Familia Ya Kikristo

Sura Ya Ishirini Na Moja

 

Ni dhahiri kwamba Mungu ndiye aliyeleta wazo la familia. Basi, ni halali kutazamia kwamba atatupa maelekezo jinsi familia zinavyotakiwa kuishi na kutuonya juu ya matatizo yanayoweza kuangamiza au kuharibu familia. Bwana ametupa kanuni nyingi sana katika Neno Lake kuhusu jinsi familia inavyotakiwa kuwa, na wajibu wa kila mshirika katika familia. Maagizo hayo ya KiBiblia yanapofuatwa, familia zitapata baraka zote ambazo Mungu alikusudia wazifurahie. Zinapovunjwa, matokeo yake ni maumivu makali moyoni, na vurugu.

Nafasi Ya Mume Na Mke

Mungu amepanga kwamba familia ya Kikristo iwe katika mfumo fulani. Kwa sababu mfumo huo unaleta uthabiti katika maisha ya familia, Shetani hufanya kazi sana kupotosha mpango aliokusudia Mungu.

Kwanza kabisa ni kwamba, Mungu amepanga mume awe kichwa cha familia. Hii haimpi mume ruhusa ya kutawala mke wake na watoto katika ubinafsi. Mungu amewaita waume kupenda, kulinda, kutimiza mahitaji na kuongoza familia zao kama kichwa. Pia, Mungu alikusudia wake wawe watiifu kwa uongozi wa waume zao. Hili ni wazi, kama Maandiko yanavyosema.

Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo (Waefeso 5:22-24).

Mume si kichwa wa mkewe kiroho – Yesu ndiye mwenye nafasi hiyo. Yesu ni kichwa wa kanisa kiroho, na mke wa Kikristo ni mshirika wa kanisa sawa na mume wake ambaye ni Mkristo pia. Ila, katika familia, mume Mkristo ndiye kichwa wa mke wake na watoto, nao wanapaswa kutii na kunyenyekea mamlaka yake hayo aliyopewa na Mungu.

Je, mke anapaswa kumtii mumewe kwa kiwango gani? Kama Paulo anavyosema, ni katika kila jambo. Wakati pekee anaporuhusiwa kuvunja sheria hiyo ni kama mume wake anamtaka kuvunja Neno la Mungu au kufanya kitu ambacho kinapinganana dhamiri yake. Ni wazi kwamba hakuna mume Mkristo atakayemtaka mke wake kufanya chochote kinachovunja Neno la Mungu au kwenda kinyume na dhamiri yake. Mume si Bwana kwa mkewe – Yesu tu ndiye mwenye nafasi hiyo maishani mwake. Kama itafikia uchaguzi kuhusu nani wa kumtii, anapaswa kuchagua kumtii Yesu.

Waume wanapaswa kukumbuka kwamba Mungu hayuko upande wao mara zote. Kuna wakati ambapo Mungu alimwambia Ibrahimu afanye kama alivyoambiwa na Sara mkewe (ona Mwanzo 21:10-12). Maandiko pia yanataja jinsi Abigaili alivyoacha kumtii Nabali mumewe, aliyekuwa mpumbavu, na kwa kufanya hivyo aliepusha tatizo (ona 1Samweli 25:2 – 38).

Neno La Mungu Kwa Waume

Mungu anawaambia hivi waume:

Enyi waume, wapendeni wake zetu kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake… Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe, maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. … Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe (Waefeso 5:25, 28-30, 33).

Waume wanaagizwa kuwapenda wake zao kama Kristo anavyolipenda Kanisa. Si wajibu mdogo huo! Mke yeyote atajinyenyekeza kwa furaha kabisa kwa mtu anayempenda kama Yesu – aliyetoa uhai Wake kwa sababu ya upendo wa kujitoa. Sawa na jinsi Kristo anavyoupenda mwili Wake – yaani Kanisa – ndivyo na waume wanavyotakiwa kumpenda mwanamke ambaye ni “mwili mmoja” nao (Waefeso 5:31). Kama mume Mkristo anampenda mkewe kama anavyopaswa, atamtimizia mahitaji yake, atamtunza, atamheshimu, atamsaidia, atamtia moyo, na atatumia muda kuwa naye. Akishindwa katika wajibu wake kumpenda mkewe, mume huyo yuko hatarini kuzuia majibu ya maombi yake mwenyewe.

Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe (1Petro 3:7. Maneno mepesi kukazia).

Kihalisi ni kwamba hapajawahi kuwepo na ndoa isiyokuwa na kutokuelewana na shida mbalimbali. Ila, kwa kujitoa na kukuza tunda la Roho katika maisha yetu, waume na wake wanaweza kujifunza kuishi kwa maelewano na amani, na kufikia mahali pa kutambua baraka zinazozidi kuongezeka za ndoa ya Kikristo. Kila mwenzi anaweza kukua na kufikia ukomavu mkubwa katika kufanana na Kristo kutokana na matatizo yasiyoepukika yanayotokea katika ndoa zote.

Kwa maelezo zaidi juu ya wajibu na majukumu ya waume na wake, tazama Mwanzo 2:15-25; Mithali 19:13; 21:9, 19; 27:15, 16; 31:10-31; 1Wakor. 11:3; 13:1-8; Wakolosai 3:18, 19; 1Timo. 3:4, 5; Tito 2:3-5; 1Petro 3:1-7.

Tendo La Ndoa

Mungu ndiye mwanzilishi wa tendo la ndoa, na ni dhahiri kwamba aliliumba ili kustarehesha na kusaidia katika uumbaji. Pamoja na hayo, Biblia inatamka wazi kwamba tendo la ndoa ni la kufurahiwa na wale walioungana pamoja katika agano la ndoa, la kudumu.

Kukutana kimwili nje ya mipaka ya ndoa huitwa zinaa au uasherati. Mtume Paulo alisema kwamba wale watendao mambo kama hayo hawataurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-11). Ingawa Mkristo anaweza kujaribiwa na pengine kufikia kuanguka katika tendo la uzinzi au uasherati, atajisikia hatia kubwa sana rohoni mwake, itakayompelekea kutubu.

Paulo pia alitoa mafundisho wazi kabisa kuhusu majukumu ya mume na mke kwa mwenzake, kuhusu tendo la ndoa.

Lakini kwa sababu ya zinaa, kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe. Vivyo hivyo, mume hana amari juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu (1Wakor. 7:2-5).

Mistari hii inaweka wazi kabisa kwamba tendo la ndoa lisitumiwe kama “zawadi” na mume au mke, maana hakuna mwenye mamlaka juuya mwili wake mwenyewe.

Tena, tendo la ndoa ni zawadi kutoka kwa Mungu. Si dhambi wala najisi inapokuwa katika ndoa. Paulo aliwatia moyo Wakristo wenye ndoa kushirikiana kimwili. Tena, tunapata ushauri huu kwa waume Wakristo katika kitabu cha Mithali:

Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake ytakutoshe siku zote; na kwa upendo wake ushangilie daima (Mithali 5:18, 19).[1]

Kama wanandoa Wakristo wanataka kufurahia mahusiano kimwili yenye kutosheleza, waume na wake wanahitaji kuelewa kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya wanaume na wanawake kwa habari ya kushirikiana kimwili. Kiasili, mwanamume ni mtu wa kimwili sana kwa habari ya kukutana kimwili. Asili ya mwanamke kwa habari ya kukutana kimwili ni kitu cha hisia. Wanaume husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke kwa kuona tu (ona Mathayo 5:28). Wanawake wao husisimka na kuwa tayari kukutana kimwili kwa mahusiano ya karibu sana, na kwa kuguswa na kushikwa-shikwa (ona 1Wakor. 7:1). Wanaume huvutiwa na wanawake wanaowapendeza macho; ila wanawake huvutiwa na wanaume wanaowapendeza kwa sababu zaidi ya kuvutia kimwili. Hivyo, wanawake wenye busara hupendeza ili kuwavutia waume zao wakati wote. Na waume wenye hekima huonyesha upendo wao kwa wake zao kutwa nzima kwa kuwakumbatia na kuwatendea mambo ya ukarimu, badala ya kuwatazamia wake zao “kuwa tayari” kwa ghafula wakati wa usiku.

Kiwango cha ashiki ya mwanamume kukutana kimwili na mwenzake huongezeka kulingana na kuongezeka kwa mbegu za uzazi katika mwili wake. Kiwango cha ashiki ya mwanamke huongezeka au kupungua kutegemeana na siku zake za mwezi. Wanaume wana uwezo wa kusisimka na kuwa tayari kukutana kimwili na mwanamke, na kufikia kilele cha tendo la ndoa baada ya muda mfupi sana – nukta chache tu au dakika, ila wanawake huchukua muda mrefu. Ingawa mwanamume yuko tayari kimwili kukutana na mwanamke upesi sana, mwili wa mwanamke unaweza usiwe tayari, mpaka baada ya nusu saa au zaidi. Basi, waume wenye hekima huchukua muda katika kuanza kuwasisimua wenzao kwa kuwapapasa, kuwabusu na kuwashika-shika sehemu za mwili ambazo zinasisimua, ili kumsababisha mwanamke kuwa tayari kukutana kimwili. Ikiwa hajui sehemu zinazohusika, amwulize. Tena, anapaswa kujua kwamba, japo yeye anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara moja tu, mwenzake anaweza kufikia kilele cha tendo la ndoa mara nyingi. Mume anapaswa kuhakikisha kwamba mwenzake anapokea anachotaka.

Ni muhimu sana kwa waume Wakristo na wake zao kuzungumza kuhusu mahitaji yao kwa uwazi, na kujifunza juu ya tofauti zao kiasi wanachoweza. Mahusiano kimwili kati ya waume na wake yanaweza kuwa baraka inayozidi kuongezeka kutokana na mawasiliano ya miezi mingi na miaka, na kugunduana na kuzoeana.

Watoto Wa Familia Ya Kikristo

Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kunyenyekea na kutii kabisa wazazi wao Wakristo. Wakifanya hivyo, wameahidiwa maisha marefu na baraka zao.

Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso 6:1-3).

Akina baba Wakristo kama vichwa wa familia zao, wanapewa wajibu wa msingi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivi:

Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana (Waefeso 6:4).

Ona kwamba wajibu wa baba ni wa namna mbili: kuwalea watoto wake katika adabu na maonyo ya Bwana. Hebu tuanze kwa kutazama haja ya kuwafundisha watoto adabu.

Nidhamu Ya Watoto

Mtoto asiyetiwa nidhamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa mbinafsi na muasi kwa mamlaka. Watoto wanapaswa kutiwa nidhamu wakati wowote wanapoacha kwa makusudi kutii sheria halali zilizowekwa na wazazi wao. Watoto wasiadhibiwe kwa makosa au kutowajibika kwa sababu ya utoto. Lakini, watakiwe kukabiliana na matokeo ya makosa yao na kutowajibika kwao, na kwa njia hiyo kuwasaidia kujiandaa kwa ajili ya uhalisi wa maisha ya utu uzima.

Watoto wadogo wanapaswa kuadhibiwa kwa kiboko, kama Neno la Mungu linavyofundisha. Lakini watoto wachanga wasipigwe viboko. Hii haina maana kwamba watoto wachanga waruhusiwe kufanya wanachotaka. Inatakiwa tangu wanapozaliwa wajue kwamba mama na baba ndiyo wenye mamlaka. Wanaweza kufundishwa wakiwa wadogo sana maana ya neno “hapana” kuwakuwakataza tu kufanya kitu wanachofanya, au wanachotaka kufanya. Wakianza kuelewa maana ya neno “hapana”, wanaweza kuchapwa kofi dogo tu matakoni ili kuwasaidia kuelewa vizuri zaidi wanapoendelea kufanya kile ambacho wazazi wanasema kisifanywe. Kama hayo yatafanyika kwa utaratibu na mara kwa mara, watoto watajifunza kuwa watiifu tangu umri mdogo sana.

Pia, wazazi wanaweza kuonyesha mamlaka yao kwa kutounga mkono tabia zisizotakiwa za watoto wao. Mfano ni kuwapa mara moja kitu wanachotaka, wakilia. Kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto walie ili wapate matakwa yao. Au, kama wazazi watakubaliana na madai ya watoto wao kila mara wanaponuna au kukasirika ni kwamba wanawatia moyo kuendelea na tabia hiyo isiyotakiwa. Wazazi wenye hekima huunga mkono tabia nzuri tu katika watoto wao.

Kuchapa kiboko kusilete madhara kimwili, ila kusababishe maumivu ya kutosha kumfanya mtoto yule asiyetii kulia kwa muda kidogo. Kwa njia hiyo, mtoto atajifunza kuunganisha uchungu na kutokutii. Hata Biblia inaunga mkono hilo.

Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; bali yeye ampendaye humrudi mapema. … Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. … Usimnyime mtoto wako mapigo; maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, na kumwokoa nafasi yake na Kuzimu. … Fimbo na maonyo hutia hekima; bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye (Mithali 13:24; 22:15; 23:13-14; 29:15).

Wazazi wanaposimamia sheria zao, hawana haja ya kuwatisha watoto ili kuwafanya watii Mtoto anapoacha kutii kwa makusudi, achapwe fimbo. Ikiwa mzazi atatishia tu kumchapa mtoto wake ambaye si mtii, anachofanya ni kuunga mkono uasi wa mtoto wake. Matokeo ni kwamba mtoto anajifunza kutokujali utii mpaka vitisho vya wazazi wake vya maneno vinapofikia kiwango fulani cha sauti.

Baada ya kiboko, mtoto anapaswa kukumbatiwa na kuhakikishiwa upendo wa mzazi aliyemchapa.

Mlee Mtoto

Wazazi Wakristo wanapaswa kutambua kwamba wana wajibu wa kuwafundisha na kuwalea watoto wao, kama tunavyosoma katika Mithali 22:6, kwamba: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee” (maneno mepesi kukazia).

Kulea (au kufundisha) si kuadhibu tu mtoto anapoacha kutii, bali ni kumpongeza pia wakati anapofanya vizuri. Watoto kila wakati wanahitaji kusifiwa na wazazi wao ili kuunga mkono tabia zao njema, na mambo mazuri wanayofanya. Watoto wanahitaji kuhakikishiwa mara kwa mara kwamba wanapenda, wanakubalika na kufurahiwa na wazazi wao. Wazazi wanaweza kuonyesha upendo wao kwa kusifu, kuwakumbatia na kuwabusu watoto, na kwa kutumia muda mwingi nao.

“Kulea” maana yake “kufanya atii.” Basi, wazazi Wakristo wasiwape watoto wao uchaguzi kama watakwenda kanisani au kuomba kila siku au hapana. Watoto hawana ufahamu wa kutosha kujua kinachowafaa, au kilicho bora. Ndiyo sababu Mungu aliwapa wazazi. Wazazi watakaofanya bidii na kuweka juhudi na nguvu zao kuhakikisha kwamba watoto wao wanalelewa vizuri, wana ahadi kutoka kwa Mungu kwamba watoto wao hawataacha njia iliyo sawa hata wakiwa wakubwa, kama tulivyosoma katika Mithali 22:6.

Pia, watoto wanapaswa kuongezewa majukumu wanavyozidi kukua. Lengo la mzazi mwenye kufanikiwa ni kumwandaa mtoto hatua kwa hatua ili kuwajibika kabisa akiwa mtu mzima. Mtoto anapozidi kukua, apewe uhuru zaidi wa kujiamulia mambo yake mwenyewe. Tena, yule kijana mkubwa anapaswa kuelewa kwamba daima akubali wajibu utokanao na maamuzi yake, na kwamba wazazi wake hawatakuwepo siku zote “kumwokoa” katika matatizo.

Wajibu Wa Wazazi Kufundisha

Kama tusomavyo katika Waefeso 6:4, akina baba si tu kwamba wanawajibika kuwafundisha adabu watoto wao, bali pia wanatazamiwa kuwafundisha katika Bwana. Si wajibu wa kanisa kumpa mtoto mafundisho kuhusu maadili ya KiBiblia, tabia za Kikristo au theolojia – ni kazi ya baba. Wazazi wanaoachia wajibu wote kwa mwalimu wa Shule ya Jumapili awafundishe watoto wao kuhusu Mungu wanakosea sana. Mungu aliwaamuru Waisraeli hivi, kwa njia ya Musa:

Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo (Kumbu. 6:6, 7. Maneno mepesi kukazia).

Wazazi Wakristo wawafundishe watoto wao kuhusu Mungu tangu wakiwa wadogo, wakiwaambia Yeye ni nani na anawapenda kiasi gani. Watoto wadogo wafundishe habari za kuzaliwa kwa Yesu, maisha Yake, kifo na kufufuka Kwake. Watoto wengi wanaweza kuelewa ujumbe wa Injili wanapokuwa na umri wa miaka mitano au sita, na wanaweza kufanya uamuzi wa kumfuata Kristo. Baada ya hivyo (wakiwa na miaka sita au saba, na wakati mwingine hata wakiwa wadogo zaidi), wanaweza kupokea ubatizo wa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha kama ishara kwamba wamejazwa. Pamoja na hayo, hatuwezi kuweka sheria kuhusu jambo hili kwa sababu kila mtoto yuko tofauti. Ila hoja ni kwamba, wazazi Wakristo wanapaswa kutoa nafasi ya kwanza kwenye kuwafundisha watoto wao mambo ya kiroho.

Amri Kumi Za Kuwapenda Watoto Wako

1). Usiwatie watoto wako mahali pagumu (ona Waefeso 6:4). Watoto wasitazamiwe kutenda kama watu wazima. Ukitazamia mengi kupita kiasi kutoka kwa watoto wako, wataacha kujitahidi kukupendeza maana wanajua haiwezekani.

2). Usilinganishe watoto wako na watoto wengine. Wajulishe jinsi unavyofurahia sifa zao za kipekee na karama au vipaji vyao kutoka kwa Mungu. Wakubali wao kama wao.

3). Wape majukumu nyumbani, ili wajue kwamba wao ni sehemu muhimu sana ya familia hiyo. Kufanikiwa ni matofali yanayojenga kujiamini katika maisha ya mtu.

4). Tumia muda kuwa na watoto wako. Hiyo inawajulisha kwamba wao ni wa maana kwako. Kuwapa vitu haichukui nafasi ya wewe kujitoa kwao. Tena, watoto hushawishiwa zaidi na wale wanaokaa nao muda mwingi.

5). Ikibidi useme kitu kibaya, jaribu kukisema kwa uzuri. Mimi sikuwahi kuwaambia watoto wangu kwamba ni “wabaya” walipoacha kunitii. Badala yake, nilikuwa namwambia hivi kijana wangu, “Wewe ni mtoto mzuri, na watoto wazuri hawafanyi ulichofanya!” (Kisha nilikuwa namchapa kiboko.)

6). Tambua kwamba, neno “hapana” linamaanisha “ninakujali”. Watoto wanaporuhusiwa mambo yao kila wakati wanatambua kwama hujali kiasi cha kutosha kuwakataza chochote wakati wowote.

7). Tazamia watoto wako kukuiga wewe. Watoto hujifunza kwa mifano ya wazazi wao. Mzazi mwenye busara hawezi kumwambia mtoto wake, “Fanya ninavyokwambia. Usifanye kama ninavyofanya mimi.”

8). Usiwaokoe watoto wako na matatizo yao yote. Ondoa mawe yanayoweza kuwakwaza tu; acha mawe ya kukanyagia yabakie mbele yao.

9). Mtumikie (na kumfuata) Mungu kwa moyo wako wote. Nimeona kwamba watoto wa wazazi waliopoa kiroho huwa hawamfuati Mungu wakiwa watu wazima. Watoto Wakristo wa wazazi ambao hawajaokoka, na watoto wa wazazi Wakristo waliojitoa kabisa kwa Mungu huendelea na wokovu hata “wakiondoka kwenye kiota” – nyumbani.

10). Wafundishe watoto wako Neno la Mungu. Mara nyingi wazazi hutoa nafasi ya kwanza kwa elimu ya watoto wao, na kushindwa kuwapa elimu ya muhimu zaidi wanayoweza kupata – elimu ya Biblia.

Nafasi Ya Huduma, Ndoa Na Familia

Pengine kosa kubwa la kawaida kabisa lifanywalo na viongozi wa Kikristo ni kutokujali ndoa zao na familia zao kwa sababu ya kujitoa kwenye huduma. Wanajihesabia haki kwa kusema kwamba kujitoa kwao “ni kwa ajili ya kazi ya Bwana.”

Kosa hili hurekebika wakati mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anapotambua kwamba utii wake halisi na kujitoa kwake kwa Mungu huonekana kwa mahusiano yake na mke wake na watoto. Mtumishi hawezi kudai kwamba amejitoa kwa Mungu ikiwa hampendi mke wake kama Kristo anavyolipenda kanisa, au kama atapuuzia kutumia muda unaotakiwa na watoto wake, ili kuwalea na kuwakuza katika kicho na kumcha Bwana.

Tena, kumpuuza mwenzi na watoto kwa sababu ya “huduma” ni ishara ya huduma ya kimwili kabisa, inayofanywa kwa nguvu za mtu binafsi. Wachungaji wengi wenye makanisa wanaobeba mizigo mizito ni mfano wa hili, maana wanajichosha ili kuhakikisha kwamba kila utaratibu wa kanisa unakwenda vizuri.

Yesu aliahidi kwamba mzigo Wake ni mwepesi na nira Yake ni laini (ona Mathayo 11:30). Hamwiti mtumishi yeyote kuonyesha anavyopenda dunia au anavyolipenda kanisa kwa kutowapenda watu wa familia yake. Sifa mojawapo ya mzee ni kwamba, “awe mwenye kuisimamia nyumba yake vema” (1Timo. 3:4). Mahusiano yake na familia yake ni kipimo cha uwezo wake kufanya huduma.

Wale walioitwa kufanya huduma za kusafiri na ambao inawabidi kuwa nje ya nyumbani mara kwa mara lazima watumie muda wa ziada kufikiri kuhusu familia zao wanapokuwa nyumbani. Washirika wengine katika mwili wa Kristo wafanye kinachowezekana ili kufanikisha hilo. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anatambua kwamba watoto wake mwenyewe ndiyo wanafunzi wake wa kwanza. Akishindwa hapo, hana haki ya kujaribu kuwafundisha wengine walio nje ya nyumbani mwake kuwa wanafunzi.


[1] Mungu anazungumzia mambo waziwazi. Hebu tazama Wimbo Ulio Bora 7:1-9 na Walawi 18:1-23.

Sifa Na Kuabudu

Sura Ya Ishirini

 

Yule mwanamke akamwambia [Yesu], ‘Bwana, naona ya kuwa u nabii. Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.’ Yesu akamwambia, ‘Mama, unisadiki. Saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu. … Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana, Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli’ (Yohana 4:19-24).

Maneno hayo kutoka kinywa cha Yesu yanaweka msingi wa sisi kuelewa juu ya mambo muhimu sana katika kuabudu. Yeye alizungumzia juu ya “waabuduo halisi” na kueleza sifa zao. Hii huonyeha kwamba wapo watu wanaoabudu, lakini si waabuduji wa kweli. Wanaweza kudhani kwamba wanamwabudu Mungu lakini ukweli si hivyo maana hawatimizi masharti Yake.

Yesu alitangaza alama za waabuduji wa kweli – wao huabudu “katika roho na kweli.” Basi, kinyume chake ni kwamba, waabuduji wasio wa kweli ni wale wenye kuabudu “katika mwili na uongo. Kimwili, waabuduji wasio wa kweli wanawea kufanya matendo yote ya kuabudu, lakini ni maonyesho tu maana hayatoki katika moyo unaompenda Mungu.

Ibada ya kweli kwa Mungu inatoka katika moyo unaompenda Mungu tu. Basi, kuabudu si kitu tunachofanya wakati tunapokutanika kanisani, bali ni kitu tunachofanya kila dakika ya maisha yetu, tunapotii amri za Kristo. Inashangaza kwamba yule mwanamke aliyekuwa anazungumza na Yesu alikuwa ameolewa mara tano, na wakati huo alikuwa anaishi na mwanamume, na bado alitaka kuhojiana na Yesu kuhusu mahali panapofaa kumwabudu Mungu! Yeye ni mfano wa watu wengi sana wenye dini, wanaohudhuria ibada huku wakiishi maisha yao kila siku katika kumwasi Mungu. Hao si waabuduji wa kweli.

Wakati fulani Yesu aliwakemea Mafarisayo na waandishi kwa sababu ya ibada yao ya uongo, isiyotoka moyoni.

Enyi wanafiki! Ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu’ (Mathayo 15:7-9. Maneno mepesi kukazia).

Ingawa Wayahudi na Wasamaria katika siku za Yesu walitilia mkazo sana kuhusu mahali pa watu kuabudia, Yesu alisema kwamba mahali hapakuwa na maana sana. Cha muhimu ni hali ya moyo wa kila mtu, na jinsi anavyomheshimu Mungu. Hayo ndiyo yanaamua jinsi ibada yake ilivyo.

“Ibada” nyingi katika makanisa siku hizi ni taratibu tu zilizokufa, zinazotendwa na waabuduji waliokufa pia. Watu wanarudia maneno ya mtu mwingine kuhusu Mungu, bila hata kuyafikiri, wanapoimba “nyimbo za kuabudu.” Kuabudu kwao ni bure, maana maisha yao yanaonyesha kilicho halisi katika mioyo yao.

Mungu angetamani hata kuambiwa “Nakupenda” rahisi tu itokayo moyoni kutoka kwa mtoto wake mmoja mtiifu, kuliko kuvumilia kelele zisizotoka moyoni za maelfu ya Wakristo wa Jumapili asubuhi, wakiimba “Jinsi Wewe Ulivyo Mkuu.”

Kuabudu Katika Roho

Kuna wanaosema kwamba kuabudu “katika Roho” ni kuomba na kuimba kwa lugha zingine. Hiyo ni tafsiri ngumu kukubali, ukitazama maneno ya Yesu. Yeye alsiema kwamba “saa inakuja, na sasa ipo, ambayo waabuduji wa kweli watamwabudu Baba katika roho na kweli,” kuonyesha kwamba tayari walikuwepo watu waliotimiza masharti ya kuabudu “katika Roho” alipotoa tamko hilo. Ni kweli kwamba hakuna yeyote aliyenena kwa lugha mpaka Siku ya Pentekoste. Basi, aaminiye yeyote, awe ananena kwa lugha au hapana, anaweza kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Kuomba na kuimba kwa lugha zingine hakika huwa ni msaada kwa mwabuduji katika kuabudu kwake, lakini hata kunena kwa lugha kunaweza kuwa utaratibu usiotoka moyoni.

Picha ya kusisimua kuhusu ibada ya kanisa la kwanza inapatikmana katika Matendo 13:1, 2.

Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanya Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, ‘Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia’ (Maneno mepesi kukazia).

Ona fungu hili linavyosema: “walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada.” Basi tunajifunza hapo kwamba ibada ya kweli humhudumia Bwana. Ila, ni hivyo wakati Bwana anapokuwa ndiyo lengo la upendo wetu.

Njia Za Kuabudu

Kitabu cha Zaburi ambacho tunaweza kusema ni kitabu cha nyimbo cha Israeli, kinatushauri kumwabudu Mungu katika njia nyingi tofauti tofauti. Kwa mfano: Katika Zaburi ya 32 tunasoma hivi:

Pigeni vigelegele vya furaha; ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo (Zaburi 32:11b. Maneno mepesi kukazia).

Japo kuabudu kimya, kwa utaratibu na heshima kuna nafasi yake, pia kuna nafasi ya kupiga kelele za shangwe.

Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni BWANA kwa kinubi, kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa. Mwimbieni wimbo mpya, pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe (Zaburi 33:1-3. Maneno mepesi kukazia).

Tunapaswa kumwimbia Bwana katika kuabudu, lakini kuimba kwetu kuwa kwa furaha, ambalo ni onyesho lingine la nje kuhusu undani wa moyo wa mtu. Pia tunaweza kuimba kwa furaha tukitumia vyombo mbalimbali vya muziki. Ila, katika mikutano mingi ya kanisa, vyombo vya muziki vinakuwa na sauti ya juu kiasi cha kwamba vinafunika kabisa sauti ya uumbaji. Ni vizuri vipunguzwe sauti au vizimwe. Ukisoma zaburi, tatizo hilo halikuwepo!

Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai. Kwa jina Lako nitaiinua mikono yangu (Zaburi 63:4. Maneno mepesi kukazia).

Tunaweza kuinua mikono yetu juu kwa Mungu kama ishara ya kujitolea Kwake na kumheshimu.

Mpigie Mungu kelele za shangwe nchi yote; imbeni utukufu wa jina lake; tukuzeni sifa zake. Mwambieni Mungu, ‘Matendo Yako yatisha kama nini! Kwa ajili ya wingi wa nguvu zako, adui zako watakuja kunyenyekea mbele zako. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia, naam, italiimbia jina lako’ (Zaburi 66:1-4. Maneno mepesi kukazia).

Tunatakiwa kumwambia Bwana jinsi alivyo mkuu na kumsifu kwa jinsi alivyo wa ajabu. Zaburi ni mahali pazuri sana pa kupa ta maneno yafaayo ya kumsifu Mungu. Tunahitaji kwenda zaidi ya kurudia rudia maneno haya: “Nakusifu, Bwana!” Kuna mengi sana ya kumwambia.

Njooni tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba (Zaburi 95:6).

Hata jinsi tulivyo ni onyesho la ibada: iwe ni kusimama, kupiga magoti au kusujudu.

Watauwa na waushangilie utukufu, waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao (Zaburi 149:5. Maneno mepesi kukazia).

Si lazima tuwe tumesimama au kupiga magoti ili kuabudu – tunaweza hata kuwa tumelala kitandani.

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru, nyuani mwake kwa kusifu. Mshukuruni, lihimidini jina lake (Zaburi 100:4. Maneno mepesi kukazia).

Hakika, kushukuru kuwe sehemu ya kuabudu kwetu.

Na walisifu jina lake kwa kucheza (Zaburi 149:3. Maneno mepesi kukazia).

Tunaweza hata kumsifu Bwana kwa kucheza. Lakini kucheza kwenyewe kusiwe kwa kimwili, kwenye kuamsha ashiki, au kwa ajili ya kustarehesha watu.

Msifuni kwa mvumo wa baragumu; msifuni kwa kinanda na kinubi. Msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi. Msifuni kwa matoazi yaliayo; msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya (Zaburi 150:3-6).

Mungu ashukuriwe kwa walio na vipawa vya muziki. Vipawa vyao vinaweza kutumika kumtukuza Mungu kama watavipiga kwa moyo wa upendo.

Nyimbo Za Kiroho

Mwimbieni BWANA wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu (Zaburi 98:1a. Maneno mepesi kukazia).

Hakuna kosa lolote kuimba wimbo wa zamani, mpaka inapokuwa mazoea. Hapo ndipo tunahitaji wimbo mpya utokao mioyoni mwetu. Katika Agano Jipya, tunajifunza kwamba Roho Mtakatifu atatusaidia kutunga nyimbo mpya. Tunaambiwa hivi:

Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu (Wakolosai 3:16).

Tena msilewe kwa mvinyo ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo (Waefeso 5:18-20).

Paulo aliandika kwamba tunapaswa kuwa tunaimbiana “zaburi, na tenzi na nyimbo za rohoni”. Basi, hizo tatu zina tofauti. Uchunguzi wa lugha ya Kiyunani hautoi msaada wowote, ila pengine “zaburi” maana yake ni kuimba zaburi kama zilivyo katika Biblia, pamoja na vyombo. Pengine “tenzi” ni nyimbo mbalimbali za shukrani zilizokuwa zimetungwa na waamini katika makanisa. “Nyimbo za rohoni” labda zilikuwa nyimbo za papo kwa papo kutoka kwa Roho Mtakatifu, ambazo ni sawa na ile karama ya unabii, ila, zenyewe ziliimbwa.

Kusifu na kuabudu vinapaswa kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku – si kitu fulani tunachofanya wakati wa kukutanika kanisani. Mchana kutwa tunaweza kumhudumia Bwana na kufanikiwa kujisikia ushirika wa karibu na Yeye.

Sifa Ni Imani Ikitenda Kazi

Kusifu na kuabudu ni madhihirisho ya kawaida kabisa ya imani yetu kwa Mungu. Kama kweli tunaamini ahadi za Neno la Mungu, basi tutakuwa watu wenye furaha, waliojaa sifa kwa Mungu. Yoshua na Waisraeli walitakiwa kupiga kelele kwanza, ndipo kuta zikaanguka. Biblia inatushauri hivi: “Furahini katika Bwana sikuzote” (Wafilipi 4:4), na “Shukuruni kwa kila jambo” (1Wathes. 5:18a).

Mfano mmoja wa hali ya juu sana kuhusu nguvu za sifa unapatikana katika 2Nyakati sura ya 20, wakati taifa la Yuda lilipovamiwa na majeshi ya Moabu na Amoni. Akijibu maombi ya Mfalme Yehoshafati, Mungu aliwaagiza Israeli hivi:

Msiogope wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao … Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu (2Nyakati 20:15b – 17).

Kisa kinaendelea, hivi:

Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama akasema, ‘Nisikieni enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.’ Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana (2Nyakati 20:20-25. Maneno mepesi kukazia).

Sifa iliyojaa imani huleta kulindwa na husababisha utoaji wa Mungu!

Kwa maelezo zaidi kuhusu mada hiyo ya nguvu za sifa, ona Wafilipi 4:6-7 (sifa huleta amani), 2Nyakati 5:1-14 (sifa huleta uwepo wa Mungu), Matendo 13:1, 2 (sifa hudhihirisha makusudi na mipango ya Mungu), na Matendo 16:22-26 (sifa huleta kuhifadhiwa na Mungu, na kufunguliwa kutoka gerezani).

Karama Za Kufanya Huduma

 

Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo … Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo (Waefeso 4:7, 11-13. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha (1Wakor. 12:28. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Karama za huduma kama zinavyojulikana, ni tendo la kuitwa kwa waamini fulani na kupewa uwezo ili kusimama katika nafasi kama mtume, nabii, mwinjilisti, mchungaji au mwalimu. Hakuna mtu awezaye kujiweka katika nafasi hizo. Ni lazima mtu aitwe na apewe karama hiyo na Mungu.

Inawezekana kwa mtu mmoja kushika nafasi zaidi ya moja kati ya hizo, lakini ni kwa makundi fulani fulani. Kwa mfano: Inawezekana mwamini mmoja akaitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwalimu, au nabii na mawalimu. Lakini si rahisi kwa mtu kuitwa kushika nafasi ya mchungaji na mwinjilisti kwa sababu, huduma ya mchungaji inadai kwamba abaki mahali pamoja akihudumia kusanyiko la mahali pamoja. Hivyo, asingeweza kutimiza wito wa uinjilisti ambao unadai mtu kusafiri mara kwa mara.

Japo hizo nafasi tano zote ni karama tofauti kwa makusudi tofauti, zimetolewa kwa kanisa kwa kusudi moja kubwa la jumla – kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kazi ya huduma” (Waefeso 4:12, TLR).[1] Lengo la kila mtumishi linapaswa kuwa kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma. Lakini, mara nyingi, wale walio katika huduma hujifanya kana kwamba wameitwa kuwastarehesha watu wa kimwili wanaofika kanisani – si kuwawezesha watakatifu kuwa tayari kwa huduma. Kila mtua liyeitwa katika nafasi mojawapo kati ya hizo zilizotajwa anapaswa kutathmini mara kwa mara mchango anaotoa kwa habari ya “kuwawezesha watakatifu kwa ajili ya kufanya huduma”. Kama kila mtumishi angefanya hivyo, wengi wangeondoa shughuli nyingi mbalimbali ambazo zinahesabiwa kwa sasa kwamba ni “huduma”.

Je, Karama Zingine Za Huduma Zilikuwa Kwa Ajili Ya Kanisa La Mwanzo Tu?

Je, karama hizi za huduma zitatolewa kwa kanisa kwa muda gani? Yesu atatizoa kwa muda wote ambapo watakatifu Wake wanahitaji kuwezeshwa kufanya huduma. Hiyo ni mpaka atakaporudi. Kila mara kanisa linapokea Wakristo waliozaliwa upya wanaohitaji kukua, na sisi wengine tunahitaji kuendelea kukua na kukomaa kiroho daima.

Kwa bahati mbaya, kuna wengine ambao wamedhani kwamba kuna aina mbili tu ya huduma siku hizi – wachungaji na wainjilisti – kana kwamba Mungu amebadilisha mpango Wake. Hapana! Bado tunahitaji mitume, manabii na waalimu, kama kanisa la mwanzo lilivyohitaji. Sababu ya kutokuona mifano ya karama hizi katika kanisa kwa wingi duniani ni kwamba, Yesu ndiye anayetoa karama hizo kwa Kanisa Lake, si hli kanisa la siku hizi la bandia, lisilokuwa takatifu, lenye kuhubiri injili za uongo. Katika kanisa hili bandia utawapata wale wanaojitahidi – kwa unyonge sana – kujaza nafasi za baadhi ya karama za huduma (sana sana wachungaji na wainjilisti wachache tu), lakini hawafanani hata kidogo na zile karama za huduma ambazo zinatolewa na Mungu, ambazo Yesu hutoa kwa kanisa Lake. Tena, hawawawezeshi watakatifu kufanya matendo ya huduma, kwa sababu injili yenyewe wanayotangaza haileti utakatifu bali huwadanganya watu wafikiri tu kwamba wamesamehewa. Na hao watu hawana haja ya kuwezeshwa wafanye huduma. Hawana nia ya kujikana wenyewe na kuibeba misalaba yao.

Utajuaje Kwamba Umeitwa?

Mtu anajuaje kwamba ameitwa kushika mojawapo ya nafasi hizo kanisani? Kwanza kabisa, atasikia mwito kutoka kwa Mungu. Atajikuta ana mzigo wa kutenda kazi fulani. Hii ni zaidi ya kuwa na haja ya kuona hitaji ambalo linaweza kutimizwa. Badala yake, ni njaa itokayo kwa Mungu, iliyoko ndani, yenye kumsukuma mtu kuingia katika huduma fulani. Kama kweli ameitwa na Mungu, hatatosheka mpaka aanze kutimiza wito wake. Wala haihusiani na watu kumchagua au kamati ya watu. Mungu ndiye anayeita.

Pili – Mtu aliyeitwa kweli atajikuta amewezeshwa na Mungu ili kutimiza kazi hiyo aliyopewa na Mungu. Kila nafasi katika zile tano ina upako wake wa KiMungu, wenye kumwezesha mhusika kufanya kile ambacho Mungu amemwita kufanya. Upako huja pamoja na mwito wenyewe. Kama hakuna upako, hakuna mwito. Mtu anaweza kutamani kufanya kazi katika huduma fulani, akaenda Shule ya Biblia kwa miaka minne kujifunza na kujiandaa kwa ajili ya huduma hiyo, lakini pasipo upako toka kwa Mungu, hana nafasi ya kufanikiwa.

Tatu – Ataona Mungu akifungua mlango au nafasi kwa ajili ya kufanyia kazi karama zake hizo. Kwa hali hiyo anaweza kujithibitisha kuwa mwaminifu, na hatimaye atapewa nafasi kubwa zaidi, majukumu makubwa zaidi na karama zaidi.

Kama mtu hajasikia mwito wa Mungu au msukumo wa ndani kuhusiana na mojawpao ya hizo karama tano za huduma, au kama hajisikii upako maalum wa aina yoyote ile ili kutekeleza kazi itolewayo na Mungu, au kama hakuna nafasi iliyojitokeza kutumia karama anayofikiri anayo, basi asijaribu kuwa kitu ambacho Mungu hajamwita kuwa. Badala yake, afanye bidii kuwa baraka katika kusanyiko lake, katika mahali anapokaa na kazini anakofanya. Hata ingawa hajaitwa kwenye “huduma tano” hizo, ameitwa kutumika kwa kufanyia kazi zile karama ambazo Mungu amempa, na anatakiwa ajithibitishe kuwa ni mwaminifu.

Ingawa Maandiko yanataja hizo karama tano za huduma, hii haimaanishi kwamba kila mtu anayeshika nafasi fulani atakuwa na huduma inayofanana na mwingine. Paulo aliandika kwamba kuna “tofauti za huduma” (1Wakor. 12:5), akionyesha uwezekano wa kutofautiana kati ya watumishi wanaoshikilia nafasi zinazofanana. Tena, inaonekana kuna viwango mbalimbali vya upako juu ya hao wanaoshikilia nafasi hizo. Basi, tunaweza kutofautisha kila nafasi kwa kiwango cha upako. Kw amfano: Kuna waalimu ambao wanaonekana kuwa na upako zaidi kuliko wengine. Ndivyo ilivyo hata katika karama zingine za huduma. Mimi ninaamini kwamba mtumishi yeyote anaweza kufanya mambo yatakayosababisha ongezeko la upako juu ya huduma yake, kama kuwa mwaminifu na kujitolea sana kwa Mungu.

Tutazame Kwa Karibu Nafasi Ya Mtume

Neno la Kiyunani linalotafsiriwa mtume ni apostolos na maana yake halisi ni “aliyetumwa”. Mtume wa kweli wa Agano Jipya ni mwamini anayetumwa na Mungu kwenda mahali fulani au maeneo fulani ili kuanzisha makanisa. Anaweka msingi wa kiroho wa “jengo” la Mungu, na anafananishwa na fundi ujenzi mkandarasi. Paulo, yeye mwenyewe akiwa mtume, aliandika hivi:

Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu. Ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi kama mkuu wa wajenzi wenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake (1Wakor. 3:9-10a. Maneno mepesi kutilia mkazo).

“Mkuu wa wajenzi” husimamia mpango mzima wa kujenga – yeye anaona jengo lililokamilika. Si mtaalamu kama vile fundi seremala au mwashi. Anaweza kuwa na uwezo wa kufanya kazi ya fundi seremala au mwashi, lakini pengine hataifanya vizuri kama wao wenyewe. Vivyo hivyo, mtume anao uwezo wa kufanya kazi ya mwinjilisti au mchungaji, lakini kwa muda tu wakati anapoanzisha makanisa. (Mtume Paulo kwa kawaida alikuwa anakaa mahali kwa miezi sita hadi miaka mitatu.)

Mtume anafaa sana kuanzisha makanisa, kisha kuyasimamia ili kuhakikisha yanaendelea kama Mungu anavyotaka. Mtume anawajibika kuweka wazee au wachungaji au wasimamizi ili kuchunga kila kundi analoanzisha (ona Matendo 14:21-23; Tito 1:5).

Mitume Wa Kweli Na Wa Uongo

Inaonekana kwamba baadhi ya watumishi siku hizi, kwa kutamani kuwa na madaraka juu ya makanisa, ni wepesi kujitangaza kwamba wameitwa kuwa mitume. Lakini wengi wao wana matatizo makubwa. Kwa kuwa hawajaanzisha makanisa (au labda wana moja au mawili) na hawana karama wala upako wa kiBiblia wa utume, inawabidi watafute wachungaji wepesi kudanganyika watakaowaruhusu wao kuwa na mamlaka juu ya makanisa yao. Kama wewe ni mchungaji, usidanganywe na hao mitume wa uongo wenye kujitukuza wenyewe na wenye njaa ya mamlaka. Wao kwa kawaida ni mbwa mwitu waliovaa mavazi ya kondoo. Mara nyingi wanachotafuta ni fedha tu. Maandiko yanaonya kuhusu mitume wa uongo (ona 2Wakor. 11:13; Ufunuo 2:2). Kama inabidi wakwambie wao ni mitume, basi ni ishara kwamba wao si mitume. Matunda yao yanapaswa kuzungumza.

Mchungaji anayeanzisha kanisa na kuendelea kulichunga kama mchungaji kwa miaka mingi si mtume. Pengine wachungaji aina hiyo wanaweza kuitwa “wachungaji wa kitume” kwa kuwa walianzisha makanisa wenyewe. Pamoja na hayo, wasishike nafasi ya mtume kwa sababu mtume huendelea kuanzisha makanisa.

“Mishenari” aliyetumwa kweli na Mungu na kutiwa mafuta – ambalo ndilo jina la mitume siku hizi – mwenye wito wa kuanzisha makanisa, anaweza kusimama kama mtume. Lakini, wamishenari wanaofanya kazi ya kuanzisha shule za Biblia au kuwafundisha wachungaji si mitume bali waalimu.

Huduma ya kweli ya mtume huonekana kwa ishara na maajabu, ambavyo ni vyombo vinavyosaidia kuanzisha kanisa. Paulo aliandika hivi:

Kwa sababu sikuwa duni ya mtume walio wakuu kwa lolote, nijapokuwa si kitu. Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza (2Wakor. 12:11b-12).

Kama mtu hana ishara na maajabu katika huduma yake, yeye si mtume. Basi, mitume wa kweli si wengi, na hawapatikani katika kanisa bandia, lisilo takatifu, lenye kuhubiri injili bandia. Sana sana wanapatikana katika maeneo mapya kabisa duniani ambayo hajapata Injili bado.

Cheo Cha Juu Cha Mtume

Katika orodha zote za karama za huduma katika Agano Jipya, nafasi ya mtume hutajwa kwanza, kuonyesha kwamba ndiyo wito wa hali ya juu zaidi (ona Waefeso 4:11; 1Wakor. 12:28).

Hakuna mtu aanzaye huduma yake kama mtume. Mtu anaweza kuwa na wito wa mtume, lakini hataanza katika nafasi hiyo. Ni lazima kwanza ajithibitishe kuwa mwaminifu kwa miaka mingi katika kuhubiri na kufundisha, kisha hatimaye atasimama katika nafasi ambayo Mungu amemwandalia. Paulo aliitwa kuwa mtume toka tumboni mwa mama yake, lakini alifanya huduma kwa miaka mingi kabla ya kuingia katika nafasi hiyo hatimaye (ona Wagalatia 1:15 – 2:1). Alianza kama mwalimu na nabii (ona Matendo 13:1-2), ndipo baadaye akapandishwa cheo na kuwa mtume, wakati alipotumwa na Roho Mtakatifu (ona Matendo 14:14).

Tunaona wengine wakitajwa kama mitume licha ya Paulo na wale Thenashara, katika Matendo 1:15-26; 14:14; Warumi 16:7; 2Wakor. 8:23; Wagalatia 1:17-19; Wafilipi 2:25 na 1Wathes. 1:1 na 2:6. (Neno mtenda kazi katika 2Wakor. 8:23 na Wafilipi 2:25 katika Kiyunani ni apostolos.) Hii hupingana na dhana iliyoko siku hizi kwamba nafasi ya mtume ilikuwa kwa ajili ya watu kumi na mbili tu.

Ila, ni mitume kumi na mbili tu wanaoweza kuhesabiwa kuwa “Mitume wa Mwanakondoo,” na ni hao kumi na mbili tu ndiyo watakaokuwa na nafasi ya pekee katika utawala wa Kristo wa miaka elfu moja (tazama Mathayo 19:28; Ufunuo 21:14). Hatuhitaji tena mitume kama Petro, Yakobo na Yohana ambao walivuviwa kipekee ili kuandika Maandiko, kwa sababu ufunuo wa Biblia umekamilika. Ila, sku hizi bado tunahitaji mitume watakaoanzisha makanisa kwa nguvu za Roho Mtakatifu, kama walivyofanya akina Paulo na wengine, kulingana na tunavyosoma katika Kitabu cha Matendo ya Mitume.

Nafasi Ya Nabii

Nabii ni mtu anayepokea mafunuo ya Mungu na kusema kwa upako wa Mungu. Kwa kawaida, anatumiwa mara kwa mara katika karama ya kiroho ya unabii pamoja na zile karama za ufunuo: neno la hekima, neno la maarifa, na kupambanua roho.

Mwamini yeyote anaweza kutumiwa na Mungu katika karama ya unabii kama apendavyo Roho, lakini hiyo haimfanyi kuwa nabii. Nabii kwanza kabisa ni mtumishi anayeweza kuhubiri au kufundisha kwa upako. Kwa kuwa nafasi ya nabii inaonekana kuwa mwito wa pili (ona orodha katika 1Wakor. 12:28), hata mtumishi wa kudumu asingeweza kutiwa katika nafasi ya nabii mpaka awe katika huduma kwa miaka kadhaa. Inapofikia wakati wake kushika nafasi hiyo, atakuwa na vitendea kazi vya kiroho vinavyoambatana na nafasi yenyewe.

Watu wawili wanaotajwa katika Agano Jipya kuwa manabii ni Yuda na Sila. Tunasoma katika Matendo 15:32 kwamba walitoa unabii mrefu kwa kanisa la Antiokia, kama ifuatavyo:

Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.

Mfano mwingine wa nabii kutoka katika Agano Jipya ni Agabo. Tunasoma hivi katika Matendo 11:27-28:

Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia. Na tulipokusanyika, akasimama mmoja wao jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.

Ona kwamba Agabo alipewa neno la hekima – kitu kuhusu wakati ujao kilifunuliwa kwake. Agabo hakujua kila kitu ambacho kingetokea katika siku zijazo, ila alifahamu yale tu ambayo Roho Mtakatifu alipenda kumfunulia.

Katika Matendo 21:10-11, kuna mfano mwingine wa neno la hekima kufanya kazi katika huduma ya Agabo. Hapa, ilitokea kwa ajili ya mtu mmoja, Paulo.

Basi, tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia, akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, “Roho Mtakatifu asema hivi, ‘Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa’.”

Je, Maandiko yanaruhusu katika kipindi hiki cha agano jipya kutafuta ushauri binasi kutoka kwa manabii? Hapana. Sababu ni hii: Waamini wote wana Roho Mtakatifu ndani yao ili kuwaongoza. Nabii anachoweza kufanya ni kuthibitisha tu kile ambacho mwamini tayari anajua ni mwongozo wa Mungu katika roho yake. Kwa mfano: Wakati Agabo alipomtabiria Paulo, hakumpa mwongozo kwamba afanye nini. Alithibitisha tu kile ambacho Paulo alikwisha fahamu kwa muda mrefu.

Kama tulivyokwisha kusema mapema, Paulo alishika nafasi ya nabii (na mwalimu) kabla ya kuitwa katika huduma ya utume (ona Matendo 13:1). Tunajua Paulo alipokea mafunuo kutoka kwa Bwana kulingana na Wagalatia 1:11-12, na pia alipata maono mengi tu (ona Matendo 9:1-9; 18:9, 10; 22:17-21; 23:11; 2Wakor. 12:1-4).

Kama ilivyo kwa habari ya mitume wa kweli, hatupati manabii wa kweli katika kanisa la uongo. Kanisa la uongo huwaepuka manabii wa kweli kama Sila, Yuda au Agabo. Sababu ni kwamba manabii wa kweli wataleta ufunuo wa Mungu kutopendezwa na kutokutii kwao (kama Yohana alivyofanya kwa makanisa mengi ya Asia Ndogo katika sura mbili za kwanza za Ufunuo). Kanisa la uongo halipendi hayo.

Nafasi Ya Mwalimu

Kulingana na orodha ya 1Wakorintho 12:28, nafasi ya mwalimu ni ya tatu. Mwalimu ni mtu ambaye ametiwa mafuta na Mungu kufundisha Neno la Mungu. Si kwamba kila mtu anayefundisha Biblia ni mwalimu kulingana na Agano Jipya. Wengi hufundisha kwa sababu wanajisikia kupenda kufanya hivyo, au wanajisikia kuwajibika kufanya hivyo, lakini mtu ambaye ana wito wa nafasi hiyo ya ualimu hupewa karama na Mungu kwa ajili ya kufundisha. Mara nyingi anapewa ufunuo wa Mungu kuhusu Neno la Mungu, naye anakuwa na uwezo wa kueleza Biblia kwa njia inayofanya ieleweke na kufanyiwa kazi.

Apolo ni mfano wa mtu aliyeshika nafasi hiyo katika Agano Jipya. Paulo alilinganisha huduma yake ya kitume na huduma ya Apolo ya kufundisha katika 1Wakorintho kwa kusema hivi:

Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. … Naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake (1Wakor. 3:6, 10b. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mwalimu Apolo hakupanda wala kuweka msingi. Ila, yeye alitia maji mimea mipya kwa Neno la Mungu, na alijenga kuta kwenye msingi uliokuwepo.

Anatajwa tena katika Matendo 18:27, hivi:

Na [Apolo] alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Ona kwamba Apolo “akawasaidia sana” watu ambao walikuwa Wakristo tayari, na kwamba mafundisho yake yanaelezwa kuwa na nguvu. Mafundisho yenye upako kila wakati yana nguvu.

Huduma ya kufundisha ni ya muhimu sana kwa kanisa kuliko hata matendo ya miujiza au karama za kuponya. Hii ndiyo sababu imeorodheshwa kabla ya karama hizo katika 1Wakorintho 12:28.

Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa (Maneno mepesi kukazia).

Kwa bahati mbaya sana, waaminio wakati mwingine huvutiwa zaidi kuona uponyaji kuliko kusikiliza mafundisho dhahiri ya Neno ambalo litaleta kukua kiroho na utakatifu katika maisha yao.

Biblia inazungumza juu ya kuhubiri na kufundisha. Kufundisha ni kitu cha utaratibu na mpango, ila kuhubiri ni kitu cha uvuvio zaidi. Mara nyingi wainjilisti huhubiri. Waalimu na wachungaji mara nyingi hufundisha. Mitume huhubiri na kufundisha. Ni kitu cha kuhuzunisha kwamba waamini wengine hawatambui thamani ya mafundisho. Wengine hata hufikiri kwamba wakati pekee ambapo msemaji amepokea upako ni wakati wanahubiri kwa sauti kubwa na kwa mwendo wa haraka! Sivyo.

Yesu ni mfano bora kabisa wa mwalimu aliye na upako. Mafundisho Yake yalikuwa na sehemu kubwa sana katika huduma Yake kiasi cha watu wengi kumwita “Mwalimu” (Mathayo 8:19; Marko 5:35; Yohana 11:28).

Kwa maelezo zaidi kuhusu waalimu na kufundisha, ona Matendo 2:42; 5:21, 25, 28, 42; 11:22-26; 13:1; 15:35; 18:11; 20:18-20; 28:30, 31; Warumi 12:6, 7; 1Wakor. 4:17; Wagalatia 6:6; Wakolosai 1:28; 1Timo. 4:11-16; 5:17; 6:2; 2Timo. 1:11; 2:2 na Yakobo 3:1. Andiko la mwisho katika orodha hii linatuambia kwamba waalimu watapata hukumu kali zaidi, kwa hiyo wanapaswa kuwa makini sana kuhusu kitu wanachofundisha. Wanapaswa kufundisha Neno tu.

Nafasi Ya Mwinjilisti

Mwinjilisti ni mtu aliyetiwa mafuta kuhubiri Injili. Jumbe zake zimepangwa kuwaongoza watu watubu na kumwamini Bwana Yesu Kristo. Zinaambatana na miujiza yenye kuvuta usikivu wa wasioamini na kuwafanya kuamini ukweli wa ujumbe wake.

Bila shaka walikuwepo wainjilisti wengi sana katika kanisa la kwanza, lakini ni mtu mmoja tu anayetajwa katika kitabu cha Matendo kama mwinjilisti. Jina lake ni Filipo. Tunasoma hivi: “…Tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake” (Matendo 21:8. Maneno mepesi kukazia).

Filipo alianza huduma yake kama mtumishi tu (au tuseme, “shemasi”) ambaye kazi yake ilikuwa kusimamia meza (ona Matendo 6:1-6). Akapandishwa kufikia nafasi ya mwinjilisti wakati wa mateso ya kanisa yaliyotokana na kuuawa kwa Stefano. Kwa mara ya kwanza alihubiri Injili huko Samaria.

Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule (Matendo 8:5-8).

Ona kwamba ujumbe wa Filipo ulikuwa mmoja tu – Kristo. Lengo lake lilikuwa kuanza kufanya watu kuwa wanafunzi, yaani, wafuasi watiifu wa Kristo. Basi, alimtangaza Kristo kama mtenda miujiza, Mwana wa Mungu, Bwana, Mwokozi na Hakimu anayerudi upesi. Akawashauri watu watubu na kumfuata Bwana wake.

Ona pia kwamba Filipo aliwezeshwa kwa ishara na maajabu, vilivyothibitisha ujumbe wake. Mtu anayesimama katika nafasi ya mwinjilisti atatiwa mafuta kwa karama za kuponya na zingine za kiroho. Kanisa la uongo lina wainjilisti wa uongo ambao wanahubiri injili ya uongo. Dunia imejaa wainjilisti wa namna hiyo, na ni dhahiri kwmaba Mungu hathibitishi mahubiri yao kwa miujiza na uponyaji. Sababu ni kwamba hawahubiri Injili Yake. Hawamhubiri Kristo. Kwa kawaida, wanahubiri kuhusu mahitaji ya watu na jinsi Kristo anavyoweza kuwapa uzima tele, au wanahubiri mfumo wa wokovu ambao hautaki toba. Wanawaongoza watu katika uongofu bandia wenye kupooza hatia yao bila kuwaokoa. Matokeo ya mahubiri yao ni kwamba watu hata hawana nafasi za kuzaliwa mara ya pili, kwa sababu hawaoni haja ya kupokea kitu ambacho wanafikiri wanacho tayari. Wainjilisti aina hiyo wanamsaidia Shetani kujenga ufalme wake.

Nafasi ya mwinjilisti haiko kwenye ile orodha ya karama zingine za huduma katika 1Wakorintho 12:28, kama inavyotajwa katika Waefeso 4:11. Ila, kwa kuwa inatajwa “miujiza na karama za kuponya”, hizo zinahusika na nafasi ya mwinjilisti kwa sababu zilikuwa kawaida katika huduma ya uinjilisti ya Filipo, nazo zinatoa uthibitisho wa Mungu kwenye huduma yoyote ya mwinjilisti.

Wengi wanaotembea kutoka kanisa hadi kanisa na kujiita wainjilisti si wainjilisti kweli kwa sababu wanahubiri katika makanisa, tena kwa Wakristo. Kisha hawana ule uwezo wa karama za kuponya wala miujiza. (Kuna wanaojifanya kuwa na karama hizo, lakini wanawadanganya wajinga tu. Miujiza yao mikubwa ni kuwaangusha watu, tena kwa kuwasukuma.) Hao watumishi wanaosafiri wanaweza kuwa waalimu au wahubiri au wenye kuonya (ona Warumi 12:8), lakini hawako kwenye nafasi ya mwinjilisti. Ila, inawezekana Mungu kuanza huduma ya mtu kwa kumfanya mwonyaji au mhubiri na baadaye kumpandisha hadi nafasi ya mwinjilisti.

Kwa maelezo zaidi kuhusu nafasi ya mwinjilisti, soma Matendo 8:4 – 40, ambayo ni taarifa ya huduma ya Filipo. Ona hapo jinsi karama za huduma zinavyotegemeana na umuhimu wake (hasa mstari wa 14 hadi 25) na jinsi Filipo alivyohubiri Injili kwa watu lakini pia akaongozwa na Mungu kuwahudumia watu binafsi (ona Matendo 8:25-39).

Inaonekana kwamba wainjilisti wameagizwa kuwabatiza waongofu wao, lakini hawajapewa agizo la kutoa ubatizo wa Roho Mtakatifu kwa waamini wapya. Hilo kimsingi ni jukumu la mitume au wachungaji/wazee/waangalizi.

Nafasi Ya Mchungaji

Tumeona katika sura mbili zilizopita mlinganisho kati ya nafasi ya mchungaji KiBiblia na jinsi ilivyo kwa kawaida. Ila, kuna mengine tena ya kusema juu ya huduma ya mchungaji.

Ili kuelewa vizuri kile ambacho Biblia inafundisha kuhusu nafasi ya mchungaji, tunahitaji kuelewa maneno matatu muhimu sana ya Kiyunani. Hayo ni (1) poimen, (2) presbuteros na (3) episkopos. Yanatafsiriwa hivi: (1) mchungaji wa mifugo au mchungaji wa watu, (2) mzee, na (3) mwangalizi au askofu.

Neno poimen linapatikana mara kumi na nane katika Agano Jipya, nalo linatafsiriwa mchungaji wa mifugo mara kumi na saba, na mchungaji wa watu mara moja. Neno lenyewe kama kitendo – poimaino – linapatikana mara kumi na moja, na mara nyingi linatafsiriwa mchungaji wa mifugo.

Neno presbuteros linapatikana mara sitini na sita katika Agano Jipya. Mara sitini limetafsiriwa mzee au wazee.

Neno episkopos linapatikana mara tano katika Agano Jipya, na linatafsiriwa mwangalizi mara nne. Biblia yetu ya Kiswahili inatumia neno askofu.

Hayo maneno yote matatu yanataja nafasi moja katika kanisa, nayo yanatumika kwa kubadilishana. Popote ambapo mtume Paulo alianzisha makanisa, aliweka wazee (presbuteros) ambao waliwaacha kushughulika na makanisa yamahali (ona Matendo 14:23; Tito 1:5). Majukumu yao yalikuwa kusimamia (episkopos) na kuchunga (poimaino) makundi yao. Angalia mfano katika Matendo 20:17, kama ifuatavyo:

Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee [presbuteros] wa kanisa (Maneno mepesi kukazia).

Je, aliwaambia nini hao wazee wa kanisa?

Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi [episkopos] ndani yake, mpate kulilisha [poimaino] kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe (Matendo 20:28. Maneno mepesi kukazia).

Ona jinsi hayo maneno matatu yanavyotumika kwa kubadilishana. Si nafasi tatu tofauti. Paulo aliwaambia wazee kwamba wao ni wasimamizi au waangalizi ambao walipaswa kufanya huduma yao kama wachungaji.

Petro naye aliandika hivi katika waraka wake wa kwanza:

Nawasihi wazee [presbuteros] walio kwenu, mimi niliye mzee mwenzi wao na shahidi wa mateso ya Kristo na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni [poimaino] kundi la Mungu lililo kwenu na kulisimamia, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka (1Petro 5:1-4. Maneno mepesi kukazia).

Petro aliwaambia wazee wawe wachungaji kwa makundi yao. Kitendo hapa kinachotafsiriwa mchungaji kinatumiwa kama jina katika Waefeso 4:11.

Naye [Yesu] alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu (Maneno mepesi kukazia).

Hilo linatufanya tuamini kwamba wazee na wachungaji ni kitu kimoja.

Pia, Paulo alitumia neno mzee (presbuteros) na mwangalizi au askofu (episkopos) kwa kubadilishana, katika Tito 1:5-7.

Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru. … Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshtakiwa neno (Maneno mepesi kukazia).

Hivyo, si rahisi kujenga hoja kwamba nafasi ya mchungaji, mzee na mwangalizi ni tatu tofauti. Basi, chochote kilichoandikwa kuhusu wasimamizi na wazee katika nyaraka za Agano Jipya kinawahusu na wachungaji pia.

Utawala Kanisani

Pia ni dhahiri kabia kutokana na maandiko yaliyotajwa hapo nyuma kwamba, wazee/wachungaji/waangalizi hawajapewa usimamizi wa kiroho tu kwa kanisa, bali pia wamepwa mamlaka ya kutawala. Yaani, wazee/wachungaji/waangalizi ndiyo wasimamizi na wenye mamlaka, na washirika wanapaswa kuwatii.

Watiini wenye kuwaongoza na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu (Waebrania 13:17).

Lakini, hakuna Mkristo anayetakiwa kumtii na kumnyenyekea mchungaji ambaye si mtii wala mnyenyekevu kwa Mungu, bali anapaswa kutambua kwamba hakuna mchungaji aliye mkamilifu.

Wachungaji/wazee/waangalizi wana mamlaka juu ya makanisa yao, sawa na jinsi ambavyo baba ana mamlaka juu ya familia yake.

Basi imempasa askofu [mchungaji/mzee] awe mtu asiyelaumika. … Mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) (1Timo. 3:2-5. Maneno mepesi kukazia).

Paulo akaendelea kusema hivi:

Wazee [wachungaji/waangalizi] watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha (1Timo. 5:17. Maneno mepesi kukazia).

Ni dhahiri kwamba wazee wanapaswa kutawala au kusimamia kanisa.

Wazee Kinyume Na Maandiko

Makanisa mengi yanaamini mpango wao wa utawala ni wa KiBiblia kwa sababu wana kundi la wazee wanaosimamia, lakini, tatizo ni kwamba wazo lao la wazee si sahihi. Wazee wao huchaguliwa kila mara na hubadilishana nafasi kutoka katika kusanyiko. Mara nyingi wanaitwa “Baraza la Wazee.” Lakini watu hao si wazee kulingana na tafsiri ya Biblia. Tukitazama sifa ambazo Paulo anataja kwa ajili ya mtu kuwa mzee, hilo linaonekana wazi kabisa. Paulo aliandika kwamba mzee hushikilia nafasi ya kudumu ya kufundisha na kuhubiri na kusimamia katika kanisa, na kwa maana hiyo analipwa (ona 1Timo. 3:4-5; 5:17-18; Tito 1:9). Katika watu wanaosemekana ni “Baraza la Wazee” kwenye makanisa mengi, ni wachache sana – kama wapo basi – ambao wanatimiza sifa hizo. Hawalipwi; hawahubiri wala kufundisha; si wafanya kazi wa kanisa; na wala hawajui jinsi ya kusimamia au kutawala kanisa.

Utawala wa kanisa ambao si wa kiMaandiko ndiyo sababu ya matatizo mengi sana kanisani kuliko kitu kingine chochote. Wakati watu wasiostahili wanaposimamia kanisa, shida ziko njiani. Mlango hufunguka kwa ajili ya vurugu, faraka na hata kuangamia kabisa kwa kanisa. Mpango wa utawala wa kanisa ambao si kulingana na Maandiko ni kama mkeka wa ukaribisho kwa Shetani.

Natambua kwamba nawaandikia wachungaji wa makanisa jengo na wa makanisa yanayokutanikia nyumbani. Baadhi ya wachungaji wa makanisa jengo wanaweza kuwa wanaongoza makanisa ambayo mfumo wa uongozi si wa kiMaandiko, ambapo wazee huchaguliwa kutoka katika kusanyiko. Mifumo hiyo haiwezi kubadilishwa bila ya kuleta vurugu.

Ushauri wangu kwa wachungaji kama hao ni huu: Fanya vizuri uwezavyo kwa msaada wa Mungu kubadilisha mfumo wa utawala wa kanisa, na uvumilie vurugu za muda zitakazotokea, maana vurugu za kudumu zinazokuja baadaye hazitaweza kuepukika kama hutafanya chochote sasa. Ukifanikiwa kuvumilia vurugu za muda, utajikuta umeepukana na vurugu zote za baadaye. Ukishindwa, anzisha kanisa jipya mahali na kufuata mpango wa Biblia.

Japo hilo linaumiza, mwisho wa siku utazaa matunda mengi zaidi kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Kama wale wanaotawala kanisa lako kwa sasa ni wafuasi wa kweli wa Kristo, unayo nafasi nzuri tu ya kufanikiwa kuwashawishi kubadilisha mfumo, kama utaweza kuwaonyesha kutoka Maandiko kinachopaswa, na jinsi ya kufanya hayo mabadiliko yanayohitajika sana.

Wazee Wengi Je?

Kuna wenye kuonyesha kwamba katika Maandiko wazee hutajwa katika wingi. Hoja hapo ni kwamba kuwa na mzee/mchungaji/mwangalizi mmoja anayesimamia kundi si kimaandiko. Huo si ushahidi wa kutosha kuamua kitu hicho. Kweli Biblia inataja kwamba, katika miji fulani fulani, waliokuwa wanasimamia kanisa walikuwa zaidi ya mzee mmoja, lakini haisemi kwamba hao wazee walikuwa wote wanalingana kimadaraka katika kusanyiko hilo. Kwa mfano: Wakati Paulo alipokusanya wazee kutoka Efeso (Matendo 20:17), ni dhahiri kwamba hao wazee walitoka kwenye mji ambao pengine kanisa lilikuwa na washirika maelfu kwa makumi elfu (ona Matendo 19:19). Basi, yawezekana kulikuwa na makundi mengi katika Efeso, na inawezekana kila mzee mmoja alisimamia kanisa moja.

Katika Maandiko, hakuna mahali popote ambapo Mungu aliita kamati ifanye kazi yoyote. Wakati alipotaka kutoa Waisraeli Misri, alimwita Musa – mtu mmoja – awe kiongozi. Wengine waliitwa kumsaidia Musa, lakini wote walikuwa chini yake kimadaraka, nao kama yeye walikuwa na majukumu binafsi juu ya kundi fulani la watu. Mtindo huo unapatikana katika Maandiko mara kwa mara. Wakati Mungu anapokuwa na kazi, anamwita mtu mmoja kuwajibika, kisha anamwita mwingine kumsaidia huyo.

Basi, haiwezekani kwamba Mungu anaweza kuita kamati ya wazee wenye mamlaka sawa ili kusimamia kila kanisa dogo linalokutania nyumbani, la watu ishirini. Hapo ni kama mwaliko kwa watu kuvurugana!

Lakini – hiyo haimaanishi kwamba kila kanisa la nyumbani lisimamiwe na mtu mmoja tu – mzee mmoja. Ila, maana yake ni kwamba, kama kuna mzee zaidi ya mmoja katika kanisa, yule ambaye ni kijana na asiyekomaa kiroho awe tayari kunyenyekea chini ya yule aliye mkubwa na aliyekomaa kiroho. Kulingana na Maandiko, makanisa ndiyo yanatakiwa kuwa maeneo ya kufundishia wachungaji vijana/wazee/waangalizi – si Shule za Biblia. Basi, inawezekana kabisa na inatakiwa kwamba wawepo wazee/wachungaji/waangalizi kadhaa katika kanisa la mahali, na wale ambao ni wadogo kiroho wafundishwe na wale ambao ni wakubwa kiroho.

Mambo hayo utayaona hata katika makanisa yanayodaiwa kusimamiwa na wazee “wanaolingana”. Yupo mmoja ambaye kila mara anapewa nafasi kubwa na wale wenzake. Au utakuta kuna mmoja ambaye ni kama mkuu, huku wengine wakiwa watazamaji tu. Vinginevyo kutakuwa na vurugu tu. Ni ukweli pia kwamba hata kamati huchagua mtu mmoja kuwa mwenyeketi. Wakati kundi la watu wanaolingana wanapochukua hatua ya kufanya kitu, wanatambua kwamba lazima kuwe na kiongozi mmoja. Ndivyo ilivyo pia kanisani.

Tena, Paulo analinganisha majukumu ya wazee na majukumu ya baba katika 1Timotheo 3:4, 5. Wazee lazima wasimamia nyumba zao, la sivyo hawafai kusimamia kanisa. Lakini tujiulize: Nyumba yenye baba wawili wenye mamlaka sawa itasimamiwaje? Bila shaka kutakuwa na matatizo.

Wazee/wachungaji/waangalizi wanapaswa kuunganika katika kusanyiko la mahali ili kuwe na uwajibikaji mmoja kwa mwingine miongoni mwao, ili kama kuna tatizo, waweze kusaidiana. Paulo aliandika kuhusu “wazee” (ktk 1Timo. 4:14). Pengine maana yake ni mkutano au mkusanyiko wa presbuteros (wazee) pamoja na watu wengine wenye karama za huduma. Kama kuna mtume mwanzilishi, yeye pia anaweza kutoa msaada ikiwa kuna matatizo katika kusanyiko, yanayotokana na mzee aliyekosea. Wachungaji wenye makanisa jengo wanapopotoka, matokeo yake huwa ni matatizo makubwa kwa sababu ya mfumo wa kanisa. Kuna jengo na taratibu za kufuata. Lakini, makanisa yanayokutanika nyumbani yanaweza kuvunjwa mara moja wakati mchungaji anayehusika anapopotoka. Washirika watajiunga na kundi lingine.

Mamlaka Ya Kutumika

Kwa kuwa Mungu anampa mchungaji mamlaka ya kiroho na kusimamia kanisani mwake, hili halimpi haki ya kutawala kwa nguvu kundi lake. Yeye si Bwana wao – Bwana wao ni Yesu. Wao si kundi lake – ni kundi la Mungu.

Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka (1Petro 5:2-4. Maneno mepesi kukazia).

Kila mchungaji atatoa hesabu ya huduma yake siku moja, mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo.

Tena, kwa habari ya fedha, mchungaji/mzee/mwangalizi asifanye kitu peke yake. Kama kuna fedha zinakusanywa kila mara au mara kwa mara kwa sababu yoyote ile, wengine katika kusanyiko wawajibike ili kusiwe na kutoaminiana kuhusu matumizi ya fedha (ona 2Wakor. 8:18-23). Hao wengine wawe kundi lililochaguliwa au kuteuliwa.

Kulipa Wazee

Maandiko yanaonyesha wazi kwamba wazee/waangalizi/wachungaji wanapaswa kulipwa, maana ni watenda kazi wa kudumu wa kanisa. Kwa habari hii, Paulo aliandika kama ifuatavyo:

Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hawa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, ‘Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka.’ Na tena, ‘Mtenda kazi astahili ujira wake.’ (1Timo. 5:17, 18).

Mada iko wazi kabisa – na Paulo anatumia neno ujira. Maneno yake yasiyokuwa wazi sana kuhusu wazee watawalao vema wahesabiwe kustahili heshima maradufu yanaeleweka kirahisi wakati mantiki inapotazamwa. Katika mistari kabla ya hii, Paulo anaandika waziwazi kuhusu jukumu la kanisa kuwasaidia kifedha wajane ambao wasingepata msaada kwa njia nyingine, na anaanza kwa maneno yale yale: “Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli” (ona 1Timo. 5:3-36). Basi, katika mantiki hii, “kuheshimu” maana yake ni kuwasaidia kifedha. Wazee wanaotawala vema wahesabiwe kustahili heshima mara mbili, yaani, wapokee mara mbili ya kiasi ambacho wajane wanapewa, na hata zaidi kama wana watoto wanaowategemea.

Makanisa jengo katika dunia nzima huwategemeza kifedha wachungaji wao (hata katika mataifa maskini), lakini inaonekana makanisa mengi yanayokutania nyumbani duniani kote – hasa nchi za Magharibi – hayafanyi hivyo. Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba makusudi hasa ya watu wengi katika nchi za Magharibi ya kujiunga na makanisa ya nyumbani ni uasi moyoni, nao wanatafuta na wamepata Ukristo usio na masharti mengi. Wanasema walijiunga na kanisa la nyumbani kwa sababu walitaka kuepukana na kifungo cha kanisa jengo, lakini ukweli ni kwamba walitaka kuepukana na aina yoyote ya kujitoa kikamilifu kwa Kristo. Wamepata makanisa yasiyotaka watu wajitolee kifedha, makansia yenye kwenda kinyumke kabisa na kile ambacho Kristo anatazamia kwa wanafunzi Wake. Hayo, mungu wao ni fedha, na wanathibitisha hilo kwa kujilundia hazina zao duniani badala ya mbinguni. Hao si wanafunzi wa kweli wa Kristo (ona Mathayo 6:19-24; Luka 14:33). Kama Ukristo wa mtu hauathiri anachofanya na fedha zake, huyo si Mkristo kabisa.

Makanisa yanayokutania nyumbani yenye kudai kwamba ni ya KiBiblia yanapaswa kuwatunza wachungaji wao kifedha, na kuwasaidia maskini na kusaidia kazi ya utume. Kwa kutoa na katika mambo yote yakifedha, wanapaswa kuzidi sana makanisa jengo, maana wao hawana majengo ya kulipia wala watumishi wengi wa kulipa mishahara. Wanahitajika watu kumi tu ambao watatoa zaka ili kumtunza mchungaji mmoja. Watu kumi wanaotoa asilimia ishirini ya mapato yao wanaweza kumtegemeza vizuri sana mchungaji mmoja na mishenari mmoja atakayeishi kwenye kiwango kile cha mchungaji wao.

Wachungaji Hufanya Nini?

Fikiri kwamba unamwuliza mshirika wa kawaida kanisani swali hili: “Je, ni kazi ya nani kufanya yafuatayo:- kuwashuhudia watu ambao hawajaokoka? Kuishi maisha matakatifu? Kuomba? Kuonya, kushauri na kusaidia waamini wengine? Kutembelea wagonjwa? Kuweka mikono juu ya wagonjwa kwa ajili ya uponyaji? Kubeba mizigo yaw engine? Kutumia karama zake kwa ajili ya kusanyiko? Kujikana, akijitoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu? Kufanya wanafunzi na kuwabatiza, na kuwafundisha kutii amri za Kristo?”

Washirika wengi wa kanisa, bila ya kusita, wangejibu kwa kusema, “Hayo yote ni majukumu ya mchungaji.” Lakini, ni sawa?

Kulingana na Maandiko, kila aaminiye anapaswa kuwashuhudia watu ambao hawajaokoka.

Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu (1Petro 3:15).

Kila aaminiye anawajibika kuishi matisha matakatifu.

Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, ‘Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu’ (1Petro 1:15, 16).

Kila mwamini anatakiwa kuomba.

Furahini sikuzote. Ombeni bila kukoma (1Wathes. 5:16, 17).

Kila aaminiye anatazamiwa kuonya, kutia moyo na kuwasaidia waamini wengine.

Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote (1Wathes. 5:14. Maneno mepesi kukazia).

Kila aaminiye anatakiwa kutembelea wagonjwa.

Nalikuwa uchi, mkanivika. Nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama. Nalikuwa kifungoni, mkanijia (Mathayo 25:36).

Majukumu Zaidi

Lakini, si hayo tu. Kila aaminiye anapaswa kuweka mikono juu ya wagonjwa na kuwaponya pia.

Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio. Kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapona (Marko 16:17, 18. Maneno mepesi kukazia).

Kila aaminiye anapaswa kubeba mizigo ya waamini wenzake.

Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo (Wagalatia 6:2).

Kila aaminiye anatazamiwa kutumia karama zake kwa ajili ya wengine.

Basi, kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha katika kufundisha kwake; mwenye kuonya katika kuonya kwake; mwenye kukirimu kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii; mwenye kurehemu kwa furaha (Warumi 12:6-8).

Kila mwamini anapaswa kujikana mwenyewe, na kujitoa kwa ajili ya Injili.

Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, ‘Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha’ (Marko 8:34, 35. Maneno mepesi kukazia).

Tena, kila mwamini anatazamiwa kufanya watu kuwa wanafunzi, na kuwabatiza, na kuwafundisha kutii amri zote za Kristo.

Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni (Mathayo 5:19. Maneno mepesi kukazia).

Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu (Waebrania 5:12. Maneno mepesi kukazia).

Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari (Mathayo 28:19, 20. Maneno mepesi kukazia).[2]

Majukumu hayo yote yametolewa kwa kila aaminiye, lakini washirika wengi wa kanisa hufikiri kwamba yametolewa kwa wachungaji tu! Pengine sababu ni kwamba wachungaji wengi pia hufikiri kwamba hayo ni majukumu yao peke yao.

Basi, Wachungaji Wanapaswa Kufanya Nini?

Kama majukumu hayo yote yametolewa kwa kila aaminiye, wachungaji basi wanatakiwa kufanya nini? Kirahisi tu ni kwamba, wao wameitwa kuwawezesha hao waaminio watakatifu kufanya mambo hayo yote (ona Waefeso 4:11, 12). Wameitwa kuwafundisha hao waaminio watakatifu kutii amri zote za Kristo (ona Mathayo 28:19, 20) kwa kuonyesha mfano pamoja na kufundisha (ona 1Timo. 3:2; 4:12, 13; 5:17; 2Timo. 2:2; 3:16 – 4:4; 1Petro 5:1-4).

Maandiko hayawezi kuwa wazi kuliko hivyo. Nafasi ya KiBiblia ya mchungaji sio kukusanya watu wengi kiasi anachoweza Jumapili asubuhi kwenye ibada kanisani. Ni “kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo” (Wakolosai 1:28). KiBiblia, wachungaji hawatekenyi masikio ya watu (2Timo. 4:3). Wanafundisha, wanaonya, wanakemea, wanakaripia, na kurekebisha, na yote hufanywa kwa msingi wa Neno la Mungu (ona 2Timo. 3:16 – 4:4).

Paulo aliorodhesha baadhi ya sifa za mtu anayetaka kusimama katika nafasi ya mchungaji, katika barua yake ya kwanza kwa Timotheo. Sifa kumi na nne kati kumi na tano zinahusu tabia yake, kuonyesha kwamba mfano wa maisha yake ndicho kitu cha muhimu zaidi sana.

Ni neno la kuainiwa [kwamba] mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kusimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibuni, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi (1Timo. 3:1-7).

Ukifananisha sifa hizi na zile ambazo mara nyingi hutolewa na makanisa yanapotafuta mchungaji mpya utagundua tatizo la msingi katika makanisa mengi. Wao hutafuta meneja wa kusimamia wafanyakazi/mtu wa kustarehesha watu/mtoa hotuba fupi/msimamizi/mwanasaikolojia/mkurugenzi wa shughuli na mipango/bingwa wa kuchangisha fedha/rafiki wa kila mtu/farasi au punda wa kazi. Wanataka mtu “wa kuendesha huduma ya kanisa.” Lakini, mwangalizi KiBiblia, zaidi ya yote lazima we mtu mwenye tabia nzuri na aliyejitolea kwa Kristo, awe mtumishi wa kweli kwa sababu lengo lake ni kujizaa mwenyewe. Lazima aweze kuwaambia washirika wake, “Niigeni mimi, kama na mimi ninavyomwiga Kristo” (1Wakor. 11:1).

Kwa maelezo zaidi kuhusu nafasi ya mchungaji, soma pia maandiko yafuatayo: Matendo 20:28-31; 1Timo. 5:17-20; na Tito 1:5-9.

Nafasi Ya Shemasi

Mwisho, hebu tutazame kidogo habari za shemasi. Nafasi ya sehmasi ni nafasi nyingine katika kanisa la mahali ambayo si miongoni mwa zile karama tano za huduma. Mashemasi si kama wazee – wao hawana mamlaka ya kiutawala katika kanisa. Neno la Kiyunani diakonos ambalo limetafsiriwa shemasi maana yake ni “mtumishi” au “atoaye huduma”.

Wale watu saba waliochaguliwa kwa ajili ya kazi ya kuwalisha wajane wa kanisa la Yerusalemu kila siku ndiyo huhesabiwa kuwa mashemasi wa kwanza (ona Matendo 6:1-6). Walichaguliwa na kusanyiko na kupewa kazi na mitume. Wawili wao – Filipo na Stefano – walipandishwa cheo na Mungu, wakawa wainjilisti wenye nguvu sana.

Pia, mashemasi wanatajwa katika 1Timo. 3:8-13 na Wafilipi 1:1. Tena, inaonekana nafasi hii inaweza kuchukuliwa na mwanamume au mwanamke (ona 1Timo. 3:11).


[1] Hiyo ni njia nyingine ya kusema hivi: “Kwa ajili ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.”

[2] Kama wanafunzi wa Yesu walitazamiwa kuwafundisha wanafunzi wao kutii kila kitu Yeye alichowaamuru, basi bila shaka wangewafundisha wanafunzi wao jinsi ya kufanya wengine kuwa wanafunzi pia, na kubatiza na kuwafundisha kuyashika yote ambayo Yesu aliamuru. Hivyo, kufanya wanafunzi, kubatiza na kufundisha wanafunzi ingekuwa amri inayoendelea, na inayofanya kazi kwa kila mwanafunzi aliyefuata.

Kuwa Ndani Ya Kristo

Sura Ya Kumi Na Tisa

 

Katika nyaraka za Agano Jipya, tunakutana na maneno “ndani ya Kristo”,

“pamoja na Kristo,” “kwa njia ya Kristo,” na “ndani Yake.” Mara nyingi, maneno hayo yanadhihirisha manufaa fulani ambayo sisi kama waamini tunayo kwa sababu ya mambo Yesu aliyotutendea. Tunapojiona kama Mungu anavyotuona – “ndani ya Kristo” – itatusaidia kuishi kama Mungu anavyotaka. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi atataka kuwafundisha wanafunzi wake nafasi yao katika Kristo, ili kuwasaidia wakue na kukomaa kiroho.

Kwanza: Nini maana ya kuwa “ndani ya Kristo”?

Tunapozaliwa mara ya pili, tunaingizwa katika mwili wa Kristo na kuwa wamoja Naye kiroho. Hebu tutazame mistari kadha katika nyaraka za Agano Jipya yenye kuthibitisha hicho.

Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo (Warumi 12:5. Maneno mepesi kukazia).

Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1Wakor. 6:17. Maneno mepesi kukazia).

Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungokila mmoja peke yake (1Wakor. 12:27. Maneno mepesi kukazia).

Sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo tunapaswa kujiona kwamba tumeunganishwa Naye, ni viungo vya mwili Wake na ni wamoja na Yeye katika roho. Yeye yu ndani yetu, nasi tu ndani Yake.

Angalia mstari huu unaotuambia baadhi ya manufaa tuliyo nayo kwa sababu ya kuwa ndani ya Kristo.

Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi (1Wakor. 1:30. Maneno mepesi kukazia).

Katika Kristo, tumefanywa kuwa wenye haki (yaani, tumehesabiwa “hatua hatia” na sasa tunatenda yaliyo sawa), tumetakaswa (yaani, tumetengwa kwa ajili ya Mungu kututumia katika kazi takatifu), na tumekombolewa (yaani, tumenunuliwa kutoka utumwani). Si kwamba tunangojea kufanywa wenye haki, au kutakaswa au kukombolewa wakati fulani katika siku za baadaye. Ni kwamba sasa hivi sisi tunazo baraka hizo zote, kwa kuwa tuko ndani ya Kristo.

Katika Kristo, dhambi zetu za zamani zimesamehewa zote.

Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani msamaha wa dhambi (Wakolosai 1:13, 14. Maneno mepesi kukazia).

Ona kwamba mstari huu unatuambia pia kwamba hatuko tena katika ufalme wa Shetani – utawala wa giza – bali sasa tuko katika ufalme wa nuru, ufalme wa Yesu.

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, yamekuwa mapya (2Wakor. 5:17. Maneno mepesi kukazia).

Msifu Mungu kwamba, kama wewe ni mfuasi wa Kristo, ni “kiumbe kipya” sawa na buu aliyebadilika na kuwa kipepeo! Roho yako imepewa asili mpya. Hapo kwanza ulikuwa na asili ya Shetani ya ubinafsi ndani ya roho yako, lakini sasa maisha yako yote ya kale “yamepita”.

Baraka Zaidi Katika Kristo

Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu (Wagalatia 3:26. Maneno mepesi kukazia).

Ni raha sana kujua kwamba sisi ni watoto wa Mungu mwenyewe, tuliozaliwa kwa Roho Wake! Tunapomwendea katika maombi, tunamwendea – si kama Mungu wetu tu – bali pia kama Baba yetu!

Maana tu kazi Yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo (Waefeso 2:10. Maneno mepesi kukazia).

Mungu hakutuumba tu. Ametuumba upya katika Kristo. Tena, Mungu ametupangia huduma ya kutimiza kila mmoja wetu, “matendo mema … tokea awali.” Kila mmoja wetu ana karima yake binafsi, iliyoandaliwa na Mungu Mwenyewe!

Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye (2Wakor. 5:21. Maneno mepesi kukazia).

Haki tuliyo nayo kwa sababu tuko ndani ya Kristo ni haki ya Mungu Mwenyewe. Hii ni kwa sababu Mungu amekaa ndani yetu na kutubadilisha kwa Roho Mtakatifu. Ukweli ni kwamba matendo yetu mema ni yale ya Mungu, kupitia kwetu.

Lakini katika mambo hayo yote tunashinda na zaidi ya kushinda kwa Yeye aliyetupenda (Warumi 8:37. Maneno mepesi kukazia).

Hayo “mambo yote” ambayo Paulo anasema, ni yapi? Mistari katika Warumi inayotangulia mstari huu inadhihirisha kwamba ni yale majaribu na kuteseka ambako waamini hupata. Hata katika kufa kwa ajili ya imani, bado sisi ni washindi, ingawa dunia inaweza kuhesabu kwamba tumeshindwa. Tunashinda na zaidi ya kushinda kwa Kristo kwa sababu, tunapokufa, tunakwenda mbinguni!

Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu (Wafilipi 4:13. Maneno mepesi kukazia).

Kwa njia ya Kristo, hakuna kisichowezekana kwetu kwa sababu Mungu anatuwezesha na kututia nguvu. Tunaweza kufanikisha kazi yoyote atakayotupa.

Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu (Wafilipi 4:19. Maneno mepesi kukazia).

Tutazamie kwamba Mungu atakutana na mahitaji yetu halisi, kama tutatafuta kwanza ufalme Wake. Bwana ndiye mchungaji wetu, naye huwatunza kondoo Wake!

Kukubaliana Na Anachosema Mungu

Kwa bahati mbaya, baadhi yetu hatuamini kile ambacho Neno la Mungu linasema juu yetu. Hayo huonekana kwa maneno kinyume tunayotamka, yenye kupingana na kinachosemwa na Biblia. Badala ya kusema, “Nayaweza mambo yote katika Kristo anitiaye nguvu,” sisi husema, “Sidhani kama nitaweza.”

Maneno kama hayo ndiyo Biblia inayaita “taarifa mbaya” kwa sababu hayakubaliani na kile anachosema Mungu (ona Hesabu 13:32). Lakini, kama mioyo yetu imejaa Neno la Mungu, tutajaa imani, na kuamini na kusema yale tu yanayokubaliana na Maandiko.

Matamko Machache Ya Biblia

Tunapaswa kuamini na kusema kwamba sisi tuko kama Mungu anavyosema.

Tunapaswa kuamini na kusema kwamba tunaweza kufanya yale Mungu anayosema tunaweza kufanya.

Tunapaswa kuamini na kusema kwamba Mungu yuko kama anavyosema.

Tunapaswa kuamini na kusema kwamba Mungu atafanya alichosema atafanya.

Yafuatayo ni matamko ya Maandiko ambayo waamini wote wanaweza kuyakiri kwa ujasiri kabisa. Si yote yanayohusu “kuwa ndani ya Kristo”, lakini yote ni kweli kulingana na Maandiko.

Nimekombolewa, nimetakaswa na kuhesabiwa haki katika Kristo (ona 1Wakor. 1:30).

Nimehamishwa kutoka ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa Mwan wa Mungu, yaani ufalme wa nuru (ona Wakolosai 1:13).

Dhambi zangu zote zimesamehewa katika Kristo (ona Waefeso 1:7).

Mimi ni kiumbe kipya ndani ya Kristo – maisha yangu ya kale yamepita (2Wakor. 5:17).

Mungu ameniandalia kabla matendo mema, ili nienende ndani yake (ona Waefeso 2:10).

Nimefanyika haki ya Mungu katika Kristo (ona 2Wakor. 5:21).

Mimi ni mshindi katika mambo yote kwa njia ya Kristo aliyenipenda (ona Warumi 8:37).

Naweza kufanya mambo yote kwa njia ya Kristo anitiaye nguvu (ona Wafilipi 4:13).

Mungu wangu hunipa mahitaji yangu yote kulingana na utajiri wake katika utukufu, katika Kristo (ona Wafilipi 4:19).

Nimeitwa kuwa mtakatifu (ona 1Wakor. 1:2).

Mimi ni mtoto wa Mungu (ona Yohana 1:12; 1Yohana 3:1, 2).

Mwili wangu ni hekalu la Roho Mtakatifu (ona 1Wakor. 6:19).

Si mimi ninayeishi tena, bali Kristo ndani yangu (ona Wagalatia 2:20).

Nimekombolewa kutoka mamlaka ya Shetani (ona Matendo 26:18).

Upendo wa Mungu umemiminwa moyoni mwangu na Roho Mtakatifu (ona Warumi 5:5).

Aliye ndani yangu ni mkuu kuliko (Shetani) aliyeko duniani (ona 1Yohana 4:4).

Nimebarikiwa kwa baraka zote za kiroho na kuketishwa mbinguni katika Kristo (ona Waefeso 1:3).

Nimeketi pamoja na Kristo mbinguni, juu sana kuliko majeshi yote ya kiroho ya Shetani (ona Waefeso 2:4-6).

Kwa kuwa nampenda Mungu na nimeitwa kulingana na kusudi Lake, anafanya mambo yote kuwa mema kwa ajili yangu (ona Warumi 8:28).

Kama Mungu yuko upande wangu, nani anayeweza kuwa kinyume changu? (ona Warumi 8:31).

Hakuna kinachoweza kunitenga na upendo wa Kristo (ona Warumi 8:35-39).

Yote yanawezekana kwangu kwa sababu mimi ni mwamini (ona Marko 9:23).

Mimi ni kuhani wa Mungu (ona Ufunuo 1:6).

Kwa kuwa ni mtoto Wake, Mungu ananiongoza kwa Roho Wake (ona Warumi 8:14).

Ninapoendelea kumfuata Bwana, njia ya maishayangu inazidi kung’aa (ona Mithali 4:18).

Mungu amenipa karama za pekee kutumia kwa ajili ya huduma Yake (ona 1Petro 4:10, 11).

Naweza kutoa pepo na kuweka mikono yangu juu ya wagonjwa, wapone (ona Marko 16:17, 18).

Kila mara, Mungu huniongoza kushinda katika Kristo (ona 2Wakor. 2:14).

Mimi ni balozi wa Kristo (ona 2Wakor. 5:20).

Nina uzima wa milele (ona Yohana 3:16).

Kila niombacho, nikiamini, ninakipokea (ona Mathayo 21:22).

Kwa kupigwa kwa Yesu nimeponywa (ona 1Petro 2:24).

Mimi ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu (ona Mathayo 5:13, 14).

Mimi ni mrithi wa Mungu, na mrithi pamoja na Yesu Kristo (ona Warumi 8:17).

Mimi ni mteule, ni ukuhani wa kifalme, ni taifa takatifu, ni milki ya Mungu (ona 1Petro 2:9).

Mimi ni kiungo cha mwili wa kristo (ona 1Wakor. 12:27).

Bwana ni mchungaji wangu, sitahitaji kitu (ona Zaburi 23:1).

Bwana ndiye mlinzi wa maisha yangu – nimwogope nani? (ona Zaburi 27:1).

Mungu atanishibisha maisha marefu (ona Zaburi 91:16).

Kristo alichukua magonjwa yangu na maumivu yangu (ona Isaya 53:4, 5).

Bwana ndiye anisaidiaye – sitaogopa (ona Waebrania 13:6).

Namtwika Bwana fadhaa zangu zote, maana Yeye ananijali sana (ona 1Petro 5:7).

Nampinga Shetani, naye ananikimbia (ona Yakobo 4:7).

Ninapata maisha yangu kwa kuyapoteza kwa ajili ya Yesu (ona Mathayo 16:25).

Mimi ni mtumwa wa Bwana (ona 1Wakor. 7:22).

Kwangu, kuishi ni Kristo na kufa ni faida (ona Wafilipi 1:21).

Uraia wangu ni mbinguni (ona Wafilipi 3:20).

Mungu ataimaliza kazi njema aliyoanza ndani yangu (ona Wafilipi 1:6).

Mungu yuko ndani yangu akitenda kazi (ona Wafilipi 2:13).

Nimekombolewa kutokana na laana ya Torati (ona Wagalatia 3:13).

Hayo ni machache tu kati ya matamko mengi sahihi tunayoweza kufanya, kutoka katika Neno la Mungu. Itakuwa jambo jema kujenga tabia ya kutamka hayo mara kwa mara mpaka kweli zake zipate kina na mizizi ndani ya mioyo yetu. Nasi tunapaswa kuchunga kila neno litokalo katika midomo yetu ili tuhakikishe kwamba hatusimami kinyume na maneno ambayo Mungu amesema.

Karama Za Roho Mtakatifu

Sura Ya Kumi Na Saba

 

Biblia imejaa mifano mingi tu ya watu – wanaume kwa wanawake – kupewa uwezo usio wa kawaida – wa kiMungu – na Roho Mtakatifu. Katika Agano Jipya, kuwezeshwa huko kusiko kwa kawaida kunaitwa “karama za Roho.” Ukweli ni kwamba ni zawadi kwa sababu haziwezi kufanyiwa kazi ndipo zipatikane. Ila, tusisahau kwamba Mungu huwainua wale anaoweza kuwaamini. Yesu alisema hivi, “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo huwa dhalimu katika lililo kubwa pia” (Luka 16:10). Basi, tungetazamia kwamba karama za Roho zitatolewa kwa wale ambao wamethibitisha kuaminika kwao mbele za Mungu. Kujitoa kabisa na kukubali kuongozwa na Roho Mtakatifu pia ni muhimu, maana Mungu atawatumia watu aina hiyo kwa njia isiyo ya kawaida. Kwa upande mwingine, Mungu aliwahi kumtumia punda kutabiri. Kwa hiyo, anaweza kumtumia yeyote apendaye. Kama ingebidi kutusubiri mpaka tukamilike ndipo atutumie, asingemtumia yeyote kati yetu!

Katika Agano Jipya, karama za Roho zimeorodheshwa katika 1Wakorintho 12, nazo ni tisa katika ujumla wake, kama ifuatavyo:

Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule. Mwingine imani katika Roho yeye yule, na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine, matendo ya miujiza. Na mwingine unabii, na mwingine kupambanua roho. Mwingine aina za lugha, na mwingine tafsiri za lugha (1Wakor. 12:8-10).

Kujua jinsi ya kufafanua kila karama moja si kigezo cha kutumiwa na Mungu katika utendaji wake. Manabii wa Agano la Kale na makuhani na wafalme, pamoja na wahudumu katika kanisa la kwanza la Agano Jipya walitenda kazi kwa karama za Roho bila hata ya kujua jinsi ya kuzipanga au kuzifafanua. Lakini, kwa kuwa karama za Roho zimepangwa kwenye orodha kwa ajili yetu katika Agano Jipya, bila shaka Mungu anataka tuzielewe. Paulo aliandika hivi: “Basi ndugu zangu, kwa habari ya karama za Roho, sitaki mkose kufahamu” (1Wakor. 12:1).

Orodha Ya Zile Karama Tisa

Zile karama tisa za Roho zimepangwa katika mafungu mengine tena siku hizi, kama matatu hivi: (1) Za kuzungumza, ambazo ni: aina za lugha, tafsiri za lugha, na unabii. (2) Za ufunuo, ambazo ni: neno la hekima, neno la maarifa, na kupambanua roho. (3) Za nguvu, ambazo ni: matendo ya miujiza, imani maalum, na karama za kuponya. Karama tatu husema kitu; tatu hufunua kitu; na tatu hufanya kitu. Karama hizo zote zilidhirishwa na kufanya kazi katika kipindi cha agano la zamani, isipokuwa tu ile ya aina za lugha na tafsiri za lugha. Hizo mbili ni maalum kwa ajili ya agano la sasa.

Agano Jipya halitoi maelezo kuhusu matumizi sahihi ya hizo “karama za nguvu”, na kuna maelezo kidogo sana kuhusu matumizi sahihi ya “karama za ufunuo”. Ila, kuna mafundisho mengi tu kuhusu matumizi sahihi ya “karama za kusema” yatolewayo na Paulo, na pengine ni kwa sababu mbili.

Kwanza – karama za kusema ndizo zenye kudhihirishwa mara nyingi sana katika makusanyiko kanisani, na zile za ufunuo hudhihirishwa kidogo sana, na zile za nguvu si mara nyingi. Basi, ni sawa kuhitaji mafundisyho mengi juu ya karama ambazo zinadhihirishwa mara kwa mara katika makusanyiko ya kanisa.

Pili – karama za kusema zinaonekana kuhitaji sehemu kubwa ya ushirikiano wa mwanadamu. Basi, ndizo rahisi sana kutumiwa vibaya. Ni rahisi zaidi kuongeza kitu kwenye unabii na kwa njia hiyo kuuharibu, kuliko karama ya kuponya.

Kama Roho Apendavyo

Ni muhimu kutambua kwamba karama za Roho hutolewa kama Roho apendavyo, si kama mtu yeyote apendavyo. Biblia inaweka jambo hilo wazi kabisa, hivi:

Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye (1Wakor. 12:11. Maneno mepesi kukazia).

Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe (Waebrania 2:4. Maneno mepesi kukazia).

Yawezekana mtu kutumiwa mara kwa mara katika karama fulani, lakini hakuna mwenye kumiliki karama yoyote. Kwa kuwa tu ulipata upako mara moja kufanya muujiza si ishara kwamba wewe waweza kufanya muujiza wakati wowote utakapo, wala si uhakikisho kwamba utatumiwa tena kufanya muujiza.

Tutajifunza kwa kifupi na kutazama mifano michache ya kiBiblia ya kila karama. Ila, kumbuka kwamba Mungu anaweza kudhihirisha neema Yake na nguvu Zake kwa njia nyingi zisizo na mipaka, hivyo si rahisi kufafanua hakika jinsi ambavyo kila karama itakavyofanya kazi kila mara. Tena, hakuna maelezo ya zile karama tisa za kiroho katika Maandiko – kuna majina yake tu. Hivyo, tunaweza tu kutazama Maandiko na kuona mifano itolewayo, kisha kujaribu kuamua kwamba kila moja iangukie wapi, na hatimaye kuzifafanua kwa tofauti zake zilizo dhahiri. Kwa kuwa zipo njia nyingi san asana ambazo Roho Mtakatifu anaweza kujifunua Mwenyewe kwa njia ya karama za kiroho, si busara kujaribu kubana sana mafafanuzi yetu. Kuna karma zingine ambazo ni kama muunganiko wa karama kadhaa. Paulo aliandika hivi kwa habari hiyo:

Basi, pana tofauti za karama, bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi [au matokeo], bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini, kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana (1Wakor. 12:4-7. Maneno mepesi kukazia).

Karama Za Nguvu

1) Karama za kuponya: Karama za kuponya bila shaka zinahusika na wagonjwa kupokea uponyaji. Mara nyingi zimefafanuliwa kwamba ni kuwezeshwa kusiko kawaida ili kuponya watu wagonjwa. Hakuna haja ya kuongezea hapo. Katika sura iliyopita tulitzama mfano mmoja wa karama ya kuponya ikidhihirishwa kwa Yesu wakati alipomponya mtu kiwete pale Birika la Betzata (ona Yohana 5:2-17).

Mungu alimtumia Elisha kumponya ukoma Naamani wa Shami, ambaye alikuwa mwabudu sanamu (ona 2Waf. 5:1-14). Kama tulviyojifunza wakati wa kutazama maneno ya Yesu katika Luka 4:27 kwa habari ya uponyaji wa Naamani, Elisha asingeweza kumponya mwenye ukoma yeyote wakati wowote aliotaka. Mara tu aliwezeshwa kwa njia isiyo ya kawaida kumshauri Naamani akajichovye mara saba katika Mto Yordani, na wakati Naamani alipotii, alitakaswa na ukoma wake.

Mungu alimtumia Petro kumponya yule kiwete pale kwenye mlango wa Hekalu ulioitwa Mzuri kwa njia ya karama ya kuponya (ona Matendo 3:1-10). Si kwamba yule kiwete aliponywa tu, bali ishara hiyo isiyo ya kawaida iliwavutia watu wengi wasikilize Injili kutoka kinywani kwa Petro, na kiasi cha watu elfu tano waliokoka na kuongezeka kanisani siku hiyo. Karama za kuponya mara nyingi hufanya kazi mbili: kuponya wagonjwa na kuwavutia watu ambao hawajaokoka, wamjie Kristo.

Wakati Petro alipokuwa anahubiri ujumbe wake kwa watu waliokusanyika siku hiyo, alisema hivi:

Enyi Waisraeli! Mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa wetu sisi? (Matendo 3:12).

Petro alitambua kwamba Mungu hakumtumia kumponya yule kiwete kwa sababu ya nguvu aina yoyote aliyokuwa nayo yeye, au kwa sababu ya jinsi alivyokuwa mtakatifu. Kumbuka kwamba Petro, miezi miwili tu kabla ya muujiza huo alikuwa amemkana Yesu akasema hamjui kabisa! Ukweli kwamba Mungu alimtumia Petro kwa miujiza kiasi hicho katika kurasa za kwanza za Matendo ya Mitume ukuze imani yetu na uhakika kwamba Mungu atatutumia sisi pia kama apendavyo.

Wakati Petro alipojaribu kueleza jinsi huyo mtu alivyoponywa, sidhani kama angesema ni “karama ya kuponya”. Kitu alichojua Petro ni kwamba yeye na Yohana walikuwa wanapita karibu na mtu kiwete, na ghafula akapata upako wa imani kwa ajili ya mtu huyo kuponywa. Basi, akamwamuru mtu huyo atembee katika jina la Yesu, akamshika mkono wake wa kuume na kumwinua. Yule kiwete akaanza “kutembea na kuruka ruka, na kumsifu Mungu.” Petro anafafanua kama ifuatavyo:

Na kwa imani katika jina lake, jina lake limetia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua, na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote (Matendo 3:16).

Inatakiwa imani maalum sana kumshika mtu kiwete kwa mkono na kumwinua, na kutazamia atatembea! Pamoja na hiyo karama ya kuponya, kulikuwepo pia na kutolewa kwa imani ili kuwezesha hilo kufanyika.

Kuna wanaodhani kwamba sababu ya karama hii kuwa “za” ni kwamba zipo karama mbalimbali zinazoponya aina mbalimbali za magonjwa. Wale ambao wametumika sana katika karama za kuponya wanagundua wkati mwingine kwamba magonjwa fulani huponywa zaidi katika huduma zao kuliko mengine. Kwa mfano: Mwinjilisti Filipo alionekana kuwa na mafanikio sana katika kuponya watu waliopooza na vilema (Matendo 8:7). Kuna baadhi ya wainjilisti wa karne za nyuma ambao, kwa mfano, wamefanikiwa sana kwa habari ya kuponywa vipofu au viziwi au wenye shida za moyo na kadhalika, kutegemeana na karama gani za kuponya zilizodhihirishwa kupitia kwao mara nyingi.

2) Karama ya imani na matendo ya miujiza: Karama ya imani na ya matendo ya miujiza ni kama zinafanana. Katika hizi mbili, mwenye kutumiwa hupokea ghafula imani kwa ajili ya yasiyowezekana. Tofauti kati ya hizo mbili mara nyingi hufafanuliwa kama ifuatavyo: Kuhusu karama ya imani, ni kwamba yule anayetiwa upako hupewa imani ili apokee muujiza kwa ajili yake mwenyewe, ila, kwa habari ya karama ya matendo ya miujiza ni kwamba, mhusika hupewa imani ili kutenda muujia kwa ajili ya mwingine.

Karama ya imani wakati mwingine huitwa “imani maalum” au ya kipekee kwa sababu ni kupewa imani inayozidi ya kawaida. Imani ya kawaida huja kwa kusikia ahadi ya Mungu, wakati ambapo imani maalum huja kwa toleo la ghafula la Roho Mtaka tifu. Wale ambao wamewahi kufahamu karama hii ya imani maalum hutaarifu kwamba mambo ambayo walikuwa wanayahesabu hayawezekani yanawezekana, na ukweli ni kwamba wanajikuta haiwezekani kuwa na shaka. Mambo ni hivyo hivyo kuhusu karama ya matendo ya miujiza.

Habari ya rafiki watatu wa Danieli – Shadraka, Meshaki na Abednego – ni mfano mzuri sana jinsi ambavyo “imani maalum” inavyofanya isiwezekane kuwa na shaka. Wakati walipotupwa katika tanuru la moto kwa kukataa kusujudia sanamu ya mfalme, wote walipewa karama hiyo ya imani maalum. Kweli – kukubali kuingia katika tanuru la moto mkali kulihitaji imani zaidi ya kawaida! Hebu tutazame imani waliyo-onyesha hao vijana watatu, mbele ya mfalme.

Ndipo Shadraka na Meshaki na Abednego wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza! Hamna haja kukujibu kat ika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo [yaani, kama hutatutupa katika tanuru hiyo ya moto], ujue ee mfalme ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hio sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha (Danieli 3:16-18. Maneno mepesi kukazia).

Ona kwamba karama ilikuwa inafanya kazi hata kabla hawajatupwa katika tanuru la moto. Hapakuwa na shaka katika akili zao kwamba Mungu angewakomboa.

Eliya alifanya kazi chini ya karama hiyo ya imani maalum wakati alipolishwa kila siku na kunguru, katika kipindi cha njaa ya miaka mitatu wakati wa utawala wa Mfalme mwovu, Ahabu (ona 2Waf. 17:1-6). Unahitaji imani ya ziada kumwamini Mungu kwamba atatumia ndege wakuletee chakula asubuhi na jioni. Ingawa Mungu hajatuahidi popote katika Neno Lake kwamba kunguru watatuletea chakula kila siku, tunaweza kutumia imani ya kawaida kumtegemea Mungu kwamba mahitaji yetu yatatoshelezwa – kwa sababu hiyo ni ahadi iliyopo (ona Mat hayo 6:25-34).

Matendo ya miujiza yalifanyika mara kwa mara katika huduma ya Musa. Karama hii ilikuwa kazini wakati alipogawa Bahari ya Shamu (ona Kutoka 14:13-31), na mapigo mbalimbali yalipoishukia nchi ya Misri.

Karama hii ilikuwepo katika huduma ya Yesu wakati alipowalisha watu elfu tano kwa kuongeza mikate michache na samaki (ona Mathayo 14:15-21).

Mfano mwingine wa karama hii ni wakati Paulo alipomfanya Elima mchawi kuwa kipofu kwa muda kwa sababu alikuwa anapingana na huduma yake pale kisiwani Kipro (ona Matendo 13:4-12).

Karama Za Ufunuo

1) Neno la maarifa na neno la hekima: Karama ya neno la maarifa mara nyingi hufafanuliwa kwamba ni kupewa kwa ghafula kufahamu habari fulani, ya wakati uliopita au uliopo. Mungu ambaye ana maarifa yote, wakati mwingine atatoa kiasi kidogo cha maarifa hayo. Pengine ndiyo sababu huitwa neno la maarifa. Neno ni sehemu ndogo ya sentensi, na neno la maarifa linaweza kuwa sehemu ndogo ya maarifa ya Mungu.

Neno la hekima ni sawa tu na neno la maarifa, ila mara nyingi hufafanuliwa kama uwezo wa ghafula usio wa kawaida, wa kujua matukio yajayo. Wazo la hekima mara nyingi huhusiana na kitu fulani cha baadaye. Hapa tena si kwamba tafsiri hizi ni kamilifu.

Hebu tutazame mfano wa Agano la Kale kuhusu neno la maarifa. Baada ya Elisha kumtakasa ukoma Naamani Mshami, Naamani alimpa Elisha fedha nyingi sana kama shukrani kwa kuponywa. Elisha alikataa zawadi hiyo, mtu yeyote asije akafkiri kwamba uponyaji wa Naamani ulinunuliwa badala ya kutolewa na Mungu kwa neema tu. Mtumishi wa Elisha aliyeitwa Gehazi, akaona nafasi ya kujipatia utajiri binafsi, naye kwa siri akapokea kiasi fulani cha malipo yaliyokusudiwa kumfikia Naamani. Baada ya Gehazi kuficha fedha yake aliyopata kwa udanganyifu, alisimama mbele ya Elisha. Tunasoma hivi:

Elisha akamwambia, Watoka wapi Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali. Akamwambia, Je! Moyo wangu haukwenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? (2Waf. 5:25b, 26a).

Mungu ambaye alifahamu vizuri tendo baya la Gehazi, alimfunulia nabii Elisha kwa njia ya ajabu. Habari hii inaonyesha dhahiri ya kwamba Elisha “hakumiliki” karama ya neno la maarifa – yaani, hakujua kila kitu kuhusu kila mtu kila wakati. Kama ingekuwa hivyo, Gehazi asingeota ndoto kwamba angeweza kuficha dhambi yake. Elisha alifahamu vitu kwa njia isiyo ya kawaida wakati tu Mungu alipomfunulia vitu hivyo, mara kwa mara. Karama ilifanya kazi kama Roho alivyopenda.

Yesu alitumia karama hiyo wakati alipomwambia yule mwanamke pale kisimani Samaria kwamba alikuwa na wanaume watano (ona Yohana 4:17, 18).

Petro alitumia karama hii wakati alipojua kimuujiza kwamba Anania na Safira walikuwa wanadanganya kusanyiko kwamba walichokuwa wanatoa ndiyo bei kamili ya uwanja wao waliokuwa wameuuza karibuni (ona Matendo 5:1-11).

Kuhusiana na karama ya neno la hekima, inadhihirishwa mara kwa mara katika Agano la Kale kwa manabii wote. Kila walipotabiri tukio la wakati ujao, neno la hekima lilikuwa kazini. Yesu alipewa karama hii mara kwa mara pia. Alitabiri kuhusu kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu, kuhusu kusulubiwa Kwake, na matukio ambayo yangetokea duniani kabla ya kuja Kwake mara ya pili (ona Luka 17:22-36; 21:6-28).

Mtume Yohana alitumiwa katika karama hii wakati alipofunuliwa zile hukumu za Wakati wa Dhiki Kuu. Ametuandikia hayo yote katika Kitabu cha Ufunuo.

2) Karama ya kupambanua roho: Hii karama mara nyingi inafafanuliwa kuwa ni kuwezeshwa kwa njia isiyo ya kawaida, kuona au kutambua kitu kinachoendelea katika ulimwengu wa roho.

Maono katika akili au macho ya mwamini yanaweza kuwekwa katika fungu la kupambanua roho. Hii karama inaweza kumruhusu mwamini aone malaika, mapepo, au hata amwone Yesu Mwenyewe, kama ilvyotokea kwa Paulo mara kadha (ona Matendo 18:9, 10; 22:17-21; 23:11).

Wakati Elisha na mtumishi wake walipokuwa wanatafutwa na jeshi la Shamu, walijikuta wamenaswa katika mji wa Dotani. Mtumishi wa Elisha alitazama juu ya kuta za mji na baada ya kuona makundi ya askari yanajikusanya, alipata wasiwasi sana.

[Elisha] Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba akasema, Ee BWANA! Nakusihi mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote (2Waf. 6:16, 17).

Je, ulifahamu kwamba malaika husafiri kwa farasi wa kiroho na magari ya kiroho? Siku moja utawaona mbinguni, lakini mtumishi wa Elisha alipewa uwezo wa kuwaona hapa duniani.

Kwa njia ya karama hii, aaminiye anaweza kumtambua pepo mchafu anayemtesa mtu fulani na kuwa na uwezo wa kutambua ni roho ya aina gani.

Pia, karama hii haiwezeshi kuona katika ulimwengu wa roho tu bali hata kupambanua kwa namna nyingine yoyote katika ulimwengu wa kiroho. Kwa mfano: inakuwezesha kusikia kitu kutoka katika ulimwengu wa kiroho, kama sauti ya Mungu Mwenyewe.

Mwisho – hii karama si “ya utambuzi” kama ambavyo wengine wanazoea kuiita. Watu wenye kudai kuwa nayo wakati mwingine hudhani kwamba wanaweza kutambua makusudi au nia za wengine, lakini si kweli. “Karama” wanayodai kuwa nayo ni sahihi ikielezwa kwamba ni “karama ya kukosoa na kuhukumu wengine.” Ukweli ni kwamba pengine hata wewe ulikuwa nayo kabla ya kuokoka, na sasa kwa kuwa umeokoka, Mungu anataka akuweke huru kutokana nayo moja kwa moja!

Karama Za Kusema

1) Karama ya unabii: Karama ya unabii ni uwezo usio wa kawaida kusema kwa uvuvio wa Mungu maneno kwa lugha ya msemaji. Kila mara inaweza kuanza kwa maneno yafuatayo: “Bwana asema hivi.

Karama hii si kuhubiri wala kufundisha. Mahubiri na mafundisho yaliyovuviwa yana kiwango fulani cha unabii kwa sababu hutokea kwa upako wa Roho Mtaka tifu, lakini si unabii halisi. Mara nyingi mhubiri mwenye upako au mwalimu atasema mambo kwa uvuvio wa papo kwa papo, ambayo hakupanga kuyasema, lakini huo si unabii japo anayosema yanaweza kuhesabika kuwa ya kinabii.

Karama ya unabii yenyewe hufanya kazi ya kujenga, kufariji na kutia moyo.

Bali yeye ahutubuye asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji na kuwatia moyo (1Wakor. 14:3).

Hivyo basi, karama ya unabii peke yake haina ufunuo wowote. Yaani, haifunui chochote kuhusu wakati uliopita, uliopo au ujao, tofauti na neno la hekima au neno la maarifa. Kama tulivyo-ona mwanzoni, karama za Roho zinaweza kufanya kazi kwa kushirikiana. Basi, neno la hekima au neno la maarifa yanaweza kufikishwa yanakotakiwa kwa njia ya unabii.

Tunaposikia mtu akitoa unabii katika kusanyiko, wenye kueleza matukio ya wakati ujao, si kwamba tumesikia unabii tu, bali tunakuwa tumesikia neno la hekima likifikishwa kwetu kwa karama ya unabii. Ile karama ya unabii kama ilivyo itasikika kana kwamba ni mtu anasoma maneno ya kujenga kutoka kwenye Biblia, kama vile “Mwimarike katika Bwana na katika uwezo Wake,” au “Sitakuacha wala sitakupungukia.”

Kuna wanaoamini kwamba unabii wa Agano Jipya haupaswi kuwa na chochote ambacho ni “kinyume” maana hautatimiza masharti ya “kujenga, kufariji na kutia moyo”. Si kweli. Kuweka mipaka kuhusu atakachosema Mungu kwa watu Wake, na kumruhusu aseme yaliyo “mazuri” tu hata kama wanastahili kukemewa, ni kujitukuza juu ya Mungu. Yawezekana kukemea kukaangukia kwenye kufariji na kutia moyo. Utaona kwamba hata zile jumbe za Bwana Yesu kwa yale makanisa saba ya Asia katika Ufunuo wa Yohana zina maneno ya kukemea. Je, tuziache? Hapana!

2) Karama ya aina za lugha na tafsiri za lugha: Karama ya aina za lugha ni ule uwezo wa ghafula wa kusema lugha ambayo haijulikani na msemaji. Hii karama kwa kawaida inaambatana na ile ya tafsiri za lugha, ambayo ni kuwezeshwa ghafula kufasiri kilichosemwa katika lugha isiyojulikana.

Karama hii inaitwa tafsiri za lugha. Basi, tusitazamie tafsiri ya neno kwa neno ya jumbe zinazotolewa kwa lugha. Kwa maana hiyo, inawezekana kuwa na “ujumbe mfupi kwa lugha” na tafsiri ndefu, na hata kinyume chake.

Karama hii ya kutafsiri lugha inafanana sana na unabii kwa sababu yenyewe kama ilivyo haina ufunuo, na kwa kawaida huwa ni kwa ajili ya kujenga, kufariji na kutia moyo. Kulingana na 1Wakorintho 14:5, tunaweza kusema kwamba lugha na tafsiri ya lugha ni sawa na unabii, kwa sababu hii:

Maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa.

Kama tulivyokwisha ona kabla, hakuna mafundisho katika Biblia kuhusu jinsi ya kufanya kazi na karama za nguvu. Yapo mafundisho kidogo kuhusu jinsi ya kutumia karama za ufunuo, ila, yapo mafundisho mengi sana sana kuhusu jinsi ya kufanya kazi na karama za kusema. Kwa kuwa kulikuwepo na hali ya kutoelewa katika kanisa la Korintho juu ya utendaji wa karama za kusema, Paulo alitumia karibu sura nzima ya kumi na nne ya Wakorintho wa Kwanza kushughulikia swala hilo.

Tatizo la kwanza lilihusu matumizi sahihi ya kunena kwa lugha zingine kwa sababu, kama ambavyo tumekwisha ona katika sura kuhusu ubatizo wa Roho Mtakatifu, kila aaminiye aliyebatizwa na Roho Mtakatifu ana uwezo wa kuomba katika lugha wakati wowote anaotaka. Wakorinto walikuwa wananena sana kwa lugha katika ibada zao za kanisani, lakini sehemu kubwa walifanya kinyume cha utaratibu.

Matumizi Mbalimbali Ya Lugha Nyingine

Ni muhimu sana sana kwamba tuelewe tofauti kati ya matumizi ya hadharani ya lugha, na matumizi ya binafsi. Ingawa kila mwamini aliyejazwa na Roho Mtakatifu aweza kunena kwa lugha wakati wowote, hiyo haimaanisha kwamba Mungu atamtumia katika karama ya aina za lugha, ifanyayo kazi hadharani au mbele za watu. Matumizi ya msingi ya kunena kwa lugha ni katika maisha ya maombi ya binafsi ya kila aaminiye. Ila, Wakorintho walikuwa wanakusanyika pamoja na kunena kwa lugha wote kwa mara moja, bila tafsiri yoyote, tena, bila yeyote kupata msaada au kujengwa (ona 1Wakor. 14:6-12, 16-19, 23, 26-28).

Njia moja ya kutofautisha kati ya matumizi ya lugha hadharani na binafsi ni kusema kwamba matumizi binafsi ni kuomba katika lugha, na matumizi hadharani ni kunena kwa lugha. Paulo anataja matumizi hayo mawili katika sura ya kumi na nne ya barua yake ya kwanza kwa Wakorintho. Tofauti zenyewe ni nini?

Tunapoomba katika lugha, roho zetu zinamwomba Mungu, au, zinasema na Mungu (ona 1Wakor. 14:2, 14). Lakini, wakati mtu anapopata upako ghafula na kupewa karama ya aina za lugha, ni ujumbe kutoka kwa Mungu kwenda kwa kusanyiko (ona 1Wakor. 14:5), nao hueleweka mara tafsiri inapotolewa.

Kulingana na Maandiko, tunaweza kuomba kwa lugha kama tupendavyo (ona 1Wakor. 14:15), lakini karama ya aina za lugha hufanya kazi kama Roho Mtakatifu apendavyo tu (ona 1Wakor. 12:11).

Kwa kawaida, karama ya aina za lugha ingeambatana na karama ya tafsiri za lugha. Ila, matumizi ya binafsi ya kuomba katika lugha hayana tafsiri. Paulo alisema kwamba wakati alipoomba kwa lugha akili yake ilikuwa haina matunda (1Wakor. 14:14).

Mtu binafsi anapoomba kwa lugha yeye tu ndiye anayejengwa (ona 1Wakor. 14:4), lakini karama ya aina za lugha inapofanya kazi pamoja na ile ya tafsiri za lugha, kanisa zima hujengwa (ona 1Wakor. 14:4b, 5).

Kila aaminiye anapaswa kuomba kwa lugha kila siku, kama sehemu ya ushirika wake na Bwana. Kitu kizuri kimojawapo kuhusu kuomba kwa lugha ni kwamba huna haja ya kutumia akili yako. Maana yake ni kwamba unaweza kuomba kwa lugha wakati akili zako zimesongwa na kazi yako au vitu vingine. Paulo aliwaambia hivi Wakorintho, “Namshukuru Mungu ya kuwa nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote” (1Wakor. 14:18. Maneno mepesi kukazia). Bila shaka alitumia muda mwingi sana kunena kwa lugha mpaka akawazidi washirika wote wa Kanisa la Korintho!

Vile vile, Paulo aliandika kwamba tunapoomba kwa lugha, wakati mwingine “tunambariki Bwana” (1Wakor. 14:16, 17). Mara tatu “lugha ya maombi” ninayotumia ime-eleweka na mtu aliyekuwa hapo nikiomba. Mara zote tatu nilikuwa nanena Kijapani. Kuna wakati mmoja nilimwambia Bwana kwa Kijapani, “Wewe ni mzuri sana!” Wakati mwingine nilisema, “Asante sana.” Wakati mwingine nilisema, “Njoo upesi! Njoo upesi! Ninangojea!” Si ajabu hiyo? Sijawahi kujifunza Kijapani hata neno moja, lakini mara tatu nimewahi “kumbariki Bwana” katika lugha hiyo!

Maagizo Ya Paulo Kuhusu Kunena Kwa Lugha

Maagizo aliyotoa Paulo kwa kanisa la Korintho yalikuwa wazi kabisa, na ya kueleweka. Katika kila kusanyiko au mkutano, idadi ya watu walioruhusiwa kunena kwa lugha kwa sauti ni wawili au watatu. Tena, wasinene wote kwa wakati mmoja, bali wangojane na kunena kwa zamu (ona 1Wakor. 14:27).

Maana yake si kwamba ni “jumbe tatu tu za lugha” zinazoruhusiwa. Maana yake ni kwamba watu wasizidi watatu katika ibada, watakaonena jumbe kwa lugha. Inadhaniwa na wengine kwamba kama wangekuwepo watu zaidi ya watatu ambao wanatumiwa mara kwa mara katika karama hiyo ya aina za lugha, yeyote angeweza kujiachilia kwa Roho na kutoa “ujumbe katika lugha” ambao Roho Mtakatifu alitamani kuudhihirisha kanisani. Kama si hivyo, maagizo ya Paulo yangemwekea mipaka Roho Mtakatifu kwa kuweka mipaka ya idadi ya jumbe katika lugha ambazo zingeweza kudhihirishwa katika mkutano mmoja. Kama Roho Mtakatifu asingeweza kutoa karama zaidi ya tatu za aina za lugha katika kusanyiko, isingekuwepo haja ya Paulo kutoa maagizo aliyotoa.

Ni hivyo hivyo hata kwa habari ya tafsiri za lugha. Inadhaniwa kwamba mtu zaidi ya mmoja katika kusanyiko anaweza kujiachilia kwa Roho na kutoa tafsiri ya “ujumbe katika lugha”. Watu aina hiyo walihesabiwa kuwa “watafsiri” (ona 1Wakor. 14:28), maana wangetumiwa mara kwa mara katika karama hiyo ya kutafsiri lugha. Kama ndivyo, pengine ndicho Paulo alichomaanisha aliposema, “na mmoja afasiri” (1Wakor. 14:27). Pengine hakuwa anasema mtu mmoja afasiri jumbe zote katika lugha. Pengine alikuwa anaonya tu dhidi ya “tafsiri shindani” za ujumbe huo huo mmoja. Kama mfasiri mmoja angefasiri ujumbe wa lugha, basi mfasiri mwingine hakuruhusiwa kufasiri ujumbe ule ule, hata ingawa alidhani angeweza kutoa tafsiri bora zaidi.

Kwa ujumla ni kwamba kila kitu kilitakiwa kufanyika “vizuri na kwa utaratibu” katika makusanyiko au mikutano ya kanisa – sio mchanganyiko wa usemaji usio na mpango, wa ghafula, unaochanganya watu na wa mashindano. Tena, waainio wawe makini na kuwajali wasioamini wowote wanaoweza kuwepo katikati yao. Paulo aliandika hivi kuhusu hilo:

Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je, hawatasema ya kwamba mna wazimu? (1Wakor. 14:23)

Hilo ndilo tatizo lililokuwepo Korintho – kila mtu alikuwa ananena kwa lugha kwa wakati mmoja, na mara nyingi hazikuwepo tafsiri.

Maagizo Kuhusu Karama Za Ufunuo

Paulo alitoa maagizo machache kuhusu “karama za ufunuo” kwa habari ya jinsi zinavyodhihirishwa katika manabii, kama ifuatavyo:

Na manabii wanene wawili au watatu, na wengine wapambanue. Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze. Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe. Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu (1Wakor. 14:29-33).

Kama ambavyo katika kanisa la Korintho walikuwepo washirika waliokuwa wanatumiwa mara kwa mara katika karama ya kufasiri lugha na wakajulikana kuwa “watafsiri”, walikuwepo pia wale waliokuwa wanatumiwa mara kwa mara katika karama za unabii na ufunuo, ambao walihesabiwa kuwa “manabii”. Hawakuwa manabii kwa maana ya wale wa Agano la Kale, au kama Agabo katika Agano Jipya (ona Matendo 11:28; 21:10). Wao huduma zao zingekuwa za kanisani kwao tu.

Ingawa wanaweza kuwepo zaidi ya manabii watatu wa namna hiyo katika kusanyiko la kanisa, hapo tena Paulo aliweka mipaka ya huduma ya kinabii kwamba, “ni wawili au watatu”. Hii inaonyesha kwamba wakati Roho alipokuwa anatoa karama za kiroho katika kusanyiko, mtu zaidi ya mmoja angeweza kujitoa ili kupokea karama hizo. Kama si hivyo, mashauri ya Paulo yangeishia kwa Roho Mtakatifu kutoa karama ambazo zisingefurahiwa na kusanyiko lote, maana aliweka mipaka ya idadi ya manabii waliokuwa na ruhusa ya kusema.

Kama wangekuwepo manabii zaidi ya watatu, wale wengine, japo wamezuiwa kusema, wangesaidia katika kupambanua (au kupima) yale yaliyokuwa yanasemwa. Hilipia lingeonyesha uwezo wao wa kutambua kile ambacho Roho alikuwa anakisema, nap engine maana yake ni kwamba wangekuwa wao wenyewe wamejitoa kwa Roho, ili watumiwe katika kmarama zile zile zilizokuwa zinadhihirishwa kupitia manabii wale wengine. La sivyo, wangepima unabii na mafunuo tu kwa njia ya jumla, kwa kuhakikisha kwamba yalikuwa yanakubaliana na mafunuo ambayo Mungu alikwisha toa tayari (kama katika Maandiko), kitu ambacho kingweza kufanywa na aaminiye yeyote aliyekomaa vizuri.

Paulo akasema kwamba hao manabii wote wangeweza kutabiri kwa zamu (ona 1Wakor. 14:31) na kwamba “roho za manabii huwatii manabii” (1Wakor. 14:32), kuonyesha kwamba kila nabii angeweza kujizuia asimwingilie mwingine kumkata kauli, hata wakati akipewa unabii au ufunuo kutoka kwa Roho ili kushirikisha kusanyiko lote. Hii inaonyesha kwamba Roho anaweza kutoa karama mbalimbali kwa manabii kadhaa kwa wakati mmoja katika kusanyiko, lakini kila nabii angeweza na anatakiwa kutawala wakati mafunuo yake au unabii wake utasemwa kwa kusanyiko.

Hiyo ni kweli pia kuhusu karama yoyote yakusema ambayo inaweza kudhihirishwa kupitia mwamini yeyote. Kama mtu akipokea ujumbe katika lugha au unabii toka kwa Bwana, anaweza kuuzuia mpaka wakati unaofaa katika kusanyiko. Ni kosa kuingilia unabii wa mtu mwingine na kumkata kauli au mafundisho, ili kutoa unabii wako.

Paulo aliposema, “Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja” (1Wakor. 14:31), kumbuka kwamba alikuwa anasema kwa habari ya manabii waliopokea unabii. Kwa bahati mbaya, kuna watu wamepotosha maana ya maneno ya Paulo na kusema kwamba kila aaminiye anaweza kutabiri katika kila kusanyiko. Karama ya unabii hutolewa kama Roho apendavyo.

Siku hizi kanisa linahitaji msaada wa Roho Mtakatifu, na nguvu Zake, uwepo Wake na karama Zake. Paulo aliwapa waamini wa Korintho ushauri kwamba “takeni sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu” (1Wakor. 14:1). Hii inaonyesha kwamba kiwango chetu cha kutamani au shauku huhusiana na jinsi karama za kiroho zinavyodhihirishwa, la sivyo Paulo asingetoa ushauri wa namna hiyo. Basi, mtumishi afanyaye watu kuwa wanafunzi, anayetamani kutumiwa na Mungu kwa ajili ya utukufu Wake, atatamani mno karama za kiroho, na kuwafundisha wanafunzi wake kufanya vivyo hivyo.

Huduma Ya Yesu Ya Kuponya

Sura Ya Kumi Na Sita

 

Mara nyingi imedhaniwa kwamba, kwa kuwa Yesu alikuwa Mwana wa Mungu, alikuwa na uwezo wa kufanya muujiza au kumponya mtu wakati wowote ambao Angetaka. Lakini tunapochunguza Maandiko kwa makini, tunagundua kwamba hata ingawa Yesu kweli alikuwa Mungu, ni kama alikuwa amejiwekea mipaka wakati wa huduma Yake hapa duniani. Aliwahi kusema hivi: “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda” (Yohana 5:19). Hii inaonyesha dhahiri kabisa kwamba Yesu alikuwa na mipaka, na alikuwa anamtegemea Baba Yake.

Kulingana na maelezo ya Paulo ni kwamba, wakati Yesu alipofanyika mwanadamu “alijipunguzia Mwenyewe” mambo fulani ambayo alikuwa na haki nayo kama Mungu. Tunasoma hivi:

Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu (Wafilipi 2:5-7. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Je, Yesu “alijipunguzia” nini? Si uungu Wake, wala si utakatifu Wake, wala si upendo Wake. Bila shaka ni nguvu Zake kama Mungu. Ni wazi kwamba hakuwepo kila mahali, tena, hakujua kila kitu, na hakuwa na nguvu zote. Yesu alifanyika mwanadamu. Katika huduma Yake, alifanya huduma kama mtu aliye na upako wa Roho Mtakatifu. Hili linakuwa dhahiri tunapotazama kwa makini zile Injili nne.

Kwa mfano – hebu tuulize hivi: Kama Yesu alikuwa Mwana wa Mungu, mbona ilikuwa lazima Kwake kubatizwa kwa Roho Mtakatifu alipoanza huduma akiwa na umri wa miaka thelathini? Kwa nini Mungu ajazwe Mungu?

Ni dhahiri kwamba Yesu alihitaji ubatizo wa Roho Mtakatifu ili aweze kupata upako kwa ajili ya huduma. Hii ndiyo sababu mara tu baada ya kubatizwa Kwake, tunasoma habari Zake akihubiri maneno haya: “Roho wa Bwana yu juu yangu, maana amenitia mafuta nihubiri … niwatangazie … niwaweke huru …” (Luka 4:18. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ndiyo sababu pia Petro alihubiri hivi: “Habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu, naye akazunguka huko na huko akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi, kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye” (Matendo 10:38. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Vile vile, ndiyo sababu Yesu hakufanya miujiza yoyote mpaka alipobatizwa kwa Roho Mtakatifu, alipokuwa na umri wa miaka thelathini. Je, alipokuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alikuwa Mwana wa Mungu? Ndiyo – bila shaka. Sasa basi, kwa nini hakufanya miujiza yoyote mpaka alipotimiza miaka thelathini? Kwa sababu Yesu “alijipunguzia Mwenyewe” nguvu zisizo za kawaida ambazo Mungu anakuwa nazo, na ilibidi asubiri mpaka wakati wa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu.

Uthibitisho Zaidi Kwamba Yesu Alifanya Huduma Kama Mtu Mwenye Upako Wa Roho

Tunaposoma Injili tunagundua kwamba kuna nyakati ambapo Yesu alikuwa na maarifa ya kiMungu, na wakati mwingine hakuwa nayo. Ukweli ni kwamba mara nyingi, Yesu aliuliza maswali ili kupata habari.

Kwa mfani: Alimwambia yule mwanamke Msamaria kisimani kwamba aliwahi kuwa na wanaume watano, na kwa wakati huo alikuwa anaishi na mtu ambaye hakuwa mume wake (o0na Yohana 4:17, 18). Je, Yesu alijuaje hayo? Je, ni kwa sababu alikuwa Mungu, na Mungu anajua kila kitu? Hapana, maana ingekuwa hivyo, angefanya hivyo wakati wote. Ingawa alikuwa Mungu na Mungu anajua kila kitu, Yesu “alijipunguzia Mwenyewe” uwezo Wake wa kujua kila kitu alipofanyika mwanadamu. Yesu alijua habari za ndoa ya mwanamke huyo kisimani kwa sababu Roho Mtakatifu alimpa wakati huo karama ya “neno la maarifa” (1Wakor. 12:8), ambalo ni uwezo wa kiMungu kujua kitu kuhusu wakati uliopo, au wakati uliopita. (Tutajifunza kwa upana zaidi mada ya karama za Roho katika sura ifuatayo).

Je, Yesu alijua kila kitu kila wakati? Hapana. Wakati mwanamke aliyekuwa anatokwa damu alipogusa pindo la vazi Lake na akajisikia nguvu za kuponya zikimtoka, aliuliza hivi: “Nani aliyenigusa mavazi yangu?” (Marko 5:30b). Wakati mwingine, Yesu alipoona mtini kwa mbali katika Marko 11:13, “alikwenda ili aone kama atapata kitu (tunda) kwake”.

Mbona Yesu hakumjua aliyemgusa? Mbona hakujua kama mtini ule ulikuwa na matunda? Kwa sababu alikuwa anatenda kazi kama mtu mwenye upako wa Roho Mtakatifu, aliye na karama za Roho. Karama za Roho hufanya kazi kadiri Roho apendavyo (ona 1Wakor. 12:11; Webr. 2:4). Yesu hakujua mambo kimuujiza kama wakati huo Roho Mtakatifu hakumpa karama ya “neno la maarifa”.

Ndivyo ilviyokuwa hata kuhusu huduma Yake ya kuponya. Maandiko yanaweka wazi kabisa kwamba Yesu hakuweza kumponya kila mtu kila wakati. Kwa mfano: Tunasoma katika Injili ya Marko kwamba, alipotembelea mji wa kwao wa Nazareti, hakuweza kufanya kila kitu alichotaka.

Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wowote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao (Marko 6:1 – 6. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ona kwamba Marko hasemi Yesu alikataa kufanya muujiza wowote huko. Anasema, hakuweza. Kwa nini? Kwa sababu watu wa Nazareti walikuwa hawaamini. Hawakumpokea Yesu kama Mwana wa Mungu mwenye upako, bali kama mtoto wa seremala wa pale, sawa tu na jinsi Yesu Mwenyewe alivyosema, kwamba “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake” (Marko 6:4). Matokeo yake ni kwamba alichoweza kufanya sana ni kuwaponya watu wachache tu, “wenye maradhi madogo madogo” (kama inavyosema tafsiri nyingine ya Biblia). Hakika – kama kuna mahali popote ambapo Yesu angependa kufanya miujiza mikubwa na kuwaponya watu sana, ingekuwa ni katika mji wa kwao nyumbani – mahali alipoishi muda mrefu wa maisha Yake. Lakini Biblia inasema, hakuweza.

Maelezo Zaidi Kutoka Kwa Luka

Kimsingi, Yesu aliponya kwa njia mbili tofauti: (1) Kwa kufundisha Neno la Mungu ili kuwatia moyo wagonjwa wawe na imani ya kuponywa, na (2) Kwa kufanya kazi katika “karama za kuponya”, kadiri Roho Mtakatifu alivyopenda. Basi, katika huduma Yake ya kuponya, Yesu alikuwa na mipaka aina mbili: (1) Kutokuamini kwa wagonjwa, na (2) Mapenzi ya Roho Mtakatifu kutaka kujidhihirisha kupitia “karama za kuponya”.

Ni dhahiri kwamba idadi kubwa ya wakazi wa mjini kwao Yesu hawakuwa na imani Naye. Ingawa walikuwa wamesikia juu ya miujiza Yake ya uponyaji katika miji mingine, hawakuamini kwamba alikuwa na nguvu za kuponya, na kwa sababu hiyo, Yeye asingeweza kuwaponya. Tena, inaonekana kwamba Roho Mtakatifu hakumpa Yesu “karama za kuponya” zozote zile alipokuwa Nazareti – na hakuna awezaye kuju7a sababu yake.

Luka anaeleza zaidi kuliko Marko, mambo yaliyotokea wakati Yesu alipofanya ziara huko Nazareti. Ni hivi:

Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifngua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa: Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo…Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?( Luka 4:16 – 22).

Yesu alitaka wasikilizaji Wake waamini kwamba Yeye ndiye mtiwa mafuta aliyeahidiwa katika unabii wa Isaya, akitumaini kwamba wangeamini na kupokea faida zote za upako Wake ambazo, kulingana na Isaya, ni pamoja na uhuru kutoka utumwani na kufungwa, pamoja na kuona kwa vipofu.[1] Lakini, hawakuamini, na ingawa walipendezwa na kuvutiwa na uwezo Wake wa kuzungumza, hawakuweza kuamini kwamba mwana wa Yusufu alikuwa mtu maalum. Akitambua kutokuamini kwao, Yesu alijibu hivi:

Hapana shaka mtaniambia mitahli hii, Tabibu, jiponye nafsi yako. Mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe … Amin nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe (Luka 4:23, 24).

Watu katika mji wa nyumbani kwao Yesu walikuwa wanangojea kuona kama angefanya yale waliyokuwa wamesikia ameyafanya huko Kapernaumu. Moyoni, hawakuwa na hali ya kutarajia ka imani, bali ya mashaka. Kukosa kwao imani kulimzuia Yeye asifanye miujiza yoyote, wala asiponye magonjwa makubwa.

Kingine Kilichomzuia Yesu Huko Nazareti

Maneno ya Yesu yaliyofuata, aliyowaambia watu wa Nazareti yanadhihirisha pia kwamba alikuwa amezuiwa na mapenzi ya Roho Mtakatifu, kujidhihirisha Mwenyewe kwa njia ya “karama za kuponya”. Anasema hivi:

Lakini kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu (Luka 4:25 – 27).

Hoja ya Yesu ni kwamba Eliya asingeweza kuongeza mafuta na unga ili kumtunza mjane yeyote aliyetaka yeye katika kipindi cha miaka mitatu cha ukame huko Israeli (ona 1Waf. 17:9-16). Ingawa walikuwepo wajane wengi tu wenye kuteseka huko Israeli, Roho alimpaka mafuta Eliya kwenda kumaidia mjane mmoja tu ambaye wala hakuwa Mwisraeli. Vivyo hivyo, Elisha asingeweza kumtakasa mkoma yeyote aliyetaka yeye. Hii ilithibitishwa kwa ukweli kwamba walikuwepo wakoma wengi tu Israeli wakati Naamani anatakaswa. Kama ingekuwa ni uchaguzi wake, bila shaka Elisha angewatakasa Waisraeli wenzake waliokuwa wakoma, kabla ya kumtakasa Naamani, aliyekuwa mwabudu sanamu (ona 2Waf. 5:1-14).

Eliya na Elisha walikuwa manabii – watu waliopakwa mafuta na Roho Mtakatifu, waliotumiwa kwa karama mbalimbali za Roho, kama alivyopenda Mwenyewe. Mbona Mungu hakumtuma Eliya kwa wajane wengine? Hatujui. Mbona Mungu hakumtumia Elisha kuwaponya wenye ukoma wengine? Hatujui. Hakuna ajuaye isipokuwa Mungu.

Hata hivyo, hizo hadithi mbili maarufu sana za Agano la Kale hazithibitishi kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kuwapa wajane wote mahitaji yao au kumponya kila mwenye ukoma. Watu wa Israeli wangeweza kukomesha njaa yao katika wakati wa Eliya kama wao na mfalme wao mwovu (Ahabu) wangetubia dhambi zao. Njaa ilikuwa ni aina ya adhabu ya Mungu. Na, wakoma wote wa Israeli wangeweza kuponywa kwa kutii na kuamini maneno ya agano lao kutoka kwa Mungu, ambalo, kama tulivyokwisha ona mapema, lilihusisha uponyaji wa mwili.

Yesu aliwafunuliwa wasikilizaji Wake pale Nazareti kwamba alikuwa chini ya mipaka hiyo hiyo kama Eliya na Elisha. Kwa sababu fulani, Roho Mtakatifu hakumpa Yesu “karama za kuponya” aina yoyote ile huko Nazareti. Hilo, pamoja na kutokuamini kwa watu wa Nazareti, vilisababisha isitendeke miujiza yoyote mikubwa katika mji wa kwao Yesu.

Tutazame Yesu Akitumia “Karama Ya Kuponya” Katika Tukio Moja

Tunapojifunza maelezo ya Injili kuhusu uponyaji aina mbalimbali uliofanywa na Yesu, tunagundua kwamba sehemu kubwa ya watu waliponywa, si kwa sababu ya “karama za kuponya” bali kwa sababu ya imani yao. Hebu tufikiri kidogo juu ya tofauti kati ya uponyaji wa aina mbili huo, kwa kutazama mifano. Kwanza tutajifunza habari za yule mtu aliyepooza aliyekuwepo katika Birika la Betzatha ambaye, hakuponywa kwa sababu ya imani yake, bali kwa kupitia “karama ya kuponya” ya Yesu.

Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Betzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke. Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.] Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda (Yohana 5:2 – 9).

Tunajuaje kwamba mtu huyu aliponywa kwa njia ya “karama ya kuponya” na si imani yake? Sababu ziko kadha.

Kwanza – ona kwamba mtu huyu hakuwa anamtafuta Yesu. Badala yake, yesu alimkuta ameketi kando ya birika. Kama mtu huyo angekuwa anamtafuta Yesu, hiyo ingekuwa ishara kwamba ana imani kwa sehemu fulani.

Pili – Yesu hakumwambia huyo mtu kwamba imani yake imemponya, kama alivyokuwa na kawaida ya kufanya mara nyingi alipowaponya watu.

Tatu – wakati huyo mponywa alipohojiwa baadaye na Wayahudi kwamba nani amemwambia “simama uende”, alijibu kwamba wala hakumjua. Kwa hiyo, ni hakika kabisa kwamba si imani yake katika Yesu iliyosababisha uponyaji huo. Hapa ni mtu aliyeponywa kwa njia ya “karama ya kuponywa” iliyodhihirishwa kama Roho Mtakatifu alivyopenda.

Ona pia kwamba ingawa walikuwepo watu wengi wagonjwa waliokuwa wanasubiri maji yatibuliwe, Yesu alimponya mtu mmoja tu, akawaacha wengine wengi tu wakiwa wagonjwa. Kwa nini? Hapo tena hatuna jibu. Lakini tena, hii si uthibitisho kwamba ni mapenzi ya Mungu kwa watu wengine kubakia wagonjwa. Yeyote na wote katika hao wagonjwa wangeweza kuponywa kwa njia ya kumwamini Yesu. Labda hiyo ndiyo sababu ya huyo mtu mmoja tu kuponywa – ili kuwafanya watu wavutwe kwa Yesu – Yule ambaye angewza kuwaponya, kama tu wangeamini.

Mara nyingi, “karama za kuponya” huangukia katika fungu la “ishara na maajabu”. Yaani, miujiza iliyokusudiwa kuwafanya watu wavutwe kwa Yesu. Hii ndiyo sababu wainjilisti wa Agano Jipya kama Filipo waliwezeshwa kuwa na “karama za kuponya” za aina mbalimbali, kwa sababu miujiza waliyofanya iliwavuta watu waisikilize Injili iliyokuwa ikihubiriwa (ona Matendo 8:5-8).

Wakristo wagonjwa wasingoje mpaka mtu mwenye “karama za kuponya” aje walipo ili kuponywa maana, mtu wa aina hiyo na mwenye karama hiyo anaweza asitokee. Uponyaji unapatikana kwa imani katika Yesu, na hata ingaa si kila mtu atakayueponywa kupitia karama za kuponywa, kila mtua naweza kuponywa kupitia imani yake. Karama za kuponywa zimewekwa kanisani kwa kusudi la kuwaponya wasioamini, na ili watu wavutwe kusikiliza Injili. Hii haimaanishi kwamba Wakristo hawatakaa waponywe kwa njia ya karama za kuponywa. Ila ni kwamba, Mungu anawatazamia watoto Wake wapokee uponyaji kwa imani.

Mfano Wa Mtu Kuponywa Kwa Imani yake

Batimayo alikuwa kipofu aliyeponywa kwa imani yake kwa Yesu. Tusome habari zake katika Injili ya Marko, kama ifuatavyo:

Wakafika Yeriko. Hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando yanjia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupata zaudi, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo! Inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu! Nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani (Marko 10:46 – 52).

Kwanza – ona kwamba Yesu hakumtafuta Batimayo. (Hii ni kinyume kabisa na mambo ya pale Betzata.) Ukweli ni kwamba Yesu alikuwa anampita, na kama Batimayo asingepaza sauti, Yesu angeendelea kutembea na angepita. Maana yake ni kwamba Batimayo asingeponywa.

Fikiri kidogo juu ya hilo. Ingekuwaje kama Batimayo aneketi hapo na kujiambia hivi: “Kama ni mapenzi ya Yesu mimi niponywe, atakuja nilipo, aniponye”? Nini kingetokea? Batimayo asingeponywa kamwe, ingawa habari hii inaonyesha kwamba yalikuwa mapenzi ya Yesu aponywe. Ishara ya kwanza kwamba Batimayo alikuwa na imani ni kwamba alimpazia Yesu sauti.

Pili – ona kwamba Batimayo hakukubali kukatishwa tamaa na wale waliokuwa wanajaribu kumnyamazisha. Watu walipojaribu kumyamazisha, “alizidi kupiga kelele” (Marko 10:48). Hiyo inaonyesha imani yake.

Tatu – ona kwamba Yesu hakuitikia kilio cha Batimayo mwanzoni. Inawezekana kwamba pengine alikuwa hasikii, lakini kama alisikia, Yesu hakuitika. Yaani, aliruhusu imani ya mtu huyo ipimwe.

Kama Batimayo angekata tamaa baada ya kupiga kelele mara moja tu, asingeponywa. Sisi pia lazima wakati mwingine tukaze imani kwa sababu mara nyingi inaonekana ni kana kwamba maombi yetu hayatajibiwa. Hapo ni imani yetu inapimwa. Basi, tunahitaji kudumu kusimama, tukikataa kuvunjwa moyo na mazingira kinyume.

Ishara Zaidi Za Imani Ya Batimayo

Yesu alipomwambia aje, Biblia inasema Batimayo “alitupa vazi lake”. Kwa ufahamu wangu, vipofu wa siku za Yesu walikuwa wanavaa aina fulani ya vazi lililowatambulisha kwa jamii kama vipofu. Kama ndivyo, pengine Batimayo alitupa vazi lake alipoitwa na Yesu kwa sababu aliamini kwamba asingehitaji tena kutambuliwa kama kipofu. Kama ndivyo, imani yake hapo inaonekana tena.

Tena – Batimayo alipotupa vazi lake, Biblia inasema “aliruka” kuonyesha msisimko wake kwa matarajio kwamba kitu kizuri kilikuwa kitatokea kwake. Watu wenye imani ya kuponywa huwa wamesisimka wanapomwomba Mungu awaponye, kwa sababu wanatarajia kupokea kitu.

Ona kwamba Yesu aliipima imani ya Batimayo mara nyingine tena aliposimama mbele Yake. Alimwuliza alitaka nini, na kutokana na itikio la Batimayo, ni wazi kwamba aliamini Yesu angeweza kumponya upofu wake.

Mwisho – Yesu alimwambia imani yake ndiyo ilikuwa imemponya. Kama Batimayo aliweza kuponywa kwa imani, hata mwingine yeyote anaweza, kwa sababu Mungu “hana upendeleo”.

Ili Kujifunza Zaidi

Yafuatayo ni maelezo kuhusu uponyaji mara ishirini na moja uliofanywa na Yesu, kama tupatavyo katika zile Injili nne. Yesu aliponya watu wengi zaidi ya ishirini na moja, lakini katika haya yote tunajua mambo muhimu kuhusu mgonjwa husika na jinsi alivyoponywa.

Orodha yenyewe imegawanywa katika makundi makubwa mawili – walioponywa kwa imani na wale walioponywa kwa njia ya karama za kuponywa. Mara nyingi itaonekana kwamba, watu walipoponywa kwa imani zao, Yesu aliwaambia wanyamaze kuhusu uponyaji huo. Hii inazidi kuonyesha kwamba hizo hazikuwa “karama za kuponya” kwa sababu wagonjwa hawakuponywa ili kumtangaza Yesu, au Injili.

Nyakati Ambapo Imani Au Kuamini Hutajwa Kama Sababu Ya Kuponywa:

1. Mtumwa wa akida (au “kijana”): Mathayo 8:5-13; Luka 7:2-10. “Na iwe kwako kama ulivyoamini.”

 

2. Aliyepooza akiteremshwa kutoka kwenye paa: Mathayo 9:2-8; Marko 2:3-11; Luka 5:18-26. “Alipoiona imani yao … Alisema … Enenda Zako”.

 

3. Binti yake Yairo: Mathayo 9:18-26; Marko 5:22-43; Luka 8:41-56. “Usiogope – amini tu. … Naye akawaagiza wasimwambie mtu yeyote habari hizi.”

 

4. Mwanamke mwenye kutokwa na damu: Mathayo 9:20-22; Marko 5:25-34; Luka 8:43-48. “Imani yako imekuponya.”

 

5. Vipofu wawili: Mathayo 9:27-31. “Kadiri ya imani yenu mpate. … Angalieni, hata mtu mmoja asijue.”

 

6. Kipofu Batimayo: Marko 10:46-52; Luka 18:35-43. “Imani yako imekuponya.”

 

7. Wenye ukoma kumi: Luka 17:12-19. “Imani yako imekuokoa.”

 

8. Mwana wa diwani: Yohana 4:46-53. “Yule mtu akaliamini neno ambalo Yesu alimwambia.”

 

Katika matukio haya manne yafuatayo, imani ya yule mgonjwa haitajwi moja kwa moja, lakini inaonekana kwa maneno au matendo yake. Kwa mfano: Wale vipofu wawili (katika namba 10) walimpazia Yesu sauti alipokuwa akipita, kama Batimayo alivyofanya. Wagonjwa wote katika mifano minne ifuatayo walimtafuta Yesu, ishara ya wazi kabisa ya imani yao. Katika matukio matatu kati ya manne yafuatayo, Yesu aliwaambia wale aliowaponya wasimwambia mtu yeyote juu ya mambo yaliyokuwa yamewapata, kuonyesha tena kwamba hayo hayakuwa uponyaji kwa “karama za kuponya”.

9. Mkoma ambaye hakujua mapenzi ya Mungu: Mathayo 8:2-4; Marko 1:40-45; Luka 5:12-14. “Angalia! Usimwambia mtu yeyote jambo hili.”

 

10. Vipofu wawili (pengine mmoja alikuwa Batimayo): Mathayo 20:30-34. “Wakapaza sauti wakisema, Bwana! Tuhurumie!”

 

11. Yule bubu kiziwi: Marko 7:32-36. “Akawaagiza wasimwambie mtu yeyote.”

 

12. Kipofu mmoja: Marko 8:22-26. “Hata mjini usiingie.”

 

Matukio mawili ya mwisho yanayohusu watu walioponywa kwa njia ya imani hayakuwa uponyaji – walitolewa mapepo. Lakini, Yesu alisema imani yao ndiyo iliwezesha kukombolewa kwao.

13. Mvulana kichaa: Mathayo 17:14-18; Marko 9:17-27; Luka 9:38-42. “Yesu akamwambia, Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara ile, baba yake akapaza sauti na kusema, Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu!”

 

14. Binti ya mama MsiroFoinike: Mathayo 15:22-28; Marko 7:25-30. “Mwanamke! Imani yako ni kuu. Na iwe kwako kama utakavyo.”

 

Matukio ya Watu Kuponywa Kupitia “Karama Za Kuponya”:

Haya matukio saba ya mwisho ni watu ambao inaonekana waliponywa kwa njia ya karama za kuponya. Ila, katika matukio matatu ya kwanza, kutii agizo maalum la Yesu kulitakiwa kabla ya mtu mgonjwa kuponywa. Hakuna hata wakati mmoja ambapo Yesu alimzuia aliyeponywa asimwambie yeyote kuhusu uponyaji wake. Pia, hakuna ha ta mara moja ambapo mgonjwa alimtafuta Yesu.

15. Mtu mwenye mkono uliopooza: Mathayo 12:9-13; Marko 3:1-5; Luka 6:6-10. “Simama … nyosha mkono wako.”

 

16. Yule mtu katika birika la Betzata: Yohana 5:2-9. “Inuka, jitwike godoro lako, uende.”

 

17. Yule mtu kipofu tangu kuzaliwa: Yohana 9:1-38. “Enenda ukanawe katika Ziwa la Siloamu”.

 

18. Mama mkwe wa Petro: Mathayo 8:14, 15; Marko 1:30, 31; Luka 4:38, 39.

 

19. Mwanamke mwenye kibyongo kwa miaka 18: Luka 13:11-16.

 

20. Mtu mwenye safura: Luka 14:2-4.

 

21. Mtumishi wa kuhani mkuu: Luka 22:50, 51.

 

Ona kwamba katika mifano yote hiyo ishirini na moja, hakuna mahali popote

ambapo mtu mzima anaponywa kwa imani ya mwingine kama yeye. Katika kila tukio ambapo tu fulani aliponywa kwa imani ya mtu mwingine, alikuwa ni mtoto kupitia imani ya mzazi wake (ona mfano wa 1, wa 3, wa 8, wa 13 na wa 14).

Tukio pekee ambalo linaweza kuwa tofauti ni mfano wa 1 – mtumwa wa Akida. Lakini, neno la Kiyunani linalotafsiriwa mtumwa ni neno pais ambalo linaweza pia kutafsiriwa na kumaanisha kijana kama inavyoonekana katika Mathayo 17:18 – “Yule kijana akapona saa ile ile” (maneno mepesi kutilia mkazo).

Kama kweli alikuwa mtumwa wa akida na si mtoto wake mvulana, basi mtumwa wake alikuwa kijana mdogo. Basi, akida aliwajibika kwa kijana huyo kama mlezi wake halali, na angeweza kufanyia kazi imani yake kwa niaba yake, sawa na mzazi yeyote ambavyo angeweza kufanya kwa ajili ya mtoto wake.

Hii inatufundisha kwamba haiwezekani imani ya mtu mzima isababishe uponyaji wa mtu mzima mwingine. Ndiyo – mtu mzima anaweza kuomba katika makubaliano na mwingine anayehitaji uponyaji, lakini kutokuamini kwa huyo mgonjwa kuna uwezo wa kubatilisha matokeo ya imani ya yule mwingine.

Lakini, watoto wetu wanaweza kuponywa kwa imani yetu, mpaka umri fulani. Na wao watafikia umri ambapo Mungu anawatazamia kupokea kutoka Kwake kwa msingi wa imani yao wenyewe.

Nakutia moyo ujifunze kwa undani zaidi kila mfano uliotajwa hapo juu kwa kusoma zaidi katika Biblia yako ili kutia nguvu imani yao kwa habari ya toleo la uponyaji la Bwana wetu.

Upako Wa Kuponya

Mwisho – ni muhimu kujua kwamba Yesu alitiwa mafuta kwa nguvu dhahiri za kuponya wakati wa huduma Yake hapa duniani. Yaani, alikuwa anaweza kuhisi kabisa wakati upako wa kuponya ulipokuwa unaondoka mwilini Mwake. Tena wakati mwingine, yule mgonjwa alikuwa anaweza kuhisi upako huo ukiingia mwilini mwake. Kwa mfano: Luka 6:19 inasema, “Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.”

Yamkini hata huo upako wa uponyaji ulijaa kwenye mavazi ya Yesu kiasi kwamba, kama mgonjwa angegusa vazi Lake kwa imani, upako huo wa uponyaji ungebubujika mpaka mwilini mwake. Tunasoma katika Marko 6:56, ifuatavyo:-

Na kila alikokwenda, aliingia vijijini au mijini au mashambani. Wakaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

Yule mwanamke aliyekuwa akitokwa damu (ona Marko 5:25-34) aliponywa kwa kuligusa tu pindo la vazi la Yesu, na kutarajia kwa imani kwamba ataponywa.

Si Yesu tu aliyekuwa na upako dhahiri wa uponyaji – hata mtume Paulo pia alikuwa hivyo hivyo katika miaka ya baadaye ya huduma yake. Tunasoma hivi:-

Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza yakupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka (Matendo 19:11, 12).

Upako dhahiri wa kuponya ulijaa kwenye mavazi yoyote yaliyoguswa na mwili wa Paulo, kuonyesha kwamba nguo ni kipitisho kizuri cha nguvu za kuponya!

Mungu hajabadilika tangu siku za Yesu au za Paulo, hivyo tusishangae kama Mungu atawatia mafuta baadhi ya watumishi Wake siku hizi kwa upako mkubwa hivyo wa uponyaji, kama alivyofanya kwa Yesu na kwa Paulo. Ila, karama hizo hazitolewi kwa watu wanaoanza tu kazi ya Mungu, bali kwa wale ambao wamejithibitisha kuwa waaminifu na wasiosukumwa na ubinafsi, kwa kipindi kirefu.


[1] Hayo yote yanaweza kuhusishwa na uponyaji kimwili pia. Magonjwa yanaweza kuhesabiwa kuwa ni kifungo, maana Maandiko yanasema kwamba “Mungu alimtia mafuta [Yesu] kwa Roho Mtakatifu na nguvu, … Naye akaenda huko na huko akitenda mema, na kuwaponya wote waliokuwa wameonewa na Ibilisi” (Matendo 10:38, TLR).

 

Uponyaji Wa Mungu

Sura Ya Kumi Na Tano

Ingawa jambo la uponyaji wa Mungu lina utata kiasi fulani, si kitu kilichofichika katika Maandiko. Ukweli ni kwamba, kiasi cha moja ya kumi yakila kitu kilichoandikwa katika zile Injili nne kinahusu huduma ya uponyaji ya Yesu. Zipo ahadi za uponyaji wa Mungu katika Agano la Kale, Injili na katika nyaraka za Agano Jipya. Wale walio wagonjwa wanaweza kupokea faraja kubwa sana katika wingi wa maandiko yenye kujenga imani.

Nimeona katika safari zangu duniani kote kwamba, kwa ujumla, uponyaji wa Mungu ni kitu cha kawaida katika makanisa yaliyojaa waamini waliojitolea kikamilifu (wanafunzi wa kweli). Mahali ambapo kanisa limepoa na ni la kimaendeleo, uponyaji unatokea kwa nadra sana.[1] Hayo yote yasitushangaze kwa sababu Yesu alisema kwamba ishara moja itakayofuatana na waaminio ni kwamba wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapona (ona Marko 16:18). Tungepima makanisa kwa ishara ambazo Yesu alisema zitafuatana na waamini, tungefikia mahali pa kuamua kwamba makanisa mengi hayana waamini.

[Yesu] Akawaambia, Enendeni ulimwengu mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya (Marko 16:15-18).

Mtumishi afanyaye watu kuwa wanafunzi, akiwa anaiga huduma kamilifu ya Kristo, hakika atatumia vipawa vyake kuendeleza huduma ya uponyaji wa Mungu katika eneo lake la ushawishi. Anajua kwamba uponyaji wa Mungu hukuza ufalme wa Mungu kwa njia mbili. Kwanza – miujiza ya uponyaji ni matangazo mazuri sana kwa Injili, kama mtoto yeyote anayesoma Injili au kitabu cha Matendo atakavyoelewa (ingawa watumishi wengi wenye madigirii makubwa wanaonekana hawaelewi). Pili – wanafunzi wenye afya njema hawazuiwi kufanya huduma kwa magonjwa binafsi.

Pia, mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anahitaji kuwa makini kwa wale katika mwili wa Kristo wanaohitaji uponyaji, ila wana shida ya kupokea. Mara nyingi wanahitaji mafundisho ya taratibu na kutiwa moyo kwa upole, hasa kama wamefikia mahali pa kupingana na ujumbe wowote wa uponyaji. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi anakabiliwa na uchaguzi: anaweza kuepuka kufundisha kuhusu uponyaji wa Mungu moja kwa moja. Akifanya hivyo, hakuna atakayekwazika wala hakuna atakayeponywa. Au, anaweza, kwa upendo sana, kufundisha somo hilo na kudiriki kuwakwaza wengine huku akiwsaidia wengine kupokea uponyaji. Mimi binafsi nimeamua kufanya la pili, nikiamini kwamba ni kufuata mfano wa Yesu.

Uponyaji Pale Msalabani

Mahali pazuri pa kuanza kujifunza kuhusu uponyaji wa Mungu ni katika sura ya hamsini na tatu ya kitabu cha Isaya, ambayo huhesabika kuwa unabii kuhusu Masiya. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Isaya anaeleza vizuri sana juu ya kifo cha Yesu cha kujitoa dhabihu na kazi ambayo angetimiza msalabani.

Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu. Lakini tuimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu. Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, na BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote (Isaya 53:4-6).

Kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, Isaya alitangaza kwamba Yesu alibeba huzuni na masikitiko yetu. Tafsiri nzuri ya lugha ya asili ya Kiebrania inaonyesha kwamba Yesu alichukua magonjwa na maumivu yetu.

Neno la Kiebrania huzuni katika Isaya 53:4 ni neno choli, ambalo pia linapatikana katika Kumbu. 7:15; 28:61; 1Wafalme 17:17; 2Wafalme 1:2; 8:8; na 2Nyakati 16:12; 21:15. Katika maandiko haya yote linatafsiriwa kama magonjwa au maradhi.

Neno masikitiko katika Kiebrania ni makob, ambalo pia linapatikana katika Ayubu 14:22 na 33:19. Pote hapo linatafsiriwa maumivu.

Kwa hali hiyo, Isaya 53:4 inatafsiriwa vizuri kama ifuatavyo: “Hakika magonjwa yetu Yeye Mwenyewe aliyabeba, na maumivu yetu aliyachukua.” Ukweli huu unatiwa muhuri na Mathayo kurejea maneno ya Isaya 53:4 katika Injli yake, hivi: “Yeye Mwenyewe alichukua udhaifu wetu na kuyabeba maradhi yetu” (Mathayo 8:17, TLR).

Kwa kuwa si rahisi kuepuka kweli hizi, kuna wanaojaribu kutufanya tuamini kwamba Isaya alikuwa anasema juu ya “magonjwa ya kiroho” na “maradhi ya kiroho” tuliyo nayo. Lakini maneno ya Isaya 53:4 yanayotumiwa na Mathayo yanaonyesha bila shaka yoyote kwamba Isaya alikuwa anazungumzia magonjwa halisi ya kimwili na maradhi. Hebu tuyatazame katika mantiki yake.

Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, ‘Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu’ (Mathayo 8:16-17. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mathayo alieleza waziwazikwamba uponyaji wa kimwili uliotendwa na Yesu ulikuwa kutimizwa kwa Isaya 53:4. Basi hakuna shaka kwamba Isaya 53:4 ni maandiko yanayosema kuhusu Kristo kuchukua udhaifu wetu na magonjwa.[2] Sawa na jinsi Maandiko yanavyosema kwamba Yesu alichukua maovu yetu (ona Isaya 53:11), yanasema pia kwamba alichukua maradhi yetu na udhaifu wetu. Hizo ni habari za kumfanya mgonjwa yeyote kufurahi. Kwa dhabihu Yake ya kupatanisha, Yesu alikwisha weka mpango kwa ajili ya sisi kupata wokovu na uponyaji.

Swali

Wengine wanauliza hivi: Kama hayo ni kweli, mbona si kila mtu anayeponywa? Jibu zuri ni kuuliza swali lingine: Mbona si watuwote waliozaliwa mara ya pili? Si wote waliozaliwa mara ya pili kw sababu, aidha hawajasikia Injili, au pengine hawajaiamini. Vivyo hivyo, kila mtu binafsi lazima ajipatie uponyaji wake kupitia imani yake. Wengi bado hawajasikia kweli hiyo ya kupendeza kwamba Yesu alichukua magonjwa yao. Wengine wamesikia lakini wamekataa.

Jinsi Mungu Baba anavyotazama magonjwa ni kitu kimedhihirishwa wazi kwa huduma ya Mwana Wake mpendwa, aliyejishuhudia mwenyewe kama ifuatavyo:

Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile (Yohana 5:19).

Tunasoma katika kitabu cha Waebrania kwamba Yesu alikuwa “mfano halisi wa asili Yake [Baba]” (Waebrania 1:3, TLR). Hakuna shaka kwamba jinsi Yesu alivyotazma magonjwa ni sawa na jinsi Baba Yake alivyotazama.

Yesua lionaje magonjwa? Hakuna hata mara moja ambapo alimrudisha yeyote aliyemjia akitaka kuponywa. Hakuna hata mara moja alipomwambia mtu aliyetaka kuponywa, “Si mapenzi ya Mungu wee uponywe, hivyo itabidi ubakie mgonjwa.” Kila wakati Yesu aliwaponya wagonjwa waliomjia, na mara walipoponywa, mara nyingi aliwaambia kwamba ni imani yao ndiyo imewaponya. Zaidi ya hayo, Biblia inatangaza kwamba Mungu habadiliki (ona Malaki 3:6) na kwamba Yesu Kristo ni “yule yule, jana, na leo na hata milele” (Waebrania 13:8).

Uponyaji Unatangazwa

Kwa bahati mbaya, wokovu siku hizi umechujwa na kubaki kuwa msamaha wa dhambi tu. Lakini maneno ya Kiyunani yanayosema kuhusu “kuokoka” na “wokovu” yana maana kubwa – si msamaha tu bali ukomozi kamili na uponyaji.[3] Hebu tumtazame mtu katika Biblia aliyepokea wokovu kwa ukamilifu. Yeye aliponywa na imani yake alipokuwa anamsikiliza Paulo akihubniri Injili mjini kwao.

Wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda (Matendo 14:6-10).

Ona kwamba ingawa Paulo alikuwa anahubiri “Injili”, yule mtu alisikia kitu kilichosababisha imani moyoni make ili apokee uponyaji wa mwili wake. Kwa kiasi kidogo, bila shaka alimsikia Paulo akisema kitu juu ya huduma ya Yesu ya uponyaji, na jinsi Yesu alivyomponya kila mtu aliyeomba uponyaji kwa imani. Pengine Paulo alitaja pia unabii wa Isaya kuhusu Yesu kuchukua magonjwa yetu na maradhi. Hatujui – lakini kwa kuwa “imani huja kwa kusikia” (Warumi 10:17), yule mtu aliyepooza pengine alisikia kitu kilichowasha moto imani katika moyo wake, kwamba ataponywa. Kitu fulani alichosema Paulo kilimshawishi kwamba Mungu hakutaka aendelee kupooza.

Bila shaka Paulo mwenyewe aliamini kwamba Mungu alitaka mtu huyo aponywe, la sivyo maneno yake yasingemshawishi mtu huyo kuwa na imai ya kuponywa, wala asingemwambia asimame. Je, kungeotkea nini kama Paulo angesema yale ambayo wahubiri wengi wa siku hizi wanasema? Ingekuwaje kama angehubiri hivi: “Si mapenzi ya Mungu kwa kila mtu kuponya”? Huyo mtu asingekuwa na imani ya kuponywa. Pengine hii inaeleza kwa nini watu wengi hawaponywi siku hizi. Wahubiri wale wale wanaotakiwa kuwahamasisha watu wawe na imani ya kuponywa, ndiyo wenye kuharibu imani hiyo.

Hapa tena ona kwamba mtu huyu aliponywa kwa imani yake. Kama asingeamini angebaki amepooza tu, hata ingawa ulikuwa ni mpango wa Mungu kwake kuponywa. Tena, pengine walikuwepo wagonjwa wengine pia katika kundi lile siku hiyo, lakini hatuambiwi yeyote mwingine kuponywa. Kama ni hivyo, mbona hawakuponywa? Kwa sababu ile ile iliyowazuia wengi wasio-okoka waliokuwepo katika kundi hilo kuokoka – kwa sababu hawakuamini ujumbe wa Paulo.

Hatupaswi kuamua kwamba si mapenzi ya Mungu kumponya kila mtu kwa kuwa kuna watu hawaponywi. Hiyo ni sawa na kuamua kwamba si mpaenzi ya Mungu kwa wote kuokoka kwa sababu watu wengine hawaokoki. Kila mtu lazima aiamini Injili kibinafsi kama anataka kuokoka, na kila mtu lazima aamini mwenywe kama anataka kuponywa.

Uthibitisho Zaidi Kwamba Ni Mapenzi Ya Mungu Kuponya

Chini ya agano la zamani, uponyaji wa mwili ulikuwemo katika agano la Israeli na Mungu. SIku chache tu baada ya Waisraeli Kutoka Misri, Mungu aliwaahidi hivi:

Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yoyote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye (Kutoka 15:26).

Yeyote aliye mkweli atakubali kwamba uponyaji ulikuwemo katika agano la Mungu na Israeli, kutegemeana na utii wa watu. (Hata Paulo anaweka wazi kabisa katika 1Wakor. 11:27-31) kwamba afya ya kimwili katika agano jipya hutegemeana na utii wetu pia.)

Vile vile, Mungu aliwaahidi Waisraeli hivi:

Nanyi mtamtumikia BWANA Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza (Kutoka 23:25-26. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Utabarikiwa kulio mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu wala kati ya wanyama wenu wa mifugo. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao (Kumbu. 7:14-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ikiwa uponyaji ulihusishwa katika agano la kale, mtu atashangaa kiwa hautahusishwa katika agano jipya, ikiwa agano jipya ni bora kuliko la zamani kama yanavyosema Maandiko.

Lakini sasa [Yesu] amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora (Waebrania 8:6. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Uthibitisho Zaidi Tena

Biblia ina Maandiko mengi sana yenye kutoa uthibitisho usiopingika kwamba ni mapenzi ya Mungu kumponya kila mtu. Hebu nitaje mistari mitatu iliyo bora zaidi.

Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naama, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote (Zaburi 103:1-3. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ni Mkristo gani atakayepingana na tamko la Daudi kwamba Mungu anapenda kusamehe maovu yetu yote? Ila, Daudi aliaminipia kwmaba Mungu anataka kuponya magonjwa yetu yote.

Mwanangu: sikiliza maneno yangu; tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, na afya ya mwili wao wote (Mithali 4:20-22. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa (Yakobo 5:14-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ona kwamba ahadi hii ya mwisho ni kwa yeyote aliye mgonjwa. Tena, ona kwamba si wazee wala mafuta yanayoleta uponyaji, bali ni “maombi ya imani.”

Je, ni imani ya wazee au ya mgonjwa? Ni imani ya wote wawili. Imani ya mgonjwa inaonyeshwa kwa sehemu anapowaita wazee wa kanisa. Kutokuamini kwa mgonjwa kungeweza kubatilisha matokeo ya maombi ya wazee. Aina hii ya maombi inayosemwa na Yakobo ni mfano mzuri kuhusu “maombi ya makubaliano” ambayo Yesu alitaja katika Mathayo 18:19. Wote wanaohusika katika maombi aina hii lazima “wakubaliane.” Kama mmoja anaamini na mwingine haamini, hawakubaliani.

Pia tunajua kwamba katika vifungu kadhaa, Biblia inamtaja Shetani kama mhusika wa magonjwa (ona Ayubu 2:7; Luka 13:16; Matendo 10:38; 1Wakor. 5:5). Basi, ni sawa kabisa kwamba Mungu apingane na kazi ya Shetani katika miili ya watoto Wake. Baba yetu anatupenda sana kuliko baba yeyote wa duniani anavyoweza kuwapenda watoto wake (ona Mathayo 7:11), nami sijawahi kukutana na baba aliyetamani watoto wake kuwa wagonjwa.

Kila uponyaji wa Yesu wakati wa huduma Yake hapa duniani na kila uponyaji unaotajwa katika kitabu cha Matendo unapaswa kututia moyo kuamini kwamba Mungu anataka sisi tuwe na afya njema. Mara nyingi sana Yesu aliponya watu waliomtafuta ili waponywe, Naye alisema imani yao ilihusika na muujiza wao. Hii inathibitisha kwamba Yesu hakuchagua watu fulani aliotaka kuwaponya. Mtu yeyote mgonjwa angeweza kumjia kwa imani na kuponywa. Alitaka kuwaponya wote, lakini alitaka wawe na imani.

Majibu Kwa Baadhi Ya Hoja Pinzani

Pengine hoja pinzani ya kawaida kabisa kwa hayo yote ni ile itokanayo na mambo waliyopitia watu, bila kuw ana msingi kwenye Neno la Mungu. Mara nyingi inasemekana hivi: “Nilimjua mwanamke mmoja – Mkristo mzuri sana – ambaye aliomba aponywe kensa, lakini akafa. Hii inathibitisha kwamba si mapenzi ya Mungu kuwaponya wote.”

Hatupaswi kamwe kuamua mapenzi ya Mungu kwa kutumia kitu kingine ambacho si Neno Lake. Kw amfano: Kama ungerudi nyuma katika wakati na kuwaona Waisraeli wakitangatanga nyikani kwa miaka arobaini huku nchi ya ahadi iliyojaa maziw ana asali ikisubiri ng’ambo tu ya Mto Yordani, ungedhani kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi. Lakini kama unaijua Biblia, basi ungetambua kwamba si hivyo. Hakika ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa Israeli kuingia katika Nchi ya Ahadi, lakini walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao wenyewe (ona Waebrania 3:19).

Vipi kuhusu watu wote ambao kwa sasa wako jehanamu? Ulikuwa mpango wa Mungu wao wawe mbinguni, lakini hawakutimiza masharti ya toba na imani katika Bwana Yesu. Vivyo hivyo, hatuwezi kuamua mapenzi ya Mungu kuhusu uponyaji kwa kuwatazama watu wagonjwa. Kwa kuwa Mkristo anaweza kuomba uponyaji na akashindwa kupokea hakumaanishi kwamba si mapenzi ya Mungu kuponya kabisa. Kama huyo Mkristo angetosheleza masharti ya Mungu, angeponywa, la sivyo Mungu ni mwongo. Tunaposhindwa kupokea uponyaji halafu tumlaumu Mungu kwa kusema kwamba uponyaji haukuwa mapenzi Yake, hatuwi na tofauti yoyote na Waisraeli wasioamini waliokufa nyimani wakidai kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwao kuingia katika Nchi ya Ahadi. Ni afadhali tumeze mate na kiburi chetu na kukiri kwamba sisi ndiyo wenye matatizo.

Kama tulivyoona katika sura iliyotangulia kuhusu imani, Wakristo wengi wa kweli wamemalizia maombi yao kuhusu uponyaji kimakosa kwa kusema maneno yafuatayo, ambayo yanaharibu imani: “Kama ni mapenzi Yako.” Hii inadhihirisha waziwazi kwamba hawaombi kwa imani kwa sababu hawana uhakika wa mapenzi ya Mungu. Kwa habari ya uponyaji, mapenzi ya Mungu ni wazi kabisa, kama ambavyo tumekwisha ona. Kama unajua Mungu anataka kukuponya, hakuna haja ya kuongeza “Kama ni mapenzi Yako” kwenye hiyo sala yako ya kuponywa. Hiyo ni sawa na kumwambia Mungu hivi: “Bwana, najua uliahidi kuniponya, lakini endapo hukumaanisha hivyo, naomba uniponye kama tu ni mapenzi Yako.”

Pia ni kweli kabisa kwamba Mungu anaweza kuwaadhibu waamini wasiokuwa watii kwa kuruhusu magonjwa yawatese, mpaka kufikia mahali pa kuruhusu kifo chao kabla ya muda wao, mara zingine. Waamini hao wanahitaji kutubu kabla ya kupokea uponyaji (ona 1Wakor. 11:27-32). Kuna wengine pia ambao kwa kutokujali miili yao, wanafungua milango wapate magonjwa. Wakristo wanatakiwa kuwa na akili za kutosha kula chakula chenye kuleta afya, kula kwa kiasi, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kupumzika inapotakiwa.

Hoja Pinzani Nyingine

Mara nyingi imesemekana hivi: “Paulo alikuwa na mwiba katika mwili wake, na Mungu hakumponya.”

Wazo kwamba mwiba wa Paulo ulikuwa ugonjwa ni wazo baya tu la kitheolojia, maana Paulo mwenyewe alituambia mwiba huo ulikuwa nini. Ulikuwa malaika wa Shetani.

Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi kwa wingi wa mafunuo hayo, nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajli ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi ili uweza wa Kristo ukae juu yangu (2Wakor. 12:7-9. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Katika Kiyunani, neno mjumbe ni “aggelos,) ambalo linatafsiriwa kuwa malaika katika sehemu zaidi ya 160 katika Agano Jipya. Basi, mwiba wa Paulo mwilini ulikuwa malaika wa Shetani aliyetumwa kumpiga – haukuwa ugonjwa au maradhi.

Onapia kwamba Paulo hakuomba aponywe, wala hakuna dalili kwamba Mungu alikataa kumponya. Mara tatu, Paulo alimwomba Mungu kama angeweza kumwondoa huyo malaika anayempiga, na Mungu akamwambia neema Yake inamtosha.

Ni nani aliyempa Paulo mwiba huu? Kuna wanaoamini kwamba ni Shetani, kwa sababu mwiba wenyewe unaitwa “mjumbe wa Shetani.” Wengine wanaamini ni Mungu kwa sababu mwiba ulitolewa ili Paulo asijivune. Paulo mwenyewe alisema kwamba ni “makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi”.

Tafsiri nyingine iko tofauti kidogo. Badala ya kusema, “makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi” inasema, “nisije nikatukuzwa kupita kiasi.” Kuna tofauti kubwa hapo kwa sababu Mungu hapingi sisi kutukuzwa. Ukweli ni kwamba, ameahidi kututukuza kama tutajinyenyekeza. Basi, inawezekana kabisa kwamba Mungu ndiye aliyekuwa anamtukuza, na Shetani alikuwa anajaribu kuzuia kutukuzwa kwa Paulo kwa kumpangia malaika wa kumpiga ili kusababisha fujo kokote Paulo alikokwenda. Lakini Mungu alisema angetumia mazingira hayo kwa ajili ya utukufu Wake kwa sababu uwezo Wake ungedhihirishwa zaidi katika maisha ya Paulo kwa sababu ya udhaifu wake.

Vyovyote vile – kusema kwamba Paulo alikuwa mgonjwa na Mungu akakataa kumponya ni upotoshaji mkubwa sana wa kinachosemwa na Biblia. Katika fungu kuhusu mwiba katika mwili wake, Paulo hakutaja ugonjwa wowote, na hakuna kinachofanana na Mungu kukataa kumponya ugonjwa wake. Kama mtu mkweli atasoma orodha ya majaribu yake yote katika 2Wakorintho 11:23-30, hatakuta ugonjwa hata mmoja ukitajwa, wala maradhi.

Maelezo Zaidi Juu Ya Mada Hiyo

Kuna wanaopinga maelezo haya kuhusu mwiba wa Paulo, wakisema hivi: “Si Paulo mwenyewe aliwaambia Wagalatia kwamba alikuwa mgonjwa alipowahubiria Injili mara ya kwanza? Je, hapo hakuwa anasema kuhusu mwiba wake katika mwili?”

Yafuatayo ni maneno halisi ya Paulo, aliyoandika katika barua yake kwa Wagalatia.

Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu (Wagalatia 4:13-14).

Neno la Kiyunani asthenia linalotumika hapa katika Wagalatia 4:13 maana yake ni udhaifu. Linaweza kumaanisha udhaifu kwa sababu ya ugonjwa, lakini si lazima iwe hivyo.

Kwa mfano: Paulo aliandika hivi: “Udhaifu wa Mungu ni nguvu kuliko nguvu za wanadamu” (1Wakor. 1:25, TLR. Maneno mepesi kutilia mkazo). Neno linalotumiwa hapo pia ni asthenia. Kama watafsiri wangetafsiri na kusema hivi: “Ugonjwa wa Mungu una nguvu kuliko nguvu za wanadamu” isingeleta maana yoyote. (Ona pia Mathayo 26:41 na 1Petro 3:7, ambapo neno hilo hilo asthenia linatafsiriwa kuwa ni udhaifu na haliwezi kutafsiriwa ugonjwa).

Paulo alipotembelea Galatia kwa mara ya kwanza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Matendo, hakuna taarifa yoyote ya yeye kuwa mgonjwa. Lakini, tunaambiwa kwamba alipigwa mawe na kuachwa akiwa amekufa. Basi, aidha alifufuliwa kutoka kwa wafu au alipona kimuujiza (ona Matendo 14:5-7, 19-20). Bila shaka mwili wa Paulo ulikuwa katika hali mbaya baada ya kupigwa mawe na kuachwa amekufa. Ulikuwa na michubuko na kukatika-katika sana kila mahali.

Paulo hakuwa na ugonjwa wa aina yoyote huko Galatia, uliokuwa jaribu kwa wasikilizaji wake. Ila, mwili wake ulikuwa dhaifu kutokana na kupigwa kwake mawe. Bila shaka alikuwa na mabakio au alama za kuteswa kwake huko Galatia wakati aliowaandikia barua Wagalatia, maana alimaliza waraka huo kwa maneno yafuatayo:

Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu (Wagalatia 6:17).

Hoja Nyingine: “Ninateseka Kwa Utukufu Wa Mungu”

Hoja hii hutumiwa na baadhi ya watu ambao wamechukua mstari kutoka katika kisa cha kufufuliwa kwa Lazaro na kuufanya msingi wa kudai kwamba wanaugua ugonjwa kwa utukufu wa Mungu. Yesu alisema hivi kumhusu Lazaro:

Ugonjwa huu hautaishia kifoni, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa (Yohana 11:4).

Yesu hakuwa anasema kwamba Mungu alikuwa anatukuzwa kwa sababu ya Lazaro kuwa mgonjwa. Alimaanisha kwamba Mungu angetukuzwa wakati ambapo Lazaro angeponywa na kufufuliwa kutoka kwa wafu. Yaani, mwisho wa ugonjwa huo usingekuwa mauti bali Mungu angetukuzwa. Mungu hatukuzwi katika ugonjwa; anatukuzwa katika uponyaji (ona pia Mathayo 9:8; 15:31; Luka 7:16; 13:13 na 17:15, mahali ambapo uponyaji ulileta utukufu kwa Mungu.)

Hoja Nyingine: “Paulo Alisema Amemwacha Trofimo Akiwa Mgonjwa Huko Mileto”

Maneno haya yanaandikwa katika mji fulani huko Ujerumani. Nilipoondoka nyumbani, niliwaacha watu wengi wakiwa wagonjwa. Niliacha hospitali zimejaa wagonjwa. Hiyo haimaanishi kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa wote kuponywa. Kwa kuwa Paulo aliacha mtu mmoja tu mgonjwa katika mji aliotembelea si ushahidi kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwa mtu huyo kuponywa. Vipi kuhusu makundi ya watu wasio-okoka ambayo Paulo aliyaacha pia? Je, inathibitisha kwamba hayakuwa mapenzi ya Mungu kwao kuokoka? La sivyo, hata kidogo.

Hoja Nyingine: “Mimi Ni Kama Ayubu!”

Bwana Asifiwe! Kama umesoma mwisho wa habari za Ayubu, unajua kwamba aliponywa. Hayakuwa mapenzi ya Mungu kwamba Ayubu aendelee kuwa mgonjwa, na si mapenzi ya Mungu kwako pia kuendelea kuwa mgonjwa. Habari za Ayubu zinatilia mkazo kwamba mapenzi ya Mungu sikuzote ni kuponya.

Hoja Nyingine: Ushauri Wa Paulo Kwa Timotheo Kuhusu Tumbo Lake

Tunajua kwamba Paulo alimwambia Timotheo atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lake, na magonjwa yake ya mara kwa mara (ona 1Timo. 5:23).

Ukweli ni kwamba Paulo alimwambia Timotheo aache kunywa maji na atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lake, na magonjwa ya mara kwa mara. Hii inaonyeha kwamba maji yalikuwa na matatizo fulani. Ni hivi: Kama unakunywa maji machafu, acha kuyanywa uanze kunywa kitu kingine, la sivyo utakuwa na matatizo ya tumbo kama Timotheo.

Hoja Nyingine: “Yesu Aliponya Ili Kuthibitisha Uungu Wake Tu”

Watu wengine wanataka tuamini kwamba sababu ya pekee ya Yesu kuponya ilikuwa kuthibitisha Uungu Wake. Kwa vile Uungu Wake umethibitishwa vizuri kabisa, inasemekana haponyi tena.

Hayo ni makosa kabisa. Ni kweli kwamba miujiza ya Yesu ilihalalisha Uungu Wake, lakini hiyo si sababu ya pekee iliyomfanya aponye watu wakati wa huduma Yake hapa duniani. Mara nyingi sana aliwaambia watu aliowaponya wasimwambie yeyote mambo yaliyokuwa yametokea kwao (ona Mathayo 8:4; 9:6, 30; 12:13-16; Marko 5:43; 7:36; 8:26). Ikiwa Yesu aliwaponya watu kwa kusudi moja tu la kuthibitisha Uungu Wake, angewaambia watu hao kumwambia kila mtu yale aliyokuwa amewatendea.

Nini kilichokuwa nyuma ya matendo ya kuponya yaliyofanywa na Yesu? Mar anyingi Maandiko yanasema aliponya kwa sababu “aliwahurumia watu” (ona Mathayo 9:35-36; 14:14; 20:34; Marko 1:41; 5:19; Luka 7:13). Yesu aliponya watu kwa sababu aliwapenda na alikuwa amejaa huruma. Je, Yesu amepunguza huruma baada ya huduma Yake ya hapa duniani? Je, upendo Wake umepungua? Hapana hata kidogo!

Hoja Nyingine: “Mungu Anataka Niwe Mgonjwa Kwa Sababu Fulani”

Hiyo haiwezekani kwa sababu ya Maandiko yote tuliyokwisha angalia. Kama wewe umedumu katika kutokutii, yawezekana ni kweli kwamba Mungu ameruhusu ugonjwa wako ili akufikishe kwenye toba. Lakini, bado si mapenzi Yake kwamba ubakie mgonjwa. Anataka utubu na kuponywa.

Tena, kama Mungu anataka uwe mgonjwa, mbona unakwenda kwa daktari na kupokea dawa, ukitazamia kuponywa? Kwani unajaribu kuepuka “mapenzi ya Mungu”?

Hoja Ya Mwisho: “Tusipopata Magonjwa, Tutakufaje?”

Tunajua Biblia inafundisha kwamba miili yetu inachakaa (ona 2Wakor. 4:16). Hakuna tunachoweza kufanya kuzuia nywele zetu kuwa na mvi, na miili yetu kuzeeka. Mwishoni, hatu taweza kuona vizuri wala kusikia vizuri kama ilivyokuwa tukiwa vijana. Hatuwezi kukimbia. Mioyo yetu haiwi na nguvu sana. Tunachakaa pole pole.

Lakini haimaanishi kwamba lazima tufe kwa ugonjwa au maradhi. Miili yetu inaweza kuchoka kabisa, na ikifikia hapo, roho zetu zitaiacha miili yetu Mungu atakapotuita nyumbani huko mbinguni. Waamini wengi wamekufa katika hali hiyo. Mbona na wewe isiwe hivyo kwako?


[1] Katika makanisa mengine ya Marekani, mchungaji akifundisha somo hili atakuwa anajihatarisha sana kwa sababu ya upinzani mkubwa ambao angepata kutoka kwa wanaojiita waamini. Hata Yesu alikutana na upinzani na kutokuamini wakati mwingine, vitu vilivyozuia huduma Yake ya kuponya (ona Marko 6:1-6).

[2] Katika kushika chochote kitakachowawezesha kuunga mkono kutokuamini kwao, wengine hujaribu kutushawishi kwamba Yesu alitimiza kabisa Isaya 53:4 kwa kuwaponya watu kadhaa jioni ile pale Kapernaumu. Lakini, Isaya alisema kwamba Yesu aliyachukua magonjwa yetu, sawa tu na alivyosema kwamba Yesu alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu (lingansiha Isaya 53:4 na 5). Yesu alichukua magonjwa ya watu wengi kama wale ambao maovu yao yalimfanya achubuliwe. Kwa hiyo, Mathayo alikuwa anaonyesha tu kwamba huduma ya Yesu ya kuponya pale Kapernaumu ilithibitisha kwamba alikuwa ndiye Masiya anayetajwa katika Isaya 53, yeye ambaye angeyachukua magonjwa yetu na maradhi yenye kutusumbua.

[3] Kwa mfano: Yesu alimwambia mwanamke aliyekuwa amemponya kutokwa damu, “Binti, imani yako imekuponya” (Marko 5:34, TLR). Neno la Kiyunani linalotumika kusema “imekuponya” katika mstari huu (sozo) na katika sehemu zingine kumi katika Agano Jipya lina maana ya “kuokoa” au “okoa” na linatumika zaidi ya mara themanini katika Agano Jipya. Kwa mfano, ndiyo neno linalotumiwa kusema “kuokoa” katika Waefeso 2:5, hivi: “Kwa neema ninyi mmeokolewa kwa njia ya imani.” Ni kwamba uponyaji wa kimwili upo katika mantiki ya neno la Kiyunani linalotumiwa mara nyingi kusema kuhusu “kuokoka.”

Mambo Ya Msingi Kuhusu Imani

Sura Ya Kumi Na Nne

 

Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aaini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao (Waebrania 11:6).

Kama waaminio, imani yetu imejengwa kwenye msingi kwamba Mungu yupo, naye huwatendea watu wanaomtafuta kitofauti na wale wasiomtafuta. Tukiamini kweli kweli mambo hayo, tunaanza kumpendeza Mungu, kwa sababu mara moja tunaanza kumtafuta. Kumtafuta Mungu ni pamoja na (1) Kujifunza mapenzi Yake, (2) Kumtii, na (3) Kutumainia ahadi Zake. Hayo yote matatu yanapaswa kuwa sehemu ya mwenendo wetu wa kila siku.

Sura hii inatazama mwendo wetu wa imani. Ni bahati mbaya kwamba wengi wamekazia imani mpaka ikapita mipaka ya KiBiblia – hasa mkazo kuhusu mafanikio kimwili. Kwa sababu hiyo, kuna watu ambao wana hofu kulishughulikia swala hili kabisa. Lakini, kwa kuwa kuna watu wanaozama katika madimbwi yao ya kuogelea, si sababu kwetu kuacha kunywa maji. Tunaweza kuwa na msimamo na ukweli wa Maandiko. Biblia ina mengi sana inayofundisha kuhusu mada hiyo, na Mungu anataka tuitumie imani yetu kwa habari ya ahadi Zake nyingi sana.

Yesu aliweka mfano wa mwenye kuwa na imani katika Mungu, Naye anatazamia wanafunzi Wake kufuata mfano Wake. Vivyo hivyo, mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi hujitahidi kuweka mfano wa kumtumaini Mungu, naye huwafundisha wanafunzi wake kuziamini ahadi za Mungu. Hii ni muhimu sana sana. Sit u kwamba haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo imani, ni kwamba haiwezekani kupokea majibu ya maombi yetu pasipo imani (ona Mathayo 21:22; Yakobo 1:5-8). Maandiko yanafundisha wazi wazi kabisa kwamba wenye mashaka wanakosa baraka ambazo waamini hupokea. Yesu alisema hivi: “Yote yanawezekana kwake yeye aaminiye” (Marko 9:23, TLR).

Maana Ya Imani

Tafsiri ya KiBiblia ya imani inapatikana katika Waebrania 11:1, kama ifuatavyo:

Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyo-onekana.

Kutokana na tasiri hii, tunapata sifa kadhaa za imani. Kwanza – mtu mwenye imani ana uhakika. Hii ni tofauti na tumaini, kwa sababu imani ni “uhakika wa mambo yatarajiwayo.” Tumaini hutoa nafasi kwa mashaka. Tumaini kila wakati linasema, “labda”. Mfano: Ninaweza kusema hivi: “Natumaini leo mvua itanyesha ili shamba langu lipate maji.” Ni kwamba natamani mvua, lakini sina hakika kama itanyesha. Lakini imani ina uhakika wakati wote, “wa mambo yatarajiwayo.”

Kile ambacho watu wanaita imani mara nyingi si imani kwa tafsiri ya Biblia. Wanaweza kutazama mawingu meusi juu na kusema, “Naamini mvua itanyesha.” Ila, hawana hakika kwamba itanyesha – wao wanafikiri tu kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba pengine itanyesha. Hiyo si imani ya KiBiblia. Imani ya Biblia haina sehemu ya mashaka. Haitoi nafasi yoyote kwa chochote kingine isipokuwa kile ambacho Mungu ameahidi.

Imani Ni Uhakika Wa Mambo Yasiyo-onekana

Tafsiri ipatikanayo katika Waebrania 11:1 pia inasema kwamba imani ni “bayana ya mambo yasiyo-onekana.” Basi, kama tunaweza kuona kitu au kukitambua kwa hisia zetu tano, imani haitakiwi.

Hebu fikiri kwamba mtu hivi: “Kwa sababu ambayo siwezi kueleza, nina imani kwmaba kuna kitabu mikononi mwako.” Bila shaka ungedhani kwamba ana matatizo fulani. Ungemwambia hivi: “Ha! Huna haja ya kuamini kwamba nina kitabu mikono mwangu, maana unaweza kuona dhahiri kabisa kwamba nimeshika kitabu.”

Imani ni ya dunia isiyo-onekana na macho. Kwa mfano: Ninapoandika maneno haya, ninaamini kwamba kuna malaika karibu na mimi. Yaani, nina hakika kabisa. Ninawezaje kuw ana uhakika kiasi hicho? Je, nimemwona? Hapana. Je, nimehisi au kusikia malaika akiruka karibu? Hapana. Kama ningekuwa nimemwona au kumsikia au kuguswa na mmoja, nisingekuwa na haja ya kuamini kwamba kuna malaika karibu nami – ningejua kwamba yupo.

Basi, ni kitu gani kinachonifanya kuwa na hakika kwamba malaika yupo? Uhakika wangu unatokana na ahadi moja ya Mungu. Katika Zaburi 34:7, aliahidi hivi: “Malaika wa Bwana hufanya kituo karibu na wale wamchao, na kuwaokoa” (TLR). Sina ushahidi wa kile ninachoamini isiokuwa Neno la Mungu. Hiyo ndiyo imani ya kweli ya Biblia – ‘bayana ya mambo yasiyo-onekana’. Watu wa dunia mara nyingi wanatumia msemo huu: “Kuona ni kuamini.” Katika ufalme wa Mungu ukweli ni kinyume: “Kuamini ni kuona.”

Tunapofanyia kazi imani yetu kuhusu ahadi mojawapo ya Mungu, mara nyingi tunakabiliana na mazingira yatakayotujaribu kuwa na mashaka, au kupitia kipindi ambapo inaonekana kana kwamba Mungu hatimizi ahadi yake kwa sababu mazingira yetu hayabadiliki. Kwa hali hiyo, tunachohitaji kufanya ni kupinga mashaka, kudumu katika imani, na kuendelea kuamini mioyoni mwetu kwamba Mungu siku zote hutimiza Neno Lake. Yeye hawezi kudanganya kamwe (ona Tito 1:2).

Tunapataje Imani?

Kwa kuwa imani imejengwa kwenye ahadi za Mungu tu, kuna mahali pamoja tu pa kupata imani ya KiBiblia – Neno la Mungu. Warumi 10:17 inasema hivi: “Basi, imani huja kwa kusikia, Neno la Kristo (TLR, maneno mepesi kutilia mkazo). Neno la Mungu hufunua mapenzi Yake. Tunapoyajua mapenzi ya Mungu ndipo tunapoweza kuyaamini.

Basi, ukitaka kuwa na imani, lazima usikie (au usome) ahadi za Mungu. Imani haiji kwa maombi, kwa kufunga, au kwa mtu kukuwekea mikono ili uipate. Inakuja kwa kusikia Neno la Mungu. Na, ukiisha kulisikia, bado inakubidi ufanye uamuzi kuliamini.

Zaidi ya kupata imani, imani yetu pia inaweza kuwa na nguvu. Biblia inataja viwango kadhaa vya imani – kutoka imani ndogo hadi imani yenye kuhamisha milima. Imani hukua na kupata nguvu sana inapolishwa na kufanyiwa kazi, sawa tu na musuli ya kibinadamu. Tunapaswa kuendelea kuilisha imani yetu kwa kutafakari Neno la Mungu. Tunapaswa kuifanyisha kazi kwa kutenda na kuitikia kila kitu kulingana na Neno la Mungu. Hata nyakati zile tunapokabiliana na matatizo, wasiwasi na mambo yanayotusumbua. Mungu hataki watoto Wake kuwa na wasiwasi kuhusu lolote, bali kumtumaini katika kila hali (ona Mathayo 6:25-34; Wafilipi 4:6-8; 1Petro 5:7). Kukataa kuwa na wasiwasi ni njia moja ya kufanyia kazi imani yetu.

Kama kweli tunaamini aliyosema Mungu, tutatenda na kusema kana kwamba ni kweli. Ukiamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, utasema na kutenda kama mtu anayeamini hayo. Kama unaamini kwamba Mungu atakupa mahitaji yako yote, utasema na kutenda hivyo. Ukiamini kwamba Mungu anataka uwe mwenye afya, utatenda nakuzungumza hivyo. Biblia imejaa mifano ya watu ambao wakiwa katikati ya mazingira magumu, walifanyia kazi imani yao katika Mungu na wakapata miujiza. Tutawatazama baadhi yao katika sura hii baadaye, na katika sura inayofuata kuhusu uponyaji wa Mungu. (Ukitaka mifano mingine mizuri, tazama 2Wafalme 4:1-7; Marko 5:25-34; Luka 19:1-10 na Matendo 14:7-10).

Imani Ni Kitu Cha Moyo

Imani ya KiBiblia haifanyi kazi katika akili zetu – ni moyoni. Paulo aliandika hivi: “Maana kwa moyo mtu huamini” (Warumi 10:10a, TLR). Yesu naye alisema hivi:

Yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini’, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake (Marko 11:23. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Yawezekana kabisa kuwa na mashaka kichwani mwako na ukawa bado na imani moyoni mwako na kupokea kile ambacho Mungu ameahidi. Ukweli ni kwamba mara nyingi tunapojaribu kuamini ahadi za Mungu, aili zetu, zikishawishiwa na hisia zetu za kimwili na uongo wa Shetani, hushambuliwa na mashaka. Katika nyakati hizo tunahitaji kuondoa mawazo yenye mashaka na kutia ahadi za Mungu mahali pake, na kudumu katika imani bila ya kusita au kuyumba.

Makosa Ya Kawaida Kuhusu Imani

Tunapojaribu kuwa na imani katika Mungu, wakati mwingine tunashindwa kupokea tunachotaka kwa sababu hatufanyi kulingana na Neno la Mungu. Kosa moja la kawaida sana hutokea wakati tunapojaribu kuamini kupata kitu ambacho Mungu hajatuahidi.

Kwa mfano: Ni halali KiMaandiko kwa wenye ndoa kumwamini Mungu kupata watoto kwa sababu Neno la Mungu lina ahadi ambayo wanaweza kuisimamia. Ninajua wana ndoa ambao wameambiwa na daktari kwamba hawatapata watoto. Wao waliamua kumwamini Mungu, wakisimama kwenye ahadi mbili zinazofuata hapo chini, na leo hii ni wazazi wa watoto wenye afya nzuri sana.

Nanyi mtamtumikia BWANA Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba wala aliye tasa katika nchi yako; na hesabu ya siku zao nitaitimiza (Kutoka 23:25-26).

Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo (Kumbu. 7:14).

Ahadi hizi ziwatie moyo wana ndoa wasiokuwa na watoto! Lakini, kujaribu kuamini kwamba lazima mtoto awe mvulana au msichana ni jambo lingine. Katika Biblia hakuna ahadi zinazosema tutachagua jinsia ya watoto tutakaozaa. Lazima tukae katika mipaka ya Neno la Mungu kama tunataka imani yetu itende kazi. Tunaweza kumwamini Mungu kwa kile alichotuahidi tu.

Hebu tuone ahadi nyingine ya Neno la Mungu, kisha tuamue tunachoweza kuamini kutokana na ahadi hiyo.

Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza (1Wathes. 4:16).

Kutokana na andiko hilo, tunaweza kuamini kabisa kwamba Yesu atarudi. Lakini je, tuombe na kuamini kwamba Yesu atarudi kesho? Hapana, kwa sababu andiko hili halituahidi hivyo, wala lingine lolote. Tena, Yesu mwenyewe alisema hakuna ajuaye saa wala siku ya kurudi Kwake.

Ila, tunaweza kuomba tukitumaini kwamba Yesu anaweza kurudi kesho, lakini hatuna uhakika kwamba itatokea kama tunavyoomba. Tunapoomba kwa imani, tuna hakika kwamba kile tunachokiomba kitatokea kwa sababu tuna ahadi ya Mungu kuhusiana nacho.

Kwa andiko hilo hilo, tunaweza kuamini kwamba miili ya wale waaminio waliokufa itafufuliwa wakati Yesu atakaporudi. Lakini je, sisi tulio hai wakati wa kurudi kwa Kristo tuamini kwamba tutapokea miili ya ufufuo wakati huo huo kama “waliokufa katika Kristo”, au hata kabla yao? Hapana, maana andiko hili linatuambia tofauti kabisa, kwamba: Wale “waliokufa katika Kristo” watafufuliwa kwanza.” Mstari unaofuata unaendelea hivi: “Kisha sisi tulio hai tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu” (1Wathes. 4:17). Basi, hakuna uwezekano kwamba “waliokufa katika Kristo” hawatakuwa wa kwanza kupokea miili yao ya ufufuo wakati Yesu atakaporudi. Neno la Mungu limeahidi kwamba watakuwa wa kwanza.

Hivyo – kama tunatakiwa kumwamini Mungu kwa habari ya kitu fulani, lazima tuwe na uhakika kwamba ni mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu kupokea tunachotaka. Mapenzi ya Mungu yanaweza kujulikana vizuri sana kwa kutazama ahadi Zake zilizoandikwa katika Biblia.

Imani inafanya kazi hivyo hivyo katika dunia ya kawaida. Utakuwa mjinga kuamini kwamba nitakutembelea nyumbani kesho mchana kama sikuwa nimekuahidi hivyo.

Imani bila ahadi ya kuisimamia, si imani kweli – ni upumbavu. Kwa hiyo – kabla hujamwomba Mungu chochote, kwanza jiulize swali hili – ni andiko gani katika Biblia linaloniahidi kile ninachotaka? Kama huna ahadi, huna msingi wa imani yako.

Kosa La Pili La Kawaida

Mara nyingi Wakristo hujaribu kutegemea ahadi moja ya Mungu kutimizwa maishani mwao bila ya kutimiza masharti yote yenye kuambatana na ahadi yenyewe. Kwa mfano: Nimesikia Wakristo wengi wakirejea maneno ya Zaburi 37 na kusema hivi: “Biblia inasema Mungu atanipa matakwa ya moyo wangu. Ninamwamini kwa hilo.”

Tatizo ni kwamba, Biblia haisemi tu kwamba Mungu atatupa matakwa ya mioyo yetu. Angalia inachosema:

Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini BWANA ukatende mema, ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa BWANA, naye atakupa haja za moyo wako. Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya (Zaburi 37:1-5).

Kuna masharti kadha ambayo lazima tutumize ikiwa tunataka kumwamini Mungu atupe matakwa ya moyo. Ukihesabu utaona masharti nane katika ahadi hiyo. Tusipotimiza masharti hayo, hatuna haki ya kupokea baraka zilizoahidiwa. Imani yetu inakuwa haina msingi.

Pia, Wakristo wanapenda kureje ahadi inayopatikana katika Wafilipi 4:19, kwamba “Mungu wangu atanipa mahitaji yangu yote kulingana na utajiri Wake katika utukufu.” Sawa – je, kuna masharti katika ahadi hiyo? Bila shaka.

Ukichunguza mantiki ya ahadi ya Wafilipi 4:19, utaona kwamba si ahadi itolewayo kwa Wakristo wote. Ila ni ahadi itolewayo kwa Wakristo ambao ni watoaji. Paulo alijua Mungu angewapa Wafilipi mahitaji yao yote kwa sababu walikuwa wamemtumia sadaka. Kwa kuwa walitafuta kwanza ufalme wa Mungu kama Yesu alivyoagiza, Mungu angewapa mahitaji yao yoe, kama Yesu alivyoahidi (Mathayo 6:33). Ahadi nyingi katika Biblia zinazohusu Mungu kutupa mahitaji yetu ya kawiada zina sharti kwamba sisi tuwe watoaji kwanza.

Kweli hatuna haki ya kumtumaini Mungua kutane na mahitaji yetu kama hatutii amri Zake kuhusu fedha yetu. Katika agano la kale, Mungualiwaambia watu Wake kwamba walikuwa wamelaaniwa maana hawakuwa wanatoa zaka zao. Ila, aliahidi kuwabariki kama wangetoa zaka na sadaka zao kwa uaminifu na kwa utii (ona Malaki 3:8-12).

Baraka nyingi zilizoahidiwa kwetu katika Biblia zinategemeana na sisi kumtii Mungu. Basi, kabla ya kujaribu kumwamini Mungu kwa kitu fulani, tujiulize kwanza hivi: “Je, ninatimiza masharti yanayoambatana na ahadi hiyo?”

Kosa La Kawaida La Tatu

Katika Agano Jipya, Yesu aliweka sharti ambalo linafanya kazi kila wakati tunapo-omba kuhusu kitu.

Mwaminini Mungu. Amin nawaambia, ‘Yeyote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu (Marko 11:22-24, maneno mepesi kutilia mkazo).

Sharti ambalo Yesu alitaja ni kuamini kwamba tumekwisha pkea tunapoomba. Wakristo wengi hukosea kwa kujaribu kufanyia kazi imani yao kwa kuamini kwamba wamepokea wanapo-ona jibu la maombi yao. Wanaamini kwamba watapokea, si kwamba wamekwisha pokea.

Tunapomwomba Mungu kitu ambacho ametuahidi, tunatakiwa kuamini kwamba tunapoikea jibu wakati tunapo-omba, kisha tuanze kumshukuru Mungu kwa jibu wakati huo. Lazima tuamini kwamba tumejibiwa kabla ya kuona, si baada ya kuona. Tunatakiwa kumjulisha Mungu haja zetu pamoja na shukrani, kama anavyoandika Paulo.

Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu (Wafilipi 4:6).

Kama tulivyokwisha ona, tukiwa na imani mioyoni mwetu, maneno yetu na matendo yetu vitalingana na kile tunachoamini. Yesu alisema hivi: “Mdomo hunena yale yaujayazo moyo” (Mathayo 12:34).

Kuna Wakristo wengine wanaofanya kosa la kurudia kuomba kitu kile kile. Hiyo inadhihrisha kwamba hawajaamini bado kwamba wamekipokea. Kama tunaamini kwamba tunapokea tunapoomba, hakuna haja ya kurudia kuomba ombi lile lile. Kurudia kuomba kitu kile kile ni kuonyesha mashaka kwamba Mungu hakutusikia tulipomwomba mara ya kwanza.

Je, Yesu Hakurudia Ombi Zaidi Ya Mara Moja?

Yesu alirudia ombi moja mara tatu, alipokuwa anaomba katika Bustani ya Getsemane (ona Mathayo 26:39-44). Lakini kumbuka hakuwa anaomba kwa imani kulingana na mapenzi ya Mungu. Alipoomba mara hizo tatu ili ikiwezekana asiende msalabani, alijua kwamba ombi Lake lilikuwa kinyume na mapenzi ya Mungu. Ndiyo sababu alijinyenyekeza kwa mapenzi ya Baba Yake mara tatu pia katika sala hiyo hiyo.

Hiyo sala mara nyingi hutumiwa kimakosa kwamba ni mfano wa maombi yote, maana kuna wengine wanaofundisha kwamba kila sala inapaswa kumalizika kwa kusema hivi: “Kama ni mapenzi Yako” au “Si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi Yako yatendeke.”

Hapa tena tunapaswa kukumbuka kwamba Yesu alikuwa anaomba kitu alichojua kwamba si mapenzi ya Mungu. Kufuata mfano Wake wakati sisi tunaomba kitu kulingana na mapenzi ya Mungu ni kosa, na kutokuwa na imani. Kwa mfano: Kuomba hivi: “Bwana! Naungama dhambi yangu kwako, nami naomba unisamehe ikiwa ni mapenzi Yako” ni kuonyesha kwamba yawezekana si mapenzi ya Mungu kusamehe dhambi yangu. Tunajua kwamba Biblia inaahidi Mungu atatusamehe tunapoziungama dhambi zetu (ona 1Yohana 1:9). Hivyo, sala kama hiyo itadhihrisha kutokuwa na imani kwa mtu, kuhusu mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa wazi.

Yesu hakumaliza kila sala kwa kusema, “Si kama nitakavyo mimi, bali mapenzi Yako yatimizwe.” Kuna mfano mmoja tu wa Yeye kuomba hivyo, na ni wakati alipokuwa anajitolea kufanya mapenzi ya Baba Yake, akijua mateso ambayo angepitia kwa sababu hiyo.

Kwa upande mwingine, kama hatujui mapenzi ya Mungu katika hali fulani kwa sababu hajayafunua, basi inafaa kumalizia maombi yetu kwa maneno haya: “Kama ni mapenzi yako.” Yakobo aliandika hivi:

Haya basi ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya (Yakobo 4:13-16).

Tufanye nini tukiisha omba kulingana na ahadi ya Mungu, na kutimiza masharti yote? Tuendelee kumshukuru Mungu kwa majibu ambayo tumeamini kwamba tumeyapokea mpaka tupokee tulichokiomba. Tunapokea na kurithi ahadi za Mungu kwa imani na subira (Waebrania 6:12). Shetani atajaribu kutushinda kwa kuleta mashaka, nasi lazima tutambue kwamba akili zetu ndiyo uwanja wa mapambano. Wakati mawazo ya mashaka yanaposhambulia akili zetu, tunahitaji kuyabadilisha kwa mawazo yenye msingi kwenye ahadi za Mungu na kulitamka Neno la Mungu kwa imani. Tukifanya hivyo, Shetani lazima akimbie (ona Yakobo 4:7; 1Petro 5:8-9).

Mfano Wa Imani Katika Matendo

Mfano mmoja maarufu sana katika Biblia kuhusu imani katika matendo ni habari ya Petro akitembea juu ya maji. Hebu tusome habari yenyewe, tuone tutajifunza nini.

Mara [Yesu] akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi, maana upepo ulikuwa wa mbisho. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari wakafadhaika wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena akawaambia, Jipeni moyo, ni mimi, msiogope. Petro akamjibu akasema, Bwana! Ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe akisema, Bwana, niokoe. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka? Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu! (Mathayo 14:22-33).

Kabla ya hapa, wanafunzi wa Yesu walikuwa wamenaswa katika dhoruba nyingine kali wakiwa mtumbwini katika Bahari ya Galilaya (ona Mathayo 8:23-27). Wakati wa tukio hilo, Yesu alikuwa nao, na baada ya kutuliza dhoruba kwa neno lake, aliwakemea wanafunzi Wake kwa kutokuwa na imani kwao. Kabla ya kuanza safari alikuwa amewaambia kwamba ni mapenzi Yake wavuke hadi ng’ambo ya pili ya ziwa (Marko 4:35). Lakini, dhoruba ilipotokea, walishawishika zaidi na mazingira yao, na kuna wakati waliamini watakufa wote. Yesu alitazamia haidhuru wasiogope basi.

Safari hii, Yesu aliwatuma wavuke ng’ambo ya ziwa wakiwa peke yao. Hakika aliongozwa na Roho kufanya hivyo, na hakika Mungu alijua kwamba upepo wa mbisho ungetokea usiku huo. Kwa hiyo Bwana aliwaruhusu wakabiliwe na changamoto ndogo tu kwa imani yao. Kwa sababu ya hizo pepo za mbisho, safari ambayo ingechukua masaa machache tu ilichukua usiku kucha. Kweli tunastahili kuwasifu wanafunzi kwa jitihada zao, lakini hatuachi kushangaa ikiwa kuna mmoja wao aliyejaribu hata kuwa na imani kwamba hizo pepo zitulie – kitu ambacho walikuwa wamemwona Yesu akifanya siku chache kabla ya hapo. Cha ajabu ni kwamba, katika Injili ya Marko, tunasoma kwamba wakati Yesu alipowaendea akitembea juu ya maji, “akataka kuwapita” (Marko 6:48). Alikuwa anataka awaache wakabiliane na tatizo lao peke yao, huku yeye anapita hapo kimuujiza! Hii inaonyesha kwamba hawakuwa wanaomba au kumtazama Mungu. Changamoto kwetu ni kwamba Mtenda Miujiza hutupita mara ngapi tunapong’ang’ana na maisha dhidi ya upepo wa matatizo.

Kanuni Za Imani

Yesu aliitikia wito wa Petro kwa neno moja tu: “Njoo.” Kama Petro angejaribu kutembea juu ya maji kabla ya neno hilo, angezama mara moja, maana asingekuwa na ahadi ya kutegemeza imani yake. Angekuwa anajitokeza kwa kudhania badala ya imani. Vile vile hata baada ya Yesu kusema neno Lake, kama mwanafunzi mwingine yeyote angejaribu kutembea juu ya maji, angezama mara moja, kwa sababu Yesu alimpa Petro tu ahadi. Hakuna mwingine ambaye angeweza kutimiza masharti ya ahadi hiyo, maana hawakuwa Petro. Basi, kabla yeyote kati yetu hajajaribu kutegemea ahadi moja ya Mungu, lazima kuhakikisha kwamba ahadi hiyo ni yetu na kwamba tunatimiza masharti yake.

Petro akaweka mguu kwenye maji. Hapo ndipo alipoamini, japo hakuna shaka kwamba yeye aliyekuwa anapiga kelele kwa kuogopa mzuka muda mfupi kabla ya hapo, pia alikuwa na mashaka ichwani mwake alipopiga hatua ya kwanza. Lakini ili aweze kupokea muujiza, ilibidi afanyie kazi imani yake. Kama angeshikilia mlingoti wa mtumbwi na kutia dole gumba la mguu ndani ya maji aone kama maji yana uwezo wa kumbeba, asingepata muujiza. Vivyo hivyo na sisi – kabla ya kupokea muujiza wowote, lazima tujitolee kuamini ahadi ya Mungu, kisha tutende kama tunavyoamini. Kila mara kuna wakati ambapo imani yetu lazima ipimwe. Wakati mwingine kipindi ni kifupi, wakati mwingine kirefu. Lakini kuna muda ambapo itabidi tupuuze ushahidi wa hisia zetu na kutenda kulingana na Neno la Mungu.

Petro aliendelea vizuri mwanzoni. Lakini alipotafakari jinsi hicho alichokifanya kisivyowezekana, akikumbuka upepo na mawimbi, aliogopa. Pengine aliacha kutembea, akihofia hatua inayofuata. Sasa – yeye aliyekuwa anapokea muujiza akajikuta anazama. Twahitaji kuendelea katika imani tukiisha anza – kuendelea kutenda kulingana na imani yetu. Tuzidi kusonga mbele.

Petro alizama kwa sababu alikuwa na mashaka. Mara nyingi watu hawapendi kujilaumu wenyewe kwa kukosa imani kwao. Wanaona ni afadhali kumlaumu Mungu. Lakini, unadhani Yesu angeitikiaje kama angemsikia Petro, baada ya kurudi mtumbwini salama, akiwaambia wanafunzi wenzake hivi: “Kweli, mpango wa Mungu kwa ajili yangu ilikuwa kufika hapo nilipofika?”

Petro alishindwa kwa sababu aliogopa, akapoteza imani. Huo ndiyo ukweli. Yesu hakumlaumu, bali alinyosha mkono wake mara moja kumpa Petro kitu thabiti zaidi cha kushika. Na mara moja akamhoji Petro kwa nini aliona shaka. Petro hakuwa na sababu yoyote nzuri ya kuwa na shaka, kwa sababu neno la Mwana wa Mungu ni thabiti kuliko kitu chochote. Hakuna yeyote kati yetu mwenye sababu nzuri ya kutilia shaka Neno la Mungu, au kuogopa, au kuwa na wasiwasi.

Maandiko yamejaa ushindi ambao ulitokana na imani, na kushindwa kulikotokana na mashaka. Yoshua na Kalebu waliingia Nchi ya Ahadi kwa sababu ya imani yao. Wenzao wengi walikufa jangwani kwa sababu ya mashaka yao (ona Hesabu 14:26-30). Wanafunzi wa Yesu walipata mahitaji yao waliposafiri wawili wawili kuhubiri Injili (Luka 22:35), lakini waliwahi kushindwa kutoa pepo kwa sababu ya kutokuamini kwao (ona Mathayo 17:19-20). Wengi walipokea miujiza ya uponyaji katika huduma ya Kristo, lakini wagonjwa wengi katika mji wa Nazareti – nyumbani Kwake – walibakia wagonjwa kwa sababu ya kutoamini kwao (Marko 6:5-6).

Kama wote, hata mimi nimepata mafanikio na kushindwa kulingana na imani yangu au mashaka yangu. Lakini sitaskia uchungu kwa kushindwa kwangu au kumlaumu Mungu. Sitajihesabia haki kwa kumlaumu Yeye. Sitatafuta maelezo yasiyoeleweka kirahisi, yenye kutengeneza upya mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa wazi. Najua Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo, ninaposhindwa, ninatubu kutokuamini kwangu na kuanza kutembea juu ya maji tena. Nimeona kwamba Yesu kila mara ananisamehe na kuniokoa nisizame!

Tunamalizia hivi: Waamini hubarikiwa; wenye mashaka hawabarikiwi! Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi hufuata mfano wa Yesu. Yeye mwenyewe amejaa imani, na anawashauri wanafunzi wake hivi: “Mwaminini Mungu!” (Marko 11:22).

Swala La Talaka Na Kuoa Tena

Sura Ya Kumi Na Tatu

Jambo la talaka na kuoa tena baada ya talaka hujadiliwa sana miongoni mwa Wakristo wa kweli. Yapo maswali mawili ambayo ndiyo msingi wa mjadala huo. (1) Ni wakati gani – kama upo – ambapo talaka inaruhusiwa machoni pa Mungu? Na (2) Ni wakati gani – kama upo – ambapo kuoa tena kunaruhusiwa machoni pa Mungu? Madhehebu mengi na makanisa binafsi yana msimamo rasmi kimafundisho kuhusu kinachoruhusiwa na kisichoruhusiwa, kutokana na tafsiri yao ya Maandiko. Tunapaswa kuwaheshimu wote kw akuwa na misimamo na kuishi kulingana nayo – ikiwa misimamo hiyo inasukumwa na kumpenda Mungu kwao. Hakika ingekuwa vizuri kama sisi wote tungekuwa na misimamo ambayo inaungwa mkono na Maandiko mia kwa mia. Mchungaji anayefanya wengine kuwa wanafunzi hataki kufundisha kitu kinachopungua kwenye kusudi la Mungu. Wala hataki kuweka mizigo juu ya watu, ambayo Mungu hakukusudia wao waibebe. Basi, hayo yakiwa hivyo, hebu nijitahidi kufasiri Maandiko yanayohusiana na mada hii tata, na kukuacha wewe uamue kama unakubaliana na tafsiri hiyo au hapana.

Nianze kwa kusema kwamba mimi – kama wewe – nahuzunishwa sana na ukweli kwamba talaka imezidi sana duniani siku hizi. Kibaya zaidi ni kwamba kuna Wakristo wengi wanaoachana na wenzao, hata walio katika huduma. Hili ni janga kubwa sana. Tunahitaji kufanya kila kinachowezekana ili kuzuia hayo kuongezeka, na ufumbuzi mzuri zaidi wa tatizo la talaka ni kuhubiri Injili na kuwaita watu kutubu. Wakati watu wawili wenye ndoa wanapokuwa wamezaliwa tena kweli kweli na wote wanamfuata Kristo, hawataachana. Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi atafanya kila anachoweza kuimarisha ndoa yake, akijua kwamba mfano wa maisha yake ndiyo mwalimu mkuu.

Niseme pia kwamba mimi nina ndoa yenye furaha sana ya miaka zaidi ya ishirini na tano, na sijawahi kuoa kabla ya ndoa hii. Siwezi kufikiri kwamba tutakuja kuachana. Kwa hiyo, sina kusudi lolote la kurahisisha maandiko magumu yanayohusu kuachana kwa faida yangu mwenyewe. Ila, ninawahurumia sana watu walioachana, nikijua kwamba hata mimi nilipokuwa kijana ningeweza kufanya uamuzi mbaya kirahisi tu, na kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye baadaye ningejaribiwa sana kumwacha, au mtu ambaye asingeweza kuchukuliana nami kama huyu niliye na ndoa naye. Yaani, ningeishia kwenye talaka, lakini haijawa hivyo kwa sababu ya neema ya Mungu. Nadhani watu wengi wenye ndoa wanaelewa ninachosema. Basi, tunahitaji kujizuia tusitupe mawe kwa watu walioachana. Kwani sisi ni nani, wenye ndoa zisizo na matatizo sana, kuwahukumu walioachana, bila ya kujua wamepitia nini? Mungu anaweza kuwahesabu kuwa wenye haki kuliko sisi, maana anajua kwamba sisi, kama tungekuwa katika hali kama hizo, pengine tungevunja ndoa mapema zaidi.

Hakuna anayeoa akitazamia kuvunja ndoa, na sidhani kama kuna wanaochukia kuachana kama waliokwisha achana. Kwa hiyo, tujaribu kuwasaidia watu wenye ndoa kuendelea kuwa katika ndoa, na tuwasaidie walioachana kupata neema yoyote ile ambayo Mungu anaitoa kwa watu kama wao. Ninaandika ninayoandika kwa misingi hiyo.

Nitajitahidi sana kuruhusu maandiko yafafanue mengine. Nimeona kwamba mistari inayohusu mada hii mara nyingi hutafsiriwa kwa njia kwamba inapingana na Maandiko mengine, ambayo ni ishara kwamba haijaeleweka vizuri kwa sehemu.

Msingi

Hebu tuanze kwa kweli ya msingi ambayo sote tutakubaliana nayo. Ni hivi: Maandiko yanasema wazi kwamba Mungu hapendi kuachana kwa ujumla. Katika kipindi ambapo wanaume fulani wa KiIsraeli walikuwa wanatalakiana na wake zao, alitamka hivi kupitia nabii wake aitwaye Malaki:

Maana mimi nakuchukia kuachana … naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia … Basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana (Malaki 2:16).

Hilo si jambo la kushangaza kwa mtu yeyote ajuaye tabia ya Mungu ya upendo na haki, au mtu anayejua jinsi kuachana kunavyoharibu waume, wake na watoto. Mtu anayekubaliana na talaka kwa ujumla tungehoji tabia yake. Mungu ni upendo (ona 1Yohana 4:8), na kwa sababu hiyo anachukia talaka.

Kuna wakati fulani ambapo baadhi ya Mafarisayo walimwuliza Yesu swali kuhusu uhalali wa talaka “kwa sababu yoyote” (TLR). Jibu lake linaonyesha jinsi asivyokubali talaka. Tena, talaka halikuwa kusudi Lake kwa yeyote yule.

Basi Mafarisayo wakamwendea wakamjaribu wakimwambia, ‘Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?’ Akajibu akawaambia, ‘Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe’ (Mathayo 19:3-6).

Tunajua kihistoria kwamba yalikuwepo makundi mawili yaliyokuwa na mitazamo tofauti katika vongozi wa kidini wa Kiyahudi wakati wa Yesu. Tutatazama mitazamo ya makundi hayo mawili kwa upana zaidi baadaye, lakini kwa sasa inatosha tu kusema kwamba kundi moja lilikuwa na msimamo mkali na lingine msimamo mwepesi. Wenye msimamo mkali waliamini kwamba mwanamume aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu nzito sana kiadili. Wale wenye msimamo mwepesi waliamini kwamba mwanamume aliruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu yoyote ile, hata kama amempata mwanamke mrembo zaidi. Mitazamo hiyo miwili tofauti ndiyo ilisababisha swali la Mafarisayo kwa Yesu.

Yesu akarejea kwenye mistari ya Maandiko kutoka kurasa za kwanza kabisa za kitabu cha Mwanzo, yenye kuonyesha jinsi ambavyo mpango wa kwanza wa Mungu ulikuwa kuwaunganisha wanaume na wanawake pamoja daima, si kwa muda tu. Musa alisema kwamba Mungu aliumba jinsia hizo mbili akilenga ndoa, na kwamba ndoa ni uhusiano wa maana sana kiasi cha kwamba ndiyo wa msingi – au, ndiyo wa kwanza kabisa. Ukiisha undwa, ni wa hali ya juu kuliko mahusiano ya mtu na wazazi wake. Wanaume wanaachana na wazazi wao ili kuambatana na wake zao.

Tena, muungano wa kimwil katika tendo la ndoa baina ya mwanamume na mkewe huonyesha mpango wa Mungu kwao kwamba wawe mwili mmoja. Ni dhahiri kwamba uhusiano wa aina hiyo – ambao unasababisha kuzaa – haukukusudiwa na Mungu uwe wa muda, bali wa kudumu. Jinsi Yesu alivyojibu swali la Mafarisayo lilionyesha kuvunjwa moyo Kwake kwamba wamediriki kuuliza hata swali la aina hiyo. Hakika Mungu hakukusudia kwamba wanaume waachane na wake zao “kwa sababu yoyote.”

Mungu hakukusudia kwamba yeyote atende dhambi kwa namna yoyote ile, lakini wote tumefanya dhambi. Kwa rehema zake, Mungua liweka mpango wakutuokoa kutokana na utumwa wetu wa dhambi. Tena, ana mambo ya kutuambia baada ya kufanya yale ambayo hakutaka tuyafanye. Vivyo hivyo, Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na mwenzake, lakini talaka ikawa haiepukiki kwa watu wasiojitoa kwa Mungu. Mungu hakushangazwa na talaka ya kwanza, wala zile zilizofuata kwa mamilioni. Basi, hasemi tu kwamba anachukia kuachana, lakini pia ana mambo ya kuwaambia watu baada ya kuachana.

Hapo Mwanzo

Baada ya kuweka msingi, tunaweza sasa kuendelea kuchunguza zaidi mambo ambayo Mungu amesema kuhusu talaka na kuoa tena. Kwa kuwa maneno mengi yenye kuleta utata kuhusu talaka na kuoa tena ni yale ambayo Yesu aliwaambia Waisraeli, itatusiadia kwanza kuona Mungu alichosema miaka mia nyingi kabla, juu ya jambo hilo hilo kwa Waisraeli wa zamani. Tukikuta kwamba alichosema Mungu kwa njia ya Musa na alichosema Mungu kwa njia ya Yesu vinapingana, basi tujue kwamba sheria ya Mungu ilibadilika au kwamba sisi tumetafsiri isivyo kitu fulani kilichosemwa na Musa au na Yesu. Basi, tuanze kwa kutazama yale ambayo Mungu alifunua hapo mwanzo kuhusu talaka na kuoa tena baada ya talaka.

Tayari nimekwisha taja Maandiko ya Mwanzo 2 ambayo kulingana na Yesu, yana umuhimu kwa mada ya talaka. Hebu sasa tuyaone moja kwa moja kutoka Mwanzo kwenyewe.

Na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, ‘Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kw ahiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (mwanzo 2:22-24).

Basi huo ndiyo mwanzo wa ndoa. Mungu alimfanya mwanamke wa kwanza kutoka kwa mwanamume wa kwanza, na kwa ajili ya mwanamume wa kwanza, kisha Yeye Mwenyewe binafsi akamleta kwa Adamu. Yesu anaeleza hilo hivi, “Mungu … aliwaunganisha [pamoja]” (Mathayo 19:6, maneno mepesi kutilia mkazo). Hii ndoa ya kwanza iliyopangwa na Mungu ikatoa mfano kwa ajili ya ndoa zingine zote zilizofuata. Mungu huumba wanawake wa kutosha wanaume, Naye huwaumba ili kila mmoja avutiwe na mwenzake. Tunaweza kusema kwamba Mungu bado anapanga ndoa za watu kwa hali ya juu sana (japo siku hizi kuna wanaoweza kuwa wenzi wengi zaidi kwa kila mtu kuliko ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa). Basi, kama Yesu alivyosema, mwanadamu yeyote asitenganishe wale ambao Mungu amewaunganisha. Halikuwa kusudi la Mungu kwamba wale wana ndoa wa kwanza waishi maisha binafsi kila mmoja, bali kwamba wapate baraka katika kuishi pamoja kwa hali ya kutegemeana. Kuhalifu mapenzi ya Mungu yaliyo dhahiri ni dhambi. Basi, kutoka katika sura ya pili ya Biblia, ukweli ni kwamba talaka haikuwa kusudi la Mungu kwa ndoa yoyote ile.

Sheria Za Mungu Kuandikwa Mioyoni

Pia niseme kwamba hata wale ambao hawajawahi kusoma sura ya pili ya Mwanzo wanajua ndani yao kwamba talaka ni kosa, kwa sababu agano la ndoa za maisha ni kawaida katika tamaduni nyingi tu za kipagani, ambapo hakuna maarifa yoyote ya Biblia. Kama alivyoandika Paulo katika barua yake kwa Warumi:

Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao wakionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao yenyewe kwa yenyewe, yakiwashtaki au kuwatetea (Warumi 2:14-15).

Taratibu za Mungu za maadili zimeandikwa katika moyo wa kila mwanadamu. Ukweli ni kwamba kanuni hiyo ya maadili inayozungumza kupitia dhamiri ndiyo sheria pekee ambayo Mungu aliwahi kumpa yeyote, isipokuwa Waisraeli, tangu Adamu mpaka wakati wa Yesu. Yeyote anayefikiri talaka atagundua kwamba kuna dhamiri ya kushughulika nayo. Na njia ya pekee ya kuishinda dhamiri yake ni kutafuta haki nzuri kwa ajili ya talaka. Akiendelea na talaka bila ya haki nzuri, dhamiri yake itamshtaki, hata kama atajaribu kuigandamiza.

Kwa kadiri tunavyofahamu, tangu Adamu mpaka wakati wa kutolewa Torati ya Musa kwa Waisraeli mwaka wa 1440 KK, sheria ya dhamiri ndiyo ufunuo pekee ambao Mungu alitoa kwa yeyote kwa vizazi 27 hivi – hata kwa Waisraeli – kuhusiana na talaka na kuoa tena. Na Mungu alihesabu kwamba hiyo inatosha. (Kumbuka tu kwamba Musa hakuandika habari za uumbaji katika Mwanzo 2 mpaka wakati wa Kutoka Misri.) Basi, ni halali kabisa kufikiri kwamba katika kipindi cha vizazi hivyo 27 kabla ya Torati ya Musa – ambapo ni pamoja na kipindi cha gharika ya Nuhu – kiasi fulani cha ndoa katika zile milioni nyingi za miaka mia nyingi zilimalizika kwa kuachana. Pia inaonekana ni sawa kusema kwamba, Mungu asiyebadilika, alikuwa tayari kuwasamehe wale waliopatikana na hatia ya talaka kama walitubu na kuacha dhambi yao. Tuna hakika kwamba watu walikuwa wanaokoka au kutangazwa kuwa wenye haki na Mungu kabla ya Torati ya Musa kutolewa, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu kwa imani yake (ona Warumi 4:1-12). Kama watu waliweza kutangazwa kuwa wenye haki kwa njia ya imani yao – tokea Adamu hadi kwa Musa – maana yake ni kwamba wangeweza kusamehewa chochote, pamoja na dhambi ya talaka. Basi, tunapoanza kuchunguza swala la talaka na kuoa tena baada ya talaka, kuna swali hapa: Je, watu waliopatikana na dhambi katika talaka zao kabla ya Torati ya Musa, waliosamehewa na Mungu, waliweza kuhukumiwa na dhamiri zao na kupata hatia kama wangeoa tena? (Maana haikuwepo sheria iliyoandikwa.) Ni swali la kufikiri.

Vipi kuhusu wahanga wa talaka ambao hawakuwa na dhambi – yaani, walioachwa kwa kosa lisilokuwa lao, bali kwa sababu ya wenzi wenye ubinafsi? Je, dhamiri zao zingewazuia kuoa tena? Nadhani si hivyo. Kama mwanamume alimwacha mke wake kwa sababu ya mwanamke mwingine, nini kingemwongoza huyo mwanamke aliyeachwa kufikia uamuzi kwamba hana haki ya kuolewa tena? Maana, aliachwa, lakini si kosa lake.

Torati Ya Musa

Hatusomi habari za talaka na kuoa tena baada ya talaka mpaka tunapofikia kitabu cha tatu cha Biblia. Katika Torati ya Musa kulikuwa na agizo la kuwakataza makuhani kuona wanawake walioachwa.

Wasimwoe mwanamke aliye kahab, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake (Walawi 21:7).

Hakuna popote katika Torati ya Musa penye katazo la namna hiyo kwa wanaume wengine wa Israeli kwa ujumla. Tena, andiko hilo linabeba yafuatayo: (1) Walikuwepo wanawake waliokuwa wameachika katika Israeli, na (2) Kusingekuwepo kosa lolote kwa wanaume Waisraeli ambao si makuhani kuoa wanawake waliokuwa wameachika. Sheria inayotajwa katika mstari huo inawahusu makuhani tu na wanawake walioachika, wanaotaka kuolewa na makuhani. Hapakuwa na ubaya wowote katika Torati ya Musa kwa mwanamke yeyote aliyeachika kuolewa tena, mradi tu hakuolewa na kuhani. Na hakukuwa na kosa lolote kwa mwanamume, kuoa mwanamke aliyeachika, mradi si kuhani.

Kuhani mkuu (pengine kwa sababu ni mfano wa Kristo) alitakiwa kuishi kwa viwango vya juu zaidi kuliko hata makuhani wa kawaida. Yeye hakuruhusiwa hata kuoa mjane. Mistari kadhaa baadaye tunasoma hivi katika Walawi:

Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe (Walawi 21:14).

Je, andiko hili linathibitisha kwamba ilikuwa dhambi kwa wajane wote wa Israeli kuolewa tena, au kwamba ilikuwa dhambi kwa wanaume wote wa Israeli kuoa wajane? Hapana! Mstari huu unasema – tena kwa nguvu sana – kwamba isingekuwa dhambi kwa mjane yeyote kuolewa na mwanamume yeyote, mradi si kuhani mkuu. Tena unasema mwanamume mwingine yeyote alikuwa huru kuoa mjane, mradi si kuhani mkuu. Maandiko mengine yanathibitisha uhalali wa wajane kuolewa tena (ona Warumi 7:2-3; 1Timo. 5:14).

Mstari huo vile vile unaonyesha kwamba kusingekuwa na kosa lolote kwa mwanamume yeyote Mwisraeli kuoa mwanamke aliyeachika, au hata mwanamke ambaye hakuwa bikira – “aliyenajisika katika ukahaba” – mradi si kuhani au kuhani mkuu. Hoja hiyo inaungwa mkono na Walawi 21:7 pia. Tena, unasema kwamba katika Torati ya Musa, hapakuwa na kosa lolote kwa mwanamke aliyeachika kuolewa tena, au mwanamke “aliyenajisika katika ukahaba” kuolewa, mradi tu asiolewe na kuhani. Kwa neema sana, Mungu aliwapa wazinzi na walioachika nafasi nyingine, japo alikuwa kinyume kabisa na uzinzi na talaka.

Katazo La Pili Lililo Dhahiri Kinyume Cha Kuoa Tena

Je, Mungu alitoa “nafasi nyingine” ngapi kwa wanawake walioachika? Je, tuamue kwamba Mungu aliwapa wanawake walioachika nafasi moja zaidi katika Torati ya Musa, akiwaruhusu kuolewa tena mara moja tu? Huo ni uamuzi usio sahihi. Tunasoma hivi baadaye katika Torati ya Musa,

Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake. Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha na kumpa mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa aliyemtwaa kuwa mkewe; yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za BWANA; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo BWANA Mungu wako, iwe urithi (Kumbu. 24:1-4).

Ona kwamba katika mistari hii, kitu kinachokatazwa peke yake ni yule mwanamke aliyeachika mara mbili (au aliyeachika mara moja na kuwa mjane mara moja) kuolewa tena na mumewe wa kwanza. Hakuna kinachosemwa kwamba ana hatia kwa sababu ameolewa mara ya pili. Na baada ya kuachika mara ya pili (au kuwa mjane kwa mume wake w apili), alichokatazwa tu ni kumrudia mumewe wa kwanza. Ni kwamba, angekuwa huru kuolewa na mwanamume mwingine yeyote (ambaye yuko tayari kujaribu bahati yake!). Ingekuwa ni dhambi kwake kuolewa na mtu mwingine yeyote, kusingekuwepo haja kwa Mungu kutoa maagizo hayo ambayo ni wazi kabisa. Kitu cha pekee ambacho Mungu angesema ni hiki: “Watu walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa tena.”

Tena – Kama Mungu alimruhusu mwanamke aina hii kuolewa mara ya pili, basi yule mwanamume aliyemwoa baada ya kuachika mara ya kwanza asingekuwa na hatia yoyote. Na kama aliruhusiwa kuolewa mara ya tatu, basi mwanamume yeyote ambaye angemwoa baada ya kuachika mara mbili asingekuwa na dhambi (isipokuwa kama alikuwa ndiye mumewe wa kwanza). Basi – Mungu anayechukia talaka anawapenda watu walioachika, na kwa rehema aliwapa nafasi nyingine.

Hitimisho

Hebu kwa muhtasari tuone yale ambayo tumejifunza mpaka hapa. Hata ingawa Mungu alitangaza kwamba anachukia t alaka, hakuonyesha kabla au wakati wa agano la kale kwamba kuoa na kuolewa tena ni dhambi, isipokuwa katika haya mawili yafuatayo: (1) mwanamke aliyeachika mara mbili – au aliyeachika mara moja na kufiwa na mume wa pili – kuolewa na mumewe wa kwanza, na (2) mwanamke aliyeachika kuolewa na kuhani. Tena, Mungu hakuonyesha kwamba kumwoa aliyeachika ni dhambi kwa yeyote, isipokuwa makuhani.

Hayo yanaonekana kupingana na yale Yesu aliyosema juu ya watu walioachika wanao-oa tena, na wale wenye kuoa walioachika. Yesu alisema watu kama hao wanazini (ona Mathayo 5:32). Basi, yaonekana tumemwelewa vibaya Yesu au Musa, au pengine Mungu alibadilisha sheria Yake. Mimi nadhani tunaweza kuwa tunatafsiri vibaya yale aliyofundisha Yesu, kwa sababu ni ajabu kwa Mungu kutangaza ghafula kitu kuwa dhambi kiadili, kilichokuwa kinakubalika kwa miaka elfu na mia tano katika Torati ambayo Yeye aliitoa kwa Israeli.

Kabla ya kukabiliana na hili kwa upana zaidi, hebu pia tuone kwamba ruhusa ya Mungu kwa watu kuoa tena katika agano la kale haikuwa na masharti yoyote yaliyotokanana sababu za talaka ya mtu, au kiwango cha hatia ambacho mtu alipata kwa sababu ya talaka husika. Mungu hakusema kwamba watu fulani walioachika hawaruhusiwi kuoa au kuolewa kwa sababu talaka yao haikuwa halali. Hakusema kwamba kuna watu fulani wanaoruhusiwa kuona kwa sababu ya uhalali wa talaka zao. Lakini mara nyingi wachungaji wa siku hizi wanajaribu kufanya maamuzi hivyo, kutokana na ushuhuda wa mtu mmoja. Kwa mfano: Mwanamke aliyeachika anajaribu kumshawishi mchungaji wake kwamba anastahili kuruhusiwa kuolewa kwa sababu yeye ni mwathirika wa talaka. Mume wake wa kwanza ndiye alimwacha – si yeye. Lakini, kama huyo mchungaji atapewa nafasi ya kusikiliza upande wa mume naye, anaweza kumhurumia kwa namna fulani. Pengine huyo mama alikuwa mkorofi na anastahili lawama kiasi fulani.

Mimi najua mume na mke ambao wote wawili walijitahidi kukorofishana ili mmoja atoe talaka, kusudi waepukane na hatia kwamba ndio walioanzisha talaka. Wote walitaka waweze kusema baada ya kuachana kwamba, ni yule mwingine ndiye aliyeanzisha, na kwa njia hiyo, kuhalalisha ndoa zao za pili. Twaweza kuwadanganya watu, lakini hatuwezi kumdanganya Mungu. Kwa mfano: Mungu anamwonaje mwanamke ambaye anamnyima mumewe huduma za kitandani kila wakati, kisha anamwacha kwa sababu amekosa uaminifu kwake? Je, hahusiki na hiyo talaka kwa sehemu?

Lile jambo la mwanamke aliyeachika mara mbili katika Kumbukumbu 24 halisemi chochote kwamba talaka zake zote mbili ni halali. Mume wake wa kwanza aliona “neno ovu” kwake. Kama hilo “neno ovu” ni uasherati, angestahili kufa kulingana na Torati ya Musa (Walawi 20:10). Basi, kama uasherati tu ndiyo sababu halali ya talaka, pengine mume wake wa kwanza hakuwa na sababu nzuri ya kumwacha. Kwa upande wa pili, pengine alikuwa amezini, naye, akiwa mtu mwenye haki kama Yusufu wa Mariamu, “aliazimu kumwacha kwa siri” (Mathayo 1:19). Hapo kuna mengi yanayowezekana.

Mume wa pili anasemekana “akimchukia”. Hapa tena, hatujui wa kulaumiwa ni nani, au hata kama wote wanastahili kulaumiwa. Lakini bado haiweki tofauti. Neema ya Mungu ilitolewa kwake kwamba aolewe na yeyote ambaye angekubali kujaribu bahati yake kwa mwanamke aliyeachika mara mbili, isipokuwa mume wake wa kwanza.

Pingamizi

Watu mara nyingi wamesema hivi: “Kama watu wataambiwa ni halali kwao kuoa tena baada ya kuachana kwa sababu yoyote, itawatia moyo wao kuachana kwa sababu zisizo halali.” Yawezekana ikawa kweli kiasi fulani kwa watu wa dini ambao hawajitahidi kumpendeza Mungu. Lakini, kujaribu kuwazuia watu ambao hawajajitoa kwa Mungu kabisa wasitende dhambi ni swala gumu. Ila, watu waliojitoa kwa Mungu kabisa hawatafuti njia za kutenda dhambi. Wanajaribu kumpendeza Mungu. Na watu aina hiyo kwa kawaida wana ndoa zenye nguvu. Tena, Mungu hakusumbuka sana kwamba watu katika agano la kale wataachana kwa sababu zisizo halali kwa sababu ya kuwapa sheria nyepesi ya kuoa au kuolewa tena, maana sheria aliyotoa kwa Israeli kuhusu jambo hilo ilikuwa nyepesi kabisa.

Je, tuepuke kuwaambia watu kwamba Mungu yuko tayari kuwasamehe dhambi yoyote, wasije wakatiwa moyo kutenda dhambi kwa sababu wanajua msamaha unapatikana? Kama ndivyo, itabidi tuache kuhubiri Injili. Kila kitu kinategemea hali ya moyo ya wanadamu. Wale wanaompenda Mungu wanataka kumtii. Ninajua vizuri sana kwamba msamaha wa dhambi unapatikana kwangu nikiomba, hata kama nitatenda dhambi gani. Lakini hiyo hainisukumi kufanya dhambi hata kidogo, kwa sababu nampenda Mungu na nimezaliwa mara ya pili. Nimebadilishwa kwa neema ya Mungu. Ninataka kumpendeza.

Mungu anajua hakuna haja ya kuongeza tokeo lingine baya kwenye matokeo mabaya mengi yasiyoepukika ya talaka, kwa matumaini ya kuwahamasisha watu wakae katika ndoa. Kuwaambia watu wenye ndoa zenye shida kwamba wasiachane kwa sababu hawataruhusiwa kuoa au kuolewa tena hakutoi hamasa kwa watu kuendelea katika ndoa. Hata kama atakuamini, uwezekano wa kuishi peke yake ukilinganisha na maisha ya mateso ya ndoa daima utasikika kama paradiso kwa mtu mwenye ndoa mbaya.

Asemavyo Paulo Kuhusu Kuoa Tena

Kabla ya kupambana na tatizo la kulinganisha maneno ya Yesu nay a Musa kuhusu kuoa tena, tunahitaji kutambua kwamba yupo mwandishi mwingine mmoja wa Biblia anayekubaliana na Musa, naye ni Paulo Mtume. Paulo aliandika waziwazi kabisa kwamba kuoa au kuolewa tena kwa walioachika si dhambi, na kukubaliana na kinachosemwa na Agano la Kale.

Kwa habari za wanawali sina amri ya Bwana, lakini natoa shauri langu, mimi niliyejaliwa kwa rehema za Bwana kuwa mwaminifu. Basi naona hili kuw ajema kwa ajili ya shida iliyopo, kwamba ni vema mtu akae kama alivyo. Je, umefungwa kwa mke? Usitake kufunguliwa. Umefunguliwa? Usitafute mke. Lakini kama ukioa, huna hatia; wala mwanamwali akiolewa, hana hatia. Lakini watu kama hao watakuwa na dhiki katika mwili nami nataka kuwazuilia hayo (1Wakor. 7:25-28. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Bila shaka Paulo alikuwa anasema na watu walioachika katika fungu hili. Anawashauri walio na ndoa, wasio na ndoa na walioachika wabaki katika hali zao kwa sababu ya mateso ambayo Wakristo walikuwa wanapitia wakati huo. Ila, Paulo alisema wazi wazi kwamba watu walioachika na wanawali hawatatenda dhambi wakiingia katika ndoa.

Ona kwamba Paulo hafafanui uhalali wa kuoa au kuolewa tena kwa walioachika. Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa kama walioachika hawana lawama yoyote katika talaka ya ndoa iliyopita. (Kwani, nani mwenye sifa za kutosha kuhukumu kitu kama hicho, zaidi ya Mungu?) Hakusema kwamba kuoa au kuolewa tena kunaruhusiwa tu kwa wale ambao waliachana kabla ya kuokoka. Hapana! Yeye alisema tu kwamba kuoa au kuolewa tena si dhambi, kwa walioachika.

Je, Paulo Alilegeza Masharti Kuhusu Talaka?

Je, ina maana Paulo alilegeza masharti kuhusu talaka kwa kuwa aliruhusu kanuni ya neema kwa habari ya kuoa na kuolewa tena? Hapana! Paulo alikuwa anapingana na talaka kwa ujumla. Katika mistari ya mwanzoni ya sura hiyo hiyo ya barua ya kwanza kwa Wakorintho, aliweka sheria kuhusu talaka ambayo inalingana na chuki ya Mungu kwa talaka.

Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi ila Bwana; mke asiachane na mumewe. Lakini ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe. Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye, asimwache. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi, bali sasa ni watakatifu. Lakini, yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyu ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani. Kwa maana wajuaje wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo? Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungualivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote (1Wakor. 7:10-17).

Angalia kwamba Paulo anasema na waamini kwanza, ambao wana ndoa na waamini wenzao. Hawapaswi kuachana, na Paulo anasema hayo si maagizo yake, bali ya Bwana. Bila shaka hayo yanakubaliana kabisa na kila kitu tulichotazama katika Biblia mpaka hapa.

Yanayofuata yanasisimua. Paulo alikuwa mkweli wa kutosha kutambua kwamba hata waamini wanaweza kuachana, japo kwa nadra. Hayo yakitokea, Paulo anasema kwamba yule aliyemwacha mwenzake akae bila ndoa au wapatane. (Japo ushauri wa Paulo unawalenga zaidi wake, kanuni hiyo bila shaka inawahusu hata waume.)

Hapa tena – alichoandika Paulo kisitushangaze. Anatangulia kuweka sheria ya Mungu kwanza kuhusu talaka, lakini ana akili ya kutosha kutambua kwamba kutii sheria ya Mungu si kitu kinachofanyika kila wakati. Hivyo, dhambi ya kuachana inapotokea kati ya waamini wawili, anatoa maagizo zaidi. Yule aliyemwacha mwenzake abaki bila kuoa au apatane na mwenzake. Hicho ndicho kinachofaa endapo waamini wawili wataachana. Muda wote watakaobaki hawana ndoa, kuna tumaini la wao kupatana, na hilo ndiyo bora. Kama mmoja wao akioa tena, hapo ndiyo mwisho wa matumaini na uwezekano wa kupatana. (Tena, kama wametenda dhambi isiyosameheka kwa kuachana, isingekuwepo sababu ya Paulo kuwaaambia wabaki bila ndoa au wapatane.)

Unaonaje? Paulo alikuwa na akili za kutosha kujua kwamba agizo lake la pili kwa waamini walioachana halitafuatwa? Bila shaka! Labda ndiyo sababu hakutoa ushauri zaidi kwa waamini walioachana kwa sababu alitazamia kwamba waamini wa kweli wangefuata agizo lake la kwanza la kutoachana, na kwamba katika mazingira adimu sana, agizo lake la pili lingehitajika. Kwa hakika, wafuasi wa kweli wa Kristo wangefanya kila kinachowezekana ili kuhifadhi ndoa yao, kama walikuwa na matatizo ya ndoa. Na kwa hakika, mwamini ambaye, baada ya juhudi zote za kuhifadhi ndoa angejisikia kwamba hana jinsi isipokuwa kuachana, kutokana na aibu yake binafsi na shauku ya kumheshimu Kristo asingefikiri kuwa na ndoa nyingine, na bado angetumainia mapatano. Inaonekana kwamba tatizo halisi katika kanisa la kisasa kuhusu talaka ni kwamba kuna waamini bandia wengi sana – watu ambao hawajawahi kumwamini Bwana Yesu kweli, na kujitoa kwake.

Ni dhahiri basi kutokana na yale Paulo anayoandika katika 1Wakorinto 7 kwamba, Mungu ana matazamio makubwa sana kwa waamini – watu waliojazwa na Roho Mtakatifu – kuliko aliyo nay kwa wasioamini. Kama tulivyosoma, Paulo aliandika kwamba waamini wasiwaache hata wenzao wasioamini mradi wako tayari kuishi nao. Hapo tena, agizo hili halitushangazi kwa sababu linakubaliana kabisa na kila kitu tulichosoma katika Manadiko kuhusu jambo hilo hadi sasa. Mungu anapinga talaka. Lakini Paulo anaendelea kusema kwamba, kama yule asiyeamini anataka talaka, mwamini aruhusu hiyo. Paulo anajua kwamba asiyeamini hajajitolea kwa Mungu, na hivyo hamtazamii asiyeamini kutenda kama anayeamini. Nyongeza ndogo hapo: Asiyeamini anapokubali kuishi na aaminiye, ni ushuhuda mzuri kwamba, pengine asiyeamini ana mwelekeo wa kupokea Injili, au yule anayeamini amerudi nyuma au ni Mkristo bandia.

Sasa, nani atakayesema kwamba mwamini aliyeachwa na asiyeamini hayuko huru kuoa tena? Paulo hasemi hivyo kamwe, kama alivyosema kwa habari ya waamini wawili walioachana. Itabidi kushangaa ni kwa nini Mungu apinge mwamini aliyeachwa na asiyeamini kuoa au kuolewa tena. Hilo lingetimiza kusudi gani? Lakini, ruhusa hiyo inaonekana inapingana na maelezo ya Yesu kuhusu kuoa tena, kwamba, “Yeyote amwoaye mwanamke aliyeachwa, azini” (Mathayo 5:32, TLR). Hapo tena, kuna mashaka kwamba pengine tumefasiri vibaya yale ambayo Yesu anasema.

Tatizo Lenyewe

Ni wazi kwamba Yesu, Musa na Paulo wanakubaliana kwamba kuachana au talaka ni dhihirisho la dhambi kwa mhusika mmoja au wote wawili. Wote wanapinga talaka kwa ujumla. Lakini tatizo letu ni hili: Tunaowanishaje yale ambayo Musa na Paulo wanasema kuhusu kuoa tena, na yanayosemwa na Yesu kuhusu jambo hilo hilo? Ni sawa tukitazamia kwamba yatalingana kwa sababu wote walivuviwa na Mungu kusema waliyosema.

Hebu tutazame kwa uhakika kwamba Yesu alisema nini, na tuwaone aliowaambia hayo. Katika Injili ya Mathayo, tunamwona Yesu mara mbili akisema jambo la talaka na kuoa tena – mara ya kwanza katika Hotuba ya Mlimani, na mara nyingine alipohojiwa na Mafarisayo fulani. Tuanze na mazungumzo ya Yesu na Mafarisayo hao.

Basi Mafarisayo wakamwendea wakamjaribu wakimwambia, ‘Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?’ Akajibu akawaambia, ‘Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.’ Wakamwambia, ‘Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?’ Akawaambia, ‘Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uahserati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa, azini’ (Mathayo 19:3-9).

Katika mazungumzo yao na Yesu, Mafarisayo walirejea Maandiko katika Torati ya Musa, ambayo tulikwisha yatazama mapema – Kumbukumbu la Torati 24:1-4. Hapo imeandikwa hivi: “Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake” (Kumbu. 24:1, Maneno mepesi kutilia mkazo).

Katika siku za Yesu yalikuwepo makundi mawili kimtazamo, kuhusu hicho kinachoitwa “neno ovu.” Miaka kama ishirini kabla ya swali hilo kuulizwa, mwalimu mmoja aliyeitwa Hileli alifundisha kwamba neno ovu lilikuwa ni tofauti isiyorekebika. Wakati huu ambapo Yesu anafanya majadiliano na Mafarisayo, tafsiri ya “Hileli” ilikuwa imepanuliwa sana na kuwa nyepesi mno, ikiruhusu talaka kwa “sababu yoyote” kama swali la Mafarisayo lilivyotoka. Mtu aliweza kumwacha mkewe kama ameunguza chakula, au chumvi ikizidi kwenye chakula, au kama alijizungusha sana mbele za watu magoti yake yakaonekana, au kama aliruhusunywele zake kuonekana, au kama alizungumza na mwanamume mwingine, au kama alisema maneno mabaya kuhusu mama mkwe wake, au kama alikuwa tasa. Mwanamume aliruhusiwa hata kumwacha mkewe kama angemwona mwingine ambaye ni mrembo zaidi – hivyo kuona “neno ovu” kwa mkewe.

Mwalimu mwingine maarufu aliitwa Shammai. Yeye aliishi kabla ya Hileli, na alifundisha kwamba “neno ovu” lilikuwa kitu kibaya sana, kama vile uzinzi. Bila shaka utatambua kwamba miongoni mwa Mafarisayo wa siku za Yesu, tafsiri ya Hileli ndiyo ilipendwa zaidi kuliko ya Shammai. Mafarisayo waliishi na kufundisha kwamba talaka ilikuwa halali kwa sababu yoyote. Basi, talaka iliongezeka sana. Na Mafarisayo – kama kawaida yao kiFarisayo – walikazia sana umuhimu wa kumpa mke hati ya talaka unapomwacha, ili usi”halifu Torati ya Musa.”

Usisahau Kwamba Yesu Alikuwa Anazungumza Na Mafarisayo

Baada ya kujua hayo, tutaelewa vizuri zaidi kilichokuwa kinamkabili Yesu. Mbele yake walisimama kundi la waalimu wa dini wanafiki, wengi ambao – kama si wote basi – walikuwa na talaka moja au zaidi, na pengine ni kwa sababu walikuwa wamepata wanawake warembo zaidi. (Si bahati kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka katika Mahubiri ya Mlimani yanafuata maonyo Yake makali sana kuhusu tamaa, na kusema ni aina ya uzinzi.) Na bado walikuwa wanajihesabia haki, wakidai kwamba wameishika Torati ya Musa.

Swali lao tu linadhihirisha jinsi walivyoegemea upande mmoja. Waliamini kabisa kwamba mtu angeweza kumwacha mke wake kwa sababu yoyote. Yesu akadhihirisha ufahamu wao mbovu wa kusudi la Mungu kuhusu ndoa kwa kurejea maneno ya Musa juu ya ndoa katika Mwanzo sura ya 2. Mungu hakukusudia kuwepo na talaka zozote, achilia mbali talaka “kwa sababu yoyote,” lakini viongozi wa Israeli walikuwa wanawaacha wake zao kiholela tu!

Inaonekana Mafarisayo walijua tayari msimamo wa Yesu kuhusu talaka, maana alikwisha kuutamka hadharani. Basi wakawa na pingamizi tayari: “Mbona basi Musa aliagiza apewe hati ya talaka na kumwacha?” (Mathayo 19:7, TLR).

Hapo tena swali lao linaonyesha jinsi walivyogemea upande mmoja. Limeulizwa kana kwamba Mus aalikuwa anawaagiza wanaume wawaache wake zao baada ya kugundua “neno ovu,” mradi tu watoe hati ya talaka. Lakini, kama tujuavyo kutokana na Kumbukumbu 24:1-4, Musa hakusema hivyo hata kidogo. Yeye alikuwa anaweka sawa ndoa ya tatu ya mwanamke – akimzuia asiolewe tena na mume wake wa kwanza.

Kwa vile Musa alitaja talaka, bila shaka talaka ilikuwa inaruhusiwa kwa sababu fulani. Lakini ona kwamba neno alilotumia Yesu katika jibu lake – aliruhusu – ni tofauti na chaguo la Mafarisayo – aliamuru. Musa aliruhusu talaka, hakuamuru. Na sababu ya Musa kuruhusu talaka ni ugumu wa mioyo ya Waisraeli. Yaani – Mungu aliruhusu talaka kama tendo la huruma tu kwa hali ya dhambi ya watu. Alijua watu wasingekuwa waaminifu kwa wana ndoa wenzao. Alijua uchafu ungekuwepo. Alijua mioyo ya watu ingevunjika. Basi, akatoa ruhusa kwa talaka. Hakuwa amekusudia hivyo tangu mwanzo, lakini dhambi ililazimisha hivyo.

Kisha Yesu akaweka sheria ya Mungu wazi kwa Mafarisayo, akifafanua kile ambacho Musa anakiita “neno ovu”. “Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akamwoa mwanamke mwingine, azini” (Mathayo 19:9, TLR. Maneno mepesi kutilia mkazo). Machoni pa Mungu, uzinzi ndiyo sababu halali pekee kwa mwanamume kumwacha mke wake. Na ni rahisi kueleweka. Ni kitu gani kingine amb acho mwanamume au mwanamke anaweza kufanya, kikawa kibaya kwa mwenzake kuliko hicho? Mtu anapozini, anatuma ujumbe mchungu sana. Kwa hakika Yesu hakuwa anazungumzia uzinzi tu aliposema hayo. Bila shaka hata kumbusu mwenzi wa mwingine na kumshika-shika ni kitu kibaya sana, kama ilivyo tabia ya kuangalia picha mbaya za ngono, au matendo mengine yasiyofaa ya mahusiano kimwili. Kumbuka kwamba Yesu alifananisha tamaa na uzinzi katika Mahubiri Yake ya Mlimani.

Tusije kusahau Yesu alikuwa anasema na nani – ni Mafarisayo waliokuwa wanaachana na wake zao kwa sababu yoyote na kuoa haraka haraka, lakini hao hao wasingezini kamwe ili wasivunje amri ya saba. Yesu aliwaambia wanajidanganya wenyewe. Walichokuwa wanafanya hakikuwa tofauti na uzinzi. Ndiyo ukweli huo. Yeyote aliye mkweli anaweza kuona kwamba mwanamume anayemwacha mkewe ili amwoe mwanamke mwingine anafanya kitu ambacho mzinzi hufanya. Tofauti ni kwamba, huyu mwingine anahalalisha uzinzi wake.

Ufumbuzi

Huu ndiyo ufunguo wa kulinganisha maneno ya Yesu na ya Musa na ya Paulo. Yesu alikuwa anadhihirisha unafiki wa Mafarisayo tu. Hakuwa anaweka sheria inayozuia kuoa au kuolewa tena. Kama alikuwa anafanya hivyo, basi alipingana na Musa na Paulo, na kusababisha vurugu kwa mamilioni ya watu walioachika, na mamilioni ya watu walioingia kwenye ndoa nyingine. Kama Yesu alikuwa anaweka sheria kuhusu kuoa au kuolewa tena, tuwaambie nini wale ambao wameachika na kuoa au kuolewa tena kabla ya kusikia habari za Sheria ya Yesu? Je, tuwaambie kwamba wanaishi katika mahusiano ya kiasherati? Na, kwa kuwa tunajua Biblia inaonya kwamba hakuna wazinzi au waasherati watakaorithi ufalme wa Mungu (1Wakor. 6:9-10), tuwashauri kwamba waachane na wenzao? Pengine ni sawa, lakini, Mungu si anachukia kuachana?

Je, tuwaambie waachane kitandani mpaka wana ndoa wenzao wa kwanza wafe ili kuwaepusha na zinaa ya kila wakati? Lakini, Paulo si anawakataza wana ndoa kunyimana? Tena, ushauri kama huo si utapelekea watu kujaribiwa kimwili na hata kuamsha hamu za kutaka wana ndoa wenzao wafe?

Je, tuwaambie watu kama hao waachane na wenzao wa sasa na kurudiana na wenzao wa kwanza (kama wengine wanavyosema) – kitu ambacho kinakatazwa na Torati ya Musa katika Kumbukumbu 24:1-4?

Halafu – vipi kuhusu watu walioachana ambao hawajaoa tena? Kama wanaruhusiwa kuoa au kuolewa tena ikiwa wenzao walioachana nao walitenda uzinzi, nani atakayejizatiti kuthibitisha kama kweli uzinzi ulifanyika? Je, itabidi wana ndoa fulani wathibitishe kwamba wenzao walioachana nao walikuwa na hatia ya tamaa tu ili waweze kurudiana? Je, wengine itabidi watafute mashahidi wa kuthibitisha uasherati wa wenzao ili waweze kurudiana?

Kama swali lililopita – vipi kuhusu swala la mwenzi kuzini kwa sababu alikuwa katika ndoa na mtu aliyemnyima tendo la ndoa? Je, ni halali kwa huyo aliyekuwa anamnyima mwenzake tendo la ndoa aruhusiwe kuolewa, na yule mtu aliyezini akatazwe kuoa au kuolewa?

Vipi kuhusu mtu aliyezini kabla ya ndoa? Je, uzinzi wake huo si kukosa uaminifu kwa mwenzi wa baadaye? Je, dhambi hiyo hailingani na uzinzi, kama yeye au mwenzake wangekuwa katika ndoa wakati walipofanya dhambi yao? Mbona huyo aruhusiwe kuoa au kuolewa?

Vipi kuhusu watu wawili wanaokaa pamoja – bila ndoa – halafu wanatengana. Mbona wanaruhusiw akuoa na kuolewa na wengine baada ya kutengana, kwa kuwa hawakuwa na ndoa rasmi? Wana tofauti gani na wale wenye kuachana kisha wakaoa na kuolewa tena?

Vipi kuhusu kweli kwamba “mambo ya zamani yanapita” na “mambo yanakuwa mapya” wakati mtu anapo-okoka (ona 2Wakor. 5:17)? Je, inamaanisha kila dhambi iliyowahi kufanywa isipokuwa dhambi ya kuachana isivyo halali?

Yote hayo na maswali mengine mengi[1] yanaweza kuulizwa, ambayo ni hoja zenye nguvu kabisa kuunga mkono wazo kwamba Yesu hakuwa anaweka sheria mpya kuhusu ndoa. Yesu alikuwa na akili za kutosha kutambua matokeo ya sheria Yake mpya ya ndoa kama ndivyo ilivyokuwa. Hilo tu linatosha kutuambia kwamba alikuwa anaweka wazi unafiki wa Mafarisayo – wanaume wenye tamaa, wanafiki, washika dini, waliokuwa wanaachana na wake zao “kwa sababu yoyote” na kuoa tena.

Sababu ya Yesu kusema kwamba walikuwa “wanazini” badala ya kusema tu kwamba walichokuwa wanafanya ni kosa ni kwa sababu alitaka wao waone kwamba talaka kwa sababu yoyote na kuoa tena baada ya hapo si tofauti na uzinzi, kitu ambacho wao walidai hawafanyi. Je, tuamue kwamba kitu pekee alichojali Yesu ni tendo la ndoa tu katika ndoa ya pili, na kwamba angeunga mkono ndoa ya pili mradi tu watu wasijihusishe katika tendo la ndoa? Hapana. Basi, tusimfanye aseme kitu ambacho hakumaanisha kusema.

Mlinganisho Unaofanya Kufikiri

Hebu tufikiri kuhusu watu wawili. Mmoja ana ndoa, ni mtu wa dini, anayedai kumpenda Mungu kwa moyo wake wote, ambaye ameanza kumtamani mwanamke kijana anayekaa jirani. Muda si muda anamwacha mkewe na haraka anamwoa yule msichana aliyemvutia.

Yule mwingine si mtu wa dini. Yeye hajawahi kusikia hata Injili, na anaishi maisha mabaya ambayo hatimaye yanaharibu ndoa yake. Miaka kadhaa baadaye, akiwa peke yake tu, anaisikia Injili, anatubu, na anaanza kumfuata Yesu kwa moyo wake wote. Miaka mitatubaadaye anampenda mwanamke mwenye kumpenda Mungu sana anayekutana naye kanisani. Wote wawili wanatafuta mapenzi ya Mungu na ushauri wa wengine kwa bidii, kisha wanapanga kuoana. Wanakuja kuonana, na wanakuwa waaminifu kwa Bwana na wao kwa wao mpaka kifo.

Sasa – hebu tudhanie kwamba wote wawili wametenda dhambi kwa kuoa tena. Katika hao wawili, ni yupi mwenye dhambi kubwa zaidi? Bila shaka ni yule wa kwanza. Yeye ni sawa na mzinzi tu.

Lakini – vipi kuhusu yule mtu wa pili? Je, ni kwamba ametenda dhambi? Je, tunaweza kusema kwamba yeye hana tofauti na mzinzi – kama yule wa kwanza? Hapana. Je, tumwambie yale ambayo Yesu alisema kuhusu watu wanaoachana na kuoa tena, na kumjulisha kwamba sasa anaishi na mwanamke ambaye Mungu hakumwunganisha naye kwa sababu anamhesabu bado ana ndoa na mke wake wa kwanza? Je, tumwambie kwamba anaishi katika zinaa?

Majibu yako dhahiri kabisa. Uzinzi hutendwa na watu ambao wameoana, wanaomwona mwingine asiyekuwa mwenzi wao. Kwa hiyo, kuachana na mwenzako kwa sababu umepata mrembo zaidi ni sawa na uzinzi. Lakini, mtu ambaye hajaoa hawezi kufanya uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu, na mtu ambaye ameachika hawezi pia kutenda uzinzi kwa sababu hana mwenzi wa kumkosea uaminifu. Tukielewa mantiki ya kihistoria na kiBiblia kuhusu maneno ya Yesu, hatuwezi kufikia maamuzi yatakayopotosha watu, na yenye kupingana na Maandiko yote.

Wanafunzi waliposikia itikio la Yesu kwa jibu la Mafarisayo, walijibu hivi, “Kama mahusiano ya mwanamume na mke wake yako hivyo, ni afadhali kutokuoa” (Mathayo 19:10, TLR). Tambua kwamba walikuwa wamekulia chini ya mafundisho na ushawishi wa Mafarisayo, na katika utamaduni uliokuwa umeathiriwa sana na Mafarisayo. Hawakuwahi kudhani kwamba ndoa ni kitu cha kudumu kiasi hicho. Ukweli ni kwamba, muda mfupi uliopita, hata wao waliamini ni halali kwa mwanamume kumwacha mkewe kwa sababu yoyote. Basi kwa haraka wakaamua kwamba ingekuwa bora kuepukana na ndoa kabisa, ili kuepuka hatari ya kuachana na kuingia kwenye uzinzi. Yesu alijibu hivi:

Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumboni mwa mama zao; tena wako matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee (Mathayo 19:11-12).

Yaani – kinachoamua ni ile hamu ya kushirikiana kimwili aliyo nayo mtu, au uwezo wake wa kuitawala. Hata Paulo alisema hivi: “NI afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa” (1Wakor. 7:9, TLR). Wale waliozaliwa wakiwa matowashi au wale wanaofanywa matowashi na watu (kama ilivyokuwa zamani: watu waliwafanya wanaume wengine kuwa matowashi, ili wawape jukumu la kuwalinda wake zao) hawana hamu ya kushirikiana na mwanamke kimwili. Wale “wanaojifanya wenyewe kwa ajili ya ufalme wa mbinguni” ni wale ambao wamejaliwa na Mungu kipekee kuwa na uwezo wa kujitawala zaidi. Ndiyo maana “si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa” (Mathayo 19:11).

Mahubiri Ya Mlimani

Tusisahau kwamba wale watu Yesu aliosema nao wakati akihubiri Mlimani pia walikuwa wameishi maisha yao chini ya ushawishi wa Mafarisayo wanafiki, waliokuwa viongozi na waalimu wa Israeli. Kama tulivyokwisha jifunza hapo mapema tulipotazama Mahubiri ya Mlimani, ni dhahiri kwamba sehemu kubwa ya yale ambayo Yesu alisema yalikuwa kama masahihisho tu ya mafundisho ya uongo ya Mafarisayo. Yesu hata aliwaambia watu kwamba hawataingia mbinguni ikiwa haki yao haitazidi ile ya waandishi na Mafarisayo (Mathayo 5:20), ambayo ilikuwa njia nyingine ya kusema kwamba waandishi na Mafarisayo walikuwa njiani kwenda jehanamu. Mwisho wa mahubiri yake, watu walishangazwa kwa sehemu kwa sababu Yesu alikuwa anafundisha kitofauti, “si kama waandishi wao” (Mathayo 7:29, TLR).

Mapema katika mahubiri Yake, Yesu aliweka wazi unafiki wa wale waliodai kwamba hawajawahi kuzini, ila wanatamani na kuachana na wenzi wao na kuoa tena. Akapanua maana ya uzinzi kwamba ni zaidi ya tendo la kimwili la dhambi baina ya watu wawili walio na ndoa. Na aliyosema yalikuwa wazi kabisa kwa yeyote mwenye akili nzuri na mkweli, ambaye angefikiri kidogo tu. Lakini kumbuka kwamba, mpaka wakati wa mahubiri ya Yesu, wengi wa watu katika lile kundi wangekuwa na mawazo kwamba ilikuwa halali kwao kuachana “kwa sababu yoyote” ile. Yesu alitaka wafuasi Wake pamoja na wengine wote wajue kwamba kusudi la Mungu tangu mwanzo lilikuwa kiwango cha juu zaidi.

Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini’. Lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamey mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanmum. Imenenwa pia, ‘Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya usherati, amfanya kuwa mzinzi, na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini (Mathayo 5:27-32).

Kama tulivyokwisha ona mapema, ona kwamba maneno ya Yesu kuhusu talaka na kuoa tena yanafuata moja kwa moja maagizo aliyotoa kuhusu tamaa, hivyo kuyaunganisha pamoja. Tena, Yesu anasema vyote viwili ni uzinzi, na kuviunganisha zaidi. Basi tunaona kwamba kuna muunganiko wa kitu kinachofanana katika maelezo hayo ya fungu hili lote la Maandiko. Yesu alikuwa anawasaidia wafuasi Wake kuelewa maana ya kutii amri ya saba. Maana yake ni kutotamani, na kutoachana na kuoana tena.

Kila mtu katika wasikilizaji Wake wa Kiyahudi alikuwa amesikia amri ya saba ikisomwa katika sinagogi (maana hawakuwa na Biblia binafsi siku zile), pamoja na mafafanuzi yaliyotolewa, na kuona jinsi waalimu wao – waandishi na Mafarisayo – walivyoyafanyia kazi maishani mwao. Ndipo Yesu akasema, “lakini mimi nawaambia”, ila hakuwa anataka kuongeza sheria zingine mpya. Yeye alitaka kudhihirisha tu mpango wa Mungu tokea mwanzo.

Kwanza – tamaa ilikuwa inakatazwa kabisa na amri ya kumi, na hata bila amri ya kumi, yeyote aliyefikiri vizuri angetambua kwamba ilikuwa ni kosa kutamani kufanya kitu ambacho Mungu amekataza.

Pili – tangu mwanzoni kabisa mwa kitabu cha Mwanzo, Mungu aliweka wzi kwamba ndoa ilitaiwa kuwa makubaliano ya maisha yote. Tena, yeyote aliyefkiri vizuri juu ya hilo angetambua kwamba kuachana na kuoana tena ni sawa tu na uzinzi, hasa kama mmoja atapanga kumwacha menzake kwa kusudi la kuoa tena.

Lakini tena katika mahubiri haya, ni wazi kwamba Yesu alikuwa anawasaidia tu watu waone ukweli kuhusu tamaa na ukweli kuhusu kuachana kwa sababu yoyote, na kuoana tena. Yeye hakuwa anaweka sheria mpya ya kuoana tena ambayo haikuwa “vitabuni” hadi wakati huo.

Inashangaza kwamba ni watu wachache sana kanisani ambao wamewahi kutimiza maneno ya Yesu ya kung’oa jicho au kukata mikono, maana mawazo hayo yanapingana sana na Maandiko mengine, na ni dhahiri kwamba kazi yake ni kutia nguvu hoja kuhusu kuepukana na kujaribiwa kuwa na mahusiano kimwili yasiyofaa. Lakini wengi sana kanisani wanajaribu kutafsiri moja kwa moja maneno ya Yesu juu ya yule mwenye kuoa au kuolewa tena kufanya uzinzi, hata ingawa tafsiri hizo zinapingana moja kwa moja na Maandiko mengine. Lengo la yesu lilikuwa kuwafanya wasikilizaji Wake wakabiliane na ukweli, kwa tumaini kwamba talaka zingepungua baada ya hapo. Kama wafuasi Wake wangepkea moyoni yale aliyosema kuhusu tamaa, kusingekuwepo na uasherati au uchafu miongoni mwao. Kama usingekuwepo, kusingekuwepo na sababu halali za talaka. Basi, talaka isingekuwepo, kama Mungu alivyokusudia tangu mwanzo.

Mwanamume Anamfanyaje Mkewe Azini?

Ona maneno ya Yesu, kwamba, “Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi.” Hili tena linatufanya tuamini kwamba hakuwa anaweka sheria mpya ya kuoana tena, bali alikuwa anadhihirisha tu ukweli kuhusu dhambi ya mtu anayemwacha mkewe bila sababu nzuri. “Amfanya kuwa mzinzi.” Kuna wanaosema kwamba Yesu alikuwa anamzuia huyo mwanamke kuolewa tena, kwa sababu anasema huo ni uzinzi. Lakini si hivyo. Mkazo uko kwenye dhambi ya mwanamume anayemwacha mkewe, kwamba, kwa sababu ya kile anachokitenda, mke wake atakuwa hana lingine la kufanya isipokuwa kuolewa tena, ambayo si dhambi kwa upande wake maana yeye ameathirika kutokana na ubinafsi wa mumewe. Machoni pa Mungu ni kwamba, kwa kuwa mwanamume alimwacha mkewe na kumwingiza kwenye kuolewa tena, ni kama amemlazimisha aingie kitandani na mwanamume mwingine. Basi, yule anayedhani hajatenda uzinzi anakuwa na hatia kwa uzinzi mara mbili – wa kwake na wa mkewe.

Yesu hakusema kwamba Mungu anamhesabu mke aliyeathiriwa na talaka kwamba ana hatia ya uzinzi, maana hiyo isingekuwa halali, tena ingekuwa haina maana kabsia kama huyo mke aliyeathiriwa asingeolewa. Mungu angewezaje kusema kwamba ni mzinzi kama asingeolewa? Isingekuwa na maana kabisa. Basi, ni dhahiri kwamba Mungu anamhesabu huyo mwanamume kuwa na hatia kwa uzinzi wake mwenyewe na “uzinzi” wa mkewe, ambao kweli si uzinzi kwake maana ni ndoa ya pili ambayo ni halali kabisa.

Sasa – vipi kuhusu maneno ya Yesu yafuatayo kwamba, “na mtu akimwoa mwanamke aliyeachwa anazini”? Ni mawili tu yanayoweza kueleweka. Aidha Yesu alikuwa anaongeza hatia ya uzinzi wa tatu dhidi ya mtu anayedhani kwamba hajawahi kuzini (kwa sababu ile ile kama aliyotumia kuongeza hatia ya pili), au Yesu alikuwa anasema kuhusu huyo mwanamume anayemtia moyo mwanamke aachane na mumewe ili waoane, “asizini”. Kama Yesu alikuwa anasema kwamba mwanamume yeyote duniani anayemwoa mwanamke aliyeachwa anazini, basi kila mwanamume wa Israeli alizini katika kipindi cha miaka mia nyingi ambaye, katika kutimiza Torati ya Musa, alimwoa mwanamke aliyeachika. Ukweli ni kwamba kila mwanamume siku hiyo aliyekuwa anamsikiliza Yesu, aliyekuwa amemwoa mwanamke aliyeachika kwa kufuatana na Torati ya Musa, alikuwa na hatia ya kosa ambalo hakuwa na hatia yake muda mfupi kabla ya hapo, na Yesu akawa amebadilisha sheria ya Mungu hapo hapo. Tena, kila mtu katika wakati ujao ambaye alimwoa mtu aliyeachwa, kwa kuamini neno la Paulo katika barua yake kwa Wakorintho kwamba hilo si dhambi, alikuwa ametenda dhambi – ni mzinzi.

Jinsi Biblia ilivyo inapelekea mtu kumstahi sana mwanamume aliyeoa mwanamke aliyeachwa. Kama yeye ni mwathirika wa ubinafsi wa mume wake wa kwanza, asiye na hatia, ningemstahi sana mwanamume huyo, kama ambavyo ningemstahi sana mwanamume anayeoa mjane na kumtunza. Kama huyo mwanamke alikuwa na sababu ya kulaumiwa kwa talaka yake, bado ningemstahi sana kwa kuwa na moyo wa Kristo kwa kuamini kwamba kuna kilicho bora kwake, na kwa neema yake ya kukubali kusahau yaliyopita na kujaribu. Kwa nini mtu yeyote aliyesoma Biblia, mwenye Roho Mtakatifu ndani yake aamue kwamba Yesu alikuwa anamkataza kila mtu asioe au kuolewa na yeyote aliyeachika? Hilo linaingiaje kwenye ukweli kwamba Mungu ni mwenye haki – haki ambayo haimwadhibu yeyote kwa kuwa mwathirika – kama mwanamke ambaye anaachwa pasipo kuwa na kosa? Hoja kama hiyo inaingiaje kwenye ujumbe wa Injili, wenye kutoa msamaha na nafasi nyingine kwa wenye dhambi wanaotubu?

Kuhitimisha

Biblia inasema tena na tena kwamba talaka inahusisha dhambi kwa mmoja au kwa wenzi wote wawili. Mungu hakukusudia mtu yeyote aachane na mwenzake katika ndoa, lakini kwa rehema Zake alitoa mwanya wa talaka kama uasherati ukitokea. Kwa rehema pia aliweka mpango kwa watu walioachika kuoa na kuolewa tena.

Kama si kwa sababu ya maneno ya Yesu kuhusu kuoa na kuolewa tena, hakuna msomaji yeyote wa Biblia ambaye angedhani kwamba kuoa na kuolewa tena ni dhambi (isipokuwa kwa habari za matukio mawili nadra sana katika agano la kale, na moja la nadra sana katika agano jipya, yaani, kuoa na kuolewa tena baada ya mtu kuachana na mwingine aliyeokoka). Ila, tumepata njia inayokubalika ya kulinganisha kile alichosema Yesu kuhusu kuoa na kuolewa tena, na sheria kali zaidi yenye kukataza kuoa au kuolewa tena kwa kila hali. Hii sheria haifanyi kazi kwa wale ambao wamekwisha achana na kuingia katika ndoa zingine (maana ni sawa na kurudisha mayai yaliyopikwa yawe mabichi), na ni moja ambaye ingesababisha mkanganyiko wa hali ya juu na kuwapelekea watu kuvunja sheria zingine za Mungu. Badal ayake, tumeona kwamba Yesu alikuwa anawasaidia watu kutambua unafiki wao. ALikuwa anawasaidia wale walioamini kwamba hawatazini kamwe waone kwamba wlaikuwa wanazini kwa njia zingine, kwa tamaa zao na kwa mtazamo wao mwepesi kuhusu sababu za kuachana.

Kama Biblia nzima inavyofundisha, msamaha hutolewa kwa wenye dhambi wanaotubu, bila ya kujali dhambi yao, na nafasi ya pili na ya tatu hutolewa kwa wenye dhambi – pamoja na walioachika. Hakuna dhambi katika kuoa na kuolewa tena kwa aina yoyote katika agano jipya, isipokuwa kwa mwamini aliyeachana na mwamini mwenzake. Na hilo halipaswi kutokea kwa sababu waamini wa kweli hawafanyi uchafu, na kwa sababu hiyo hakuna sababu halali ya kuachana. Ikitokea kwa nadra, wote wawili wabaki kama walivyo au wapatane.


[1] Kwa mfano: Fikiri maneno ya mchungaji mmoja aliyeachika, aliyetengwa na mwili wa Kristo baada ya kuoa tena. Alisema hivi: “Afadhali hata ningemwua mke wangu kuliko kumwacha. Kama ningemwua, ningetubu, nikasamehewa, nikaoa tena kihalali, na kuendelea katika huduma yangu.”

Wanawake Katika Huduma

Sura Ya Kumi Na Mbili

 

Kwa kuwa ni kitu kinachojulikana kwamba wanawake ni zaidi ya nusu katika kanisa la Bwana Yesu Kristo, ni muhimu kuelewa nafasi yao waliyopewa na Mungu katika mwili wa kristo. Katika makanisa mengi na huduma, wanawake huonekana kama watenda kazi wa maana sana, kama ambavyo ni kawaida hata katika huduma ya jumla.

Lakini, si wote wanaokubaliana kuhusu nafasi zao. Wanawake mara nyingi wanazuiwa kufanya maeneo fulani ya huduma kanisani, yenye kuhusiana na kusema na uongozi. Makanisa mengine yanaruhusu wanawake wachungaji; mengi hayaruhusu. Mengine yanaruhusu wanawake kufundisha, na mengine hayaruhusu. Wengine wanawazuia wanawake wasiseme kabisa wakati wa ibada za kanisa.

Kutofautiana huko kwa sehemu kubwa kumejengwa kwenye tafsiri mbalimbali za maneno ya Paulo kuhusu nafasi za wanawake katika 1Wakor. 14:34-35 na 1Timo. 2:11 hadi 3:7. Maandiko hayo tutayatazama zaidi katika sura hii, hasa pale mwishoni.

Kuanza Mwanzo

Tunapoanza, hebu tutazame Maandiko yanadhihirisha nini kuhusu wanawake, tangu mwanzo kabisa. Sawa na wanaume, wanawake wameumbwa katika mfano wa Mungu.

Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba (Mwanzo 1:27).

Bila shaka tunajua kwamba Mungu alimwumba Adamu kabla ya kumwumba Hawa, na hilo ni jambo lenye umuhimu wa kiroho kulingana na Paulo (ona 1Timo. 2:3). Baadaye tutatazama umuhimu wa mpango huo katika uumbaji kama unavyoelezwa na Paulo, lakini inatosha tu kwa sasa kusema kwamba hiyo haithibitishi ubora wa wanamume juu ya wanawake. Wote tunajua kwamba Mungu aliwaumba wanyama kabla ya binadamu (ona Mwanzo 1:24-28)[1]

Mwanamke aliumbwa awe msaidizi wa mumewe (ona Mwanzo 2:18). Hapa tena, huo si uthibitisho wa udogo wake bali huonyesha tu nafasi yake katika ndoa. Roho Mtakatifu ametolewa kuwa msaidizi wetu, lakini si wa hali ya chini kuliko sisi. Roho Mtakatifu yuko juu yetu! Na ni sahihi kabisa kusema kwamba Mungu alipomwumba mwanamke awe msaidizi wa mumewe inathibitisha kwamba wanaume wanahitaji msaada! Mungu ndiye aliyesema kwamba haikuwa vema kwa manamume kuwa peke yake (ona Mwanzo 2:18). Ukweli huo umethibitishwa mara nyingi sana katika historia, wakati wanaume wanapoachwa wenyewe bila wake wa kuwasaidia.

Mwisho – tunaona tangu kurasa za kwanza kabisa za Mwanzo kwamba mwanamke wa kwanza aliumbwa kutoka nyama ya mwanamume wa kwanza. Alichukuliwa kutoka kwake, kuonyesha kwamba kuna anachokosa pasipo yeye, na kwamba hao wawili walikuwa mmoja hapo kwanza. Zaidi ni kwamba, kile ambacho Mungu alikitenga kilikusudiwa kuunganika tena kwa njia ya mahusiano ya kushirikiana kimwili, jambo ambalo si la kuzaana na kuongezeka tu, bali la kuonyesha upendo na kufurahiana wote wawili, ambapo kila mmoja anamtegemea mwingine.

Kila kitu juu ya masomo haya kutoka uumbaji kinapingana na wazo la jinsia moja kuwa juu au bora kuliko nyingine, au moja kuwa na haki ya kutawala nyingine. Na kwa kuwa Mungu ameweka wajibu tofauti kwa wanawake au huduma haihusiani na usawa wao na wanaume ndani ya Kristo, ambako “hakuna mtu mume wala mtu mke” (Wagalatia 3:28, TLR).

Wanawake Katika Huduma – Agano La Kale

Baada ya kuweka msingi huo, hebu sasa tutazame baadhi ya wanawake ambao Mungu aliwatumia kutimiza makusudi Yake katika Agano la Kale. Ni dhahiri kwamba Mungu aliwaita wanaume kuingia katika huduma kama kazi katika kipindi cha Agano la Kale, kama alivyofanya katika kipindi cha Agano Jipya. Habari za wanaume kama vile Musa, haruni, Yoshua, Yusufu, Samweli na Daudi zimejaa katika kurasa za Agano la Kale.

Ila, kuna wanawake wengi tu wanaotokezea hapo kama ushahidi kwamba Mungu anaweza kumwita na kumtumia yeyote atakaye, na wanawake waliowezeshwa na Mungu wanatosha kufanya kazi yoyote atakayowaitia.

Kabla ya kutazama mwanamke mmoja, ni vizuri ijulikane kwamba kila mtu maarufu wa Mungu katika Agano la Kale alizaliwa na kulelewa na mwanamke. Asingekuwepo Musa bila ya mwanamke aliyeitwa Yokebedi (ona Kutoka 6:20). Wala wasingekuwepo watu wengine maarufu na wakuu wa Mungu kama si akina mama wa hao watu. Wanawake wamepewa na Mungu wajibu mzito na huduma yenye sifa kubwa ya kuwakuza watoto katika Bwana (ona 2Timo. 1:5).

Yokebedi hakuwa mama wa wanaume wawili walioitwa na Mungu tu – Mus ana Haruni – bali pia alimzaa mwanamke aliyeitwa na Mungu. Huyo ni Miriamu dada yao, nabii wa kike na kiongozi wa kuabudu (ona Kutoka 15:20). Katika Mika 6:4, Mungu anamweka Miriamu pamoja na Musa na Haruni, kama viongozi wa Israeli.

Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako (maneno mepesi kutilia mkazo).

Ni kweli kwamba nafasi ya Miriamu ya uongozi katika Israeli haikuwa kubwa sana kama Musa. Lakini, kama nabii wa kike, Miriamu alinena kwa niaba ya Mungu, nami nadhani kwamba ni salama kusema kwamba jumbe za Mungu kupitia kwake zililengwa kwa wanaume wa Israeli, si wanawake tu.

Mwamuzi Mwanamke Juu Ya Israeli

Mwanamke mwingine ambaye Mungu alimwinua kuwa kiongozi katika Israeli ni Debora, aliyeishi wakati wa kipindi cha waamuzi wa Israeli. Yeye naye alikuwa nabii wa kike, na alikuwa mwamuzi juu ya Israeli sawa na akina Gidioni, Yefta na Samsoni wakati wao. Tunaambiwa kwamba “wana wa Israeli walimwendea awaamue” (Waamuzi 4:5, TLR). Basi, akatoa maamuzi kwa ajili ya wanaume, si wanawake tu. Angalia usikose hili: Mwanamke aliwaambia wanaume kitu cha kufanya, na Mungu alimtia mafuta afanye hivyo.

Kama wanawake wengi ambao Mungu huwaita katika uongozi, Debora alikabiliwa na mwanamume mmoja ambaye aliona taabu kupokea neno la Mungu kupitia chombo cha kike. Jina lake aliitwa Baraki, na kwa sababu alikuwa na mashaka kuhusu maagizo ya Dobora ya kinabii kwake kwamba akapigane vita na jemadari Mkanani aliyeitwa Sisera, Debora alimwambia kwamba heshima ya kumwua huyo Sisera ingemwendea mwanamke. Ndivyo ilvyokuwa, na mwanamke aitwaye Yaeli anakumbukwa katika Maandiko kwamba ndiye aliyemtoboa kichwa Sisera akiwa amelala, kwa kigingi cha hema (ona Waamuzi 4). Kisa hiki kinamalizika kwa Baraki akiimba wimbo wa kupokezana, na Debora! Baadhi ya mafungu yamejaa sifa kwa ajili ya Debora na Yaeli (ona Waamuzi 5), kwa hiyo, pengine Baraki alikuja kuamini “huduma ya wanawake” mwishowe!

Nabii Wa Tatu Mwanamke

Mwanamke wa tatu anayetajwa katika Agano la Kale kwamba ni nabii wa kuheshimika ni Hulda. Mungu alimtumia kutoa mtazamo unaoaminika wa kinabii na maagizo kwa mwanamume, mfalme aliyekuwa na wasiwasi sana, wa Yuda (ona 2Wafalme 22). Hapa tena tunaona mfano wa Mungu akimtumia mwanamke kumfundisha mwanamume. Bila shaka Hulda alitumiwa na Mungu kwa huduma kama hiyo mara kwa mara, vinginevyo Yosia asingekuwa na imani kubwa katika aliyomwambia.

Kwa nini Mungu alimwita Miriamu, Debora na Hulda kufanya kazi kama manabii wanawake? Mbona asiwaite wanaume?

Hakika Mungu angeweza kuwaita wanaume kufanya hayo hayo yaliyofanywa na wanawake watatu. Lakini hakuwaita. Na hakuna ajuaye sababu. Tunachotakiwa kujifunza kutokana na hili ni kwamba ni vizuri tujihadhari juu ya kumweka Mungu kwenye sanduku kwa habari ya anamwita nani kwenye huduma. Ingawa Mungu kawa kawaida alichagua wananume kufanya kazi wa uongozi katika Agano la Kale, wakati mwingine alichagua wanawake.

Mwisho – ijulikane kwamba hiyo mifano yote mitatu ya watumishi wanawake katika Agano la Kale walikuwa manabii. Zipo huduma zingine za Agano la Kale ambazo wanawake hawakuitwa kuzifanya. Kwa mfano: Hakuna wanawake walioitwa kuwa makuhani. Hivyo, yawezekana Mungu ametenga huduma fulani kwa ajili ya wanaume tu.

Wanawake Katika Huduma – Agano Jipya

Cha kushangaza ni kwamba tunamkuta mwanamke aliyeita na Mungu kuwa nabii mwanamke katika Agano Jipya. Yesu alipokuwa na umri wa siku chache tu, Ana alimtambua na kuanza kutangaza kwamba ndiye Masiya.

Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi. Alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake (Luka 2:36-38. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ona kwamba Ana aliwaambia wote waliokuwa “wanautarajia wokovu wa Yerusalemu” habari za Yesu. Bila shaka walikuwemo na wanaume. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba Ana alikuwa anawafundisha wanaume habari za Kristo.

Kuna wanawake wengine katika Agano Jipya ambao Mungu aliwatumia kwa karama ya unabii. Mama yake Yesu – Mariamu – yuko katika fungu hilo (ona Luka 1:46-55). Kila mara maneno ya kinabii ya Mariamu yanaposomwa katika ibada ya kanisa, ni sawa kusema kwamba mwanamke analifundisha kanisa. (Na Mungu aliwaheshimu wanawake bila swali kwa kumtuma Mwana Wake duniani kwa njia ya mwanamke. Angeweza kufanya kwa njia zingine nyingi!)

Orodha hii inaendelea. Mungu alitabiri kwa kinywa cha nabii Yoeli kwamba wakati atakapomwaga Roho Wake, wana wa kiume na wa kike katika Israeli wangetabiri (ona Yoeli 2:28). Petro alithibitisha kwamba unabii wa Yoeli ulikuwa unafanya kazi katika kipindi cha agano jipya (ona Matendo 2:17).

Tunaambiwa katika Matendo 21:8-9 kwamba mwinjilisti Filipo alikuwa na binti wanne waliokuwa manabii.

Paulo aliandika kuhusu wanawake wakitoa unabii katika ibada za kanisa (ona 1Wakor. 11:5). Ni dhahiri kutokana na mantiki kwamba, wanaume walikuwepo.

Kwa mifano yote hiyo ya Maandiko kuhusu wanawake kutumiwa na Mungu kama manabii na kutoa unabii, kweli hatuna sababu nzuri ya kukataa wazo kwamba Mungu anaweza kuwatumia wanawake katika huduma hizo! Tena, hakuna kitu chochote kinachoweza kutupelekea sisi kufikiri kwamba wanawake hawawezi kuwatabiria wanaume kwa niaba ya Mungu.

Wanawake Kama Wachungaji?

Vipi kuhusu wanawake kutumika kama wachungaji? Inaonekana dhahiri kwamba nafasi ya mchungaji au mzee au mwangalizi imekusudiwa na Mungu ishikiliwe na wanaume.

Ni neno la kuaminiwa: Mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja (1Timo. 3:1-2. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru; ikiwa mtu hakushtakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja (Tito 1:5,6. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Paulo hasemi moja kwa moja kwamba wanawake wamekatazwa kushika wadhifa huo, kwa hiyo, tuwe makini tusitoe uamuzi wa mwisho. Inaonekana kwamba kuna wachungaji wengi wa kike, na wazee na waangalizi duniani kote siku hizi – hasa katika nchi zinazoendelea – ambao wanafanya vizuri sana. Ila, bado ndiyo wachache. Pengine Mungu mara moja moja anawaita wanawake kufanya kazi hiyo wakati ambapo katika hekima Yake, makusudi ya ufalme Wake yatatimizwa vizuri zaidi, au wakati kuanpokuwepo upungufu wa uongozi wa kiume wenye sifa zinazotakiwa. Pia yawezekana kwamba wachungaji wengi wa kike walio katika mwili wa kristo leo wana wito wa kushika nafasi zingine za huduma ambazo zinafaa KiBiblia kwao, kama vile nafasi ya nabii, ila, mfumo uliopo wa kanisa unawarhusu kufanya kazi kama wachungaji tu.

Kwa nini nafasi ya mchungaji au mzee au mwangalizi imetengwa kwa ajili ya wanaume tu? Kuelewa utendaji wa nafasi hiyo kutatusaidia. Sharti moja la Maandiko kuhusu mchungaji au mzee au mwangalizi ni kwamba,

[Awe] Mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) (1Timo. 3:4-5).

Sharti hili linaleta maana kabisa tunapotambua kwamba mzee wa Agano Jipya alisimamia kanisa dogo la nyumbani. Wajibu wake ulikuwa ni sawa na baba kusimamia familia yake. Hili linatusaidia kuelewa ni kwa nini nafasi ya mchungaji ishikwe na mwanamume – kwa sababu inafanana sana na mfumo wa familia, ambayo, kama inalingana na mpango wa Mungu, inatakiwa kuongozwa na mume, si mke. Tutasema zaidi juu ya hilo baadaye.

Wanawake Kama Mitume?

Tumegundua kwamba wanawake wanaweza kufanya kazi katika nafasi ya nabii (wakiitwa na Mungu). Vipi kuhusu aina zingine za huduma? Inasaidia kusoma salamu za Paulo katika Warumi 16, ambapo anawasifu baadhi ya wanawake waliofanya huduma kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Yawezekana hata mmoja akawa amepangwa kama mtume. Katika mafungu matatu yanayofuata, nimeandika majina ya wanawake wote kwa herufi nyepesi kama hizi.

Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea; kwamba mmpokee katika Bwana, kama iwapasavyo watakatifu; mkamasaidie katika neno lolote atakalohitaji kwenu; kwa sababu yeye naye amekuwa mssaidizi wa watu wengi, akanisaidia mimi pia (Warumi 16:1, 2. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Amesifiwa kweli kweli! Hatujui Fibi alikuwa anafanya huduma gani, lakini Paulo anamwita “mtumishi wa kanisa la Kenkrea” na “msaidizi wa wengi” pamoja na yeye (TLR). Chochote alichokuwa anafanya kwa ajili ya Bwana kinaonekana kilikuwa kikubwa sana mpaka Paulo anamsifu kwa kanisa lote la Rumi.

Kisha tutasoma habari za Priska (au Priskila), ambaye, pamoja na Akila mume wake, walikuwa na huduma muhimu sana kiasi cha kwamba makanisa yote ya Mataifa yaliwafurahia.

Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika Kristo Yesu, waliokuwa tayari hata kukatwa kichwa kwa ajili ya maisha yangu; ambao ninawashukuru, wala si mimi tu, ila na makanisa ya Mataifa yote pia. Nisalimieni na kanisa lililomo katika nyumba yao. Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa Kristo. Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika Kristo kabla yangu (Warumi 16:3-7. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kwa habari ya Yunia – inaonekana kwamba mtu ambaye ni “maarufu miongoni mwa mitume” bila shaka naye ni mtume tu. Kwa mahesabu hayo, Yunia alikuwa mtume wa kike. Priska na Mariamu walikuwa watenda kazi kwa ajili ya Bwana.

Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana. Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika Kristo, na Stakisi, mpenzi wangu. Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika Kristo. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo. Nisalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana. Msalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana. Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana. Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana, na mamaye, aliyae mama yangu pia. Nisalimieni Asinkrito, Flegoni, Herme, Patroba, Herman a ndugu walio pamoja nao. Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote walio pamoja nao (Warumi 16:8-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Basi ni dhahiri kwamba wanawake wanaweza kuwa “watenda kazi” katika huduma.

Wanawake Kama Waalimu?

Vipi kuhusu waalimu wa kike? Agano Jipya halitaji hata mmoja. Wala Biblia haitaji wanaume wowote walioitwa kuwa waalimu. Priska (aliyetajwa hapo juu) mke wa Akila, alihusika katika kufundisha kwa sehemu ndogo. Kwa mfano: Wakati yeye na Akila walipomsikia Apolo akihubiri Injili yenye upungufu mwingi sana huko Efeso, “walimchukua na kumwelezea njia ya Mungu kwa usahihi zaidi” (Matendo 18:26, TLR). Hakuna awezaye kupinga kwamba Priska alimsaidia mume wake kumfundisha Apolo, aliyekuwa mwanamume. Tena, Paulo anawataja Priska na Akila mara mbili katika Maandiko, wakati anaposema juu ya “kanisa lililoko nyumbani mwao” (ona Warumi 16:3-5; 1Wakor. 16:19), na anawaita wote wawili “watenda kazi wenzangu katika Kristo” katika Warumi 16:3. Hapana shaka kwamba Priska alikuwa na nafasi tendaji katika huduma pamoja na mume wake.

Wakati Yesu Alipowaamuru Wanawake Wawafundishe Wanaume

Kabla hatujashughulikia maneno ya Paulo kuhusu wanawake kunyamaza kimya kanisani nay eye kuwakataza wanawake kufundisha wanaume, hebu tutazame andiko moja litakalotusaidia kulinganisha vizuri hayo.

Yesu alipofufuka, malaika aliwaagiza wanawake watatu kwenda kuwafundisha wanafunzi wa kiume wa Yesu. Hao wanawake waliamriwa kuwaambia wanafunzi kwamba Yesu amefufuka, na kwamba angewatokea huko Galilaya. Si hayo tu. Muda mfupi baadaye, Yesu Mwenyewe aliwatokea wanawake hao na kuwaamuru wakawaambie wanafunzi waende Galilaya (ona Mat hayo 28:1-10; Marko 16:1-7).

Kwanza, mimi nadhani ni kitu muhimu sana kwamba Yesu alichagua kuwatokea wanawake kwanza, kisha wanaume. Pili, kama kungekuwepo na kitu chochote kibaya kimsingi au kiadili, kuhusu wanawake kuwafundisha wanaume, ungetarajia kwamba Yesu asingewaambia wanawake wawafundishe wanaume kuhusu kufufuka Kwake – jambo ambalo si dogo – na ambalo Yeye Mwenyewe angeweza kuwafikishia (kama alivyofanya baadaye). Hakuna mtu awezaye kupinga hoja hii: Bwana Yesu aliwaagiza wanawake wafundishe kweli muhimu sana na kutoa maagizo fulani ya kiroho, kwa wanaume.

Maandiko Yenye Utata

Sasa kwa kuwa tunafahamu kidogo yale ambao Biblia inatuambia kuhusu nafasi za wanawake katika huduma, tutaweza kutafsiri vizuri yale “Maandiko yenye utata” katika nyaraka za Paulo. Hebu kwanza tutazame maneno yake kuhusu wanawake kunyamaza makanisani.

Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. Nao wakitaka kujifunza neno lolote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa (1Wakor. 14:34-35).

Kwanza – Kuna wenye swali kutokana na sababu nyingi, ikiwa hayo ni maagizo ya Paulo au anarudia kusema yale ambayo Wakorintho walikuwa wamemwandikia. Ni dhahiri kwamba katika sehemu yapili ya barua yake hiyo, Paulo alikuwa anajibu maswali ambayo Wakorintho walikuwa wamemwuliza kwa barua (ona 1Wakor. 7:1, 25; 8:1; 12:1; 16:1, 12).

Pili – katika mstari unaofuata, Paulo anaandika kitu kinachoweza kuhesabiwa kuwa ni itikio lake kwa desturi ya Wakorintho ya jumla ya kuwanyamazisha wanawake makanisani. Anaandika hivi:

Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu? (1Wakor. 14:36).

Vyovyote vile, Paulo ni kama anayeuliza maswali mawili ambayo majibu yake ni dhahiri. Jibu kwa yote ni Hapana. Si Wakorintho waliotoa Neno la Mungu, wala Neno la Mungu halikutolewa kwao tu. Maswali ya Paulo basi ni kama makemeo, yanayoelekezwa kwenye viburi vyao. Kama ndiyo itikio lake kwa mistari hiyo miwili inayotangulia, inaonekana ni kama ifuatavyo: “Hivi, ninyi mnafikiri ni nani? Tangu lini mnatoa amri kuhusu Mungu amtumie nani kulisema Neno Lake? Mungu anaweza kuwatumia wanawake akitaka, nanyi ni wapumbavu kuwanyamazisha.”

Tafsiri hii inafaa kama tutafikiria kwamba Paulo – katika barua hii hii – tayari amekwisha andika juu ya njia inayofaa kwa wanawake kutoa unabii makanisani (ona 1Wakor. 11:5), kitu ambacho kinawataka wasinyamaze. Tena, mistari michaceh baada yah ii tunayochunguza, Paulo anawahimiza Wakorintho wote[2], ikiwa ni pamoja na wanawake, “watamani sana kutabiri” (1Wakor. 14:39, TLR). Basi itakuwa anajipinga mwenyewe kama kweli alikuwa anatoa amri ya jumla kwa wanawake kunyamaza katika ibada makanisani katika maandiko ya 14:34-35.

Mawazo Mengine

Lakini – hebu tuseme tu kwamba pengine hayo maneno ya 1Wakor. 14:34-35 ni maneno ya Paulo mwenyewe, naye anawaagiza wanawake wanyamaze. Tutafsirije maneno hayo?

Hapa tena, tutalazimika kushangaa ni kwa nini Paulo anatoa amri ya jumla namna hiyo kwa wanawake kunyamaza kabisa katika mikutano ya kanisa, wakati aliposema katika barua hiyo hiyo kwamba wanaweza kuomba hadharani na kutabiri – bila shaka katika mikutano ya kanisa.

Tena – Bila shaka Paulo aliijua mifano ile yote ambayo tumeitoa hapo mwanzoni kuhusu Mungu kuwatumia wanawake kulisema Neno Lake hadharani, hata kwa wanaume. Sasa – kwa nini awanyamazishe kabisa wale ambao Mungu amewahi kuwatia mafuta mara kwa mara ili waseme?

Kweli mawazo ya kawaida tu yanadai tukubali kwamba Paulo hakumaanisha kwamba wanawake wanyamaze kimya kabisa wakati wa ibada za kanisa. Kumbuka kwamba kanisa la kwanza walikutanikia majumbani na kula chakula pamoja. Kweli tufikiri kwamba wanawake hawakusema chochote tangu walipoingia nyumbani humo mpaka walipotoka? Kwamba hawakuzungumza chochote wakati wa kuandaa au kula chakula cha pamoja? Kwamba hawakusema chochote kwa watoto wao muda wote? Kufikiri hivyo ni ujinga.

Ikiwa mahali ambapo “wawili au watatu wamekusanyika” kwa jina la Yesu Yeye yuko katikati yao (ona Mathayo 18:20), na kama hiyo ni idadi halali ya mkutano wa kanisa, inakuwaje basi wakati wanawake wawili wanapokutanika pamoja katika jina la Yesu? Je, wasisemezane?

Hapana! Kama 1Wakorintho 14:34-35 kweli ni maagizo ya Paulo, basi alikuwa anashughulikia tatizo dogo la utaratibu katika makanisa. Kuna wanawake waliokuwa hawafuati utaratibu kwa namna fulani, kwa habari ya kuuliza maswali. Paulo hakumaanisha wanawake wanyamaze kimya kabisa kwa kipindi chote cha mkutano. Hata alipotoa maagizo yanayofanana na hayo mistari michache kabla ya hapo, yanayowahusu manabii, hakuwa na maana hiyo.

Lakini [nabii] mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze (1Wakor. 14:30, Maneno mepesi kutilia mkazo).

Hapa, maneno “anyamaze” maana yake “aache kusema kwa muda.”

Paulo pia aliwaagiza wale wanaonena kwa lugha kunyamaza kama hakuna mtafsiri kwenye kusanyiko.

Lakini asipokuwepo mwenye kufasiri, na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu (1Wakor. 14:28, Maneno mepesi kutilia mkazo).

Je, Paulo alikuwa anawaagiza watu kama hao kunyamaza kabisa wakati wote wa mkutano? Hapana! Alikuwa anawaambia wanyamaze kwa habari ya kunena kwao kwa lugha wakati hakuna mfasiri. Ona kwamba Paulo anawaambia “wanyamaze katika kanisa,” ambayo ndiyo maagizo anayotoa kwa wanawake katika 1Wakor. 14:34-35. Basi, kwa nini tutafsiri maneno ya Paulo kwa wanawake kwamba wanyamaze kanisani kuwa maana yake ni “wanyamaze kwa kipindi chote cha ibada”, kisha tutafsiri maneno yake kwa wanaonena kwa lugha bila utaratibu kuwa maana yake ni “wasiseme katika kipindi fulani cha ibada”?

Mwisho ni vizuri tuone kwamba Paulo hakuwa anazungumzana wanawake wote katika fungu hilo. Maneno yake yanawahusu wanawake walio na ndoa tu, kwa sababu wanaagizwa “wakawaulize waume zao nyumbani” kama wana maswali.[3] Pengine sehemu ya tatizo au tatizo zima kwa ujumla ni kwamba wanawake wenye ndoa walikuwa wanawauliza wanaume wengine maswali, zaidi ya waume zao. Kama ni hivyo, hali hiyo si halali, na ingedhihirisha aina fulani ya kutokuheshimu na kutokutii waume zao wenyewe. Kama hilo ndilo tatizo analoshughulikia Paulo, ndiyo sababu anajenga hoja yake kwenye ukweli kwamba wanawake wanapaswa kuwa watiifu (kwa waume zao bila shaka!) kama Torati ilivyodhihirisha kwa namna nyingi katika kurasa za kwanza kabisa za kitabu cha Mwanzo (ona 1Wakor. 14:34).

Kwa kuhitimisha, ni hivi: Kama Paulo kweli anatoa maagizo kuhusu wanawake kunyamaza kimya katika 1Wakor. 14:34-35, basi anawaambia wanawake walio-olewa tu wanyamaze kwa habari ya kuuliza maswali kwa wakati usiofaa, au kwa namna ambayo ilionyesha kutowaheshimu waume zao. Vinginevyo, wanaweza kutabiri, kuomba na kusema.

Andiko Lingine Lenye Utata

Mwisho, tunafikia fungu la pili “lenye utata” linalopatikana katika barua ya kwanza ya Paulo kwa Timotheo.

Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna. Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa (1Timo. 2:11-14).

Hakika Paulo alijua kuhusu Miriamu, Debora, Hulda na Ana – manabii wanne wanawake waliosema kwa niaba ya Mungu na kuwaambia wanawake na wanaume maneno ya Mungu na kuwafundisha mapenzi ya Mungu. Hakika alifahamu kwamba Debora, mwamuzi wa Israeli, alikuwa na mamlaka kiasi fulani juu ya wanaume na wanawake. Hakika alijua kwamba Mungu alimimina Roho Wake siku ile ya Pentekoste, akitimiza kwa sehemu unabiiw a Yoeli kuhusu siku za mwisho wakati ambapo Mungu angemimina Roho Wake juu ya wote wenye mwili, ili wana na binti watabiri na kutangaza Neno la Mungu. Hakika alijua kwamba Yesu aliwaagiza wanawake fulani wapeleke ujumbe kutoka Kwake kwa mitume Wake wanaume. Bila shaka alijua maneno yake mwenyewe, ya kuunga mkono wanawake kuomba na kutoa unabii katika mikutano ya kanisa, aliyowaandikia Wakristo wa Korintho. Bila shaka alikumbuka kwamba aliwaambia Wakorintho kwamba yeyote kati yao anaweza kupokea fundisho la kuwaambia wengine kutoka kwa Roho Mtakatifu (ona 1Wakor. 14:26). Sasa, alitaka watu wapate nini alipoandika maneno haya kwa Timotheo?

Ona kwamba Paulo anajenga hoja yake kwenye kweli mbili zinazokubaliana kutoka Mwanzo, kwa ajili ya kufundisha: (1) Adamu aliumbwa kabla ya Hawa, na (2) Hawa ndiye alidanganywa, si Adamu, naye akaangukia katika kosa. Kweli ya kwanza inathibitisha mahusiano sahihi kati ya mume na mke. Kama uumbaji unavyofundisha, mume anatakiwa kuwa kichwa – jambo ambalo Paulo analifundisha mahali pengine (ona 1Wakor. 11:3; Waefeso 5:23-24).

Kweli ya pili anayotaja Paulo haikusudii kuonyesha kwamba wanawake ni rahisi zaidi kudanganywa kuliko wanaume. Si hivyo. Ukweli ni kwamba, kwa kuwa wanawake ni wengi kuliko wanaume katika mwili wa Kristo, hoja inaweza kutolewa kwamba wanaume ndiyo rahisi kudanganyika kuliko wanawake. Hata hivyo – kweli yapili inaonyeah kwamba wakati mpango uliokusudiwa wa Mungu katika familia unapopuuzwa, Shetani anaweza kuingia. Tatizo la binadamu lilianza bustanini, wakati mahusiano kati ya mume na mke wake yalipotoka kwenye utaratibu – mke wa Adamu hakumtii. Adamu lazima alimwambia mke wake agizo la Mungu kuhusu tunda lililokatazwa (ona Mwanzo 2:16-17; 3:2-3). Shida ni kwamba yeye hakufuata alichoambiwa na mumewe. Kuna jinsi alivyotumia mamlaka juu yake wakati alipompa tunda hilo ale (ona Mwanzo 3:6). Hapo, si Adamu aliyemwongoza Hawa, ni Hawa alimwongoza Adamu. Matokeo yakawa balaa.

Kanisa – Mfano Wa Familia

Utaratibu ambao Mungu amekusudia kwa ajili ya familia unapaswa kuonyeshwa na kanisa. Kama nilivyosema mapema, ni muhimu kukumbuka kwamba kwa miaka mia tatu ya kwanza ya historia ya kanisa, vikundi vya kanisa vilikuwa vidogo. Walikutania majumbani. Wachungaji na wazee na waangalizi walikuwa kama baba wa familia. Huo mpango wa kanisa wa KiMungu ulifanana sana na familia, na kwa kweli ulikuwa ni familia ya kiroho, kiasi cha kwamba uongozi wa kike juu yake ungepeleka ujumbe usio sahihi kwa familia za nje na hata ndani ya kanisa. Hebu fikiri mchungaji au mzee au mwangalizi wa kike akifundisha kila wakati katika kanisa la nyumbani, na mume wake ameketi kwa utii pale, akimsikiliza akifundisha na kutii mamlaka yake. Hiyo ingekwenda kinyume na utaratibu wa Mungu katika familia, na kuweka mfano usio sahihi.

Hicho ndicho Paulo anashughulikia. Ona kwamba maneno hayo yako karibu tu na maelezo kuhusu masharti ya mtu kuwa mzee (ona 1Timo. 3:1-7). Shartri moja ni kwamba awe mwanamume. Pia ijulikane kwamba wazee walipaswa kufundisha mara kwa mara kanisani (ona 1Timo. 5:17). Maneno ya Paulo kuhusu wanawake kupokea mafundisho kwa utulivu na kutoruhusiwa kufundisha au kutawala wanaume bila shaka yanahusiana na utaratibu sahihi wa kanisa. Anachosema kwamba si sahihi ni mwanamke – kwa sehemu au kikamilifu kabisa – kutimiza kazi ya mzee au mchungaji au mwangalizi.

Hii si kusema kwamba mwanamke au mke hawezi kuomba, kutabiri, kupokea fundisho fupi la kuwaambia washirika, au kusema kwa ujumla katika mkutano wa kanisa – akiwa chini ya mamlaka ya mume wake. Hayo yote anaweza kufanya kanisani bila ya kuharibu utaratibu wa Mungu, kama ambavyo anaweza kufanya hayo yote nyumbani bila kuwa amekiuka mpango wa Mungu. Alichokatazwa kufanya kanisani ni sawa na alichokatazwa kufanya nyumbani – kumtawala mume wake, au kuwa na mamlaka juu ya mume wake.

Kutokana na mistari ya baadaye tunaona kwamba wanawake wangeweza kufanya kazi kama shemasi, sawa na wanaume (ona 1Timo. 3:12). Kuhudumu kanisani kama shemasi au mtumishi (ambayo ndiyo maana ya neno lenyewe) hakudai kuvunjwa kwa utaratibu wa Mungu kati ya mume na mke.

Hii ndiyo njia pekee ya kulinganisha maneno ya Paulo katika 1Timo. 2:11-14 na mengine yote yanayofundishwa na Maandiko. Katika kila mfano wa Maandiko tuliotazama wa Mungu kuwatumia wanawake, hakuna uliokuwa mfano wa familia kama kanisa lilivyo, na kwa hali hiyo, hakuna unaovunja utaratibu wa Mungu. Hatupati popote mfano wa wanawake wakiwa na mamlaka juu ya waume zao katika familia. Kumbuka tena kusanyiko dogo la familia kadhaa katika nyumba, na mke ndiye anasimamia kundi hilo: akifundisha na kulisimamia wakati mume wake ameketi tu na kutii uongozi wake. Mungu hataki hayo, maana ni kinyume na utaratibu Wake kwa ajili ya familia.

Ila – kwa Debora kuwa mwamuzi wa Israeli, Ana kuwaambia wanaume habari za kristo, na Mariamu na rafiki zake kuwaambia mitume kuhusu ufufuo wa Kristo – hakuna ujumbe wowote mbaya unaopelekwa au kwa njia yoyote ile kuonyesha isivyostahili utaratibu wa Mungu katika familia. Kusanyiko la kila mara la kanisa ni nyeti, ambapo ipo hatari kwa ujumbe usiostahili kutumwa ikiwa wanawake au wake watakuwa na mamlaka na kuwafundisha wanaume au waume kila mara.

Kumalizia

Kama tukijiuliza tu hivi: “Ni kitu gani kinachoweza kuwa kosa kimsingi kwa wanawake kufanya huduma, wakiwatumikia wengine kwa moyo wa huruma na kutumia vipawa vyao walivyopewa na Mungu? Kuna kanuni gani ya kiadili inayovunjwa?” Ndipo baadaye tunatambua kwamba kuvunjwa kwa kanuni ni kama huduma ya mwanamke kwa namna moja au nyingine ingehalifu utaratibu wa Mungu kwa habari ya mahusiano kati ya wanaume na wanawake, kati ya waume na wake zao. Katika mafungu yote mawili “yenye utata” tuliyotazama, Paulo anataja utaratibu wa Mungu katika ndoa kama sababu yake ya kusema anachosema.

Basi, tunatambua kwamba wanawake wamezuiliwa kufanya huduma kwa sehemu ndogo sana. Kwa njia zingine nyingi tena kubwa, Mungu anataka kuwatumia wanawake kwa ajili ya utukufu Wake, Naye amekuwa akifanya hivyo kwa maelfu ya miaka. Maandiko yanazungumza kuhusu michango mingi inayofaa ambayo wanawake wameitoa kwa ufalme wa Mungu – na tumekwisha tazama baadhi yake. Tusije kusahau kwamba baadhi ya marafiki wa Yesu wa karibu sana walikuwa wanawake (ona Yohana 11:5), na kwamba wanawake walisaidia huduma Yake kifedha (ona Luka 8:1-3). Hakuna mwanamume anayetajwa kuwa alifanya hivyo. Yule mwanamke kisimani Samaria aliwaambia wanaume habari za Kristo kijijini kwake, na wengi walimwamini Yesu (ona Yohana 4:28-30, 39). Mwanafunzi mwanamke aitwaye Tabitha anasemekana kuwa “alizidi katika matendo ya wema na fadhili aliyofanya daima” (Matendo 9:36, TLR). Mwanamke ndiye alimtia Yesu mafuta kwa ajili ya maziko Yake, na alimsifu kwa hilo wakati wanaume wengine wlaipolalamika (ona Marko 14:3-9). Mwisho, Biblia inaandika kwamba wanawake ndiyo waliomwombolezea Yesu alipobeba msalaba Wake katika mitaa ya Yerusalemu. Hakuna mwanamume anayetajwa katika hilo. Hii mifano na mingi kama hiyo inapaswa kuwatia moyo wanawake kuinuka na kutimiza huduma zao walizopewa na Mungu. Tunawahitaji wote!


[1] Ijulikane kwamba kila mwanamume mwingine tangu Adamu ameumbwa na Mungu baada ya Mungu kuwaumba wanawake ambao walimzaa. Kila mwanamume baada ya Adamu ametoka kwa mwanamke, kama Paulo anavyotukumbusha katika 1Wakor. 11:11-12. Sidhani kama kuna yeyote ambaye atatoa hoja kwamba huo utaratibu wa KiMungu unathibitisha kwamba wanaume ni wadogo ukilinganisha na mama zao.

[2] Ushauri wa Paulo ni kwa “ndugu” – neno analotumia mara 27 katika barua hii, na ambalo linawahusu Wakristo wote katika Korintho, si wanaume tu.

[3] Ni vizuri kujua kwamba katika lugha ya asili ya Kiyunani, hakuna maneno tofauti kwa wanawake na mke, au mwanamume na mume. Hivyo inabidi kutambua kutoka mantiki ikiwa mwandishi anazungumza juu ya wanaume na wanawake, au waume na wake. Katika fungu tunalotazama, Paulo anazungumza na wake, kwa sababu wao ndiyo wangeweza kuwauliza waume zao chochote wakiwa nyumbani.