Kwa sababu ya shauku yake ya kutaka kufanya watu kuwa wanafunzi na kuwafundisha kuyashika yote ambayo Kristo aliagiza, mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi atavutiwa sana na Mahubiri ya Yesu pale Mlimani. Hakuna ujumbe mwingine mrefu wa Yesu ulioandikwa, nao umejaa maagizo au amri Zake. Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi atataka kutii mahubiri hayo na kuwafundisha wanafunzi wake kila kitu alichoamuru Yesu katika mahubiri hayo.
Kwa kuwa ni hivyo, nitakushirikisha ninayoelewa kuhusu mahubiri hayo, yapatikanayo katika Mathayo sura ya 5 hadi 7. Ninawatia moyo watumishi kuwafundisha wanafunzi wao Mahubiri ya Yesu ya Mlimani mstari kwa mstari. Natumaini kwamba niliyoandika yatasaidia kufanikisha jambo hilo.
Ufuatao ni ufupisho au muhtasari wa Mahubiri ya Yesu Mlimani, ili kutusaidia kuyaona kwa mtazamo wa jumla pamojana kuonyesha mada kuu.
I) Yesu akusanya wasikilizaji Wake (5:1-2)
II) Utangulizi (5:3-20)
A) Sifa na baraka za wenye heri (au waliobarikiwa) (5:3-12)
B) Wito wa kuendelea kuwa chumvi na nuru (5:13-16)
C) Uhusiano kati ya Torati na wafuasi wa Kristo (5:17-20)
III) Mahubiri Yenyewe: Kuwa na haki kuliko waandishi na Mafarisayo (5:21 – 7:12)
A) Pendaneni, si kama waandishi na Mafarisayo (5:21-26)
B) Usafi katika maadili ya kimwili. Msiwe kama waandishi na Mafarisayo (5:27-32)
C) Uwe mkweli, si kama waandishi na Mafarisayo (5:33-37)
D) Msilipe kisasi, kama wanavyofanya waandishi na Mafarisayo (5:38-42)
E) Msiwachukie adui zenu, kama wanavyofanya waandishi na Mafarisayo (5:43-48)
F) Tenda mema kwa nia njema, si kama waandishi na Mafarisayo (6:1-18)
1) Wape maskini kwa nia njema (6:2-4)
2) Omba kwa nia njema (6:5-6)
3) Maelezo kidogo kuhusu maombi na msamaha (6:7-15)
a) Mafundisho kuhusu maombi (6:7-13)
b) Umuhimu wa kusameheana (6:8-15)
4) Funga kwa nia njema (6:16-18)
G) Usitumikie fedha, kama waandishi na Mafarisayo (6:19-34)
H) Usitafute makosa madogo madogo kwa ndugu yako (7:1-5)
I) Usipoteze wakati kuwapa ukweli watu wasio na shukrani (7:6)
J) Himizo kuhusu kuomba (7:7-11)
IV) Hitimisho: Ufupisho wa Mahubiri Yenyewe
A) Maneno ya ufupisho (7:12)
B) Ushauri kuhusu kutii (7:13-14)
C) Jinsi ya kutambua manabii na waamini wa uongo (7:15-23)
D) Onyo la mwisho kuhusu kutokutii, na ufupisho (7:24-27)
Yesu Akusanya Wasikilizaji Wake
Naye alipowaona makutano alipanda mlimani; na baada ya kuketi, wanafunzi Wake walimjia. Naye, akifunua kinywa Chake alianza kuwafundisha (Mathayo 5:1-2, TLR).
Inaonekana kwamba Yesu alipunguza ukubwa wa wasikilizaji Wake kwa makusudi, maana aliondoka kuwaacha “makundi”, akapanda mlimani. Tunaambiwa “wanafunzi Wake wakamwendea,” kama ishara kwamba ni wale tu waliokuwa na njaa ya kumsikiliza ndiyo walikuwa radhi kupambana na kilima mpaka kufikia mahali alipopumzikia. Bila shaka walikuwa wengi maana katika 7:28 wanaitwa “makutano”.
Yesu akaanza mahubiri Yake akizungumza na wanafunzi Wake, na tangu mwanzo tunapata kidokezo kuhusu mada Yake kuu. Anawaambia wamebarikiwa (au wana heri) kama watakuwa na tabia fulani, kwa sababu tabia hizo ni za wanaokwenda mbinguni. Hiyo ndiyo mada itakayotawala mahubiri haya – Watakatifu tu ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu. Kiini hicho kinatawala sehemu ya mahubiri hayo yenye kuzungumza kuhusu “Heri”, katika 5:3-12.
Yesu aliorodhesha vitu mbalimbali vinavyoonyesha watu waliobarikiwa (au wenye heri), na akaahidi baraka nyingi mbalimbali kwao. Wasomaji wa juu juu mara nyingi hufkiri kwamba kila Mkristo anapaswa kujitafuta katika “Heri” mojawapo – moja tu. Ila – wasomaji waangalifu wanatambua kwamba Yesu hakuwa anapanga orodha ya waamini wa aina tofauti watakaopokea baraka mbalimbali, bali alizungumza juu ya waamini wote wa kweli watakaopokea baraka moja tu ya jumla katika siku za baadaye: kuurithi ufalme wa mbinguni. Hakuna njia nyingine inayofaa ya kutafsiri maneno yake, yafuatayo:
Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibirishwa. Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu (Mathayo 5:3-12).
Baraka Zenyewe, Na Tabia
Kwanza, hebu tutazame zile baraka zote zilizoahidiwa. Yesu alisema hivi: Hao wenye heri – (1) wataurithi ufalme wa mbinguni, (2) watafarijiwa, (3) watairithi nchi, (4) watashibishwa, (5) watapata rehema, (6) watamwona Mungu, (7) wataitwa wana wa Mungu, na (8) wataurithi ufalme wa mbinguni (marudio ya namba 1).
Je, Yesu anataka tudhani kwamba ni walio maskini wa roho na ambao wameteswa kwa ajili ya haki ndiyo tu watakaorithi ufalme wa Mungu? Je, ni wale walio safi moyoni tu ndiyo watakaomwona Mungu, na ni wale wapatanishi tu ndiyo watakaoitwa watoto wa Mungu, lakini hakuna atakayerithi ufalme wa Mungu? Tukifikiri hivyo tutakuwa tunakosea. Basi, ni salama kusema kwamba zile baraka nyingi zilizoahidiwa ni baraka mbalimbali zilizomo katika baraka moja kuu – kuurithi ufalme wa Mungu.
Sasa, hebu tufikiri zile tabia mbalimbali ambazo Yesu alitaja: (1) maskini wa roho, (2) wenye huzuni, (3) wapole, (4) wenye njaa na kiu ya haki, (5) wenye rehema, (6) wenye moyo safi, (7) wapatanishi, na (8) wenye kushutumiwa na kuudhiwa.
Je, Yesu anataka tufikiri kwmaba mtu anaweza kuwa na moyo safi lakini akakosa rehema? Je, mtu anaweza kushutumiwa na kuudhiwa kwa ajili ya haki na asiwe mwenye njaa na kiu ya haki? Hapo tena tunasema haiwezekani. Zile tabia au sifa nyingi za walio na heri ni tabia mbalimbali ambazo, kwa pamoja – kwa kiwango fulani – zinapatikana katika wote wenye heri.
Ni dhahiri basi kwamba Maandiko hayo yanaeleza tabia au sifa za wafuasi wa kweli wa Yesu. Kwa kuorodhesha sifa hizo kwa wanafunzi Wake, aliwahakikishia kwamba wao wana heri na wameokoka, na ndiyo wangefurahia mbingu siku moja. Kwa wakati huo wanaweza wasijisikie kuwa ni heri kwa sababu ya mateso yao, na dunia inayowatazama inaweza ikawaona si heri, lakini machoni pa Mungu wao ni heri.
Ni hivi: Watu wasiolingana na maelezo ya Yesu si heri, na hawataurithi ufalme wa mbinguni. Kila mchungaji anayefanya watu kuwa wanafunzi anawajibika kuhakikisha kwamba watu katika kundi lake wanajua hayo.
Tabia Za Walio Heri
Hizo sifa au tabia nane za walio heri zinatakiwa kutafsiriwa kiasi fulani. Kwa mfano: Nini cha kujisifia ukiwa “maskini wa roho”? Mimi nadhani kwamba Yesu alikuwa anaeleza sifa ya kwanza muhimu ambayo mtu lazima awe nayo kama ataokolewa – lazima atambue umaskini wake kiroho. Mtu lazima kwanza aone kwamba anamhitaji Mwokozi ndipo aokolewe, na walikuwepo watu aina hiyo katika wasikilizaji wa Yesu waliokuwa ametambua hali yao mbaya. Kweli, wao walikuwa na heri, ukiwalinganisha na Israeli wenye kiburi, waliokuwa hawaona dhambi zao!
Hiyo sifa ya kwanza inaondoa hali yoyote ya kujitegemea au kujitosheleza, na wazo lolote kwamba mtu anastahili wokovu. Mtu mwenye heri kweli kweli ni yule anayetambua kwamba hana chochote cha kumpa Mungu, na kwamba haki yake binafsi ni sawa na “matambara machafu” (Isaya 64:6, TLR).
Yesu hakutaka mtu yeyote afikiri kwamba kwa juhudi zake mwenyewe anaweza kujipatia sifa za kuwa heri. Hapana. Watu wana heri – yaani, kubarikiwa na Mungu – kama watakuwa na tabia au sifa za wenye heri. Hayo yote yanatoka katika neema ya Mungu. Watu wenye heri ambao Yesu alizungumza juu yao walikuwa heri, si kwa sababu ya kilichokuwa kinawangojea mbinguni, bali kwa sababu ya kazi Mungu aliyokuwa amefanya katika maisha yao duniani. Ninapoona sifa za mwenye heri maishani mwangu zinatakiwa kunikumbusha juu ya kile ambacho Mungu amefanya ndani yangu kwa neema Yake, si kunikumbusha kile nilichofanya mimi.
Wenye Huzuni
Kama sifa ya kwanza kutajwa imetajwa kwa sababu ndiyo sifa ya kwanza inayotakiwa kwa wanaokwenda mbinguni, pengine ya pili nayo imetajwa ya pili kwa sababu maalum. “Heri wenye huzuni” (Mathayo 5:4). Je, Yesu alikuwa anazungumza kuhusu toba kutoka moyoni pamoja na kujisikia vibaya? Yawezekana. Maana, Maandiko yako wazi kabisa kwamba huzuni ya kiMungu huzaa toba ambayo ni ya lazima kwa wokovu (ona 2Wakor. 7:10). Yule mtoza ushuru aliyekuwa na huzuni, ambaye Yesu alimtaja katika mfano, ni mtu wa aina hiyo mwenye heri. Yeye aliinamisha kichwa chake Hekaluni kwa unyenyekevu sana, akipiga-piga kifua chake na kuomba rehema za Mungu. Farisayo jirani yake ambaye, alipoomba, alimkumbusha Mungu – tena kwa kiburi – kwamba yeye alitoa fungu la kumi na kufunga mara mbili kwa juma. Yule mtoza ushuru aliondoka hapo akiwa amesamehewa dhambi zake. Katika kisa hicho, mtoza ushuru alikuwa heri; Farisayo hakuwa (ona Luka 18:9-14). Mimi nadhani kwamba, katika wasikilizaji wa Yesu walikuwepo wengine ambao kwa kusukumwa na Roho Mtakatifu, walikuwa wana huzuni. Faraja ya Roho Mtakatifu ingewafikia!
Kama Yesu hakuwa anazungumza juu ya ile huzuni ya mwanzo, ya mwenye dhambi anayetubu na kumjia Kristo, basi pengine alikuwa anazungumza juu ya huzuni ambayo waamini wote huipata wanapokabiliana kila siku na dunia inayomwasi Mungu, anayewapenda. Paulo alieleza hilo kuwa “huzuni kubwa na uchungu usiokoma moyoni” (Warumi 9:2).
Wenye Upole
Sifa ya tatu – upole – inatajwa pia katika Maandiko kwamba ni tunda mojawapo la Roho (tazama Wagalatia 5:22-23). Upole si tabia itokanayo na mtu binafsi. Wale ambao wamepokea neema ya Mungu na Roho anakaa ndani yao wamebarikiwa pia kufanyika wapole. Siku moja watairithi nchi, maana ni wenye haki tu watakaoishi kwenye dunia mpya ambayo Mungu anaiumba. Wanaojiita Wakristo ambao ni wakali na wenye fujo wajiangalie. Wao si heri.
Njaa Na Kiu Ya Haki
Sifa ya nne – kuwa na njaa na kiu ya haki – hueleza ile shauku ya ndani, itokayo kwa Mungu, ambayo kila mtu aliyezaliwa mara ya pili anayo. Yeye anahuzunishwa na maovu yote duniani, na sehemu inayobaki ndani yake. Anachukia dhambi (ona Zaburi 97:10; 119:128, 163), na anapenda haki.
Mara nyingi tunaposoma neno haki katika Maandiko, tunatafsiri upesi kwamba ni “kuhesabiwa kuwa wenye haki na Kristo”. Lakini, neno hilo halimaanishi hivyo wakati wote. Mara nyingi maana yake ni: “Hali ya kuishi kwa haki kulingana na viwango vya Mungu”. Bila shaka hiyo ndiyo maana aliyokusudia Yesu hapa, maana hakuna sababu kwa Mkristo kuwa na njaa na kitu alicho nacho tayari. Wale waliozaliwa na Roho hutamani kuishi kwa haki, na uhakikisho ni kwamba “watashibishwa” (Mathayo 5:6). Ni hakika kwamba Mungu kwa neema Yake atakamilisha kazi aliyoianza ndani yao (ona Wafilipi 1:6).
Maneno ya Yesu hapa ni kama utabiri wa wakati wa dunia mpya – dunia ambayo “haki yakaa ndani yake” (2Petro 3:13). Hiyo haitakuwa na dhambi. Kila mtu atampenda Mungu kwa moyo wote na kumpenda jirani yake kama nafsi yake. Wale ambao sasa wana njaa na kiu ya haki watashibishwa wakati huo. Hatimaye, sala yetu ya dhati kabisa kutoka moyoni itajibiwa kikamilifu: “Mapenzi Yako yatimizwe hapa duniani, kama huko mbinguni” (Mathayo 6:10).
Wenye Rehema
Sifa ya tano – rehama – nayo inapatikana na kila mtu aliyezaliwa mara ya pili kwa sababu ya Mungu mwenye rehema kuishi ndani yake. Wale wasiokuwa na rehema hawana heri ya Mungu, nao wanadhihirisha kwamba si washiriki wa neema Yake. Mtume Yakobo anakubali – “Hukumu haitakuwa na rehema kwa asiyekuwa na rehema” (Yakobo 2:13, TLR). Unaonaje – mtu akisimama mbele za Mungu na kuhukumiwa pasipo rehema, ataingia mbinguni au jehanamu?[1] Nadhani jibu ni dhahiri kabisa.
Yesu alisimulia kisa fulani, cha mtumishi aliyepata rehema kutoka kwa bwana wake, ambaye hakuweza kumwonyesha mtumwa mwenzake rehema hata kidogo. Bwana wake alipogundua kilichokuwa kimetokea, alimpeleka “kwa watesaji mpaka atakapolipa kila alichokuwa anadaiwa” (Mathayo 18:34). Deni lake la zamani alilokuwa amesamehewa likarudi pale pale. Kisha Yesu akawaonya wanafunzi wake hivi: “Baba yangu wa mbinguni atafanya hivyo hivyo kwenu, kama ninyi hamtawasamehe ndugu zenu kutoka moyoni” (Mathayo 18:35). Kwa hiyo, kukataa kumsamehe ndugu au dada katika Kristo anayeomba msamaha husababisha dhambi zetu za zamani kurudishwa. Matokeo ni sisi kukabidhiwa kwa watesaji mpaka tulipe kitu ambacho hatuwezi kulipa. Na hapo si mbinguni. Narudia tena – wasio na rehema hawatapokea rehema kutoka kwa Mungu. Wao si heri.
Wenye Moyo Safi
Tabia au sifa ya sita ya wanaokwenda mbinguni ni usafi wa moyo. Tofauti na wengi wanaokiri Ukristo, wafuasi a kweli wa Kristo si watakatifu kwa nje tu. Mioyo yao imefanywa kuwa safi kwa neema ya Mungu. Wanampenda Mungu kweli kutoka ndani ya mioyo yao, na hali hiyo inaathiri tafakari zao na makusudi yao ya moyo. Yesu aliahidi kwamba watamwona Mungu.
Naomba niulize tena: Je, tuamini kwamba kuna waamini wa kweli Wakristo ambao si safi moyoni, na kwamba hawatamwona Mungu? Je, Mungu atawaambia, “Mnaweza kuingia mbinguni, lakini hamtaniona kamwe?” Hapana. Bila shaka, kila mwamini wa kweli aendaye mbinguni ana moyo safi.
Wapatanishi
Wapatanishi ndiyo wanaofuata. Wataitwa wana wa Mungu. Hapo tena ni kwamba Yesu anazungumza juu ya kila mfuasi wa kweli wa Kristo, maana kila amwaminiye Kristo ni mtoto wa Mungu (ona Wagalatia 3:26).
Wale waliozaliwa na Roho ni wapatanishi kwa namna tatu:
Kwanza – Wamefanya mapatano na Mungu, ambaye hapo kwanza alikuwa adui yao (ona Warumi 5:10).
Pili – Wanaishi kwa amani na watu wengine, kwa kiasi kinachowezekana. Si watu wenye tabia za vurugu na magomvi. Paulo aliandika kwamba wale wenye kutenda vurugu, fujo, wenye wivu, wenye ghadhabu, wenye mafarakano, wenye magomvi na kuleta mafarakano hawataurithi ufalme wa Mungu (ona Wagalatia 5:19-21). Waaini wa kweli watakwenda maili ya pili ili kuepuka ugomvi na kuhifadhi amani katika mahusiano yao. Hawadai kuwa na amani na Mungu na huku hawawapendi ndugu zao (ona Mathayo 5:23-24; 1Yohana 4:20).
Tatu – Kwa kuwaambia wengine Habari Njema (Injili), wafuasi wa kweli wa Kristo huwasaidia wengine nao kuwa na amani na Mungu, na wanadamu wenzao. Pengine Yakobo alikuwa anaunganisha hoja yake na Mahubiri ya Mlimani alipoandika hivi: “Na mbegu ile ambayo mazao yake ni haki, hupandwa katika amani na wale wafanyao amani” (Yakobo 3:8, TLR).
Wenye Kushutumiwa Na Kuudhiwa
Mwisho – Yesu alisema wale wanaoshutumiwa na kuteswa kwa ajili ya haki wana heri. Ni dhahiri kwamba alikuwa anazungumza na watu wenye kuishi maisha ya haki, si wale ambao wanafikiri tu kwamba haki ya Kristo imehesabiwa kwao. Watu wenye kutii amri za Kristo ndiyo wanaoshutumiwa au kuudhiwa na wasioamini. Hao wataurithi ufalme wa Mungu.
Sasa – Yesu alikuwa anazungumza juu ya kuudhiwa au shutuma za aina gani? Mateso kimwili? Kuteswa mpaka kufa? Hapana. Alichotaja hasa ni kutukanwa na kunenewa mabaya kwa ajili Yake. Hili tena linaonyesha kwamba wakati mtu anapokuwa Mkristo wa kweli, ni kitu kinachoonekana kwa wasioamini. Vinginevyo, wasioamini wasingejaribu kusema maovu kinyume chake. Je, ni wangapi wanaoitwa Wakristo wasioweza hata kutofautishwa na wasioamini kiasi cha kwamba wasioamini hawana la kusema vibaya juu yao? Ukweli ni kwamba hao si Wakristo wa kweli. Yesu alisema hivi: “Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo” (Luka 6:26). Watu wote wanapowasema vizuri, ni ishara kwamba wewe ni mwamini bandia. Dunia inawachukia Wakristo wa kweli (ona pia Yohana 15:18-21; Wagalatia 4:29; 2Timo. 3:12; 1Yohana 3:13-14).
Chumvi Na Nuru
Baada ya Yesu kuwahakikishia wanafunzi Wake watiifu kwamba walikuwa miongoni mwa waliobadilishwa na watu wenye heri, watakaourithi ufalme wa mbinguni, anatoa onyo. Yesu aliwapenda kweli kweli wanafunzi Wake halisi kiasi cha kuwaonya kwamba wangejiondoa katika fungu la wenye heri. Hii ni tofauti na wahubiri wengi wa siku hizi ambao wanawatia moyo tu mbuzi wa kiroho kwamba hawawezi kupoteza wokovu wanaodhani wanao.
Ninyi ni chumvi ya dunia. Lakini, chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru yaulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pichi, bali juu ya kiango, nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo, nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni (Mathayo 5:13-16).
Ona kwamba Yesu hakuwashauri wanafunzi Wake kufanyika chumvi au kufanyika nuru. Alisema (kimfano) kwamba wao ni chumvi tayari, na akawashauri wadumu kuwa chumvi. Alisema (kimfano) kwamba wao ni nuru tayari, na akawashauri wasiache nuru yao isifichike bali iendelee kung’aa. Hiyo ni tofauti sana na yale mahubiri wanayoambiwa wanaojiita Wakristo, kwamba kuna haja kwao kufanyika chumvi na nuru. Kama watu si chumvi na nuru tayari, si wanafunzi wa Kristo hao. Hawako miongoni mwa walio na heri. Hawaendi mbinguni hao.
Katika siku za Yesu, chumvi ilitumiwa kimsingi kama kihifadhi nyama. Sisi kama wafuasi watiifu wa Kristo ndiyo tunaohifadhi dunia hii yenye dhambi isioze kabisa na kupotoka. Lakini, tukiwa kama dunia kwa tabia, kweli “hatufai kwa chochote” (ms. 13). Yesu aliwaonya walio heri kudumu kuwa chumvi, yaani, wahifadhi tabia zao za kipekee. Ni lazima wawe tofauti na dunia inayowazunguka, wasije wakapoteza ladha yao, wakastahili “kutupwa nje na kukanyagwa na watu.” Hili ni onyo mojawapo kati ya mengi ya wazi kabisa kuhusu kurudi nyuma, yapatikanayo katika Agano Jipya, lenye kuelekezwa kwa waamini wa kweli. Kama chumvi ni chumvi kweli, itakuwa na ladha ya chumvi. Vivyo hivyo, wafuasi wa Yesu hutenda kama wafuasi wa Yesu. Vinginevyo, wao si wafuasi wa Yesu hata kama waliwahi kuwa hapo zamani.
Pia, wafuasi wa kweli wa Kristo ni nuru ya dunia. Nuru hung’aa kila wakati. Kama haing’ai, hiyo si nuru. Kwa mfano huu, nuru inafananishwa na matendo yetu mema (ona Mathayo 5:16). Yesu hakuwa anawashauri wale wasio na matendo mema wafanye bidii wapate. Aliwashauri wale wenye matendo mema wasifiche wema wao kwa watu. Kwa kufanya hivyo, wangemtukuza Baba yao wa mbinguni kwa sababu kazi Yake ndani yao ndiyo asili ya wema wao. Hapo tunaona mlingano mzuri sana kati ya kazi ya Mungu ya neema na ushirikiano wetu sisi – pande zote mbili hizo zinahitajiana ili mtu awe mtakatifu.
Uhusiano Wa Torati Na Wafuasi Wa Kristo
Tumefikia mahali muhimu katika mafundisho haya. Ni sehemu ya msingi na yenye maana sana – ni kama utangulizi wa mengi ambayo Kristo atasema katika sehemu inayosalia ya mahubiri Yake.
Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii. La! Sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni (Mathayo 5:17-20).
Ikiwa Yesu aliwaonya wasikilizaji Wake wasifikiri kwamba alikuwa anaitangua Torati au manabii, tunaweza kuamua kwamba bila shaka walikuwepo wachache katika kundi lililomsikiliza waliodhani hivyo. Kilichosababisha wafikiri hivyo hatukijui. Pengine ni kwa sababu Yesu aliwakemea vikali sana waandishi na Mafarisayo walioshika sana sheria.
Vyovyote vile ni kwamba, Yesu alitaka wanafunzi Wake watambue wazi wazi kosa la kufikiri hivyo. Yeye ndiye alivuvia Agano la Kale lote. Basi, asingeweza kutangua kila kitu alichosema kupitia kwa Musa na Manabii. Kinyume chake – angetimiliza Torati na Manabii, kama alivyosema.
Angetimilizaje Torati na Manabii? Kuna wanaofikiri kwamba Yesu alimaanisha kutimizwa kwa unabii uliomhusu Masiya. Ingawa kweli Yesu alitimiza (na bado atatimiza) kila unabii uliomhusu Masiya, hiyo haikuwa maana yake tu. Ni wazi kwamba mantiki ya mistari hiyo inaonyesha kwamba alikuwa anazungumza kuhusu yote yaliyoandikwa katika Torati na Manabii, mpaka “yodi ndogo kabisa” (ms. 18) ya Torati, na mpaka amri “iliyo ndogo kabisa” (ms. 19).
Kuna wengine wanaodhani kwmaba Yesu alimaanisha atatimiza Torati kwa kutimiza matakwa yake kwa niaba yetu, kwa maisha Yake ya kumtii Mungu na kifo Chake cha kujitoa (ona Warumi 8:4). Lakini ukitazama mantiki ya mistari husika, utaona kwamba hiyo haikuwa maana yake. Katika mistari inayofuata, yesu hasemi chochote kuhusu maisha Yake au kufa Kwake kwamba ni kitu kitakachotimiza Torati. Badala yake utaona kwamba katika mstari uliofuata alisema kwamba Torati itadumu mpaka “mbingu na nchi zitakapopita” na “kila kitu kitimizwe”. Hiyo inasema juu ya kipindi kirefu baada ya kifo Chake msalabani. Kisha akatangaza kwamba hali za moyo za watu kuhusu Torati zingeamua hata nafasi zao mbinguni (ms. 19), na kwamba watu lazima waitii Torati vizuri zaidi kuliko waandishi na Mafarisayo, la sivyo hawataingia mbinguni (ms. 20).
Basi, ni wazi kwamba, zaidi ya kutimiza tu unabii kuhusu Masiya na mifano yake ya Torati, pamoja na kutimiza matakwa ya Torati kwa niaba yetu, Yesu pia alikuwa anafikiri juu ya wasikilizaji Wake kuzishika amri za Torati na kufanya yaliyosemwa na Manabii. Kwa sehemu moja, Yesu angeitimiza Torati kwa kufunua kusudi la kweli la Mungu ndani yake, kwa kulifafanua na kuiunga mkono, na kukamilisha kilichokuwa kimepungua katika ufahamu wa wasikilizaje Wake.[2] Neno la Kiyunani linalotafsiriwa kutimiza katika mstari wa 17 ndilo linalotafsiriwa kukamilisha, kumaliza, kujaza na kutekeleza kikamilifu katika Agano Jipya. Hayo ndiyo Yesu aliyokuwa anataka kufanya, kama itakavyoonekana hapo baadaye.
Hapana. Yesu hakuja kutangua Torati wala Manabii. Alikuja kutimiliza – yaani – “kujazia.” Ninapofundisha fungu hili la Mahubiri ya Mlimani, mara nyingi ninawaonyesha watu bilauri ya maji ambayo iko nusu, ili kuwa mfano wa ufunuo wa Mungu aliotoa katika Torati na Manabii. Yesu hakuja kutangua Torati na Manabii (na ninaposema hivyo, ninajifanya kama anayetaka kumwaga yale maji). Kinyume chake, angetimiliza Torati na Manabii (na hapo, ninachukua chupa ya maji na kuijaza ile bilauri mpaka juu). Hilo huwasaidia watu kuelewa maana ya Yesu.
Umuhimu Wa Kushika Torati
Kuhusu kushika zile amri zipatikanazo katika Torati na Manabii, Yesu alisema mambo waziwazi kabisa. Aliwatazamia wanafunzi Wake kuziti. Zilikuwa za maana kama nini! Ukweli ni kwamba: Jinsi walivyothamini amri zile ingeamua nafasi yao mbinguni. “Basi, mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni” (5:19).
Ndipo tunafikia mstari wa 20 sasa – “Maana nawaambia ya kwamba haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”
Ona kwamba hilo si wazo jipya, bali wazo la kumalizia mistari ile mingine yote iliyotangulia. Imeunganishwa na neno maana. Je, ni muhimu kiasi gani kuzishika amri? Ni muhimu sana. Mtu anapaswa azishike vizuri zaidi kuliko waandishi na Mafarisayo ili aweze kuingia katika ufalme wa mbinguni. Hapo tena tunamwona Yesu akibakia kwenye mada Yake kuu – Ni watakatifu tu watakaorithi ufalme wa Mungu.
Ili asipingane na Kristo, yule mtumishi mwenye kufanya watu kuwa wanafunzi hawezi kumhakikishia mtu yeyote kwamba wokovu wake uko salama kama haki yake haizidi ya waandishi na Mafarisayo.
Je, Yesu Alikuwa Anazungumzia Haki Ya Namna Gani?
Je, Yesu alipotamka kwamba haki yetu lazima izidi ile ya waandishi na Mafarisayo, hakumaanisha ule msimamo kisheria wa haki ambao tungehesabiwa baada ya wokovu kama zawadi? Hapana, na ni kwa sababu nzuri tu. Kwanza: Mantiki yenyewe hailingani na tafsiri hiyo. Kabla na baada ya kusema hivyo (na katika mahubiri yote), Yesu alikuwa anazungumza juu ya kushika amri – yaani, kuishi maisha ya haki. Tafsiri ya karibu kabisa ya maneno Yake ni kwamba lazima tuishi kwa haki zaidi ya waandishi na Mafarisayo. Na ni upuuzi kufikiri kwamba Yesu aliwabana waandishi na Mafarisayo washike kiwango ambacho hakutaka wanafunzi Wake washike. Itakuwa ni upuuzi kabisa kufikiri kwamba Yesu angewahukukumu waandhsi na Mafarisayo kwa ajili ya kufanya dhambi ambazo asingewahukumia wanafunzi Wake kwa kuwa waliomba “sala ya wokovu” tu.[3]
Tatizo letu ni kwamba hatutaki kukubali maana halisi ya mstari huo, kwa sababu tunaona ni kukazia ushikaji wa sheria. Lakini, tatizo letu hasa ni kwamba hatuelewi umoja ulioko kati ya haki inayohesabiwa na haki halisi ya vitendo. Mtume Yohana alielewa, na akaandika hivi: “Watoto wadogo! Mtu yeyote asiwadangaye. Yeye atendaye haki ni mwenye haki” (1Yohana 3:7, TLR). Tena, hatuelewi umoja ulipo kati ya kuzaliwa upya na haki halisi ya vitendo. Yohana alielewa, na anasema hivi: “Kila atendaye haki amezaliwa na Yeye” (1Yohana 2:29, TLR).
Yesu angeweza kuongezea maneno, katika yale aliyosema katika 5:20. Angeweza kusema hivi: “Mkitubu, na kuzaliwa mara ya pili kweli, na kupokea zawadi yangu ya haki kw anjia ya imani hai, haki yenu ya vitendo itazidi ile ya waandishi na Mafarisayo mtakaposhirikiana na nguvu za Roho Wangu, akaaye ndani yenu.”
Jinsi Ya Kuwa Mtakatifu Kuliko Waandishi Na Mafarisayo
Bila shaka swali linalojitokeza hapo kama itikio la maneno ya Yesu katika 5:20 ni hili: Hao waandishi na Mafarisayo walikuwa na haki kiasi gani? Jibu ni hili: Haikuwa Nyingi.
Wakati fulani Yesu aliwaita “makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanapendeza, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote” (Mathayo 23:27, TLR). Yaani, walionekana kuwa wenye haki kwa nje, lakini ndani walikuwa waovu. Walijitahidi sana kushika andiko la Torati, lakini walipuuzia maana yake, na mara nyingi walijihesabia haki kwa kupindisha au hata kubadili amri za Mungu.
Hili tatizo la ndani la waandishi na Mafarisayo ndilo Yesu alikazia zaidi katika sehemu inayosalia ya Mahubiri Yake pale Mlimani. Tunakuta kwamba alitaja baadhi ya amri zinazojulikana sana za Mungu, na baada ya kutaja kila moja, alionyesha tofauti kati ya kushika andiko na maana ya kila sheria. Kwa kufanya hivyo, alifunua tena na tena mafundisho ya uongo na unafiki wa waandishi na Mafarisayo, na kudhihirisha matazamio halisi ambayo Yeye alikuwa nayo kwa wanafunzi Wake.
Yesu alianza kila mfano kwa kusema hivi: “Mmesikia”. Alikuwa anazungumza na watu ambao hawakuwahi kusoma magombo ya Agano la Kale bali walisikia yakisomwa katika masinagogi na waandishi na Mafarisayo. Ni sawa kusema kwamba wasikilizaji Wake walikuwa wameketi chini ya mafundisho ya uongo maisha yao yote, wakisikiliza maelezo na mafafanuzi potofu ya waandishi na Mafarisayo kuhusu Neno la Mungu, na kuona jinsi walivyoishi maisha yasiyokuwa matakatifu.
Mafarisayo kuhusu Neno la Mungu, na kuona jinsi walivyoishi maisha yasiyokuwa matakatifu.
Mafarisayo kuhusu Neno la Mungu, na kuyaona maisha waliyoishi, ambayo hayakuwa matakatifu.
Pendaneni. Si Kama Waandishi Na Mafarisayo
Kwa kutumia amri ya sita kama kianzio, Yesu alianza kufundisha wanafunzi Wake matazamio ya Mungu kwao, na hapo hapo akifunua unafiki wa waandishi na Mafarisayo.
Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, ‘Usiue’, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanamu ya moto (Mathayo 5:21-22).
Kwanza: Ona kwamba Yesu alikuwa anaonya kuhusu kitu kinachoweza kumsababisha mtu kwenda jehanamu. Hiyo ndiyo iliyokuwa mada Yake kuu – Watakatifu tu ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu.
Waandishi na Mafarisayo walihubiri na kukataza kuua, wakitumia amri ya sita, japo inaonekana wao walisema kuua kungemfikisha mtu mahakamani.
Yesu alitaka wanafunzi Wake wajue kitu ambacho ni kama waandishi na Mafarisayo hawakukitambua – yalikuwepo makosa mengine “madogo” ambayo yangemfikisha mtu mahakamani – mahakama ya Mungu. Kwa sababu ni muhimu sana sisi kwa sisi tupendane (ni amri ya pili iliyo kuu), tunapomkasirikia ndugu tunapaswa kujihesabu kwamba tayari tumepatikana na hatia katika mahakama ya Mungu. Kama tutaitamka hasira yetu kwa kusema maneno mabaya, kosa letu ni kubwa zaidi, na tunatakiwa kujihesabu kuwa na hatia katika mahakama ya juu sana ya Mungu. Na kama tutazidi hapo – na kumwaga chuki yetu dhidi ya ndugu kwa maneno mengine mabaya, tuna hatia mbele za Mungu ya kutosha kutupwa jehanamu![4] Hiyo si mchezo!
Uhusiano wetu na Mungu unapimwa na mahusiano yetu na ndugu zetu. Tukimchukia ndugu inadhihirisha kwamba hatuna uzima wa milele. Yohana aliandika hivi:
Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mwajua kwamba hakuna mwuaji aliye na uzima wa milele ndani yake (1Yohana 3:15, TLR).
Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu’ naye amchukia ndugu yake, ni mwongo huyo. Kwa maana, mtu asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hajamwona (1Yohana 4:20, TLR).
Ni muhimu sana tupendane, na kama Yesu alivyoamuru, tujitahidi kutafuta upatanisho wakati tunapokwazana (ona Mathayo 18:15-17). Yesu aliendelea hivi:
Basi, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, na hapo ukumbuke kwamba ndugu yako ana jambo nawe, iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu uende zako. Patana kwanza na ndugu yako, kisha rudi na uitoe sadaka yako (Mathayo 5:23-24, TLR).
Maana ya hayo yote ni kwamba, kama mahusiano yetu na ndugu si mazuri, hata mahusiano yetu na Mungu si mazuri. Mafarisayo walikuwa na hatia ya kutilia mkazo vitu vilivyokuwa na umuhimu mdogo na kupuuzia vitu vilivyokuwa na umuhimu mkubwa, “wakichuja mbu na kumeza ngamia” kama Yesu alivyosema juu yao (Mathayo 23:23-24). Wao walikazia umuhimu wa kutoa zaka na sadaka, lakini walipuuza yaliyokuwa ya muhimu zaidi sana, yaani ile amri ya pili iliyo kuu ya kupendana. Ni unafiki ulioje, kuleta sadaka ambayo inadhanishia kuonyesha upendo wa mtu kwa Mungu, huku akihalifu ile amri kuu ya pili! Yesu alikuwa anaonya dhidi ya hayo. Kuhusu msimamo mkali wa mahakama ya Mungu, Yesu anaendelea kusema hivi:
Patana na mshitaki wako upesi wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin nakuambia, hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho (Mathayo 5:25-26).
Ni vizuri kuepuka kuingia mahakama ya Mungu kabisa kwa kuishi kwa amani na ndugu zetu kiasi inachowezekana. Kama ndugu au dada atatukasirikia, nasi kwa kujivuna tukatae kutafuta upatanisho “njiani kuelekea mahakamani”, yaani, katika safari yetu maishani kwenda kusimama mbele za Mungu, tutajutia jambo hilo. Alichosema Yesu hapa ni sawa na maonyo Yake kuhusu sisi kumwiga yule mtumwa ambaye hakumsamehe mwenzake katika Mathayo 18:23-35. Yule mtumwa aliyekuwa amesamehewa lakini yeye akakataa kusamehe alirudishiwa deni lake, akakabidhiwa kwa watesaji “mpaka atakapolipa yote aliyodaiwa” (Mathayo 18:34). Hapa, Yesu anaonya dhidi ya matokeo mabaya ya milele ya sisi kutowapenda ndugu zetu kama Mungu anavyotazamia.
Usafi Katika Maadili ya Kimwili. Msiwe Kama Waandhsi Na Mafarisayo
Amri ya saba ikatumiwa na Yesu kama mfano wa pili kuonyesha jinsi waandishi na Mafarisayo walivyoshika andiko la Torati huku wakipuuza maana yake. Yesu aliwatazamia wanafunzi Wake kuwa safi zaidi katika maadili ya kimwili kuliko waandishi na Mafarisayo.
Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini. Lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe. Kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu (Mathayo 5:27-30).
Ona tena kwamba Yesu alikuwa bado kwenye mada Yake kuu – Watakatifu tu ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu. Alionya tena kuhusu jehanamu na kile kinachotakiwa kufanywa na mtu ili asiende huko.
Waandishi na Mafarisayo wasingeweza kuipuuza amri ya saba. Basi, waliitii kwa nje na kusalia waaminifu kwa wake zao. Lakini walikuwa wanafanya mapenzi na wanawake katika mawazo yao. Walipokuwa sokoni au barabarani, waliwavua nguo kimawazo wanawake waliokuwa wanawaona. Moyoni walikuwa wazinzi, na kwa njia hiyo walikuwa wanavunja maana ya amri ya saba. Je, ni wangapi siku hizi kanisani ambao hawana tofauti na hao?
Mungu alikusudia watu wawe safi kabisa kimaadili katika mahusiano ya kimwili. Ni wazi kwamba kama ni kosa kuwa na mahusiano kimapenzi na mke wa jirani yako, ni makosa pia kufikiri au kuwaza hayo hayo. Si kwamba Yesu aliongezea sheria kali zaidi kwenye ile iliyokuwepo katika Torati ya Musa. Amri ya kumi ilikuwa na maneno haya ya kukataza tamaa mbaya: “Usimtamani mke wa jirani yako” (Kutoka 20:17).
Je, kati ya wasikilizaji wa Yesu kuna aliyejisikia hatia? Bila shaka walikuwepo. Je, wafanye nini? Wangetubu mara moja, kama Yesu alivyoagiza. Wale wenye tamaa mbaya walitakiwa kuiacha – kwa gharama yoyote – maana, watu aina hiyo wanakwenda jehanamu.
Hakuna mtu mwenye akili timamu anayedhani kwamba Yesu alimaanisha kwamba watu wenye tamaa mbaya wang’oe jicho kweli au kukata mkono. Mtu mwenye tamaa anayeng’oa jicho anakuwa mwenye tamaa chongo tu! Yesu alikuwa anakazia tu umuhimu wa kutii maana ya amri ya saba – kwamba, umilele wa mtu ulitegemeana na jinsi anavyoitii.
Basi – akifuata mfano wa Kristo, mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi atawashauri wanafunzi wake “kukatilia mbali” chochote kinachowafanya kujikwaa. Kama ni televisheni ya kulipia, iache kulipiwa. Kama ni ya kawaida, iondolewe. Kama ni gazeti linalolipiwa, liache kulipiwa. Kama ni mtandao, achana nao. Kama ni dirisha lisilofungwa, lifungwe. Hakuna hata kimoja katika vitu hivyo kinachostahili kumfanya mtu aende jehanamu milele, na kwa sababu mtumishi anayewafanya watu kuwa wanafunzi anawapenda kondoo wake, atawaambia ukweli na kuwaonya, sawa na jinsi Yesu alivyofanya.
Njia Nyingine Ya Kuzini
Mfano unaofuata wa Yesu unafanana na huo tuliomaliza. Pengine ndiyo sababu unatajwa sasa. Unatakiwa kuonekana kama ufafanuzi wa zaidi badala ya kuonekana kwamba ni mada mpya. Mada ni hii: “Kitu kingine Mafarisayo wafanyacho kinacholingana na uzinzi”.
Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe na ampe hati ya talaka. Lakini mimi nawaambia, kila mtu amwachaye mkewe isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini (Mathayo 31-32).
Ufuatao ni mfano tu, jinsi waandishi na Mafarisayo walivyopindisha sheria ya Mungu ili kutosheleza maisha yao ya dhambi.
Hebu tujiundie Farisayo wa kufikirika, aliyeishi siku za Yesu. Kuna mwanamke mzuri tu anayemtamani sana, anayeishi ng’ambo ya barabara. Wanataniana kila wanapo-onana. Inaonekana huyo mwanamke amevutiwa naye, na tamaa ya Farisayo inazidi kuongezeka. Angependa kumwona akiwa hana nguo, naye humfikiria sana kila wakati, kimapenzi. Laiti ingewezekana akampata!
Lakini ana tatizo. Yeye ana ndoa, na dini yake inakataza uzinzi. Hataki kuivunja amri ya saba (ingawa amekwisha ivunja kila wakati anapotamani). Sasa, afanye nini?
Lipo jibu! Akiachana na mwenzake, anaweza kumwoa huyo mwanamke anayemtamani! Lakini, talaka inaruhusiwa? Farisayo mwenzake anamwambia, Ndiyo! Tena hata andiko lipo! Kumbukumbu 24:1 inasema kitu juu ya kumpa mke wako cheti cha talaka unapomwacha. Basi, talaka bila shaka ni halali kwa mazingira fulani! Sasa – ni mazingira gani hayo? Anasoma kwa makini maneno ya Mungu, kwamba:
Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake na kumtoa katika nyumba yake (Kumbu. 24:1).
Loo! Kumbe inawezekana kumwacha mke wake akipata hitilafu kwake! Na amekwisha ipata! Havutii kama yule mwanamke anayekaa ng’ambo ya barabara! (Na huu si mfano usiowezekana. Kulingana na Rabbi Hillel, ambaye alikuwa na mafundisho kuhusu talaka yaliyopendwa sana katika siku za Yesu, mtu angeweza kumwacha mke wake kihalali kabisa kama angempata mwingine aliyekuwa wa kupendeza zaidi, maana tendo hilo lilimfanye mke wake “kutokuwa na kibali” machoni pake. Vile vile Rabbi Hillel alifundisha kwamba mwanamume angeweza kumwacha mke wake kama akizidisha chumvi katika chakula, au kama angezungumza na mwanamume mwingine, au kama asingezaa mtoto wa kiume).
Basi, Farisayo wetu mwenye tamaa anaachana na mke wake kihalali kabisa kwa kumpa hati ya talaka, na haraka sana anamwoa yule mwanamke anayemtamani. Tena, hayo yote yanafanyika bila yeye kujisikia hatia hata kidogo kwa sababu Torati ya Mungu imefuatwa!
Mtazamo Tofauti
Mungu anaona mambo kwa njia tofauti. Yeye hakutaja kwamba “kutokuwa na kibali” ni kitu gani katika Kumbukumbu 24:1. Wala haisemi kwamba sababu halali ya kuachana na mke ni nini. Maandiko hayo hayasemi chochote kuhusu wakati ambapo kuachana kunaruhusiwa au hakuruhusiwi. Hapo tunaambiwa tu juu ya katazo kuhusu mwanamke aliyeachwa mara mbili au mara moja, au hata aliyefiwa, kuolewa tena na mume wake wa kwanza. Kusema kwamba kuna hali ya “kutokuwa na kibali” mbele za Mungu, yenye kuhalalisha kuachana katika mistari hii ni kulazimisha maana nyingine kabisa.
Tena – mbele za Mungu, huyo mwanamume wa kufikirika ambaye nimesimulia habari zake hana tofauti na mzinzi. Amekwisha vunja ile amri ya saba. Tena ana hatia kuliko hata mzinzi wa kawaida, maana yeye ana kosa la uzinzi “mara mbili”. Utasema, kivipi? Kwanza: Amefanya uzinzi mwenyewe. Baadaye Yesu alisema hivi: “Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akaoa mwanamke mwingine, anazini” (Mathayo 19:9, TLR).
Pili: Kwa sababu, huyo mkewe ambaye ameachika lazima atafute mwanamume mwingine ili aendelee kuishi. Machoni pa Mungu, huyo Farisayo amekwisha fanya kitendo kinacholingana na kumlazimisha mke wake kushirikiana kimwili na mwanamume mwingine. Basi, anakuwa na hatia kwa “uzinzi” wa huyo mwanamke.[5] Yesu alisema hivi: “Yeyote amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya azini” (Mathayo 5:32, TLR. Maneno mepesi kukazia).
Yawezekana Yesu alikuwa anamhukumu hata huyo Farisayo wetu mwenye tamaa kwa kosa la “kuzini mara tatu” ikiwa maneno Yake yaliyofuata, kwamba “yeyote amwoaye mwanamke aliyeachwa azini” (Mathayo 5:32, TLR) yanamaanisha kwamba Mungu anamhesabia Farisayo huyo hatia kwa sababu ya “zinaa” ya mume mpya wa mke wake wa zamani. [6]
Hili lilikuwa jambo moto katika siku za Yesu, maana tunasoma mahali pengine Mafarisayo walipomwuliza hivi: “Je, ni halali kwa mtu kumwacha mkewe kwa sababu yoyote?” (Mathayo 19:3). Swali lao linadhihirisha mioyo yao. Bila shaka kuna waliotaka kuamini kwamba kuachana au talaka ni halali kwa sababu yoyote.
Ila, naomba niseme kwamba ni aibu sana kwa Wakristo kuchukua mistari hii kuhusu talaka, na kuitafsiri vibaya, kisha kuweka mizigo mizito juu ya watoto wa Mungu. Yesu hakuwa anazungumza juu ya Mkristo ambaye alikuwa na talaka wakati hajaokoka, na ambaye akiisha kumpata mwenzake mzuri tu anayempenda Kristo pia, wanaamua kuoana. Hiyo si uasherati. Kama Yesu alimaanisha hivyo, itabidi tubadilishe Injili maana haitoi nafasi ya msamaha kwa dhambi zote za wenye dhambi. Itabidi tangu sasa tuhubiri hivi: “Yesu alikufa kwa ajili yako, nawe ukitubu na kumwamini, utasamehewa dhambi zako zote. Lakini, kama umeachana na mwenzake, hakikisha kwamba huingii katika ndoa nyingine maana hapo utaishi katika uasherati, na Biblia inasema waasherati watakwenda jehanamu. Pia, kama umeachika na kuingia tena katika ndoa, unahitaji kufanya dhambi nyingine moja kabla ya kumjia Kristo – achana na mwenzako. La sivyo, utaendelea katika uasherati, na watu aina hiyo hawajaokoka.”[7] Je, hiyo ni injili?[8]
Uwe Mkweli. Si Kama Waandishi Na Mafarisayo
Mfano wa tatu wa Yesu kuhusu mwenendo usio wa haki na matumizi mabaya ya Maandiko ya waandishi na Mafarisayo unahusiana na amri ya Mungu kuhusu kusema ukweli. Waandishi na Mafarisayo walikuwa wabunifu sana kwa habari ya kudanganya. Tunajifunza kutoka Mathayo 23:16-22 kwamba wao hawakujihesabu kuwa na wajibu wa kutunza nadhiri zao kama wangeapa kwa hekalu, madhabahu au mbingu. Lakini, kama wangeapa kwa dhahabu ya hekalu, au sadaka iliyoko juu ya madhabahu, au kwa Mungu aliyeko mbinguni, basi walikuwa na wajibu wa kutunza nadhiri au viapo vyao! Hayo ni mawazo ya mtu mzima akifikiri kitoto kwamba ana haki ya kutosema ukweli mradi vidole vyake vimeshikana kwa nyuma. Yesu anatazamia wanafunzi Wake waseme ukweli.
Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, ‘Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako.’ Lakini mimi nawaambia, ‘Usiape kabisa; hat a kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mmuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu’ (Mathayo 5:33-37).
Amri ya Mungu kuhusu viapo na nadhiri haikusema chochote juuya kufanya kiapo kwa kuapa na kitu kingine. Mungu alikusudia watu Wake waseme kweli wakati wote. Basi, isingekuwepo haja ya kuapa kamwe.
Hakuna kosa kuapa, kwa sababu kiapo si kitu zaidi ya nadhiri au ahadi. Kwa kweli, viapo vya kumtii Mungu ni vizuri sana. Wokovu huanza kwa kiapo cha kumfuata Yesu. Lakini watu wanapotakiwa kuapa kwa kitu kingine ili kuwafanya wengine waamini wanachosema, ni ukiri wa moja kwa moja kwamba kwa kawaida wao husema uongo. Watu wanaosema kweli sikuzote hawana haja ya kuapa hata siku moja. Lakini makanisa mengi siku hizi yamejaa waongo, na watumishi mara nyingi ndio viongozi katika udanganyifu na hila.
Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi huonyesha mfano wa kusema kweli na kuwafundisha wanafunzi wake kusema kweli sikuzote. Anajua Yohana alionya kwamba waongo wote watatupwa katika ziwa liwakalo moto na kibiriti (ona Ufunuo 21:8).
Msilipe Kisasi, Kama Wanavyofanya Waandishi Na Mafarisayo
Kinachofuata katika orodha ya malalamiko ya Yesu ni kupotoshwa kwa Kifarisayo kwa andiko maarufu sana katika Agano la Kale. Tumekwisha kutazama maandiko hayo katika sura kuhusu kutafsiri maandiko.
Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, ‘Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo’ (Mathayo 5:33-37).
Torati ya Musa ilitamka kwamba mahakama ikimpata mtu na hatia ya kumjeruhi mwingine, adhabu yake italingana na madhara aliyoleta. Kama alimtoa mtu jino, kwa haki na uhalali kabisa jino lake na yeye litang’olewa. Amri hii ilitolea ili kuhaikisha kwamba haki ingetendeka katika mashauri ya mahakamani kwa makosa makubwa. Mungu alianzisha utaratibu wa mahakama na mahakimu katika Torati ili kupinga uhalifu, kuhakikisha haki na kuzuia visasi. Na Mungu aliwaamuru mahakimu kutokuwa na upendeleo, na kuwa wenye haki katika hukumu zao. Walitakiwa kuhukumu “jicho kwa jicho na jino kwa jino”. Lakini, maneno hayo pamoja na amri hiyo hupatikana katika maandiko yanayohusiana na haki katika mahakama.
Lakini tena, waandishi na Mafarisayo walikuwa wamebadilisha amri yenyewe na kuifanya kuwa amri ya kulipiza kisasi kuwa wajibu mtakatifu. Walikuwa wamekubali kutokuwa na uvumilivu, wakitafuta kulipiza kisasi hata kwa makosa madogo madogo kabisa.
Mungu daima ametazamia viwango vya juu zaidi kutoka kwa watu Wake. Kisasi ni kitu alichokataza Yeye (ona Kumbu. 32:35). Agano la Kale lilifundisha kwamba watu wa Mungu wanatakiwa kuwaonyesha adui zao wema (ona Kutoka 23:4, 5; Mithali 25:21-22). Yesu aliunga mkono kweli hii kwa kuwaambia wanafunzi Wake wageuze shavu la pili na kwenda maili nyingine zaidi katika kushughulika na watu waovu. Tunapokosewa, Mungu anataka tuwe na rehema, tukilipa jema kwa ovu tulilotendewa.
Lakini je! Yesu anatazamia kwamba tutawaachia watu watutumie vibaya tu, wakiharibu maisha yetu kama wapendavyo? Je, ni makosa kumpeleka asiyeamini mahakamani na kutafuta haki kwa uovu tunaotendewa? Hapana. Yesu hakuwa anazungumza juu ya kupata haki tunayuostahili kwa makosa makubwa mahakamani. Alikuwa anazungumzia juu ya kutafuta kulipa kisasi kwa mambo madogo madogo.Ona kwamba Yesu hakusema tutoe shingo yetu ili tunyongwe na mtu ambaye ametuchoma kisu mgongoni. Hakusema tutoe nyumba kwa mtu anayetaka gari. Alichokuwa anatuambia ni jinsi ya kuonyesha uvumilivu na rehema kwa kiwango cha juu sana, tunapokutana na vikwazo vidogo vidogo kila siku, na zile changamoto za kawaida zinazotokana na kushughulika kwetu na watu wenye kujipenda, au ubinafsi. Anataka tuwe wakarimu kuliko watu wenye ubinafsi wanavyotazamia. Waandishi na Mafarisayo hawakukaribia kufikia kiwango hicho.
Mbona Wakristo wengi wanakwazika kirahisi? Mbona ni wepesi sana kukasirishwa na vikwazo vidogo ambavyo ni vidogo mara kumi kuliko kupigwa kofi? Je, hao watu wameokoka kweli? Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi huonyesha mfano wa kumgeuzia mtu shavu la pili, naye anawafundisha wanafunzi wake kufanya hivyo hivyo.
Msiwachukie Adui Zenu, Kama Wanavyofanya Waandishi Na Mafarisayo
Kwa kumalizia, Yesu anaorodhesha amri nyingine iliyotolewa na Mungu ambayo waandishi na Mafarisayo waliibadili ili kutosheleza mioyo yao yenye chuki.
Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Umpende jirani yako na umchukie adui yako’. Lakini mimi nawaambia, ‘Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni. Maana Yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshe amvua wenye haki na wasio haki. Maana, mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu’ (Mathayo 5:43-48).
Katika Agano la Kale Mungua likuwa amesema hivi: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” (Walawi 19:18, TLR). Waandishi na Mafarisayo wakatafsiri jirani kuw ani wale watu waliowapenda tu. Kila mwingine yeyote alikuwa adui, na kwa kuwa Mungu alisema kuwapenda jirani zetu tu, bila shaka ni sawa kuwachukia adui zetu. Lakini, kulingana na mafundisho ya Yesu, Mungu hakuwa amekusudia hayo.
Yesu baadaye angefundisha katika habari za Msamaria Mwema kwamba, tunatakiwa kumhesabu kila mtu kuwa jirani yetu.[9] Mungu anataka tumpende kila mtu, mpaka adui zetu. Hicho ndicho kiwango cha Mungu kwa ajili ya watoto Wake – na ni kiwango ambacho Yeye Mwenyewe anakitumia. Anatuma jua na mvua kwa ajili ya kuotesha mimea, kwa watu wote – wema na wabaya. Tunatakiwa kufuata mfano Wake, tukonyesha wema kwa watu wasiostahili. Tunapofanya hivyo, inaonyesha kwamba sisi ni “wana wa Baba [yetu] aliye mbinguni” (Mathayo 5:45). Watu waliozaliwa upya kweli kweli hutenda kama Baba yao.
Upendo ambao Mungu anatazamia tuuonyeshe kwa adui zetu si hisia au kukubaliana na uovu wao. Mungu hatutaki tuendelee kujisikia vizuri juu ya wale wanaotupinga. Hatuambii tuseme kisichokuwa kweli – kwamba adui zetu ni watu wazuri sana. Lakini, anatazamia kwamba tutawahurumia na kuchukua hatua ya makusudi kuonyesha jambo hilo – haidhuru hata kwa kuwasalimu tu na kuwaombea.
Ona tena kwamba Yesu anatilia mkazo mada Yake kuu – Ni watakatifu tu watakaorithi ufalme wa Mungu. Aliwaambia wanafunzi wake kwamba, kama watawapenda wale wawapendao tu, hawana tofauti na wapagani na watoza ushuru – aina mbili za watu ambao kila Myahudi alikubali kwamba wanakwenda jehanamu. Ilikuwa ni njia nyingine ya kusema kwamba watu wanaowapenda wale wanaowapenda tu wanakwenda jehanamu.
Tenda Mema Kwa Nia Njema, Si Kama Waandishi Na Mafarisayo
Yesu hatazamii wafuasi Wake kuwa watakatifu tu. Anawatazamia wawe watakatifu kwa sababu sahihi. Inawezekana kabisa kutii amri za Mungu na bado usimpendeze ikiwa utii wa mtu unatokana na nia mbaya. Yesu aliwahukumu waandishi na Mafarisayo kwa sababu walitenda matendo yao mema yote ili wasifiwe na watu (ona Mathayo 23:5). Yesu anatazamia wanafunzi Wake wawe tofauti.
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume. Sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi (Mathayo 6:1-4).
Yesu alitazamia kwamba wafuasi Wake watawapa maskini sadaka. Torati iliagiza hivyo (Kutoka 23:11; Walawi 19:10; 23:22; 25:35; Kumbu. 15:7-11), lakini waandishi na Mafarisayo walifanya hivyo huku tarumbeta zikipigwa, bila shaka ili kuwaita masini waje kupokea sadaka zao za ukarimu. Pamoja na hayo, ni Wakristo wangapi wanaotoa chochote kwa maskini? Hawajawahi kufikia hata mahali pa kuchunguza tu nia yao ya kutoa sadaka. Kama ubinafsi uliwasukuma waandishi na Mafarisayo kutangaza kutoa kwao, ni kitu gani kinachowasukuma Wakristo kupuuza matatizo ya maskini? Kwa hali hiyo, haki yao inazidi ile ya waandishi na Mafarisayo?
Kama Paulo atakavyorudia katika 1Wakorintho 3:10-15, tunaweza kufanya mema kwa nia mbaya. Kama nia yetu si safi, matendo yetu mema hayatapata thawabu. Paulo aliandika kwamba inawezekana hata kuhubiri Injili kwa nia isiyo safi (ona Wafilipi 1:15-17). Kulingana na maneno ya Yesu, njia nzuri yakuhakikisha kwamba utoaji wetu ni kwa nia safi ni kutoa kwa siri kiasi iwezekanavyo – bila ya kuruhusu mkono wa kushoto kujua kinachofanywa na mkono wa kuume. Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi huwafundisha wanafunzi wake kuwapa vitu maskini (kama wanaweza), naye anatenda kama mahubiri yake, kimya kimya tu.
Kufunga Na Kuomba Kwa Sababu Zilizo Sahihi
Yesu pia alitazamia kwamba wafuasi Wake wataomba na kufunga, na kwamba wangefanya mambo hayo ili kumpendeza Baba yao, si ili kuonekana na watu. Vinginevyo wasingekuwa tofauti na wale waandishi na Mafarisayo wanaokwenda jehanamu, waliokuwa wanafunga na kuomba ili wasifiwe na watu. Hiyo ni thawabu ya muda sana. Yesu aliwashauri hivi wafuasi Wake:
Tena msalipo, msiwe kama wanafiki. Kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia ili waonekane na watu. Amin nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi (Mathayo 6:5-6, 16-18).
Je, ni Wakristo wangapi wenye kuishi maisha yasiyo na maombi, na ambao hata hawajawahi kufunga?[10] Sasa, haki yao inalinganishwaje na ile ya waandishi na Mafarisayo, waliofanya yote mawili – japo ni kwa sababu mbaya?
Machache Kuhusu Maombi Na Msamaha
Akiendelea na somo la maombi, Yesu alifoa mafundisho ya ziada kwa wanafunzi Wake kuhusu jinsi wanavyotakiwa kuomba. Yesu anataka sisi tuombe kwa njia ambayo haimtukani Baba Yake kwa kukana yale aliyofunua juu Yake Mwenyewe. Kwa mfano: Kwa kuwa Mungu anajua tunachohitaji kabla ya kumwomba (maana anafahamu mambo yote), hakuna sababu ya kurudia-rudia maneno tunapoomba.
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba (Mathayo 6:7-8).
Kweli – maombi yetu hudhihirisha jinsi tunavyomjua Mungu vizuri. Wale wanaomjua kama alivyojidhihirisha katika Neno Lake huomba ili mapenzi Yake Yeye yafanyike, na Yeye atukuzwe. Shauku yao kuu ni kuwa watakatifu – wenye kumpendeza Yeye kabisa. Hili linaonekana katika sala ya Yesu ya mfano, ambayo sisi tunaiita Sala ya Bwana. Imo katika sehemu inayofuata ya mafundisho ya Yesu kwa wanafunzi Wake. Inadhihirisha matazamio Yake kwa habari ya mambo tunayotanguliza, na upendo wetu.[11]
Basi ninyi salini hivi: ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu’ (Mathayo 6:9-11).
Basi, inatakiwa wajibu wa kwanza kabisa wa wanafunzi wa Kristo uwe jina la Mungu kutukuzwa – kwamba liheshimiwe, listahiwe na kutakatifuzwa.
Wale wanaoomba kwamba jina la Mungu litakaswe wanatakiwa kuwa watakatifu wao wenyewe – watu wenye kulitakasa jina la Mungu. Vinginevyo ni unafiki tu. Kwa hiyo, sala hii huonyesha shauku tuliyo nayo kwamba wengine wajinyenyekeze mbele za Mungu kama ambavyo sisi tumekwisha fanya.
Ombi la pili katika sala hiyo mfano linafanana: “Ufalme wako uje”. Wazo la ufalme linamaanisha kuwepo kwa Mfalme mwenye kutawala ufalme Wake. Mfuasi Mkristo anatamani kumwona Mfalme wake – yule anayetawala maisha yake – atawale dunia nzima. Laiti kila mmoja angepiga goti lake kwa Mfalme Yesu – katika imani tiifu!
Ombi la tatu katika sala hiyo linarudia la kwanza na la pili, hivi:
Mapenzi yako yatendeke hapa duniani kama huko mbinguni”. Hapa tena – tunawezaje kuomba kwa dhati sala kama hiyo bila sisi wenyewe kuwa tumekubali kukaa chini ya mapenzi ya Mungu maishani mwetu? Mwanafunzi wa kweli huwa na shauku kwamba mapenzi ya Mungu yafanyike duniani kama yafanyikavyo huko mbinguni – kikamilifu na kabisa.
Yanayotakiwa kuwa muhimu zaidi kwetu kuliko hata chakula – “riziki yetu” – ni jina la Mungu litakaswe, mapenzi Yake yafanyike, na ufalme Wake uje. Hili ombi la nne linawekwa la nne kwa kusudi. Hata kwa mtazamo huo tu inaonyesha mpangilio unaofaa wa mambo muhimu maishani mwetu, na hakuna dalili ya uchoyo au ubinafsi hapa. Wanafunzi wa Kristo wanamtumikia Mungu, sio mali. Lengo lao si kujiwekea hazina duniani.
Hebu niongeze pia kwamba ombi hili la nne linaonyesha kwamba sala hii mfano inapaswa kuombwa kila siku – mwanzo wa kila siku.
Sala Mfano Inaendelea
Je, wanafunzi wa Kristo hutenda dhambi? Wakati mwingine wanatenda, maana Yesu aliwafundisha kuomba msamaha wa dhambi zao.
“Utusamehe deni zetu kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” (Mathayo 6:12-15).
Wanafunzi wa Yesu hutambua kwamba kutokutii kwao humkwaza Mungu, na wanapotenda dhambi, wanajisikia aibu. Wanataka doa hilo liondolewe, na Baba yao wa mbinguni, kwa neema sana, yuko tayari kuwasamehe. Lakini lazima waombe msamaha, ambalo ndilo ombi la tano lipatikanalo katika Sala ya Bwana.
Ila – kusamehewa kwao kunategemea sana wao kuwasamehe wengine. Kwa sababu wamesamehewa vingi, wanawajibika kumsamehe kila mtu anayewaomba msamaha (na kumpenda na kutafuta upatanisho na wale wasioomba msamaha). Wakikataa kusamehe, Mungu hatawasamehe.
Ombi la sita na la mwisho pia linaonyesha shauku ya mwanafunzi wa kweli kuwa mtaka tifu: “Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu [au, ‘maovuni’].” Mwanafunzi wa kweli ana shauku na utakatifu kiasi cha kwamba anamwomba Mungu asimwongoze katika hali anayoweza kujaribiwa, asije akashindwa. Tena, anamwomba Mungu amwokoe na maovu yoyote yanayoweza kumnasa. Hakika hii ni sala kubwa sana ya kuomba mwanzoni mwa kila siku, kabla hatujaingia katika dunia yenye maovu na majaribu. Na hakika tunaweza kumtazamia Mungu kujibu sala hii aliyotuambia tuiombe!
Wale wamjuao Mungu wanaelewa ni kwa nini maombi yote sita katika sala hii yanafaa. Sababu inafunuliwa katika mstari wa mwisho wa sala: “Kwa kuwa [au kwa sababu] ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele” (Mathayo 6:13). Mungu ni Mfalme mkuu anayetawala ufalme Wake ambao ndani yake sisi ni watumishi. Yeye ndiye mwenye nguvu zote, na hakuna anayethubutu kupingana na mapenzi Yake. Utukufu wote ni Wake milele. Anastahili watu wamtii.
Je, somo kubwa katika Sala ya Bwana ni nini? Utakatifu. Wanafunzi wa Kristo wanatamani jina la Mungu litukuzwe, utawala Wake uimarishwe duniani kote, na mapenzi Yake yafanyike kikamilifu kila mahali. Hii ni muhimu sana kwao kuliko hata riziki yao ya kila siku. Wanataka kumpendeza, na wanaposhindwa, wanataka msamaha Wake. Kama watu waliosamehewa, wanawasamehe wengine. Wanatamani kuwa watakatifu kabisa mpaka wanataka kuepuka majaribu kwa sababu majaribu huongeza nafasi zao za kutenda dhambi. Mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi hufundisha mambo hayo kwa wanafunzi wake.
Mwanafunzi Na Vitu Alivyo Navyo
Somo linalofuata katika Mahubiri ya Mlimani linaweza kuwakorofisha Wakristo ambao lengo lao kubwa maishani ni kuzidi kujipatia vitu.
Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi. Kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho. Basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi, ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili. Kwa maana atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali (Mathayo 6:19-24).
Yesu aliagiza kwamba tusijiwekee hazina hapa duniani. Sasa – “hazina” ni kitu gani? Hazina halisi huwekwa katika masanduku ya hazina, na kuhifadhiwa mahali. Hazitumiki kwa kitu chochote kinachofaa. Yesu alifafanua hizo kuwa ni vitu vinavyovutia kutu, nondo na wezi. Yaani ni kusema kwamba “si vya muhimu”. Nondo hula vilivyo ndani kabisa ya makabati yetu – hawali vile tunavyotumia kila siku. Kutu hula vtu tusivyotumia sana. Katika nchi zilizoendelea sana, kwa kawaida wevi huiba vitu ambavyo watu hawavihitaji sana: picha, lulu, vitu vya thamani, na kitu kinachoweza kuuzwa haraka.
Wanafunzi wa kweli wamekwisha “toa mali zao zote” (ona Luka 14:33). Wao ni wasimamizi tu wa fedha za Mungu. Basi, kila uamuzi wa kutumia fedha ni wa kiroho. Tunachofanya na fedha yetu huonyesha nani anayetawala maisha yetu. Tunapokusanya “hazina” na kwa njia hiyo kulundika fedha na kununua visivyo muhimu, tunadhihirisha kwamba Yesu si anayetawala maishani mwetu. Maana, kama angekuw andiye mtawala, tungefanya vitu bora zaidi na zile fedha alizotukabidhi.
Hivyo vitu bora zaidi ni kama nini? Yesu anatuagiza tujiwekee hazina mbinguni. Inawezekanaje kufanya hivyo? Anatuambia katika Injili ya Luka: “Viuzeni mlivyo navyo mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu” (Luka 12:33).
Kwa kutoa fedha kuwasaidia maskini na kueneza Injili, tunajiwekea hazina mbinguni. Yesu anatuambia tuchukue kile kitakachopungua thamani mpaka kufikia kutokuwa nayo, tukitie katika kitu kingine ambacho hakipotezi thamani kamwe. Hayo ndiyo afanyayo mtumishi anayefanya watu kuwa wanafunzi, naye anawafundisha wanafunzi wake kufanya hivyo hivyo.
Jicho Bovu
Je, Yesu alimaanisha nini alipozungumza juu ya watu wenye macho mazuri ambao miili yao imejaa nuru, na watu wenye macho mabovu, ambao miili yao imejaa giza? Bila shaka maneno Yake yalihusu mambo ya fedha na vitu, kwa sababu kabla ya kusema hayo alikuwa anazungumzia vitu hivyo, na baada ya kusema hivyo alizungumzia vitu hivyo.
Neno la Kiyunani lililotafsiriwa “bovu” katika 6:23 ndiyo limetafsiriwa “ovu” katika Mathayo 20:15. Hapo tunasoma kuhusu mwajiri aliyemwambia mfanya kazi wake hivi: “Je, jicho lako limekuwa ovu kwa kuwa mimi ni mkarimu?” (TLR) Ni wazi kwamba jicho haliwezi kuwa ovu. Sasa – “jicho ovu (au bovu)” maana yake mtu mwenye choyo. Hii inatusaidia sisi kuelewa vizuri zaidi maana ya Kristo katika Mathayo 6:22-23.
Mtu mwenye jicho safi ni mfano wa yule mwenye moyo safi, anayeruhusu mwangaza wa kweli kuingia ndani yake. Basi, anamtumikia Mungu na kujiwekea hazina – si duniani – bali mbinguni, mahali ambapo moyo wake upo. Mtu mwenye jicho bovu hufungia nje mwanza wa kweli usiingie, kwa sababu yeye hudhani tayari ana ukweli. Basi amejaa giza, akiaini uongo. Anajiwekea hazina duniani mahali moyo wake ulipo. Yeye anaamini kwamba kusudi la maisha yake ni kujitosheleza. Fedha ni mungu wake. Haendi mbinguni.
Nini maana ya fedha kuwa mungu wako? Maana yake ni kwamba fedha ina nafasi ambayo Mungu anapaswa kuwa nayo maishani mwako. Fedha inatawala maisha yako. Ndiyo inayochukua nguvu zako, mawazo yako na muda wako. Ndiyo chanzo kikuu cha furaha yako. Unazipenda.[12] Ndiyo maana Paulo alifananisha tamaa (au choyo) na kuabudu sanamu, akisema kwamba hakuna yeyote mwenye tamaa atakayeurithi ufalme wa Mungu (ona Waefeso 5:5; Wakolosai 3:5-6).
Mungu na fedha hutaka kutawala maisha yetu, na Yesu alisema hatuwezi kuwatumikia wote wawili. Hapo tena tunaona Yesu alibakia kwenye somo Lake kuu – Ni watakatifu tu watakaorithi ufalme wa Mungu. Aliweka wazi kabisa kwamba watu waliojaa giza, ambao mungu wao ni fedha, ambao mioyo yao ipo duniani na wenye kujiwekea hazina za kidunia hawako kwenye ile njia nyembamba iongozayo watu kwenda uzimani.
Maskini Mwenye Kutamani
Kutaka sana kupata vitu si kosa wakati vitu hivyo ni vya anasa. Mtu anaweza kukosea na kuwaza sana kuhusu vitu hata kama hivyo vitu ni mahitaji ya msingi. Yesu aliendelea kufundisha hivi:
Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani ya kwamba hawapandi wala hawavuni wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba jinsi yameavyo; hayafanyi kazi wala hayasokoti, nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani hapa? Msisumbuke basi mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta. Kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake (Mathayo 6:25-34).
Wasomaji wengi wa kitabu hiki hawataweza kujilinganisha hata kidogo na watu ambao Yesu alikuwa anazungumza nao. Je, wewe ulipata wasiwasi lini mara ya mwisho kuhusu chakula, kinywaji au mavazi?
Maneno ya Yesu kwa hakika yanatuhusu sisi wote. Ikiwa ni makosa kuwaza sana na kuchukuliwa na upatikanaji wa mambo muhimu maishani, vipi kuhusu yasiyokuwa muhimu? Yesu anawatazamia wanafunzi Wake kuhusika zaidi na kutafuta mambo mawili: Ufalme Wake na haki Yake. Mkristo anaposhindwa kutoa zaka – fungu la kumi – (na hiyo ni amri ya agano la kale) lakini aweze kujipatia vitu vingi tu visivyo muhimu, je, anaishi kulingana na kanuni ya Kristo ya kutafuta kwanza ufalme na haki Yake? Jibu ni wazi kabisa!
Usiwe Mtafuta Makosa
Maagizo ya Yesu yanayofuata kwa wafuasi Wake yanahusu dhambi za kuhukumu na kutafuta makosa kwa wengine.
Msihukumu msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kila mpimiacho ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe. Itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako (Mathayo 7:1-5).
Ingawa Yesu hakuwashtaki waandishi na Mafarisayo moja kwa moja au vinginevyo katika fungu hili, wao walikuwa na hatia ya dhambi hii. Walimkosoa Yeye!
Je, Yesu alimaanisha nini hasa katika onyo hili la kuwahukumu wengine?
Kwanza: Hebu tufikiri hakumaanisha nini. Yeye hakumaanisha kwamba tusiwe wenye uwezo wa kupambanua na kufanya maamuzi ya msingi kuhusu tabia za watu kwa kuwatazama matendo. Hilo ni wazi kabisa. Mara tu baada ya sehemu hii, Yesu aliwaagiza wanafunzi Wake wasitupe lulu zao mbele ya nguruwe na wasiwape mbwa kilicho kitakatifu (ona 7:6). Bila shaka alikuwa anazungumza kwa mifano juu ya watu fulani, akiwaita nguruwe na mbwa – watu ambao hawakuthamini thamani ya vitu vitakatifu – “lulu” – walivyokuwa wanapewa. Bila shaka hawajaokoka hao. Kwa kweli ni lazima kupima kama watu ni nguruwe na mbwa ikiwa tutatii agizo hili.
Tena, Yesu akawaambia wafuasi Wake baadaye kidogo jinsi ya kupima waalimu wa uongo – “mbwa mwitu waliovaa mavazi ya kondoo” (7:15) – kwa kukagua matunda yao. Basi, ni dhahiri kwamba ili tuweze kutii maagizo ya Yesu lazima tutazame jinsi watu wanavyoishi na kutoa hukumu.
Paulo vile vile aliwaambia waamini Wakorintho hivi:
Lakini mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye (1Wakor. 5:11).
Ili kutii agizo hili inatakiwa tuchunguze maisha ya watu na kufanya maamuzi juu yao – kuhukumu – kutokana na kile tunachokiona.
Hata mtume Yohana pia alituambia tunaweza kutambua kirahisi tu nani ni wa Mungu na nani ni wa Shetani. Kwa kutazama maisha ya watu, ni dhahiri kwetu nani ameokoka na nani hajaokoka (ona 1Yohana 3:10).
Kama mambo ni hayo, Kristo hasemi kwamba ni dhambi kutambua tabia za watu kwa kuyatazama maisha yao na kuhukumu kama wao ni wa Mungu au wa Shetani. Sasa, alimaanisha nini basi?
Hebu gundua kwamba Yesu alikuwa anazungumza juu ya kutafuta makosa madogo – vibanzi katika ndugu – tafadhali ona kwamba Yesu anatumia neno ndugu mara tatu katika fungu hili. Yesu hakuwa anatuonya dhidi ya kuwahukumu watu kwamba ni wasioamini kwa kutazama makmosa yao makubwa sana (kama tutakavyoona punde tu katika mahubiri haya). Kinyume chake – haya ni mafundisho kuhusu jinsi Wakristo wanavyopaswa kuwatendea Wakristo wengine. Hawapaswi kuwa watafutaji makosa madogo madogo miongoni mwao – hasa kama wao wenyewe hawaoni makosa yao makubwa sana. Ikifikia hapo wanakuwa wanafiki. Yesu aliwahi kuwaambia watu wengine waliokuwa wanafiki, hivi: “Yeyote asiyekuwa na dhambi miongoni mwenu, na awe wa kwanza kutupa jiwe” (Yohana 8:7, TLR).
Mtume Yakobo, ambaye barua yake inafanana na Mahubiri ya Mlimani sehemu sehemu, aliandika hivi, “Ndugu! Msinung’unikiane msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango” (Yakobo 5:9). Pengine hili nalo litatusaidia kuelewa kidogo kuhusu kitu Yesu alichokuwa anaonya – kutafuta makosa katika waaminio kisha kutangaza tulichopata – kunung’unikiana. Hii ni dhambi moja kubwa sana katika kanisa, na wale wenye hatia ya dhambi hiyo wanajiweka katika nafasi hatari sana ya kuhukumiwa. Tunapomsema mwamini mwenzsetu, tukionyesha makosa yake kwa wengine, tunahalifu Amri Kuu, kwa sababu sisi hatupendi watu waseme ubaya wetu wakati hatupo.
Tunaweza kwa upendo kabisa kumwendea mwamini ambaye ana tatizo, lakini wakati tunapoweza kufanya hivyo bila ya unafiki, tukiwa na uhakika kwamba hatuna hatia (au hatia zaidi) ya dhambi hiyo hiyo kama mtu tunayembana. Ila, ni kupoteza wakati kabisa kufanya hivyo na asiyeamini, na hicho ndicho kisemwacho katika mstari unaofuata. Yesu alisema hivi:
Msiwape mbwa kilicho kitakatifu wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua (Mathayo 7:6).
Vivyo hivyo kuna mithali inayosema hivi: “Usimkaripie mwenye dharau asije akakuchukia. Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda” (Mithali 9:8). Mahali pengine Yesu aliwaambia wanafunzi Wake kukung’uta mavumbi ya miguu yao kama kulalamika kinyume cha wanaokataa injili yao. “Mbwa” wakiisha tambuliwa kwa kutokufurahia na kupenda kweli, Mungu hataki watumishi Wake wapoteze muda wao kujaribu kuwafikia, huku kuna wengine ambao hawajapata nafasi hata moja.
Himizo Kuomba
Hatimaye tunafikia sehemu ya mwisho ya mahubiri ya Yesu. Inaanza kwa ahadi za kutia moyo sana kuhusu maombi, kama ifuatavyo:
Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu ambaye, mwanamwe akimwomba mkate atampa jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? (Mathayo 7:7-11).
Msomaji mmoja anaweza kusema, “Aha! Nimepata sehemu ya Mahubiri ya Mlimani ambayo hayahusiani na utakatifu.”
Inategemeana na tunachokomba, na kwamba tunabisha na kutafuta nini katika sala. Kama wenye kuwa na “njaa na kiu ya haki”, tunatamani kutii yote ambayo Yesu ameamuru katika mahubiri Yake, na hiyo shauku inaonekana katika sala zetu. Ukweli ni kwamba ile sala mfano ambayo Yesu amefundisha hapo nyuma katika Mahubiri haya ni onyesho la shauku kwamba mapenzi ya Mungu yafanyike, na utakatifu upatikane.
Tena, tafsiri ya Luka ya ahadi hizo hizo za sala tunazotazama humalizika kwa maneno yafuatayo: “Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13). Yesu hakuwa anafikiria vituv ya starehe alipotuahidi “mema”. Katika akili Yake, Roho Mtakatifu ni “kipawa chema” kwa sababu hutufanya sisi kuwa watakatifu na kutusaidia kueneza Injili inayowafanya wengine kuwa watakatifu pia. Na watakatifu ndiyo wanaokwenda mbinguni.
Zawadi zingine nzuri ni chochote kilicho katika mapenzi ya Mungu. Ni wazi kwamba Mungu anashughulika zaidi na mapenzi Yake na ufalme Wake. Basi na sisi tutazamie kwamba sala zetu kuhusu chochote kitakachoongeza faida yetu katika ufalme wa Mungu zitajibiwa kila wakati.
Maneno Ya Kuhitimisha
Sasa tunafikia mstari ambao unapaswa kuhesabiwa kuwa ni hitimisho la kila kitu ambacho Yesu amesema kufikia hapa. Waandishi wengi wa mafafanuzi ya Biblia hushindwa kuona hilo, lakini ni muhimu sisi tusikosee. Mstari huu ni wa kumalizia maana unaanza kwa neno hili: Basi. Kwa hali hiyo umeunganika na mafundisho yaliyopita, na swali ni hili: Je, ni muhtasari kiasi gani wa yale ambayo Yesu amesema? Hebu tuusome na kufikiri kidogo juu yake.
Basi, yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo Torati na Manabii (Mathayo 7:12).
Maneno hayo hayawezi kuwa muhtasari wa ile mistari michache inayosema kuhusu maombi. Ingekuwa hivyo, haileti maana yoyote.
Kumbuka kwamba mapema kabisa katika mahubiri yake, Yesu alikuwa ameonya kuhusu kosa la kudhani kwamba amekuja kuitangua Torati na Manabii (ona Mathayo 5:17). Kuanzia hapo na kuendelea, mpaka mstari huu tunaotazama sasa, hakufanya kitu kingine isipokuwa kuunga mkono na kufafanua amri za Mungu katika Agano la Kale. Kwa hiyo sasa anahitimisha kila kitu kilichoagizwa – yote yaliyotoka katika Torati na Manabii – “Basi, yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo Torati na Manabii” (7:12). Maneno “Torati na Manabii” huunganisha kila kitu alichosema Yesu kati ya Mathayo 5:17 na 7:12.
Sasa, anapoanza kuhitimisha mahubiri Yake, anakariri tena fundisho Lake kuu – Ni watakatifu tu ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu.
Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba. Maana mlango ni mpana na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache (Mathayo 7:13-14).
Bila shaka huo mlango mwembamba na njia endayo uzimani ambayo wachache wanaiona, ni mfano wa wokovu. Ule mlango mpana na njia pana iendayo upotevuni ambayo ndiyo inafuatwa na wengi, ni mfano wa kupotea. Kama kila kitu alichosema Yesu kabla ya maneno haya kinamaanisha chochote – kama mahubiri haya yanakwenda kwa mpangilio unaofaa – kama Yesu alikuwa msemaji fundi mwenye ufahamu kuhusu kuwasiliana na watu, basi tafsiri halisi kabisa ni kwamba njia nyembamba ni njia ya kumfuata Yesu na kutii mafundisho Yake. Ile pana ni kinyume chake. Je, ni Wakristo wangapi walio kwenye njia hiyo nyembamba yenye kuelezwa katika mahubiri haya? Mtumishi anayefanya wengine kuwa wanafunzi yuko kwenye ile njia nyembamba, naye anawaongoza wanafunzi wake kuipitia.
Inawashangaza Wakristo wengine kwamba Yesu hakusema chochote kuhusu imani au kumwamini katika mahubiri haya ambayo kwa sehemu kubwa sana alizungumzia juu ya wokovu na kupotea. Kwa wale wanaoelewa kiungo kilichoko kati ya kuamini na mwenendo, mahubiri haya hayana matatizo yoyote. Watu wanaomtii Yesu huonyesha imani yao kwa matendo yao. Wale wasiomtii hawaamini kwamba ni Mwana wa Mungu. Wokovu wetu si onyesho tu la neema ya Mungu kwetu, bali hata lile badiliko lililotokea maishani mwetu ni onyesho pia. Kihalisi ni kwamba utakatifu wetu ni utakatifu Wake.
Jinsi Ya Kutambua Viongozi Waongo Wa Dini
Yesu alipoendelea kumalizia mahubiri Yake, alitoa onyo kwa wanafunzi Wake kuhusu manabii wa uongo ambao wanawaongoza wasioweza kuwatambua kuelekea upotevuni kwa njia ile pana. Hao si wa Mungu kweli, lakini wamejigeuza na kuonekana hivyo. Waalimu wote wa uongo na viongozi wa aina hiyo wako katika fungu hili. Wanawezaje kutambuliwa?
Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila aniambiaye ‘Bwana, Bwana’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?’ Ndipo nitawaambia dhahiri, ‘Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu’ (Mathayo 7:15-23).
Yesu alionyesha waziwazi kwamba waalimu wa uongo ni wadanganyifu sana. Wanaonekana kwa nje kuwa ni halisi. Wanaweza kumwita Yesu Bwana wao, wakatabiri, wakatoa pepo na kutenda miujiza. Lakini yale “mavazi ya kondoo” huficha “mbwa mwitu wakali”. Wao si kondoo wa kweli. Itajulikanaje kwamba ni wa kweli au wa uongo? Tabia yao ya kweli inaweza kutambulika kwa kuchunguza “matunda” yao.
Nini matunda anayozungumzia Yesu? Bila shaka si matunda ya miujiza. Ila, ni matunda ya kutii yote ambayto Yesu alifundisha. Wale walio kondoo wa kweli hufanya mapenzi ya Baba. Wale walio wa uongo ni “watenda maovu” (7:23). Wajibu wetu basi ni kulinganisha maisha yao na yale ambayo Yesu alifundisha na kuamuru.
Siku hizi waalimu wa uongo ni wengi sana makanisani, na hilo lisitushangaze kwa sababu Yesu na Paulo walituonya kwamba, kadiri mwisho unavyokaribia, tutazamie hivyo (ona Mathayo 24:11; 2Timo. 4:3-4). Manabii wa uongo walio wengi siku hizi ni wale wanaofundisha kwamba mbinguni wataingia wasiokuwa watakatifu. Hao wanawajibika kwa kupotea kwa mamilioni ya watu. John Wesley – mhubiri maarufu wa siku za nyuma – aliandika hivi juu yao:
Kitu hiki ni kibaya sana! – wakati wawakilishi wa Mungu wanapofanyika watendaji wa Shet ani! – wakati wale ambao wameagizwa kuwafundisha watu njia ya kufika mbinguni wanapowafundisha njia ya kwenda jehanamu … Kama mtu akiuliza, “Nani amewahi kufanya hviyo?” … Ninajibu hivi: Watu elfu kumi, wenye hekima na wanaoheshimiwa sana. Naam, wale wote, wa dhehebu lolote lile, wanaowatia moyo watu wenye kiburi, wenye kuchukulia mambo kirahisi-rahisi tu, wenye tamaa, wanaopenda dunia, wanaopenda starehe, wasiotenda haki au wema, watu rahisi kudanganyika, wasiojali, wasiodhuru chochote, wasiofaa, wasiokuwa tayari kuteseka kwa ajili ya haki, kwamba hao watakwenda mbinguni. Hao ni manabii wa uongo wa hali ya juu sana. Hao ni wasaliti wa Mungu na mwanadamu … Daima wanawaongoza watu kuelekea katika nchi za giza; na watakapowafuata hao maskini waliowapoteza, “kuzimu chini itataharuki ili kuwapokea!”[13]
Maneno hayo aliyasema katika kufafanua juu ya waalimu wa uongo ambao Yesu alionya juu yake katika Mathayo 7:15-23.
Ona tena kwamba Yesu alisema wazi kabisa – kinyume na tunavyoambiwa na waalimu wengi wa uongo siku hizi – wale wasiozaa matunda mema watatupwa jehanamu (7:19). Tena, hilo si kwa ajili ya waalimu na manabii tu, bali ni kwa wote. Yesu alisema hivi: “Si kila mtu aniitaye ‘Bwana, Bwana’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni wale watendao mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21, TLR). Kinachohusu manabii kinawahusu wote. Hiyo ndiyo mada kuu ya Yesu – Walio watakatifu tu ndiyo wataurithi ufalme wa Mungu. Watu wasiomtii Yesu wanakwenda jehanamu.
Ona pia jinsi Yesu anavyounganisha hali ya mtu ndani na jinsi alivyo nje. Miti “mizuri” huzaa matunda mazuri. Miti “mibaya” haiwezi kuzaa matunda mazuri. Chanzo cha matunda mazuri yanayoonekana kwa nje ni ile asili ya mtu. Mungu kwa neema Yake amebadilisha asili ya watu ambao wamemwamini Yesu kweli.[14]
Onyo La Mwisho Na Hitimisho
Yesu alimalizia mahubiri Yake kwa onyo la mwisho pamoja na hitimisho kwa njia ya mfano. Kama unavyotazamia, ni mfano kuhusu kweli kuu aliyozungumzia – Watakatifu ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu.
Basi kila asikiaye hayo maneno yangu na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye atafananishwa na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga. Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa (Mathayo 7:24-27).
Mfano wa mwisho wa Yesu sio ufunguo wa “mafanikio maishani” kama wengine wanavyosema. Mantiki inaonyesha kwamba hakuwa anatoa ushauri kuhusu jinsi ya kufanikiwa kifedha katika nyakati ngumu kwa kuwa na imani katika ahadi Zake. Huu ni muhtasari wa yote ambayo yesu alisema katika Mahubiri Yake ya Mlimani. Wale wanaofanya anayosema ni wenye hekima na watadumu. Hawahitaji kuogopa hasira ya Mungu itakapokuja. Wasiomtii ni wapumbavu nao watateseka sana. Watalipa gharama ya “adhabu ya kuangamizwa milele” (2Wathes. 1:9).
Jibu La Swali
Je, haiwezekani kwamba Mahubiri ya Yesu Mlimani yalikuwa ni kwa ajili ya wafuasi Wake tu, walioishi kabla ya kifo na kufufuka Kwake? Si wao walikuwa chini ya Torati kama njia ya muda tu ya wokovu, na baada ya Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zao ndipo waliokolewa kwa imani na kutangua kweli kuu inayotawala mahubiri haya?
Wazo hilo ni baya sana. Hakuna yeyote aliyewahi kuokolewa kwa matendo yake. Kila wakati imekuwa ni kwa imani – kabla na katika kipindi cha agano la kale. Paulo anatoa hoja katika Warumi 4 kwamba Ibrahimu (kabla ya agano la kale) na Daudi (wakati wa agano la kale) walihesabiw ahaki kwa imani, si kwa matendo.
Tena, ilikuwa ni vigumu kwa yeyote katika wasikilizaji wa Yesu kuokolewa kwa matendo, maana wote walikuwa wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (ona Warumi 3:23). Neema ya Mungu tu ndiyo ingewaokoa, na imani tu ndiyo ingepokea neema hiyo ya Mungu.
Kwa bahati mbaya sana – wengi katika kanisa siku hizi wanaona amri za Yesu kuwa hazina kusudi lingine isipokuwa kutufanya tujisikie hatia ili tuone jinsi isivyowezekana kupata wokovu kwa matendo. Kwa kuwa sasa “tumepata ujumbe” na kuokolewa kwa imani, tunaweza kupuuza amri Zake. Ila, kama tunataka wengine “waokolewe” basi tuzifuate. Tuzichomoe na kuwaonyesha watu jinsi walivyo na dhambi, ili waokolewe kwa “imani” isiyo na matendo.
Pamoja na hayo, Yesu hakuwaambia wanafunzi Wake hivi: “Enendeni ulimwenguni mwote mkawafanye watu kuwa wanafunzi, na mhakikishe kwamba, wakiisha tambua hatia yao na kuokolewa kwa imani, amri zangu zimemaliza kusudi lake katika maisha yao.” Badala yake alisema hivi: “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi … na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mathayo 28:19-20. Maneno mepesi kukazia). Watumishi wanaofanya watu kuwa wanafunzi wanafanya hayo hayo.
[1] Cha kuvutia ni kwamba, mstari unaofuata katika kitabu cha Yakobo unasema hivi: “Ndugu zangu, inafaa nini mtu akisema anayo imani, pasipo matendo? Je, imani hiyo yaweza kumwokoa?” (Yakobo 2:14).
[2] Hii ingekuwa kweli kwa habari ya kinachoitwa “sehemu za kuabudu katika Torati” pamoja na zile sehemu za “kiadili za Torati”, japo sehemu kubwa ya maelezo Yake kamili kuhusu Yeye kutimiza ile sehemu ya Torati ya kuabudu ingetolewa na Roho Wake Mtakatifu kwa mitume, baada ya kufufuka Kwake. Sasa tunaelewa ni kwanini hakuna haja ya kutoa dhabihu ya wanyama katika agano jipya. Ni kwa sababu Yesu alikuwa Mwanakondoo wa Mungu. Wala hatufuati zile sheria za vyakula zha agano la zamani kwa sababu Yesu alisema vyakula vyote vimetakaswa (ona Marko 7:19). Hatuna haja ya kuombewa na kuhani mkuu mwanadamu kwa sababu sasa Yesu ni Kuhani wetu Mkuu, n.k. Lakini – tofauti na sheria za kuabudu – hakuna sehemu yoyote ya sheria za maadili iliyobadilishwa na chochote alichosema au kutenda Bw2ana Yesu, kabla au baada ya kufa na kufufuka Kwake. Badala yake, Yesu alifafanua na kuunga mkono sheria ya Mungu ya maadili, kama walivyofanya wanafunzi kwa uvuvio wa Roho, baada ya kufufuka Kwake. Sehemu za maadili katika Torati ya Musa ziko kwa ukamilifu kabisa katika Sheria ya Kristo – sheria ya agano jipya. Kumbuka pia kwamba Yesu alikuwa anazungumza na Wayahudi waliokuwa chini ya Torati ya Musa. Basi maneno Yake katika Mathayo 5:17-20 yanapaswa kutafsiriwa katika mwangaza wa mafunuo Yake yanayoendelea yapatikanayo katika Agano Jipya.
[3] Tena, kama Yesu alikuwa anazungumza juu ya ile haki ya kisheria tunayohesabiwa na kuipokea kama zawadi kwa sababu ya kumwamini, mbona hakusema hivyo? Mbona akasema kitu ambacho kingekuwa rahisi kueleweka vibaya na wale watu waliokuwa wanamsikiliza, wasiosoma, ambao wasingeweza hata kukisia tu kwamba alikuwa anazungumza juu ya kuhesabiwa haki?
[4] Hilo linahusika katika mahusiano yetu na ndugu na dada zetu katika Kristo. Yesu aliwaita viongozi fulani wa kidini wapumbavu (tazama Mathayo 23:17), na utaona Maandiko mengine yakifanya hivyo kwa ujumla (ona Mithali 1:7; 13:20).
[5] Mungu hamhesabii hatia akiolewa tena, maana alinaswa katika dhambi ya mumewe. Maneno ya Yesu hayana maana yoyote kama hataolewa, maana kwa hali hiyo hawezi kuhesabiwa kuwa mzinzi.
[6] Hapa tena ni kwamba, Mungu hamhesabii hatia ya uasherati yule mume mpya. Yeye anafanya kitu cha kiungwana, kumwoa na kumtunza mwanamke aliyeachwa. Lakini, kama mwanamume atamtia mwanamke moyo amwache mume wake ili waoane, hapo ana hatia ya uzinzi, na yawezekana hiyo ndiyo maana ya maneno ya Yesu hapa.
[7] Kuna mazingira mengine ambayo lazima yashughulikiwe. Kwa mfano: Mwanamke aliyeokoka anayeachwa na mume wake asiyeokoka hana hatia ya uasherati kama ataolewa na mwanamume aliyeokoka.
[8] Huko mbele katika sura nyingine kuhusu talaka na ndoa tena, ninashughulikia swala hili kwa upana zaidi.
[9] Myahudi mmoja aliyekuwa mwalimu wa Torati alimwuliza Yesu swali hili: “Jirani yangu ni nani?” ili kujihesabia haki. Naomba ujue kwamba alikuwa anajua jibu sahihi. Bwana Yesu alimjibu kwa kusimulia habari ya Msamaria, mtu kutoka kabila lililochukiwa sana na Wayahudi, aliyejionyesha kuwa jirani kwa Myahudi aliyekuwa ametendewa vibaya. Jisomee Luka 10:25-37.
[10] Katika kitabu hiki huko mbele kuna sura nzima kuhusu hilo somo la kufunga.
[11] Kwa bahati mbaya, kuna wengine wanaosema haya si maombi yanayopaswa kutumiwa na Wakristo kwa sababu si “katika jina la Yesu”. Tukishika hoja hiyo, itabidi tuseme pia kwamba sala nyingi za mitume zinazopatikana katika Matendo na nyaraka mbalimbali hazikuwa “za Kikristo”.
[12] Wakati mwingine tena Yesu alisema haiwezekani kumtumikia Mungu na mali. Luka anatuambia hivi: “Basi Mafarisayo, ambao wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki” (Luka 16:14). Basi – hapa tena katika Mahubiri ya Mlimani, Yesu alikuwa anafunua wazi kawaida na mafundisho ya Mafarisayo.
[13] Hayo yametoka katika kitabu cha John Wesley kiitwacho The Works of John Wesley (Baker: Grand Rapids, 1996). Kimechapishwa upya kutoka toleo la 1872 la Wesleyan Methodist Book Room, London. Ukurasa wa 441, 416.
[14] Sitaacha kusema hapa kuhusu msemo wa kawaida watu wanaotumia, wanapojaribu kutetea dhambi ndani ya wengine. Wansema hivi: “Hatujui yaliyomo moyoni mwake.” Kinyume cha maneno hayo, Yesu anasema hapa kwamba mambo ya nje hudhihirisha mambo ya ndani. Mahali pengine alisema hivi: “Kinywa hunena yaujazayo moyo” (Mathayo 12:34). Mtu anapozungumza maneno ya chuki, inaonyesha chuki imejaa moyoni mwake. Yesu pia alituambia hivi: “Kutoka ndani – moyoni mwa mtu – hutokea mawazo maovu, uasherati, wizi, mauaji, uzinzi, tamaa na uovu, pamoja na udanganyifu, ashiki, wivu, matukano, kiburi na upumbavu” (Marko 7:21-22). Mtu anapozini, tunajua kilicho moyoni mwake: ni uzinzi.