana ndiyo sababu kuna ukahaba sana pale”? Ukweli ni huu: Popote ambapo watu hawamfuati Kristo, kuna ufalme wa giza. Pepo wengi hufanya kazi katika eneo hilo la giza, wanaoshawishi watu wao kutenda dhambi na kuendelea katika uasi wao dhidi ya Mungu. Hizo pepo zitawajaribu watu katika kila eneo la dhambi, na mahali pengine, watu watakubali dhambi moja zaidi ya zingine. Tumaini lao ni Injili, ambayo ndiyo tumeitwa kuitangaza.
Hata kama kuna aina fulani za mapepo ambao ni mafundi katika dhambi fulani, na ambao wanatawala maeneo fulani ya kijiografia, haitusaidii kujua juu yake kwa sababu hakuna tunachoweza kufanya kuwaondoa pale. Wajibu wetu ni kuomba (kulingana na Maandiko) kwa ajili ya watu walioko pale, waliodanganywa, na kuwahubiri Injili.
Uzuri pekee wa kugundua dhambi zinazotawala mji fulani ni ili tuweze kuhubiri jumbe zinazowagusa watu wasio-okoka wanaokaa pale – kwa kutaja dhambi zile zinazowafanya kuwa na hatia mbele za Mungu. Lakini hakuna haja ya kufanya utafiti wa historia ya mji ili kujua hilo. Mtu anahitaji kutembelea mji huo kwa muda mfupi tu na kutazama kwa makini na kusikiliza kwa makini. Dhambi kuu hapo zitadhihirika tu kirahisi.
Mwisho – Hakuna mfano wowote katika Agano Jipya wa mtu yeyote kufanya “matembezi ya kiroho” kama namna ya kujiandaa kwa ajili ya vita ya kiroho, au uinjilisti. Wala hakuna maagizo yoyote katika Nyaraka kuhusu hilo. Katika Agano Jipya, mitume walimfuata Roho Mtakatifu kwa habari ya mahali pa kuhubiri, kisha wakatangaza Injili kwa uaminifu na kuwaita watu kutubu, na wakamtumaini Bwana kulithibitisha Neno kwa ishara. Njia yao ilifanikiwa sana!
Hekaya Ya Tisa: “Kuna Wakristo Wanaohitaji Kuwekwa Huru Kutokana Na Laana Za Ukoo Au Za Kishetani.”
Dhana nzima ya “laana za ukoo” hutokana na mafungu manne ya Maandiko katika Agano la Kale, yenye kusema kitu kimoja yote. Hayo ni Kutoka 20:5; 34:7; Hesabu 14:18 na Kumbukumbu la Torati 5:9. Tutazame Hesabu 14:18.
BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yoyote ile, mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne (maneno mepesi kukazia).
Sasa – tunatafsiri vipi Maandiko haya? Je, maana yake ni kwamba Mungu atamlaani mtu au kumwadhibu kwa sababu ya dhambi za wazazi wake, au babu zake, au babu wa babu, au mababu wakuu? Je, ni sawa kuamini kwamba Mungu anaweza kumsamehe mtu dhambi zake anapomwamini Yesu, kisha amwadhibu kwa sababu ya dhambi za wazazi wake na babu zake?
Si hivyo kamwe, la sivyo, Mungu angeshtakiwa kwa kutokuwa na haki, na kwa unafiki mkubwa. Yeye Mwenyewe alisema kwamba kumwadhibu mtu kwa sababu ya dhambi za wazazi wake ni kosa.
Lakini ninyi [Waisraeli] mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi. Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa. Mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe. Haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake (Ezekieli 18:19, 20. Maneno mepesi kukazia).
Tena, kulingana na Torati ya Musa, Mungu aliamuru kwamba baba wala mtoto wasichukue adhabu kwa ajili ya dhambi za yeyote kati yao.
Mababa wasiuawe kwa aili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe (Kumbu. 24:16).
Haiwezekani kwamba Mungu mwenye upendo na haki atoe laana au adhabu kwa mtu kwa sababu ya dhambi za wazee wake.[6] Basi, nini maana ya Maandiko kusema kwamba Mungu “hataacha kuwahesabia hatia wenye hatia, naye atapatiliza maovu ya baba juu ya wana wao, mpaka kizazi cha tatu na cha nne”?
Bila shaka maana yake ni kwamba Mungu anawawajibisha watu kwa ajili ya mifano ya dhambi wanayo-onyesha mbele ya uzao wao, na kwa njia hiyo anawahusisha kwa kiasi fulani na zile dhambi ambazo watoto wao wanazifanya kwa sababu ya mfano wao. Mungu anawawajibisha watu kwa sehemu, kwa sababu ya mifano yao miovu, kwa ajili ya dhambi za wajukuu zao! Mungu ni mtakatifu kiasi hicho. Na hakuna awezaye kusema kwamba anaonea mtu anapofanya hivyo.
Ona fungu tunalotazama, kwamba linasema, Mungu “atawapatiliza wana maovu ya baba zao.” Yanayopatilizwa ni maovu ya baba kwa watoto wao.
Basi, dhana nzima ya “laana za ukoo” ni potofu na mbaya, maana inamfanya Mungu aonekane asiye haki.
Laana Za Kishetani Je?
Lakini, vipi kuhusu “laana za Kishetani”?
Kwanza – Hakuna kitu katika Biblia nzima chenye kuonyesha kwamba Shetani anaweza “kumlaani” mtu, wala hakuna mifano yoyote kuonyesha akifanya hivyo. Kweli tunamwona akiwatesa watu katika Biblia, lakini hatumkuti “akilaani” familia ambayo baada ya hapo, inaendelea na balaa au maisha mabaya pamoja na vizazi vinavyofuata.
Kila Mkristo husumbuliwa na Shetani na mapepo wabaya (kwa kiwango fulani) maisha yake yote, lakini hii haina maana kwamba tunahitaji “kuvunja laana ya Kishetani” juu yetu ambayo imetoka kwa wazazi wetu. Tunachohitaji kufanya ni kusimama kwenye Neno la Mungu na kumpinga She tani kwa imani, kama tunavyoambiwa na Maandiko (ona 1Petro 5:8, 9).
Katika Biblia, Mungu ndiye mwenye uwezo wa kubariki na kulaani (ona Mwanzo 3:17; 4:11; 5:29; 8:21; 12:3; Hesabu 23:8; Kumbu. 11:26; 28:20; 29:27; 30:7; 2Nyakati 34:24; Zaburi 37:22; Mithali 3:33; 22:14; Ombolezo 3:65; Malaki 2:2; 4:6). Wengine wanaweza kutulaani kwa midomo yao, lakini laana zao hazina nguvu – haziwezi kutudhuru.
Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu (Mithali 26:2).
Balaamu alikuwa sahihi baada ya kuajiriwa na Balaki kuwalaani wana wa Israeli. Alisema hivi: “Nimlaanije yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje yeye ambaye BWANA hakumshutumu?” (Hesabu 23:8).
Wakristo wengine wamepita kiasi kwa wazo la watu kuwalaani wengine, kutokana na maneno ya Yesu katika Marko 11:23. “Amin nawaambia, Yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake ila aamin kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.”
Ila, ona kwamba hakuna nguvu katika kusema maneno tu, bali, katika kusema maneno ya imani kutoka moyoni. Hakuna jinsi mtu anavyoweza kuwa na imani kwamba laana yake dhidi ya mtu fulani inaweza kumdhuru huyo, kw sababu imani ni uhakika thabiti (Waebrania 11:1), na imani hutokana na kusikia Neno la Mungu tu (Warumi 10:17). Mtu anaweza kutazamia kwamba laana yake kwa mtu italeta balaa, lakini hawezi kuamini hivyo, kwa sababu Mungu hajatoa ahadi yenye kuleta imani hiyo kuhusu kuwalaani watu.
Tofauti pekee ni kama Mungu atampa mtu “karama ya imani” pamoja na “karama ya unabii” (ambazo ni mbili katika zile tisa za Roho) ili atamke kitu kama baraka au laana. Tunaona hayo mara kwa mara katika maisha ya watu fulani katika Agano la Kale (ona Mwanzo 27:27-29, 38-41; 49:1-27; Yoshua 6:26. Pia 1Wafalme 16:34; Waamuzi 9:7-20, 57; 2Wafalme 2:23, 24). Hata katika nyakati kama hizo, baraka au laana zilitoka kwa Mungu, si kwa mtu. Basi, dhana nzima ya mtu kuweka “kumlaani” mwingine ni potofu. Ndiyo sababu Yesu hakutuagiza “tuvunje laana ambazo zimetamkwa kinyume chetu,” bali “kuwabariki wanaotulaani.” Hatupaswi kuogopa laana ya mtu yeyote. Kuogopa laana ya mtu ni kuonyesha utovu wa imani kwa Mungu. Ila – kwa bahati mbaya sana – nakutana na wachungaji mara nyingi ambao wanaamini zaidi nguvu za Shetani kuliko za Mungu. Pamoja na safari zangu nyingi kila mwezi katika nchi tofauti tofauti ili kuharibu ufalme wa Shetani, siogopi hata kidogo kwamba nitatupiwa laana, wala simwogopi Shetani kwamba atanilaani. Hakuna haja ya kuogopa.
Laana Za Kichawi Je?
Je, yawezekana kupata laana za Kishetani kwa sababu ya kujihusisha katika uchawi siku za nyuma?
Tusisahau kwamba tunapozaliwa mara ya pili, tunakombolewa kutokana na nguvu za Shetani na ufalme wa giza (ona Matendo 26:18; Wakolosai 1:13). Shetani hana nguvu tena juu yetu, isipokuwa tukimpa ruhusa. Japo Biblia inaonyesha kwamba Wakristo wa Efeso walikuwa wanahusika sana katika mambo ya uchawi kabla ya kuokoka kwao (ktk Matendo 19:18, 19), hakuna taarifa yoyote ya Paulo kuvunja “laana za kishetani” juu yao, au kufunga nguvu za Shetani juu yao, baada ya wao kuzaliwa mara ya pili. Sababu ni kwamba waliwekwa huru kutokana na utawala wa Shetani mara tu walipomwamini Yesu mara ya kwanza.
Tena – Paulo alipowaandikia Waefeso, hakutoa maagizo yoyote kwao kuhusu kumweka mtu huru kutokana na laana za kishetani au za ukoo. Alichowaambia ni hiki: “Msimpe Shetani nafasi” (Waefeso 4:27), na “vaeni silaha zote za Mungu” ili kuweza “kuzipinga hila za Ibilisi” (Waefeso 6:11). Huo ni wajibu wa kila Mkristo.
Lakini, mbona mara zingine kuwa Wakristo ambao walisaidiwa baada ya mtu fulani kuvunja “laana ya ukoo” au “ya kishetani” kwao? Pengine ni kwa sababu huyo mtu aliyehitaji msaada aliamini kwamba Ibilisi atakimbia baada ya “laana” hiyo kuvunjwa. Imani humfukuza Shetani, na kila Mkristo anaweza na anapaswa kuwa na imani kamba anapompinga Shetani, atakimbia. Ila, hakuna haja ya kumwita “bingwa wa ukombozi” ili kumfanya Shetani akimbie.
Mwisho – Biblia inatuambia kwamba Kristo “alifanyika laana kwa ajili yetu,” na kwa kufanya hivyo, “akatukomboa na laana ya Torati” (Wagalatia 3:13. Maneno mepesi kukazia). Sote tulikuwa chini ya laana ya Mungu kwa sababu ya dhambi, lakini kwa kuwa Yesu alichukua adhabu yetu, tumewekwa huru kutokana na laana hiyo. Sifa kwa Mungu! Kwa kuwa hatuna laana tena, tunaweza kufurahi kwamba sasa tumebarikiwa “kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani ya Kristo” (Waefeso 1:3).
Hekaya Ya Kumi: “Tunaweza Kuvunja Vifungo Vya Mapepo Kwa Kufunga.”
Wakristo wengine wanahesabu kufunga kuwa ni sehemu kubwa sana katika maisha ya Kikristo, na jukumu muhimu sana. Inashangaza sana, hasa ukizinga tia kwamba katika nyaraka zote za Agano Jipya, hakuna fundisho hata moja kuhusu kufunga litolewalo kwa Wakristo. Wala Wakristo hawatiwi moyo kufunga katika nyaraka za Agano Jipya. Ukweli ni kwamba hakuna chochote kuhusu kufunga kinachotajwa katika nyaraka, isipokuwa Paulo anataja mara chache ambazo ilibidi ashinde na njaa – mfungo bila kupanga!
Katika kitabu cha Matendo, kuna mifano miwili tu ya kufunga kwa hiari.
Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakat ifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweak mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao (Matendo 13:2, 3. Maneno mepesi kukazia).
Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini (Matendo 14:23. Maneno mepesi kukazia).
Hapo tunajifunza kwamba faida ya msingi ya kufunga katika agano jipya ni kutupa muda zaidi wa kuomba kwa dhati. Hii ni muhimu sana wakati tunapomtafuta Mungu ili kujua mwelekeo fulani maalu, au tunaposubiri maongozi Yake kuwa dhahiri katika roho zetu.
Kama kila Mkristo ajuavyo, kitu kigumu sana kuhusu kuwa na wakati mrefu katika maombi ni kupata nafasi ya kufanya hivyo. Wakati mwingine njia pekee ya kupata masaa kadhaa ya kuomba ni kuondoa kitu kingine. Pengine hii ndiyo sababu Yesu wakati fulani aliomba usiku kucha (kumbuka ilikuwa kabla hajawachagua mitume Wake), na ndiyo sababu aliamka asubuhi na mapema ili aombe. Ndiyo sababu Paulo aliwaandikia Wakristo wenye ndoa kwamba wasinyimane tendo la ndoa, “isipokuwa mmepatana kwa muda ili mpate faragha kwa kusali” (1Wakor. 7:5. Maneno mepesi kukazia). Ili kuweza kupata muda wa kutosha wa maombi, itabidi tuache kwa muda baadhi ya starehe halali kabisa za maishani, kama vile chakula, usingizi na kushirikiana kimwili katika ndoa.
Ni Kufunga, Au Ni Kugoma Kula?
Ni vizuri kujua kwamba kufunga hakumbadilishi Mungu. Tusije tukadhani kwamba kwa kuwa tunajitesa kwa kufunga, Mungu atatusikiliza kirahisi zaidi tunapoomba. Mambo yakiwa hivyo, huko ni kugomea chakula.
Kufunga hakutupi nguvu zaidi kiroho, wala mamlaka juu ya pepo. Kama viungo katika mwili wa Kristo, tayari sisi tumeketi “katika ulimwengu wa roho, juu sana kuliko falme na mamlaka na nguvu na utawala, na kila jina litajwalo” (Waefeso 1:21). Tayari tuna mamlaka ya kutoa pepo kulingana na ahadi ya Yesu katika Marko 16:17 kwamba, “Na ishara hizi zitafuatana na waaminio. Kwa jina Langu watatoa pepo.”
Lakini, vipi kuhusu maneno ya Yesu kuhusu pepo mmoja aliyemtoa, kwamba, “Aina hii haitoki isipokuwa kwa kuomba na kufunga” (katika Mathayo 17:21)?
Kwanza: Biblia yangu inaonyesha kwamba nakala za mwanzo kabisa za Injili ya Mathayo hazina mstari huo. Maana yake ni kwamba, yawezekana Yesu hakusema hivyo.
Katika maelezo ya Marko ya tukio hilo hilo, Yesu anasema hivi: “Namna hii haitoki isipokuwa kwa maombi” (katika Marko 9:29), na hapo pembeni kuna maelezo kwamba, nakala nyingi za kale huongeza “na kufunga” mwishoni mwa mstari wenyewe.
Sasa je – Yesu alisema kufunga ni kitu muhimu katika kutoa pepo aina fulani? Jibu ni kwamba hatujui. Tena, kama Yesu alisema hivyo kweli, basi huo ndiyo wakati pekee ambapo Yeye na waandishi wengine wa Agano Jipya walipounganisha kufunga na kutoa pepo katika watu.
Pengine itafaa kujiuliza jinsi ambavyo kufunga kunaweza kuwa msaada katika kutoa pepo. Hakika kufunga hakuongezi mamlaka ya mtu juu ya mapepo. Kama Mungu amempa mtu mamlaka ya kutoa pepo, anayo tu. Kitu pekee kinachoweza kufanywa kwa kufunga ni kumpa mtu huyo muda zaidi wa kutafakari juu ya ahadi ya Mungu kwa habari ya mamlaka yake, na kwa njia hiyo kuongeza imani yake katika kile ambacho Mungu amesema. Imani ni swala muhimu sana katika kuleta ukombozi.
Katika hili tukio husika, wanafunzi walikwisha pewa mamlaka ya kutoa pepo wachafu (katika Mathayo 10:1), lakini wakashindwa kutoa pepo katika kijana mmoja. Yesu aliposikia juu ya kushindwa kwao, alisikitishwa sana na kutokuamini kwao (ona Mathayo 17:17), na walipomwuliza kwa nini wameshindwa, alijibu hivi: “Kwa sababu ya uhaba wa imani yenu” (Mathayo 17:20). Mistari michache baadaye ndipo tunakuta tamko la Yesu kuhusu kufunga.
Basi, twaweza kusema kwamba sababu ya kushindwa kwao ni kati ya hizi mbili: Ama hakuwakuwa na imani katika mamlaka yao waliyopewa na Mungu, pamoja na hawakuwa wameomba na kufunga kabla, au, hawakuwa na imani katikamamlaka yao waliyopewa na Mungu, na muda ambao wangeweza kutumia katika kufunga na kuomba kungesaidia kukuza imani yao. Afadhali la pili, maana linaleta maana. La kwanza linamfanya Yesu ajipinge. Kumbuka kwamba yote mawili yamejengwa juu ya dhana kwamba Yesu alisema maneno hayo kuhusu kufunga.
Pamoja na hayo, hatupaswi kusahau kwamba mitajo yote juu ya vita ya kiroho na kukombolewa kutoka mapepo haitaji kuhusu kufunga. Kufunga hakutajwi kabisa kwa habari ya via yetu binafsi dhidi ya Shetani na mapepo wabaya. Hivyo, kusema kwamba lazima tufunge ili kupata ushindi binafsi juu ya Shetani ni kinyume cha Maandiko.
Mfungo Mungu Anaochagua
Maandiko mengine yanayotumika vibaya mara kwa mara kuthibitisha kwamba kufunga kunaweza kuvunja mamlaka ya mapepo yanapatikana katika Isaya 58:6.
Je! Saumu niliyoichagua siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
Je, mstari huu unafundisha kwamba tunaweza kuvunja vifungo vya mapepo juu ya watu kwa kufunga? Labda, kama utatolewa katika mantiki yake. Hebu tumshinde Shetani kwenye mchezo wake mwenyewe (kutoa maandiko katika mantiki yake) na kusoma sehemu kubwa ya sura ya 58 ya Isaya, ili tujue Mungu alikuwa anasema nini hapo.
Piga kelele, usiache. Paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao (58:1)
Hapo, Mungu alikuwa anazungumza na Isaya, akimwagiza kuwatangazia Israeli dhambi zao. Katika mstari unaofuata, Mungu akaanza kuorodhesha dhambi zenyewe.
Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu (58:2).
Ni wazi kwamba Waisraeli walidai kuwa wenye haki, lakini dini yao ilikuwa mfano tu. Walikuwa wanaigiza ibada. Wnamwuliza Mungu hivi:
Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? (58:3a).
Mungu akajibu hivi:
Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumu ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanga nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? (58:3b – 5).
Inaonekana kwamba Waisraeli walikuwa wanafunga ili kumfanya Mungu awaone au kupata upendeleo fulani Kwake, nao wakashangaa maana hali zao hazikubadilika. Mungu akawajibu kwa kuwakumbusha juu ya maisha yao ya kibinafsi, yaliyokuwa yanaonyeshwa hata siku za kufunga kwao. Hata sababu zao za kufunga zilikuwa za kibinafsi tu, na kufanya kufunga huko kusikubalike kwa Mungu. Kisha akawaambia aina ya kufunga anayotafuta – mfungo usiotokana na ubinafsi.
Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo, wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? (58:6, 7).
Je, Mungu alikuwa anasema tendo la kufunga litawaweka watu huru wasifungwe na pepo? Hapana. Mungu aliwataka waache ubinafsi, si chakula. Alitaka wawapende jirani zao kama nafsi zao. Alitaka wavunje nira, “kuwaacha huru walioonewa,” kugawana chakula chao na wenye njaa, kuwaingiza maskini wasio na makao nyumbani mwao, na kuwavika nguo walio uchi. Tendo la kuacha kula pekee halitaleta mambo hayo. Hayo ni mambo ambayo watu lazima wafanye.
Tafsiri hii inakuwa dhahiri tunapoendelea kusoma. Kama Waisraeli wangeanza kufunga bila kufuata maisha yao ya ubinafsi, ahadi ya Mungu ni hii:
Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na BWANA ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyoshakidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani, na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri (58:8-10. Maneno mepesi kukazia).
Mstari wa 9 unaweka wazi kabisa kwamba Mungu hakuwa anasema juu Yake Mwenyewe kuondoa nira ya kipepo kama itikio la kufunga kwao. Badala yake, alikuwa anasema kwamba wao ndiyo walitakiwa kuondoa vifungo vya kibinadamu – si vya kipepo – kutoka kwa watu, kama vile kutowatendea haki na umaskini.
Mungu alikuwa anajali zaidi Waisraeli wajiepushe na ubinafsi na choyo, kuliko alivyojali kujiepusha kwao na chakula. Bila shaka huo ndiyo ukweli hata kwetu sisi. Amri ya pili iliyo kuu ni “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” (Marko 12:31), siyo “Hakikisha kwamba unafunga mara nyingi”!
Wazo kwamba tunaweza kuwafungua watu kutoka vifungo vya Shetani kwa tendo la kufunga ni kosa. Njia ya msingi ya kuwafungua watu kutokana na kufungwa kwao na Shetani ni kuwaambia habari njema – Injili. Wakipokea kwa imani, watawekwa huru. Ndipo tunapoweza kuuwafundisha jinsi ya kumpinga Shetani kwa imani katika Neno la Mungu.
Vita Ya Kiroho Ya Kimaandiko
Tumetaja hekaya nyingi za kisasa zinazohusiana na vita ya kiroho mpaka hapa. Lakini tujiulize: Je, kuna aina ya vita ya kiroho ambayo ni ya kimaandiko? Jibu ni ndiyo, na tutashughulika na hilo wakati huu.
Pengine kitu cha kwanza tunachohitaji kufahamu kuhusu vita ya kiroho ni kwamba, haipaswi kuwa kiini cha maisha yetu ya Kikristo. Tunatakiwa kumtazama Kristo, kumfuata na kumtii Yeye, kadiri tunavyoendelea kukua na kufanana Naye. Ni sehemu ndogo sana ya Maandiko ya Agano Jipya yenye kusema juu ya vita ya kiroho, na hilo linatuonyesha kwamba kinapaswa kuwa kitu chenye kupewa mtazamo mdogo katika maisha yetu ya Kikristo.
Cha pili tunachohitaji kujua ni kwamba Biblia inatueleza kila tunachohitaji kufahamu juu ya jambo hilo. Hatuna haja ya utambuzi wa kpekee (au mhubiri mwenye kudai kwamba ana utambuzi wa kipekee) kuhusu “mambo ya ndani sana ya Shetani.” Vita ya kiroho KiBiblia ni rahisi tu. Mbinu za Shetani zinafunuliwa vizuri katika Maandiko. Wajibu zetu zimeainishwa vizuri kabisa. Ukiisha fahamu na kuamini yote aliyosema Mungu, unahakikishiwa ushindi katika mapambano hayo ya kiroho.
Kurudi Mwanzo
Hebu turudi mpaka mwanzo – katika kitabu cha Mwanzo – mahali tunapokutana na Shetani kwa mara ya kwanza. Katika sura za mwanzo hapo, Shetani anatokea katika umbo la nyoka. Kama kuna mashaka kwamba ni Shetani, Ufunuo 20:2 inaondoa mashaka hayo, hivi: “Akamshika yule nyoka, yule joka wa zamani, yaani Ibilisi na Shetani” (maneno mepesi kukazia).
Mwanzo 3:1 inasema hivi: “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu.” Unapofikiri juu ya werevu wa baadhi ya viumbe wa Mungu wanaposhindana katika kuishi na wanapowinda wenzao, utatambua jinsi Shetani alivyo mwerevu. Ila kwa upande mwingine, Shetani hajui kila kitu wala si mwenye hekima yote kama Mungu. Basi, hatupaswi kudhani kwamba katika kukabiliana naye, tunazidiwa akili. Yesu alitushauri sisi kuwa “wajanja kama nyoka” (Mathayo 10:16. Maneno mepesi kukazia). Paulo anadai kwamba sisi hatukosi kuzijua hila za Shetani (ktk 2Wakor. 2:11) na kwamba sisi tunayo “nia ya Kristo (1Wakor. 2:16).
Shetani alitupa mshale wake wa kwanza wa moto ulioandikwa katika Biblia kwa kumwuliza Hawa maswali juu ya alichosema Mungu. Jibu lake lingemfunulia kama alikuwa na nafasi ya kumdanganya asimtii Mungu. Shetani hana njia yoyote ya kumdanganya mtu anayemwamini na kumtii Mungu kwa alichosema. Ndiyo sababu mkakati wake wote umejengwa kwenye mawazo yenye kupingana na Neno la Mungu.
Shetani akamwuliza, “Kwa hiyo Mungu amesema, ‘Msile matunda ya mti wowote katika bustani’?” (Mwanzo 3:1). Utadhani ni swali tu la kawaida kutoka kwa mtu anayeuliza kitu kidogo, lakini Shetani alijua lengo lake.
Hawa akaitika hivi: “Tunaweza kula matunda ya miti yote bustanini, isipokuwa ule wa katikati. Mungu alisema, ‘Msile matunda yake wala msiuguse, msije mkafa’!” (Mwanzo 3:2, 3).
Hawa alikaribia. Ukweli ni kwamba Mungu hakuwakataza kuugusa mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Aliwakataza kula matunda yake tu.
Hawa alijua ukweli kiasi cha kutosha kutambua uongo wa jibu la Shetani, kwamba, “Hakika hamtakufa!” (Mwanzo 3:4). Maneno hayo yalikuwa kinyume kabisa na kile alichosema Mungu, na isingewezekana Hawa aamini. Hivyo, Shetani akatia sukari uongo wake, kwa kuongeza ukweli kidogo, kama ilivyo kawaida yake ili kurahisisha kumeza. Aliendelea hivi: “Maana, Mungu anajua kwamba siku mtakayokula matunda yake mtafunguliwa macho na kuwa kama Mungu, wenye kujua mema na mabaya” (Mwanzo 3:5).
Shetani alisema mambo matatu ambayo yalikuwa ya kweli, baada ya kusema uongo. Tunajua kwamba baada ya Adamu na Hawa kula lile tunda, macho yao yalifunguliwa (Mwa. 3:7) kama Shetani alivyokuwa amesema. Tena, Mungu Mwenyewe baadaye alisema kwamba huyo mtu amekuwa kama Mungu na kwamba alikuwa anajua mema na mabaya (Mwanzo 3:22). Angalizo: Shetani huchanganya kweli na uongo mara kwa mara ili kuwadanganya watu.
Ona vile vile kwamba Shetani alikashifu tabia ya Mungu. Mungu hakutaka Adamu na Hawa wale tunda lililokatazwa kwa faida yao na furaha yao, lakini Shetani akaligeuza ikawa kana kwamba Mungu anawaficha kitu kizuri. Sehemu kubwa ya uongo wa Shetani humkashifu Mungu kuhusu tabia Yake, nia Yake na makusudi Yake.
Bahati mbaya ni kwamba wanandoa wa kwanza duniani walikataa ukweli ili waamini uongo, nao wakapatikana na matokeo ya hilo. Lakini, ona vipengele vyote vya vita ya kiroho ya kisasa katika kisa chao: Silaha pekee ya Shetani ilikuwa uongo, uliochanganywa na ukweli. Wanadamu hao walikabiliwa na uchaguzi kati ya kuamini kilichosemwa na Mungu au kilichosemwa na Shetani. Kuamini ukweli ingekuwa “ngao ya imani” kwao, lakini wao hawakuichukua wala kuishika.
Vita Ya Kiroho Ya Yesu
Tunaposoma juu ya mapambano ya Yesu na Shetani wakati wa kujaribiwa Kwake huko nyikani tunapata kuona upesi kwamba Shetani hajabadilisha mbinu zake kwa miaka elfu nyingi. Njia yake ya kushambulia ilikuwa kukashifu alichosema Mungu, naye alijua njia pekee adui ni kumwondoa kwenye kuamini au kutii kweli ya Mungu. Hapa tena, kiini cha mapambano ni Neno la Mungu. Shetani akatupa uongo wake, na Yesu akausukumia pembeni kwa ukweli. Yesu aliamini na kutii yale ambayo Mungu alikuwa amesema. Hiyo ndiyo vita ya kiroho kulingana na Biblia.
Yesu alikabiliwa na hali kama ya Hawa, Adamu na sisi wengine wote. Ilibidi aamue kama atamsikia Mungu au Shetani. Yesu alipigana vita Yake ya kiroho kwa “upanga wa Roho” ambao ni Neno la Mungu. Hebu tuone tunachoweza kujifunza kutokana na mapambano ya kiroho na Shetani.
Akisimulia jaribu la pili la Yesu, Mathayo anasema hivi:
Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; na mikononi mwao watakuchukua; usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako (Mathayo 4:5-7).
Hapo tena jambo kuu lilikuwa Mungu kasema nini. Shetani alikariri mpaka maandiko ya Zaburi ya tisini na moja, lakini aliyageuza ili kuyafanya yamaanishe kitu tofauti na maana ya Mungu.
Yesu akajibu kwa kutaja andiko lingine lililofanya ahadi ya Mungu kuhusu ulinzi katika Zaburi 91 ieleweke vizuri. Mungu atatulinda, ila, hatafanya hivyo tukitenda kwa ujinga, – yaani, “kumtia majaribuni”.
Ndiyo sababu ni muhimu sana kwamba hatuondoi mistari ya Biblia katika mantiki yake. Kila andiko lazima lilinganishwe na kinachosemwa na Maandiko mengine.
Kupindua Maandiko ni mbinu ya kawaida kabisa ya Shetani katika vita ya kiroho, na inasikitisha kwamba amefanikiwa sana kuwapata Wakristo wengi walionaswa katika kundi la vita ya kiroho ya kisasa kwa njia hiyo. Mfano mzuri wa hilo ni jinsi alivyopindua neno la KiBiblia kabisa – “kuangusha ngome” – ili kuunga mkono dhana ya kuwaangusha mapepo kutoka katika anga. Kama tulivyokwisha ona mapema, maneno hayo, yakisomwa katika mantiki yake, hayahusiani na kuangusha mapepo katika anga hata kidogo. Ila, Shetani angependa sana tudhani hivyo, ili tupoteze muda wetu tukipiga kelele dhidi ya falme na mamlaka angani.
Tunasoma hivi katika maelezo ya Mathayo kuhusu jaribu la tatu la Yesu,
Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake (Mathayo 4:8-10).
Hilo lilikuwa jaribu la kupata uwezo. Kama Yesu angemwabudu Shetani, na kama Shetani angetimiza ahadi yake, Yesu angepata umakamu katika ufalme wa giza. Angetawala juu ya kila mwanadamu ambaye hajaokoka, na juu ya mapepo wote, na angekuwa na mamlaka duniani kote, sawa tu na Shetani alivyokuwa nayo. Ni kitu kisichofikirika kwamba nini kingetokea, kama Yesu angekubali jaribu hilo.
Ona tena hapa kwamba Yesu alipingana na mawazo ya Shetani kwa Neno la Mungu lililoandikwa. Katika kila jaribu kati ya majaribu yale matatu, Yesu alishinda kwa kusema hivi: “Imeandikwa.” Sisi pia, lazima tulijue Neno la Mungu na kuliamini, kama tunataka kuepuka kudanganywa na kutumbukia katika mitego ya Shetani. Hayo ndiyo mambo ya vita ya kiroho.
Uwanja Wa Vita
Kwa sehemu kubwa ni kwamba, nguvu pekee Shetani na pepo zake waliyo nayo ni uwezo wa kupanda mawazo katika mioyo na akili za watu (na hata katika hilo wamewekewa mipaka na Mungu – ona 1Wakor. 10:13). Hebu basi tutazame Maandiko machache, yafuatayo:
Petro akasema, Anania! Kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? (Matendo 5:3. Maneno mepesi kukazia).
Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti … (Yohana 13:2. Maneno mepesi kukazia).
Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani … (1 Timo. 4:1. Maneno mepesi kukazia).
Lakini nachelea, kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo (2Wakor. 11:3. Maneno mepesi kukazia).
Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:5. Maneno mepesi kukazia).
Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nalituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida (1Wathes. 3:5. Maneno mepesi kukazia).
…ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazuikie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu (2Wakor. 4:4. Maneno mepesi kukazia).
Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye (Ufunuo 12:9. Maneno mepesi kukazia).
Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za baba yenbu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo (Yohana 8:44. Maneno mepesi kukazia).
Maandiko hayo na mengine yanaweka wazi kabisa kwamba uwanja wa vita wa msingi katika vita ya kiroho KiBiblia ni mioyo yetu na akili zetu. Shetani hutushambulia kwa mawazo – ushauri mwovu, mawazo mabaya, misimamo ya uongo, majaribu, udanganyifu mbalimbali na kadhalika. Njia pekee yetu ya kujilinda ni kujua, kuamini na kutenda kulingana na Neno la Mungu.
Ni muhimu sana sana uelewe kwamba kila wazo unalowaza halitoki ndani yako. Shetani ana wasemaji wengi sana wanaomsaidia kupanda mawazo yake katika akili za watu. Anafanya kazi ya kutushawishi kwa njia ya magazeti, vitabu, televisheni, majarida, redio, marafiki na majirani, na hata kupitia wahubiri. Hata mtume Petro kuna wakati alitumiwa kama msemaji wa Shetani bila kujua, akimshauri Yesu kwamba haukuwa mpango wa Mungu Kwake afe msalabani (ona Mathayo 16:23).
Ila, Shetani na pepo wachafu hufanya kazi ya kushambulia mawazo na akili za binadamu moja kwa moja, bila ya kutumia mwanadamu mwingine, na Wakristo wote watakutana na hali hiyo wakati fulani. Hapo ndipo vita huanza.
Namkumbuka mwanamke mmoja Mkristo – mpendwa sana – aliyekuja kwangu kutubu tatizo alilokuwa nalo. Yeye alisema kwamba kila anapoingia katika sala, alijikuta anawaza mawazo ya kufuru na maneno ya kulaani. Alikuwa mama mpole, mwema, mkarimu, muungwana, mzuri sana na aliyejitoa katika wanawake wote kanisani, lakini alikuwa na tatizo hilo la mawazo mabaya.
Nilimweleza kwamba hayo mawazo mabaya si yake, bali alikuwa anashambuliwa na Shetani, aliyekuwa anataka kumharibia uombaji wake. Ndipo akaniambia kwamba ameacha kuomba kwa sababu alikuwa anaogopa sana kwamba atawaza mawazo hayo mabaya. Shetani akawa amefanikiwa.
Nikamwambia ni vizuri aanze kuomba tena, na mawazo hayo ya kufuru yakimjia, ayapinge kwa ukweli kutoka Neno la Mungu. Wazo likimjia kwamba, “Yesu alikuwa ——,” yeye alipinge kwa kusema, “Hapana! Yesu alikuwa na bado ni Mwana wa Mungu.” Wazo likimjia ambalo ni neno la kufuru, alibadilishe kwa kuwaza sifa kwa Yesu, na kadhalika.
Nikamwambia vile vile kwamba kwa kuogopa kwamba atawaza makosa, alikuwa anayakaribisha, maana hofu ni imani kinyume – ni kumwamini Shetani. Kwa kujaribu kutowaza kitu, inabidi tukiwaze ili tuache kukiwaza (asomaye na afahamu!)
Kwa mfano: Nikikwambia, “Acha kufikiri kuhusu mkono wake wa kuume,” mara moja utaanza kufikiri juu yake unapojaribu kunitii. Kadiri utakavyojitahidi kutowaza, ndivyo utakavyozidi kuwaza. Njia pekee ya kutowaza juu ya mkono wako wa kuume ni kuamua kufikiri juu ya kitu kingine, kama, viatu vyako. Ukisha fikiri kuhusu viatu vyako, hutafikiri juu ya mkono wako.
Nilimtia moyo yule mama “asiogope”, kama Biblia inavyotuagiza. Na kila alipotambua wazo kinyume na Neno la Mungu, nilimshauri alibadilishe na lingine lililokubaliana na Neno la Mungu.
Nafurahi kusema kwamba alifuata ushauri wangu, na ingawa alishambuliwa mara kadhaa tena katika vipindi vya maombi, alipata ushindi kamili juu ya tatizo lake. Aliweza kushinda vita ya kiroho.
Vile vile nilishangaa kugundua baada ya kufanya utafiti katika makanisa kadha kwamba tatizo lake lilikuwa kawaida ya wengi. Zaidi ya nusu ya Wakristo ambao niliwahoji wanaonyesha kwamba wakati mmoja au mwingine wamewahi kuwa na mawazo ya kufuru wakati wakiomba. Shetani hagundui mbinu mpya – anatumia zile zile.
“Jihadhari Unasikiliza Nini”
Hatuwezi kumzuia Shetani na pepo wabaya kushambulia akili na mawazo yetu, lakini si lazima turuhusu mawazo yao yawe mawazo yetu. Yaani – hatupaswi kufikiri mawazo ya kipepo na ushauri wao, na kuyafanya yawe yetu. Kama inavyosemekana, “Huwezi kuwazuia ndege kuruka juu ya kichwa chako, lakini unaweza kuwazuia wasijenge kiota katika nywele zako.”
Tena – tuwe makini tusiruhusu akili zetu kupata ushawishi mwovu kila tunapoweza. Tunapoketi mbele ya televisheni kwa saa nzima, au kusoma gazeti, tunakuwa tumetoa nafasi kwa akili zetu kushawishiwa na kuingiwa na mawazo ya kishetani. Mara tu baada ya kusimulia mfano wa mpanzi na mbegu, Yesu alitoa onyo lifuatalo: “Angalieni msikialo” (Marko 4:24). Yesu alijua matokeo mabaya ya kusikiliza uongo – ya kumruhusu Shetani apande “mbegu” zake katika mioyo na akili zetu. Mbegu hizo zinaweza kukua na kuwa “miiba na michongoma” ambayo mwishoni italisonga Neno la Mungu katika maisha yetu (ona Marko 4:7, 18, 19).
Asemavyo Petro Kuhusu Vita Ya Kiroho
Mtume Petro alielewa vita ya kiroho ya kweli, kulingana na Biblia. Hakuna popote katika nyaraka zake anapowashauri Wakristo waangushe ngome za falme na mamlaka katika miji. Ila, aliwashauri wakabiliane na mashambulizi ya Shetani katika maisha yao binafsi, na aliwaambia jinsi ya kufanya hivyo.
Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani (1Petro 5:8-9).
Ona kitu cha kwanza anacho-onyesha Petro ni kwamba sisi kazi yetu ni kujilinda, si kushambulia. Shetani ndiye mwenye kuzunguka-zunguka, siyo sisi. Yeye ndiye anayetutafuta, sisi hatumtafuti. Kazi yetu si kushambulia, bali ni kupinga mashambulizi, au kuyakabili.
Pili: Ona kwamba Shetani, kama simba, anatafuta wa kummeza. Anawezaje kumeza Wakristo? Je, Petro alimaanisha kwamba Shetani anaweza kula nyama yao, sawa na simba? Sivyo hata kidogo. Njia pekee ya Shetani kummeza Mkristo ni kwa kumdanganya kuamini uongo ambao utaharibu imani yake.
Tatu – ona kwamba Petro anatuambia tumpinge Shetani kwa kupitia imani yetu. Mapambano yetu si vita ya mwili, na hatuwezi kupigana na Shetani kwa kutumia ngumi zetu kupiga hewani. Yeye hutushambulia kwa uongo, nasi tunapinga uongo huo kwa kusimama imara katika imani yetu kwenye Neno la Mungu. Hiyo tena ndiyo vita ya kiroho kulingana na Maandiko.
Wakristo ambao Petro aliwaandikia walikuwa wanapitia mateso makali mno, na walikuwa katika jaribu kubwa la kuikana imani yao. Mara nyingi tunapokuwa katikati ya mazingira magumu, Shetani hushambulia kwa mashaka yake na uongo wake. Huo ndiyo wakati wa kusimama imara katika imani yako. Hiyo ndiyo “siku ya uovu” ambayo Paulo aliandika habari zake, unapohitaji “kuvaa silaha zote za Mungu, ili uweze kusimama imara kinyume cha hila za Shetani” (Waefeso 6:11. Maneno mepesi kukazia).
Asemavyo Yakobo Kuhusu Vita Ya Kiroho
Mtume Yakobo pia alisema kitu juu ya vita ya kiroho katika waraka wake. Je, aliwaambia Wakristo kwamba sala zao zingeamua matokeo ya vita za malaika? Hapana. Je, aliwaambia waangushe pepo wa ashiki, kutokujali na ulevi walio juu ya miji yao? Hapana. Je, aliwaambia wajifunze historia ya miji yao ili waweze kujua aina za pepo waliokuwepo tangu mwanzo wa mji? Hapana!
Yakobo aliamini kuhusu vita ya kiroho kulingana na Maandiko. Basi, aliandika kama ifuatavyo:
Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia (Yakobo 4:7. Maneno mepesi kukazia).
Hapo tena ona kwamba nafasi ya Mkristo ni kujilinda – tunapaswa kupinga, si kushambulia. Tukifanya hivyo, Yakobo anatuahidi kwamba Shetani atakimbia. Hana sababu ya kukaa karibu na Mkristo ambaye hatashawishiwa kuamini uongo wake, wala kufuata ushauri wake, au kukubaliana na majaribu yake.
Vile vile ona kwamba Yakobo kwanza anashauri tumtii au kumyenyekea Mungu. Tunafanya hayo kwa kulitii Neno Lake. Kumpinga kwetu Shetani kumejengwa kwenye kulitii na kulinyenyekea Neno la Mungu.
Asemavyo Yohana Kuhusu Vita Ya Kiroho
Hata mtume Yohana aliandika kuhusu vita ya kiroho katika waraka wake wa kwanza. Je, alituambia tupande juu ili kuangusha ngome za Shetani? Hapana. Je, alituambia tutoe pepo wa hasira kutoka kwa Wakristo ambao hukasirika mara kwa mara? Hapana!
Badala yake, Yohana – sawa na Petro na Yakobo – aliamini katika vita ya kiroho kulingana na Maandiko. Basi, ushauri wake unafanana na wenzake, hivi:
Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani. Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeyealiye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia. Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu (1Yohana 4:1-6).
Ona kwamba hoja nzima ya Yohana katika mistari hii inahusu uongo wa Shetani na kweli ya Mungu. Tunapaswa kuzipima roho ili tuone kama zinatoka kwa Mungu, na kipimo kimejengwa kwenye kweli. Pepo hawatakiri kwamba Yesu Kristo alikuja katika mwili. Wao ni waongo.
Pia, Yohana alituambia kwamba tunapaswa kuwashinda pepo wachafu. Yaani, kama raia wa ufalme wa nuru, hatuko chini ya utawala wao tena. Aliye mkuu zaidi – Yesu – anakaa ndani yetu. Watu walio na Kristo ndani yao hawapaswi kuogopa pepo.
Tena Yohana akasema kwamba dunia huwasikiliza pepo wabaya, kitu kinacho-onyesha kwamba pepo bila shaka huzungumza. Tunajua hawazungumzi kwa sauti, lakini wanapanda uongo ndani ya mawazo ya watu.
Kama wafuasi wa Kristo, hatupaswi kusikiliza uongo wa mapepo. Yohana anasema kwamba wale wanaomjua Mungu wanatusikiliza sisi, kwa sababu tunayo kweli. Tunalo Neno la Mungu.
Hapa tena ona kwamba mkakati wa Shetani ni kuwashawishi watu kuamini uongo wake. Shetani hawezi kutushinda kama tunajua na kuiamini kweli. Vita ya kiroho kulingana na Maandiko iko hivyo.
Ufunguo Ni Imani
Kulijua Neno la Mungu tu hakutoshi kushinda vita ya kiroho. Siri ni kuamini kweli na kwa dhati kile ambacho Mungu amesema. Hiyo ni kweli katika kumpinga Shetani na kukemea pepo. Kwa mfano: Hebu tazama tena mfano ambao tumekwisha utazama mapema, wakati Yesu alipowapa wanafunzi Wake kumi na mbili “mamlaka juu ya pepo wabaya, kwamba wawatoe” (Mathayo 10:1). Sura saba baadaye, tunawakuta wakiwa wameshindwa kutoa pepo katika mtoto aliyekuwa na kifafa.[7] Yesu aliposikia juu ya kushindwa kwao, alisikitika sana na kusema hivi:
Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? (Mathayo 17:17. Maneno mepesi kukazia).
Yesu alisikitishwa na kutokuamini kwao. Tena, baadaye wakati wanafunzi Wake walipomwuliza sababu ya wao kushindwa kumtoa huyo pepo, Yesu aliwajibu hivi: “Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu” (17:20). Basi tunaona kwamba mamlaka yao ya kutoa pepo hayakufanya kazi bila ya imani yao.
Kufaulu kwetu katika kutoa pepo na kumpinga Shetani kunategemeana na imani yetu katika Neno la Mungu. Kama kweli tunaamini alichosema Mungu, basi tutazungumza hivyo na kutenda kulingana na hivyo. Mbwa huwafukuza watu wanaowakimbia. Shetani naye yuko hivyo hivyo. Ukikimbia, Shetani atakukimbiza. Ukisimama thabiti katika imani yako, yeye ndiye atakukimbia (ona Yakobo 4:7).
Bila shaka kutokuwa na imani kwa mitume kungedhihirka kwa kila mtazamaji, walipojaribu bila kufanikiwa kutoa pepo katika yule mtoto. Kama pepo huyo alifanya vituko vile vile alivyofanya mbele za Yesu – kumwangusha mtoto chini “akitetemeka sana” (Luka 9:42) na kumfanya atoke povu mdomoni (Marko 9:20), yawezekana imani ya wanafunzi iligeuka kuwa hofu. Bila shaka walipigwa na butwaa kwa mambo waliyokuwa wanaona.
Ila, mtu mwenye imani, hatishwi na mambo anayoyaona, bali anaguswa na kile ambacho Mungu amesema. “Maana tunaenenda kwa imani, si kwa kuona” (2Wakor. 5:7. Maneno mepesi kukazia). Mungu hawezi kudanganya (ona Tito 1:2). Hivyo basi, hata kama mazingira yetu yataonekana kama yenye kuwa kinyume na kile ambacho Mungu amesema, tunapaswa kusimama imara katika imani.
Ona kwamba Yesu alimweka huru yule mtoto katika muda mfupi sana. Alifanya hivyo kwa imani. Yeye hakupoteza wakati “akikemea.” Walio na imani na mamlaka waliyopewa na Mungu hawana haja ya kutumia masaa wakitoa pepo.
Tena – hakuna taarifa kwamba Yesu alimpigia kelele yule pepo. Wenye imani hawana haja ya kupiga kelele. Wala Yesu hakumwamuru huyo pepo kumtoka kwa kurudia-rudia. Amri moja tu ilitosha. Amri ya pili ingekuwa kukiri mashaka.
Hitimisho
Mtumishi mwenye kufanya wengine kuwa wanafunzi hufundisha vita ya kiroho kulingana na Maandiko kwa mfano wake mwenyewe na kwa maneno yake. Kusudi ni ili wanafunzi wake waweze kusimama imara dhidi ya mbinu za Shetani na kuenenda katika kutii maagizo ya Kristo. Hawaongozi wanafunzi wake kufuata “kila upepo wa mafundisho” ya kisasa yenye kuendeleza njia zisizo za Biblia za vita ya kiroho, maana anajua kwamba wale wanaozitumia na kuzifuata wamepotoka kimtazamo, na ukweli ni kwamba wamedanganywa na huyo huyo Shetani wanayedai kwamba wanapambana naye kwa ushindi na kumweza.
[1] Tofauti katika kanuni hii ni matukio ambapo wahusika wamepagawa mno na mapepo kiasi cha kwamba hawana njia ya kujieleza kwamba wanapenda kufunguliwa. Kwa hali hiyo, karama maalum za Roho lazima zitumike ili kuleta ukombozi, na hizo karama hutenda kazi kama Roho apendavyo Mwenyewe.
[2] Hata maelezo ya Paulo kuhusu wasioamini katika Warumi 1:18-32 yanaunga mkono hoja hii.
[3] Ila – ni kweli kwamba katika maeneo fulani kijiografia, kuna kuzidiana wingi kwa watu wa falme hizo.
[4] Wale wanaosema “ukiisha okoka, umeokoka milele” bila shaka watapinga. Hebu wasome Warumi 11:22; 1Wakor. 15:1, 2; Wafilipi 3:18, 19; Wakolosai 1:21-23 na Waebrania 3:12-14. Kila wanapokuta neno “kama”, wazingatie kinachofuata au kinachotangulia hapo!
[5] “Pepo wa wivu” anayetajwa katika Hesabu 5:14-30 na “roho ya kutakabari” katika Mithali 16:18 ni mifano mizuri ya neno roho kutumika kuelezea hali fulani ya moyo ya kudumu, badala ya kusema juu ya pepo halisi. Tunasoma katika Hesabu 14:24 kwamba Kalebu alikuwa na “roho tofauti”, ambayo bila shaka maana yake ni hali njema ya moyo wa Kalebu.
[6] Hii haimaanishi kwamba watoto hawateseki kwa sababu ya dhambi za wazazi wao – wanateseka. Ila, wanapoteseka, si ishara kwamba Mungu anawaadhibu watoto hao kwa dhambi za wazazi wao. Ni ishara kwamba watu ni waovu kiasi kwamba wanatenda dhambi fulani ambazo wanajua zitawaletea watoto wao shida. Ni wazi pia kutoka Maandiko kwamba Mungu – kwa huruma Zake – aweza kuzuia hukumu kwa mtu mmoja na baadaye akaimimina juu ya mzao afuataye, mwovu zaidi au anayestahili zaidi. Vivyo hivyo, anaweza kuzuia hukumu Yake juu ya kizazi kiovu, na kuimimina juu ya kizazi kingine kinachofuata ambacho ni kiovu zaidi au chenye kustahili (ona Yeremia 16:11, 12). Hiyo ni tofauti na kumwadhibu mtu kwa ajili ya dhambi za babu zake!
[7] Tuwe makini – tusidhani kila tukio la kifafa linatokana na pepo kuwa ndani ya mtu.