Utangulizi

 

Kwa miaka ishirini na tano iliyopita nimepata nafasi ya kutembelea nchi zaidi ya arobaini na kusema na maelfu ya wachungaji katika makongamano ya siku tatu hadi tano. Makongamano hayo yamehudhuriwa na viongozi Wakristo wenye moyo wa huduma kutoka madhehebu mengi mbalimbali na vikundi katika mwili wa Kristo. Kila safari imethibitisha kwamba makongamano hayo ya siku tatu hadi tano hayatoshi kukutana na mahitaji yaliyopo. Kuna mengi zaidi yanayotakiwa kufanywa ili kuwawezesha viongozi wa Kikristo, na kitabu hiki ni jitihada ya kufanya hivyo.

Vile vile nimepata fursa ya miaka ishirini na kitu hivi kuchunga makanisa. Ingawa kwa kiwango fulani “nilifanikiwa”, mara nyingi nilijikuta nikipitia mambo magumu kwa sababu sikuwa na ufahamu wa kanuni za msingi sana za kufanya huduma KiBiblia. Basi, ninawahurumia sana watumishi mamilioni wanaofanya kazi kwa moyo wa dhati, ambao hawana kile nilichokosa mimi, na ambao wanahitaji kuwezeshwa zaidi kwa ajili ya kazi iliyoko mbele yao. Baadhi ya kanuni ambazo mimi sikuzifahamu ni za maana sana kiasi cha kwamba zinapoeleweka tu, zinatoa mwelekeo wa huduma kwa ajili ya maisha ya mtumishi. Zinakuwa vigezo ambavyo kwa hivyo, kila kiwango cha huduma kinapimwa. Kanuni hizo zinapatikana katika sura za mwanzo, na hazipaswi kupuuzwa na msomaji yeyote. Hii ni kwa sababu sura zile zinazofuata hazina maana yoyote bila ya msingi wake.

Kitabu hiki kinawahusu zaidi wachungaji, maana wao ndiyo viongozi wa kawaida wa Wakristo, lakini kila kitu nilichoandika kinawahusu wainjilisti pia, waalimu, wamishenari, waanzisha makanisa, waalimu wa Shule za Jumapili, na kadhalika. Hakuna yeyote katika mwili wa Kristo ambaye hatafaidika kutokana na kusoma kitabu hiki, kwa sababu kila mmoja katika mwili wa Kristo amepewa neema ya kufanya shughuli mojawapo kutoka kwa Mungu.

Nimewaandikia watumishi wanaokaa nje ya Marekani, Ulaya na Australia/New Zealand, japo haimaanishi kwamba yaliyoandikwa humu hayawahusu watumishi wa nchi hizo. Ukweli ni kwamba yale niliyoandika yanaweza kuwasaidia sana watumishi hao, lakini wao wana waalimu wengi tayari. Ila utagundua sura zingine kuwa za msaada zaidi kwako kuliko zingine, kutegemeana na ujuzi wako, maarifa uliyo nayo na taifa unalofanya huduma. Kwa mfano: Wachungaji wengi wa makanisa ya nyumbani ya Uchina, Kuba na Vietnam watagundua kwamba zile sura zenye kuzungumzia makanisa ya nyumbani hazina mengi ambayo hawayajui. Lakini, wachungaji wasiojua kitu kuhusu makanisa ya nyumbani wataona sura hizo kuwa zenye manufaa sana.

Si rahisi kwamba kila msomaji atakubaliana na kila kitu nilichoandika katika kitabu hiki. Miaka mitano iliyopita, hata mimi nisingekubaliana na baadhi ya yale niliyoandika katika kitabu hiki! Hivyo usiruhusu kutokuelewana kimawazo kidogo tu kukuzuie kujifunza mengine mengi kiasi unachoweza kutoka kila sura.

Kama Yesu alivyotufundisha, hakuna mtu awekaye divai mpya katika viriba vya zamani, maana vitapasuka. Ni viriba vipya tu vyenye uwezo wa kupanuka kiasi cha kutosha kuwezana na msukumo wa divai mpya. Japo baadhi ya mambo niliyoandika yanaweza kuhesabiwa kuwa ni divai mpya, ukweli ni kwamba ni divai ya zamani kabisa – yaani, ni ya zamani sawa na Agano Jipya. Kwa hiyo, kupasuka kwa viriba vya zamani haitakuwa shida ya divai itolewayo katika kurasa zinazofuata! Yesu alifurahia kwamba Mungu hufunua kweli Zake kwa watoto wachanga, na kuwaficha “wenye hekima na akili” (Mathayo 11:25). Vivyo hivyo, Mungu huwapa neema wanyenyekevu, bali huwapinga wenye kiburi (ona Yakobo 4:6). Mungu ashukuriwe kwa ajili ya viongozi wengi Wakristo ambao ni wanyenyekevu duniani kote. Mungu awabariki wanaposoma.

David Servant

Sura Ya Kwanza Kuweka Lengo Sahihi

Ni muhimu mtumishi aelewe lengo Mungu alilomwekea mbele yake, ili aweze kufaulu machoni pa Mungu. Asipolielewa lengo lake, hana jinsi ya kupima kama amefanikiwa au ameshindwa kulifikia.[1] Anaweza kufikiri amefanikiwa, kumbe ameshindwa, na hilo ni janga kubwa. Anafanana na mkimbiaji aliyeshika nafasi ya kwanza ambaye kwa furaha anamalizia mbio za mita 800, akiinua mikono yake mbele ya watu wanaomshangilia na kufurahia ushindi, bila ya kutambua kwamba mbio alizokuwa anashindana ni za mita 1600. Kutoelewa vizuri lengo lake kumesababisha kushindwa kwake. Kufikiri ameshinda kumehakikisha kwamba ameshindwa. Usemi ule: “Wa kwanza watakuwa wa mwisho” umetimia kwake kabisa.

Watumishi wengi wana lengo la namna fulani ambalo mara nyingi wanaliita “maono” yao. Hicho ndicho wanachojaribu kwa bidii sana kukifikia, kutokana na mwito wao maalum na karama waliyo nayo. Kila mtu ana karama na mwito wa kipekee: iwe ni kuchunga kanisa katika mji fulani, au kufanya uinjilisti katika eneo fulani, au kufundisha kweli fulani. Lakini lile lengo litolewalo na Mungu ninalozungumzia hapa ni la jumla na linamhusu kila mtumishi. Ni maono makubwa. Hayo ndiyo yanayotakiwa kuwa kiongozi – msukumo mkuu – kwa ajili ya kila maono ya kipekee. Lakini mara nyingi si hivyo. Watumishi wengi wana maono maalum ambayo hayakubaliani na yale maono ya jumla ya Mungu, na wengine wana maono maalum yenye kufanya kazi kinyume cha maono ya jumla ya Mungu. Hata mimi nilifanya hivyo wakati fulani, japo nilikuwa mchungaji wa kanisa linalokua.

Hilo lengo kuu au maono ya jumla ambayo Mungu amempa kila mtumishi, ni yapi? Tunaanza kupata jibu katika Mathayo 28:18-20, maandiko ambayo yanajulikana sana na sisi kiasi cha kwamba mara nyingi hatupati kinachosemwa nayo. Hebu tutazame fungu hilo mstari kwa mstari.

Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” (Mathayo 28:18).

Yesu aliwataka wanafunzi Wake kuelewa kwamba Baba Yake alikuwa amempa mamlaka yote. Kusudi la Baba lilikuwa (na mpaka sasa ni) wanafunzi na watu wote wamtii Yesu, maana ndiyo kawaida wakati Baba anapompa mtu mamlaka, wakati wote. Lakini Yesu ni wa pekee sana kwa sababu Baba Yake alimpa mamlaka yote mbinguni na duniani. Hayo si mamlaka yenye kipimo au mipaka kama anavyofanya wakati mwingine anapowapa wengine. Yesu Ni Bwana.

Sasa kama mambo ni hivyo, yeyote asiyehusiana na Yesu kama Bwana hafanyi sawasawa. Zaidi ya kingine chote, Yesu ni Bwana. Hii ndiyo sababu katika Agano Jipya anaitwa “Bwana” zaidi ya mara mia sita. (Anaitwa Mwokozi mara 15 tu.) Ndiyo sababu Paulo aliandika hivi: “Maana Kristo alikufa akawa hai tena ili awe Bwana wa waliokufa na walio hai pia” (Warumi 14:9, TLR – maneno mepesi kwa ajili ya kukazia). Yesu alikufa na kufufuka ili atawale (au amiliki) kama Bwana juu ya watu wote.

Imani Ya Kweli Yenye Kuokoa

Wainjilisti wa siku hizi na wachungaji wanapotoa mwito kwa watu wasio-okoka “wampokee Yesu kama Mwokozi,” jambo hilo hudhihirisha unyonge mkubwa katika kufahamu kwao Injili. Wazo hilo na jambo hilo halipo katika Maandiko kabisa! Tutumie mfano: Wakati yule mlinda gereza wa Filipi alipomwuliza Paulo afanye nini apate kuokoka, Paulo hakujibu hivi: “Mpokee Yesu kama Mwokozi wako.” Alisema hivi: “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka” (Matendo 16:31 – maneno mepesi kwa ajili ya kukazia). Watu wanaokolewa wanapomwamini Bwana yesu Kristo. Elewa tafadhali: Hawaokolewi kwa sababu wanaamini fundisho kuhusu wokovu au Yesu, bali wanapomwamini mtu – Bwana Yesu Kristo. Hiyo ndiyo imani yenye kuokoka. Wengi sana wanafikiri kwamba kwa sababu wanaamini kifo cha Yesu kilikuwa sadaka ya kutosha kwa ajili ya dhambi zao, au wokovu ni kwa imani, au vitu vingine vingi juu ya Yesu na wokovu, wana imani ya kuokoa. Hawana. Shetani anaamini vitu vyote hivyo kuhusu Yesu na wokovu. Imani yenye kuokoa ni imani katika Yesu. Na Yeye ni nani? Yeye ni Bwana.

Basi – kama ninaamini kwamba Yesu ni Bwana, nitafanya mambo yangu kwa mtazamo huo, nikijinyenyekeza Kwake kutoka moyoni mwangu. Nisipojinyenyekeza kwake, simwamini. Ni hivi: Mtu akisema, ‘naamini katika kiatu changu kuna nyoka wa sumu,’ halafu avae kiatu chake bila wasiwasi wowote, maana yake ni kwamba haamini kile anachosema anakiamini., Watu wanaosema kwamba wanamwamini Yesu lakini hawajatubu dhambi zao na kujinyenyekeza kwake mioyoni mwao, hawamwamini Yesu hata kidogo. Wanaweza kuwa wanamwamini Yesu wa kufikirika, lakini si yule Bwana Yesu, yule mwenye mamlaka yote mbinguni na duniani.

Hayo yote ni ili tuelewe kwamba ufahamu wa mtumishi kuhusu ujumbe wa msingi kabisa wa Ukristo unapokuwa mbaya, yuko katika matatizo tangu mwanzo. Hakuna jinsi atakayofanikiwa kwa kipimo cha Mungu, maana anapoeleza ujumbe wa msingi kabisa ambao Mungu anataka dunia isikie, anaupotosha. Anaweza kuwa mchungaji wa kanisa linalokua, lakini anashindwa vibaya kutimiza maono ya Mungu ya jumla kwa ajili ya huduma yake.

Maono Makubwa

Hebu sasa turudi kwenye Mathayo 28:18 hadi 19. Baada ya kutamka kuhusu Ubwana Wake wa kipekee, Yesu akatoa agizo, kama ifuatavyo:

Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mathayo 28:19-20a).

Ona kwamba Yesu alitumia neno “basi”. Alisema hivi: “Basi, enendeni, mkafanye … wanafunzi …” Yaani ni kama alisema hivi: “Kwa sababu ya hayo niliyokwisha sema … kwa sababu nina mamlaka yote … kwa sababu mimi ni Bwana … watu wanatakiwa kunitii Mimi bila shaka … nami ninawaagiza ninyi (na mnapaswa kunitii) mwende na kuwafanya watu kuwa wanafunzi, mkiwafundisha hao wanafunzi kutii amri Zangu zote.”

Na hilo basi – kwa lugha rahisi tu – ndiyo lengo kuu – ndiyo maono makuu ya Mungu kwa ajili ya huduma zetu zote – Wajibu wetu ni kufanya watu kuwa wanafunzi, wanaotii amri zote za Kristo.

Hii ndiyo sababu Paulo alisema yeye alipewa neema ya Mungu kama mtume, ili “kuleta utii utokanao na imani miongoni mwa Mataifa wote” (Warumi 1:5, TLR – maneno mepesi kukazia). Lengo ni utii; jinsi ya kufikia utii huo ni imani. Watu ambao wana imani ya kweli katika Bwana Yesu hutii maagizo Yake.

Ndiyo sababu Petro alihubiri hivi Siku ya Pentekoste: “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo” (Matendo 2:36). Petro alitaka hao waliomsulubisha Kristo wajue kwamba Mungu amemfanya Yesu kuwa Bwana na Kristo. Wao walimwua ambaye Mungu alitaka watu wamtii! Wakijisikia hukumu kuu, waliuliza: “Tutendeje?” na Petro akajibu kwanza kwa kusema hivi: “Tubuni”! Yaani, geukeni mwache kutokutii, mtii. Mfanyeni Yesu kuwa Bwana. Kisha, Petro akawaambia wabatizwe kama Kristo alivyoagiza. Petro alikuwa anafanya watu kuwa wanafunzi – wafuasi watiifu wa Kristo – na alikuwa anaanza vizuri kwa ujumbe ulio sahihi.

Kama ni hivyo, kila mtumishi anatakiwa aweze kupima au kutathmini mafanikio yake. Sote tunapaswa kujiuliza hivi: “Je, huduma yangu inawaongoza watu kutii amri zote za Kristo?” Kama tunafanya hivyo, tunafanikiwa. Kama hatufanyi hivyo, tunashindwa.

Mwinjilisti anayeshawishi tu watu “wampokee Yesu” bila ya kuwaambia watubu dhambi zao, anashindwa. Mchungaji anayejaribu kuwa na kanisa kubwa kwa kuwafurahisha watu wote na kuweka mambo mengi ya kijamii anashindwa. Mwalimu anayefundisha “upepo wa mafundisho” mapya tu ya kiroho anashindwa. Mtume anayeanzisha makanisa yenye watu wanaosema wanamwamini Yesu bila kumtii, anashindwa. Nabii anayetabiri baraka zinazokuja maishani mwa watu karibuni tu anashindwa.

Kushindwa Kwangu

Miaka kadhaa iliyopita wakati nikiwa mchungaji wa kanisa lenye kukua, Roho Mtakatifu aliniuliza swali lililofungua macho yangu, nione jinsi nilivyokuwa ninashindwa kutimiza maono ya jumla ya Mungu. Roho Mtakatifu aliniuliza swali lifuatalo, nilipokuwa nasoma juu ya hukumu ijayo ya kondoo na mbuzi, kama inavyotajwa katika Mathayo 25:31 hadi 46. Aliniuliza hivi: “Kama kila mtu katika kanisa lako angekufa leo na kusimama kwenye hukumu ya kondoo na mbuzi, wangapi wangekuwa kondoo, na wangapi wangekuwa mbuzi?” Akauliza tena, kwa kumaanisha sana: “Katika mwaka uliopita, ni wangapi katika kanisa lako wamewapa chakula wapendwa katika Kristo waliokuwa hawana? Ni wangapi wametoa maji kwa wapendwa wasiokuwa nayo? Ni wangapi wamewasaidia wapendwa wasio na makao kuwa na makao? Ni wangapi wamekaribisha wapendwa wasafiri kulala kwao? Ni wangapi wametoa mavazi kwa wapendwa wasiokuwa nayo? Ni wangapi waliwatembelea wagonjwa au wapendwa waliofungwa?” Nikatambua kwamba ni wachache sana waliofanya lolote katika hayo, japo walikuja kanisani, waliimba nyimbo za kuabudu, walisikiliza mahubiri yangu na kutoa fedha zao katika vyombo vya sadaka. Kumbe kwa kiwango cha Kristo wao ni mbuzi, na kwa sehemu mimi ninahusika na wao kuwa hivyo maana sikuwa nawafundisha jinsi ilivyo muhimu kwa Mungu sisi kusaidia katika mahitaji mazito yanayowakabili ndugu zetu na dada zetu katika Kristo. Sikuwa nawafundisha kutii yote ambayo Yesu aliagiza. Nikatambua kwamba nilikuwa napuuza kilichokuwa cha maana sana kwa Mungu – amri kuu ya pili: kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda wenyewe – licha ya kupuuza ile amri mpya aliyotupa Yesu: tupendane sisi kwa sisi, kama Yesu alivyotupenda.

Zaidi ya hayo – nikatambua kwamba kile nilichokuwa nafundisha kilikuwa kinyume kabisa na lile lengo kuu la Mungu la kuwafanya watu kuwa wanafunzi, maana mimi nilifundisha aina nyepesi ya “injili ya mafanikio” kanisani kwangu. Ingawa ni mapenzi ya Yesu kwamba watu Wake wasijiwekee hazina duniani (Mathayo 6:19-24), na kwamba watosheke na walicho nacho, hata kama ni mavazi tu na chakula (ona Waebrania 13:5; 1Timo. 6:7-8), mimi nilikuwa nafundisha Wamarekani wangu matajiri kwamba Mungu alitaka wao wazidi kuwa na mali. Niliwafundisha watu wasimtii Yesu katika eneo moja (sawa tu na jinsi ambavyo mamia ya maelfu ya wachungaji wengine wanavyofanya duniani kote).

Nilipotambua hayo, nilitubu na kuomba msamaha mbele ya kanisa langu. Nilianza kujaribu kufanya watu kuwa wanafunzi, nikiwafundisha kutii yote ambayo Kristo aliagiza. Nilifanya hivyo kwa hofu na kutetemeka, nikifikiri kwamba wangi katika kusanyiko langu hawakutaka kutii amri zote za Kristo, wakipenda Ukristo rahisi tu ambao haukudai kujitoa sana. Na ndivyo ilivyokuwa. Wengi hawakujali kuhusu waamini wanaoteseka duniani kote. Hawakujali juu ya kuipeleka Injili kwa ambao hawajaisikia. Badala yake, wao walijali zaidi juu ya kujipatia vitu vingi wenyewe. Kwa habari ya utakatifu ni kwamba, waliepuka sana zile dhambi zenye kuleta aibu – dhambi ambazo hata wasio-okoka walikuwa wanazipinga, nao waliishi maisha ya kawaida tu – kama Wamarekani wa kawaida wasio na Ukristo. Lakini ukweli ni kwamba hawakumpenda Bwana kwa sababu hawakutaka kuzishika amri za Yesu – sawa tu na Yeye mwenyewe anavyosema kwamba ndiyo uthibitisho wa pendo letu Kwake (ona Yohana 14:21).

Nilichokiogopa kikawa kweli – washirika wengine kumbe walikuwa mbuzi katika ngozi za kondoo. Nilipowataka wajikane na kujitwika misalaba yao, wengine walikasirika. Kwao, kanisa lilikuwa kitu cha kijamii tu chenye kuambatana na muziki mzuri – sawa tu na jinsi dunia inavyofurahia vilabu na majumba ya starehe. Wangevumilia mahubiri fulani mradi tu yathibitishe wokovu wao na upendo wa Mungu kwao. Lakini – hawakutaka kusikia yale Mungu aliyotaka kutoka kwao. Hawakutaka mtu yeyote kuhoji juu ya wokovu wao. Hawakuwa tayari kulinganisha maisha yao yakubaliane na mapenzi ya Mungu kama ingewagharimu chochote. Kweli walikuwa tayari kutoa fedha zao kidogo wakishawishiwa kwamba Mungu angewarudishia zaidi, na kama watapata faida moja kwa moja kutokana na walichotoa – yaani, kama fedha zao zingetumiwa kuboresha majengo au kitu fulani kanisani.

Wakati Wa Kujichunguza

Pengine huu ungekuwa wakati mzuri kwa kila mtumishi anayesoma kitabu hiki kujiuliza mwenyewe swali lile lile ambalo Roho Mtakatifu aliniuliza mimi. Jiulize hivi: “Kama wote ninaowahudumia wangekufa sasa na kusimama kwenye hukumu ya kondoo na mbuzi, wangapi wangekuwa kondoo na wangapi wangekuwa mbuzi?” Watumishi wanapowahakikishia watu wenye matendo kama mbuzi katika makusanyiko yao kwamba wameokoka, wanawaambia kinyume kabisa cha yale ambayo Mungu anataka wasikie. Mtumishi wa aina hiyo anafanya kazi kinyume na Kristo. Anajiweka upande kinyume na yale ambayo Yesu anataka watu kama hao waambie, kulingana na maneno Yake katika Mathayo 25:31 hadi 46. Sababu ya Yesu kusema aliyosema hapo ni kutoa onyo kwa mbuzi. Yeye hataki wafikiri kwamba wanakwenda mbinguni.

Yesu alisema watu wote watajua kwamba sisi ni wanafunzi Wake kwa jinsi tunavyopendana (ona Yohana 13:35). Bila shaka alimaanisha upendo unaozidi ule wa watu wasio-okoka maana vinginevyo, wanafunzi Wake wasingeweza kutofautishwa na wasioamini. Upendo aliozungumzia Yeye ni upendo wa kujitoa – tunapopendana kama Yeye alivyotupenda – mpaka kutoa maisha yetu kwa ajili ya wenzetu (ona Yohana 13:34; 1Yohana 3:16-20). Yohana pia aliandika kwamba tunajua tumepita kutoka mautini hadi uzimani – yaani, tumezaliwa mara ya pili – wakati tunapopendana sisi kwa sisi (1Yohana 3:14). Je, watu wanaonung’unika, na kuwasema, na kuwachukia watumishi wenye kufundisha amri za Kristo wanaonyesha upendo ule ambao ni ishara kwamba wamezaliwa mara ya pili? HAPANA – wao ni mbuzi wanaokwenda jehanamu.

Wanafunzi Wa Mataifa Yote

Kabla ya kusonga mbele, hebu tutazame tena Mathayo 28:19-20 – Agizo Kuu ambalo Yesu alitoa kwa wanafunzi Wake – ili tuone kama tunaweza kupata mengine kutoka humo.

Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mathayo 28:19-20a).

Ona hapo kwamba Yesu anataka wanafunzi wapatikane katika mataifa yote – au kama neno la Kiyunani linavyomaanisha – katika kila kundi la kikabila hapa duniani. Ikiwa Yesu alitoa agizo hilo, mimi naamini ni kitu kinachowezekana. Tunaweza kufanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu katika kila kundi la kikabila hapa duniani. Kazi haikutolewa kwa wale wanafunzi kumi na mmoja tu bali kwa kila mwanafunzi aliyekuja baada yao, kwa sababu Yesu aliwaambia wale kumi na moja kuwafundisha wanafunzi wao kuyashika yote aliyokuwa amewaamuru wao. Kwa hiyo, wale kumi na moja wakawafundisha wanafunzi wao kushika amri ya Kristo ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi katika mataifa yote. Basi, amri hiyo intgekuwa ikijiendeleza katika kila mwanafunzi. Kila mwanafunzi wa Yesu anatakiwa kujihusisha kwa nmana fulani katika shughuli ya kuwafanya watu wa mataifa yote kuwa wanafunzi.

Hii kwa sehemu inatoa sababu ya kutotimizwa kwa “Agizo Kuu” kufikia sasa. Hata ingawa kuna wanaojiita Wakristo mamilioni kwa mamilioni, idadi ya wanafunzi halisi ambao wamejitolea kumtii Yesu ni ndogo sana. Sehemu kubwa ya wanaokiri Ukristo hawajali kuhusu watu kufanyika wanafunzi katika kila kundi la kikabila kwa sababu hawajajitolea kutii amri za Kristo. Mada hiyo inapogusiwa, watatoa hoja kama zifuatazo: “Hiyo si huduma yangu,” au “Sijisikii kuongozwa upande huo”. Wachungaji wengi tu hutoa maneno kama hayo, sawa tu na mbuzi wote wenye kuchagua ni amri zipi za Kristo zinazolingana na mipango na maisha yao.

Kama kila Mkristo angemwamini Bwana Yesu Kristo kweli kweli, isingechukua muda mrefu – kila mtu angesikia injili hapa duniani. Kujitolea kwa wanafunzi wote wa Kristo kungefanikisha hilo. Wangeacha kupoteza wakati wao wote na fedha kwenye vitu vya muda tu na vya kidunia, na kuzitumia kutimiza yale ambayo Bwana wao aliwaagiza wafanye. Lakini, inapotokea mchungaji mcha Mungu atangaze kwamba kuna mishenari atakayehubiri katika ibada inayofuata, mara nyingi atazamie idadi ya watu kupungua. Mbuzi wengi watakaa nyumbani au kwenda mahali pengine. Hawajali sana kutii amri ya mwisho ya Bwana Yesu Kristo. Lakini kondoo kila mara wanasisimka kupata nafasi ya kujihusisha katika kuwafanya watu kuwa wanafunzi katika mataifa yote.

La mwisho kuhusu Mathayo 28:18 hadi 20 – Yesu pia aliwaambia wanafunzi Wake wawabatize wanafunzi wao, na mitume walitii agizo hilo kwa uaminifu sana. Walikuwa wanawabatiza mara moja wale waliotubu na kumwamini Bwana Yesu. Ubatizo ni mwamini kujitambulisha na kifo, kuzikwa na kufufuka kwa Kristo. Waamini wapya wamekufa na wamefufuliwa kama viumbe vipya ndani ya Kristo. Yesu alitaka kweli hiyo muhimu kuonyeshwa kwa tendo la ubatizo wa kila mwamini mpya – kama kupiga muhuri akilini mwake kwamba sasa amekuwa mtu mpya mwenye asili mpya. Yeye ni roho moja pamoja na Kristo, na sasa ametiwa nguvu za kumtii Mungu kwa njia ya Kristo akaaye ndani yake. Alikuwa amekufa katika dhambi zake, lakini sasa ameoshwa na kuwa safi, na amefanywa hai kwa Roho Mtakatifu. Yeye ni zaidi ya “aliyesamehewa tu”. Badala yake, amebadilishwa kabisa. Basi, Mungu anaonyesha tena kwamba waamini wa kweli ni watu tofauti, ambao wanatenda kitofauti na jinsi walivyotenda walipokuwa wafu kiroho. Hiyo ndiyo maana ya maneno ya mwisho ya Yesu, anaposema, “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20). Je, ni sahihi kufikiri kwamba kuwepo kwa Kristo daima miongoni mwa watu kungeathiri tabia na mwenendo wao?

Yesu Afafanua Uanafunzi

Tumekwisha onyesha kwamba lengo kuu la Yesu kwa ajili yetu ni tufanye watu wote kuwa wanafunzi, yaani, watu ambao wametubu dhambi zao na wenye kujifunza na kutii amri Zake. Yesu alifafanua zaidi maana ya mwanafunzi, katika Yohana 8:31 na 32.

Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

Basi, wanafunzi wa kweli – kulingana na maelezo ya Yesu – ni wale ambao wanadumu, au wanakaa katika Neno Lake. Wanapojifunza kweli Yake kutoka katika Neno Lake, wanaendelea “kuwekwa huru”, na inaonekana Yesu alikuwa anazungumza juu ya kuwekwa huru kutokana na dhambi (angalia Yohana 8:34-36). Basi tunaona tena kwamba maelezo ya Yesu yanatuonyesha wanafunzi ni wanaojifunza na kutii amri Zake.

Baadaye Yesu alisema hivi:

Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mnathibitisha kuwa ni wanafunzi Wangu” (Yohana 15:8, TLR – maneno mepesi kukazia).

Basi, kwa maelezo ya Yesu – wanafunzi wanamtukuza Mungu kwa kuzaa matunda. Wale wasiozaa matunda wanathibtishwa kwamba si wanafunzi Wake.

Tena Yesu akazidi kufafanua hayo matunda yenye kuwatambulisha wanafunzi Wake wa kweli, katika Luka 14:25 hadi 33. Hebu tutazame kwanza mstari wa 25.

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia …

Je, Yesu aliridhika kwa kuwa makutano mengi “walifuatana” Naye? Je, alikuwa sasa amefikia lengo Lake kwa vile alifanikiwa kuwa na kusanyiko kubwa?

Hapana – Yesu hakuridhika kwamba makundi makubwa yalikuwa yanamfuata, kwamba wengi walikuwa wanasikiliza mahubiri Yake na kutazama miujiza Yake na wakati mwingine kula chakula Chake. Yesu anatafuta watu wanaompenda Mungu kwa moyo wote, akili, nafsi na nguvu. Anataka watu wanaotii amri Zake – anataka wanafunzi. Kwa hiyo, aliwaambia hivi hao watu wengi waliokuwa wanamfuata:-

Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu (Luka 14:26).

Hapo hakuna kufanya kosa: Bwana Yesu aliweka sharti la kutimizwa na mtu yeyote anayetaka kuwa mwanafunzi Wake. Lakini, lazima wanafunzi Wake kweli wawachukie watu hao ambao ndiyo kwa asili wangewapenda sana? Hiyo si maana yake maana tunaagizwa na Maandiko kuwaheshimu wazazi wetu na kuwapenda wenzetu na watoto wetu.

Bila shaka Yesu alikuwa anatumia lugha ya mfano. Lakini bila shaka alimaanisha hivi: Kama tunataka kuwa wanafunzi Wake, lazima tumpende Yeye kuliko vyote – zaidi kuliko watu ambao kwa asili tungewapenda sana. Matazamio ya Yesu ni halisi kwa sababu Yeye ni Mungu ambaye tunapaswa kumpenda kwa moyo wote, akili zote, nafsi yote na nguvu zote.

Usisahau – kazi ya watumishi ni kufanya watu kuwa wanafunzi, ambayo inamaanisha kwamba wanatakiwa kuzaa watu wenye kumpenda Yesu tu, wenye kumpenda sana, zaidi sana kuliko wanavyowapenda hata wenzao katika ndoa, na watoto na wazazi. Ingekuwa vizuri kila mtumishi anayesoma maneno haya sasa kujiuliza hivi: “Nimefanikiwa kiasi gani kuzaa watu wa aina hiyo?”

Tutajuaje kwamba mtu anampenda Yesu? Yeye mwenyewe alituambia hivi katika Yohana 14:21 – “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Basi, ni kitu sahihi kabisa kufikia uamuzi kwamba, watu wanaompenda Yesu kuliko wanavyowapenda wenzao katika ndoa, kuliko watoto na wazazi ndiyo watu watakaoshika amri Zake. Wanafunzi wa Yesu huzitii amri Zake.

Sharti La Pili

Yesu aliendelea kuzungumza na watu wengi siku ile, waliokuwa wanamfuata njiani kwa kusema hivi:

Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu (Luka 14:27).

Hili ndiyo sharti la pili ambalo Yesu aliweka kwa mtu kuwa mwanafunzi Wake. Je, alimaanisha nini? Je, wanafunzi wanapaswa kubeba mbao kubwa? Hapana – hapa tena, Yesu anatumia lugha ya mfano.

Bila shaka, Wayahudi wengi miongoni mwa wasikilizaji Wake walikuwa wameona wahalifu waliohukumiwa kifo wakisulubiwa msalabani. Warumi waliwasulubisha wahalifu kwenye njia kuu nje ya malango ya mji, ili watu wengi waone jambo hilo, ili liwe kama kizuizi cha watu kujihusisha katika uhalifu.

Basi, mimi nadhani kwamba ule msemo – “Beba msalaba wako” – ulikuwa wa kawaida katika siku za Yesu. Kila mtu aliyesulubiwa alisikia askari wa Kirumi akimwambia, “Chukua msalaba wako, unifuate.” Hayo ni maneno ambayo mhalifu aliogopa kuyasikia, kwa sababu alijua ndiyo mwanzo wa masaa na siku za mateso makali sana. Kwa hiyo, msemo huo ungeweza kuwa wa kawaida tu uliomaanisha hivi: “Kubaliana na magumu yanayokujia, ambayo hayaepukiki.”

Ninakisia kwamba hata akina baba waliwaambia watoto wao wa kiume, “Mwanangu, najua unachukia kuchimba choo. Ni kazi chafu yenye harufu kali. Lakini, ni wajibu wako mara moja kwa mwezi, hivyo, chukua msalaba wako. Nenda ukachimbe choo.” Nakisia kwamba wake waliwaambia waume zao, “Mpenzi, najua jinsi unavyochukia kulipa kodi kwa Warumi. Lakini leo kodi inatakiwa, na Mkusanya Kodi anapanda kwenye njia yetu sasa hivi. Basi, chukua msalaba wako. Nenda umlipe.”

Kuchukua msalaba ni sawa na kujikana, na Yesu alitumia maneno hayo kumaanisha hivyo katika Mathayo 16:24 – “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Kwa maneno mengine ni hivi: “Mtu yeyote akitaka kunifuata, aweke kando mambo yake mwenyewe, akubali magumu yasiyoepukika yanayokuja kwa sababu ya uamuzi wake, kisha anifuate.”

Basi, wanafunzi wa kweli wako tayari kuteseka kwa ajili ya kumfuata Yesu. Tayari wamekwisha hesabu gharama kabla ya kuanza, na, kwa sababu wanajua kwamba magumu hayaepukiki, wanaanza mwendo kwa nia ya kumaliza safari. Tafsiri hii inakubaliana na maneno yaliyofuata, aliyosema Yesu, kuhusu kuhesabu gharama ya kumfuata. Alitumia mifano miwili kukazia jambo hilo.

Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali (Luka 14:28-32).

Anachosema Yesu hapa ni wazi kabisa: “Ukitaka kuwa mwanafunzi Wangu, hesabu gharama mapema, usije ukakata tamaa mambo yatakapokuwa magumu. Wanafunzi wa kweli hukubali magumu yanayokuja kwa sababu ya kunifuata.”

Sharti La Tatu

Yesu alitaja sharti lingine moja la uanafunzi kwa wasikilizaji Wake siku hiyo.

Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu (Luka 14:33).

Hapa tena inaonekana kwamba Yesu alikuwa anatumia lugha ya mfano. Hatutakiwi kuacha kila kitu tulicho nacho kwa maana kwamba tunabaki bila makao, mavazi na chakula. Lakini, ni lazima tuachilie kila kitu tulicho nacho kwa maana ya kumkabidhi Mungu avimiliki, na kufikia kiwango cha kutotumikia mali, bali kumtumikia Mungu kwa mali zetu. Bila shaka maana yake ni kuachana na vitu vingi visivyo vya lazima na kuishi maisha rahisi tu ya kushrikishana vitu na uwakili mbele za Mungu, kama walivyofanya Wakristo wa kwanza tunaosoma habari zao katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Maana ya kuwa mwanafunzi wa Yesu ni kuzishika amri Zake, Naye aliwaagiza wafuasi Wake kutojiwekea hazina duniani, bali mbinguni.

Tuhitimishe yote yaliyokwisha sema: Kulingana na Yesu, ikiwa mimi ninataka kuwa mwanafunzi Wake, lazima nizae matunda. Lazima nimpende Yeye kuliko vyote, hata zaidi ya watu wa familia yangu. Lazima niwe tayari kukabiliana na magumu yote yatakayokuja kwa sababu ya uamuzi wangu wa kumfuata. Na ni lazima nifanye anachosema, kuhusu mapato yangu na mali zangu. (Na amri Zake nyingi zinasema kitu juu ya hilo, kwa hiyo nisijidanganye, kama wengi wanavyofanya, kwamba, “Kama Bwana angeniambia nifanye kitu na mali zangu, ningefanya chochote alichosema.”

Na hao ndiyo wafuasi waliojitoa kwa Kristo, ambao sisi kama watumishi tunatakiwa kuwaszaa! Ndilo lengo tulilopangiwa na Mungu! Tumeitwa kuwa watumishi wenye kufanya watu kuwa wanafunzi!

Huo ni ukweli wa msingi sana ambao watumishi wengi duniani hawana habari nao kabisa. Kama watatathmini huduma zao kama nilivyofanya mimi, itabidi wafikie uamuzi kwamba hawafikii shauku na matazamio ya Mungu – kama mimi nilivyogundua. Nilipotazama kiwango cha kujitoa kwa Kristo kwa watu katika kanisa langu, sikuwa na mashaka kwamba, wengi sana wasingestahili kuwekwa katika fungu la wanafunzi wa Yesu kweli.

Wachungaji: Tazameni washirika wenu. Kulingana na masharti ya Yesu katika Luka 14:26-33, ni washirika wangapi ambao Yesu anaona kuwa ni wanafunzi Wake? Wainjilisti: Je, ujumbe mnaohubiri unazaa watu wanaojitolea kutii amri zote za Kristo?

Huu ndiyo wakati wa kutathmini huduma zetu, kabla ya kusimama mbele za Yesu wakati wa hukumu ya mwisho. Kama ninashindwa kufikia lengo Lake, ni afadhali kujua sasa kuliko wakati huo. Au wewe unaonaje?

Wazo La Mwisho, La Kushtua

Ni dhahiri kwamba Yesu anataka watu kuwa wanafunzi Wake, kama inavyodhihirishwa kwa maneno Yake kwa wale watu wengi waliomfuata katika Luka 14:26-33. Je, ni muhimu kiasi gani kuwa mwanafunzi Wake? Inakuwaje kama mtu ataamua asiwe mwanafunzi Wake? Yesu alijibu maswali hayo yote mwishoni mwa mafundisho aliyotoa katika Luka 14.

Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee? Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie (Luka 14:34-35).

Chumvi inatakiwa kuwa na ladha. Ndiyo inayoifanya kuwa chumvi. Ikipoteza ladha yake, haifai kwa lolote, nayo “hutupwa nje”.

Hayo yanahusianaje na mambo ya kuwa mwanafunzi? Ni hivi: Kama ambavyo chumvi inatazamiwa kuwa na ladha, ndivyo Yesu anavyowatazamia watu kuwa wanafunzi Wake. Kwa kuwa ni Mungu, jukumu letu la maana ni kumpenda Yeye kabisa na kuichukua misalaba yetu. Tusipokuwa wanafunzi Wake, tunakataa sababu anayotoa Yeye ya kuwepo kwetu. Hatufai kwa lolote, na mwisho wetu ni “kutupwa nje”. Hapo hakuna kuingia mbinguni – au sivyo?

Wakati mwingine tena, Yesu aliwaambia hivi wanafunzi Wake (katika Mathayo 5:13):-

Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu (Mathayo 5:13).

Hayo ni maonyo yenye kushtua kweli kweli. Kwanza: Ni wale tu walio chumvi yenye ladha (mfano wa “kutii kwa kujitoa”) ndiyo wenye maana kwa Mungu. Wengine “hawafai kwa lolote … ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.” Pili: Inawezekana kwa mtu ambaye ni “chumvi yenye ladha” kupoteza “ladha” yake. Ingekuwa sivyo, Yesu asingekuwa na haja ya kuwaonya wanafunzi Wake. Kweli hizo mbili zinapingana na mafundisho ya wengi siku hizi, wanaosema kwamba mtu anaweza kuwa Mkristo aaminiye na anayekwenda mbinguni, na asiwe mwanafunzi wa Kristo. Mengine yanasema haiwezekani kupoteza wokovu wa mtu. Tutayatazama zaidi mawazo hayo ya makosa katika sura za baadaye.


[1] Katika kitabu kizima ninazungumza juu ya wachungaji (au watumishi) kwa mtazamo kwamba ni wanaume kwa sababu ndiyo wengi. Lakini ninaamini kutokana na Maandiko kwamba Mungu huwaita wanawake kufanya huduma ya kudumu, nami ninafahamu kadhaa wenye huduma nzuri sana. Mada hiyo tutaitazama katika sura inayoitwa Wanawake Katika Huduma.

Uhakika Wa Wokovu

SURA YA KUMI NA MOJA

Je, inawezekana kuwa na uhakika wa wokovu? Je, mtu anaweza kujua hakika kwamba, akifa sasa, ataokoka? Ndiyo. Mtume Yohana aliandika hivi:

Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu (1Yohana 5:13).

Waalimu wa neema bandia mara nyingi hutumia andiko hili moja tu kutia nguvu ujasiri wa wote wanaokiri kwamba wanamwamini Yesu. Lakini mara nyingi wanakosea kabisa maana ya Yohana.

Kwanza: Yohana anasema aliwaandikia wale wanaoliamini jina la Mwana wa Mungu, si wale wanaoamini kwamba wameokolewa kwa kuamini fundisho la wokovu. Hatuokoki kwa kuamini kwamba wokovu ni kwa neema kwa njia ya imani – tunaokoka kwa kumwamini Mtu. Na kama tunaamini kwamba Yesu ni Mungu, tutatenda, tutaishi na kuzungumza kama tunavyoamini.

Tena: Ona kwamba Yohana alisema ameandika “mambo hayo” ili wasomaji wake wapate kujua kwamba wanao uzima wa milele. Ni mambo gani hayo? Yohana alitoa tamko lake mwishoni mwa barua yake, kuhusu kila kitu alichokuwa ameandika. Yeye alikuwa ameandika barua yake nzima ili wasomaji wake wajue kwamba wanao uzima wa milele. Kwa kutathmini maisha yao kulingana na kila kitu alichokisema, chenye kuwa ishara ya waamini wote wa kweli, wangeweza kutambua kama wameokoka kweli au hapana.

Kwa kujilinganisha na yale ambayo Yohana anasema ni ishara ya waamini wa kweli, sisi pia tunaweza kuamua ikiwa neema ya Mungu imetubadilisha kweli au hapana. Kama imetubadilsha, basi tuna uhakika kwamba tumeokoka. Hii si kutegemea matendo yetu kutuokoa. Badala yake, ni kupata uhakikisho wa wokovu kwa ushahidi wa neema ya Mungu kwa njia ya matendo Yake ndani yetu na kupitia kwetu. Wengi wanaopinga kushika sheria hushikilia kumbukumbu ya ombi moja tu ambalo limewahi kuombwa ili kupata uhakika ambao ni bandia, wa wokovu wao. Lakini waamini wa kweli wanaweza kutazama maisha yao na kuona kazi ya neema ya Mungu inayobadilisha maisha. Tunaweza kujua kwamba tumeokoka.

Je, Yohana aliandika nini ambacho kinatusaidia kufanya tathmini yetu? Nini alama zenye kuonyesha waamini wa kweli? Yohana anarudia mara kwa mara kutaja vipimo vitatu. Kimoja ni cha maadili (ona 2:3-6; 2:28 hadi 3:10); kingine ni cha kijamii (ona 2:7-11; 3:11-18; 4:7-21) na kingine ni cha mafundisho (ona 2:18-27; 4:1-6). Hebu tuyatazame yote matatu.

Kipimo Cha Maadili: Kutii Amri Za Yesu

Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, ‘Nimemjua,’ wala hazishiki amri zake ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda (1Yohana 2:3-6. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Tukizishika amri za Yesu, (1) tunajua kwamba tumemjua, na (2) tunajua kwamba tumo ndani Yake.

Kuna ambao wangependa tuamini kwamba “kumjua Yesu” ni lugha yenye kuzungumza juu ya Wakristo waliokomaa zaidi katika Kristo. Wakristo wachanga ambao hawajakomaa hawa”mjui” Yesu vizuri sana kama wale wa zamani kidogo. Basi, kuna wanaofikia mahali pa kuamua kwamba Yohana alimaanisha kwamba tunaweza kujua kama sisi ni Wakristo waliokomaa au ambao bado, kwa utii wetu au kutokutii. Lakini je, hiyo ndiyo maana ya Yohana?

Bila shaka sivyo, kwa sababu kadhaa. Katika mstari tuliosoma, Yohana pia anatumia maneno haya: “ndani Yake”, akionyesha kwamba tunaweza pia kujua kama tuko ndani ya Kristo ikiwa tutazishika amri Zake. Mtu ambaye amesoma Agano Jipya anajua kwamba waamini wote wa kweli wako ndani ya Kristo, si wale tu waliokomaa zaidi ya wengine. Kwa kuwa wale ambao wako ndani Yake na wale wanaomjua Yeye wote wanajulikana kwa kuzishika amri za Yesu, kumjua ni sawa na kuwa ndani Yake.

Pili: Yesu Mwenyewe alitumia maneno hayo hayo – kumjua – kwamba ni sawa na kuokoka.

Basi [Mafarisayo] wakamwambia, ‘Yuko wapi Baba yako?’ Yesu akajibu, ‘Mimi hamnijui, wala Baba yangu hamumjui; kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba yangu’.” (Yohana 8:19 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

“Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu [yaani, wote walio-okoka] nawajua; nao walio wangu wanijua mimi” (Yohana 10:14 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

“Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona” (Yohana 14:7; linganisha na 1Yohana 3:6 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

“Na uzima wa milele ndiyo huu – Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” (Yohana 17:3 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Tatu: Yohana pia alitumia maneno hayo – kumjua Yeye – mahali pengine katika barua yake ya kwanza, na hapo anaweka wazi kwamba kumjua Yesu ni sawa na kuokoka.

Tazameni ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye (1Yohana 3:1 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Nne: Mantiki ya maneno haya – kumjua Yeye – katika waraka wa kwanza wa Yohana, ambao unahusu vipimo vya imani halisi, huongezea nguvu ukweli kwamba hayo maneno yanawahusu waamini wote wa kweli. Kwa mfano: Katika maelezo ya pili ya Yohana kuhusu kipimo cha maadili, anasema bila kukosea kwamba “kutenda haki” ni ushahidi kwamba mtu amezaliwa mara ya pili. Anasema hivi:

Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake. Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye (1Yohana 2:28-29. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kwa sababu hizo tunaweza kufikia uamuzi kwamba wakati Yohana anapoandika kuhusu “kumjua Yesu” hasemi juu ya kufahamiana na Yesu vizuri sana kama Wakristo waliokomaa zaidi walivyo, bali anazungumzia juu ya kuokoka. Wale wanaomjua watamtii Yeye.

Anarudia tena kipimo cha adili katika mafungu mengine, kama ifuatavyo:

Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa kama yeye alivyo mtakatifu. Kila atendaye dhambi afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao: Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu (1Yohana 3:2-10a. Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Je, iwe wazi kuliko hivyo? Kwa neema Yake, Mungu huwabadilisha wale wenye kumwamini Yesu kweli, wawe watoto watiifu. Yohana aliandika “mambo hayo” ili tuweze kujua “kwamba [tuna] uzima wa milele” (1Yohana 5:13).

Je, wewe unatii amri za Yesu? Pengine ni vizuri sasa ufanye marudio ya zile amri za Yesu katika sura ya tisa. Hakuna Mkristo hata mmoja anayezitii kikamilifu, lakini Wakristo wote wa kweli wanajulikana kwa kutii zaidi kuliko kutokutii.

Kipimo Cha Kijamii: Kuwapenda Ndugu

Maana hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. Ndugu zangu, msistaajabu ulimwengu ukiwachukia. [Je, Yohana anataka kuonyesha nini hapa kuhusu tabia ya waamini, ukilinganisha na wasioamini?] Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake (1Yohana 3:11-15. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Tunapozaliwa mara ya pili, Mungu kwa Roho Wake Mtakatifu anakuja kuishi ndani yetu. Bila shaka haachi asili Yake anapokuja hivyo. Yohana anasema Mungu ni upendo (1Yohana 4:8). Basi, wakati Mungu anapohamia, upendo unahamia pia. Paulo aliandika kwamba “Pendo la Mungu limemiminwa ndani yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, tuliyepewa” (Warumi 5:5).

Wale waliozaliwa kiroho hugundua kwamba, wanakuwa na upendo maalum sana kwa ajili ya waamini wenzao – ndugu na dada zao kiroho. Hata inakuwa kwamba kama ndugu zao wa kimwili hawajaokoka, wanajikuta wakipenda kutumia muda mwingi na ndugu zao wa kiroho. Au, wakati gari linapowapita lenye karatasi iliyobandikwa isemayo “Mimi nampenda Yesu” wanajisikia kuwapenda wale walio kwenye hilo gari. Kama wangeishi siku za mwanafilosofia Myunani aliyeitwa Celsus, wangelaumiwa naye, maana alisema hivi: “Hawa Wakristo wanapendana kabla hata hawajafahamiana!”

Huu upendo wa KiMungu unaingia ndani kuliko kukumbatiana tu na kushikana mikono baada ya ibada. Ni upendo ule ule ambao Mungu anao kwa watoto Wake, yaani, hali ya kujali na kuwa na huruma.

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli (1Yohana 3:16-18).

Upendo ambao Wakristo wa kweli wanao mmoja kwa mwenzake ni halisi mno mpaka unawatambulisha kwamba wao ni wanafunzi wa Kristo kwa wasioamini (ona Yohana 13:35), na unawatofautisha na wasioamini mbele za Mungu (ona Mathayo 25:31-46). Wale wasiowapenda ndugu zao hawampendi Mungu (ona 1Yohana 4:20).

Upendo huu unaweza kukua, na wale walio nao kweli hawauonyeshi kikamilifu mara zote. Lakini, kila mwamini wa kweli anatambua akiba ya ndani iliyoko ambayo wakati mwingine inavuja kupitia machoni, mikononi, mawazoni na katika maneno yake. Anawapenda wanafunzi wengine wa Yesu. Vipi wewe? Yohana aliandika “mambo hayo” ili tupate “kujua kwamba tunao uzima wa milele” (1Yohana 5:13).

Kipimo Cha Mafundisho

Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia … Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. … Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu (1Yohana 2:22, 23; 4:15; 5:1).

Hiki kipimo cha mafundisho mara nyingi ndicho huhesabiwa kuwa halali na wale wanaopinga kushika sheria. Kama mtu atakiri kwamba Yesu ndiye Kristo Mwana wa Mungu, anahesabiwa kwamba ameokoka, hata kama atashindwa vile vipimo vingine viwili vya Yohana. Kumbuka kwamba inawezekana mtu akakiri kwamba anamwamini Yesu kuwa ni Kristo na ni Mwana wa Mungu kwa mdomo, huku akipinga hayo hayo kwa matendo yake. Yohana anaandika mara nne katika waraka wake wa kwanza kuhusu wale ambao matendo yao yanabatilisha maneno yao.

Yeye asemaye, ‘Nimemjua’ wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake (1Yohana 2:4 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda (1Yohana 2:6 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Yeye asemaye kwamba yumo nuruni naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa (1Yohana 2:9 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mtu akisema, ‘Nampenda Mungu,’ naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona (1Yohana 4:20 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kutokana na hayo, tutakuwa wajinga kufikiri kwamba kweli tunafaulu kipimo cha Yohana cha mafundisho ikiwa tunashindwa katika vipimo vyake vya maadili na kijamii. Vyote vinalingana kwa umuhimu. Ona jinsi Yohana anavyounganisha vipimo hivyo vyote katika hitimisho anapokaribia kumaliza barua yake.

Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo [kipimo cha mafundisho] amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye [kipimo cha kijamii]. Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu na kuzishika amri zake [kipimo cha maadili] (1Yohana 5:1-2).

Yohana aliandika mambo hayo ili “mpate kujua ya kuwa mna uzima wa milele” (1Yohana 5:13). Barua ya Yohana inawajaza uhakika wale ambao wamezaliwa mara ya pili kweli. Lakini pia inawaonya wale ambao imani yao ni bandia. Kama nilivyoandika mwanzoni mwa kitabu hiki, kama ningekuwa nimedanganyika kuhusu wokovu wangu, ni afadhali kujua sasa kuliko baada ya kufa. Sasa kuna wakati wa kutubu na kumwamini Yesu – wakati huo, nitakuwa nimechelewa sana.

Kwa Wenye Dhamiri Nyepesi

Nimegundua kwamba kuna idadi ndogo ya waamini wa kweli wa Kristo ambao watashtushwa bure juu ya hali yao kiroho baada ya kusoma kitabu kama hiki. Sababu hasa ni jinsi walivyo. Tayari wanampenda Yesu sana, na wamejiwekea viwango vya juu sana katika maisha yao. Mara nyingi ni watu wenye kulenga ukamilifu katika maisha yao binafsi. Wakati mwingine ni kwa sababu walilelewa chini ya mzazi mwenye kudai ukamilifu katika mambo yote, na wao wakajiona kwamba hawakufikia kiwango. Wakati mwingine ni kwa sababu wamekaa sana katika makanisa yenye kushika sana sheria, ambayo mahubiri yao mengi yalikuwa dhambi badala ya neema, au viwango vya nje vilitumiwa kupima wokovu wa mtu – kama vile mitindo ya nywele au mavazi. Pengine walifundishwa kwamba kila walipotenda dhambi walikuwa wamepoteza wokovu wao.

Hao ni Wakristo ambao, kwa kukosa lugha nzuri, ninawaita wenye dhamiri nyepesi. Ni wepesi kujihukumu. Wakitoa zaka na kuwategemeza kifedha watoto watatu maskini, wanajisikia hatia kwa kutosaidia wanne, na wanafikia mahali pa kujiuliza kama wameokoka. Wanawatumikia wengine bila ubinafsi wowote kanisani kwao, lakini kwa sababu wanapata shida kuchukuliana na shemasi mmoja mzee, tena mwenye fujo, wanajiuliza ikiwa wameokoka kweli. Wanawashuhudia wenzao wanaofanya kazi pamoja, lakini wanajisikia hatia kwa kuwa hawajaacha kazi wakawe wamisionari huko Haiti. Ni Wakristo kiasi cha thelathini, ila sio kiasi cha mia moja (ona Marko 4:8). Si wazinzi, waasherati, walawiti, waabudu sanamu, walevi, waongo wala wezi, lakini kwa kuwa si wakamilifu, wanaogopa wanaweza kwenda jehanamu, ingawa maisha yao ni ya haki.

Waamini wa jinsi hiyo wanaweza kurekebishwa na Neno la Mungu tu. Kama wewe ni Mkristo wa aina hiyo, nakushauri usome Agano Jipya lote na uone kutokukamilika kwa wengi ambao walikombolewa. Sote tunajikwaa bado katika mambo mengi, hasa katika maneno yetu (ona Yakobo 3:2). Tunda la Roho bado lina nafasi ya kukua na kukomaa katika maisha yetu sote. Kazi ya Mungu ndani yetu bado haijakamilika. Kwa hiyo, usiruhusu Shetani apindue kile ambacho Mungu amesema, na ujihukumu. Mungu anakupenda, na mpaka sasa, aliye mkamilifu katika watoto Wake ni Yesu tu.

Lini Uamsho?

SURA YA KUMI NA MBILI

 

Nimepokea barua kutoka kwa mtu aliyenisikia nikipinga mafundisho ya wanaopinga kushika sheria kwenye redio. Anasema ni barua yake ya kwanza kuandika baada ya miaka kumi na mbili.

Alikiri kwamba yeye alikuwa shoga mtendaji. Kwa muda mrefu alikuwa akijihesabia haki kwamba, kama alikuwa anatenda matendo mema na kuamini kuhusu Yesu, alikuwa salama. Lakini akanisikia nikisema jinsi Biblia inavyosema kuhusu neema ya Mungu inayobadilisha, ipatikanayo kwa ajili ya wenye dhambi, ikiwa ni pamoja na walawiti. Alinisikia nikisoma Maandiko yasemayo kwamba hakuna mlawiti atakayeurithi ufalme wa Mungu. Baada ya kutambua kwamba imani yake iliyokufa inampeleka jehanamu, alitubu. Ameniandikia kuniambia kwamba yeye si mlawiti tena, na kwa herufi kubwa akakariri maneno machache ya 1Wakorintho 6:11, kwamba: “NA BAADHI YETU TULIKUWA HIVYO.” Ameokolewa kwa neema ya Mungu na kubadilishwa.

Kama wanaofundisha kwamba kushika sheria ni makosa wangefanikiwa, huyu mtu angedumu kuwa mlawiti mtendaji, anayekwenda jehanamu milele. Lakini – sifa kwa neema ya Mungu – aliskia kweli na kuiamini. Kama Yesu alivyoahidi katika Yohana 8:32, ukweli umemweka huru.

Je, Huru Kutokutii?

Pengine hakuna andiko ambalo limetumiwa vibaya na wale wanaopinga kushika sheria kama Yohana 8:32. Wao wanazungumzia jinsi kweli inavyotuweka huru kutokana na kile wanachokiita “utumwa wa Torati”, lakini kinachoitwa na Biblia utii kwa amri zilizo wazi kabisa za Mungu. Wakati Yesu alipozungumza kuhusu kweli kutuweka huru, alikuwa anazungumza juu ya uhuru kutoka dhambini.

Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, ‘Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.’ Wakamjibu, ‘Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wowote; nawe wasemaje Mtawekwa huru?’ Yesu akawajibu, ‘Amin amin nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli (Yohana 8:31-36. Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Huu ndiyo ujumbe wa neema ya Mungu inayobadilisha. Hiyo ndiyo Injili. Yesu husamehe na kuwaweka wamwaminio huru kutoka dhambi. Wale wanaomwamini Yeye kweli watadumu – wataishi – katika Neno Lake, wakijithibitisha kwamba ni wanafunzi Wake.

Uamsho Wa Kishetani

Sasa hivi ni wakati wa giza. Jamii yetu ni kama gari moshi la mizigo ambalo halina breki, na linaongeza mwendo. Litaendelea kwa muda gani kabla ya kuondoka kwenye reli? Lakini, tunawezaje kulia kuhusu kuporomoka kwa hali ya kiroho ya taifa letu na wakati huo huo tunatoa injili ambayo haina nguvu zozote za kubadilisha maisha – injili ambayo si kitu zaidi ya nafasi ya watu kutenda dhambi? Tunawezaje kutazamia uamsho wakati neema ya Mungu inageuzwa kuwa kibali cha ufisadi?

Muda wote ambao lengo letu litakuwa kujaza viti kwa jina la “kukuza kanisa” badala ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi, hautakuwepo uamsho wa kweli. Tutakapoendelea kuwaona watu kwamba “hawaendi kanisani” badala ya kuwaona kwamba hawajaokoka, hautakuwepo uamsho wa kweli. Muda wote ambapo wachungaji na wainjilisti wanajali zaidi kuwapendeza watu badala ya kumpendeza Mungu, uamsho wa kweli hautakuja. Uamsho wa kweli hauwezi kuwepo mpaka kanisa litakaporudisha ile Injili ya Biblia, na kuwa na sifa ya utakatifu mpaka liwe tofauti na dunia. Kabla ya hapo, uamsho wa pekee utakuwa ule unaoendelea kwa sasa wa Kishetani, wenye kuchochewa na neema bandia, imani bandia na wokovu bandia. Wakitumia bango la uhuru kiroho, wainjilisti wake (Shetani) wataendelea kumwaga uongo wake kwa maandishi, kwenye redio na televisheni za Kikristo, na kutoka kwenye mimbari makanisani. “Nendeni mkatende dhambi. Hamtakufa.”

Kweli, wakati ni wa giza. Makundi ya waalimu maarufu wanatangaza kwamba kama mtu anamwamini Yesu hata kwa nukta kumi tu maishani mwake, kisha aiache imani na kurudia maisha ya kutenda dhambi, ameokoka, na ni salama milele. Kumbuka kwamba mtu huyo tunayemfikiri tu anaweza kuwa kahaba anayeendelea na ukahaba wake, au mbakaji mpaka wakati wa kifo chake. Bado atakwenda mbinguni. Atakachopoteza ni thawabu fulani huko mbinguni ambazo angeweza kupata kama angekuwa Mkristo bora zaidi kidogo! Je, huko sio kugeuza neema ya Mungu kuwa ufisadi? Je, mahubiri aina hiyo kweli yataleta uamsho? Lakini, Biblia bado inasema hivi:

Ni neno la kuaminiwa: Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia. Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye. Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi. Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa maana hawezi kujikana mwenyewe (2Timo. 2:11-13. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Je, mstari huu unafasiriwaje na waalimu wa kisasa wa neema bandia? Wakipuuza au kupindua mistari ile mitatu ya kwanza, wao wanakaza kwamba mstari wa nne unathibitisha hoja yao. Wanasema hivi: “Hata kama sisi hatuamini, tukiacha imani yetu, yeye hudumu kuwa mwaminifu wa kutuokoa.”

Lakini, hiyo ndiyo maana yake? Hapana kamwe!

2Timotheo 2:11-13 Inafundisha Nini?

Kwanza: Paulo anasema, “Kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia.” Kuishi kwetu pamoja Naye kunategemeana na kufa kwetu pamoja Naye. Maandiko yanafundisha kwamba wote wanaomwamini Yesu kweli wamekufa na kufanywa hai ndani ya Kristo. Huko ndiko kuzaliwa mara ya pili, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Ni badiliko kubwa sana.

Pili: Paulo anasema, “Tukistahimili, tutamiliki pamoja naye.” Hapa si kwamba anatoa ahadi ya thawabu maalum ya kutawala wakati ujao kwa kundi maalum la Wakristo watakaostahimili. Anaahidi kitu kinachomngojea kila mwamini wa kweli ambaye imani yake itastahimili. Maandiko yanafundisha kwamba si kundi maalum la Wakristo litakalotawala pamoja na Yesu. Wote walionunuliwa kwa damu Yake watatawala pamoja Naye.

Nao waimba wimbo mpya wakisema, ‘Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi’ (Ufunuo 5:9-10. Maneno mepesi kutilia mkazo. Pia ona 20:6; 22:3-5).

Waamini wale watakaostahimili katika imani ya kweli wanayo ahadi ya kutawala pamoja na Yesu. Ni lazima tudumu katika imani ili tuokoke mwishoni, na kama tutafanya hivyo, tutatawala pamoja na Yesu.

Tatu: Paulo anatoa onyo kuhusu kutostahimili. “Tukimkana, yeye naye atatukana sisi.” Hayo ni maneno yaliyokaririwa kutoka kwa Bwana Yesu Mwenyewe. Alisema hivi:

“Basi kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni “ (Mathayo 10:32-33. Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Hapo Yesu – bila ya kutafuna maneno – aliahidi kwamba kama tukimkana, Naye atatukana. Ni onyo kwa yeyote anayefikiria kuacha imani yake, au kutostahimili kwa sababu ya mawazo ya watu au watakachomfanyia. Je, watu ambao Yesu atawakana mbele za Baba Yake wataruhusiwa kuingia mbinguni? Je, tukimkana Yesu kwa kusema, “Simjui” mbele ya watu, na Yeye atukane mbele za Baba akisema, “Simjui”, tutaokoka? Jibu unalo wewe.

Mwisho Paulo anasema, “Tusipomwamini, Yeye anadumu kuwa wa kuaminika; maana hawezi kujikana mwenyewe.” Ni maendeleo ya kile alichosema kuhusu kumkana Yesu. Hata ingawa tunaweza kushindwa kutimiza ahadi yetu ya kumfuata, Yesu atatimiza ahadi Zake zote kila wakati. Aliahidi kutukana ikiwa tutamkana, Naye atafanya hivyo. (Tukirejea kwa toba na imani, atatunza ahadi Yake ya kutupokea.)

Ona kwamba katika tamko la nne Paulo hakusema hivi: “Tusipoamini na tukimkana, Yeye atadumu kuwa mwaminifu, na hatatukana.” Hiyo ingekuwa kinyume kabisa na alichokisema katika tamko la tatu!

Hapana. Mungu daima ni mwaminifu japo watu sio. Yeye kila mara anatimiza ahadi Zake pamoja na hukumu Zake. Hebu fikiri wanavyosema Musa na Yoshua kuhusu uaminifu wa Mungu.

Basi jueni ya kuwa BWANA Mungu wenu ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake hata vizazi elfu; naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake (Kumbu. 7:9-10. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, BWANA Mungu wenu aliyowaahidia ninyi, kadhalika BWANA atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, BWANA Mungu wenu aliyowapa (Yoshua 23:15 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Hayo yakiwa bado akilini mwetu, hebu tuone jinsi ambavyo mmoja katika waalimu maarufu sana wanaopinga kushika sheria, ambaye jina lake linajulikana sana, anavyotafsiri 2Timotheo 2:11-13. Anasema hivi:

Kama ambavyo walio waaminifu watakavyotambuliwa na kupokelewa na Baba, ndivyo na wasio waaminifu watakavyokosa kutambuliwa … Mwamini asiye mwaminifu hatapata nafasi maalum katika ufalme wa Kristo kama wale watakaobahatika kuruhusiwa kutawala pamoja naye. … Maana ya mtume ni dhahiri, kwamba: Hata kama mwamini atafanyika asiyeamini – kwa hali yoyote ile – wokovu wake hauko hatarini. Kristo atadumu kuwa mwaminifu (Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Wakati kanisa – tena kwa furaha – linapomeza mafundisho yenye kubadilisha kabisa maana ya Maandiko, kuna haja ya kuuliza ni kwa nini hakuna uamsho? Ujumbe mtakatifu wa Mungu umehaririwa, umetolewa kila sababu ya mtu yeyote kutubu dhambi na kumfuata Yesu Kristo. Watu wasiomwamini Yesu sasa wanaweza kufika mbinguni, hakika kabisa. Mtu anaweza kuwa asiyeamini kwamba kuna Mungu, au Mbuda, au Mwislamu au mwenye kumwabudu Shetani na bado aende mbinguni, mradi ametamka kwamba anamwamini Yesu kwa nukta chache tu katika maisha yake. Na uongo huu unatangazwa na waalimu walio maarufu katika imani ya kiinjili katika duniani.

Sasa?

Kama ulikuwa huelewi Injili ya kweli kabla ya kuanza kusoma kitabu hiki, bila shaka sana unaielewa. Labda uamsho umeanza maishani mwako. Kwani, uamsho mkubwa ni kitu gani kama siyo watu wengi binafsi wakihuishwa? Unaweza na unatakiwa kuwaambia wengine kile unachojua mpaka sasa. Sawa na mimi, wewe sasa una wajibu mtakatifu wa kueneza ukweli, bila kujali gharama. Ujumbe wetu ni ule ule uliotangazwa na Yesu, na Yuda, na Petro, na Paulo, na Yakobo na Yohana, na mamilioni ya waamini wa kweli waliotutangulia. Tusije tukaionea “haya injili, ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16).

Je, utakuwepo uamsho wa kweli? Ndiyo – katika maisha ya kila atakayesikia na kujali Injili ya kweli. Wale walioamshwa kweli kweli wataomba na kujitahidi ili wengine waweze kushiriki furaha yao. Wazo hilo likiwa akilini mwako, naomba nimalizie kwa mfano ambao Bwana alinipa, unaonijaza matumaini makubwa sana ………

Mfano Wa Uamsho …

Nilipokuwa nafunga na kuomba kuhusu hitaji la uamsho na kazi ya Roho Mtakatifu, nilipokea ufunuo ulionisaidia kuelewa ni kitu gani kinachotokea na kitakachotokea kwa kanisa. Hayakuwa maono niliyoona kwa macho yangu, bali ufunuo “niliouona” katika moyo wangu. Naomba niseme kwamba mimi si mtu “wa mafunuo,” na hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kitu kama hicho kunitokea. Hebu nieleze nilichoona.

KWANZA: Niliona makundi ya watu. Mengine yalikuwa makubwa sana, mengine ya wastani, mengine madogo sana. Makundi yale makubwa yalikuwa na watu maelfu. Makundi yale madogo sana yalikuwa na watu kichele – wachache tu. Watu wa kila kundi walisogeleana na kujikunyata pamoja ili wapate joto, maana kulikuwa baridi sana sana. Wote walikuwa wanatetemeka, na mtu aliposema kitu, ungeweza kuona pumzi yake ikitokea. Tena, wengi katika makundi hayo walikuwa wachafu. Kuna waliokuwa wachafu kuliko wengine, kana kwamba walikuwa wafanyakazi katika machimbo ya makaa ya mawe, wamefunikwa na majivu na masizi toka kichwani hadi vidoleni. Hao walikuwa wananuka pia, kama takataka. Wengine hawakuwa wachafu hivyo, lakini wengi walihitaji kusafishwa.

Watu wote hao walikuwa wamesimama chini ya bwawa kubwa sana lililokuwa na maji mengi mno. Lilikuwa refu sana – futi mia nyingi kwenda juu – na lilikuwa pana, kiasi cha upeo wa macho kwenda pande zote. Maji yaliyokuwemo ndani yake yalikuwa mengi sana.

Nilipotazama kwa karibu zaidi, niliona kwamba lilikuwa limejengwa kwa kutumia matofali. Kuna maneno yaliyokuwa yameandikwa kwenye kila tofali, nami nilipoanza kuyasoma, niligundua kwamba yote yanafanana, maana kilichoandikwa kilikuwa dhambi fulani. Kwa mfano: Tofali moja lilikuwa limeandikwa “Msengenyaji”, na lingine, “Mwenye Tamaa”. Pia, chini ya kila dhambi lilikuwepo jina la mtu. Kwa mfano: Tofali lililoandikwa “Mwongo” lilikuwa na jina la mtu chini yake: “Sauli”. Yalikuwepo matofali mengi yaliyokuwa yameandikwa dhambi ile ile moja, na majina mengi ya watu yalikuwa yameandikwa kwenye tofali zaidi ya moja.

Nikawatazama tena wale watu wengi – wachafu, wanatetemeka kwa baridi. Karibu wote walikuwa wamesimama, ila mmoja-mmoja katika kundi angepiga magoti, au angeanguka kifudifudi na kuanza kuomboleza na kutubu dhambi zake na kumwomba Mungu amsafishe. Kila mtu anapofanya hivyo, tofali moja lingechomoka kutoka mahali pake kwa nguvu ya maji, na likichomoka hivyo, linapasuka-pasuka na kuwa vumbi, kisha linatoweka. Kisha, maji yangetokea hapo lilipotoka tofali na kuanza kuelekea kwa huyo aliyepiga magoti, na kumsafisha uchafu wake wote. Wakati mwingine matofali zaidi ya moja yangechomoka kutoka kwenye ukuta huo – ama yote kwa pamoja au mojamoja kwa kitambo fulani – mradi yule mtu aliendelea kupiga magoti na kuomba. Maji yote yaliyotokea kwenye nafasi hizo yangemwangukia kwa nguvu sana yule mtu mmoja aliyekuwa amepiga magoti akiomba, na badiliko katika jinsi alivyokuwa anaonekana lilikuwa kubwa. Baadhi ya waliokuwa wachafu zaidi wakawa ndiyo wasafi kuliko wengine, katika kipindi kifupi tu.

Pia nikaona, yale maji yaliyotoka kwenye lile bwawa yalikuwa na joto. Yalipowapiga wale waliopiga magoti, si tu kwamba yaliwasafisha bali pia yaliwapa joto kabisa. Wangecheka kwa furaha na kuimba wakati wakisafishwa.

Wale wengine waliokuwa wamesimama na kuwatazama waliopiga magoti walikuwa na maitikio tofauti. Mara nyingi, wale waliokuwa karibu na mwenye kupiga magoti walikuwa wanasogea, wasitake kulowa. Wakati mwingine, kundi zima lingerudi nyuma mbali, na yule aliyepiga magoti angebaki peke yake katika maji yake yanayomwagika.

Ila pia, mara kadhaa wengine katika waliosimama karibu na aliyepiga magoti wangepiga magoti hata wao, wakitubu dhambi zao. Hapo tena matofali yangechomoka kutoka kwenye ule ukuta na maji yangewamwagikia, yakiwasafisha na kuwapa joto.

Wakati mwingine idadi kubwa tu ya waliokuwa wamesimama katika kundi moja mmoja baada ya mwingine wangeanza kupiga magoti au kuinama na kuanza kuomboleza kwa ajili ya dhambi zao, na nguvu ya yale maji mengi yaliyowafikia zingekuwa kubwa na nyingi, na kuleta baraka kubwa sana, upako wenye nguvu na karama nyingi. Lakini, sikuona kundi lolote ambapo kila mmoja aliyekuwemo alipiga magoti. Mara nyingi niliona wale waliokuwa wamesimama katika makundi ambayo wengi walipiga magoti wakiondoka na kujiunga na kundi lingine ambalo wengi walikuwa bado wamesimama. Pia, wakati mwingine niliona mtu akipiga magoti kwa sababu wengine wengi walikuwa wamepiga magoti. Katika hali hiyo, hakuna tofali lililochomoka, hakuna maji yaliyomwagika kwake, na alibakia mchafu na baridi.

Niliona vitu vingine viwili: Mara kwa mara mmoja wa waliokuwa wamesimama alikuwa anatazama lile bwawa na kuona tofali lenye jina lake. Kwa sababu ya aibu, alikuwa anapanda ukuta ule na kujaribu kulichomoa kwa mikono yake. Hakuna yeyote aliyejaribu kufanya hivyo aliyefanikiwa, kwa sababu isingewezekana. Pia, mara kwa mara niliona mtu aliyekuwa amepiga magoti akisimama tena. Alipofanya hivyo, alijikuta amekuwa mchafu tena kwa njia fulani, na nguvu ya maji kumwangukia ikawa imepungua. Na kama angeanza kunyoosha kidole kwa wale ambao hawakupiga magoti, akiwalaumu kwa kinywa chake kwa maneno ya kiburi, maji yangekoma kumwagika juu yake, na akawa mchafu tena. Lakini, wengi katika waliokuwa wamepiga magoti wangesema kwa upendo na huruma nyingi sana na wale waliosimama wakiwazunguka, na kuwaambia, “Ni pazuri sana hapa kwenye maji haya yenye joto na kusafisha! Unaweza kuoshwa uchafu wako! Si uje ujiunge nami?”

Hebu nikwambie baadhi ya dhambi zilizokuwa zimeandikwa kwenye matofali hayo. Moja, lililokuwa na jina langu, lilikuwa limeandikwa hivi: “Mwenye Kuwaogopa Wanadamu.” Nilipoliona nilikiri mara moja hatia yangu mbele za Mungu na kuomba msamaha Wake na neema kwamba nisimwogope yeyote isipokuwa Mungu.

Kama mchungaji, nilionyeshwa matofali mengi tu ya watu katika kanisa langu. Yalikuwepo mengi ya dhambi zile zile. Mengine yalisema “Rafiki Na Dunia.” Mengi yalikuwa yameandikwa, “Vuguvugu”. Mengine, “Mpenda Kuhukumu Wengine.” Mengine: “Mwabudu sanamu,” ambayo maana yake ni kwamba unafanya vitu vingine maishani mwako kuwa vya maana kuliko Mungu. Watu wengi kanisani wanasisimka zaidi juu ya mambo yao ya ziada na starehe zao kuliko kwa ajili ya Mungu.

Mengine yalisema “Uchafu Katika Mahusiano Kimwili” ambao si uasherati tu, bali pia kuwa na mawazo machafu. Mengine yalisema “Hujistarehesha kwa kutazama watu wakifanya mambo machafu kwenye televisheni.” Lingine lilisema, “Anatazama Ngono kwenye internet”. Lingine lilikuwa limeandikwa “Hutafakari Matendo ya Ulawiti.” Lingine: “Kijana Anayejihusisha na Mahusiano Kimwili”.

Kwenye matofali mengine kuliandikwa hivi: “Uchungu juu ya mwingine,” “Anamnyanyasa Mke Wake,” na “Huwasema Ndugu.” Yalikuwepo yaliyosema “Mpenda Fedha,” “Mpenda Starehe” na “Anayejijali Mwenyewe.” Lilikuwepo linalosema “Hulipwa Bila Risiti Ili Akwepe Kodi,” “Msimamizi Mfujaji,” “Hutumia Fedha za Mungu Kutegemeza Mambo Ambayo Mungu Hataki” na “Asiyejali Maskini.” Mengi yalisema hivi: “Hata Zaka Hatoi” na yalikuwepo matofali mengi kuzunguka hayo yenye dhambi zenye kutetea dhambi hiyo.

Yalikuwepo yaliyoandikwa “Asiye Na Staha”, “Anayeamini Yuko Sawa Sikuzote”, na “Asiyemtii Mume Wake.” Pia niliona mengi yaliyosema, “Hajali Kuhusu Wale Ambao Hawajasikia Injili.”

Mengine yalisema, “Msengenyaji,” “Mfitini,” “Mkosoaji”, “Atumiaye lugha ya kukwaza”, na “Dini Isiyofaa – Hauzuii Ulimi Wake.” Tofali moja lilisema hivi: “Hawategemezi Watoto Wake wa Ndoa ya Kwanza.” Mengine yalisema, “Hawaheshimu Wazazi,” “Si mwaminifu kwa ahadi” na “Husikiliza muziki unaosifu mambo ambayo Mungu anachukia.”

Yalikuwepo yanayosema “Amejaa Kutokuamini,” “Tabia Mbaya na Kutawaliwa,” na “Mwenye Kujitosheleza.” Pia kulikuwa na “Kutokuomba,” “Hukosa Ibada kanisani,” na “Asiyetaka Kusoma Neno la Mungu.” Matofali mengi yalisema, “Hawafundishi watoto katika kicho cha Mungu.”

Yapo na mengine mengi ambayo sikuyataja, lakini yote yanapatikana katika Biblia – hiyo hiyo ambayo sote tunakiri kwamba tunaiamini kuwa ni Neno la Mungu. Hata matofali mengine yalikuwa yameandikwa hivi: “Hubadili Maandiko Kuyafanya Yaseme Kisichokuwepo,” na “Hutafsiri Amri Ili Zilingane na Maisha Yake.”

Sementi iliyokuwa imeshikilia yale matofali nayo ilikuwa imeandikwa maneno, kuonyesha dhambi nne zilizoshikilia zile nyingine zote. Hizo ni “Kiburi,” “Unafiki,” “Kutompenda Mungu au Kumpenda Kidogo Tu,” na “Dhambi Za Wachungaji.” Kabla ya hizo dhambi nyingine kuondolewa, hizo lazima zidhoofishwe kwanza. Kiburi kinatuzuia kukiri dhambi zetu. Unafiki – kutenda kwa njia moja kanisani na kwa nyingine mahali pengine – lazima utubiwe. Hizo zote ni ishara ya dhambi moja kubwa – “Kutompenda Mungu au Kumpenda Kidogo Tu” – maana, tungempenda kwa moyo wote, akili zote, nafsi yote na nguvu zote, tungemtumikia na kumtii kwa bidii sana. Yesu alisema, “Mkinipenda mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15). Mwisho: Kama viongozi kanisani watakuwa mfano mbaya, wafuasi wao wana njia ya kujitetea kuendelea katika dhambi zao.

Turudi kwenye yale makundi ya watu. Nilipotazama, ilitokea mara moja moja kwamba mtu aliyekuwa amesimama angenyoosha kidole chake kwa kundi lililo karibu naye, ambamo watu walikuwa wanacheka na kuimba, huku wamepiga magoti chini ya maji yaliyokuwa yanawamwagikia, na kusema hivi: “Hayo maji hayawezi kutoka kwa Mungu, maana mafundisho yao si sawa katika maeneo fulani.” Lakini Bwana alinikumbusha kwamba Yeye hakusema ni wale tu wenye mafundisho safi ndiyo watakaomwona, bali wale wenye moyo safi (Mathayo 5:8). Yesu hakusema kwamba tutawatambua kwa mafundisho yao bali kwa matunda yao (Mathayo 7:20). Alisema kwamba alama ya wanafunzi Wake wa kweli si mafundisho makamilifu bali upendo kati yao (Yohana 13:35). Kwa kuwa mafundisho ya kundi fulani yana makosa katika maeneo fulani ambayo hata si muhimu haimaanishi kwamba Mungu hatawamwagia Roho Wake ikiwa watajinyenyekeza na kuanza kuwa na “njaa na kiu ya haki” (Mathayo 5:6). Baadhi ya matofali kwenye lile bwawa yalikuwa yameandikwa hivi: “Kujisifia Maarifa,” “Kujivunia Mafundisho,” na “Uaminifu kwa Dhehebu Zaidi ya Upendo kwa Mwili wa Kristo.”

Muda ulipoendelea kupita, wengi zaidi katika waliokuwa wamesimama walianza kupiga magoti, wakiomboleza na kuomba msamaha kwa dhambi zao na kutubu. Matofali yakachomoka kutoka kwenye lile bwawa mfano wa mahindi ya kuchoma, na maji zaidi yakamwagika kwa mlio wa nguvu na kishindo, mpaka pakawa kama Bwawa la Kidatu (ila, zaidi sana sana). Waliokuwa wamepiga magoti wakainua mikono yao, wakacheka, wakaimba na kuomba katika kitu ambacho kilikuja kuwa mto mkubwa uliobubujika hadi maeneo mengi makavu duniani. Mwishowe ukawa gharika mpaka wale waliokuwa wamepiga magoti ndani yake walisombwa na hayo maji, huku wakifurahi na kuimba nyimbo za sifa kwa Mungu wao.

Mwishoni maji yale yakaacha kutoka, maana lile bwawa lilikauka. Waliokuwa bado wamesimama walitazamana kwa majivuno ya kuridhika. Bado yale matofali yenye majina yao yalikuwepo, yameshikiliwa hapo hewani kwa kiburi cha mwanadamu tu. Mara – bila hata taarifa au ilani – kila tofali lililobaki kwenye ule ukuta lilianza kuanguka, likiungana na mengine yaliyokuwa na jina hilo hilo. Kwa hofu kubwa, waliokuwa wamesimama waliona matofali lundo yakiwaangukia kwa usahihi, kwanza yakiwaangusha chini, kisha yakiwaua na kuwaponda, mpaka kilichobakia kikawa ni malundo ya matofali tu. Nikakumbusha maneno aliyosema Yesu, kwamba “Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” (Luka 18:14). Vipi – wewe ni yupi kati ya hao?

Kushindana Na Dhambi

SURA YA TISA

“Dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde” (Mwanzo 4:7).

KAMA tulivyoona katika sura iliyopita, utakaso wetu ni juhudi za pamoja kati ya Mungu na sisi wenyewe. Tunaendelea kuwa kama Yesu zaidi tunapozidisha ushirikiano na Baba. Yeye anatupa uwezo na hamasa ya kuwa watakatifu. “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa” (2Petro 1:3 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Yeye hutupa sisi asili mpya na kutuongoza kwa Roho Wake anayekaa ndani yetu. Lakini, anatuachia na sisi kitu cha kufanya. Bado tuna hiari yetu. Ni lazima tumfuate Roho anayekaa ndani yetu, na hili linafanywa na kila Mkristo wa kweli kwa kiwango fulani. Vinginevyo anajionyesha kuwa ni mwamini bandia (ona Warumi 8:5-14).

Vile vile ni wajibu wetu kufanya upya nia zetu kwa Neno la Mungu, maana lazima tujue mapenzi Yake kabla ya kuyatenda. Hata katika hilo pia Mungu hutusaidia kwa njia ya huduma ya kufundisha ya Roho Mtakatifu na kwa kupitia wanadamu waliotiwa mafuta kuwa waalimu. Nia zetu zinapofanywa upya na kweli Yake, tunabadilishwa (ona Yohana 8:31-36; Warumi 12:2). Kisha, tuna wajibu wa kutokuwa wasikilizaji tu wa neno bali watendaji pia (Yakobo 1:22).

Lazima mlingano huo utunzwe. Japo Maandiko yanafundisha juu ya wajibu wa Mungu na wa binadamu, watu wengi hukazia kimoja na kuacha kingine. Yamekuwepo makundi mawili kihistoria – wanaojaribu kuwa watakatifu kwa nguvu zao wenyewe, na wanaopinga juhudi zozote za kibinadamu kwa habari ya utakatifu, wakimwachia Mungu kila kitu. Pande zote mbili zina orodha ndefu ya maandiko, na kama wangetazama orodha zao wote wangetambua kwamba wote wako sawa na wote wamekosea. Ukweli uko katikati, mahali ambapo orodha zote mbili zinaheshimiwa. Hakuna mstari mmoja unaoeleza vizuri mlingano huo kuliko Wafilipi 2:12 na 13. Unasema hivi:

Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema (Maneno mepesi kutilia mkazo).

Tunda ambalo Roho huzaa ndani yetu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi, lakini, matunda hayo yataonekana maishani mwetu kwa ushirikiano wetu tu. Ni lazima tufanye kitu fulani kwa sababu, kulingana na Maandiko, zipo nguvu kama tatu hivi zinazopinga matunda hayo.

(1) Mungu ameturuhusu sisi kubakia “duniani”, dunia ambayo inatujaribu tusiwe na upendo au kupendeka, tuwe na huzuni, tuwe na wasiwasi, tusivumilie, tusiwe wema, tuwe waovu, tusiwe waaminifu, tuwe wakali na wenye kujitosheleza.

(2) Ingawa Mungu ametujaza kwa Roho Wake, na kutupa asili mpya na kuvunja nguvu za dhambi juu yetu, Yeye pia ameruhusu mabaki ya asili yetu ya kale ya dhambi kubakia ndani yetu. Kitu hicho Paulo anakiita “mwili”.

(3) Ingawa tumekombolewa kutoka ufalme wa Shetani na sisi si watoto wake tena kiroho, tunajikuta kama wale Wakristo wa zamani tukiwa katika uwanja mkubwa uliojaa simba wanaounguruma, wenye lengo la kutumeza (ona 1Petro 5:8). Shetani na mapepo yake hutusumbua na kutunyanyasa na kutujaribu ili tufanye yale ambayo Mungu amekataza.

Hao watatu ndiyo adui zetu: dunia, mwili na shetani.

Kwa Nini Mungu Ametuacha Kwenye Eneo La Adui?

Kama Mungu anatamani tuwe watakatifu, mbona amewaruhusu adui hawa kuishi miongoni mwetu? Kwani wanatimiza kusudi gani la kimungu?

Adui zetu wanaruhusiwa kukaa miongoni mwetu ili Mungu atupime, kama alivyoruhusu mataifa maovu yabakie katika ardhi ya Israeli baada ya kufa kwa Yoshua (ona Waamuzi 2:20 hadi 3:1). Wao wanapima upendo wetu, utii wetu – yaani, imani yetu. Imani inaweza kupimwa wakati kunapokuwepo uwezekano wa kutokuamini. Upendo unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa chuki. Utii unaweza kupimwa wakati kuna uwezekano wa kutokutii.

Mungu aliwaambia hivi Waisraeli wa zamani:

Kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, ‘Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;’ wewe usiyasikilize maneno ya nabii yule au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA Mungu wenu yuawajaribu, apate kujua kwamba mnampenda BWANA Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata BWANA Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye (Kumbu. 13:1-4).

Cha ajabu ni kwamba Mungu aliwapima watu Wake kwa kutumia nabii wa uongo! Lakini je! Hana maarifa yote pamoja na uwezo wa kujua mambo kabla? Mbona kuwe na haja ya kupimwa tena?

Sababu ni hii: Ili Mungu ajue matokeo ya kipimo cha mtu mwenye hiari, lazima huyo apimwe wakati fulani. Kinachoweza kujulikana kabla ni kitu kinachoweza kujulikana wakati fulani. Basi, majaribu yetu na dhiki na vipimo, ambavyo vina mipaka katika muda fulani, hutekeleza kusudi katika mpango wa Yule aishiye nje ya majira na nyakati. Hutoa njia ambayo kwayo imani yetu inathibitishwa kuwa ya kweli. Petro aliwaandikia hivi Wakristo waliokuwa wanapitia mambo magumu:

Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo … Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe. (1Petro 1:6-7; 4:12-13. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Hata kama hakuna sababu nyingine, tunapaswa kufurahi katika mateso kwa sababu yanaturuhusu nafasi ya kuonyesha imani yetu thabiti. Imani yenye kuokoa hudumu, lakini imani inaweza kuvumilia tu wakati kuna upinzani na majaribu ili isivumilie.

Wajibu Wetu Ni Nini?

Siku hizi wengi wanaojiita Wakristo wanamwachia Mungu wajibu wao ambao wamepewa na Biblia. Hii ni kwa sababu mafundisho ya kisasa ya kiinjili yamechafuliwa sana na mawazo ya kupinga kushika sheria, yenye kupotosha neema ya Mungu na kubatilisha wajibu wa mwanadamu. Kwa sababu wamedanganyika na mafundisho ya uongo kuhusu neema, ukiwatajia tu juhudi za kibinadamu unaonekana umekufuru, na huku wakidai kwamba wanatetea utukufu wa Mungu, wanasema fundisho lolote kuhusu utakatifu ni kuwafanya watu waishi kwa kufuata sheria. Matendo ni neno chafu ambalo halifai katika msamiati wa Kikristo. Hakika hatutaki liwepo wazo lolote kwamba sisi inatupasa kutenda chochote sasa kwa kuwa kazi ya Kristo imemalizika. Hiyo ni sawa na kuongezea matendo kwenye wokovu wetu (na Mungu apishe mbali!).

Kwa matazamio ya kujaribu kutibu shida hiyo ambayo haitokani na Maandiko, nimeorodhesha mambo ambayo sehemu kubwa ya Agano Jipya inasema tunapaswa kufanya. Sehemu muhimu ya wajibu wa mwanadamu katika mpango wa utakaso inaeleweka kirahisi kutokana na mistari mingi yenye maagizo na mashauri. Tunapoisoma, hatuwezi kuwa na mashaka tena kwamba Wakristo ni watu wenye hiari wanaoweza kuamua kuwa watakatifu. Pia, ule udanganyifu kwamba Mungu anaibiwa utukufu wakati tunapoongeza juudi zetu kwa habari ya utakaso unadhihirishwa wazi. Ni hivi: Mungu anawatazamia wale walio na Roho Wake Mtakatifu kufanya mambo fulani kwa nguvu za Roho. Kwa kifupi ni kwamba, sisi tunapaswa kushindana na dhambi katika hali zake zote. Sisi lazima tutafute utakatifu, ambao “hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao” (Webrania 12:14).

Orodha ifuatayo inafunua matazamio ya Mungu juu ya tabia yetu. Orodha imetolewa katika Injili zote nne na kitabu cha Warumi. Kama Agano Jipya linasema tabia fulani ni mbaya au ni kosa au ni dhambi, basi Mungu bila shaka anawawajibisha watu kwa tabia hiyo, kuonyesha kwamba wajibu wa mwanadamu ni kitu kinachohusika katika tabia hiyo mbaya.

Japo unaweza kujaribiwa kuiruka orodha hii ifuatayo, ningekushauri uisome pole pole kwa manufaa yako mwenyewe. Inaweza kukugusa kwa njia itakayobadili maisha yako.

Je, Mungu anatutazamia tufanye nini? Ifuatayo ni orodha. Ni dhahiri kwamba hakuna chochote katika haya yafuatayo kitakachotokea maishani mwetu bila sisi kufanya Mungu anavyosema.

Mungu anatutazamia:

Tusimjaribu (Mathayo 4:7).

Tumwabudu Bwana Mungu wetu na kumtumikia Yeye tu (Mathayo 4:10).

Tutubu ili tuokolewe (Mathayo 4:17).

Tufurahi na kushangilia wakati tunapoteswa (Mathayo 5:12).

Tuache nuru yetu iangaze mbele za watu ili wayaone matendo yetu mema (Mathayo 5:16).

Tushike amri za Mungu na kuzifundisha, hata zile zilizo ndogo kabisa (Mathayo 5:19).

Tusiue, kumchukia wala kumdhuru mtu yeyote kwa njia yoyote ile (Mathayo 5:21-22).

Tujishughulishe kupatana na wale ambao tumewakosea (Mathayo 5:24-25).

Tusizini wala kuwa na tamaa mbaya (Mathayo 5:27-28).

Tuondoe chochote kinachotufanya tuangukie dhambini (Mathayo 5:29-30).

Tusivunje ndoa isipokuwa kwa uasherati (Mathayo 5:32).

Tusiape na tusidanganye. Kila mara tutimize maneno yetu (Mathayo 5:33-37).

Tusijilipize kisasi bali tuwavumilie sana wengine, hata kuwatendea mema wanaotutendea mabaya (Mathayo 5:38-42).

Tuwapende adui zetu na kuwaombea wanaotutesa (Mathayo 5:44-47).

Tujaribu kuwa wakamilifu (Mathayo 5:48).

Tusifanye mema ili tupokee sifa za watu (Mathayo 6:1).

Tutoe sadaka (Mathayo 6:2-4).

Tuombe (Mathayo 6:5-6).

Tusirudie-rudie maneno yasiyo na maana tunapoomba (Mathayo 6:7).

Tuombe kwa kufuata mfano wa “Sala ya Bwana” (Mathayo 6:9-13).

Tuwasamehe wengine (Mathayo 6:14).

Tufunge, yaani tusile chakula (Mathayo 6:16).

Tusijiwekee hazina duniani, bali mbinguni (Mathayo 6:19-21).

Tumtumikie Mungu, siyo fedha (Mathayo 6:24).

Tusiwe na wasiwasi kuhusu mahitaji yetu (Mathayo 6:25-32).

Tutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki Yake (Mathayo 6:33).

Tusiwahukumu wengine (Mathayo 7:1-5).

Tusiwape mbwa kilicho kitakatifu (7:6).

Tuombe, tutafute, tubishe (Mathayo 7:7-11).

Tuwatendee wengine tunavyotaka kutendewa (Mathayo 7:12).

Tuingie kwa kupitia mlango mwembamba (Mathayo 7:13).

Tujihadhari na manabii wa uongo (Mathayo 7:15-20).

Tufanye aliyosema Yesu au tuangamie (Mathayo 7:24-27).

Tumwombe Bwana awatume watenda kazi katika shamba Lake (Mathayo 9:38).

Tumkiri Yesu mbele ya wengine. Tusimkane (Mathayo 10:32-33).

Tumpende Yesu kuliko watu walio karibu nasi (Mathayo 10:37).

Tujitwike msalaba na kumfuata Yesu (Mathayo 10:38).

Tupoteze maisha yetu kwa ajili ya Yesu (Mathayo 10:39).

Tujitie nira ya Yesu (Mathayo 11:28-30).

Tuwe “pamoja” na Yesu kukusanya (Mathayo 12:30).

Tusimkufuru Roho Mtakatifu (Mathayo 12:31).

Tufanye mapenzi ya Baba (Mathayo 12:50).

Tuwaheshimu wazazi wetu (Mathayo 15:4-6).

Tusinajisike kwa mawazo machafu, mauaji, uasherati, uzinzi, wizi, udanganyifu na hila (Mathayo 15:19-20).

Tujikane (Mathayo 16:24).

Tuongoke na kuwa kama watoto. Tujinyenyekeze (Mathayo 18:3-4).

Tusimfanye mtoto yeyote anayemwamini Yesu ajikwae (Mathayo 18:6).

Tusimfanye yoyote ajikwae (Mathayo 18:7).

Tusiwadharau watoto (Mathayo 18:10).

Tumkemee kibinafsi ndugu yeyote anayetukosea (Mathayo 18:15).

Tutii agizo la Yesu kuhusu adhabu kikanisa (Mathayo 18:16-17).

Tuwasamehe ndugu zetu kutoka moyoni (Mathayo 18:35).

Tumpende jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe (Mathayo 19:19).

Tuwe watumishi wa wengine (Mathayo 20:26-28).

Tulipe kodi halali kwa serikali na kumpa Mungu sehemu Yake (Mathayo 22:21).

Tumpende Bwana Mungu kwa moyo wote, roho yote na akili (Mathayo 22:37).

Tusikubali yeyote kutuita ‘mwalimu’ au ‘bwana’ na tusimwite yeyote baba isipokuwa Baba yetu wa mbinguni (Mathayo 23:8-10).

Tusijiinue bali tujishushe (Mathayo 23:12).

Tusimzuie yeyote kuingia katika ufalme wa Mungu (Mathayo 23:13).

Tusiwaonee wajane (Mathayo 23:14).

Tusiwashawishi wengine kuwa wanafiki (Mathayo 23:15).

Tusipuuzie mambo makuu katika Torati kama vile haki, rehema na uaminifu (Mathayo 23:23).

Tusiwe wanafiki kwa njia yoyote ile (Mathayo 23:25-28).

Tusiogope kuhusu vita au matetesi ya vita kabla ya kurudi kwa Yesu (Mathayo 24:6).

Tusianguke, au kusaliti au kumchukia ndugu (Mathayo 24:10).

Tusikubali kupotoshwa na manabii wa uongo (Mathayo 24:11).

Tusiruhusu pendo letu kupoa kwa sababu maasi yameongezeka (Mathayo 24:12).

Tuvumilie mpaka mwisho (Mathayo 24:13).

Tusiamini taarifa za uongo kuhusu kurudi kwa Kristo (Mathayo 24:23-26).

Tutambue ishara za kurudi kwake Kristo (Mathayo 24:32-33).

Tuwe macho kwa ajili ya kurudi kwa Kristo (Mathayo 24:42).

Kila mara tuwe watumwa waaminifu, tukitazamia kurudi kwa Bwana wetu upesi. Tusirudi nyuma bali kila wakati tumtii (Mathayo 24:45-51).

Tutumie muda, vipawa na hazina ambavyo Mungu ametupa kwa ajili ya utumishi Wake (Mathayo 25:14-30).

Tuwape Wakristo maskini chakula, cha kunywa na mavazi. Tuwatembelee Wakristo waliofungwa na walio wagonjwa (Mathayo 25:34-40). Tushiriki Meza ya Bwana (Mathayo 26:26-27).

Tufanye wanafunzi katika mataifa yote, tukiwabatiza katika jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote aliyoamuru Yesu (Mathayo 28:19-20).

Tujihadhari tunasikia nini (Marko 4:24).

Tusipuuze amri za Mungu kwa ajili ya kushika mapokeo (Marko 7:9).

Tusimwonee Yesu aibu, wala maneno Yake (Marko 8:38).

Tuwe na amani sisi kwa sisi (Marko 9:50).

Tusiwazuie watoto kwenda kwa Yesu (Marko 10:14).

Tuwe na imani kwa Mungu (Marko 11:22).

Tuamini kwamba tumepokea yote tuyaombayo (Marko 11:24).

Tujihadhari na waalimu wa uongo waliovaa mavazi yanayowafanya waonekane, wanaopenda kusalimiwa kwa heshima, viti vya mbele na mahali pa heshima, wanaowaonea wajane na kuomba sala ndefu ili waonekane tu (Marko 12:38-40).

Tusiogope tutasema nini tukifikishwa mahakamani kwa ajili ya imani yetu bali tuseme kile ambacho Roho Mtakatifu atatwambia wakati huo (Marko 13:11).

Tubatizwe (Marko 16:16).

Tuwabariki wanaotulaani (Luka 6:28).

Tumpe kila atuombaye, wala tusidai vitu tulivyonyang’anywa (Luka 6:30).

Tuwakopeshe wengine, wala tusitazamie kulipwa (Luka 6:35).

Tuwe wenye rehema (Luka 6:36).

Tusiwahukumu wengine (Luka 6:37).

Tutoe (Luka 6:38).

Tusinyoshe kidole kuhusu kibanzi katika jicho la ndugu wakati sisi tuna boriti katika jicho letu (Luka 6:41-42).

Tusimwite “Bwana” kama hatufanyi asemayo (Luka 6:46-49).

Tulipokee Neno la Mungu mioyoni mwetu na kulishika ili tuzae matunda kwa saburi (Luka 8:12-15).

Tulisikie Neno la Mungu na kulitenda (Luka 8:21).

Tuwapokee watoto katika jina la Kristo (Luka 9:48).

Tusiangalie nyuma baada ya kutia mkono kwenye jembe (Luka 9:62).

Tuombe kupewa Roho Mtakatifu (Luka 11:13).

Tujihadhari nuru ndani yetu isiwe giza (Luka 11:35).

Tusipende viti vya heshima na salaamu (Luka 11:43).

Tusiwalemee watu wengine kwa mizigo mizito ambayo sisi hatuko tayari kuibeba (Luka 11:46).

Tusiwatese manabii Wake (Luka 11:49).

Tusiondoe ufunguo wa maarifa wala kuwazuia watu wasiingie katika maarifa ya kweli ya Mungu (Luka 11:52).

Tujihadhari na viongozi wa dini walio wanafiki (Luka 12:1).

Tusiogope wale wanaoweza kutuua kimwili tu (Luka 12:4).

Tumwogope yeye ambaye, baada ya kuua ana mamlaka ya kutupa kuzimuni (Luka 12:5).

Tusinene mabaya wala kumkufuru Yesu au Roho Mtakatifu (Luka 12:10).

Tujihadhari na kujilinda na choyo (Luka 12:15).

Tusijiwekee hazina bali tuwe matajiri kwa Mungu (Luka 12:21).

Tuuze mali zetu na kuwapa maskini (Luka 12:33).

Tuzae matunda (Luka 13:6-9).

Tujitahidi kuingia kwa kupitia mlango mwembamba (Luka 13:24).

Tusichukue mahali pa heshima, tukijitukuza wenyewe. Bali tujinyenyekeze, tukikaa kiti cha nyuma (Luka 14:8-10).

Tumpende Yeye kuliko wapendwa wetu (Luka 14:26).

Kwanza tuhesabu gharama ya kuwa wanafunzi Wake (Luka 14:28-32).

Tuweke mali yetu yote chini ya mamlaka Yake (Luka 14:33).

Tufurahi wakati Mungu anapowahurumia wenye dhambi kwa kuwaokoa (Luka 15:1-32).

Tuwe waaminifu katika mambo madogo, na fedha (Luka 16:9-11).

Tuwahurumie maskini (Luka 16:19-31).

Tumkemee ndugu akikosa, na kumsamehe akitubu (Luka 17:3-4).

Tujihesabu kuwa watumwa wasiofaa hata baada ya kufanya yote tuliyoagizwa kufanya (Luka 17:7-10).

Tuombe wakati wote wala tusikate tamaa (Luka 18:1).

Tusijione kwamba ni wenye haki, wala tusiwadharau wengine (Luka 18:9).

Tuupokee ufalme kama mtoto (Luka 18:17).

Tuwe macho wakati wote na kuomba ili tuweze kuepukana na majaribu yatakayokuwepo kabla ya kurudi kwa Kristo, na tuweze kusimama mbele zake (Luka 21:36).

Tutangaze toba na msamaha wa dhambi katika Jina la Yesu kwa mataifa yote (Luka 24:47).

Tuzaliwe mara ya pili (Yohana 3:3).

Tumwamini Yesu (Yohana 3:16).

Tumwabudu katika roho na kweli (Yohana 4:23-24).

Tumheshimu Yesu (Yohana 5:23).

Tutafute utukufu kutoka kwa Mungu (Yohana 5:44).

Tuamini aliyoandika Musa (Yohana 5:46-47).

Tusikitendee kazi chakula kiharibikacho, bali kidumucho mpaka uzima wa milele kinachotolewa na Yesu (Yohana 6:53-54).

Tusihukumu kwa jinsi mtu anavyo-onekana, bali kwa haki (Yohana 7:24).

Tukae katika neno la Yesu (Yohana 8:31).

Tulishike neno la Yesu (Yohana 8:51).

Tumtumikie (na kumfuata) Yesu (Yohana 12:26).

Tupendane, kama Yesu anavyotupenda (Yohana 13:34).

Tuamini kwamba Yeye ni ndani ya Baba, na Baba ndani Yake (Yohana 14:11).

Tufanye matendo ya Yesu, na hata makubwa zaidi (Yohana 14:12).

Tumpende Yesu na kuzishika amri Zake (Yohana 14:15).

Tukae katika pendo la Yesu (Yohana 15:9).

Tuombe lolote katika Jina la Yesu (Yohana 16:24).

Tuwe na ujasiri katika dhiki (Yohana 16:33).

Huo ndiyo mwisho wa amri za Yesu zipatikanazo katika Injili. Hayo ndiyo mambo ambayo tunapaswa kuwa tunawafundisha wanafunzi wa Kristo kwamba wayatii (ona Mathayo 28:20).

Amri na maagizo kwa ajili ya waamini katika nyaraka si tofauti sana na Injili. Sasa hebu tutazame wajibu wa mwanadamu kutoka kitabu cha Warumi tu.

Mungu anatazamia tufanye haya yafuatayo:

Tusifiche au kugandamiza ukweli (Warumi 1:18).

Tusiwe na hatia ya kuabudu sanamu (Warumi 1:23).

Tusibadili kweli ya Mungu kwa uongo (Warumi 1:25).

Tusihusike katika ulawiti (Warumi 1:26, 27).

Tusiwe wachoyo, wenye wivu, wadanganyifu, wabaya, wenye dharau, wakorofi, wenye kiburi, wasiotii wazazi, wasioaminika, wasiopenda na wasio na rehema (Warumi 1:29-31).

Tusiwasengenye watu wala kuwasingizia uongo (Warumi 1:29-30).

Tusiwaunge mkono watendao dhambi (Warumi 1:32).

Tusipuuzie utajiri wa wema Wake, ustahimilivu na uvumilivu (Warumi 2:4).

Tudumu katika kutenda mema (Warumi 2:7).

Tutafute utukufu, heshima na kutokuharibika (Warumi 2:7).

Tusiwe na tamaa ya ubinafsi (Warumi 2:8).

Tusilaani au kusema maneno yenye uchungu (Warumi 3:14).

Tujihesabu wafu kwa dhambi bali hai kwa Mungu katika Kristo (Warumi 6:11).

Tusiruhusu dhambi itawale miili yetu. Tusitii tamaa yake (Warumi 6:13).

Tujitoe kwa Mungu kama walio hai kutoka kwa wafu, na viungo vyetu kama vyombo kwa ajili ya haki kwa Mungu (Warumi 6:13).

Tusitamani (Warumi 7:7).

Tusiishi kulingana na mwili, bali tuyafishe matendo ya mwili kwa njia ya Roho (Warumi 8:12-13).

Tuitoe miili yetu kama dhabihu iliyo hai na takatifu (Warumi 12:1).

Tusifananishwe na dunia hii, bali tufanywe upya kwa kugeuzwa nia zetu (Warumi 12:2).

Tusinie makuu kuliko inavyopasa (Warumi 12:3).

Tutumie vipawa vyetu kulingana na neema tuliyopewa (Warumi 12:6).

Tuwapende wengine bila unafiki (Warumi 12:9).

Tukatae lililo ovu na kushika lililo jema (Warumi 12:9).

Tupendane kindugu na kupeana heshima (Warumi 12:10).

Tusilegee (Warumi 12:11).

Tuwe na juhudi tunapomtumikia Bwana (Warumi 12:11).

Tufurahi katika tumaini (Warumi 12:12).

Tuvumilie katika dhiki (Warumi 12:12).

Tudumu katika maombi (Warumi 12:12).

Tusaidie mahitaji ya watakatifu (Warumi 12:13).

Tuwe wakarimu (Warumi 12:13).

Tuwabariki wanaotulaani, tusiwalaani sisi (Warumi 12:14).

Tufurahi na wanaofurahi, tulie na wanaolia (Warumi 12:15).

Tusiwe wenye majivuno bali tushirikiane na wa hali ya chini (Warumi 12:16).

Tusiwe wenye hekima machoni petu wenyewe (Warumi 12:16).

Kamwe tusilipe ovu kwa ovu (Warumi 12:17).

Tujali lililo jema machoni pa watu wote (Warumi 12:17).

Kadiri iwezekanavyo, tukae kwa amani na watu wote (Warumi 12:18).

Tusijilipizie kisasi (Warumi 12:19).

Adui yetu akiwa na njaa tumlishe, akiwa na kiu tumnyweshe (Warumi 12:20).

Tusishindwe na ubaya, bali tuushinde kwa wema (Warumi 12:21).

Tukubali mamlaka ya wakuu wa serikali (Warumi 13:1).

Tusidaiwe chochote na mtu isipokuwa kupendana (Warumi 13:8).

Tuweke kando matendo yote ya giza na kuvaa silaha za nuru (Warumi 13:12).

Tuenende ipasavyo mchana, sio katika vurugu na ulevi, uasherati na tamaa mbaya, wivu au fujo. Tumvae Kristo na tusitoe nafasi kwa mwili na tamaa zake mbaya (Warumi 13:13-14).

Tuwapokee walio dhaifu katika imani (Warumi 14:1).

Tusimhukumu ndugu wala kumdharau (Warumi 14:10).

Tusiweke vikwazo mbele ya ndugu (Warumi 14:13).

Tufuate mambo yaletayo amani na kujengana (Warumi 14:19).

Tuichukue mizigo ya walio dhaifu kama sisi tuna nguvu. Tusijipendeze wenyewe (Warumi 15:1).

Tupokeane na kukubaliana, kama Kristo alivyofanya kwetu (Warumi 15:7).

Tuwatazame wenye kuleta matengano na vipingamizi kinyume cha kweli za Biblia na kuachana nao (Warumi 16:17).

Sasa niulize hivi: Je, Wakristo wanawajibika kama wanadamu? Tuseme nini juu ya mtu yule anayesema kwamba yeye ameliacha jambo la utakaso wake mikononi mwa Mungu, asije akamwibia Mungu utukufu wake na kuwa na hatia ya kuongezea matendo yake kwenye wokovu?

Vita Ya Kiroho

Kila moja katika zile amri na maagizo kwenye orodha hiyo iliyopita inathibitisha wazo kwamba mwanadamu anawajibika, lakini pia kwamba sisi sote tunakabiliwa na maamuzi. Tunaweza kuchagua kufanya au kutofanya yale aliyosema Yesu. Kutoka katika roho zetu zilizozaliwa upya, Roho Mtakatifu hutuongoza kutii, lakini nguvu zingine – dunia, mwili na Shetani – hutujaribu kutotii. Basi tunajikuta katika vita.

Kuna hoja mbili za kusemwa hapa. Kwanza: Wakristo wa bandia wakati mwingine – kwa makosa – hufikiri kwamba wanapitia katika hiyo vita ya kiroho. Lakini kihalisi, wao wanapitia vita inayofanana na hiyo, kati ya dhamiri zao na asili zao za dhambi. Kulingana na Paulo, hata watu ambao hawajaokoka wana dhamiri ambayo inawashtaki au kuwatetea (ona Warumi 2:15). Kwa kuwa wameikosea mara nyingi sana, dhamiri yao imekwisha najisika (Tito 1:15), na sauti yake inaendelea kupungua kadiri wanavyopuuza maonyo yake. Lakini, Mkristo wa kweli ana dhamiri ambayo imeamka kabisa, yenye kusema naye kila wakati, na si rahisi kuipuuza. Roho wa Mungu anawaongoza wote walio watoto wa Mungu kweli (ona Warumi 8:14).

Jambo la pili ni kwamba wanaojiita Wakristo mara nyingi hutumia hiyo vita ya kiroho kama kichocheo cha kutenda dhambi. Wanasema hivi: “Tuko vitani. Kama ni hivyo, lazima tutashindwa mapigano fulani fulani.” Kujitetea huko ni sawa na kusema hivi: “Bwana wee! Hakuna aliye mkamilifu! (Kwa hiyo nitakuwa dhaifu tu.)”

Mungu ndiye aliyeruhusu vita hiyo ya kiroho iwepo kwa enzi Yake, na kusudi Lake si kwamba watoto Wake waingie dhambini. Kusudi Lake ni kwamba tujithibitishe kuwa washindaji kwa utukufu Wake. Hebu fikiri maneno ya Paulo juu ya vita kati ya mwili na Roho katika Wagalatia sura ya 5.

Basi nasema, ‘Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo. Katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake (5:16-24).

Bila shaka Wakristo wana asili mbili, asili ya dhambi yenye kupingana na Roho Mtakatifu aliye ndani. Lakini je, hii ni njia tu ya kukubaliana na dhambi? Hapana! Paulo anaonya kwamba wale wanaotenda matendo ya mwili hawataurithi ufalme wa Mungu. Ukweli ni kwamba hakuna Mkristo wa kweli anayetoa nafasi kwa mwili, kwa sababu, kama anavyosema Paulo, “Walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake” (5:24). Hayo yalifanyika wakati wa wokovu, imani ya moyoni ilipoonyeshwa kwa toba na kujinyenyekeza kuwa chini ya mamlaka ya Yesu Kristo kama Bwana. Wakati huo – kwa lugha ya mfano – tulimsulubisha yule mtu wa kale wa dhambi msalabani. Naye anatakiwa kubakia hapo. Bado yuko hai na anaweza kulia aruhusiwe kufanya anachotaka, lakini kwa uwezo wa Roho kilio chake hakuna anayekisikiliza.

Katika Mwili Au Katika Roho?

Katika sura ya nane ya Warumi, Paulo anaonyesha tofauti kati ya mtu ambaye hajaokoka – anayemtaja kuwa yuko “katika mwili” – na mtu aliyeokoka – anayemtaja kuwa yuko “katika Roho”. Jambo hili ni muhimu sana kwetu kulifahamu. Hebu soma kwa makini sana maneno ya Paulo tunapotafakari Maandiko haya.

Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili; ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili bali mambo ya Roho (Warumi 8:3-4).

Ona kwamba tayari Paulo ameeleza juu ya waamini kwamba ni wale wasio “enenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya Roho.”

Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. (Warumi 8:5-9. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ni dhahiri hapo kwamba Paulo haonyeshi tofauti kati ya aina mbili za Wakristo – wale wawekao nia zao kwa mwili na wale wawekao nia zao kwa Roho. Yeye anawatofautisha wale ambao ndani yao yupo Roho wa Mungu, ambao wanaweka nia zao kwa Roho, na wale ambao hawana Roho ndani yao, wenye kuweka nia zao kwenye mwili – yaani Wakristo na wasiokuwa Wakristo.

Wakristo wanaweza kutajwa kwamba wana Kristo ndani yao, kwa yule Roho Mtakatifu anayekaa ndani yao, japo bado wana asili ya dhambi ya mwili.

Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu ni hai kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu (Warumi 8:10-11).

Mwili wetu – “utu wetu wa nje” kama anavyouita Paulo – “umekufa” au “unachakaa” kwa sababu ya dhambi (2Wakor. 4:16). Lakini roho yetu – “utu wetu wa ndani” – sasa unahuishwa na kuwa hai kwa sababu tumefanywa kuwa wenye haki. Unafanywa upya siku kwa siku (ona 2Wakor. 4:16). Lakini, tunaweza kutazamia siku ile ambapo Roho ndani yetu ataihuisha “miili yetu ya kufa,” na wakati huo miili yetu nayo itafanywa mipya. Bila shaka Mungu anakusudia kwamba Roho anayekaa ndani yetu atawale miili yetu. Imekusudiwa kwamba atawale mpaka miili yetu ibadilishwe na ile asili ya dhambi ifutiliwe mbali kabisa.

Mwishoni, Paulo anawaonya waamini ambao alikuwa anawaandikia kuhusu kujitoa kwa mwili. Kwa nguvu ya Roho aliye ndani yao, wanaweza “kuyafisha matendo ya mwili.” Hili ni jambo ambalo lazima wao walitende. Anasema hivi:

Basi kama ni hivyo ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili. Kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu (Warumi 8:12-14).

Je, wewe ni yule ambaye Paulo anasema hutakufa bali utaishi – yaani, yule ambaye “kwa Roho” unaya “fisha matendo ya mwili”? Kama ndiyo, basi wewe ni Mkristo wa kweli. Paulo aliamini kwamba Wakristo wa kweli wanatenda tofauti na wasiokuwa Wakristo. Kama alivyosema, ni wale wanaoongozwa na Roho ndiyo wana wa Mungu wa kweli (ona Warumi 8:14).

Hoja Inajibiwa

Kuna wanaoweza kupinga hivi: “Hivi, Paulo mwenyewe si alikiri kwamba hata yeye alitenda yale mabaya aliyoyachukia, mpaka akajiita ‘maskini’ mwenye ole?”

Kweli, alifanya hivyo. Ukweli ni kwamba Paulo alisema maneno hayo katika sura ya saba ya Warumi, kabla ya kile ambacho tumekuwa tukitazama katika sura ya nane. Wakristo wamejadili kuhusu jambo hilo miaka na miaka – kwamba, je, Paulo alikuwa anazungumzia ujuzi wake kabla ya kuokoka au baada? Wale wenye kufundisha kwamba kushika sheria si vizuri wanapenda kuyaweka maneno ya Paulo hayo kwamba ndiyo kawaida katika maisha ya Kikristo.

Lakini, tukisoma Warumi sura ya 7 katika mantiki ya zile sura mbili zilizotangulia, pamoja mengine yote aliyoandika Paulo na Agano Jipya, tutapata tafsiri moja tu. Bila shaka Paulo alikuwa anazungumza juu ya mambo yalivyokuwa kabla Roho Mtakatifu hajakaa ndani yake. Vinginevyo, katika sura ya 7 anapingana na yale aliyoandika mwenyewe katika sura ya 6 na ya 8 kuhusu maisha ya kawaida ya Kikristo. Kuna swali zuri sana ambalo limewahi kuulizwa: “Kama huyo anayesemwa katika sura ya 7 ni mwamini aliyeokoka, nani basi anayesemwa katika sura ya 6 na ya 8?” Bila shaka ni watu wawili tofauti!

Kwanza: Tunaona kwamba kweli kuu ya sura ya 6 ni kutokulingana kwa dhambi na uumbaji mpya. Paulo alianza kwa swali: “Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?” (6:1) Jibu lake? “Hasha!” Kisha akaandika jinsi isivyowezekana kwa mwamini kuwa katika hali hiyo, hivi: “Sisi tuliofia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (6:2)

Katika mistari inayofuata, Paulo aliweka wazi zaidi kwamba waamini wote wameunganishwa na Yesu katika mauti na kufufuka Kwake, ili waweze “kuenenda katika upya wa uzima” (6:4), kwa kuwa wao si “watumwa wa dhambi” tena (6:6, 17, 20). Wao sasa wamewekwa “huru na dhambi” (6:7, 18, 22), ni “watumwa wa haki” (6:18), na ni “watumwa wa Mungu” (6:22), baada ya wao kutii “kwa mioyo ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake” (6:17). Dhambi “haitatawala tena” juu yao, kwa hiyo, wasiiruhusu “itawale” katika miili yao, wala wasikubaliane na tamaa zake (6:12). Badala yake, watoe viungo vyao “vitumiwe na haki ili mpate kutakaswa” (6:19).

Sasa, huyu Mkristo wa sura ya 6 analinganaje na mtu wa sura ya 7, ambaye Paulo anamsema kwamba ni “wa mwilini, chini ya dhambi” (7:14), ambaye anatenda yale maovu asiyotaka kuyatenda (7:15, 19), “mateka wa ile sheria ya dhambi” (7:23), na mtu “maskini, tena ole” (7:24)? Je, yule mtu wa sura ya 6 ambaye amewekwa huru kutokana na dhambi ndiye huyo huyo maskini ole wa sura ya 7 ambaye ni mfungwa wa dhambi? Je, yule mtu wa sura ya 6, ambaye asili yake ya zamani imesulubiwa na Kristo ili mwili wake “wa dhambi ubatilishwe” (6:6) ndiye huyo huyo wa sura ya 7 anayetamani sana mtu amweke huru na “mwil huu wa mauti” (7:24)? Haiwezekani! Au wewe unaonaje?

Tena, ile mistari 14 ya kwanza katika sura ya 8 ambayo tumekwisha itazama inazua maswali mengi zaidi, ikiwa yule mtu wa sura ya 7 ameokoka. Katika sura ya 8, Paulo alimwelezea Mkristo wa kweli kwamba haenendi “kwa kuufuata mwili, bali kwa kuifuata Roho (8:4). Akili yake imemwelekea Roho, sio mwili, ambayo ni tofauti na nia ya wasiokuwa Wakristo (8:5-6). Mkristo wa kweli ni yule ambaye hayuko “katika mwili” bali yuko “katika Roho” kwa sababu Roho anakaa ndani yake (8:9). Paulo hata aliwaonya wale wanaoishi kwa kuufuata mwili kwamba lazima wafe, na anawaahidi wale ambao, “kwa Roho wanayafisha matendo ya mwili” (8:13) kwamba wataishi. Kama Paulo alikuwa anazungumza juu ya ujuzi wake binafsi katika sura ya 7, tunajaribiwa kumwambia asome barua yake mwenyewe ili agundue jinsi ya kuokoka na kuwekwa huru na dhambi! Na kulingana na mashauri yake mengine yote kuhusu utakatifu ambayo ametoa kwa watu, itabidi tumweke katika fungu la mnafiki aliyehubiri hivi: “Fanyeni ninavyosema, sio kama ninavyotenda.”

Kumweka Paulo Sawa

Kama Paulo alikuwa anafanya ule ule uovu aliokuwa anauchukia, basi kwa maneno yake mwenyewe ya kuelewa wasioamini katika barua hii na zingine, hata yeye hakuwa ameokoka. (Ona Warumi 2:8-9; 1Wakor. 6:9-11; Wagalatia 5:19-21; Waefeso 5:5-6). Kulingana na yale ambayo Yohana naye aliandika, Paulo hakuwa ameokoka. Anasema hivi: “Atendaye dhambi ni wa ibilisi … Kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi … Yeyote asiyetenda haki si wa Mungu …” (1Yohana 3:8-10, TLR).

Ikiwa Paulo katika sura ya 7 ya Warumi alizungumza juu yake mwenyewe kwamba ni mfungwa wa dhambi atendaye maovu, basi sisi wengine tuliosoma juu yake katika sehemu zingine tunashangaa kweli kweli. Ingawa alikiri kwamba hakuwa amefikia ukamilifu (ona Wafilipi 3:12), aliwaandikia Wakorintho kwamba yeye hakuwa na lawama juu yake mwenyewe (1Wakor. 4:4), na akaendelea kusema hivi:

Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi” (2Wakor. 1:12).

Aliwaandikia hivi Wakristo Wathesalonike:

Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa” (1Wathes. 2:10).

Alishuhudia kwa Timotheo kwamba alimtumikia Mungu kwa dhamiri safi (ona 2timo. 1:3). Mtu anapata picha anaposoma hadithi ya Paulo na barua zake kwamba alikuwa mtu aliyefanana na Kristo. Uaminifu wake haulinganishwi na yeyote katika Agano Jipya isipokuwa Yesu. Sasa, tunawezaje basi kumdhania akitenda maovu?

Jibu la pekee tunaloweza kulipata kutokana na ushahidi huo wote ni kwamba Paulo alikuwa anazungumza juu ya ujuzi wake kabla hajaokoka.

Mtu anaweza kuuliza hivi: “Lakini si aliandika sura ya 7 akitumia maneno ya wakati uliopo? Je, huo si ushahidi kwamba alikuwa anaandika juu ya hali yake ya wakati huo?”

Hapana. Kwamba alitumia maneno ya wakati uliopo haithibitishi chochote. Mara nyingi tunatumia maneno ya wakati uliopo ili kusimulia jambo lililopita. Ninaweza kusimulia habari ya uvuvi iliyotokea miaka kumi iliyopita kwa kusema, “Basi, niko kwenye mtumbwi wangu, mahali ninapopenda sana ziwani. Mara nasikia ndoana imenasa – sina hakika kama ni samaki au ndiyo imenaswa na majani. Kisha inajigusa! Ninaanza kuvutana na samaki mkubwa kuliko wote niliowahi kushika! Ninapomfikisha karibu na mtumbwi, mshipi unakatika, na samaki mkubwa anajiendea zake huru! Ole wangu, maskini mimi! Nani atakayeniokoa na mchezo huo?”

“Sawa, lakini, Paulo si anasema katika Warumi 7 kwamba yeye hakutaka kufanya mabaya bali mema? Hakusema, ‘Kwa utu wa ndani ninaifurahia sheria ya Mungu’ (7:22)? Angewezaje kusema hayo kama hajaokoka? Watu ambao hawajaokoka si waovu kabisa kabisa, walioharibika vibaya sana?”

Kumbuka kwamba Paulo alikuwa Myahudi Farisayo mwenye juhudi sana kabla ya wokovu. Yeye hakuwa kama mtu wa kawaida ambaye hajaokoka – yeye alikuwa anafanya kila alichoweza ili kutii amri za Mungu – mpaka kufikia hata kuliudhi kanisa! Lakini aligundua kwamba kadiri alivyojitahidi sana, asingeweza kutimiza masharti ya kiwango cha Mungu. Alikuwa mtumwa wa dhambi. Mwishoni akatambua kwamba hataweza kuwa mtakatifu bila ya msaada wa Roho Mtakatifu. Kweli – hakuna mtu maskini mwenye ole kuliko yule anayejaribu kuishi kulingana na viwango vya Mungu, lakini hajazaliwa mara ya pili!

“Wakristo” Wa Warumi 7

Inasikitisha sana kwamba, licha ya yote yaliyosemwa na Yesu, Yohana, Yakobo, Petro, Yuda na Paulo mwenyewe, yanayopinga wazo kwamba yule mtu wa Warumi sura ya 7 ameokoka, wengi siku hizi wanafikiri hivyo. Wala sababu si kwamba kuna ushahidi wa maandiko – maana haupo – bali ni kwa sababu wengi katika wanaojiita Wakristo wanajiona kama yule mtu wa Warumi sura ya 7 – wakitenda wasiyotaka, wakiwa watumwa wa dhambi. Wanafasiri Maandiko kutokana na ujuzi wao kwa hoja inayosema hivi: “Mimi ninajitambulisha na yule mtu wa Warumi sura ya 7, na mimi ni Mkristo. Basi, huyo mtu wa Warumi sura ya 7 lazima awe Mkristo.”

Hii tafsiri mbaya ya Warumi sura ya 7 inatia nguvu imani dhaifu yenye kuyumba ya walio wengi, ambao bado hawajapata uhuru kutoka kwenye nguvu za dhambi, ule ambao Paulo aliahidi katika Warumi sura ya 6 na ya 8, na ambao yeye mwenyewe aliufurahia maisha yake yote ya Kikristo. Hili ni janga kubwa sana, ukizingatia ile neema ya ajabu ya Mungu ambayo inapatikana bure kabisa kwa wote kwa njia ya Yesu Kristo, kama watu watamwendea kwa masharti Yake – kwa imani hai, yenye kunyenyekea.

Jihadhari Na Waalimu Wa Uongo

SURA YA KUMI

 

Kulingana na Agano Jipya, sifa maarufu ya mwalimu wa uongo ni jinsi anavyopuuza umuhimu wa utakatifu. Hilo linaonekana kwa mafundisho yake na maisha yake binafsi. Maandiko mengi yanathibitisha jambo hilo. Kwa mfano: Hebu tutazame kile alichofundisha Yesu kuhusu manabii wa uongo katika Mahubiri ya Mlimani.

“Jihadharini na manabii wa uongo [au, yeyote anayedai kwamba anasema neno la Mungu, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila mtu aniambaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?’ Ndipo nitawaambia dhahiri, ‘Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu’.” (Mathayo 7:15-23).

Yesu alisema manabii wa uongo wanaweza kujulikana kwa matunda yao, ambayo, kwa mantiki ya Mahubiri ya Mlimani, bila shaka ni yale matunda ya utakatifu na utii. Yesu alisema kwamba wale tu wenye kufanya mapenzi ya Baba Yake ndiyo watakaoingia “katika ufalme wa Mungu” (7:21). Wanaweza kuwa walitabiri, walitoa pepo na wakafanya miujiza, lakini kama walitenda maovu, atatangaza kwamba hakuwajua kamwe (7:23).

Neema Ya Kigeni

Si matunda ya maisha ya watu tu yenye kuwaonyesha kwamba ni waalimu wa uongo bali pia matunda ya maneno yao. Kama kile wanachofundisha ni kinyume na mafundisho ya msingi ya Agano Jipya, wao ni waalimu wa uongo.

Sasa – hakuna mwalimu kanisani atakayesimama na kutamka mbele za watu kwamba anafundisha kinyume cha Agano Jipya. Badala yake – atakuwa anapuuza maandiko fulani fulani muhimu sana, na kuyabadilisha mengine ili kuwashawishi wasikilizaji wake kwamba anachofundisha ni kweli. Hayo yanafanywa na watu wengi siku hizi – waalimu maarufu na wenye kupendwa sana, na wenye ushawishi mkubwa – wanaofundisha neema ambayo ni ngeni kabisa na haipatikani katika Biblia. Neema wanayotangaza wao si ile neema ya kweli ipelekeayo kwenye utakatifu, ambayo Paulo, mwalimu wa neema ya kweli alifundisha juu yake, hivi:

Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa …” (Tito 2:11, 12 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Badala yake, ni neema ile ya bandia ambayo Yuda alionya juu yake – neema ambayo imebadilishwa sana na kufanyika kibali cha watu kutenda dhambi. Anasema hivi:

Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo (Yuda mstari wa 3 na wa 4 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Swali: Inawezekanaje kwamba watu waliomkana Bwana wa pekee – Yesu Kristo – “wamejiingiza kwa siri”? Jibu ni hili: Hawakuwa wanasimama mbele ya makusanyiko na kutamka hivi: “Mimi namkana Yesu Kristo”. Ila, walikuwa wanamkana Yesu Kristo kwa kupitia mafundisho yao ya uongo kuhusu neema, wakiigeuza kuwa ufisadi.

Ujumbe wao unaweza kufupishwa hivi: “Jamani! Neema ya Mungu ni nzuri mno. Kwa kuwa wokovu wetu unatokana na neema Yake na wala sio matendo yetu, utakatifu si lazima kwa ajili ya wokovu. Kwa sababu ya neema ya ajabu ya Mungu, wote wanaomwamini Yesu wameokoka, hata kama wanaendelea kutenda dhambi.”

Sahau juu ya andiko linalosema bila utakatifu hakuna atakayemwona Bwana (Waebrania 12:14). Usijali Yesu alifundisha kwamba hatuwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni kama haki yetu haitazidi haki ya waandishi na Mafarisayo, na kwamba ni wale tu watendao mapenzi ya Mungu ndiyo watakaoingia katika ufalme wa mbinguni (ona Mathayo 7:21). Usijali kwamba alituambia tujitahidi kuingia kwa kupitia ule mlango mwembamba, mlango pekee wa kufika uzimani, na kwamba ndugu zake wa kweli ni wale “wanaolisikia neno la Mungu na kulitenda” (ona Mathayo 7:13-14; Luka 8:21). Puuzia ukweli kwamba Yakobo alifundisha kuwa imani bila matendo imekufa na haiwezi kutuokoa (Yakobo 2:14, 17). Usijali maonyo ya Paulo kwamba wale watendao matendo ya mwili hawataurithi ufalme wa Mungu (ona Wagalatia 5:20-21). Ufungie macho waraka wa kwanza wa Yohana na kila kitu juu ya zile alama zinazowatambulisha Wakristo wa kweli. Pia, puuza maandiko mengi sana sana katika Agano Jipya, yenye kukazia kweli hizo hizo.

Wanasema: “Hapana! Sisi si kama wale washika sheria wanaokazia sana matendo. Sisi tumegundua ukweli juu ya neema ya Mungu.”

Kumkana Bwana

Hawa waalimu wa uongo wanamkana kabisa “yeye aliye peke yake Mola na Bwana” (Yuda mstari wa 4 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Kwa kuwa katika mawazo yao wanadhani kwamba utii ni kitu cha hiari kwa wale waendao mbinguni, si lazima Yesu awe Mola na Bwana maishani. Kwa njia hiyo wanamkana kwa mafundisho yao na jinsi wanavyoishi.

Kwa asiyetambua, vidokezo na miito ya waalimu wa uongo vinatokana na Maandiko, maana wanatumia maneno ya Paulo (japo wameyaondoa katika mantiki yake). Wanasema hivi: “Hatuko chini ya sheria, bali neema!” “Mungu asifiwe kwa uhuru tulio nao ndani ya Kristo!” Tena wanasema, “Hata kama sisi si waaminifu, Yeye anabaki kuwa mwaminifu!” Kule kupotosha kwao maneno ya Paulo ni kitu cha zamani kama nyaraka za Paulo pia. Petro anawaonya wao, na waliowatangulia, hivi:

Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo. Katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe (2Petro 3:15-16. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Petro alikuwa na mengi ya kusema juu ya hao wenye kuyapotosha maandiko kwa uharibifu wao. Sura nzima ya waraka wake wa pili inaonya kuhusu “mafundisho ya uzushi” ambayo waalimu wa uongo “wataingiza kwa werevu … wakimkana hata Bwana aliyewanunua…” (2Petro 2:1).

Tunauliza tena: Inawezekanaje mafundisho yenye kumkana Bwana yaingizwe kwa siri ? Ni dhahiri kwamba wale waalimu wa uongo hawakuwa wanatangaza hadharani wakisema, “Tunamkana Bwana!” Hapana. Walikuwa wanamkana Bwana kwa kuikana nafasi Yake. Walikuwa wanapuuza umuhimu wa utii. Petro anaandika kwamba waliwaongoza watu “kufuata ufisadi wao, na kwa hao njia ya kweli itatukanwa” (2:2). Hawa waalimu wa uongo walidai kwamba mtu angeweza kufanya ufisadi na bado aokoke. Kutosheleza tamaa za mwili ilikuwa inaruhusiwa na hata watu walitiwa moyo kufanya hivyo. Basi, kwa njia hiyo, “njia ya kweli” ikatukanwa.

Akikanusha makosa hayo mabaya sana, Petro alitoa mifano ya kihistoria kuonyesha jinsi Mungu alivyoshughulika na watauwa na wasiokuwa watauwa. Anachosema ni hivi: Watakatifu wameokolewa, wasio watakatifu wanahukumiwa. Yaani: Utakatifu ni kitu cha muhimu kabisa.

Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza walindwe hata ije hukumu; wala hakuuachilia ulimwengu wa kale bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki na watu wengine saba hapo alipoleta gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu; tena akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa hawamchi Mungu baada ya haya; akamwokoa Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao wahalifu; maana mtu huyu mwenye haki akikaa kati yao kwa kuona na kusikia alijitesa roho yake yenye haki siku baada ya siku, kwa matendo yao yasiyo na sheria. Basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu; na hasa wale waufuatao mwili katika tamaa ya mambo machafu na kudharau mamlaka (2Petro 2:4-10. Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Akikubaliana kabisa na Paulo, Petro, bila kutafuna maneno, anawataja wale wenye “kutimiza matendo ya mwili na kukubaliana na tamaa zake mbaya” kwamba ni “wasio haki.” Wanakwenda jehanamu, wadai kwamba ni Wakristo au wasidai.

Hawa waalimu wa uongo hata wamewashawishi waamini wa kweli kuondoka kwenye njia ya utakatifu. Basi wamenajisika tena, wakirudia kwenye hali ya kiroho ambayo ni mbaya kuliko hata ile waliyokuwa nayo kabla hawajaokoka.

Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu. Maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, ‘Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaagaa matopeni’ (2Petro 2:18-22).

Tunapata picha nzuri zaidi kuhusu ujumbe wa hao waalimu wa uongo kutoka katika maandiko haya. Petro aliandika kwamba walishawishi watu “kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi” na waliahidi uhuru ambao ulisababisha utumwa wa dhambi. Mahubiri yao yalisikika kama mahubiri ya waalimu wa siku hizi wa neema ya bandia, ambao wametafsiri upya utakatifu na kuuita ni kufuata sheria, na utii wanasema ni “kutumaini matendo”. Wanatangaza hivi: “Furahia uhuru wako ndani ya Kristo. Usiwasikilize hao wenye kuua neema kwa kutoa orodha zao za fanyeni hiki na msifanye kile.”

Matokeo ni kwamba hata waamini wa kweli wanadanganyika, wanaiacha njia na wanaanza kuelekea kwenye njia pana ya upotevuni. Wakifikiri kwamba wameigundua ile neema ambayo Yesu anatoa na ambayo Paulo alihubiri, wanapuuza makusudi kabisa orodha ya Yesu ya mambo ya kufanya na ya kuacha katika Mahubiri ya Mlimani, na zile orodha za Paulo za dhambi zitakazowakosesha watu mbingu katika nyaraka zake.

Ona kwamba wale waamini Petro aliowataja walikuwa “wameanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu””(2:18). Hao wanaokimbiwa ni wale ambao hawajaamini. Alisema hayo hayo katika sentensi iliyofuata, akitamka kwamba walikuwa “wameyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo” (2:20). Usifanye makosa hapa. Hao hawakuwa watu waliokuwa wanafikiri kuokoka. Wala hawakuwa waamini bandia. Wao walikuwa wamezaliwa mara ya pili na walikuwa wanaishi maisha tofauti na yale waliyoishi kabla ya wokovu.

Lakini walidanganywa na mafundisho ya uongo yaliyokuwa yanapuuza umuhimu wa utakatifu na kukazia neema bandia. Kwa mara nyingine tena “wakanaswa” katika “machafu ya dunia” (2:20), na “hali yao ya mwisho” ikawa “mbaya kuliko ile ya kwanza” (2:20). Hapo kwanza, walikuwa wameijua ile “njia ya haki” lakini sasa wakawa wameiacha “ile amri takatifu” (2:21).

Cha kusikitisha ni kwamba wengi wanaojiita Wakristo siku hizi hawajawahi “kuijua njia ya haki” kwa sababu wamesikia Injili ya uongo tangu mwanzo. Wamekuwa wakifurahia utumwa wao kwa dhambi maisha yao yote “ya Kikristo”, wakifikiri kwamba wanafurahia uhuru upatikanao katika neema ya ajabu ya Mungu. Kwa hali hiyo, wao ni tofauti na wale ambao Petro aliandika juu yao. Wao si nguruwe waliorudia matope baada ya kusafishwa; wao ni nguruwe ambao hawajawahi kuondoka matopeni.

“Tafadhali Tekenya Masikio Yetu!”

Kama ilivyokuwa katika siku za Paulo, wengi leo hukusanyika kuwasikiliza waalimu wa neema bandia watakaowaambia kile wanachotaka kusikia. Paulo alikuwa ametabiri hivyo, akisema:

Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo (2Timo. 4:3-4).

Ni dhahiri kwamba ule wakati aliosema Paulo umefika. Watu wanapenda kusikiliza mahubiri juu ya upendo wa Mungu wa ajabu na neema, na jinsi dhambi zao zilivyoshughulikiwa na Yesu, na jinsi wokovu ulivyo zawadi itolewayo bure, na jinsi wokovu unavyopokelewa kwa imani wala si kwa matendo – na yote hayo ni kweli. Lakini, ikifika hapo, neema ya Mungu inaanza “kufanyiwa marekebisho”.

Siku hizi tunaambiwa toba ni kugeuza mawazo tu, kitu ambacho kinaweza kisilete mabadiliko katika matendo. Watu wanaweza kumwamini Yesu na kuendelea kutenda dhambi. Wanaweza kuzaliwa mara ya pili na wasionyeshe kwa namna yoyote ile kwamba Roho Mtakatifu anakaa ndani. Wakristo wanaweza kuwa wazinzi na waasherati, na kwa kweli, hatutaki kuwahukumu maana hatujui mioyo yao. Wale wanaodai kwamba mbinguni ni kwa watakatifu tu ni washika sheria. Imani bila matendo inaweza kuokoa. Wale wasiotenda mapenzi ya Mungu bado wanakwenda mbinguni, mradi wamekiri kwa vinywa vyao imani katika Kristo. Kama mtu ana imani kwa dakika moja tu maishani mwake, yeye ni salama milele, bila kujali kama ataiacha imani yake, awe mtu asiyemwamini Mungu na kurudia maisha ya uchafu. Wakristo wengi wa kweli hawawezi kutofautishwa na wasiokuwa Wakristo, waliowekwa katika fungu maalum la waaminio wanaoitwa “wa kimwili”.

Hayo na mengine mengi kama hayo – ambayo ni uongo – yanatangazwa kwa watu mamilioni wasioshtuka. Hebu fikiri juu ya maneno haya kutoka kwa baadhi ya waalimu maarufu siku hizi kanisani, watu ambao majina yao yanajulikana sana katika Ukristo.

Mara baada ya mkutano huo, mwinjilisti aliyemsaidia kumpokea Kristo aliondoka katika imani. Familia yake ikasambaratika. Akazunguka-zunguka Marekani kama mnyama, mwishoni akafa akiwa amelewa chakari katika mtaro wa maji machafu huko Chicago Kusini. … Kama wewe umemwamini Bwana Yesu Kristo kuwa Mwokozi wako, bado ni mtoto wa Mungu. Unaweza kumkana, lakini Yeye hatakukana.

Je, huo ni ukweli? Yesu alisema hivi: “Mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 10:33). Tena, Paulo aliandika kwamba hakuna mlevi atakayeurithi ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 6:9-10).

Tunaokoka kwa sababu wakati fulani tulionyesha imani yetu katika Bwana wetu adumuye. … Hata kama mwamini – kwa njia zote zile – atakuwa asiyeamini, wokovu wake hauko hatarini.

Je, tuko salama milele katika wokovu wetu kama tutaamini kwa “kitambo tu”? Je, hiyo ndiyo maana ya Yesu kwamba tuamini, aliposema, “Aaaminiye … ataokoka” (Marko 16:16)? Kama ndivyo, basi ni lazima tuamini kwamba kama tutaacha kuamini kwa kitambo tu, basi kupotea kwetu kumetiwa muhuri milele, maana Yesu aliendelea kusema hivi, “Asiyeamini atahukumiwa” (Marko 16:16).

Huyo huyo mwalimu maarufu wa neema, akiwa amebanwa kuyachonga Maandiko yalingane na mafundisho yake, ameigeuza jehanamu kuwa mbinguni. Anasema hivi:

Hapo mahali panapoitwa “giza la nje” katika mifano ya Yesu ni wapi? Kuwa katika “giza la nje” ni kuwa katika ufalme wa Mungu, lakini nje ya kundi la wanaume na wanawake ambao uaminifu wao kwa Mungu hapa duniani uliwapatia mahali maalum au nafasi ya pekee yenye mamlaka.

“Giza la nje” si mahali halisi, ni kiwango cha fursa na ushawishi. Sio eneo fulani katika ufalme ambapo watu fulani – wanaume na wanawake – wamepangiwa kukaa. Ni lugha ya mfano tu yenye kueleza nafasi yao ya chini au cheo chao cha chini katika ufalme wa Mungu. (Maneno mepesi ni mkazo wa kwake huyo mwalimu!)

Cha ajabu ni kwamba huyu mwalimu anataka tuamini pia kwamba “kusaga meno” … “si mfano wa kuteseka na maumivu kama ambavyo wengi wamefikiri.” Badala yake – ni mfano wa kutekewa ambako waamini wasiokuwa waaminifu watajisikia huko mbinguni watakapotambua thawabu ambazo wangeweza kuzipata kwa kutii wakiwa duniani. Anasema hivi:

Sawa tu na wale walio waaminifu watakavyofurahi, ndivyo na wale watakaopata hasara watakavyolia. Wakati wengine wakishangiliwa kwa ajili ya uaminifu wao, wengine watasaga meno yao kwa kutekewa kwa sababu ya kutokuona kwao mbali, na uchoyo.

Hatujui huu muda wa furaha na huzuni utadumu muda gani. Wale ambao kazi zao zitateketea hawatalia na kusaga meno yao milele.

Je, hayo yote ni kweli? Je, wakati Yesu alipozungumza juu ya “giza la nje,” alikuwa anazungumza kuhusu mahali mbinguni ambapo Wakristo wasiokuwa waaminifu na wenye choyo watakwenda na kuomboleza kwa muda na kusaga meno yao wakijuta kwa thawabu ambazo wangeweza kuzipata? Ukitaka jibu la swali hilo, angalia Mathayo 8:10-12; 13:24-30, 36-43; 24:42-51; 25:14-30; Luka 13:22-28. Je, watakuwepo watu wenye choyo mbinguni? Ona 1Wakor. 6:9-10; Waefeso 5:3-6.

Inashangaza jinsi ambavyo waalimu wengi watakavyojitahidi kutoa mwanya kwa Wakristo watende dhambi mbaya na bado wafanikiwe kwenda mbinguni. Kwa habari ya maonyo ya Paulo kwamba wale watendao matendo ya mwili hawataurithi ufalme wa Mungu, mhubiri mmoja maarufu sana wa redio anasema hivi:

Mambo ya kuurithi ufalme yanahusiana na zile ziada ambazo unapata katika ufalme. Sio kuingia katika ufalme. Sasa, usipotofautisha kati ya kurithi na kuingia unaweza kufikiri kwamba hutaingia katika ufalme kwa sababu ya matatizo haya [ona: hata hasemi dhambi]. Lakini unaweza kupoteza faida fulani za ufalme kwa sababu ya hayo matatizo.

Je, huo ni ukweli? Hebu fananisha 1Wakor. 6:9-10 na 1Wakor. 15:50-54, na maneno ya Yesu katika Mathayo 25:34-41.

Ingawa Yesu na Paulo walisema kwamba waasherati na wazinzi hawafiki mbinguni, mhubiri mmoja maarufu sana wa televisheni anasema hivi:

Lakini, Wakristo bado wanaweza kupoteza thawabu zao mbinguni. Tunachoweza kujiuliza tu ni jinsi Wakristo wengine watakavyojisikia siku hiyo watakapopoteza thawabu za mbinguni kwa sababu ya kupoa kiroho na matokeo mengine ya uzinzi au uasherati walipokuwa duniani. Kweli, watakuwa wamepoteza thawabu milele mbinguni kwa sababu ya dakika chache tu za starehe ya kujamiiana hapa duniani (Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Mhubiri mwingine maarufu wa redio aliulizwa hivi na msikilizaji:

SWALI: Mimi nadhani kwamba niliokoka nikiwa na miaka kumi na tano. Nilijisikia furaha sana na salama ndani ya Kristo. Lakini muda ulivyokwenda, dhambi iliingia pole pole, nami nikaelekea upotevuni. Nimekuwa katika ndoa mara tatu, nimefanya uasherati, nimelewa pombe. Je, nilikuwa nimeokoka?

JIBU: Kwamba ulisumbuliwa [na hayo mambo] inaonyesha kwamba unaposema uliokoka ukiwa na miaka kumi na tano, ni kweli uliokoka.

Je, kipimo cha uhakika wa wokovu wa mtu ni kujisikia hatia? Ona Warumi 2:14-15 kupata jibu. Je, waasherati na walevi wameokoka? Nadhani unajua jibu lake.

Kwa Nini Mungu Hawasimamishi Hao Manabii Na Waalimu Wa Uongo?

Katika agano la zamani, walikuwepo manabii wa uongo pia ambao walitokea ili kuwapotosha watu wa Mungu. Wao pia wangejulikana kwa matunda yao. Maisha yao na maneno yao yalitoa ushuhuda kuhusu uchafu wao wa ndani, na walipopuuzia umuhimu wa utakatifu, waliwaongoza watu na kuwapotosha wasimtii Mungu kwa moyo wote.

Tunaweza kuuliza kwa nini Mungu hawazuii manabii wote wa uongo na waalimu au kwa namna fulani awanyamazishe wakati wanapotoa matamko yasiyokuwa ya Biblia, yenye kuigeuza neema ya Mungu kuwa ufisadi. Pengine jibu linapatikana katika neno la Mungu kupitia mmojawapo wa manabii Wake wa kweli aliyeitwa Musa.

Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, ‘Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye. Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya BWANA, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru BWANA, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako (Kumbu. 13:1-5. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Je, kweli Mungu huwaruhusu waalimu wa uongo waeneze mafundisho yao ili kutupima? Basi, inaonyesha nini juu yetu wakati tunapovutwa kufuata mafundisho yenye kutufanya tujisikie vizuri juu ya dhambi zetu na hata kutupotosha tuondoke kwenye njia za haki? Hili ni jambo la kufikiria.

Je, wenye uwezo wa kutambua wafanyeje? Chini ya agano la zamani, walitakiwa waondoe kati yao wale wote waliojaribu kuwashawishi waondoke “kwenye njia ambayo Bwana Mungu wao aliwaagiza waipitie”. Adhabu ilikuwa kifo.

Tunajua kwamba kanisa halina ruhusa ya kuua watu, lakini hii haimaanishi kwamba waalimu wa uongo wavumiliwe tu. Labda kwa kuanzia, wanatakiwa kukabiliwa kwa upendo na kurekebishwa, isije kuwa wanakosea kwa sababu ya kutokujua Biblia. Wengi wao wanarudia tu kama kasuku mambo waliyosoma kwenye vitabu vya wengine. Wale ambao hawataacha kueneza upotofu wao huo wafichuliwe na wasisaidiwe kwa njia yoyote ile ili “huduma” zao zife (ona 3Yohana mstari wa 9 na 10). Wachache sana wataendelea kwa muda mrefu kama watu wataacha kuwapa fedha na kununua vitabu vyao na kanda zao.

Lakini, ujue kwamba chochote kile tutakachofanya, waalimu wa uongo watakuwepo mpaka mwisho, kwa sababu Biblia inasema hivyo (ona 1Timo. 4:1-3; 2Timo. 3:13; 4:3-4). Paulo anaeleza juu yao katika onyo analotoa kwa Wakristo Warumi kwamba wao si watumwa wa “Bwana wetu Yesu Kristo”. Maana yake ni kwamba hawajaokoka.

Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu (Warumi 16:17-18. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Basi tujihadhari!

Mahubiri Makuu Ya Yesu Kuhusu Wokovu, 2

SURA YA SABA

 

Ni wachungaji wangapi wangeona wameheshimiwa sana kama mtu angewaita “mhubiri wa utakatifu”? Ni wangapi wanaojiita Wakristo wangetumia maneno hayo kwa njia ambayo si ya kudhihaki? Mbona utakatifu ni somo baya sana mawazoni mwa watu wengi wanaodai kuamini kitabu ambacho kina maneno mtakatifu au utakatifu zaidi ya mara mia sita, chenye kuwaahidi wakati ujao katika mji mtakatifu ambamo ndani yake anakaa “Aliye mtakatifu”, ambaye jina Lake ni mtakatifu, anayewapa Roho Wake Mtakatifu na ambaye kiti Chake cha enzi kitakatifu kimezungukwa na wenye uhai wanne wasioacha kusema usiku na mchana, “Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu ni Mungu Mwenyezi”? (ona Ufunuo 21:2; Isaya 40:25; Walawi 22:32; 1Wathes. 4:8; Zaburi 47:8; Ufunuo 4:8 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Kama sehemu ya kwanza ya Mahubiri ya Mlimani imetufundisha kitu, ni kwamba Yesu alikuwa mhubiri wa utakatifu. Hiyo ndiyo iliyokuwa mada Yake – utakatifu, na jinsi unavyohusiana na wokovu.

Mahubiri ya Mlimani yameandikwa katika Injili ya Mathayo sura ya 5, 6 na 7. Mpaka sasa tumetazama sura ya 5 tu. Hapo, katika zile “Heri” tulijifunza tabia au sifa za wanaokwenda mbinguni. Pia tuligundua kwamba Yesu hakuja kuibatilisha au kuiondoa Torati, na kwamba kushika sheria ni muhimu sana. Tulijifunza kwamba hatuwezi kuingia katika ufalme wa mbinguni kama haki yetu haitazidi ile ya waandishi na Mafarisayo, walioishika sheria kama ilivyokuwa ila wakapuuza maana yake.

Sehemu ya pili ya Mahubiri ya Mlimani – yaani Mathayo 6 na nusu ya kwanza ya sura ya 7 – ina amri zingine tena ambazo Kristo aliwapa wafuasi Wake. Je, kuzishika kunahusika kwa lolote na wokovu? Hakika kabisa. Sehemu ya mwisho ya sura ya saba inaonyesha jambo hilo waziwazi kabisa, kama tutakavyoweza kujionea.

Hebu tuendelee kusoma yale ambayo Yesu aliwaagiza wafuasi Wake wa kweli, ambao waliamini kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, ni Masiya. Tujiulize swali hili, zito kabisa: Ikiwa wasikilizaji wa Yesu hawakumwamini, walimtii kwa sababu gani? Mbona watake hata kusikiliza akifanya madai ambayo yangeathiri kila eneo la maisha yao? Jibu ni wazi: Kwa kuwa waliamini, walitaka kutii. Wangeonyesha imani yao kwa matendo yao.

Sura Ya Sita Inaanza

Ona katika sehemu hii ya kwanza Yesu anahesabu kwamba wafuasi Wake watatenda haki, naye anawaonya wahakikishe kwamba makusudi yao ni kumpendeza Mungu badala ya kuwapendeza watu.

“Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe ya siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:1-4 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Yesu alitazamia kabisa kwamba wafuasi Wake wangetoa sadaka kwa maskini (kama tulivyojifunza katika sura ya 3 ya kitabu hiki). Torati iliagiza hivyo (ona Kutoka 23:11; Walawi 19:10; 23:22; 25:35; Kumbu. 15:7-11), na waandishi na Mafarisayo walifanya hivyo kwa kupiga matarumbeta, kwa kusudi la kuwafanya watu maskini waone utoaji wao. Lakini – ni wangapi wanaojiita Wakristo (na hata makanisa ya Kikristo) wanaotoa chochote kwa maskini? Hawajafikia hata mahali pa kutaka kuchunguza makusudi yao ya utoaji zaka! Kama uchoyo na ubinafsi uliwasukuma waandishi na Mafarisayo kutangaza kutoa kwao sadaka, ni nini kinachowasukuma wanaojiita Wakristo kupuuza hali ya maskini? Je, haki yetu inazidi ile ya waandishi na Mafarisayo?

Kama ambavyo Paulo atarudia katika 1Wakorintho 3:10-15, tunaweza kufanya matendo mema ambayo hayatapata thawabu ikiwa nia na makusudi yetu si safi. Wafuasi wa kweli wa Kristo wanapaswa kuwa na nia safi katika kila tendo jema, lakini si wote walio nayo. Paulo aliandika kwamba inawezekana hata kuihubiri Injili kwa makusudi yasiyo safi (ona Wafilipi 1:15-17). Njia iliyo bora ya kuhakikisha kwamba kutoa kwetu kunasukumwa na makusudi safi ni kutoa kwa siri kiasi iwezekanavyo.

Yesu pia aliwatazamia wafuasi Wake waombe na kufunga. Hiyo ilikuwa lazima. Hakusema “Kama mtaomba”. Alisema “Mwombapo”. Hatari ilikuwa wangeweza kuyaruhusu makusudi yao kuchafuka, kama ilivyokuwa kwa makusudi ya wasioamini waliokuwa wanaomba na kufunga. Kama hayo yangetokea, wangepoteza thawabu ile ambayo wangepata kama makusudi yao yangekuwa safi. Basi aliwapa mashauri yafuatayo:

“Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayoyahitaji kabla ninyi hamjamwomba…”

“Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso, ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:5-8; 16-18).

Narudia tena: Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo ambao hawatumii muda wao mwingi katika maombi, na ambao hawajawahi kufunga kabisa? Haki yao inalinganishwaje na haki ya waandishi na Mafarisayo, ambao walifunga na kuomba (japo kwa sababu mbaya)?

Kuomba Kitakatifu

Yesu pia aliwaambia wanafunzi Wake jinsi walivyotakiwa kuomba. Maombi Yake mfano ni ufunuo wa hali ya juu sana kuhusu matazamio Yake kwa habari ya pendo lao, utii wao na vipaumbele.

“Basi ninyi salini hivi: ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu’.” (Mathayo 6:9-11)

Jambo la kwanza muhimu sana kwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu iwe jina la Mungu litukuzwe. Yaani, jina la Mungu liheshimiwe, liabudiwe na kutakatifuzwa.

Bila shaka wale wanaoomba kwamba jina la Mungu litukuzwe wanatakiwa wao wenyewe kuwa watakatifu, wanaolitukuza jina la Mungu. Itakuwa ni unafiki kufanya vinginevyo. Kwa hiyo, sala hii inaonyesha shauku yetu kwamba na wengine wajinyenyekeze kwa Mungu kama ambavyo sisi tumefanya. Na – kama nilivyouliza katika sura nyingine hapo nyuma – mtu anaonyeshaje kiwango cha shauku yake kwamba anataka jina la Mungu litakaswe kama anajistarehesha kwa kutazama picha ambazo zinachezwa na wachezaji wenye kutumia vibaya jina la Mungu na la Mwana Wake? Kulingana na uchunguzi wangu, hiki ni kitu ambacho wengi wanaojiita Wakristo hufanya mara kwa mara. Je, wewe ungechukizwa na sinema ambayo waigizaji wanatumia jina lako kama neno la kuapa au kushangaa?

Ombi la pili katika sala hiyo linafanana na la kwanza: “Ufalme wako uje.” Wazo la ufalme huonyesha kwamba kuna Mfalme anayetawala ufalme Wake. Mwanafunzi Mkristo anatamani kuona mfalme Wake – yule atawalaye maishani mwake – akitawala dunia nzima. Laiti kila mtu angepiga goti lake kwa Mfalme Yesu, katika imani tiifu!

Ombi la tatu linarudia yale mawili ya kwanza: “Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.” Hapa tena – tunawezaje kuomba kwa dhati ombi la namna hii bila sisi wenyewe kuwa tumejinyenyekeza chini ya mapenzi ya Mungu katika maisha yetu? Mwanafunzi wa kweli anatamani kwamba mapenzi ya Mungu yatafanyika duniani kama huko mbinguni – kikamilifu na kabisa.

Kwamba jina la Mungu litakaswe, na mapenzi Yake yafanyike, na ufalme Wake uje vinatakiwa kuwa muhimu zaidi kwetu kuliko chakula cha kutuhifadhi, au “riziki yetu”. Hili ombi la nne linawekwa hapo kwa sababu. Inaonyesha mpangilio mzuri wa mambo ya muhimu maishani mwetu, na hakuna dalili za uchoyo hapo. Huyu mwanafunzi anayeomba anamtumikia Mungu, si mali.

Sala ‘Mfano’ Inaendelea

Mpaka hapa mada ya utakatifu inatokezea katika kila ombi la sala hii. Na inaendelea kujitokeza katika mistari yake ya mwisho.

“ ‘Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele, Amina’. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu” (Mathayo 6:2-15).

Mwanafunzi wa kweli wa Yesu anatamani kuwa mtakatifu, kwa hiyo, anapotenda dhambi, anasumbuliwa sana. Yeye hutambua kwamba kutokutii kwake kumemkwaza Mungu, na anajisikia aibu. Anataka doa la uchafu huo liondolewe, na shukrani ni kwamba, Baba yake wa mbinguni mwenye neema, yuko tayari kumsamehe. Lakini lazima aombe msamaha, ambalo ndiyo ombi la tano lipatikanalo katika sala ya Bwana.

Lakini, kusamehewa kwetu kunategemeana na sisi kuwasamehe wengine. Kwa sababu tumesamehewa vingi, tunawajibika kumsamehe kila mtu anayetuomba msamaha sisi, na kuwapenda wale ambao hawatuombi msamaha. Tukikataa kusamehe, Mungu hatatusamehe sisi.

Ombi la sita na la mwisho pia linahusiana na utakatifu, kwamba, “Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu [au, kutoka maovuni].” Mwanafunzi wa kweli anatamani utakatifu kiasi cha kwamba anamwomba Mungu hata asimwongoze katika hali ambapo anaweza kujaribiwa, asije akashindwa. Tena, anaomba kwamba Mungu amwokoe kutokana na uovu wowote unaoweza kumnasa. Hili ombi la mwisho katika sala ‘mfano’ ya Yesu si kitu kingine: ni kilio kwamba Mungu asaidie katika utakatifu.

Kwa nini maombi yote hayo sita katika sala hii yanayofaa? Mstari wa mwisho unatuambia: Mungu ni Mfalme mkuu anayetawala ufalme Wake, ambamo ndani yake sisi ni watumishi Wake. Ana nguvu zote, na hakuna anayetakiwa kuthubutu kupinga mapenzi Yake. Utukufu wote utakuwa Wake milele – “Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele” (Mathayo 6:13). Yeye ndiye wa kumtii, na anastahili hivyo.

Nini kiini kikuu cha sala ya Bwana? Utakatifu. Wanafunzi wa Kristo wanatamani kwamba jina la Mungu litakaswe, ufalme Wake uthibitishwe duniani, na kwamba mapenzi Yake yafanyike kila mahali kikamilifu. Hii ni muhimu sana kwao kuliko hata chakula chao cha kila siku. Wao wanataka kumpendeza, na wakishindwa, wanaomba msamaha kutoka Kwake. Kama watu waliosamehewa, wanawasamehe na wengine. Wanataka kuwa watakatifu na wakamilifu mpaka wanatamani waepuke majaribu, kwa sababu majaribu huongeza nafasi zao za kutenda dhambi.

Mwanafunzi Na Mali Zake

Mada ya pili katika Mahubiri ya Mlimani ndiyo inayosumbua zaidi kwa wanaojiita Wakristo, ambao lengo lao kubwa maishani ni kupata vitu au mali.

“Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! Hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” (Mathayo 6:19-24).

Yesu aliagiza kwamba tusijiwekee hazina duniani. Sasa, hazina ni nini? Hazina za kweli zinawekwa kwenye masanduku ya hazina na kuhifadhiwa mahali, wala hazitumiwi kwa chochote cha maana. Yesu alifafanua kwamba ni vitu vinavyosababisha nondo, kutu na wevi. Kwa maneno mengine, “visivyo kuwa vya lazima”. Nondo hula vile tunavyoweka katika stoo zetu na pande za ndani sana za makabati yetu, si zile nguo tunazovaa mara kwa mara. Kutu hula vitu vya kuchezea na “vifaa” ambavyo hatuvitumii, vilivyolundikwa katika pembe za vyumba, katika stoo na mahali pa kuhifadhi vitu. Wevi nao huvunja na kuiba vitu ambavyo watu wengi hawavihitaji: picha, vipodozi, vitu vya thamani, na kitu kinachoweza kuuzwa kwa urahisi na kwa haraka. Si mara nyingi waibe vitanda, majiko, vyakula au viatu vya raba au kanda mbili.

Cha kuona hapo ni kwamba sisi ni wa Mungu na vyote “tulivyo navyo”. Sisi ni mawakili wa fedha za Mungu. Basi, kila uamuzi wa kutumia fedha ni uamuzi wa kiroho. Tunachofanya na fedha zetu huonyesha nani anayetawala maisha yetu. Tunapolimbikiza “hazina”, kuficha fedha na kununua visivyo muhimu, tunadhihirisha kwamba si Yesu anayetawala, kwa sababu angekuwa anatawala, tungefanya vitu bora zaidi na fedha zile alizotukabidhi.

Hivyo vilivyo bora zaidi ni kama vitu gani? Yesu anatuagiza kuweka hazina mbinguni. Tunawezaje kufanya hivyo? Anatuambia katika Injili ya Luka: “Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyeni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu” (Luka 12:33). Kwa kutoa ili kusaidia watu, tunajiwekea akiba mbinguni. Yesu anatuambia tuchukue kile ambacho hakika kitapoteza thamani tukiwekeze katika kitu ambacho hakitapoteza thamani kamwe. Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo wanaofanya hivyo? Ni kwa nini idadi kubwa ya wanaojiita Wakristo wa Marekani, ambao wanafurahia kiwango cha juu cha maisha kuliko wengine wote duniani, hawatoi hata kiasi cha asilimia kumi tu ya mapato yao, ambacho ndicho kiwango cha chini kabisa kilichodaiwa na Torati? Hebu niongeze tu kwamba hiyo sheria ya zaka ilikuwa katika Torati ile ambayo katika mahubiri haya haya, Bwana Yesu alisema hakuja kuitangua.

Jicho Bovu

Je, Yesu alikuwa na maana gani alipozungumza juu ya jicho kuwa “taa ya mwili”? Bila shaka maneno Yake yalihusu jinsi tunavyotazama fedha na vitu, kwa sababu hayo ndiyo aliyozungumzia kabla na baada ya kusema hilo.

Hapa tena, Yesu alikuwa analinganisha watu wa aina mbili: mmoja mwenye jicho safi, ambaye mwili wake wote umejaa nuru, na mwingine mwenye jicho bovu ambaye mwili wake wote umejaa giza. Katika mistari inayofuata, Yeye pia analinganisha watu aina mbili: waliookoka na wasiookoka – mmoja anamtumikia Mungu na mwingine anatumikia fedha. Basi, ni salama kuhitimisha kwa kusema kwamba yule mwenye jicho safi ni mtu anayemtumikia Mungu, na yule mwenye jicho bovu ni mtu anayetumikia fedha.

Mtu mwenye jicho safi ni mfano wa yule anayetafuta ukweli, naye anaruhusu nuru ya kweli kuingia ndani yake. Anamtumikia Mungu. Mtu mwenye jicho baya hufungia nje mwanga wa kweli usiingie ndani yake, kwa sababu anafikiri yeye anao ukweli tayari, na kwa njia hiyo anajaa giza maishani mwake, akiamini mambo ya uongo. Yeye anaamini kwamba kusudi la maisha yake ni kujitosheleza. Fedha ndiyo mungu wake.

Nini maana ya fedha kuwa mungu wako? Maana yake ni kwamba fedha inakuwa na nafasi maishani mwako ambayo inatakiwa kukaliwa na Mungu tu. Fedha inatawala maisha yako na kuyaongoza. Inakula nguvu zako zote, mawazo yako na muda wako wote. Ndiyo asili kuu ya furaha yako. Unaipenda. Ndiyo sababu Paulo alilinganisha tamaa (au choyo) na kuabudu sanamu, akisema kwamba hakuna mchoyo au mwenye tamaa yeyote atakayeurithi ufalme wa Mungu (ona Waefeso 5:5; Wakolosai 3:5-6).

Mungu na fedha hutaka kuwa bwana katika maisha yetu, na Yesu alisema hatuwezi kutumikia wote wawili. Ona pia kwamba chaguo pekee linalotajwa kwa upande wa Mungu ni kumtumikia Yeye. Hakuna uchaguzi wa kumwamini Yeye bila kumtumikia au kumfuata. Kama tutamtumikia na kumfuata, atakuwa Bwana juu ya mali zetu. Hiyo si hatua ya kuchukuliwa siku zijazo wakati fulani “wa kujitoa zaidi”. Ni hatua inayochukuliwa wakati wa kuokoka kweli kweli.

Maskini Mwenye Tamaa

Kutaka sana kupata vitu si vibaya tu ikiwa vinavyotakiwa ni vitu vya anasa – yawezekana mtu kutaka sana vitu hata kama ni mahitaji ya msingi. Hicho nacho ni kitu kibaya. Yesu aliendelea hivi:

“Kwa sababu hiyo nawaambieni, ‘Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba jinsi yameavyo; hayafanyi kazi wala hayasokoti, nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojwapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke basi mkisema, Tule nini? Au, Tunywe nini? Au, Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi, msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake’.” (Mathayo 6:25-34)

Wasomaji wengi wa kitabu hiki hawawezi kujifananisha na wale watu ambao Yesu alikuwa anazungumza nao. Jiulize hivi: Mara ya mwisho ulipokuwa na wasiwasi juu ya kuwa na chakula, kinywaji au mavazi ni lini?

Lakini, maneno ya Yesu yanatuhusu hata sisi. Kama ni makosa kuhangaika kwa sababu ya mambo ya lazima maishani, bila shaka ni makosa makubwa zaidi kuhangaika kwa sababu ya mambo yasiyokuwa ya lazima! Yesu anawatazamia wanafunzi Wake kujihusisha zaidi na kutafuta vitu viwili: ufalme Wake na haki Yake. Wakati mtu anayejiita Mkristo anaposhindwa kutoa zaka, lakini anaweza kununua chakula cha mbwa, na kulipia kodi ya kutumia televisheni, na kulipia gari jipya au fanicha alizokopa, na kununua nguo za mitindo mipya, au kununua chakula cha starehe – je, anaishi kulingana na kiwango cha Kristo cha kutafuta kwanza ufalme Wake na haki Yake? Hapana! Huyo anajidanganya tu kama anafikiri kwamba ni mfuasi wa Yesu.

Vibanzi Na Boriti

Amri zinazofuata za Yesu kwa wafuasi Wake zinahusu dhambi ya kuwahukumu wengine na kupata makosa kwa watu. Anasema hivi:

“Msihukumu, msije mkahukumiwa na ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho ndicho mtakachopimiwa. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, ‘Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako;’ na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako” (Mathayo 7:1-5).

Nini maana ya kumhukumu mtu mwingine? Hakimu ni mtu anayetafuta makosa katika watu wanaofikishwa mahakamani. Hiyo ndiyo kazi yake, na hakuna kosa kufanya hivyo, mradi tu afanye hukumu yake kulingana na kweli zilizothibitishwa. Mahakimu wanapaswa kuhukumu watu, wakiwapima kwa kiwango cha sheria ya nchi. Kama wasingekuwepo mahakimu, wahalifu wasingefikishwa kwenye sheria.

Lakini, watu wengi wanafikiri kwamba wamechaguliwa kuwa mahakimu. Basi, kila wakati wanachofanya ni kutafuta makosa kwa wengine. Hilo ni kosa. Tena, mara nyingi wanawahukumu watu kimakosa, pasipo kujua ukweli wote. Kibaya zaidi ni kwamba, hao mahakimu wa kujifanya mara nyingi huwapima watu kwa viwango ambavyo wao wenyewe hawaviwezi, na kujifanya wanafiki kwa tendo hilo. “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kutupa jiwe” (Yohana 8:7).

Tabia aina hiyo ndiyo Yesu alikuwa anazungumzia. Mtume Yakobo aliandika hivi: “Ndugu! Msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango” (Yakobo 5:9). Hii ni dhambi moja ambayo ni kubwa sana katika kanisa siku hizi, na wale ambao wana hatia ya kuwahukumu wengine hujiweka kwenye nafasi hatari ya kuhumiwa na wao. Tunapozungumza kinyume cha mwamini mwingine, tukionyesha makosa yake kwa wengine, tunajifanya mahakimu. Tunaivunja amri kuu kwa sababu, sisi hatupendi wengine watuseme vibaya tukiwa hatupo. Na tunapozungumza na mwamini mwingine juu ya makosa yake wakati sisi wenyewe tuna makosa makubwa zaidi tunakuwa sawa na yule mtu mwenye boriti katika jicho lake. Lawama kwa upendo na kwa kusudi la kujenga zinapaswa kutolewa na mtu ambaye hana matatizo kama au zaidi ya huyo anayesaidiwa. Watu wengi wa kiroho ninaowafahamu mimi hawatoi ushauri mwingi bila ya kuombwa, kwa sababu wanajua kwamba watu wengi hawataki kusikiliza ushauri. Pengine hiyo ndiyo maana ya Yesu katika maneno aliyosema katika mstari huu, kwamba:

“Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua” (Mathayo 7:6).

Pia, Mithali moja inasema: “Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda” (Mithali 9:8).

Himizo Kusali

Hatimaye tunafika kwenye sehemu ya mwisho ya mahubiri ya Yesu. Sehemu hii inaanza kwa ahadi za kutia moyo sana juu ya sala, kama ifuatavyo:

“Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa. Kwa maana, kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu ambaye, mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” (Mathayo 7:7-11).

Kuna msomaji anasema, “Aha! Hii sehemu ya Mahubiri ya Mlimani haihusiki na mambo ya utakatifu.”

Inategemeana na kile tunachoomba, tunachobishia hodi na tunachotafuta katika sala. Sisi kama wenye “njaa na kiu ya haki” tunatamani kutii kila kitu ambacho Yesu ameagiza katika mahubiri yaliyotangulia, na shauku hiyo inaonekana katika sala zetu. Ukweli ni kwamba, ile sala ‘mfano’ ambayo Yesu alifundisha katika mahubiri Yake hapo nyuma ni maonyesho ya shauku kwamba mapenzi ya Mungu yafanyike, na utakatifu upatikane. Tena, tukisoma ahadi za sala kama zipatikanavyo katika Injili ya Luka, maneno yafuatayo ndiyo yanayomalizia: “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13). Bila shaka Yesu hakuwa anafikiri juu ya magari ya kulala ndani au mitumbwi ya kustarehe wakati alipotuahidi “vipawa vyema”. Kwa mawazo Yake, Roho Mtakatifu ni “kipawa chema” kwa sababu Roho Mtakatifu hutufanya watakatifu na hutusaidia kueneza Injili inayowafanya wengine kuwa watakatifu. Na watakatifu wanakwenda mbinguni.

Hitimisho

Sasa tunafikia mstari ambao unaweza kuhesabika kuwa hitimisho la kila kitu ambacho Yesu amesema mpaka hapa. Wataalamu wengi wa Biblia wanashindwa kuuona, lakini ni muhimu sisi tusiukosee. Mstari huu bila shaka ni maneno ya kuhitimisha, maana unaanza kwa neno “basi”. Unaunganika na yale mafunzo yaliyotangulia, na swali ni hili: Je, unafanya majumuisho kiasi gani cha maneno ya Yesu? Tuusome na kufikiri juu yake.

“Basi yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii” (Mathayo 7:12).

Maneno hayo si hitimisho la mistari michache iliyotangulia – yenye kuzungumza juu ya sala – kwa sababu kama ni hivyo, haileti maana.

Kumbuka mapema kabisa katika mahubiri Yake kwamba Yesu alikuwa ameonya kuhusu kosa la kudhani kwamba amekuja kuibatilisha Torati na manabii (ona Mathayo 5:17). Tangu hapo mpaka mstari huu tunaotazama sasa, hajafanya kitu kingine chochote isipokuwa kuunga mkono, kufafanua na kueleza zaidi amri za Mungu katika Agano la Kale. Kwa hiyo, sasa anahitimisha kila kitu alichoamuru – yaani, vyote alivyotaja kutoka kwenye Torati na Manabii, hivi: “Basi yoyote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo Torati na manabii” (7:12). Maneno “Torati na Manabii” huunganisha kila kitu alichosema Yesu kati ya Mathayo 5:17 na 7:12.

Uhusiano kati ya wokovu na kushika kile tunachokijua sasa kuwa ni “Amri Kuu” unawekwa wazi katika mistari miwili inayofuata, inayosema hivi:

“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache” (Mathayo 7:13-14).

Bila shaka mlango ule mwembamba na njia iendayo uzimani ambayo wachache wanaiona ni mfano wa wokovu. Mlango ule mpana na njia pana iendayo upotevuni, ambayo ni ya wengi, ni mfano wa kupotea. Kama kila kitu ambacho Yesu alisema kabla ya maneno haya kina maana, na kama mahubiri haya yanakwenda kwa mpangilio, na kama Yesu alikuwa msemaji mzuri mwenye kutumia ufahamu Wake, basi tafsiri ya kimsingi kabisa ni kwamba njia ile nyembamba ni njia ya kumfuata Yesu, kutii amri Zake. Njia ile pana ni tofauti ya hayo. Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo wanaopita kwenye ile njia nyembamba ambayo Yesu aliifunua katika Mathayo 5:17 hadi 7:12? Kama wewe ni mtu unayekwenda na wengi, ujue uko kwenye njia iliyo pana.

Inasumbua kwa wengi wanaojiita Wakristo kwamba Yesu hakusema chochote juu ya imani au kumwamini Yeye katika mahubiri haya ya wokovu. Lakini, wale ambao wanaelewa kwamba imani na mwenendo havitenganishwi hawapati shida na mahubiri haya. Watu wanaomtii Yesu huonyesha imani yao kwa matendo yao. Wale wasiomtii hawaamini kwamba ni Mwana wa Mungu. Tena, si wokovu tu ulio ishara ya neema ya Mungu kwetu, bali hata yale mabadiliko ambayo yametokea maishani mwetu. Kwa kweli, utakatifu wetu ni utakatifu Wake.

Jinsi Ya Kutambua Viongozi Wa Kidini Wa Bandia

Baada ya hayo, Bwana Yesu aliwaonya wasikilizaji Wake juu ya manabii wa uongo, viongozi wa kidini wenye kuwaongoza wasiofikiri kuifuata njia pana iendayo upotevuni. Kuna wale ambao ujumbe wao hautoki kwa Mungu kabisa, na waalimu wa uongo wanaangukia katika fungu hili pia. Wanawezaje kutambulika kwamba ni waongo? Kwa njia ile ile ya kuwatambua waamini wa bandia.

“Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua. Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana! Hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?’ Ndipo nitawaambia dhahiri, ‘Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu’.” (Mathayo 7:15-23).

Waalimu wa uongo ni wadanganyifu sana. Wana mambo ya nje yenye kuonyesha kwamba pengine ni watu sawa. Wanaweza kumwita Yesu Bwana wao, wanaweza kutoa unabii, wanaweza kutoa pepo na hata kutenda miujiza. Lakini yale “mavazi ya kondoo” yanaficha “mbwa-mwitu mkali.” Wao si kondoo kihalisi. Itajulikanaje kama ni wa kweli au si wa kweli? Tabia yao ya kweli itajulikana kwa kutazama “matunda” yao.

Je, hayo matunda anayozungumzia Yesu ni matunda gani? Ni matunda ya utii kwa kila kitu alichofundisha. Wale ambao ni wa kweli hufundisha na kufanya mapenzi ya Baba. Wale ambao si wa kweli hufundisha kisichokuwa kweli na hutenda “maovu” (7:23). Basi, wajibu wetu sisi ni kulinganisha maisha yao na mafundisho yao na kile ambacho Yesu alifundisha na kuamuru.

Waalimu wa uongo ni wengi sana siku hizi kanisani, nasi hatupaswi kushangaa kwa sababu Yesu pamoja na Paulo walituonya kwamba, kadiri siku za mwisho zinavyokaribia, tutazamie hayo (ona Mathayo 24:11; 2Timo. 4:3-4). Manabii wa uongo ambao ni maarufu katika siku zetu ni wale wenye kufundisha kwamba mbingu inawangojea wale ambao si watakatifu. Wao wanawajibika kwa kupotea kwa mamilioni ya watu. John Wesley – mhubiri maarufu wa siku zilizopita – aliandika hivi juu yao:

“Ni kitu kibaya sana wakati mabalozi wa Mungu wanapogeuka kuwa mawakala wa Shetani! Wakati wale walioagizwa kuwafundisha watu njia ya kwenda mbinguni wanapofundisha njia ya kwenda jehanamu. Nikiulizwa, ‘Nani wamewahi kufanya hivyo?’ jibu langu ni rahisi tu: ‘Makumi elfu ya wenye hekima na heshima kubwa; wale wote wa dhehebu lolote, wanaowatia moyo – wenye kiburi, wenye tamaa, wenye dhihaka, wenye kuipenda dunia, wanaopenda starehe na anasa, wasiokuwa wema, watu wa ovyo-ovyo, wasiojali, wasiodhuru, watu wasiopatikana na mateso kwa sababu ya haki – kwamba wako njiani kwenda mbinguni.’ Hao ni manabii wa uongo wa hali ya juu sana. Hao ni wasaliti, wa Mungu na mwanadamu. Wanawaelekeza watu kuingia katika dunia ya giza; na wakati wao utakapofika kuwafuata hao maskini waliowaangamiza, “kuzimu chini itataharuki” kuwalaki!”

Cha kupendeza ni kwamba Wesley alikuwa anafafanua kuhusu waalimu wa uongo ambao Yesu alionya juu yake katika Mathayo 7:15-23.

Ona tena kwamba Yesu anazungumza wazi kabisa – kinyume na jinsi waalimu wengi wa uongo wanavyotuambia siku hizi – kwamba wale wasiozaa matunda mazuri watatupwa jehanamu (ona 7:19). Hayo hayatawapata waalimu tu na manabii, bali kila mmoja. Yesu alisema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21). Niwie radhi nikirudia kusema tena kwamba haya ni mahubiri kuhusu mlingano kati ya wokovu na utakatifu. Watu ambao hawamtii Yesu wanakwenda jehanamu.

Pia ona Yesu alivyounganisha jinsi mtu alivyo ndani na jinsi alivyo nje. Miti “mizuri” huzaa matunda mazuri. Miti “mibaya” haiwezi kuzaa matunda mazuri. Chanzo cha matunda mazuri ambayo huonekana kwa nje ni asili ya mtu kwa ndani. Mungu amebadilisha asili ya wale watu ambao wamemwamini Yesu kweli kweli.

Kumalizia

Yesu anamalizia mahubiri Yake yote kwa mfano. Bila shaka ni mfano wenye kuonyesha mahusiano kati ya wokovu na utii.

“Basi, kila asikiaye hayo maneno yangu na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa” (Mathayo 7:24-27).

Mfano wa mwisho wa Yesu si “njia ya kufanikiwa maishani” kama wengine wanavyotumia. Mada siyo jinsi ya kufanikiwa kifedha wakati mambo ni magumu, kwa kuziamini ahadi za Yesu. Hili ni hitimisho la yote ambayo Bwana Yesu alisema katika Mahubiri Yake pale Mlimani. Wale wanaotenda aliyosema ni wenye hekima nao watadumu; hawana haja ya kuogopa ghadhabu au hasira ya Mungu. Wale wasiomtii Yeye ni wapumbavu na watateseka kweli, na kupata “adhabu ya kuangamia milele” (2Wathes. 1:9).

Kujibu Hoja Inayopinga

Je, haiwezekani kwamba Mahubiri ya Yesu pale Mlimani yaliwahusu wafuasi Wake walioishi kabla ya kifo Chake na kufufuka? Wao si walikuwa chini ya Torati, ambayo ilikuwa njia yao ya wokovu wakati huo, lakini baada ya Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zao wakaokolewa kwa imani, kitu kilichobatilisha njia ile ya wokovu inayotajwa katika mahubiri haya?

Nadharia hiyo ni mbaya. Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuokolewa kwa matendo yake wakati wowote. Kila mara imekuwa ni kwa imani – kabla ya Agano la Kale na hata wakati wa Agano la Kale. Paulo anaonyesha katika Warumi 4 kwamba Ibrahimu alihesabiwa haki kwa imani, sio kwa matendo.

Zaidi ya hapo, ilikuwa vigumu kabisa kwa yeyote katika wasikilizaji wa Yesu kuokolewa kwa matendo, maana wote walikuwa wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu (ona Warumi 3:23). Ni neema ya Mungu tu ndiyo ingewaokoa, na imani tu ndiyo yenye uwezo wa kupokea neema Yake.

Bahati mbaya sana ni kwamba, wengi katika kanisa siku hizi huziona zile amri zote za Yesu kwamba hazina kusudi lingine isipokuwa kutufanya tujisikie hatia, ili tuone jinsi isivyowezekana kupata wokovu kwa matendo. Sasa, kwa kuwa “tumepata ujumbe” na kuokolewa kwa imani, tunaweza kupuuzia amri Zake karibu zote. Isipokuwa kama tunataka wengine nao “waokoke”. Ndipo tunapoweza kuchomoa tena zile amri na kuwaonyesha watu jinsi walivyo wenye dhambi ili nao waweze kuokolewa kwa “imani” isiyo na matendo.

Yesu hakuwaambia wanafunzi Wake hivi: “Enendeni ulimwenguni mwote mkawafanye watu kuwa wanafunzi. Halafu, hakikisheni kwamba, wakisha jua wana hatia na kuokolewa kwa imani, amri Zangu zimemaliza makusudi yake maishani mwao.” Aliwaambia kama ifuatavyo: “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi … na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi …” (Mathayo 28:19-20 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Utakaso: Kukamilisha Utakatifu

SURA YA NANE

“Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30).

Wanaojiita Wakristo wachache sana wangebisha kwamba mistari hiyo hapo juu ni mwaliko kutoka kinywani kwa Yesu, akiwaita watu waokoke. Mara nyingi sana maandiko hayo hutumiwa kwenye mikutano ya uinjilisti. Yesu alikuwa anatoa pumziko kwa waliochoka. Bila shaka hakuwa anasema juu ya mapumziko kimwili kwa waliochoka kimwili. Alikuwa anaahidi pumziko kwa ajili ya nafsi au roho (ms. 29) ambazo zimelemewa na dhambi na hatia. Alikuwa anatoa wokovu. Lakini, wokovu huo unapokelewaje? Yesu alisema unapatikana kwa kujitia nira Yake.

Labda tafsiri inayopendwa sana na wale wanaopinga kushika sheria kuhusu maana ya kujitia nira ya Yesu ni hii: Fikiri kwamba Yesu amevaa nira yenye pande mbili ambayo anataka tuishiriki. “Uthibitisho” wa tafsiri hiyo ni kwamba Yesu anasema hiyo nira ni “Yangu” kuonyesha kwamba bila shaka ni nira ambayo iko shingoni Mwake. Sasa, yule asiyeamini kushika sheria anasema, “Sawa! Yesu hamaanishi kwamba anataka kuihamishia hiyo nira shingoni mwangu kutoka Kwake. Maana yake ni kwamba amevaa nira yenye sehemu mbili, kwa ajili ya maksai wawili! Basi, anataka mimi “nifungiwe nira” na Yeye kwa imani, ili tuunganishwe pamoja katika safari yetu kwenda mbinguni.”

Lakini, hiyo tafsiri ambayo imekwenda mbali kiasi hicho inakosa kuelewa kitu. Kujitia nira ya Yesu ni mfano wa kujinyenyekeza chini ya mamlaka Yake. Yeye hana nira yenye pande mbili shingoni kwake ambayo anataka sisi tushirikiane Naye kuivaa. Yeye – kama Bwana – ameshikilia nira mikononi Mwake, akiwa amesimama mbele ya maksai wote ambao hawajafugwa, ambao wakati huu wanahangaika na mizigo ya hatia, wakiwa wametiwa nira na dhambi. Anawaita akisema, “Mkitaka pumziko, kuna njia moja tu ya kulipata. Jitieni nira Yangu. Mimi nataka kuwa Bwana wenu, lakini lazima mkubali kujinyenyekeza kwangu. Fanyikeni wanafunzi Wangu, jifunzeni kwangu, na ule mzigo mzito ulioko nafsini mwenu utaondoka. Nira nitakayoweka kwako itakuwa laini, na mzigo nitakaokupa ni mwepesi, kwa sababu Roho Wangu Mtakatifu atakuwezesha kunitii. Ukiisha kuniamini na kukubali kuwa chini ya mamlaka yangu kama Bwana, utazaliwa upya kiroho; ndipo amri Zangu hazitakuwa mzigo kwako” (ona 1Yohana 5:3). Huu ndiyo ujumbe wa Yesu kuhusu wokovu, usiobadilika.

“Kujitia nira” ni mfano wa kuwa chini ya mamlaka ya mwingine. Mara kwa mara Maandiko hutumia huo mfano wa nira kwa njia hiyo. Wale wanaomwamini Yesu kweli hukubali kuwa chini ya mamlaka Yake. Maksai aliye na nira ana sababu moja tu ya kuwepo kwake: kufanya huduma ya bwana wake. Anaweza asijue bwana wake anataka afanye nini hasa, lakini mapenzi yake anayakubali. Yu tayari kwenda kazini.

Utakaso Unafafanuliwa

Hii sura inahusu utakaso, au, kuongezeka kwa utakatifu kunakotokea kwa wale waliozaliwa mara ya pili. Maana ya kutakaswa ni “kutengwa kwa ajili ya kutumiwa kwa kazi takatifu.” Basi, ni neno lenye kueleza mpango wa Mungu kwa ajili ya kila aaminiye vizuri sana. Agano Jipya linatumia neno hilo kwa hali mbili: wakati uliopita na wakati uliopo. Waamini wametakaswa na wanaendelea kutakaswa. Neno la wakati uliopita linadhihirisha nia ya Mungu – ametusamehe dhambi zetu na kutupa Roho Wake Mtakatifu ili kututenga kwa ajili ya matumizi matakatifu. Neno la wakati wa sasa linadhihirisha ile hali inayoendelea ya kutimizwa kwa kusudi Lake – tunaendelea kutumiwa kwa makusudi matakatifu ya Mungu, na kuzidi kufanya hivyo.

Bahati mbaya ni kwamba, kwa wengi wanaojiita Wakristo, utakaso si kitu zaidi ya nadharia kwa sababu hawajawahi kuzaliwa mara ya pili, ambacho ni kitu cha lazima kwa ajili ya utakaso. Lakini wengi wanaamini kwamba wamefanywa kuwa wenye haki ndani ya Kristo ingawa hakuna ushahidi wowote wa utakaso maishani mwao. Lakini, Maandiko yanatuambia kwamba pamoja na kuhesabiwa haki, utakaso huja.

Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu … haki na utakatifu na ukombozi … Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hiyo; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu (1Wakor. 1:30; 6:11 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Yohana naye aliandika hivi:

Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye … Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki (1Yohana 2:29; 3:7).

Wengi wanaojiita Wakristo watasikiliza kwa furaha mahubiri yenye kuangukia katika fungu liitwalo “mahubiri ya utakaso”, ambayo yanawahimiza “kutoa” maeneo mbalimbali ya maisha yao kwa Kristo ili ayatawale. Lakini, inaishia hapo kwa sababu kweli hawawi na nia ya “kutoa” eneo lolote la maisha yao kwa Kristo, hasa kama kufanya hivyo hudai kujikana. Lakini kwa namna fulani wanajishawishi kwamba kuna faida ya kusikiliza mahubiri yenye kuwashtaki hivyo, hata kama watarekebisha maisha yao au hapana. Yakobo alionya dhidi ya kitu hicho hicho, hivi: “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu” (Yakobo 1:22).

Wasikiaji ambao si watendaji wanajidanganya kwa sababu wanafikiri wameokoka, kumbe sivyo. Aina hiyo ya wanaojiita Wakristo ni tatizo kubwa kwa wachungaji wengi wanaompenda Mungu, wanaoshangazwa na jambo moja: mbona watu katika makanisa yao hawabadiliki wala kuonyesha hatua zozote za kukua kuelekea kwenye utakatifu? Sababu ni kwamba hao watu hawajawahi kujitia nira ya Yesu na hawajawahi kuzaliwa mara ya pili. Wanaweza kufikiri kwamba wamezaliwa mara ya pili kwa sababu kuna wakati waliwahi kuomba sala ya wokovu na sasa wanaelewa kwamba wokovu ni kwa neema, si kwa matendo. Lakini hawajaokoka kwa sababu hawajajitoa kuwa chini ya mamlaka ya Yesu. Juhudi zozote za kuwafanya watu kutenda kama Kristo zitakuwa bure mpaka wachukue hatua hiyo ya kwanza.

Msingi wa utakaso ni kujitoa kwa Mungu; utakaso hautatokea kwa mtu yeyote bila ya kunyenyekea kwanza. Lakini, tukisha jitoa na kunyenyekea, utakaso unaendelea maishani mwetu kadiri tunavyojifunza mapenzi ya Mungu na kweli za kiroho. Kwanza tunajitia nira ya Yesu; kisha tunajifunza “kwake” kama alivyosema Mwenyewe (Mathayo 11:29). Tunakua “katika neema na kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo” (2Petro 3:18 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mwanzoni, hatujui kikamilifu mapenzi ya Mungu au kila kitu ambacho ametutendea kwa njia ya Kristo, wala hatutambui kila kitu kinachohitaji kubadilishwa katika maisha yetu. Lakini, kama Paulo alivyoandika, tuna”jitahidi kujifunza kile kinachompendeza Bwana” (Waefeso 5:10). Hii ndiyo sababu maombi ya Paulo kwa Wakristo ni sala kwamba waongezeke katika ufahamu wa kiroho na maarifa. Na ndiyo sababu mara nyingi Paulo aliwashauri wasomaji wake akitumia maneno haya: “Au hamjui ya kuwa …?” Alitazamia kwamba waamini aliokuwa anawaandikia wangetenda kitofauti kama wangejua kweli fulani za kimungu, kama vile kwamba miili yao ni hekalu la Roho Mtakatifu.

Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kwa wafuasi wa Kristo kujipatia kila kitu ambacho Mungu amekitoa kwao ili wajifunze kweli za kiroho. Wanatakiwa kujifunza Maandiko wao wenyewe, na wafuasi wa kweli wa Kristo watafanya hivyo kwa sababu wana shauku ya kutaka kujifunza mambo ya kiroho. Wanapaswa wajitoe kwa ajili ya mafundisho kanisani kutoka kwa wale ambao Mungu amewaita kufundisha Neno Lake. Wanapaswa kuwa sehemu ya kanisa la mahali, lenye maono ya kufanya wafuasi. Hayo ndiyo anayotaka Yesu. Alisema, “Basi enendeni mkawafanye … wote kuwa wanafunzi … mkiwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi” (Mathayo 28:19-20). Wanafunzi wa kweli wanajifunza.

Kusonga Mbele Kufikia Ukamilifu

Paulo aliandika hivi katika barua yake ya pili kwa Wakorintho: “Basi wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu” (2Wakor. 7:1). Hii inatuonyesha sisi kwamba waamini wa kweli si wakamilifu, kama inavyodaiwa na watu wenye msimamo mkali. Kuchafuka kimwili na kiroho huwa sehemu ya maisha ya waamini wa kweli. Lakini, lazima tusome maneno ya Paulo katika mantiki ya Agano Jipya. Japo Wakristo wa kweli wanaweza kunajisika kidogo, wao wanahesabiwa katika haki kwa sehemu kubwa. Ona kwamba Paulo hakuwashauri wasomaji wake waanze kutenda kama watakatifu. Badala yake, aliwashauri wao kutimiza utakatifu wao. Unaweza kutimiza kile ambacho tayari unakifanya vizuri. Maneno ya Paulo yanaonyesha kwamba Wakristo Wakorintho tayari walikuwa wanatenda kitakatifu, na wakati huo utakatifu wao ulihitaji kukamilishwa. Huo ndiyo utakaso Kibiblia – kukamilisha au kutimiza utakatifu.

Maneno ya Paulo pia yanatusaidia kuelewa kwamba mpango huo unaoendelea wa utakaso maishani mwetu si kitu ambacho Mungu anafanya bila sisi. Ni lazima sisi tujitakase kutokana na uchafu wa kimwili na unajisi wa kiroho. Mwandishi wa Waebrania anasema, “Tafuteni sana … huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao” (Waebrania 12:14). Mungu haweki kando hiari yetu, na Maandiko yanasema wazi sana juu ya wajibu wetu katika mpango wa utakaso.

Lakini kwa upande wa pili, tusije tukafikiri kwamba utakaso ni kitu tunachopaswa kufanya mbali na kuhusika kwa Mungu. Paulo pia aliandika hivi: “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba Yeye aliyeanzisha kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Pengine, wajibu wetu na wajibu wa Mungu unaelezwa vizuri sana katika Wafilipi 2:12-13, kama anavyoandika Paulo, hivi:

Basi wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Maneno mepesi kutilia mkazo).

Paulo alikuwa anawaandikia waamini wa kweli, wale waliotii hata wakati yeye mwenyewe hayupo. Bila shaka Mungu alikuwa anatenda kazi ndani yao kwa Roho Wake Mtakatifu, aliyekuwa ndani yao. Basi, walikuwa na wajibu mkubwa wa kushirikiana Naye katika kila alichokuwa anafanya maishani mwao. Utakaso hutokea wakati tunaposhirikiana na Mungu.

Hatua Za Utakaso

Katika sura hii na inayofuata, tutatazama hatua za utakaso, au jinsi utakaso unavyofanyika, na jinsi Mungu anavyohusika, na sisi pia. Hebu tuanze mwanzo kabisa.

Kazi ya Mungu ilianza muda mrefu sana kabla yeyote hajatakaswa. Yeye ndiye alipanga kabla mpango wa wokovu kupitia Mwana Wake, aliyetimiza mpango huo kwa kufa kwa ajili ya dhambi zetu na kufufuka kutoka kwa wafu. Kwa njia ya mjumbe aliyetumwa na Mungu anayehubiri Injili, na kwa nguvu za kushawishi za Roho Mtakatifu, mwenye dhambi huamshwa na kuhukumiwa juu ya dhambi zake na kujisikia hitaji la wokovu.

Hapo kwenye kuokoka ndipo wajibu wa mwanadamu huingia. Tuna uchaguzi, na itikio la pekee linalofaa kwa upande wetu ni kutubu dhambi zetu na kumwamini Yesu. Mungu anatuagiza tutubu na kumwamini Yesu, kwa hiyo, kutubu na kuamini lazima kuwa wajibu wetu pia – si wa Mungu.

Lakini – mara tunapotubu na kuiamini Injili, Mungu anaingia kazini tena. Mara moja anakaa ndani yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu, akihuisha roho zetu na kuvunja nguvu za dhambi maishani mwetu, na kutuweka huru kutokana na vifungo vyake. Roho zetu zinazaliwa upya, zinaumbwa tena katika sura ya Kristo, nasi tunafanyika viumbe vipya ndani Yake (ona 1Petro 1:3; Waefeso 4:24; 2Wakor. 5:17). Mungu anakuwa Baba yetu kiroho.

Matokeo ni kiwango fulani cha utakatifu mara moja, kinachodhihirika katika maisha ya mwamini mpya. Kutokana na maandiko kama 1Wakor. 6:9-10; Wagalatia 5:19-21; Waefeso 5:5-6; 1Yohana 3:15 na Ufunuo 21:8, ni hakika kwamba kuzaliwa upya hukomesha zile tabia za kawaida za dhambi mbaya sana kama vile uzinzi, uasherati, uchafu, ufisadi, tamaa, ulawiti, ashiki, wizi, kudhulumu, ulevi, fujo, matukano, uadui, ugomvi, wivu, hasira, faraka, fitina, kuabudu sanamu, uchawi, kuua na uongo.

Hii haimaanishi kwamba mwamini wa kweli hawezi kutenda dhambi hizo. Mwamini yeyote anaweza, akitaka, kutenda dhambi hizo, kwa sababu Mungu hajamwondolea hiari yake. Lakini, atagundua kwamba ndani yake kuna upinzani na hali ya kuchukia dhambi ambayo haikuwepo kabla. Uwezo wake wa kupinga majaribu unaongezeka sana. Kama atakubali majaribu, atajisikia kuhukumiwa sana na mwenye huzuni mpaka atubu dhambi yake kwa Mungu. Hapa tena niseme, kama Maandiko yanavyotuonya sana – kutenda dhambi kama hizo ni uhakikisho kwamba mtu hataurithi ufalme wa Mungu.

Je, Dhambi Zote Ni Sawa Machoni Pa Mungu?

Kuna watakaosema kwamba “dhambi zote ni sawa” na kwa sababu hiyo, kutenda bila kutubu dhambi zote hizo zinazotajwa hapo juu si tofauti na kutenda bila kutubu dhambi zingine zozote. Lakini, hoja hii haibadilishi Maandiko tuliyokwisha yataja, wala haitii nguvu upinzani wa aina yoyote kinyume cha niliyokwisha sema. Kama dhambi zote ni sawa mbele za Mungu, basi lazima tuipanue sana ile orodha ya Paulo ya dhambi na kuweka kila dhambi, na kuamua kwamba hakuna mtu aliyeokoka! Lakini, kwa neema – kutokuwa na shukrani, wasiwasi na kusinzia wakati wa mahubiri havijatajwa katika orodha yoyote ya Paulo!

Basi, dhambi hazifanani mbele za Mungu. Yesu alizungumza kuhusu amri ndogo na kubwa (ona Mathayo 5:19). Alizungumza juu ya “dhambi kuu” na dhambi ndogo (ona Yohana 19:11). Aliihesabu amri moja kuwa “kuu, na ya kwanza” (Mathayo 22:38), na nyingine kuwa ya pili. Alitaja juu ya dhambi moja ambayo haisameheki kabisa (ona Mathayo 12:31-32). Aliwakemea Mafarisayo, ambao walipuuza “mambo makuu ya sheria, yaani: adili, na rehema, na imani,” na kutilia mkazo matakwa yale madogo madogo ya sheria kama vile kutoa zaka (Mathayo 23:23 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Ukweli kwamba dhambi fulani ni mbaya sana mbele za Mungu kuliko zingine unaonekana katika Torati ya Musa, ambamo makosa fulani yalidai adhabu kali sana. Pia tunaona kwamba Mungu aliwapa Israeli amri kumi kwanza badala ya kumi na moja au arobaini. Hii ilionyesha kwamba anazihesabu amri zingine kuwa muhimu kuliko zingine.

Tunasoma katika Ezekieli sura ya 8 jinsi Bwana alivyomwonyesha picha nne za dhambi fulani zinazotendwa Israeli. Kila iliyofuata Mungu aliitaja kuwa “chukizo zaidi” kuliko iliyokuwa imetangulia.

Mtume Yohana alisema kwamba ipo dhambi “isiyo ya mauti” na nyingine “ya mauti” (1Yohana 5:16-17).

Basi, dhambi hazifanani mbele za Mungu. Ni kweli kwamba dhambi zote hututenganisha na Mungu, na dhambi zote humhuzunisha Mungu, lakini si zote zenye kulingana katika kumhuzunisha. Kila mtu anajua kwamba kuua na kumpiga mtu konde ni makosa. Lakini pia, kila mtu anajua kwamba kosa la kwanza ni baya na kubwa kuliko lile la pili.

Badiliko La Kwanza Na Linaloendelea

Kama umezaliwa mara ya pili, Mungu amekwisha shughulika na kile kinachomwudhi zaidi. Umepata mabadiliko. Lakini Mungu hatosheki na hicho tu. Lengo Lake kwa ajili yako wewe ni ukamilifu – basi, utazamie mabadiliko yanayoendelea kutokea. Ni hivi:

Insert Chart here:

Wanadamu wote wamegawanywa katika makundi mawili: waliookoka na wasiookoka. Hakuna wengine hapo katikati. Unakuwepo katika kundi moja au la pili.

Unapotoka upande mmoja kuelekea ule mwingine, unapiga hatua kutoka kwenye uovu na kwenda kwenye utakatifu. Upande wa WASIOOKOKA una wale watu ambao ni waovu kabisa na wale ambao si waovu sana. Si watu wote wasiookoka ambao ni waovu sana.

Lakini, unapozidi kusogea kuelekea utakatifu, utavuka mstari ambao ni mfano wa kuokoka na kuzaliwa upya. Mara tu ukisha pita mstari huo, wewe umeingia katika waliookoka. Ila, katika waliookoka wapo ambao si watakatifu sana, na ambao wamepiga hatua katika utakatifu. Si wote waliookoka ambao ni watakatifu kabisa.

Lakini, tofauti inayoletwa na mtu kupita mstari wa kuokoka ni kubwa, ndiyo maana hakuna “eneo la katikati”. Mtume Yohana aliandika kwamba waliookoka na wasiookoka ni dhahiri (ona 1Yohana 3:10).

Kadiri mtu aliyeokoka anavyotakaswa kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu, anaendelea kusogea kwenye eneo la UKAMILIFU. Ila kwa wakati huu, Mungu tu ndiye mkamilifu.

Tunapozaliwa mara ya pili tu, Mungu anafanikisha kazi Yake inayoendelea ya kutubadilisha kwa kutumia njia mbalimbali ambazo tutazitazama. Lakini kwanza inatubidi tuelewe kwamba mafanikio ya Mungu yanategemea sana ushirikiano wetu. Yeye haweki kando hiari yetu. Ila pia, anatoa vivutio vingi na kutuwezesha kushirikana Naye.

Je, ni kitu gani kinachotuhamasisha tupambane na dhambi na kuzidi kufanana na Yesu? Kuna vitu vitatu ambavyo Mungu anatupa sisi: upendo, tumaini na hofu. Vyote hivyo ni halali, na vinalingana na Maandiko. Kwa upana zaidi, ni (1) upendo kwa Mungu, (2) tumaini la kupata thawabu, na (3) hofu ya kupata adhabu.

Upendo Kwa Mungu

Utii utokanao na upendo unaonekana kuwa aina ya utii ya hali ya juu sana, yenye kumpendeza Mungu. Kwa kweli tunapaswa kumtii Yeye kwa sababu tunampenda, na kila mwamini wa kweli atafanya hivyo kiasi fulani. Yesu alizungumza juu ya utii wa upendo, hivi:

“Mkinipenda, mtazishika amri zangu … Yeye aliye na amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake” (Yohana 14:15, 21).

Naye mtume Yohana aliandika hivi:

Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito (1Yohana 5:3).

Tunawezaje kuacha kumpenda wakati tunapoelewa kile alichotutendea? Tunawezaje kutokuwa na shukrani kwa kujikana Kwake kwa hali ya juu, kwa ajili yetu? Tunawezaje kuacha kutafuta kumpendeza Yeye, atupendaye sisi sana?

Hebu tufikiri tu kwamba unavuka barabara yenye magari mengi sana kwenye kona, na ghafula unatokezea mbele ya basi kubwa linalokuja kasi. Mtembea miguu mwenzako anajitahidi kukusukuma, na anafanikiwa kukuondoa katika hatari, lakini yeye mwenyewe anagongwa na basi hilo. Anakimbizwa hospitali haraka, na huko anagundua kwamba hataweza tena kutembea, bali atategemea kiti cha magurudumu maisha yake yote.

Je, wewe hutajisikia deni la shukrani kwa mtu ambaye ameokoa maisha yako kwa gharama kubwa hivyo? Je, hutajisikia wajibu wa kulipa kitu ambacho hata huwezi kukilipia? Upendo wako kwa yule aliyekuonyesha upendo mkubwa hivyo ungekuhamasisha ufanye chochote uwezacho ili kumpendeza. Kama angetaka kitu, ungefanya juu chini ili umpe. Ndivyo ilivyo kwa wale wanaomwamini Yesu. Hawana jinsi – lazima wampende, na kwa sababu wanampenda, wanajitahidi sana kumpendeza kwa utii wao.

Tumaini La Kupata Thawabu

Hamasisho la pili ambalo Mungu huwapa wale wanaomtii ni tumaini la kupata thawabu. Kweli, tunapata wokovu kwa neema ya Mungu. Lakini hiyo si kusema kwamba baraka zingine hazipatikani kwa matendo yetu. Baraka za sasa na za baadaye zimeahidiwa katika Maandiko kwamba ni thawabu kwa watii. Paulo aliandika hivi: “Utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye””(1Timo. 4:8). Kweli, Mungu “huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii” (Waebrania 11:6).

Tumaini la kupata thawabu linaweza kuonekana kama jambo la ubinafsi na uchoyo. Si la maana ukilinganisha na kuhamasishwa na kumpenda Mungu. Je, Bwana si angependa kwamba tumtumikie kwa kuwa tunampenda, badala ya kufanya hivyo kwa sababu ya faida ya kibinafsi? (Kweli hiyo inaonyeshwa vizuri sana katika kujaribiwa kwa Ayubu!)

Nafikiri ni hivyo. Lakini, Mungu ndiye aliyeanzisha mpango huo wa kutoa thawabu kwa sababu ya utii. Kama mzazi yeyote mzuri, anaweza kupenda kwamba watoto Wake wamtii wakihamasishwa na pendo safi, lakini anajua, kama mzazi mzuri, kwamba upendo wa familia wakati mwingine hautoshi. Wazazi mara nyingi huwaahidi watoto wao tuzo kwa sababu ya tabia nzuri, na inafaulu. Tena, thawabu za kidunia tunazopokea hutukuza uzuri na wema wa Mungu wetu ambaye anapenda kuwabariki watoto Wake.

Pia, lazima tukumbuke kwamba uchoyo ni kujitumikia wenyewe huku wengine wakipata shida. Basi, si kila kitu kinachofaidia kilicho kibaya. Bila ya kukemea chochote, Maandiko yanawaeleza Wakristo wa kweli kwamba ni wale ambao “kwa saburi katika kutenda mema hutafuta utukufu na heshima na umilele” (Warumi 2:7 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo). Nadhani wengi wetu tulimwamini Kristo kwa sababu ya kujijali – tunataka kwenda mbinguni, tusiende jehanamu. Lakini, tendo letu la kumwamini Kristo lisihesabiwe kwamba ni la kibinafsi na uchoyo. Sisi kupokea uzima wa milele hakumzuii mtu yeyote kupokea huo uzima. Sana sana ni kwamba kupokea kwetu uzima wa milele kuliongeza uwezekano wa wengine kuokoka pia. Basi, kupokea wokovu kwa sababu ya kujijali si kitu cha kichoyo. Na ndivyo ilivyo kuhusu thawabu ambazo Mungu ameahidi kwa watauwa. Haziji na kuwafanya wengine wazikose. Tena neema ya Mungu na thawabu Zake hazimaliziki. Si kwamba tunashindana na wengine kwamba nani atapata kipande na mwingine akose.

Basi kama ni hivyo, shauku ya kupata thawabu isionekane kuwa dhambi, au makosa, au uchoyo, hasa kwa sababu mwanzilishi na mwenye kuahidi thawabu hizo ni Mungu. Kama ingekuwa ni kosa kwetu kutamani thawabu ambayo Mungu ameahidi, basi Yeye ndiye mwenye makosa kwa kutushawishi tufanye kosa. Jambo hilo linamfanya Yeye kuwa mwenye dhambi, kitu ambacho hakiwezi kutokea kamwe!

Malipo Sawasawa Na Matendo

Katika Maandiko, watauwa wanaahidiwa thawabu maalum kwa ajili ya kutii kwao. Kwa mfano: Tunajua kwamba katika ufalme ujao wakati Kristo atakaporudi, Mungu atamlipa kila mmoja wetu kulingana na matendo yake.

“Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake” (Mathayo 16:27 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

“Tazama. Naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo” (Ufunuo 22:12 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Thawabu na ujira ambazo Yesu anazungumzia, si tu kwamba ni malipo ya jumla ambayo wote waliookoka au wasiookoka watayashiriki pamoja – yaani mbinguni au jehanamu. Malipo na ujira vilvyoahidiwa pia ni thawabu maalum na za kibinafsi ambazo zinatokana na matendo ya kila mtu kibinafsi. Paulo, akiandika kuhusu huduma yake na ya Apolo, anasema hivi:

Basi yeye apandaye na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe (1Wakor. 3:8 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo. Ona pia ms. 9-15).

Thawabu zetu wakati ujao misingi yake itakuwa ni matendo yetu wenyewe. Hii itatokana na karama zetu binafsi, vipawa na uwezo, na nafasi zilizopatikana. Mfano aliotoa Yesu wa Talanta unaliweka hilo wazi zaidi (ona Mathayo 25:14-30). Mungu anatazamia vingi kutoka kwa wale aliowapa vingi. Yesu alisema hivi, “Kwa maana, aliyepewa vingi, vingi vitatakiwa” (Luka 12:48).

Wakati Wa Thawabu Hizo

Maandiko hayaweki wazi kila wakati kwamba ni lini watauwa watapewa thawabu zao. Zipo ahadi ambazo ni kwa ajili ya wakati huu maishani, na zingine ni kwa ajili ya baadaye. Zingine hazieleweki. Basi, hebu kwanza tutazame zile chache ambazo zinaonyesha thawabu katika maisha haya:

Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, upate heri, ukae siku nyingi katika dunia (Waefeso 6:2-3. Maneno mepesi kutilia mkazo).

“Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa” (Luka 6:37, 38 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

“Kwa maana, ‘Atakaye kupenda maisha na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya na midomo yake isiseme hila’.” (1Petro 3:10 – Maneno mepesi kutilia mkazo)

Lakini aliyeitazama sheria kikamilifu iliyo ya uhuru na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake (Yakobo 1:25 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ifuatayo ni mifano michache ya ahadi ambayo ni dhahiri kwamba inahusu wakati wa maisha yetu yajayo.

“Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki” (Luka 14:13, 14 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

”Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 5:12 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

“Viuzeni mlivyo navyo mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu” (Luka 12:33 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kwamba ni thawabu gani za kimbinguni zinazotusubiri, Mungu tu ndiye ajuaye. Pamoja na kwamba mbinguni si mahali tunapojua sana, hata thawabu zinazotusubiri huko ni hivyo. Lakini, zile za hapa duniani zieleweke kwamba ni chochote tunachoweza kuhesabu kwamba ni baraka. Usimwekee mipaka Mungu kwa kusema baraka Zake ni kujisikia vizuri tu ndani ya moyo au kusisimka mpaka unasikia kuwashwa katika mgongo wako!

Mwisho: Baadhi ya ahadi ambazo muda wake wa kupewa thawabu haujulikani ni kama hizi.

“Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu” (Luka 6:35 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

“Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi … Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi … Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi” (Mathayo 6:3-4; 6; 17-18. Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu; mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana, kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru (Waefeso 6:7, 8 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Mungu anafuatilia hata tendo jema lililo dogo sana, akiwa na mpango wa kutoa thawabu kwa ajili yake.

“Kwa kuwa yeyote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin nawaambia, hatakosa thawabu yake” (Marko 9:41).

Je, ungependa kufurahia baraka zaidi kutoka kwa Baba yako wa mbinguni, sasa na baadaye huko mbinguni? Bila shaka unapenda hivyo! Basi, mtii zaidi, nawe utapata thawabu. Yesu alisema hivi: “Heri walisikiao neno la Mungu na kulishika” (Luka 11:28 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Hofu Ya Kuadhibiwa

Ukiondoa upendo kwa Mungu na tumaini la kupata thawabu, kuna njia nyingine moja ambayo Mungu anaitumia kuwahamasisha watoto Wake kutii: kwa njia ya kuogopa adhabu. Nadhani kwamba katika njia hizo tatu, hii ndiyo asiyopenda kuitumia sana. Lakini, ni kitu halisi na kukubalika na Maandiko. Wazazi wengi hutumia njia zote hizo tatu kuwahamasisha watoto wao watii, na hakuna hata moja inayostahili kulaumiwa.

Kuna wanaotoa hoja kupinga hii njia kwamba kumhofu Mungu ni kitu kisicholingana na kumpenda. Kwani Maandiko hayasemi kwamba “pendo la kweli hufukuza nje hofu” (1Yohana 4:18)?

Hofu ambayo Yohana aliandika juu yake inayofukuzwa na pendo sio hofu ya kumcha Mungu kwa utakatifu. Ni hofu ya hukumu ya milele ambayo inaanza “siku ya hukumu” (1Yohana 4:17). Baada ya kuelewa na kuupokea upendo wa Mungu, na kwa kuwa sasa tunadumu katika pendo Lake (ona Yohana 15:10), hatuna haja ya kuogopa ile jehanamu ambayo tulikuwa tunaistahili hapo kwanza.

Kumpenda na kumhofu Mungu ni vitu vinavyokwenda pamoja, kulingana na Agano Jipya. Waamini wanaagizwa kumhofu Mungu (ona 1Petro 2:17). Wanaambiwa kunyenyekeana wao kwa wao “katika hofu ya Kristo” (Waefeso 5:21), “kuutimiza wokovu kwa hofu na kutetemeka” (Wafilipi 2:12), na kuukamilisha utakatifu wao “katika hofu ya Mungu” (2Wakor. 7:1). Petro aliwashauri wale waliopokea barua yake ya kwanza waenende kwa hofu katika safari yao hapa duniani, wakijua kwamba Mungu angewahukumu kila mmoja wao bila upendeleo, kulingana na matendo yao (ona 1Petro 1:17).

Adhabu Huko Korintho

Kwa bahati mbaya sana, adhabu ya Mungu ni wazo geni kabisa kwa wengi wanaojiita Wakristo, japo si geni katika Biblia. Adhabu ya Mungu inadhihirishwa katika Maandiko tangu Adamu na Hawa hadi Anania na Safira. Inadhihirishwa tangu Waisraeli waliokufa nyikani hadi Wakristo waliokuwa wagonjwa huko Korintho. Wakati mwingine adhabu Yake inaweza kuwa kali sana wakati kuna sababu nzuri. Hebu fikiri maneno muhimu sana ya Paulo kwa Wakorintho, anaposema hivi:

Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambana ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia (1Wakor. 11:27-32. Maneno mepesi kutilia mkazo)

Kwanza: Ona kwamba, kwa sababu ya adhabu ya Mungu ambayo Paulo anaiita hukumu pia, baadhi ya Wakorintho walikuwa dhaifu na wagonjwa. Wengine walikuwa wamekufa.

Sababu ya hukumu ya Mungu: Walikuwa wanashiriki Meza ya Bwana kwa “jinsi isivyostahili” (11:27). Paulo anamaanisha nini hapo? Kutokana na mantiki tunaweza kusema kwamba alikuwa anazungumzia kitendo cha kushiriki Meza ya Bwana huku wamemwasi Bwana. Kwa mfano: Paulo aliandika kwamba tunatakiwa kwanza tujipime (au tujihoji) sisi wenyewe kabla ya Meza ya Bwana, na akaonya kwamba tuko katika hatari ya kuhukumiwa kama hatuta”pambanua mwili ipasavyo” (11:29). Inaonekana kwamba huku “kuupambanua mwili” ni sawa na kujipima na kujihoji. Tunajua kwamba “matendo ya mwili” ndiyo yanayotuletea matatizo (ona Warumi 8:12-14; 1Wakor. 9:27). “Kuupambanua mwili” bila shaka maana yake ni kutambua na kuitiisha ile asili ya dhambi iliyo ndani yetu, yenye kufanya vita kila wakati na Roho. Tunaweza kuepuka hukumu ya Mungu kama tutajipima wenyewe – kujihukumu – yaani, kama tutakataa kukubaliana na ile asili yetu ya dhambi, na tujihoji kila mara na kutubu dhambi zetu kama inabidi kufanya hivyo.

Je, Walio-okoka Wanaweza Kwenda Jehanamu?

Kama Paulo anavyoandika, Mungu hutuadhibu “ili isitupase adhabu pamoja na dunia” (11:32). Dunia itahukumiwa kupotea milele. Basi, Mungu huwaadhibu waamini watendao dhambi ili wasiende jehanamu.

Hili linaleta maswali kadhaa ya muhimu. La kwanza ni hili: Je, kweli ipo hatari ya mwamini wa kweli kufika jehanamu?

Jibu ni NDIYO. Kama mwamini wa kweli atarudia kutenda zile “dhambi zinazotenganisha” – yaani, zile ambazo Maandiko yanasema zikitendwa, mtu hataweza kuingia katika ufalme wa Mungu (ona 1Wakor. 5:11; 6:9-10; Wagalatia 5:19-21; Waefeso 5:5, 6). Anapoteza uzima wa milele. Mungu hajaondoa hiari yetu, wala uwezo wetu wa kufanya dhambi. Kinyume na jinsi waalimu wengi wa siku hizi wanavyofundisha, Biblia inafundisha kwamba mwamini yeyote atakayefuata asili yake ya kale ya dhambi – au mwili – yuko katika hatari ya kufa kiroho. Paulo anasema hivi, anapowaandikia Wakristo:

Basi kama ni hivyo ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili. Kwa maana, kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanao-ongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu (Warumi 8:12-14. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Inatubidi tuseme kwamba Paulo alikuwa anasema na waamini Wakristo walio hai kiroho, kwa sababu mbili.

Kwanza: Ona kwamba anawaita ndugu.

Pili: Walikuwa na uwezo wa kuyafisha matendo ya mwili kwa njia ya Roho. Hiki ni kitu ambacho waamini tu wanaweza kukifanya, ambao Roho wa Mungu anakaa ndani yao.

Ona sasa kwamba Paulo aliwaonya Wakristo Warumi kwamba, kama wangeishi kulingana na mwili, ni lazima wafe. Je, alikuwa anazungumza juu ya kifo cha kimwili au cha kiroho? Ni sahihi tukisema kwamba alikuwa anazungumzia juu ya kifo cha kiroho kwa sababu, kila mmoja – hata wale wenye “kuyafisha matendo ya mwili” – watakufa kimwili siku moja. Je, si kweli kwamba wale “wanaoishi kwa kuufuata mwili” mara nyingi huendelea kuishi katika mwili kwa muda mrefu tu?

Uamuzi tunaoweza kufikia kutokana na kweli hizi ni kwamba waamini Wakristo wanaweza kufa kiroho kwa “kuishi kwa kuufuata mwili”. Basi, zile orodha za “dhambi” za Paulo katika 1Wakor. 6:9-10; Wagalatia 5:19-21 na Waefeso 5:5-6 hazipaswi kufikiriwa kwamba zinawahusu wale tu wasiokiri kumwamini Kristo. Zinawahusu hata wale ambao wamekiri kumwamini Kristo. Ukweli ni kwamba, katika mantiki yake, zile dhambi ziliandikwa ili kuwa maonyo kwa waamini. NI wale wanao-ongozwa na Roho badala ya mwili ndiyo walio wana wa kweli wa Mungu, kama Paulo alivyosema waziwazi kabisa (ona Warumi 8:14).

Uthibitisho Zaidi Kwamba Walio-Okoka Wanaweza Kufa Kiroho

Paulo aliandika maneno kama hayo kwa Wakristo Wagalatia. Baada ya kuwaonya kwamba wale wanaojihusisha na “matendo ya mwili” hawataurithi ufalme wa Mungu, alisema hivi:

Msidanganyike. Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho (Wagalatia 6:7-9. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Ona hapo kwamba watu wawili wanatofautishwa. Mmoja anapanda kwa mwili wake na mwingine kwa Roho. Wa kwanza anavuna uharibifu na wa pili anavuna uzima wa milele. Kama uharibifu ndicho kinyume cha uzima wa milele, basi bila shaka maana yake nyingine ni kifo cha kiroho. Ona hapa kwamba kuvuna uzima wa milele kunaahidiwa kwa wale tu wanaopanda kwa Roho, na wanaoendelea kupanda kwa Roho. Wale wanaopanda kwa mwili hawatavuna uzima wa milele bali uharibifu. Kama Paulo alivyotoa onyo, “Msidanganyike” kuhusu hilo! (Wagalatia 6:7). Lakini, wengi sana wamedanganyika siku hizi.

Kupanda kwa mwili ni kitu kilichomkera sana mtume Paulo, ambaye, kama Mkristo mwingine yeyote wa kweli, bado alikuwa na asili ya dhambi. Aliwaandikia Wakorintho kama ifuatavyo:

Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote. Basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa (1Wakor. 9:25-27. Maneno mepesi kutilia mkazo)

Sawa na wanariadha wa Olimpiki, sisi pia lazima tuwe na kiasi kama tunatazamia kupokea zawadi yetu isiyoharibika. Paulo anataja kwamba aliutesa mwili wake na kuufanya mtumwa wake, kwa sababu kama asingefanya hivyo, alikuwa katika hatari ya “kukataliwa”. Mtu anapokataliwa, hakuna tumaini kwamba atashinda. Mantiki ya maneno ya Paulo yanaweka wazi kwamba yeye hakuwa na wasiwasi juu ya kupoteza nafasi zingine za baadaye kufanya huduma, au thawabu za mbinguni, bali kupoteza kabisa wokovu wake. Katika mistari inayofuata (1Wakor. 10:1-4) Paulo aliwaonya Wakristo Wakorintho wasifuate mfano mbaya wa Waisraeli, ambao, ingawa hapo kwanza walikuwa wamebarikiwa sana na kuwa na fursa nyingi, waliangamia nyikani baadaye kwa sababu hawakuendelea katika utii wa imani. Tofauti na Waisraeli walioangamia, waamini wa Korintho waliambiwa wakimbie choyo, kuabudu sanamu, uchafu (ambazo ni dhambi alizotaja Paulo katika orodha yake ya 6:9-10), kumjaribu Mungu na kunung’unika. Pia aliongeza ushauri huu: “Kwa hiyo, anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Wakor. 10:12).

Yakobo Anaongezea “Amina” Yake

Fikiri vile vile kile ambacho Yakobo aliwaandikia waamini Wakristo kuhusu kuvumilia wakati wa dhiki au majaribu. Wale wanaofaulu kufanya hivyo ndiyo watakaopokea “taji ya uzima” – yaani, wokovu. Wale watakaorudi kwenye tabia ya kutenda dhambi watakufa.

Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. Mtu ajaribiwapo asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike (Yakobo 1:12-16. Maneno mepesi kutilia mkazo.)

Yakobo alisema kwamba si Mungu anayetujaribu, bali “kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa” (1:14). Matokeo ni kwamba “tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi” (1:15). Mwishoni, ile dhambi “ikikomaa” huzaa mauti. Sasa: kwamba dhambi inachukua muda gani “kukomaa” ni swala la kutafiti, lakini, kwa hakika, dhambi moja inayotendwa na mwamini haimsababishii kufa kiroho wakati huo huo. Lakini, kuendelea katika dhambi, au kuzidi kuenenda katika matendo ya mwili mwisho wake ni kifo cha kiroho. Yakobo anatuonya kwamba tusidanganyike kuhusu hilo.

Hapa tena tunauliza: Inawezekanaje Yakobo awe anaonya juu ya kifo cha kimwili badala ya kifo cha kiroho, kama wengine wanavyosema? Wote watakufa kimwili wakati fulani, awe mwenye dhambi au mtakatifu.

Tena, wanawezaje watu wengine kusema kwamba Yakobo anazungumza na wasioamini katika maandiko haya? Haiwezekani dhambi “kuzaa mauti” kwao kwa sababu wao tayari “ni wafu katika dhambi na makosa yao” (Waefeso 2:1). Ni dhahiri kwamba Yakobo alikuwa anawaandikia Wakristo – “ndugu wapendwa” – kama tunavyoona katika Yakobo 1:16.

Halafu, mwishoni mwa barua yake aliandika hivi:

Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi (Yakobo 5:19-20. Maneno mepesi kutilia mkazo)

Ona kwamba Yakobo alikuwa anazungumza na ndugu. Alisema kwamba ‘mtu wa kwenu akipotelea mbali na kweli.” Basi bila shaka alimaanisha waamini wengine ambao walikuwa katika kweli mwanzoni kisha wakapotea kutoka kwenye kweli hiyo. Yakobo kwa maneno yake anaonyesha kwamba hawakuwa wamepotea katika mafundisho tu, maana anasema, “yeye amrejezaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu” (5:20). Hao ni watu waliotoka kwenye utakatifu.

Lakini, tukimrudisha yule ambaye amepotea kama Yakobo alivyoeleza, tuta”okoa roho yake na mauti.” Angalia kwamba Yakobo hakusema tunaokoa mwili wake na mauti, bali alisema roho yake. Hapa tena, cha kutoa katika maneno ya Yakobo ni kwamba yeye aliamini kuwa mtu aliye hai kiroho angeweza kufa kiroho kwa kurudia matendo ya dhambi.

Petro Naye Anajiunga Hapa

Si Paulo na Yakobo tu waliokubaliana katika jambo hili. Hata Petro pia. Akionya juu ya kudanganywa kwa waamini na waalimu wa uongo, aliandika hivi:

Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu. Maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Maana ingekuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki kuliko kuijua kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa. Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni (2Petro 2:18-22. Maneno mepesi kutilia mkazo)

Kwanza: Ona Petro aliandika kwamba waalimu wa uongo “huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu (2:18). Petro bila shaka alikuwa anawaandikia Wakristo wa kweli, kwa sababu wao walianza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu, yaani wasioamini. Pia, Petro alisema kwamba wao “walikwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi Yesu Kristo” (2:20). Maana ya pekee ya maneno hayo ni kwamba walikuwa wamezaliwa mara ya pili na hawakuwa wanaendelea kutenda dhambi. (Ona kitu ambacho Petro alikihesabu kuwa alama ya mwamini wa kweli.) Walikuwa hai kiroho.

Lakini Petro anasema, “walinaswa tena” katika kile kilichowachafua zamani, na waka”shindwa” (2:20). Matokeo ni kwamba, “hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza” (2:20). Kama ni hivyo, bado wangekuwa hai kiroho na wanaokwenda mbinguni? Hapana bila shaka. Petro anawalinganisha na mbwa wanaorudia matapiko yao, na nguruwe wanaorudia matope yao. Je, tufikiri kwamba watu hao kweli wako hai kiroho, na ni watoto wa Mungu, ambao ndani yao Roho Mtakatifu anakaa, na wako kwenye njia hakika ya kwenda mbinguni?

Ushuhuda Wa Yohana

Mtume Yohana bila shaka aliamini kwamba mtu aliye hai kiroho anaweza kufa kiroho. Anasema hivi:

Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi (1Yohana 5:16-18).

Kwanza: Ona kwamba Yohana alikuwa anazungumza juu ya Wakristo kutenda dhambi.

Pili: Ona kwamba Yohana hakuamini kwamba dhambi yoyote au kila dhambi ambayo Mkristo anaweza kutenda inaweza kusababisha kifo chake, kama wengine wenye msimamo mkali. Lakini, Yohana aliamini kwamba ipo “dhambi ya mauti” na kwamba haikuwepo haja ya kuomba kwa ajili ya ndugu aliyetenda dhambi hiyo. Tunaweza kujadili kwa kirefu kwamba dhambi hiyo ni ipi, lakini kwa sasa itatosha tu kusema dhambi hiyo ipo.

Je, Yohana alimaanisha kwamba kuna dhambi isababishayo mauti ya kimwili? Kuna wengi wanaodhani hivyo, hasa kwa sababu mafundisho yao hayatoi nafasi kwa mtu aliye hai kiroho kufa kiroho. Lakini tunapotazama mantiki kabla na baada ya maneno ya Yohana, alikuwa anazungumzia uzima wa milele katika kuandika kwake (ona 1Yohana 5:13, 20). Dhambi ya mauti ni dhambi inayomaliza uzima wa milele.

Yesu Aliwaonya Wafuasi Wake Kuhusu Jehanamu

Hata Yesu aliamini kwamba wokovu wa sasa si uhakikisho kabisa juu ya wokovu ujao. Aliwaonya wanafunzi Wake Mwenyewe wamwogope “yule awezaye kuuangamiza mwili na roho katika jehanamu” (Mathayo 10:28). Hebu fikiri pia maneno Yake kama yalivyoandikwa katika Luka 12:35-46, anayowaambia wanafunzi Wake.

“Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin nawaambieni, atajifunga na kuwakaribisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili au akija zamu ya tatu na kuwakuta hivi, heri watumwa hao. Lakini fahamuni neno hili: Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.”

“Petro akamwambia, ‘Bwana! Mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia?’ Bwana akasema, ‘Ni nani basi, aliye wakili mwaminifu mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule akisema moyoni mwake, ‘Bwana wangu anakawia kuja’, akaanza kuwapiga wajoli wake wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini” (Maneno mepesi kutilia mkazo).

Hata Mathayo aliandika juu ya maonyo hayo ya Yesu, pamoja na mafafanuzi Yake kuhusu hatima ya mwisho ya yule mtumishi asiyekuwa mwaminifu, kwamba “huko kutakuwa na kilio na kusaga meno” (Mathayo 24:51). Basi, kulingana na Yesu, mtu ambaye alikuwa anamtumikia Bwana mwanzoni bado anaweza kupotea kama atarudia maisha ya dhambi.

Ona kwamba yule mtumwa aliyerudi nyuma katika mfano huu ana sifa ya kuwachukia watumwa wenzake na ulevi, dhambi miili ambazo zinaonyesha kwamba mtu hajaokoka (ona 1Yohana 3:13-15; 1Wakor. 6:10).

Ona pia kwamba Yesu alikuwa anazungumza mfano huu kwa wanafunzi Wake mwenyewe, kama inavyotajwa katika Luka 12:22 na 41. Wokovu wa sasa si uhakikisho wa wokovu wa baadaye. Ni lazima tuendelee katika imani hai. Mifano miwili inayofuata katika Injili ya Mathayo – ule wa Wanawali Kumi na Talanta – pia hutusaidia kuona ukweli wa jambo hilo (ona Mathayo 25:1-30).

Hoja ya Yesu ni dhahiri mno kiasi cha kwamba wale wanaoamini fundisho la uongo kuhusu usalama wa milele wa wokovu bila kujali chochote wanalazimika kusema kwamba “giza la nje” ambako kutakuwepo na “kilio na kusaga meno” ni mahali fulani huko mbinguni ambapo Wakristo wasiokuwa waaminifu sana watakwenda ili kuomboleza kwa muda juu ya kupoteza kwao thawabu zao!

Yesu pia alilionya kanisa la Sardi juu ya hatari ya waamini waliozaliwa mara ya pili kufa kiroho. Inaonekana kwamba wengi katika Wakristo wa Sardi walikuwa wamerudia dhambi. Basi walikuwa katika hatari ya kutovikwa mavazi meupe, na kwamba Yesu asingewakiri mbele za Baba Yake, na majina yao yangefutwa kutoka katika kitabu cha uzima. Lakini bado walikuwa na muda wa kutubu. Hebu jisomee vizuri na polepole anachosema.

Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai nawe umekufa. Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu. Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako. Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Hao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili. Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele za malaika zake” (Ufunuo 3:1-5. Maneno mepesi kutilia mkazo.)

Pamoja na hayo ambayo Yesu, na Petro, na Yakobo, na Yohana na Paulo walifundisha, inakuwaje kwamba waalimu wengi wa siku hizi wanadai kwamba kama mtu ameokoka kweli hawezi kupoteza wokovu wake hata kama anaishi maisha gani? Huo ni ongo kutoka kwa Shetani kabisa, ulioanza wakati alipomwambia mtu hai kiroho aliyekuwa anafikiri kutenda dhambi, kwamba “Hakika hamtakufa!” (Mwanzo 3:4). Mbona Wakristo wengi wasitambue huo uongo wa tangu mwanzo wa Shetani, ambao unaenezwa na mafundisho ya kisasa ya uongo?

Wakati Mwamini Anapoacha Kuamini

Kutokuwa mwenye haki si hatari ya pekee kwa waaminio. Kama mwamini wa kweli ataacha kuamini, atapoteza wokovu wake maana wokovu umeahidiwa kwa wale tu wanaoamini na wanaoendelea kuamini. Agano Jipya la Kiyunani linapozungumza kuhusu wokovu, linatumia neno kuamini katika hali ya kuendelea. Wokovu ni kwa wale wanaoamini na wanaoendelea kuamini, si kwa wale walioamini wakati fulani zamani. Kwa sababu hiyo na nyingine, Agano Jipya limejaa mashauri yenye kuwaonya waamini waendelee kwenye njia ya haki. Yesu aliwaonya wanafunzi Wake Mwenyewe kwamba “atakayevumia mpaka mwisho, huyo ndiye atakayeokoka” (Mathayo 10:22).

Ona maneno ya Paulo kwa Wakristo Wakolosai juu ya jambo hili.

Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarakanishwa, tena adui katika nia zenu kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu (Wakolosai 1:21-23. Maneno mepesi ni kutilia mkazo.)

Wengi wanaofuata mafundisho ya Calvin wanadai maana ya Paulo ni kwamba, Wakristo wote wa kweli wataendelea kudumu katika imani mpaka kifo, na kama wakati fulani wataacha kuamini, hiyo inathibitisha kwamba hawakuwahi kuokoka wakati wowote. Kwa sababu ya waamini wengi wanaozaa matunda ambao huanguka, baadhi ya wanaCalvin pia hudai kwamba Mkristo wa bandia, ambaye hajajazwa na Roho Mtakatifu anaweza kuonekana kama mwamini wa kweli. Anaweza hata kuonyesha matunda zaidi ya Roho kuliko Wakristo wa kweli, lakini mwishowe atakwenda jehanamu kwa saabu hakuwa na imani ya wokovu! Sasa ni kwamba mwanaCalvin ambaye lazima asimamie mafundisho yake inambidi kila wakati aishi huku kukiwa na uwezekano kwamba imani yake inaweza kuthibitishwa kuwa ya bandia kama ataacha kuamini. Ikiwa imani halisi ya kipekee ni ile imani inayovumilia mpaka kifo, basi mwanaCalvin hawezi kuwa na uhakika wa wokovu wake, maana hatajua kama imani yake ni halisi mpaka anapovuta pumzi yake ya mwisho. Hapo ndipo atakapojua kama imani yake ilidumu hadi kifo na kuthibitisha kwamba ilikuwa ya kweli.

Nadharia hiyo ni kinume na mawazo ya Paulo katika Wakolosai 1:23. Yeye aliwataka Wakristo Wakolosai wajue kwamba wakati huu walikuwa wamepatanishwa na Mungu, na kwamba wangeendelea kuwa na msimamo huo huo bila hatia mbele Zake, kama wangedumu kuamini.

Angalia pia maneno ya Paulo kuhusu wokovu wa Wakorintho.

Basi ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri … (1Wakor. 15:1, 2 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Paulo aliwahakikishia wokovu wao, kutokana na imani yao. Wangedumu kuwa wameokoka kama wangeshikilia Injili. Hakuwaambia wakati huo kwamba kitakachoamua ni muda, kama kweli wameokoka, ikiwa watadumu katika imani mpaka kufa.

Linda Moyo Wako Na Kutokuamini

Mwandishi wa kitabu cha Waebrania alionya kuhusu hatari za kweli za kuruhusu kutokuamini au dhambi kuingia maishani mwetu. Ona kwamba anawaambia ndugu Wakristo maneno haya yafuatayo:

Angalieni ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho (Waebrania 3:12-14. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Sisi ni “washirika wa Kristo” muda wote tutakao”shikamana” katika imani. Dhambi ina uwezo wa kutudanganya na kutufanya wagumu, basi, tujihadhari na kutokuamini pamoja na dhambi, visiingie maishani mwetu.

Baadaye katika barua yake, mwandishi wa kitabu cha Waebrania anataja maneno ya maandiko maarufu sana katika Agano la Kale – Habakuki 2:4 – kisha, anaongezea yafuatayo, chini ya uvuvio:

‘Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisitasita, roho yangu haina furaha naye.’ Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu (Waebrania 10:38-39. Maneno mepesi kutilia mkazo.)

Je, kuna kuwa wazi kuliko hivyo?

Kupandikizwa Na Kuvunjwa

Miongoni mwa maandiko mengine mengi, Warumi 11:13 hadi 24 pia husimama kama ushahidi kwamba waamini wa kweli wanaweza kupoteza wokovu wao kama wataacha imani yao. Hili ni jambo ambalo kila msomaji aliye mkweli atakubali. Angalia yafuatayo:

Lakini nasema na ninyi mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu, nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao. Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa? Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika. Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake, usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe. Basi utasema, ‘Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.’ Vema, yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe. Tazama basi, wema na ukali wa Mungu. Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali. Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena. Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeitumi mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa kinyume cha asili katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe? (Warumi 11:13-24. Maneno mepesi kutilia mkazo.)

Basi, ni dhahiri kwamba upo uwezekano wa kupoteza nafasi yako kwenye mti wa Mungu wa wokovu. Tunasimama kwa imani yetu na tunahakikishwa nafasi yetu tukikaa “katika wema Wake” tu (11:22).

Turudie Tena Adhabu Ya Mungu

Baada ya hayo yote, hebu turudi tena kwenye maneno ya Paulo kuhusu adhabu ya Mungu katika 1Wakorintho 11:27 hadi 34, na tuulize swali lingine: Je, adhabu ya Mungu inahakikisha kwamba Mkristo mwenye dhambi atatubu na kutokuhukumiwa kama dunia?

Jibu bila shaka ni hapana kwa sababu kadha. Kwanza ni kwa sababu ya maandiko yale yote ambayo tumesoma, yenye kuonyesha kwamba mwamini wa kweli anaweza kupoteza wokovu wake kwa kuacha imani yake au kurudia matendo yasiyo haki. Mwamini yeyote anayepotea bila shaka anapendwa na Mungu, na Maandiko yanafundisha kwamba Yeye humwadhibu kila ampendaye (Waerania 12:6). Lakini, kwa kuwa inawezekana kwa waamini kurudi kwenye kutokutenda haki au kutokuamini na hatimaye kufa kiroho, tunachoweza kusema tu ni kwamba adhabu ya Mungu haiwarudishi kila mara wale wanaopotea.

Pili: Mungu kamwe haweki pembeni hiari yetu kwa habari ya wokovu wetu. Kama hatutaki kumtumikia, hakuna lazima, na Biblia inatoa mifano ya watu wengi sana ambao Mungu aliwaadhibu na hawakutubu. Kwa mfano: Mfalme Asa alikuwa mfalme mzuri sana mwanzoni. Lakini baadaye maishani mwake alifanya dhambi na akakataa kutubu hata wakati akipata adhabu ya Mungu ambayo ilikuwa maradhi katika miguu yake. Mwishoni, ugonjwa huo ulimwua (ona 2Nyakati sura ya 14 hadi 16).

Kulingana na mwandishi wa kitabu cha Waebrania, inawezekana kabisa kwa watoto wa Mungu kuitikia vibaya adhabu ya Mungu. Anasema hivi juu ya hilo:

Tena mmeyasahau yale maonyo yasemayo nanyi kama kusema na wana, ‘Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye…’ Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? (Webrania 12:5, 9).

Wakati tunapoadhibiwa na Baba yetu, tunaweza “kudharau” au “kunywea”, yaani, tunaweza kushindwa au kulemewa na kuachia mbali. Lakini Mungu anatamani kwamba tujinyenyekeze na kukubali adhabu Yake ili “tuishi”. Ni dhahiri kwamba kama tutakataa kujinyenyekeza hatutaishi, tutakufa. Mwandishi bila shaka alikuwa anaandika kuhusu maisha ya kiroho (na bila shaka kifo cha kiroho), kwa sababu hata Wakristo watii hatimaye hufa kimwili, licha ya ukweli kwamba wengi ambao hawako chini ya “Baba wa roho zetu” huendelea kuishi kimwili kwa muda mrefu sana.

Hili linatufikisha kwenye swali linalofuata: Vipi kuhusu kifo cha kimwili kabla ya wakati wake? Kama ni aina moja ya adhabu ya Mungu, ambayo kusudi lake ni kwamba “tusihukumiwe pamoja na dunia”, si ingekuwa vizuri kwa Bwana kumpeleka nyumbani kila Mkristo atendaye dhambi, kabla ya kufa kiroho?

Kama mambo yangekuwa hivyo kila wakati, isingewezekana kwa mtu kupoteza wokovu wake. Kama mtu ameokoka, asingekuwa na haja ya kuwa na wasiwasi juu ya kuacha imani yake au kurudia tabia ya dhambi, maana angetulia kwa uhakika kwamba Bwana atafupisha maisha yake kabla ya kufa kiroho na kupoteza wokovu wake. Lakini, wazo hili linapingana na maandiko mengi yenye kuonyesha kwamba kweli mtu aliyeokoka anaweza kupoteza wokovu wake. Sasa, jibu ni nini?

Labda mfano wa kibinadamu unaweza kutusaidia – Mwananchi anaweza kuvunja sheria na kupata adhabu ya serikali. Lakini, akikimbia nchi atakuwa amejiondoa kwenye mamlaka ya serikali hiyo. Basi, hatapatikana na adhabu ya serikali wala hawezi kushiriki faida za wananchi.

Au mfano mwingine: Mtoto anaweza kukataa kumtii baba yake na kupata adhabu yake ya upendo. Lakini kama mtoto huyo atatoroka nyumbani na kwenda kufanya kile ambacho baba yake anakataa, hana haja ya kuhofu adhabu ya baba yake. Amekwisha kujiondoa kwenye familia ile. Basi, kwa wale wanaoiacha imani yao au wanaorudi moja kwa moja kwenye kuufuata mwili, faraja ya adhabu iliyoahidiwa, na ikibidi, kifo kabla ya wakati, si vitu vinavyowezekana. Wanakuwa wamepoteza kila kitu kilichokuwa chao. Wanaweza kufa kabla ya wakati kweli, lakini hawaendi mbinguni hatimaye.

Lakini, wale miongoni mwa watoto wa Mungu wanaojikwaa na kuingia katika dhambi, lakini ambao mioyo bado inataka kumtumikia Mungu, wanajiweka katika nafasi ya kuadhibiwa na Baba yao kama hawajihukumu wenyewe kwa toba na kuungama. Hawa watoto kwa kawaida ni watii: hawakimbii wala kuitoroka familia yao, ila, kwa kiwango fulani si watiifu. Kama wataendelea katika kutokutii kwao, wakiacha kuungama na kutubu dhambi zao, wanaweza kuhukumiwa kwa kifo cha kimwili kabla ya wakati, ila wanapokufa bado wameokoka.

Kwa mfano: Mungu anaweza kumwita mtoto Wake mmoja awe mchungaji. Kama huyo mtoto wa Mungu atapingana na mwito huo, anaweza kupatikana na adhabu ya Mungu kwa namna fulani. Akidumu katika kutokutii anaweza kufa kabla ya wakati, lakini bado atakwenda mbinguni. Si kwamba aliishi “kwa kuufuata mwili,” bali alikuwa anayafisha matendo ya mwili kwa Roho. Alikuwa na matunda maishani mwake, lakini alikuwa anapungua kwenye kile ambacho Mungu alitazamia. Yeye si kama Mkristo ambaye ameacha imani yake au kurudia matendo ya dhambi.

Tunaweza kujiuliza hivi: “Ni kitu gani ambacho ni kibaya kuhusu kufa kabla ya wakati, na kwenda mbinguni? Si hiyo ni thawabu nzuri zaidi kuliko adhabu?”

Swali kama hilo linafunua kutokuelewa kwetu jinsi ambavyo Mungu atawapa thawabu kubwa wale watauwa katika maisha yajayo. Ikiwa hata kutoa kikombe cha maji baridi tu kutasababisha thawabu; ikiwa kwa kuvumilia “dhiki ndogo ya muda” tutazamie “utukufu wa uzito upitao” (2Wakor. 4:17); ikiwa kwa kuwapa wenye mahitaji tunaweza kujiwekea “hazina mbinguni” (Luka 12:33), basi kila sekunde tunayoweza kumtumikia Mungu hapa duniani inapaswa kuhesabiwa kama nafasi ya hali ya juu sana. Ni huzuni sana tunapopoteza wakati ambao hatuwezi kuupata tena. Katika siku zijazo, tutatazama nyuma kwa majuto makubwa sana. Hii itakuwa kweli sana kwa wale waliokufa kabla ya wakati na hawakupata nafasi zaidi za kumtumikia Bwana hapa duniani.

Je, Magonjwa Yote Ni Ishara Ya Adhabu Ya Mungu?

Ni dhahiri kutokana na yale ambayo Paulo aliwaandikia Wakorintho, udhaifu, magonjwa na kifo kabla ya wakati vinaweza kuwa madhihirisho ya adhabu ya Mungu. Ingawa haitakuwa sawa kufikia mahali pa kusema kwamba udhaifu wote, magonjwa au kifo kabla ya wakati ni onyesho la adhabu ya Mungu, yapo Maandiko mengine mengi licha ya 1Wakorintho 11:27-32 yenye kushuhudia uwezekano huo. Hivyo basi, Mkristo yeyote anayejikuta akiteseka kimwili atakuwa na busara kutafuta muda wa kujichunguza. Ikiwa tunapitia katika adhabu ya Mungu, inaonekana haiwezekani kwamba tupate nafuu ya kudumu kimwili bila ya toba na msamaha wa Mungu.

Adhabu ya Mungu kweli inaweza kuja kwa njia nyingine zaidi ya ugonjwa wa kimwili. Mungu anaweza kupanga mazingira kwa njia mbalimbali ili kukamilisha makusudi Yake. Yakobo ambaye wakati mmoja alijifanya ni ndugu yake ili kumdanganya baba yake, aliamka asubuhi fulani akiwa ameoa mwanamke ambaye alijifanya ndiye mpenzi wake! Wakristo wengi ambao si watii wamewahi kuamkia katika mazingira kama hayo, wakati Bwana alipowafundisha polepole juu ya kupanda na kuvuna.

Zaidi ya yote, tusisahau kwamba adhabu ya Mungu ni ishara ya pendo Lake kwetu. Mkristo anayepata adhabu asifikiri jambo lingine lolote. Yesu alisema hivi: “Wote niwapendao mimi, ninawakemea na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu” (Ufunuo 3:19 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatwambia kwamba Mungu hushughulika nasi kama baba yeyote mwema anavyofanya na mtoto wake:

Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi; tena mmeyasahau yale maonyo yasemayo nanyi kama kusema na wana:

“Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye.”

Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; basi si afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? Maana ni hakika hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani (Waebrania 12:3-11).

Ukifikiri vizuri juu ya kile tulichosoma sasa hivi, inaonekana kwamba tunapaswa kujali ikiwa hatuadhibiwi kuliko kama tunaadhibiwa! Mwandishi wa Waebrania aliandika kwamba “wote tumekuwa washirika” wa adhabu ya Mungu, na wale ambao hawahusiki ni “wana wa haramu, si wana wa halali” (12:8).

Mungu anatamani kwamba tushiriki utakatifu Wake. Hilo ndilo kusudi Lake tangu mwanzo. Kuadhibiwa si kitu kizuri, lakini baada ya kuvumilia na kupitia, huleta haki maishani mwetu. Mtunga Zaburi aliandika hivi: “Kabla sijateswa mimi nalipotea, lakini sasa nimelitii neno lako … Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, nipate kujifunza amri zako” (Zaburi 119:67; 71).

Wakati Kanisa Linapotekeleza Adhabu Ya Mungu

Kuna sehemu moja nyingine ya adhabu ya Mungu ambayo tunahitaji kuiangalia. Hiyo nayo ni kitu ambacho Mungu hutumia kutuhamasisha kuwa watakatifu. Ni adhabu inayotolewa na kanisa.

Kwa bahati mbaya sana, maneno ya Yesu juu ya jambo hilo hayatiliwi maanani sana. Kimsingi ni kwa sababu mara nyingi mtazamo wa makanisa mengi na wengi wanaojiita Wakristo si utakatifu wa kibinafsi wala wa kusanyiko. Lakini, Wakristo wa kweli ambao wanajitahidi pamoja kumpendeza Bwana hawatapuuza maneno ya Yesu aliyosema, hivi:

“Na ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru” (Mathayo 18:15-17).

Mtu haachi kushangaa kitu kinachoweza kutokea ikiwa amri hizo zitatiliwa mkazo kanisani. Bila shaka katika makanisa mengi mahudhurio yangepungua. Ni wazi kwamba kama washirika wa mwili wa Kristo tunao wajibu, si kwa ajili ya utakatifu wetu tu, bali pia tunawajibika kiasi fulani kwa ajili ya utakatifu wa waamini wengine na usafi wa kanisa la Kristo.

Ni vizuri kufikiri kwamba maneno ya Yesu kuhusu adhabu ya kanisa yanahusu zile nyakati ambazo ndugu hutukosea kibinafsi, na si wakati ndugu anapotenda dhambi kwa ujumla. Hii tafsiri inatiwa nguvu kwa maneno ya Yesu yaliyoandikwa katika Luka 17:3-4: “Jilindeni; kama ndugu yako akikukosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja na kurudi kwako mara saba, akisema ‘Nimetubu’ msamehe” (maneno mepesi kutilia mkazo). Ona Yesu alivyosema: “Kama akikukosea.” Pia, Yesu alitwambia tumsamehe ndugu yeyote anayetubu na ambaye tunamkemea. Tunaweza kusamehe makosa ya binafsi ya wengine, lakini si dhambi zao za jumla. Tena, tunaona kwamba baada ya kufuata maneno ya Yesu kuhusu adhabu ya kanisa katika Mathayo 18 ni mfano wa mtumishi asiyesamehe, uliotokana na swali la Petro kwamba ni mara ngapi amsamehe ndugu yake. Katika swali la Petro na jibu la Yesu katika mfano huo kuna wazo la makosa ya kibinafsi.

Utaratibu Wenyewe

“Adhabu ya kanisa” haipaswi kuhusisha kusanyiko lote, isipokuwa mara chache sana. Huanza na mtu mmoja ambaye amejitoa kuwa mtakatifu. Lazima ni mtakatifu kwa sababu kama mbili hivi. Kwanza: Kama yeye si mtakatifu kibinafsi kwa kiwango fulani, atakuwa na sehemu ile ya mtu mwenye boriti katika jicho lake, anayejaribu kutoa kibanzi katika jicho la mwingine (ona Mathayo 7:3-5). Je, nina haki gani ya kumrekebisha ndugu anayetenda dhambi, kama mimi ni mwenye dhambi zaidi?

Pili: Kama kosa lililotendwa ni la kibinafsi, basi huyo aliyekosewa lazima awe mtakatifu kiasi cha kutosha kuhitaji mapatano. Wengi wetu tunapokosewa, tunazungumza na kila mtu juu ya kukosewa huko isipokuwa yule mkosaji. Tunapenda kusengenya badala ya kutafuta mapatano. Maandiko yanatuonya kwamba tunapofanya hivyo, tuko katika hatari ya hukumu (ona Mathayo 7:1-2; Yakobo 4:11; 5:9).

Basi – Hebu tufikiri kwamba mwamini ametenda dhambi, na tuseme amekukosea. Unachotakiwa ni kumwendea na kusema naye kwa upendo, upole na unyenyekevu. Mara nyingi utagundua kwamba yule mkosaji hakutambua alichofanya, na atakuomba msamaha mara moja. Wewe unachotakiwa kufanya ni kumsamehe, na unaweza kutaka kuhoji maswali kama ni mtu mwenye kuumia sana. Mara nyingi, “makosa” ambayo watu “yanawaumiza” yanatakiwa kupuuzwa kwa kudhani kwamba mhusika hakukusudia madhara. Kwa mfano: Kwa kuwa ilionekana kana kwamba mchungaji wako alikuwa anakukwepa kanisani haimaanishi kwamba alikuwa anakukwepa. Pengine alikuwa akishughulika na kuwatafuta wengine.

Uwezekano mwingine unapomkabili yule ndugu ni kwamba anaweza kukujulisha mchango wako na wewe katika kosa lile. Pengine anaweza kukwambia kwamba alifanya hicho alichofanya kwa sababu wewe ulimkwaza. Kama ni hivyo, alitakiwa kuwa ameshakuja kwako. Lakini, sasa unatambua kwamba wewe ndiye uliyesababisha tatizo, na unahitaji kuomba msamaha. Hapo ndugu yako atawajibika kukusamehe, na mapatano yatakuwepo.

Hatua Ya Pili Na Ya Tatu

Hebu tuseme kwamba hakuna lolote katika hayo hapo juu kinachotokea. Yule mkosaji anakataa kukubali kosa lake au kukuomba msamaha. Hapo sasa, “chukua mwingine mmoja au wawili umwendee, ili kwa kinywa cha mashahidi wawili au watatu kila jambo lithibitishwe” (Mathayo 18:16).

Ni hivi: Kabla ya kuwashawishi hao wengine wamkabili mkosaji, itakubidi uwashawishi juu ya jambo unalotaka kufanya. Wanaweza kutaka kumhoji mkosaji kabla ya kukubaliana nawe. Wanaweza hata kushawishika kwamba mkosaji anayedaiwa si mkosaji, wakakurekebisha wewe! Kama ni hivyo, wewe unapaswa kumwomba msamaha “yule mkosaji”!

Ila, ukiweza kuwashawishi wengine kwamba wewe ndiye mwenye haki katika jambo hilo, basi kwa pamoja mnakwenda kumkabili yule mkosaji tena. Inatazamiwa kwamba wao kuungana na wewe kutatosha kumfanya yeye akiri kosa lake na kuomba msamaha, jambo ambalo litaleta mapatano.

Lakini tena, kama bado anakataa kukiri kosa lake – japo haitokei mara nyingi – basi jambo hilo lifikishwe mbele ya kanisa zima. Maana yake ni kwamba uongozi wa kanisa utahusishwa. Bila shaka watataka kuchunguza kila kitu kikamilifu kabla ya kuamua kujiunga na wewe. Hapo tena kuna uwezekano kwamba wanaweza kugundua kwamba wote wawili mna madai halali, na kwamba wote wawili mnahitaji kuombana msamaha. Lakini, wakikuunga mkono ujue kwamba una madai halali dhidi ya ndugu yako.

Akigundua kwamba kanisa zima limeungana na wewe na linapanga kumkabili, aidha atatubu au ataondoka kanisani. Hakutakuwa na haja ya kumtenga. Yesu alisema awe kama “mtu wa Mataifa na mtoza ushuru” (18:17). Yaani, ahesabiwe kama mtu ambaye hajaokoka, kwa sababu inaonekana ndivyo alivyo. Mtu ambaye amezaliwa mara ya pili hawezi kupingana na uamuzi wa kanisa zima. Basi, ahesabiwe kwamba si mwamini – ni mtu anayehitaji kushuhudiwa tena na kuzaliwa mara ya pili.

Kama Mkosaji Atatubu …

Ikiwa wakati wowote kabla au wakati mambo yanaendelea kushughulikiwa au baada ya adhabu hiyo ya kanisa kutolewa, mhusika ataomba msamaha, lazima asamehewe la sivyo ninyi mtapata adhabu ya Mungu. Mara tu baada ya kutoa maelezo juu ya adhabu ya kanisa, Yesu alisimulia kisa juu ya mtumwa aliyekuwa amesamehewa deni kubwa sana na mfalme. Lakini huyo naye akakataa kumsamehe mtumwa mwenzake ambaye alikuwa anamdai kiasi kidogo sana. Akaagiza atupwe gerezani. Mfalme aliposikia juu ya kutosamehe kwa mtumwa wake, “alighadhabika sana” na “akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote” (Mathayo 18:34). Kisha Yesu akatoa ahadi hii: “Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake” (Mathayo 18:35).

Wengine wanatafsiri onyo la Yesu kwamba ni kupoteza nafasi yetu kama watu waliosamehewa, na kutupwa jehanamu. Ni dhahiri kwamba yule mtumwa ambaye hakusamehe aliwajibishwa juu ya deni lake la zamani, ambalo asingeweza kulilipa, na akajikuta amerudia hali ile aliyokuwa nayo kwanza: kutosamehewa. Je, hii inaonyesha “alipoteza wokovu wake?”

Kuna watakaosema kwamba hiyo ni kuingiza mengi katika maneno ya Yesu kuliko alivyosema. Wangependa kufikiri kwamba Yeye alimaanisha adhabu fulani ya kidunia, na kwamba kule “kupelekwa kwa watesaji” ni kusumbuliwa kidogo na mapepo. Baada ya kuteseka kidogo, atatubu na kumsamehe ndugu yake.

Lakini Yesu aliahidi kwamba tusiposamehe dhambi za wengine, sisi wenyewe hatutasamehewa (ona Mathayo 6:14-15). Je, alimaanisha tutapoteza hali yetu kwamba tumesamehewa, au alimaanisha tu kwamba hatutasamehewa dhambi zozote za baadaye, na kwa njia hiyo kupoteza ushirika na Mungu na baraka fulani za kidunia lakini bado tumeokoka? Paulo alitushauri tusameheane sisi kwa sisi kama ambavyo tumesamehewa pia, lakini hakuongezea kitisho (ona Waefeso 4:32). Mimi nadhani kama Yesu alimaanisha kwamba tunapokataa kumsamehe mwamini mwingine tunaweza kupoteza wokovu wetu, Paulo angetilia mkazo jambo hilo. Lakini tena, ingawa Paulo hakutaja kutokusamehe kuwa ni dhambi ambayo ingesababisha kupotea kwetu kabisa, alisema kwamba mtu akiwa na tabia za dhambi kama vile uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka na husuda hataurithi ufalme wa Mungu (Wagalatia 5:20-21).

Hata kama hatujui tafsiri sahihi ya maneno ya Yesu kuhusu msamaha, mimi siwezi kucheza na wokovu wangu kwa kukataa kumsamehe ndugu aliyetubu. Ni afadhali kusamehe.

Msamaha Bandia

Je, tuna wajibu wa kuwasamehe wale wanaotukosea ambao hawakiri makosa yao? Je, tuwahesabu wakosaji wasiotubu kana kwamba hakuna chochote kilichotokea? Haya ni maswali muhimu yanayowasumbua Wakristo wengi.

Kwanza: Ni lazima tutambue kwamba haiwezekani kuwepo na mapatano ya kweli bila ya kuwasiliana, toba na kusameheana. Hili linaeleweka kirahisi katika ndoa. Mwenzi mmoja anapomkosea yule mwingine, kunakuwa na kutokuelewana. Pengine hata hawazungumzi tena. Mmoja analala kwenye kiti.

Ni kitu gani kitakachorudisha mahusiano yao? Ni mawasiliano, toba na kusameheana. Wanaweza kujaribu kupuuza yaliyotokea. Wanaweza kujilazimisha kuchekeana na kuzungumzia mambo mengine. Lakini bado kuna kitu kati yao. Mahusiano yao yameharibika, na yatabaki hivyo mpaka kuwepo mawasiliano, toba na kusameheana.

Kama mmoja ndiye mkosaji, yule aliyekosewa anaweza kujaribu “kusamehe” huku akijaribu kusahau yaliyotokea na kuendelea na maisha kana kwamba hakuna kilichotokea. Lakini kila anapomwona mkosaji lile kosa linarudi akilini. Anawaza kwa masikitiko, “Mbona siwezi kusamehe?”

Sababu ni kwamba anajaribu kufanya kisichowezekana: Kitu ambacho hata Mungu hafanyi. Mungu huwasamehe wale wanaotubu tu. Hatazamii mwamini aliyekosewa kujifanya kana kwamba hakuna kosa lililotendwa, huku akijaribu kujishawishi kwamba kwa kweli yule aliyemkosea ni ndugu mzuri tu ambaye hana matatizo. Hii ndiyo sababu Yesu alituambia tumkabili mkosaji, na kama hatatubu tumpitishe katika zile hatua za adhabu kikanisa. Lakini, wakati wowote katika hizo hatua, akitubu, hatuna budi kumsamehe. Kama Yesu alitazamia mwamini aliyekosewa “kusamehe” tu na kuendelea na maisha, asingesema alichosema juu ya adhabu kikanisa. Anasema tena kama ifuatavyo:

“Jilindeni! Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja na kurudi kwako mara saba akisema, ‘Nimetubu,’ msamehe” (Luka 17:3, 4 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Inawezekana, na ni sawa kutazamia kwamba waamini wote watampenda kila mmoja – hata wakosaji wasiotubu – kama Mungu. Lakini kuwapenda hakumaanishi msamaha bila masharti. Mungu anampenda kila mmoja, lakini si kila mmoja aliyesamehewa Naye.

Yasiyowezekana

Lakini, vipi kama haiwezekani kwa sababu zilizo nje ya uwezo wako, kufuata ule utaratibu wa adhabu kikanisa ambao Yesu aliutoa? Kwa mfano: Umekosewa sana na mwamini ‘maarufu’ kama mchungaji, naye anakataa kuonana na wewe. Au unamkabili mkosaji anayekataa kutubu, na umekosa mtu aliye tayari kurudi kwake na wewe kwa ajili ya hatua ya pili.

Katika hali kama hiyo, maneno ya Paulo yanafaa. Anasema hivi: “Ikiwezekana, kwa upande wenu, kaeni kwa amani na watu wote” (Warumi 12:18, TLR). Fanya unachoweza – hicho ndicho Mungu anachotazamia kwako.

Vyovyote inavyokuwa, kila mara Bwana anataka sisi tugeuze “shavu la pili” na kwenda “maili ya pili”. Kama nilivyokwisha kusema mwanzoni, hii haimaanishi turuhusu kuonewa au kutendewa mabaya. Maana yake ni kwamba tufanye zaidi ya matazamio ya watu. Hiyo ni kweli hasa tunaposhughulika na wasioamini. Wao hawajadai kwamba ni wafuasi wa Kristo. Kwa hiyo, kujaribu kuwapitisha kwenye ule utaratibu ambao Mungu amekwisha utoa kwa kanisa ni upuzi.

Kama nilivyokwisha sema, ingawa Mungu hamsamehe mtu mpaka atubu, bado anawapenda watu wasiotubu na anawasubiri kwa upendo na mikono wazi kuwapokea wakati wowote. Hiyo ndiyo inayotakiwa kuwa hali yetu ya moyo kwa habari ya mkosaji yeyote asiyetubu. Hatuwezi kumsamehe mpaka atubu, lakini tunaweza kumpenda, kumwombea na kumngoja huku mikono ya upendo ikiwa wazi. Baba yake mwana mpotevu hakusafiri kwenda nchi ya mbali kumpa mtoto wake mkopo wenye masharti nafuu, lakini pia alipomwona mtoto wake akirudi nyumbani kwa aibu hakumpa kisogo. Alimkimbilia akamkumbatia. Yusufu hakujitambulisha kwa ndugu zake walipomtembelea Misri mara ya kwanza, lakini walipoonyesha toba yao baadaye, aliwapokea kwa machozi.

Upande Wa Pili Wa Shilingi

Vipi kama wewe ndiye unayehusika kupokea hiyo adhabu ya kanisa? Ndugu anakujia kwamba umemkosea. Ufanyeje? Unatakiwa ujinyenyekeze, usikilize kwa makini na ufikiri anachosema. Ukifikiri hoja yake ni halali, tubu na uombe msamaha. Ukifikiri siyo, zungumza naye taratibu na ushughulike kutafuta maelewano na mapatano. Pengine utafaulu.

Kama atarudi na mmoja au wawili wengine, na waungane na huyo mlalamikaji baada ya kusikiliza upande wako, unatakiwa ufikiri kwa makini sana kile wanachokwambia, ukiri kwamba umekosea na uombe msamaha.

Kama unaamini kwamba wote watatu wamekosea na wapeleke jambo hilo mbele ya kanisa zima, unatakiwa ukubali kukutana na yeyote katika uongozi anayetaka mkutane. Eleza kwa makini upande wako, na kama kanisa zima litasimama na ndugu aliyekosewa, unatakiwa utambue kwamba una makosa, ukiri na kuomba msamaha.

Adhabu Ya Kanisa Kwa Kinyume

Adhabu ya kikanisa ni aina ya adhabu ya Mungu kwa kuwa inafanyika kwa agizo Lake. Ni njia nyingine anayotumia kutuhamasisha tuwe watakatifu, na ni njia anayotumia kulitunza kanisa Lake katika hali ya usafi.

Katika makanisa yaliyojaa Wakristo wa bandia, mambo ni tofauti kabisa. Mimi namjua mchungaji mmoja mcha Mungu aliyekataa kushirikiana kuimba na mtu aliyekuwa mshirika wake na ambaye alikuwa katika ndoa isiyo halali. Huyo mtu alitoka katika familia maarufu ya ‘vigogo’ hapo kanisani, na waliposikia hicho alichofanya mchungaji wao, walifanya mpango wa kumwondoa. Walisema kwamba alikuwa amezidi sana kuhukumu watu na alikuwa hawezi kuchukuliana na watu, na washirika wengi wakawaunga mkono. Mwishowe walifaulu kumwondoa. Hiyo ni adhabu ya kanisa kwa kinyume, na ni njia nyingine ambayo Mungu analitunza kanisa Lake kwa usafi!

Tunapaswa kufikiri juu ya yote matatu – kumpenda Mungu kwetu, matumaini ya thawabu na hofu kwamba tutaadhibiwa – kuwa ni ishara nyingine ya neema ya Mungu kwetu. Kila moja ni zawadi ambayo hakulazimika kutoa, lakini ameitoa, kwa neema Yake. Yeye apokee utukufu wote kwa utakatifu wetu!

“Mkristo” Asiyeshika Sheria

SURA YA TANO

Ni Jumapili asubuhi kanisani kwenu – kama saa tano na dakika arobaini hivi. Kipindi cha sifa kimekwisha, sadaka zimeshakusanywa, na sasa wakati umefika wa kusikia Maandiko yakisomwa na mahubiri kutolewa. Mchungaji wako anapanda mimbarani, anafungua kitabu kikubwa cheusi, anavuta pumzi yake kisha anapaza sauti yake huku akiwa ameinua mikono juu na kusema kwa mamlaka: “Mtu anahesabiwa haki kwa matendo, si kwa imani tu!”

Je, walio wengi kanisani kwenu wangeitikiaje maneno hayo? Je, wangeshangazwa na kupotoka kwa mchungaji? Au je, wangekasirishwa kwamba anapingana na maandiko yote ya Paulo kuhusu wokovu, ambayo yanataja kweli zenye thamani kubwa sana, zilizogunduliwa tena wakati wa Matengenezo ya Kanisa? Au je, wangemwita mkazia kushika sheria? Au, wangetambua kwamba amesoma maneno ya Yakobo 2:24?

Wale ambao wangeitikia vibaya wanawakilisha makundi ya watu wanaojiita Wakristo, waliokosea vibaya sana. Pasipo kuelewa asili ya imani yenye kuokoa, wao hudhani kwamba matendo yanapingana na imani, wakati ambapo kihalisi ni kwamba matendo yameunganika na imani ya kweli. Kama alivyoandika Martin Luther: “Haiwezekani kutenganisha kamwe matendo na imani, kama ambavyo haiwezekani kutenganisha joto na nuru kutoka kwenye moto.”

Luther aliwakatia jina wale walioamini kwamba kwa kuwa wokovu ni zawadi itolewayo bure kwa neema ya Mungu, kuzitii sheria za Mungu si muhimu. Aliwaita “wapingao kushika sheria” – antinomians – kutokana na maneno ya Kilatini mawili: anti – kinyume cha; na nomos – sheria au torati.

Leo hii makanisa ya KiProtestanti yamejaa watu wanaopinga kushika sheria, na kama Luther angekuwa hai, angepinga sana upotovu huo na kudai watu wafanye upya imani zao. Wala asingekosa kuungwa mkono na Maandiko mengi kuhusu jambo hilo, kwa sababu Bwana Yesu Mwenyewe, na Paulo, na Petro, na Yakobo, na Yohana, na Yuda pia walionya juu ya jambo hilo. Ukweli ni kwamba Luther angepata maandiko mengi sana ya kuunga mkono hoja yake kuliko aliyokuwa nayo ili kuunga mkono kweli za Matengenezo wakati alipoyafanya. Maonyo yatolewayo na Agano Jipya juu ya kosa la kupuuza sheria ni mengi sana kuliko maonyo yatolewayo kinyume cha kushika sheria.

Makosa Hatari Mawili

Katika siku za Luther, kanisa lilikuwa limezama katika kushika sheria. Wengi katika watu waliokwenda makanisani walijua kwamba wokovu unapatikana kwa kufanya kitu. Mtu angeweza kujipatia alama ambazo zingepunguza mamia na hata maelfu ya miaka ya adhabu yake ya baadaye huko Toharani (au purgatori) kama angenunua cheti cha msamaha, kama angekwenda kutazama mabaki ya miili ya watakatifu au vitu vilivyoitwa vitakatifu, kama angefanya kitubio na kadhalika. Injili ilikuwa imepotea.

Lakini, wakati Luther aliposoma kitabu cha Warumi aligundua kwamba wokovu ni zawadi itolewayo bure, inayopokelewa kwa imani tu. Akazaliwa mara ya pili, na mara moja akaanza kuwabana wenzake akitumia zile kweli zilizomweka huru. (Yaani, imani yake ilianza kufanya kazi!) Ukazuka ubishi mkali, lakini mwishowe, kupitia kwa Luther mwenyewe na watenda kazi wengine waliohusika na Matengenezo ya Kanisa, wengi walikuja kuamini Injili ya neema ya Mungu.

Lakini, kulikuwepo na hatari iliyojificha ya Injili kama hiyo, na hata hao watengenezaji walifahamu. Iliwezekana kwamba neema ya Mungu ingeweza kutumiwa kama kibali cha kutenda dhambi. Umuhimu wa matendo mema ungeweza kupuuzwa, na uzushi mpya ungechukua nafasi pa ule wa zamani, ambao ungekuwa mbaya tu na wa kupotosha kabisa. Hivyo, watengenezaji wa Kanisa walitangaza kwa uangalifu sana ujumbe huu: “Ni imani tu inayookoa; lakini imani yenye kuokoa haiko peke yake.”

Leo hii, miaka mia nyingi baadaye, kile walichohofu kimetujia sisi. Waenda kanisani leo hawana haja ya kuambiwa kwamba matendo yao mafu hayawezi kuwaokoa, kama ilivyokuwa kwa washika sheria wa siku za Martin Luther. Badala yake, wanachohitaji kuambiwa ni kwamba imani yao iliyokufa haiwezi kuwaokoa. Wengi wamenunua hisa katika injili ya uongo inayoahidi kwamba kuna mbingu pasipo utakatifu. Neema wanayoitumaini inapelekea kwenye ruhusa ya kutenda dhambi badala ya kumtii Kristo. Lakini Yesu Kristo – ambaye ni yeye yule jana na leo na hata milele – bado anawaonya wanaopinga kushika sheria kila mahali kwa maneno haya: “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa minguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21 – Maandiko mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Kushika Sheria Maana Yake Nini?

Maneno “kushika sheria” yameeleweka na kutumiwa vibaya sana kuliko kawaida. Kila anayehubiri kujikana, utii au utakatifu siku hizi yuko hatarini kubandikwa jina kwamba yeye ni mhubiri wa kushika sheria. Ni mara nyingi utawasikia wanaojiita Wakristo wakisema hivi: “Nilikuwa mshirika kwenye kanisa linaloshika sheria sana. Mchungaji wetu alikuwa anahubiri kinyume cha kutazama sinema chafu.” Tamko kama hilo linaonyesha kwamba kwa kweli huyo anayesema haelewi maana ya kushika sheria. Maana ya kushika sheria si kushikilia kiwango cha utakatifu kitokanacho na Neno la Mungu. Ni kujaribu kujipatia wokovu – kwa sehemu au wote kabisa – kwa matendo ya mtu. Kama mtu akisema hivi: “Nilikuwa mshirika kwenye kanisa linaloshika sheria sana. Mchungaji wetu alikuwa akihubiri na kutuambia kwamba tungeweza kujitengenezea mahali petu mbinguni kwa kuacha kutazama sinema chafu,” hapo angekuwa amepata kabisa maana ya kushika sheria.

Upotofu wa fundisho hili ni kwamba linatoa njia nyingine ya kupata wokovu kuliko ambayo Mungu amekwisha itoa kwa njia ya Kristo. Ujinga wa mwenye kuamini fundisho hilo ni kwamba yeye anatazamia kisichowezekana – yaani, kwamba anaweza kuwa mzuri kiasi cha kutosha kustahili kuingia mbinguni. Ukweli ni huu: Uwezekano wa sisi kuwa wazuri kiasi cha kutosha kustahili kupata nafasi mbinguni ulimalizika zamani sana: Mara ile ya kwanza Mungu alipotuwajibisha kwa ajili ya dhambi yetu. Kinadharia, kama mtu angeweza kuishi maisha bila dhambi, angeweza kuingia mbinguni bila ya kuhitaji Mwokozi. Lakini kwa sababu sisi sote tumetenda dhambi, kama tunahitaji kuokolewa, basi tunahitaji njia nyingine ya wokovu. Ni dhahiri kwamba njia hiyo inawezekana tu kwa kupitia neema ya Mungu. Habari njema za Injili ni kwamba Mungu amekwisha itoa neema Yake kwetu bila kukiuka viwango Vyake vya utakatifu kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye alichukua mahali petu.

Labda tafsiri bora zaidi ya fundisho la kushika sheria linaelezwa kwa mchoro huu rahisi ufuatao:

MATENDO = WOKOVU

Maana ya mshale ni “hupelekea…”. Mwenye kushika fundisho hilo anafikiri kwamba matendo yake yatapelekea yeye apate wokovu. Kwa sababu moyo wake haujazaliwa mara ya pili, na hauna imani wala pendo kwa Mungu, mtu mwenye kuamini kuhusu kushika sheria hutokeza utii wa nje tu wa Torati huku akijitahidi sana kupata upendeleo wa Mungu kwa matendo yake.

Aina nyingine ya fundisho hili yaweza kuonyeshwa kwa mchoro huu ufuatao:

IMANI + MATENDO = WOKOVU

Huyu anayeamini hivi huongeza imani na matendo pamoja, akifikiri kwamba jumla yake itahakikisha wokovu wake. Kwa sehemu anategemea matendo yake. Hili ndilo fundisho kuhusu kushika sheria ambalo Paulo alilipinga katika waraka wake kwa Wagalatia.

Jinsi Biblia inavyofundisha kuhusu swala hilo inaweza kuonyeshwa kwa mchoro huu rahisi:

IMANI = WOKOVU + MATENDO

Wale wanaoiamini Injili kweli kweli, hawawi wameokolea tu bali wanabadilishwa na ile neema ya Mungu, nao huonyesha kazi ya Mungu katika maisha yao kwa utiifu wao wa furaha. Tofauti na yule anayeshika sheria, utii wa mwamini wa kweli hutoka ndani yake kwa sababu moyo wake umebadilishwa.

Hatimaye tuonyeshe juu ya fundisho linalopinga kushika sheria kwa mchoro ufuatao:

IMANI = WOKOVU – MATENDO

Huyu anayepinga kushika sheria anadhani kwamba imani yake inaleta wokovu wake, hata ingawa matendo ya kuthibitisha kwamba maisha yamebadilishwa hayaonekani. Tena, mara nyingi anakosa kuelewa vizuri vitu vingine vitano, kama ifuatavyo: (1) asili ya imani yenye kuokoa; (2) kusudi la Mungu kuwaokoa watu; (3) kazi kamili ya neema ya Mungu katika maisha ya wale wanaoamini; (4) uhusiano wa Mkristo na sheria ya Mungu; na (5) sababu halisi na umuhimu wa toba. Hebu tutazame hayo yote hatua kwa hatua.

Asili Ya Imani Yenye Kuokoa

Asiyeshika sheria anahesabu imani kuwa si kitu zaidi ya kukubali au kukiri kitu fulani akilini. Yeye hudhani kwamba kukubali kwake kweli fulani za kimafundisho ndiyo imani yenye kuokoa. Kwa kuwa anajua kwamba Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za kila mtu, na kwa kuwa anajua kwamba wokovu si kwa matendo bali ni kwa imani, anafikiri ameokoka.

Hata shetani anajua kwamba Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi za wote! Shetani pia anajua kwamba watu hawaokolewi kwa matendo bali kwa njia ya imani. Ni kitu gani basi kinachotufanya sisi tufikiri kwamba kujua hayo kunatufanya kuwa wenye haki machoni pa Mungu?

Imani ya kweli yenye kuokoa ni zaidi ya kukiri au kujua kitu kwa akili. Biblia inafafanua imani kwamba ni “kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyo-onekana” (Waebrania 11:1 – Maneno mepesi ni ili kutilia mkazo). Kinachosababisha wokovu ni kuamini kwa moyo (ona Warumi 10:10). Imani ya kweli kila mara inadhihirishwa kwa matendo ya nje.

Lakini, hawa wanaopinga kushika sheria mara nyingi hujaribu kuondoa matendo kwenye imani, na hata wanafikia mahali pa kupambanisha hayo mawili. Wanatamka – kwa utauwa sana – kwamba, kwa sababu wokovu unatokana na neema ya Mungu tu, hawatatazama matendo yao hata moja kwa ajili ya kupata uhakika wa wokovu, wasije “wakatumainia matendo yao.”

Lakini – kama tutakavyoona sasa hivi – hayo hayakuwa mawazo ya Bwana Yesu, au Yohana Mbatizaji, au mtume Yohana, au Paulo, au Petro na hata Yakobo. Kwa mfano: Yohana aliandika kwamba upendo tunaoonyesha kwa waamini wenzetu ni njia mojawapo kati ya nyingi ambazo kwazo tunaweza kutambua ikiwa kweli tumezaliwa mara ya pili. Anasema hivi:

Sisi tunajua [angalia neno hilo: tunajua] ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. … Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote (1Yohana 3:14, 17-20. Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Yohana aliamini kwamba matendo yetu yanaweza kutuhakikisha juu ya kazi ya neema ya Mungu maishani mwetu. Hii ni tofauti na kutegemea kwamba matendo ya mtu yanampatia wokovu. Matendo yetu mema hayatupi aina fulani ya hisa – yanathibitisha tu kwamba kuna kitu kimetokea. Hutoa uhakikisho wa ziada wa wokovu wetu zaidi ya ule utolewao kwa ahadi za Injili. Tunapoyatazama matendo maishani mwetu, tunaweza kusema, “Mungu asifiwe kwa ajili ya ushahidi huu wa neema ya Mungu itendayo kazi maishani mwangu!” Matendo yetu mema yametendwa “katika Mungu” (Yohana 3:21).

Vile vile Yohana aliandika hivi katika waraka wake wa kwanza:

Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake (1Yohana 3:9-10).

Je, Yohana aliamini kwamba kuzaliwa upya hubadilisha jinsi mtu anavyoishi? Ndiyo! Wale ambao wamezaliwa kweli na Mungu hutenda haki na kuwapenda waamini wenzao. Hii haimaanishi kwamba waamini wa kweli hawatendi dhambi au kwamba kila wakati wanaonyesha pendo kamilifu (ona 1Yohana 1:8-9; 4:17-18). Inachoonyesha ni kwamba haki na upendo ni alama au tabia kuu katika maisha yao, kinyume na wale ambao hawajaokoka, ambao kawaida yao ni tabia isiyo ya haki na ubinafsi. Yohana aliandika mara nyingi sana katika barua yake kuhusu kuishi maisha ya haki na kuwapenda ndugu wengine waaminio ili kuwapa uhakika wa wokovu wale wasomaji wake. Anasema hivi:

Nimewaandikia ninyi mambo hayo [yaani, yaliyomo katika barua hii], ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu (1Yohana 5:13 – Maneno mapesi ni kwa ajili ya mkazo).

Yohana aliamini kwamba wanaokiri Ukristo lazima wachunguze maisha yao ili kupata uhakika kuhusu utendaji kazi wa neema ya Mungu ndani yao, kwa sababu yeye pia aliamini kwamba kuna mlingano kati ya imani na mwenendo.

Asemavyo Paulo Kuhusu Uhusiano Wa Imani Na Matendo

Mtume Paulo hakuamini kwamba matendo na utii vinaweza kuondolewa kwenye imani, au kwamba vitu hivyo vinapingana. Badala yake, katika kitabu cha Warumi aliandika juu ya “utii utokanao na imani” (Warumi 1:5; 16:26). Tafsiri iliyo wazi ya maneno hayo ni kwamba imani huonekana kwa utii. Nikisema hivi: “utii wa Paulo”, maana inayoeleweka ni kwamba Paulo huonyesha utii. Nikisema hivi: “furaha ya wokovu” bila shaka maana yangu ni kwamba wokovu unaonekana kwa furaha. Katika yote hayo mawili ambacho nisingekuwa nasema ni kwamba kimoja ni badala ya kingine, kama wale wanaopinga kushika sheria wanavyotaka tuamini kwamba ndiyo maana ya Paulo anaposema “utii wa imani”. Wao wanadai maana yake ni kwamba hatuna haja ya kuwa na utii, kwa sababu imani ndiyo inasimama badala yake. Hiyo ingekuwa sawa na kusema kwamba ninaposema “utii wa Paulo” maana yake ni kwamba sina haja ya Paulo kwa sababu ninao utii wake, au, kwa mfano ule mwingine, kwamba sihitaji wokovu kwa sababu nina furaha, ambayo ni mbadala unaokubalika.

Paulo hakuona tu kwamba Injili ni kitu cha kuaminiwa, bali pia aliihesabu kuwa ni kitu tunachotakiwa kukitii. Aliwaambia Wakristo Wathesalonike kwamba wale “wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu … wataadhibiwa kwa maangamizi ya milele” (2Wathes. 1:8, 9 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Swali: Kuna nini cha kutii kuhusu Injili? Kwanza: Tunaamriwa na Mungu kuiamini Injili, na tendo la kuamini ni utii (ona Marko 1:15). Basi, inawezekanaje wengine wadai kwamba utii na imani vinapingana, wakati kuamini ni tendo la utii?

Pili ni kwamba, Yesu aliwaagiza watu watubu na kuiamini Injili. Pia alituagiza sisi tuhubiri “toba na msamaha wa dhambi” (Luka 24:47). Paulo alifanya hivyo, akiwatangazia watu kwamba sharti “watubu na kumgeukia Mungu, na kufanya matendo yanayostahili toba” (Matendo 26:20). Kutubu ni tendo la utii, ni itikio kwa agizo la kimungu. Wokovu huanza maishani mwa mtu kwa tendo la utii ambalo nalo ni tendo la imani.

Paulo aliwaandikia Wathesalonike akiwasifu kwa “kazi yao ya imani na upendo” (1Wathes. 1:3 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo). Hakuona imani na matendo kuwa vitu viwili visivyoweza kuchanganywa. Sawa na mtume Yakobo, yeye aliamini kwamba imani ya kweli inatenda kazi. Aliwaandikia Wakristo Wagalatia waliokuwa hatarini kudanganywa na kutekwa wafikiri kwamba tohara ilikuwa lazima kwa ajili ya kuokoka, kama ifuatavyo:

Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo (Wagalatia 5:6 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kama mtume Yohana, Paulo aliamini kwamba imani ya kweli ilifanya kazi kupitia upendo. Upendo ni tunda la msingi sana katika imani. Kwa maneno mengine, Paulo anasema hivi: “Maana, katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana yoyote; ni matendo ya kibinadamu, ila imani huanza kazi ya kimungu katika maisha ya mtu mpaka kumfikisha kwenye mahali ambapo matendo yake ya upendo yanatoka kwa Mungu.”

Maelezo Ya Kitabu Cha Waebrania Kuhusu Imani

Mwandishi wa kitabu cha Waebrania aliamini kwamba kumtii Yesu Kristo ni kitu muhimu kwa ajili ya wokovu. Aliandika hivi:

Naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii (Waebrania 5:9).

Mwandishi angeweza pia kusema kwamba Yesu alifanyika asili ya wokovu wa milele kwa wote wanaomwamini, na angekuwa anasema kitu kile kile. Kwake yeye, imani – kitu ambacho anakitaja zaidi ya mara thelathini katika kitabu chake – ilikuwa inasababisha matendo. Kila mmoja katika wale “mashujaa wa imani” wa sura ya 11 walifanya kitu fulani kwa sababu waliamini.

Katika sura ya tatu na nne ya kitabu cha Waebrania, ona jinsi mwandishi anavyotumia maneno kutokuamini na kutokutii mara kwa mara.

Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao … wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao … (Waebrania 3:19; 4:6 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Kwa sababu wengi katika Waisraeli hawakuziamini habari njema, hawakumtii Mungu. Kwa sababu hawakufanya kile ambacho Mungu aliamuru, walithibitisha kwamba hawakuamini ahadi Yake.

Maneno Ya Yohana Mbatizaji Na Yesu Kuhusu Matendo

Yohana Mbatizaji aliamini kwamba hakuna kutengana kati ya imani na mwenendo. Hebu soma jinsi alivyotumia maneno kuamini na kutii.

Amwaminiye [pisteuo] Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini [apeitheo] Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia (Yohana 3:36 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Kuna kuwa wazi zaidi ya hapo? Na je, inawezekanaje mtu kusema kwamba ni makosa kuchunguza maisha yetu ili kuamua msimamo wetu kiroho tusije “tukategemea matendo yetu kutuokoa”? Narudia tena: Tunapaswa kuchunguza matendo yetu kwa sababu Maandiko yako wazi kabisa kwamba inawezekana kuwa na imani isiyozaa. Kutumaini imani isiyofanya kazi kwamba itatuokoa ni hatari sana, sawa tu na kutumaini kwamba matendo yetu yatatusaidia kupata wokovu. Ulinzi wa pekee unaofaa kinyume cha hatari zote hizo ni kuchunguza matendo yetu ambayo ni uthibitisho wa imani ya kweli, yenye kuokoa.

Yesu vile vile aliamini kwamba imani ilibadilisha mwenendo. Alisema kwamba wale wamwaminio Yeye watatenda matendo yale yale aliyotenda (ona Yohana 14:12). Alitabiri pia kwamba wale ambao “wangetenda matendo mema” wangefurahia “ufufuo wa uzima”, na wale ambao “wangetenda matendo maovu” wangepatikana na “ufufuo wa hukumu” (Yohana 5:29). Pia alionya kwamba wale tu wanaotenda mapenzi ya Mungu ndiyo watakaoingia mbinguni, na kwamba waamini wa kweli na wasio wa kweli wanaweza kujulikana kwa matunda yao (ona Mathayo 7:19-23). Njia ya pekee iliyo sahihi ya kutafsiri maonyo Yake ni kwamba imani yenye kuokoa inathibitishwa kwa utii, isipokuwa kama alikuwa anafundisha kwamba wokovu unapatikana kwa matendo.

Vile vile Yesu alionya kwamba wale tu watendao mapenzi ya Baba Yake ndiyo ndugu na dada Zake (ona Mathayo 12:49-50). Kama tulivyojifunza katika sura iliyopita, mara nyingi Yesu hakusema chochote juu ya imani alipowaita watu waje kuokoka. Aliwaambia wamtafutao kujikana, wajitwike msalaba wao na kumfuata wasije wakapoteza nafsi zao (ona Marko 8:34-38). Aliwaita watu kuingia kwenye uanafunzi wenye gharama, na kujitoa kweli kweli, au imani ya kweli.

Akijaribu kueleza maana ya kumwamini, Yesu alifikia mahali pa kuwaambia watu kwamba walihitaji kumla Yeye (ona Yohana 6:47-56), kitu ambacho hata sisi tunakumbushwa kila mara tunaposhiriki Meza ya Bwana. Kumwamini Yesu ni kufanyika mmoja Naye. Tendo la kwanza la imani la mwamini mpya – yaani ubatizo katika maji – ni tangazo hadharani kwamba yeye na Yesu wameunganika katika mauti Yake, kuzikwa na kufufuka Kwake.

Kumwamini Yesu ni kujiunga Naye. Angalia: “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye” (1Wakor. 6:17). Kumwamini Yesu ni kukaa ndani Yake, kama anavyosema Mwenyewe: “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu … Mtu yeyote asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; nao huyakusanya na kuyatupa motoni, yakateketea” (Yohana 15:4, 6). Itawezekanaje mtu awe na umoja wa namna hiyo na Kristo, na isibadilishe tabia yake?

Asemavyo Yakobo Kuhusu Imani Yenye Kuokoa

Pengine, maelezo maarufu zaidi kuhusu imani yenye kuokoa, na ambayo yanawasumbua sana wale wanaopinga kushika sheria, yanapatikana katika waraka wa Yakobo katika maandiko tuliyotazama kwa kifupi katika sura zilizopita. Anasema hivi:

Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? (Yakobo 2:14).

Jibu dhahiri kwa swali la Yakobo ni Hapana. Imani bia matendo haiokoi.

Pamoja na kwamba kweli hiyo iko wazi hivyo, wanaopinga kushika sheria wa kisasa wangependa tuamini kwamba imani bila matendo inaweza kumwokoa mtu. Wanashikiliaje msimamo kama huo licha ya maneno ya Yakobo? Maelezo yao kuhusu mafundisho ya Yakobo ni magumu kiasi kwamba wasomaji wa Yakobo mwenyewe wasingeweza kuelewa. Cha kwanza: Hawa watu wanataka sisi tuamini kwamba Yakobo hakuwa anazunguma juu ya kuokoka kutokana na kwenda jehanamu, bali kuokoka kutokana na “maisha ya dhambi hapa duniani”. Eti, Yakobo alikuwa anajaribu kuwashawishi wasomaji wake waamini kwamba walipaswa kuwa na matendo pamoja na imani yao kama walitaka kuokolewa kutoka “maisha ya dhambi na mauti” hapa duniani.

Hayo maneno “maisha ya dhambi na mauti” bila shaka maana yake ni maisha ya dhambi. Na, kuokolewa kutoka “maisha ya dhambi na mauti hapa duniani” bila shaka maana yake ni kuishi maisha ya utii, yaani, kutenda matendo mema. Basi, baadhi ya hao wanataka tuamini kwamba Yakobo alikuwa anarekebisha kosa kubwa katika mafundisho ya wasomaji wake, kwamba wao walifikiri wanaweza kuishi maisha ya kutii wakiwa na imani isiyokuwa na matendo ya utii! Je, inawezekana kweli kwamba Yakobo aliwaona wasomaji wake kuwa wapumbavu kiasi cha kutojua tayari mambo ambayo wote waliyajua? Na je, hao wanafikiri na sisi ni wapumbavu kiasi hicho, tukubali tafsiri isiyo sahihi ya mafundisho ya Yakobo ambayo yako wazi kabisa?

Katika kuendelea kupinga hoja hiyo, tunasema kwamba maandiko yanayotangulia na yanayofuata maneno ya Yakobo kuhusu uhusiano kati ya imani na matendo ni hukumu ijayo (ona Yakobo 2:12-13; 3:1). Kilichokuwa mawazoni mwa Yakobo ni wokovu wa milele, si wokovu wa muda wa kidunia kutoka “maisha ya dhambi na mauti”.

Imani Ikitenda Kazi Kwa Upendo

Hii tafsiri ya wanaopinga kushika sheria inazidi kuonekana ni ujinga wakati mtu anaposoma maneno ya Yakobo, kama ifuatavyo:

Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, ‘Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba’, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake (Yakobo 2:15-17).

Kuna wafuasi wa fundisho hili wanaotaka tuamini kwamba imani iliyokufa bado ni imani yenye kuokoa, ni kwamba tu ni imani iliyokufa na siyo imani hai yenye kuokoa. Lakini Yakobo tayari amekwisha sema kwamba imani bila matendo haiwezi kumwokoa yeyote, na hiyo ndiyo imani iliyokufa – imani isiyo na matendo.

Inapendeza sana kwamba mfano aliotumia Yakobo kueleza juu ya imani iliyokufa ni picha ya mtu anayekiri Ukristo ambaye hafanyi chochote kumsaidia ndugu au dada ambaye ni maskini. Sawa tu na Yesu, Yohana na Paulo, Yakobo naye aliamini kwamba matunda ya imani ya kweli ni upendo kwa ndugu, wenye kuonyeshwa kwa kukutana na mahitaji yanayowabana.

Yakobo anaendelea kuandika juu ya kutowezekana kwa imani ya kweli kukosa matendo. Anasema hivi:

Lakini mtu atasema, ‘Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?’ (akobo 2:18-20).

Kama anavyosema Yakobo, tena vizuri tu, mtu anaweza kudai kwamba ana imani, lakini hawezi kuthibitisha kwamba ana imani pasipo matendo. Kwa upande mwingine, mtu mwingine anaweza asidai kwamba anayo imani, lakini matendo yake yanasema kitu asicholazimika kudai. Matendo yana sauti kubwa kuliko maneno. Basi, wale wanaosema kwamba wanaamini Mungu ni mmoja (Kumbu. 6:4) lakini hawana matendo yenye kulingana na maneno yao wanajidanganya wenyewe. Pepo pia wanaamini kwamba Mungu ni mmoja, nao wanatenda kama wanavyoamini – wanatetemeka! Ni “wapumbavu” tu ndiyo wasiotambua kwamba imani pasipo matendo “haizai” (au haifai kitu) (Yakobo 2:20). Maana yake ni kwamba haifai kwa lolote.

Imani Hai Ya Ibrahimu

Yakobo anaendeleza hoja yake akimtaja Ibrahimu, ambaye alihesabiwa haki kwa imani kuwa kama mfano wa mtu mwenye imani hai. Anasema hivi:

Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu’. Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake (Yakobo 2:21-14).

Sasa, Yakobo aseme kwa uwazi upi kuliko huo? Imani ya Ibrahimu ilikuwa imani hai iliyomtii Mungu. Si imani bila matendo iliyomfanya kuhesabiwa haki bali ni imani iliyothibitishwa kwa matendo. Yakobo anaendelea mpaka anafikia mahali pa kusema kitu ambacho, kikiondolewa kwenye mantiki yake, kinaweza kuhesabiwa kuwa uzushi. Anasema hivi: “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:24).

Sasa: Baadhi ya hao wenye kuamini kutokushika sheria wanajiondoaje katika tatizo ambalo Yakobo anawaingiza? Wanafikiri kwamba Yakobo hakumaanisha Ibrahimu alihesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo yake, bali alihesabiwa haki mbele za wanadamu. Lakini hilo nalo ni upuzi. Je, tuamini kwamba wasomaji wa Yakobo waliamini mtu angeweza kuhesabiwa haki mbele za wanadamu bila matendo, na kwamba Yakobo aliona kosa hilo kuwa ni kubwa sana kiasi cha kuwaandikia ili kuwakemea? Je, kweli hicho ndicho kitu alichoandika Yakobo ili kirekebishwe?

Ona pia kwamba Yakobo hakusema chochote kuhusu Ibrahimu kuhesabiwa haki mbele za watu. Zaidi: Wakati Ibrahimu alipokuwa karibu kumtoa Isaka kama dhabihu, hapakwepo watu wengine ili kuona tendo lake hilo la utii ambalo inasemekana lilimfanya ahesabiwe haki mbele za watu. Ila, Mungu alikuwa anatazama, Naye alisema kitu mara moja baada ya kuona tendo la utii la Ibrahimu. Alisema hivi:

“Sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee… Kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu” (Mwanzo 22:12; 16-18).

Tukio zima lilikuwa kipimo kutoka kwa Mungu (ona Mwanzo 22:1), ili kuona kitu ambacho Ibrahimu angefanya. Zaidi ni kwamba, Yakobo anasema wakati Ibrahimu alipomtii Mungu, andiko lilitimizwa linalosema, “Na Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki” (Yakobo 2:23). Sasa, Ibrahimu alihesabiwa kuwa mwenye haki mbele za nani – Mungu au wanadamu? Ni dhahiri kwamba alihesabiwa haki mbele za Mungu.

Hii haimaanishi kwamba Ibrahimu hakuhesabiwa haki na Mungu miaka kabla ya kukaribia kumtoa Isaka sadaka. Maandiko yanatuambia hivyo (ona Mwanzo 15:6; Warumi 4:3). Lakini, tendo la kushangaza la Ibrahimu la kutii, alipokuwa karibu kumtoa mwana wake sadaka, lilionyesha imani hai aliyokuwa nayo tangu alipoanza kuamini. Wakati huu imani yake ilikuwa inakamilishwa kwa matendo yake. Imani iliyosababisha Ibrahimu kutangazwa mwenye haki na Mungu ilikuwa imani ya kweli, iliyothibitishwa kwa utii wake.

Je, Yakobo Hapingani Na Paulo?

Lakini, mbona Paulo aliandika kwamba “mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria” (Warumi 3:28 – Maneno mepesi ili kutilia mkazo)? Je, hayo hayapingani na kile ambacho Yakobo anasema juu ya sisi kuhesabiwa haki kwa matendo yetu, kama yeye naye anasema anachosema Paulo – kuhusu kuhesabiwa haki mbele za Mungu?

Jibu ni hapana – Paulo na Yakobo walikuwa wanazungumza juu ya kuhesabiwa haki mbele za Mungu, na maneno yao yanayoonekana kama yanapingana ni rahisi tu kuyaunganisha. Paulo alikuwa anasema na washika sheria waliohesabu kwamba Torati ndiyo njia ya kuokoka. Alitaka wao wajue kwamba wokovu hauwezi kupatikana kwa juhudi zozote dhaifu za mwanadamu za kushika Torati. Wokovu ni zawadi itolewayo bure, ambayo imepatikana kwa neema ya Mungu, yenye kupokelewa kwa imani.

Ila – Yakobo alikuwa anasema na wale ambao walikuwa wamepotosha kweli ya wokovu kwa neema kwa njia ya imani, na kuifanya kibali cha kutenda dhambi. Wito wao ulikuwa “kuhesabiwa haki kwa imani tu,” lakini, kama wapingao kushika sheria wa kisasa, walikuwa wameifasiri imani kuwa si kitu zaidi ya ukiri tu wa kinywa – imani inayoweza kukosa matendo yoyote yanayoambatana nayo. Yakobo aliandika kupinga uongo huo, akifafanua vizuri sana ili aeleweke, kama ifuatavyo: “Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake” (Yakobo 2:24). Sababu iliyomwezesha Yakobo kutoa tamko kama hilo ni kwamba matendo yetu huonyesha imani yetu, ambayo kwa hiyo tunahesabiwa kuwa wenye haki mbele za Mungu.

Maandiko yanafundisha kwamba katika hukumu za siku za baadaye, karima (au mwelekeo) ya milele kwa watu fulani itaamuliwa na matendo yao (ona Mathayo 12:36-37; 25:31-46; Yohana 5:28-29; Ufunuo 20:12-13). Hii ni kwa sababu matendo ndiyo huthibitisha imani. Basi kwa hali hiyo, kama Yakobo alivyotamka, matendo ya watu huwahesabia haki mbele za Mungu.

Yakobo anamalizia mafundisho yake kuhusu asili ya imani yenye kuokoa kwa kutumia mfano mwingine wa Biblia wa mtu aliyeokolewa kwa imani iliyotenda kazi.

Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:25-26).

Je, nini kingempata Rahabu kama angekuwa na imani isiyokuwa na matendo (kama basi inawezekana)? Angeangamia na kila mtu aliyeangamia Yeriko. Lakini imani yake hai inasimama siku hizi kama mfano kwa wote ambao wanataka kuokolewa kutokana na ghadhabu ya Mungu. Rahabu hakuwa mkataa kushika sheria.

Wenye kufuata imani hiyo wanapenda kutumia yule mwizi pale msalabani kwamba ni mfano wa mtu aliyeokolewa kwa imani ambayo haikuwa na matendo. Lakini, wasome Maandiko vizuri zaidi. Huyo mwizi aliyetubu alionyesha imani yake hai kwa matendo katika masaa yake ya mwisho maishani. Kwanza alitubu waziwazi kwamba alikuwa mwenye dhambi. Pili: Alitamka kwamba Yesu hakuwa na hatia, na hakustahili kifo, akifikia mahali pa kumtetea kwa yule mwizi mwingine, hata kumkemea. Tatu: Yeye alimtazama Yesu kuwa asili ya wokovu, na mbele ya kundi lenye kudhihaki, alimwomba waziwazi ampe wokovu (ona Luka 23:40-43). Yule mwizi aliyetubu alikuwa hana nafasi ya kuonyesha imani yake kwa njia nyingine zaidi ya hiyo. Hata hivyo, katika dakika chache alizokuwa nazo, alionyesha imani yake kuliko inayoonyeshwa na wanaojiita Wakristo kwa miaka mingi ya maisha yao.

Kweli ya pili ambayo wapingao kushika sheria wanashindwa kuipata ni hii:

Kusudi La Mungu Kuwaokoa Watu

Muda mrefu tu kabla ya kuandikwa kwa Agano Jipya na Yesu kutembea hapa duniani, Mungu alidhihirisha wazi wazi kusudi Lake kuwaokoa watu – alitaka kuwafanya watakatifu. Kwa mfano, Bwana anasema hivi kupitia nabii Yeremia:

“ ‘Angalia, siku zinakuja’ asema BWANA, ‘nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililofanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao’, asema BWANA. ‘Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile,’ asema BWANA; ‘Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake na kila mtu ndugu yake wakisema, Mjue BWANA; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao,’ asema Bwana; ‘maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena’.” (Yeremia 31:31-34)

Unabii huu mzima unarudiwa tena katika Waebrania 8:8-12, na mwandishi wa Waebrania anahesabu kwamba unawahusu waamini wote wa Agano Jipya.

Kwanza: Ona kwamba Mungu anaahidi kufanya agano jipya ambalo halitakuwa kama lile la kale (31:31-32). Lingekuwaje tofauti? Agano la kale lilivunjwa na wengi katika Israeli, lakini isingekuwa hivyo kwa wale walio chini ya agano jipya. Kwa nini? Kwa sababu Mungu angefanya kazi isiyo ya kawaida maishani mwao.

Angeiweka sheria Yake ndani yao, akiiandika kwenye mioyo yao. Matokeo ni kwamba angekuwa Mungu wao na wao wangekuwa watu Wake (31:33). Chini ya agano la kale, Bwana alikusudia kuwa Mungu wa Waisraeli nao wawe watu Wake, lakini haikufanyika hivyo kwa sababu waliasi agano lile. Hawakumtii, na kwa kufanya hivyo walithibitisha kwamba hakuwa Mungu wao, nao hawakuwa watu Wake. Lakini kupitia kwa Yeremia, Bwana aliwaahidi wale wote chini ya agano jipya kwamba Yeye angekuwa Mungu wao na wao wangekuwa watu Wake. Ingekuwa hivyo kwa sababu wangemtii. Asili ya utii wao ingekuwa ile kazi Yake ndani yao.

Kila mmoja katika agano jipya ange”mjua Bwana” kweli kweli, kwa sababu wamesamehewa dhambi zao. Hii ni picha nyingine kuhusu uhusiano wao thabiti. Yohana aliandika hivi: “Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, ‘Nimemjua,’ wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake” (1Yohana 2:3-4). Kusudi la Mungu kwa ajili yetu tangu zamani ni kwamba tumjue kweli kweli.

Unabii mwingine unaofanana na huo, wenye kuwahusu waamini wote wa agano jipya unapatikana katika Ezekieli 36:27. Hapo Mungu aliahidi hivi: “Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.” Matokeo ya kumweka Roho Mtakatifu ndani yetu yangekuwa utii wetu. Kama Mungu alitaka kutusamehe tu, asingemweka Roho Mtakatifu ndani yetu. Lakini, hakutaka kutusamehe tu, bali pia alitaka kutubadilisha. Hakutaka kutufanya wenye haki kisheria tu, bali alitaka kutufanya wenye haki kimatendo. Hakutaka Yesu awe kama sisi tu, alitaka na sisi tuwe kama Yesu. Kama jinsi mtume Paulo alivyoandika: “Maana wale aliowajua tangu asili [yaani sisi] aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake … (Warumi 8:29). Hilo ndilo lililokuwa kusudi Lake tangu mwanzo.

Kweli ya tatu ambayo huwa wanaipuuza ni hii:

Kazi Kamilifu Ya Neema Ya Mungu Maishani Mwa Waaminio

Mada iliyopita inapelekea tuingie kwenye hii vizuri sana. Wale wanaopinga kushika sheria wanaamini neema ya Mungu itatusamehe, lakini wanashindwa kutambua kwamba Mungu hutoa vingi zaidi katika neema Yake. Neema ile ile yenye kusamehe pia hutubadilisha.

Neema imeelezwa kuwa ni upendeleo ambao mtu hastahili kuupata. Ndivyo ilivyo. Licha ya uasi wetu, Mungu amemtuma Mwana Wake ili kufa kama dhabihu badala yetu, na kutupa sisi utajiri usiopimika. Hatustahili neema kama hiyo. Lakini wengine, kama anavyosema Yuda, wana “badili neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi” (uda ms. 4). Yaani, wanahesabu upendeleo wa Mungu kuwa kibali cha kutenda dhambi, wakirahisisha kile ambacho kimemgharimu Yeye sana, wakiendelea kwenye njia yao ya kutaka kujitosheleza.

Hilo si itikio ambalo Mungu analitazamia kutoka kwa wale waliopokea neema Yake. Yeye anatazamia kwamba mioyo yetu itayeyuka tunapoanguka mbele Zake kifudifudi, tukiona aibu, tukitubu na tukijaa shukrani. Kama Paulo alivyoandika, neema ya Mungu “yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:12).

Ni dhahiri kwamba tangu siku za kwanza za kanisa, walikuwepo watu wenye imani hii japo hawakuitwa hivyo. Paulo alipinga hoja zao pamoja na maoni yao ya makosa kuhusu neema ya Mungu katika barua zake nyingi. Kwa mfano: Aliwaandikia hivi Warumi:

Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? (Warumi 6:1-2).

Hiyo ndiyo hoja ya hao watu, mbaya kabisa: Hebu tumpe Mungu nafasi zaidi ya kuongeza neema Yake kwa kuendelea kutenda dhambi! Kwa Paulo, wazo la kuishi hivyo ni baya na lenye kuchukiza, kama ambavyo haliwezekani pia. “Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (6:2) Paulo anaelekeza hoja yake kwenye nguvu ya kubadilisha maisha ya neema ya Mungu katika kuzaliwa upya. Wale ambao wamemwamini Yesu kweli kweli wamekufa kwa dhambi.

Paulo anaeleza katika mistari michache inayofuata jinsi hayo yanavyotokea: Ni kwa sisi kuwa ndani ya Kristo aliyekufa na kufufuka. Hivyo na sisi tumekufa na kurudi kuishi tena ili “kuenenda katika upya wa uzima” (Warmi 6:4). Tulipokufa ndani ya Kristo, nguvu ya dhambi ilivunjwa juu yetu. Dhambi ilikuwa nguvu ya kiroho iliyotushika mateka, lakini sasa sisi si watumwa wa dhambi tena kwa sababu “yeye aliyekufa amehesabiwa haki mbali na dhambi” (Warumi 6:7). Ingawa bado tuna uwezo wa kujaribiwa na dhambi na hata kujitolea kwake, hali yetu ya sasa si kama ilivyokuwa kabla hatujazaliwa mara ya pili. Wakati huo, dhambi ilikuwa sehemu ya asili yetu kiroho na ilikuwa na nguvu juu yetu. Basi, ilikuwa kama haiwezekani kwetu sisi kumtii Mungu. Lakini kwa sasa, inawezekana sana kwetu kumtii Mungu, na bila shaka wale ambao wamejitolea wenyewe kwa Kristo katika imani tiifu watatenda kitakatifu sasa kwa sababu wanaweza kufanya hivyo.

Neema Ili Kuwa Watakatifu

Ahadi ya habari njema za neema ya Mungu si tu kwamba tunaweza kusamehewa, bali kwamba tunaweza kufanywa watakatifu. Maandiko yanaonyesha kwamba kuna mabadiliko ya msingi wakati wa kuzaliwa upya, kazi ya Mungu ambayo inatusafisha kabisa kihalisi. Baada ya hapo kuna kazi ya Mungu inayoendelea maishani mwetu, ambayo Maandiko mara nyingi yanaitaja kuwa ni utakaso. Hebu fikiri juu ya ujumbe wa ajabu unaopatikana katika mistari hii ifuatayo:

Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu (1Wakor. 6:9-11).

Katika kanisa la Korintho walikuwepo wenye dhambi wa zamani ambao walikuwa wamefungwa na baadhi ya dhambi hizo za kutisha sana kwa wanadamu. Lakini wakawa wamewekwa huru na kubadilishwa kwa Roho Mtakatifu. Je, si huzuni sana kwamba neema ya Mungu inavyongojea kwa upendo ili kusamehe na kuwaweka huru walawiti, wezi, wazinzi na walevi, kanisa linaandaa mipango ya kuunda makundi ya kuwasaidia “Wakristo” waelewe na waweze kuishi na shida zao hizo? Wakati Neno la Mungu la milele linaposhuhudia juu ya nguvu za kushinda dhambi zilizomo katika Injili, kanisa linaingia katika nadharia za kidunia na kufuata ushauri wa saikolojia. Paulo hakuionea haya Injili – tofauti na wengi walio kanisani leo – kwa sababu alijua kwamba ni “uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16). Neno la Kiyunani alilotumia kwa “wokovu” katika mistari hii – sozo – linaweza kufasiriwa ukombozi. Nguvu za Mungu katika Injili zinaweza kumkomboa yeyote kutoka kwa chochote.

Lakini, sehemu kubwa ya kanisa siku hizi aidha wanaona aibu au hawajui kuhusu nguvu za kukomboa zilizo katika Injili. Wakijficha chini ya upendo, watenda dhambi waliozoea wanaambiwa “kwa huruma” kwamba Mungu katika neema Yake anawapokea kama walivyo. Ni kweli kwamba Mungu anampenda kila mtu kama alivyo, lakini atawakubali tu kama watamwamini Mwana Wake na kugeuka na kuacha dhambi. Wakifanya hivyo, hatawaacha kama walivyo, bali atawaweka huru. Mimi binafsi nimeona mashoga, walevi, walevi wa dawa za kulevya, wazinzi na waasherati wengi tu wakiwekwa huru kutokana na dhambi zao dakika ile walipotubu na kumwita Yesu. Je, Mungu hana nguvu kiasi hicho? Kulingana na 1Wakorintho 6:9-11, anazo nguvu kiasi hicho na zaidi!

Kusema Ukweli Katika Upendo

Kama kweli tulikuwa tunawapenda watu waliofungwa na dhambi, tungewaambia ukweli. Je, tunafikiri kwamba sisi tuna upendo kuliko Mungu, tunapowashauri watu kwa bidii sana kwamba wajitahidi tu kuchukuliana na hali huku wanaendelea kutenda dhambi ambazo Mungu anataka kuwakomboa nazo? Je, Yesu alikuwa mkali sana alipomwambia yule mwanamke aliyeshikwa katika uzinzi, “Enenda zako, na usitende dhambi tena” (Yohana 8:11)? Je, ilitakiwa awe na huruma kidogo na kusema, “Ninakukubali kama ulivyo. Inaonekana wewe umeshikwa sana na ngono, na bila shaka inatokana na jinsi ulivyolelewa. Matendo yako yanaonyesha kwamba unatamani upendo ambao baba yako hakukupa. Kwa hiyo, usijisikie hatia. Hatia inaweza kuharibu haiba zetu sana. Ninakushauri kwamba uende na ujiunge na kundi la watu wanaotoka katika tabia kama hiyo yako. Baada ya muda, ninatumaini kwamba utaweza kushinda tamaa yako kwa msaada wa nguvu kuu zaidi”?

Ujumbe wa Yesu kwetu sisi sote baada ya kukutana Naye ni huu: “Enenda zako, na usitende dhambi tena.” Kwa nguvu za Roho Mtakatifu katika kuzaliwa upya halisi, nguvu za dhambi huvunjwa na kufanya iwezekane kwetu kutii. Wale ambao wamezaliwa upya kweli ni viumbe vipya ndani ya Kristo (ona 2Wakor. 5:17) ambao wanaweza kusema kwa uhakika kabisa, “Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu” (Wagalatia 2:20). Mungu anatenda kazi ndani yao, “kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema” (Wafilipi 2:13), Naye anaahidi kwamba ataikamilisha ile kazi njema aliyoianza ndani yao (ona Wafilipi 1:6).

Kama nilivyokwisha sema kabla, kama Mungu alichotaka ni kutusamehe dhambi tu, asingemweka Roho Wake Mtakatifu ndani yetu. Ni dhahiri kwamba kwa sehemu, kusudi Lake la kutupa sisi Roho Mtakatifu ilikuwa kutufanya watakatifu. Neema ya Mungu inafanya zaidi ya kutusamehe – inatukomboa na kutubadilisha.

Wazo la nne ambalo wanaopinga kushika sheria hawalielewi ni:

Uhusiano Wa Mkristo Na Sheria Ya Mungu

Msemo unaopendwa sana na hawa wanaopinga kushika sheria ni huu: “Ninafurahi sana kwamba siko chini ya Torati bali neema.” Ingawa huo ni msemo wa Kibiblia, hao wanautoa katika mantiki yake. Wanautumia kumaanisha hivi: “Ninafurahi sana kwamba sina haja ya kujali ninapotenda dhambi fulani.” Au: “Ninafurahi sana kwamba si lazima kila mara kuwa na wasiwasi kwamba Mungu anakubaliana na hiki au hakubali, kama ilivyokuwa chini ya Torati.” Tafsiri za aina hiyo zinaonyesha makosa makubwa katika kufasiri msemo muhimu sana wa Biblia.

Kweli Agano Jipya linatuambia kwamba wale walio ndani ya Kristo hawako tena “chini ya Torati bali neema” (Warumi 6:14). Lakini, Maandiko yanaweka wazi kabisa kwamba, pamoja na maana ya maneno hayo, haimaanishi kwamba wale walioko chini ya neema wana kibali cha kutenda dhambi. Kwa kupotosha mistari kadhaa, hao wasioamini kushika sheria wanalazimisha maana nyingine kabisa kwenye msemo wa Biblia, inayopinga kabisa mtazamo wa Maandiko. Mfano ni maneno ya Paulo katika Warumi 3:31. Anasema hivi:

Basi je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.

NI wazi kwamba baadhi ya vitu anavyoandika Paulo katika Warumi ni utetezi dhidi ya hoja ya Kiyahudi kwamba Injili yake ya neema ingewaongoza watu kutenda dhambi. Ni kama tunaweza kuwasikia wapinzani wa Paulo wakimpigia kelele na kusema: “Kama watu wanaokolewa kwa imani na si kwa kutii Torati kama unavyosema, basi unaifanya Torati ya Mungu kuwa batili!”

Paulo anajibu na kusema, “Si hivyo. Ninyi ambao mmekuwa mkijaribu kuokoka kwa kuishika Torati hamjawahi kukaribia hata kidogo kuitii kikamilifu. Lakini wale wenye imani ndani ya Yesu wamezaliwa mara ya pili. Sheria ya Mungu imeandikwa ndani ya mioyo yao, nguvu ya dhambi imevunjwa maishani mwao, nao ndani wana Roho wa Mungu. Kutokana na vitu hivyo pamoja na vingine, wanaanza kuishika Torati kama ilivyoandikwa na maana yake halisi kiadili. Sasa, tunabatilisha Torati kwa njia ya imani? Kamwe isiwe hivyo! Kinyume chake ni kwamba, tunaithibitisha hiyo Torati.”

Paulo Alikuwa Na Maana Gani?

Baadaye katika Warumi Paulo anatumia usemi ule tunaotazama, kwamba “hatuko chini ya sheria bali neema.” Lakini hebu soma mantiki ya maneno yake, kama ifuatavyo:

Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha! Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki? (Warumi 6:15-16. Maneno mepesi ni kutilia mkazo)

Japo hatuko chini ya Torati, hii haimaanishi kwamba Mungu ametupa uhuru wa kutenda dhambi. Paulo alionyesha kutowezekana kwa wazo kama hilo kwa kutaja kitu ambacho kila mwamini wa kweli hufanya wakati anapokata shauri: anajitoa mwenyewe kwa Mungu kuwa mtumwa Wake wa kumtii, na matokeo ni haki. Chaguo lingine la pekee linalopatikana kwa mwanadamu ni kujitoa kama watumwa kwa dhambi, kitu ambacho kila mtu alifanya kabla ya kumwamini Yesu, na matokeo ni kifo cha kiroho na cha milele.

Tatizo ni kwamba wengi wanaokiri kuwa Wakristo hawajawahi kujitoa wenyewe kwa Mungu kama watumwa watiifu. Wamesikia Injili inayowaahidi mbingu bila ya kutubu. Kumfanya Yesu Kristo kuwa Bwana ni kitu kinachohesabiwa kuwa cha hiari kwenye njia hakika ya kwenda mbinguni. Wanafikiri hakika ni hatua ya hiari, la sivyo wokovu usingekuwa wa neema. Tena, si Biblia inasema kwamba hatuko chini ya Torati, bali chini ya neema?

Lakini, kama Paulo alivyosema wazi wazi, hakuna kitu kama hicho. Kumfanya Yesu kuwa Bwana ni hatua ya kwanza tu kuelekea mbinguni. Kujitoa mwenyewe kama mtumwa Wake mtiifu ndiyo itikio pekee la kweli la imani yenye kuokoa na ndiyo njia ya pekee ya kupokea zawadi ya haki ya Mungu.

Sheria Ya Kristo

Kwa kuwa hatuko chini ya Torati ya Mungu aliyoitoa kupitia kwa Musa hakumaanishi kwamba hatuko chini ya sheria za Mungu zilizotolewa kwa Kristo. Paulo alitaja waziwazi katika andiko tulilosoma la Warumi kwamba hatupaswi kutenda dhambi. Bila shaka ni kwamba kama tunaweza kuwa na hatia ya dhambi basi kuna kiwango cha kujipimia. Sheria lazima iwepo ili dhambi iwepo. “Maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa” (Warumi 4:15).

Chini ya agano jipya kuna sheria inayotufunga. Si njia ya kujipatia wokovu kwa sababu wokovu wetu unatokana na neema ya Mungu. Lakini, ni sheria inayotakiwa kufuatwa na kuitii, la sivyo isingetolewa. Sheria hiyo inaitwa na Maandiko, “Sheria ya Kristo.” Sheria ya Kristo ni kila kitu alichoamuru Kristo, kama ambavyo “Torati ya Musa” ni kila kitu alichoagiza Musa. Kumbuka kwamba Yesu alitwambia tukawafanye watu kuwa wanafunzi, tukiwafundisha kuyashika yote aliyotuamuru (Mathayo 28:18-20).

Hebu tutazame mistari mingine, mahali ambapo Paulo anasema waziwazi kwamba yeye hayuko chini ya Torati ya Musa, lakini yuko chini ya sheria ya Kristo. Anasema hivi:

Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nilijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria,) ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo,) ili niwapate hao wasio na sheria (1Wakor. 9:19-21. Maneno mepesi ili kutilia mkazo)

Sasa, hiyo sheria ya Kristo inalinganishwaje na Torati ya Musa? Kujifunza amri za Kristo hufunua kwamba, katika maeneo mengine, aliweka pembeni sheria zingine za agano la zamani. Katika maeneo mengine, alianzisha sheria mpya ambazo hazikuwepo chini ya agano la zamani. Na katika maeneo mengine, alifafanua maana na kuunga mkono sheria fulani za agano la zamani. Hebu tutazame mifano kuhusu hayo yote matatu.

Mfano wa eneo la kwanza ni Yesu kuondoa vizuizi vyote kuhusu vyakula, kama ilivyo katika agano la zamani. Tunasoma katika Injili ya Marko kwamba alitangaza vyakula vyote “kuwa ni safi” (Marko 7:19). Chini ya agano la sasa tunaweza kula nguruwe bila ya kuwa na hatia (ona pia Matendo 10:10-15; 1Timotheo 4:3-5).

Mfano wa eneo la pili ni amri ya Kristo kuanzisha ubatizo wa maji, kitu ambacho hakikutakiwa kwa yeyote katika watu wa Mungu wa agano la zamani (ona Mathayo 28:19). Pia, kuna wakati Yesu alitupa sisi kitu alichoita amri mpya, kwamba tupendane sisi kwa sisi kama Yeye alivyotupenda (ona Yohana 13:34).

Mfano wa eneo la tatu ni jinsi Yesu alivyounga mkono amri ya saba, inayozuia kuzini. Alipohubiri mahubiri Yake ya Mlimani, alifafanua maana ya kukatazwa huko, akifunua kusudi la Mungu la tangu mwanzo. Inaonekana kwamba wengi waliokuwa wanamsikiliza hapo walijihesabu kuwa watakatifu kwa habari ya uzinzi, ingawa mara kwa mara wote walikuwa wanatamani katika mioyo yao. Lakini, kama Yesu alivyoonyesha, kama ni makosa kuwa na mahusiano ya kimapenzi kimwili na mke wa jirani yako, ni makosa pia kumvua nguo katika mawazo yako.

Sisi sote ambao tuko katika Kristo kweli tuna wajibu – na msukumo kutoka ndani – na uwezo wa kuitii sheria ya Kristo. Tuko chini ya sheria Yake. Amri za Yesu zimehusisha matakwa yote ya kiadili yaliyokuwepo katika Torati ya agano la zamani.

Mwisho: Wazo lingine la Maandiko ambalo wanaopinga kushika sheria hulipuuza ni:

Asili Ya Kweli Na Umuhimu Wa Toba

Wengine katika kundi hilo hupuuza kabisa agizo na fundisho la Agano Jipya kwamba toba ni sharti la lazima kwa ajili ya wokovu. Kuna wanaotoa hoja kwamba kuwaambia watu ambao hawajaokoka kwamba lazima watubu ni kuwaambia kwamba matendo yao au kitu wanachofanya huchangia kwenye wokvou wao, ambayo ni sawa na lile fundisho la kushika Torati. Lakini, hayo si kweli. Toba ni tendo ndiyo, lakini kama tendo lingine lolote, haichangii chochote kwamba ni malipo ya wokovu. Kama kazi nyingine yoyote maishani mwa mwamini wa kweli, toba ni tendo linalotokana na imani, na ndiyo tendo la kwanza la imani iliyo hai. Toba ndiyo itikio la pekee kwa Injili.

Wengine ambao wanajua Maandiko kidogo wanatambua kwamba kudai toba iondolewe katika mahubiri ya Injili ni sawa na kusema kwamba mahubiri ya Yohana Mbatizaji, Yesu, Petro, na Paulo yalikuwa na hitilafu. Basi, wao wanatumia mbinu ya kutafsiri toba upya. Kwa tafsiri yao mpya, toba si zaidi ya kubadili mawazo juu ya Yesu, na ni kitu ambacho – ajabu sana! – si lazima kibadilishe mwenendo wa mtu. Sawa. Hebu tutafute maana ya toba katika Biblia. Je, wahubiri wa Agano Jipya walimaanisha nini walipowaita watu kutubu?

Paulo aliamini kwamba toba ya kweli, si tu kwamba ilihitaji mabadiliko ya nia, bali pia mabadiliko ya mwenendo. Akieleza kuhusu maono yake ya kwanza na jinsi alivyofanya huduma katika miaka iliyofuata, Paulo anashuhudia mbele ya Mfalme Agripa na kusema hivi:

“Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni, bali kwanza naliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao” (Matendo 26:19-20. Maneno mepesi ni kutilia mkazo.)

Yohana Mbatizaji naye aliamini kwamba toba ilikuwa zaidi ya badiliko la mawazo kuhusu kweli fulani za mafundisho. Yeye aliwaambia wasikilizaji wake watubu. Walipomwliza wafanye nini, aliorodhesha mabadiliko fulani ya mwenendo (ona Luka 3:3, 10-14). Aliwalaumu Mafarisayo na Masadukayo kwa kujifanya wametubu, na akawaonya juu ya ukali wa moto wa jehanamu kama wasingetubu kweli. Alisema hivi:

“Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba… Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni” (Mathayo 3:7-10. Maneno mapesi kutilia mkazo.)

Bwana Yesu naye alihubiri ujumbe huo huo wa toba, kama Yohana (ona Mathayo 3:2; 4:17). Yeye wakati fulani alisema kwamba Ninawi ilitubu baada ya mahubiri ya Yona (ona Luka 11:32). Yeyote ambaye amewahi kusoma kitabu cha Yona anajua kwamba watu wa Ninawi walifanya zaidi ya kubadili mawazo yao. Walibadili matendo yao, wakaacha dhambi.

Je, toba Kibiblia ni kitu gani? Ni badiliko la mwenendo kwa hiari ya mtu, kama itikio la imani ya kweli izaliwayo moyoni mwa mtu.

Ulazima Wa Toba

Je, toba ni muhimu kiasi gani? Je, mtu anaweza kuokoka bila kutubu? Kulingana na Maandiko jibu ni hapana.

Yohana Mbatizaji alitangaza Injili (na Luka anaiita “Injili”) ambayo ujumbe wake mkuu ulikuwa toba (ona Luka 3:1-18). Wale ambao wasingetubu wangekwenda jehanamu (ona Mathayo 3:10-12; Luka 3:17).

Yesu alihubiri toba tangu mwanzo wa huduma Yake (ona Mathayo 4:17). Aliwaonya watu kwamba kama wasingetubu, wangeangamia (ona Luka 13:3, 5).

Wakati Yesu alipowatuma wanafunzi Wake kumi na mbili kwenda kuhubiri katika miji mbalimbali, “walikwenda wakihubiri kwamba watu watubu” (Marko 6:12 — Maneno mepesi kutilia mkazo).

Baada ya ufufuo Wake, Yesu aliwaambia wale Thenashara wapeleke ujumbe wa toba kwa dunia nzima, kwa sababu ndiyo ufunguo wenye kufungua mlango wa msamaha.

Akawaambia, ‘Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu’ (Luka 24:46-47. Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mitume walitii agizo la Yesu. Wakati mtume Petro alipohubiri siku ya Pentekoste, wasikilizaji wake walioguswa na neno, baada ya kutambua ukweli juu ya Yule waliyekuwa wamemsulubisha siku za karibuni tu, walimwuliza Petro wafanye nini. Jibu lake likawa kwamba kwanza, lazima watubu (Matendo 2:38).

Mahubiri ya Petro ya pili katika ukumbi wa Sulemani yalikuwa hivyo hivyo. Dhambi zisingefutwa pasipo toba.

Tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe …” (Matendo 3:19a – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Kama ambavyo tumekwisha jifunza tayari kutokana na ushuhuda wa Paulo mbele ya Mfalme Agripa, Injili yake kila wakati ilikuwa na ujumbe wa toba. Huko Athene, Paulo aliwaonya wasikilizaji wake kwamba kila mtu lazima asimame hukumuni mbele ya Kristo, na wale ambao hawajatubu hawatakuwa tayari kwa ajili ya siku hiyo kuu.

“Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu” (Matendo 17:30-31 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Katika mahubiri yake ya kuagana na wazee wa kanisa la Efeso, Paulo alitaja toba pamoja na imani kuwa vitu muhimu kwa ajili ya wokovu.

“Ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia… Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo” (Matendo 20:20a, 21 – Maneno mepesi kutilia mkazo).

Mwandishi wa kitabu cha Waebrania alisema kwamba “kutubia matendo mafu” ni sehemu ya mafundisho ya msingi ya Kristo (ona Waebrania 6:1).

Tunatumaini kwamba orodha hii ya Maandiko yenye kuthibitisha kweli hii yanatosha kumfanya mtu yeyote kuamini kwamba uhusiano na Mungu huanza kwa toba. Hakuna msamaha wa dhambi bila toba. Kama hukutubu “ulipompokea Yesu” mara ya kwanza, na hukufanya “matendo yastahiliyo toba”, basi hukuokoka. Kama hujatubu tangu hapo, bado hujaokoka.

Je, Mungu Anatazamia Tutubu Nini?

Wakati mtu anapoiamini Injili mara ya kwanza, anatakiwa atubu dhambi zote anazojua. Haiwezekani atubu kila kitu anachofanya ambacho ni kibaya kwa sababu hajui kila kitu ambacho ni kibaya anachofanya. Mungu anatuhukumu kwa yale tunayojua tu (ona Luka 23:34; 1Timo. 1:13). Huyo mwamini mpya anapozidi kukua katika ufahamu wake wa mapenzi ya Mungu (ona Waefeso 5:10), itakuwepo toba ya kuendelea. Huo ndiyo mpango wa utakaso.

Katika nyakati zingine itabidi kufanya marejesho au malipizi na kuomba msamaha kwa makosa yaliyofanywa. Bila shaka mtu aliyeiba shilingi elfu mbili jana, akamwamini Yesu leo na bado akakaa na hiyo fedha ya wizi, ni mwizi bado. Anacho kitu ambacho ni cha mwingine. Anawezaje kudai kwamba yeye ni mfuasi wa Kristo? Dhamiri ya mwamini mpya wa kweli haitampa kumpumzika mpaka atakaporudisha kile alichoiba.

Ila, yapo makosa ambayo hayawezekani kurekebishwa. Lakini kila kilichoibiwa kinachoweza kurudishwa kirudishwe. Kila kosa linaloweza kurekebishwa lirekebishwe. Labda itabidi kuandika barua au kupiga simu, kuomba msamaha kwa waliokosewa.

Kama kila anayejiita Mkristo duniani angetubu, kungetokea mapinduzi makubwa sana.

Kutawaliwa na Torati na kutokushika sheria – maneno yenye kueleza mafundisho hatari. Je, ni lipi katika hayo ambalo umelisikia sana midomoni mwa Wakristo? Je, ni wangapi ambao hawajawahi kusikia juu ya fundisho la kutoshika sheria? Ingawa Agano Jipya linaonya kuhusu kutokushika sheria mara nyingi kuliko linavyo-onya juu ya kutawaliwa na Torati, bado fundisho hilo linapata nguvu katika makanisa mengi ya KiProtestanti siku hizi.

Wenye kuamini fundisho hilo mara nyingi huwasema Wakristo halisi kwamba ni watu wanaopenda kutawaliwa na Torati. Lakini, hao hawajali kwa sababu – kinyume cha wale wanaofundisha kutoshika sheria – wao wanatazamia mateso, wakijua kwamba “na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2Timo. 3:12 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Wanatafuta sifa kutoka kwa Mungu badala ya watu, wakiitazamia siku ile ambapo watamsikia Bwana wao akisema, “Vema mtumwa mwema na mwaminifu … ingia katika furaha ya bwana wako” (Mathayo 25:21 – Maneno mepesi kutilia mkazo). Ni wale tu ambao wamekuwa wema na waaminifu kwa Bwana wao ndiyo watakaoingia katika furaha Yake.

Mahubiri Makuu Ya Yesu Kuhusu Wokovu, 1

SURA YA SITA

Miaka elfu mbili iliyopita, Mwana wa Mungu akiwa anaishi duniani katika mwili wa mwanadamu alizungumza na kundi la watu waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza pembeni ya kilima karibu na Bahari ya Galilaya. Siku hizi maneno Yake hayo tunayaita “Mahubiri ya Mlimani”.

Yesu alikuwa bingwa wa mawasiliano kuliko wote waliowahi kuwepo, Naye alikuwa anawafundisha watu ambao tunaweza kuwahesabu kuwa wenyeji ambao hawakuwa na elimu. Kwa hiyo, mafundisho Yake yalikuwa rahisi tu kuelewa. Alitumia vitu vya kila siku ili kufafanua hoja Zake. Lakini siku hizi kuna wengi wanaofikiri kwamba unahitaji mtu mwenye digrii ya Udaktari wa Falsafa (PhD) ili kuweza kutafsiri yale aliyosema Yesu. Na bahati mbaya kabisa ni kwamba, baadhi ya hao watafsiri wanasema kwamba Yesu hakumaanisha alichosema. Basi, wameunda nadharia nyingi za ajabu ili kujaribu kueleza kile ambacho Yesu alisema kweli, na nadharia hizo zisingeweza kueleweka na wale watu wa kawaida ambao Yesu alisema nao hata kwa miaka elfu nzima, wala wasingeweza kuelewa nadharia hizo kama zingefafanuliwa. Kwa mfano: Kuna “wataalamu wa Biblia” wa kisasa wanaotaka tuamini kwamba maneno ya Yesu hayakuwa yanawahusu wasikilizaji Wake wala Wakristo wa siku hizi, bali yatafanya kazi wakati tutakapokuwa tunaishi katika ufalme Wake wa milele! Nadharia ya ajabu hiyo, ukizingatia ukweli kwamba wakati Yesu alipokuwa anazungumza na wasikilizaji Wake alitumia neno ninyi (sio wao) zaidi ya mara mia moja katika mahubiri hayo mafupi. Hawa “wasomi wa Biblia” wanamfanya Yesu kuwa mwongo.

Naomba pia nionyeshe kwamba mahubiri ya Yesu yalikuwa yamelengwa kwa watu wengi waliokuwa wamekusanyika ili kumsikiliza, si kwa wanafunzi Wake tu (ona Mathayo 7:28). Na yalikuwa yanawahusu wanadamu wote tangu wakati ule, ikiwa tutasoma mahubiri hayo kwa udhati wa moyo.

Kusudi la sura hii na ijayo ni kujifunza Mahubiri ya Mlimani ya Yesu. Tutakapofanya hivyo, tutagundua kwamba yalikuwa mahubiri kuhusu wokovu, utakatifu na mahusiano kati ya hivyo viwili. Ni mahubiri yenye kutoa maonyo mara kadhaa kuhusu hatari ya kutoshika sheria. Akiwa anawajali sana wale watu maskini lakini wenye njaa ya kiroho ambao walikusanyika kumsikiliza, Yesu alitaka waelewe kilicho muhimu zaidi – jinsi ambavyo wangeweza kurithi ufalme wa mbinguni. Ni muhimu kwamba hata sisi tujali kile alichosema. Huyu ndiye aliyeandikiwa na Musa, hivi: “Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake” (Matendo 3:22-23). Acha tuanzie mwanzo.

Wenye Heri

Katika sehemu ya kwanza ya mahubiri ya Yesu – sehemu ya “heri” – aliahidi baraka maalum kwa watu wenye kuwa na tabia au hali fulani. Zipo tabia mbalimbali zinazotajwa na baraka nyingi kuahidiwa. Wasomao kwa haraka haraka mara nyingi husoma sehemu hii kama watu wanavyotazama utabiri wa nyota zao, wakifikiri kwamba kila mtu anapaswa kujikuta kwenye moja tu. Tunaposoma kwa makini zadi, tunatambua kwamba Yesu hakuwa anaorodhesha aina tofauti za watu watakaopata baraka mbalimbali, bali alikuwa anaorodhesha mtu aina moja atakayepokea baraka moja ya jumla: kuurithi ufalme wa Mungu. Hakuna njia nyingine ya kufafanua hicho vizuri.

Tuone basi mistari kumi na mbili ya kwanza ya Mahubiri ya Mlimani.

“Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia. Akafumbua kinywa chake akawafundisha akisema,

‘Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao. ‘Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika. ‘Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. ‘Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa. ‘Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema. ‘Heri wenye moyo safi; maana hao watamwona Mungu. ‘Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. ‘Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; maana ufalme wa mbinguni ni wao. ‘Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu’.” (Mathayo 5:1-12).

Baraka Zenyewe Na Hali-Tabia

Kwanza, hebu fikiri juu ya baraka zote zilizoahidiwa. Waliobarikiwa (au wenye heri) (1) wataurithi ufalme wa mbinguni, (2) watafarijiwa, (3) watairithi nchi, (4) watatoshelezwa katika haki, (5) watapata rehema, (6) watamwona Mungu, (7) wataitwa wana wa Mungu, (8) wataurithi ufalme wa mbinguni (ni marudio ya namba 1,) mahali ambapo watapewa thawabu.

Sasa basi: Yesu anataka sisi tufikiri kwamba ni wale walio maskini wa roho tu na wale ambao wameteswa kwa ajili ya haki ndiyo watakaorithi ufalme wa Mungu? Je, ni wale walio safi tu moyoni ndiyo watakaomwona Mungu na ni wapatanishi tu ndiyo watakaoitwa wana wa Mungu lakini hawatarithi ufalme wa Mungu? Je, wapatanishi hawatapokea rehema, na wenye rehema hawataitwa wana wa Mungu? Bila shaka sivyo Yesu anavyotaka tufikiri.

Sasa hebu fikiri zile halitabia tofauti ambazo Yesu anazitaja: (1) maskini wa roho, (2) mwenye huzuni, (3) mpole, (4) mwenye njaa na kiu ya haki, (5) mwenye rehema, (6) mwenye moyo safi, (7) mpatanishi, na (8) mwenye kuudhiwa au kuteswa.

Je, Yesu anataka tufikiri kwamba mtu anaweza kuwa msafi wa moyo na asiwe na rehema? Je, mtu anaweza kuteswa kwa ajili ya haki na asiwe mwenye njaa na kiu ya haki? Tunasema tena, si hivyo.

Basi, ni salama kabisa kufikiri kwamba hizo baraka nyingi zinazoahidiwa hao ni vipengele vya baraka moja kubwa – kuurithi ufalme wa Mungu. Na halitabia nyingi za hao waliobarikiwa zinapatikana kwa wote walio heri.

Ni dhahiri kwamba mahubiri haya yanaeleza halitabia za wafuasi wa kweli wa Yesu, na kwa kuziorodhesha alikuwa anawatia moyo wafuasi Wake kwa ahadi za baraka nyingi za wokovu. Waliobarikiwa ni watu walio-okoka, kwa hiyo, Yesu alikuwa anaeleza halitabia za watu wanaokwenda mbinguni. Watu wasioingia katika maelezo hayo hawajabarikiwa na hawataurithi ufalme wa mbinguni. Basi ni sawa kwetu kujiuliza kama tunaingia katika maelezo ya Yesu. Haya ni mahubiri kuhusu wokovu, utakatifu na uhusiano uliopo kati ya hayo mawili.

Hali-Tabia Za Waliobarikiwa

Zile sifa nane ambazo Yesu anaziorodhesha za watu waliobarikiwa zinaweza kufafanuliwa au kutafsiriwa kwa njia inayoeleweka zaidi. Kwa mfano: Kuna uzuri gani kuwa “maskini wa roho”? Mimi nadhani kwamba Yesu alika anataja sifa ya kwanza ya lazima ambayo mtu lazima awe nayo kama ataokoka – yaani, atambue umaskini wake kiroho. Ni lazima mtu aone hitaji la Mwokozi kwanza kabla hajaokoka.

Hii sifa ya kwanza inaondoa hali ya kujitosheleza na wazo lolote la kustahili wokovu. Yule aliyebarikiwa kweli ni mwenye kutambua kwamba hana chochote cha kumpa Mungu, kwamba haki yake ni kama “matambara machafu.” Anajiona miongoni mwa wale ambao “wametengwa na Kristo, wametengwa na Israeli, wageni kwa maagano na ahadi, wasio na matumaini na bila Mungu duniani” (Waefeso 2:12).

Tena, Yesu hakutaka mtu yeyote afikiri kwamba kwa juhudi zake mwenyewe anaweza kufikia viwango vile ambavyo alikuwa anataka kuvitaja. Hapana. Watu hubarikiwa na Mungu kama watakuwa na sifa hizo zinazotajwa. Vyote vinatoka katika neema ya Mungu. Wenye heri ambao Yesu aliwazungumzia hapa wamebarikiwa, si kwa sababu ya kile kinachowangojea mbinguni tu, bali kwa sababu ya kazi ambayo Mungu ameifanya maishani mwao hapa duniani. Ninapoona sifa za kubarikiwa maishani mwangu zinatakiwa kunikumbusha kile ambacho Mungu amefanya ndani yangu kwa neema Yake, siyo kile ambacho mimi nimefanya.

Kama halitabia ya kwanza imeorodheshwa kwanza kwa sababu ndiyo ya kwanza ya lazima kwa wanaokwenda mbinguni, basi hata ya pili ina maana: “Heri wenye huzuni” (Mathayo 5:4). Je, Yesu hapa alikuwa anazungumzia toba ya kutoka moyoni na kujisikia hatia kwa sababu ya dhambi? Nafikiri hivyo, hasa kwa sababu Maandiko yanasema wazi kwamba huzuni ya kimungu husababisha toba ambayo ni muhimu na lazima kwa ajili ya wokovu (2Wakor. 7:10). Kama sivyo, basi pengine Yesu alikuwa anazungumzia huzuni ambayo Wakristo wote wa kweli wanayo wanapoendelea kukabiliana na dunia iliyo katika hali ya kumwasi Mungu anayewapenda. Paulo anaieleza hiyo kuwa ni “huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni [mwake]” (Warumi 9:2).

Halitabia ya tatu – upole – inaorodheshwa pia katika Maandiko kwamba ni tunda mojawapo la Roho (ona Wagalatia 5:22-23). Upole si sifa inayotokana na mtu. Wale ambao wamepokea neema ya Mungu na Roho Mtakatifu anakaa ndani yao pia wamebarikiwa kuwa wapole. “Wakristo” wakali na wakorofi, jihadharini. Hampo miongoni mwa watakaorithi nchi.

Kuwa Na Njaa Na Kiu Ya Haki

Sifa ya nne – kuwa na njaa na kiu kwa ajili ya haki – hueleza juu ya shauku ya ndani itokayo kwa Mungu ambayo kila mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa nayo. Anatamani kuwa mtakatifu na mwenye kumpendeza kabisa Bwana wake.

Mara nyingi tunaposoma neno haki katika Maandiko tunalitafsiri kuwa ni “haki tunayohesabiwa na Kristo,” lakini hiyo si maana yake kila wakati. Mara nyingi maana yake ni, “hali ya kuishi sawa kulingana na kiwango cha Mungu.” Hiyo ndiyo maana ya Yesu hapa, kwa sababu hakuna sababu ya kuwa na njaa ili kupata haki tuliyokwisha hesabiwa huku ni yetu tayari. Wale ambao wamezaliwa kwa Roho wanatamani kuishi kwa haki, na hilo pia linatusaidia sisi kuelewa kwamba hakuna Mkristo wa kweli aliye mkamilifu. Vinginevyo asingetamani kitu alicho nacho tayari. Lakini, sisi tunaotamani tunajua kwamba tuta”toshelezwa” (Mathayo 5:6), uhakika kwamba Mungu kwa neema Yake ataikamilisha kazi aliyoianza ndani yetu (ona Wafilipi 1:6). Hii ndiyo faraja ya pekee tuliyo nayo katika hali yetu ya kutokamilika sasa, kitu ambacho kinaendelea kutusumbua. Tunaichukua dhambi ambayo bado imo ndani yetu. Ila – kwa upande mwingine – mahubiri hayo na heri hizo zenyewe zinathibitisha kwamba kila mtu anayekwenda mbinguni, aliyebarikiwa na Mungu, anao utakatifu kiasi fulani sasa hivi.

Sifa ya tano – rehema – pia ni kitu ambacho kila mtu aliyezaliwa upya anakuwa nacho kwa sababu ya kuwa na Mungu mwenye rehema akikaa ndani yake. Wale wasiokuwa na rehema hawajabarikiwa na Mungu, na wanadhihirisha kwamba si washiriki wa neema Yake. Mtume Yakobo anakubaliana na hayo anaposema: “Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma” (Yakobo 2:13). Ukisimama mbele za Mungu na upokee hukumu isiyo na huruma, utakwenda mbinguni au jehanamu?

Sifa ya sita ya mwenye kwenda mbinguni ni usafi wa moyo. Tofauti na wengi wanaojiita Wakristo, wafuasi wa kweli wa Kristo si watakatifu kwa nje tu. Kwa neema ya Mungu, mioyo yao imefanywa kuwa safi. Kweli wanampenda Mungu kutoka mioyoni mwao, na inagusa makusudi yao na tafakari zao. Yesu aliahidi kwamba hao watamwona Mungu.

Tena narudia kuuliza: Je, tuamini kwamba kuna waamini wa kweli Wakristo ambao si wasafi moyoni ambao kwa sababu hiyo hawatamwona Mungu? Je, Mungu atawaambia, “Ingia mbinguni, lakini hutaniona kamwe”? Hapana. Bila shaka kila anayekwenda mbinguni kweli ana moyo safi.

Waliobarikiwa Kuwa Wapatanishi

Wapatanishi wanafuata katika orodha. Wao wataitwa wana wa Mungu. Hapa tena, Yesu bila shaka alikuwa anasema juu ya kila mfuasi wa kweli wa Kristo, kwa sababu kila amwaminiye Kristo ni mwana wa Mungu (ona Wagalatia 3:26).

Wale waliozaliwa kwa Roho ni wapatanishi kwa njia kama tatu hivi:

Kwanza: Wamejipatanisha na Mungu, ambaye hapo kwanza alikuwa adui yao.

Pili: Wanaishi kwa amani, kadiri iwezekanavyo na pasipo kumkosea Mungu, na watu wengine pia. Wao si wagomvi au watu wa fujo. Paulo aliandika kwamba watu wa aina hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu (ona Wagalatia 5:19-21). Waamini wa kweli watakwenda maili ya ziada kuepuka ugomvi na kutunza amani katika mahusiano yao. Hawadai kuwa na amani na Mungu huku wakiwa na tofauti na ndugu (ona Mathayo 5:23-24; 1Yohana 4:20).

Tatu: Kwa kuwaambia wengine Injili, wafuasi wa kweli wa Kristo pia huwasaidia wengine kuwa na amani na Mungu na wenzao.

Mwisho: Yesu alisema wamebarikiwa wale wanaoudhiwa (au kuteswa) kwa ajili ya haki. Bila shaka alikuwa anazungunza juu ya watu wanaoishi maisha ya haki. Hao ndiyo wanaoteswa na wasioamini. Hao ndiyo watu watakaorithi ufalme wa Mungu.

Je, Yesu alikuwa anazungumza kuhusu mateso aina gani? Kuuawa? Kuteswa kimwili? Hapana. Yeye alisemea kuudhiwa kwa kusemwa vibaya na kutukanwa kwa ajili Yake. Maana yake ni kwamba wakati mtu anapokuwa Mkristo wa kweli, ni kitu kinachojulikana kwa wasioamini, la sivyo wasioamini wasingemsema vibaya. Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo ambao hawana tofauti na wasioamini kiasi cha kwamba hakuna asiyeamini hata mmoja anayesema kinyume chao? Hao si Wakristo wa kweli. Yesu alisema hivi: “Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo” (Luka 6:26). Wakati watu wote wanapokusema vizuri, hiyo ni ishara kwamba wewe ni mwamini bandia. Dunia inawachukia Wakristo wa kweli (ona pia Yohana 15:18-21; Wagalatia 4:29; 2Timo. 3:12; 1Yohana 3:13-14). Je, kuna yeyote anayekuchukia? Haya ni mahubiri kuhusu wokovu, utakatifu na mahusiano ya hayo mawili.

Chumvi Na Nuru

Katika mistari inayofuata, Yesu aliendelea kueleza kuhusu wafuasi Wake wa kweli – waliobarikiwa – akiwalinganisha na chumvi na nuru. Vyote hivyo viwili vina sifa zinazoweza kuonekana. Chumvi ina ladha na nuru huangaza. Kama haina ladha, si chumvi. Kama haiangazi, si nuru.

“Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:13-16).

Siku za Yesu chumvi ilitumiwa kwa sehemu kubwa kwa kuhifadhia nyama. Kama wafuasi watiifu wa Kristo, sisi ndiyo tunaohifadhi dunia hii isiharibike kabisa kabisa na kuoza. Lakini, kama na sisi tutakuwa kama dunia katika mwenendo wetu, kweli hatufai kwa lolote. Yesu aliwaonya wale waliobarikiwa wadumu kuwa na ladha, wakitunza upekee wao. Lazima wabakie tofauti na dunia inayowazunguka, wasije wakapoteza “ladha” na kustahili “kutupwa nje na kukanyagwa na watu”. Hili ni onyo mojawapo kati ya mengi kuhusu kurudi nyuma wanalopewa waamini wa kweli katika Agano Jipya. Kama chumvi ni chumvi kweli, inakuwa na ladha. Vivyo hivyo, wafuasi wa Yesu wanatenda kama wafuasi wa Yesu. La sivyo si wafuasi wa Yesu, hata kama walikuwa hapo kwanza.

Wafuasi wa kweli wa Kristo pia ni nuru ya dunia. Kila mara nuru huangaza. Kama haiangazi, basi si nuru. Katika mfano huu, nuru huwakilisha matendo yetu mema (Mathayo 5:16). Kristo aliwashauri wafuasi Wake kutenda matendo yao mema ili watu wengine wayaone. Kwa njia hiyo, watamtukuza Baba yao wa mbinguni kwa sababu Yeye ndiye chanzo cha kazi au matendo hayo mema.

Ona kwamba Yesu hakusema tutengeneze mwanga, bali tuache nuru tuliyo nayo iangaze mbele ya wengine ili watu waone mwanga wetu. Hakuwa anashauri wale wasiokuwa na matendo wafanye mpango wa kuyapata, bali aliwashauri wale wenye matendo mema wasiyafiche. Wafuasi wa Kristo ni nuru ya ulimwengu. Wamebarikiwa, kwa neema ya Mungu, kuwa mianga gizani.

Umuhimu Wa Kushika Amri Za Mungu

Hapo tunafikia mahali pa kuanza fungu lingine la maneno. Katika fungu hili, Yesu alianza kuzungumza kuhusu Torati na uhusiano wake kwa wafuasi Wake.

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua bali kutimiliza. Kwa maana, amin nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 5:17-20).

Kama Yesu aliwaonya wasikilizaji Wake dhidi ya kufikiri kwamba alikuwa anaibatilisha Torati au hata Manabii, basi tunaweza kufikiri kwamba kuna waliokuwa wakimsikiliza waliodhani hivyo. Tunaweza kukisia kilichosababisha wafikiri hivyo. Pengine ni kule kukemea kwa ukali sana mambo ya Mafarisayo na waandishi.

Vyovyote vile, Yesu alitaka kila mtu ajue wakati ule na sasa kwamba kufikiri hivyo ni makosa. Yeye alikuwa Mungu – aliyevuvia Agano la Kale zima – kwa hiyo hakika asingeondoa kila kitu alichokuwa amesema kwa njia ya Musa na manabii. Kinyume chake, angeitimiza Torati na Manabii.

Je, angetimizaje Torati na Manabii? Wengine wanafikiri kwamba Yesu alikuwa anazungumzia tu kule kutimizwa kwa unabii wa Masiya. Ingawa kweli Yesu alitimiza (na atatimiza bado) kila utabiri wa Kimasiya, Yeye hakumaanisha hivyo. Mantiki inaonyesha kwamba alikuwa anazungumza juu ya yote yaliyoandikwa katika Torati na Manabii, mpaka “yodi na nukta ndogo sana” (ms. 18) ya Torati, na mpaka iliyo “ndogo” kabisa (ms. 19) katika amri (si utabiri wa Masiya tu).

Kuna wanaofikiri Yesu alimaanisha kwamba angeitimiza Torati kwa kutosheleza masharti yake kwa niaba yetu kupitia maisha Yake ya utii na kifo Chake cha kujitoa kama dhabihu. Lakini hilo nalo, kulingana na mantiki, silo alilokuwa akisema. Katika mistari inayofuata, Yesu hasemi chochote juu ya maisha au kifo Chake kwamba ndiyo kipimo cha kutimizwa Torati. Badala yake, katika sentensi inayofuata, anataja kwamba Torati itaendelea kufanya kazi mpaka “mbingu na nchi” zitakapopita” na kila kitu “kitimizwe”. Kisha anataja kwamba jinsi watu wanavyoifikiria na kuiona Torati itaamua nafasi yao mbinguni (ms. 19), na kwamba watu lazima waitii Torati vizuri zaidi kuliko waandishi na Mafarisayo, la sivyo hawataingia mbinguni (ms. 20).

Bila shaka, kitu alichokuwa anasema Yesu hapa ni watu kuishika Torati na kufanya kile kilichosemwa na Manabii. Angeitimiza Torati kwa maana kwamba Yeye angefunua kusudi la kweli la Mungu katika Torati Yake, akiifafanua kikamilifu, akikamilisha kile kilichokuwa kimekosekana katika ufahamu wa watu juu yake. Neno la Kiyunani linalotafsiriwa kutimiza katika mstari wa 17 ndilo linalotafsiriwa katika Agano Jipya sehemu nyingine na maana yake ni kukamilisha, kumaliza, kujaza na kutekeleza kabisa. Hayo ndiyo Yesu angefanya, akianzia sentensi kama nne hivi baadaye!

Hapana – Yesu hakuja kuondoa Torati bali kuitimiza, yaani, “kuijazia ikamilike.” Kwa habari ya zile amri zipatikanazo katika Torati na Manabii, Yesu aliweka wazi kabisa alichosema. Alitazamia kila mtu atii. Yote yaliyokuwemo yalikuwa muhimu kabisa. Ni hivi: Jinsi mtu anavyozistahi amri itaamua jinsi na yeye atakavyostahiwa mbinguni: “Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni” (5:19).

Tunafika kwenye mstari wa 20: “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”

Ona kwamba hilo si wazo jipya: ni la kumalizia ambalo lina uhusiano na ile mistari mingine yote kwa neno lile dogo – maana. Je, kushika amri ni muhimu kiasi gani? Ni lazima mtu azishike vizuri zaidi kuliko waandishi na Mafarisayo ili aweze kuingia katika ufalme wa mbinguni! Hapo tena tunaona kwamba haya ni mahubiri juu ya wokovu na utakatifu, na jinsi vinavyohusiana.

Je, Yesu Alikuwa Anazungumzia Haki Ya Namna Gani?

Yesu aliposema kwamba haki yetu lazima izidi ya waandishi na Mafarisayo, hakuwa anasema juu ya haki ile ya kisheria ambayo tungehesabiwa kama zawadi itolewayo bure? Hapana, kwa sababu mbili.

Kwanza: Mantiki haikubaliani na tafsiri hiyo. Kabla na baada ya kusema hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuzishika amri, yaani, kuishi kwa haki. Tafsiri rahisi kabisa ya maneno Yake ni kwamba lazima tuishi kwa haki zaidi kuliko waandishi na Mafarisayo.

Pili: Ikiwa Yesu alikuwa anazunguma kuhusu haki tunayohesabiwa kisheria na kuipokea kama zawadi itolewayo bure kwa kumwamini, mbona hakutoa hata kidokezo? Mbona akasema kitu ambacho kingeweza kueleweka vibaya kirahisi tu na wale wakulima waliokuwa hawana elimu waliomsikiliza ambao wasingeweza kukisia kwamba alikuwa anazungumza nao juu ya haki ambayo tunahesabiwa na Mungu?

Tatizo letu ni kwamba hatutaki kukubali maana iliyo dhahiri ya mstari wenyewe, kwa sababu kwetu inasikika kama ni kutawaliwa na sheria. Lakini tatizo halisi ni kwamba hatuelewi muunganiko ulioko kati ya haki ya kuhesabiwa na haki halisi ya kivitendo. Mtume Yohana yeye alielewa, maana aliandika hivi: “Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki” (1Yohana 3:7). Wala hatuelewi mlingano kati ya kuzaliwa upya na haki ya matendo kama Yohana alivyoelewa. Anasema hivi: “Kila atendaye haki amezaliwa na yeye” (1Yohana 2:29).

Yesu angeweza kuongezea haya yafuatayo katika tamko Lake la Mathayo 5:20 – “Na kama mkitubu na kuzaliwa kweli mara ya pili na kupokea zawadi yangu itolewayo bure ya haki ipatikanayo kwa imani, haki yenu ya matendo itazidi ile ya waandishi na Mafarisayo kwa uwezo wa Roho wangu anayekaa ndani yenu.”

Haki Ya Waandishi Na Mafarisayo

Swali lingine ambalo ni muhimu, linalotokana na tamko la Yesu katika 5:20 ni hili: Je, waandishi na Mafarisayo walikuwa na haki kiasi gani (kimatendo)?

Kuna wakati mwingine ambapo Yesu aliwaita “makaburi yaliyopakwa chokaa ambayo kwa nje yanapendeza lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na uchafu wote” (Mathayo 23:27). Yaani, kwa nje walionekana ni wenye haki, lakini kwa ndani walikuwa waovu. Walifanya vizuri sana katika kushika Torati kama ilivyosema, lakini walipuuzia kusudi au maana yake, wakijitetea mara nyingi kwa kupindua kidogo au hata kubadilisha maagizo ya Mungu.

Hilo liliwekwa wazi na Yesu katika sehemu iliyofuata ya Mahubiri ya Mlimani. Alitaja amri kadhaa za Mungu, kisha akaonyesha tofauti kati ya kutimiza sheria na kutimiza kusudi au maana yake. Yesu alionyesha jinsi ambavyo waandishi na Mafarisayo walitafsiri na kutii kwa nje kila amri, kisha akafunua kusudi la kweli la Mungu kwa kila amri. Alianza kila mfano: “Mmesikia,” kisha akaeleza maoni ya Mungu kuhusu kile walichokuwa wamesikia. Anatumia amri ya sita kama mfano Wake wa kwanza.

“Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, ‘Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.’ Bali mimi nawaambieni, ‘Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanamu ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshtaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshtaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho’.” (Mathayo 5:21-26).

Waandishi na Mafarisayo walijivuna sana kwamba hawakuwa wauaji. Yaani, hawakuwahi kumwua mtu yeyote. Kwa mawazo yao, walikuwa wanaishika kabisa amri ya sita. Lakini, wangependa kumwua mtu kama isingekatazwa, kama inavyodhihirishwa kwa ukweli kwamba walifanya kila kitu kingine isipokuwa kuwaua waliowachukia. Yesu aliorodhesha mifano michache ya tabia yao ya kuua. Kutoka vinywani mwao walisema maneno mabaya ya matusi kwa wale waliokuwa wamewakasirisha. Kwa ndani walikuwa na uchungu, hawakusamehe, na wasiotaka mapatano, waliojitia katika kesi, ama kushtaki wengine au kushtakiwa kwa matendo yao ya kufisha na ya kichoyo. Waandishi na Mafarisayo walikuwa wauaji moyoni ambao walijizuia tu wasifanye kitendo chenyewe.

Lakini, yule ambaye ni mwenye haki wa kweli ni tofauti. Kiwango chake ni cha juu zaidi. Anajua kwamba Mungu anamtazamia ampende ndugu yake, na kama mahusiano yake na ndugu yake si mazuri, mahusiano yake na Mungu si sawa. Hatafanya matendo ya dini kinafiki, akijifanya kumpenda Mungu na huku anamchukia ndugu (ona Mathayo 5:23-24). Kama ambavyo Mtume Yohana angeandika baadaye, “Yeye asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hajamwona” (1Yohana 4:20).

Waandishi na Mafarisayo walifikiri kwamba wao walipata hatia kwa tendo la kuua tu. Lakini Yesu alionya kwamba hali ya moyo ya muuaji humfanya mtu kustahili jehanamu. Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo ambao hawana tofauti na wale waandishi na Mafarisayo? Wamejaa chuki badala ya upendo. Wakristo wa kweli wamebarikiwa na Mungu mpaka kiwango cha Yeye kuweka pendo Lake ndani yao, akiwafanya wenye kupenda (ona Warumi 5:5) watu wote kwa neema Yake.

Mungu Anavyofafanua Uzinzi

Amri ya saba ikawa mfano wa pili wa Yesu kuhusu jinsi waandishi na Mafarisayo walivyoshika sheria huku wakipuuza maana yake.

“Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini;’ lakini mimi nawaambia, ‘Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanamu’.” (Mathayo 5:27-30).

Kwanza: Ona tena kwamba mahubiri haya ni kuhusu wokovu na utakatifu, na jinsi hayo mawili yanavyohusiana. Yesu alionya kuhusu jehanamu, na kinachotakiwa ili mtu asiende huko.

Waandishi na Mafarisayo wasingeweza kuipuuza amri ya saba, kwa hiyo waliitii kwa nje kwa kubaki waaminifu kwa wake zao. Lakini walikuwa wanafanya mapenzi na wanawake wengine katika mawazo yao. Walikuwa wanawavua nguo kimawazo wale wanawake waliowaona sokoni. Moyoni walikuwa wazinzi, na hivyo walikuwa wanaiasi maana ya amri ya saba. Je, ni wangapi wanaojiita Wakristo wanaoweza kusema wao ni tofauti?

Mungu alikusudia watu Wake wawe safi kabisa katika mahusiano ya kimwili. Kama nilivyokwisha sema katika kitabu hiki huko mwanzoni, ni makosa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa jirani yako, lakini pia, ni makosa kuota kwamba unafanya mapenzi naye.

Je, kuna waliojisikia hatia miongoni mwa wasikilizaji wa Yesu? Bila shaka. Wafanyeje? Watubu mara moja, kama Yesu alivyoagiza. Wale waliokuwa na tamaa walitakiwa kuacha kutamani, kwa sababu wale wanaotamani watakwenda jehanamu. Hivyo, walipaswa kulipa gharama yoyote ile ili kumaliza jambo hilo.

Bila shaka si sawa kufikiri kwamba Yesu alimaanisha watu wenye tamaa wang’oe kweli jicho lao au kukata mkono. Mtu mwenye tamaa atakayeng’oa jicho lake atabaki mwenye tamaa aliye chongo! Yesu alikuwa anasisitiza kwa lugha ya mfano umuhimu wa kuitii maana ya amri ya saba. Mustakabali wa mtu milele ulikuwa unategemea hicho.

Je, unajisikia hukumu? Basi, “kata” chochote kinachokufanya ujikwae. Kama ni televisheni ya kulipia, acha kulipia. Kama ni televisheni kawaida, itupilie mbali. Kama ni kitu unachoona ukienda mahali fulani, basi acha kwenda huko. Kama ni gazeti unaloletewa nyumbani, acha kulipokea. Kama uko kwenye mtandao, jiondoe! Hakuna hata kimoja katika hivyo kinachofaa kukupeleka jehanamu milele. Hakuna mtu atakayekuwa jehanamu atakayesema, “Sawa niko jehanamu, lakini nilifurahia sana zile sinema mbaya nilipokuwa duniani. Sijuti, japo nitateseka huku jehanamu milele kwa sababu ya hilo.”

Maoni Ya Mungu Kuhusu Talaka

Mfano unaofuata wa Yesu unafanana kidogo na ule uliopita, ambao pengine ndiyo sababu unafuata mara moja. Labda ni sawa ufikiriwe kama ni nyongeza au mafafanuzi zaidi kuliko mada mpya. Kwa sababu hii, tofauti na ile mifano mingine ya Yesu iliyoanza kwa kusema “Mmesikia”, sehemu hii fupi inaanza hivi: “Imenenwa pia.”

“Imenenwa pia, ‘Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka.’ Lakini mimi nawaambia, ‘Kila mtu amwachaye mkewe isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini’.” (Mathayo 5:31-32).

Huu ni mfano mwingine kuhusu jinsi waandishi na Mafarisayo walivyoishika sheria huku wakikataa maana yake.

Hebu tutengeneze Farisayo wa kufikirika tu, aliyeishi siku za Yesu. Ng’ambo ya pili ya mtaa alioishi kuna mwanamke mrembo ambaye anamtamani. Kila siku wakionana anamtania-tania. Mwanamke naye anaonekana kama anampenda, na tamaa yake inaongezeka. Angependa kumwona akiwa uchi, na mara nyingi anapofikiri anamwaza wakifanya mapenzi. Laiti angeweza tu kumpata!

Lakini ana tatizo. Yeye ana mke na yule mwanamke naye ana mume, na dini yake inakataza uzinzi. Hataki kuvunja amri ya saba (hata ingawa kila alipomtamani alikwisha ivunja). Je, afanye nini?

Kuna jibu! Kama wote wawili wakiachana na wenzi wao, anaweza kumwoa huyo mpenziwe! Lakini je, ni halali kupata talaka? Ndiyo! Kuna andiko kabisa! Kumbukumbu la Torati 24:1 inasema juu ya kumpa mkeo cheti cha talaka wakati unapompa talaka! Talaka inaruhusiwa katika mazingira maalum! Ni yapi hayo? Anasoma kwa makini kile Mungu alichosema.

Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake … (Kumbu. 24:1).

Aha! Anaweza kumpa mkewe talaka kama atagundua neno ovu kwake! Naye amekwisha gundua tayari! Havutii kama yule mwanamke wa mtaa wa pili!

Basi, anamwacha mke wake kihalali kabisa kwa kumpa hati ya kumwacha (na inapatikana katika ofisi ya Chama cha Mafarisayo), na kwa haraka anamwoa yule mwanamke aliyekuwa anamtaka, ambaye naye ameachika kihalali. Na hayo yanatokea bila ya kujisikia hatia hata kidogo kwa sababu Torati ya Mungu imefuatwa.

Lakini kwa kweli, Mungu anaona mambo kitofauti. “Neno ovu” linalotajwa hapo kwamba ni ruhusa ya talaka, ni kama Yesu alivyosema, “uasherati”. Yaani, mume alikuwa na ruhusa ya kumwacha mke wake kama angegundua kwamba hakuwa mwaminifu kabla ya ndoa yao (yaani, wakati wa uchumba) au wakati wakiwa na ndoa. Na Yesu mahali pengine alikuwa amesema kwamba, sababu ya pekee iliyoruhusu talaka katika mazingira hayo ilikuwa ni “ugumu wa mioyo” yao (Mathayo 19:8). Yaani, mume mwenye moyo mzuri angemsamehe mwanamke ambaye hakuwa mwaminifu ambaye angetubu. (Mke asiyetubu ni jambo lingine hilo.)

Katika mtazamo wa Mungu, huyo mwanamume wa kufikirika tuliyemsema sasa hivi hana tofauti yoyote na mwasherati. Ameivunja amri ya saba. Ukweli ni kwamba ana hatia kuliko hata yule mwasherati wa kawaida, maana yeye ni “mwasherati mara mbili”. Kwa vipi? Kwanza: Yeye mwenyewe amezini. Yesu alisema baadaye kwamba, “Yeyote amwachaye mke wake, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, akamwoa mwingine, azini” (Mathayo 19:9).

Pili: Kwa sababu, huyo mkewe aliyeachika sasa lazima atafute mume mwingine ili aendelee kuishi. Basi, katika mtazamo wa Mungu, huyo Farisayo amefanya kitendo kinacholingana na kumlazimisha mke wake awe na uhusiano wa kimwili na mwanamume mwingine. Sasa, anakuwa na hatia kwa “uasherati” wa mkewe. Yesu alisema hivi, “Kila amwachaye mke wake, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya azini” (Mathayo 5:32 – Maneno mepesi ili kutilia mkazo).

Yawezekana kwamba Yesu hata alimhukumu huyo Farisayo wetu mwenye tamaa kwa kosa la “uasherati mara tatu” ikiwa tamko Lake kwamba, “na kila amwoaye mwanamke aliyeachwa azini” (Mathayo 5:32) linamaanisha kwamba Mungu anamhesabu huyo Farisayo kuwa na hatia kwa sababu ya “uasherati” wa mume mpya wa mke wake wa zamani.

Hili lilikuwa swala kubwa katika siku za Yesu, kama tunavyosoma mahali pengine ambapo Mafarisayo fulani walimwliza hivi: “Je, ni halali kwa mwanamume kumwache mke wake kwa sababu yoyote?” (Mathayo 19:3). Swali lao linadhihirisha mioyo yao. Bila shaka baadhi yao walitaka kuamini kwamba sababu yoyote inafaa kwa talaka kutolewa.

Lazima niongeze kwamba ni aibu sana wakati Wakristo wanapochukua mistari hiyo hiyo kuhusu talaka, kuitafsiri vibaya, kisha kuweka vifungo vizito juu ya watoto wa Mungu. Yesu hakuwa anazungumza juu ya Mkristo ambaye aliachana na mwenzake wakati wote wakiwa wenye dhambi, na ambaye baada ya kumpata mwenzi mzuri tu anayempenda Kristo, wanaoana. Huo si uasherati hata kidogo! Na kama hayo ndiyo Yesu alikuwa anazungumzia, basi itabidi tubadilishe Injili, kwa sababu haitoi tena msamaha kwa dhambi zote za wenye dhambi. Tangu sasa itabidi tuhubiri hivi: “Yesu alikufa kwa ajili yako, na ukitubu na kumwamini, utasamehewa dhambi zako zote. Lakini, kama una talaka, hakikisha kwamba huingii tena katika ndoa maana utakuwa mwasherati, na Biblia inasema waasherati wote watakwenda jehanamu. Tena, kama uliachana na mwenzi kisha ukawa na ndoa tena, kabla ya kuja kwa Kristo itakubidi utende dhambi nyingine moja na kuachana na mwenzako mliye naye sasa. Vinginevyo utaendelea kuishi katika uasherati, na waasherati hawajaokoka.” Je, hiyo ndiyo Injili?

Kuhusu Kuwa Wakweli

Mfano wa tatu wa Yesu kuhusu tabia isiyo haki na kutafsiri vibaya maandiko kulikofanywa na waandishi na Mafarisayo unahusu amri ya Mungu kusema ukweli. Waandishi na Mafarisayo walikuwa wametunga njia ya kijanja sana ya kudanganya. Tunajifunza kutoka Mathayo 23:16-22 kwamba waliamini hawakuwajibika kutunza viapo vyao kama waliapa kwa hekalu, madhabahu au mbingu. Lakini kama wangeapa kwa dhahabu ya hekaluni, au sadaka iliyokuwa madhabahuni, au kwa Mungu wa mbinguni, basi walitakiwa kutimiza viapo vyao!

Huu unafiki ndiyo ukawa mada iliyofuata katika mahubiri maarufu ya Yesu.

“Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, ‘Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako.’ Lakini mimi nawaambia, ‘Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu’.” (Mathayo 5:33-37).

Amri ya Mungu kuhusu viapo haikusema chochote juu ya kufanya viapo kwa kuvijenga juu ya kitu chochote. Mungu alikusudia watu Wake wawe waaminifu kutunza maneno yao. Wakati watu wanapolazimika kutumia kiapo ili kuwafanya wengine waamini maneno yao, huo ni ukiri wa dhati kwamba wakati mwingine huwa wanadanganya. Neno letu linapaswa kuwa kama lilivyo, bila kuhitaji viapo. Je, haki yako inazidi ya waandishi na Mafarisayo katika eneo hilo?

Dhambi Ya Kulipiza Kisasi

Kinachofuata kwenye orodha ya Yesu ni kupotoshwa kwa mstari maarufu sana katika Agano la Kale kulikofanywa na Mafarisayo.

“Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, ‘Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo’.” (Mathayo 5:38-42).

Torati ya Musa ilitangaza kwamba kama mtu angepatikana na hatia katika baraza, ya kumjeruhi mtu mwingine, adhabu yake ingekuwa sawa na madhara aliyosababisha. Kama alimtoa mtu jino, yeye naye la kwake litolewe, kwa haki kabisa. Hii amri iliwekwa ili kuhakikisha kwamba haki ilikuwepo barazani kwa ajili ya makosa makubwa. Lakini tena, waandishi na Mafarisayo waliigeuza, wakaifanya kuwa amri nyingine kabisa iliyofanya kisasi kuwa wajibu mtakatifu! Inaonekana walikuwa hawana suluhu, wakitafuta kulipiza kisasi hata kwa kosa dogo kabisa.

Mungu mara zote anatazamia ziada kutoka kwa watu Wake. Kulipiza kisasi ni kitu anachokataza kabisa (ona Kumbu. 32:35). Agano la Kale lilifundisha kwamba watu wa Mungu waonyeshe wema kwa adui zao (ona Kutoka 23:4-5; Mithali 25:21-22). Yesu aliunga mkono kweli hiyo kwa kutuambia tugeuze shavu la pili na kwenda maili ya zaidi tunaposhughulika na watu waovu. Tunapokosewa, Mungu anataka tuwe na huruma, tukilipa jema mahali tulipofanyiwa uovu.

Lakini je, Yesu anatazamia kweli tuwaruhusu watu wengine watuonee na kututumia, mpaka kuwaruhusu waharibu maisha yetu kama ndicho wanachotaka? Je, ni makosa kumpeleka asiyeamini mahakamani, kutafuta haki kwa tendo lisilo halali ambalo tumetendewa? Hapana. Yesu hakuwa anazungumza juu ya kupata haki kwa ajili ya makosa makubwa mahakamani, bali alizungumza juu ya kujilipiza kisasi kibinafsi kwa ajili ya makosa madogo madogo. Ona kwamba hakusema tutoe shingo zetu ili tunyongwe na yule ambaye ametuchoma kisu mgongoni. Hakusema kwamba mtu akidai gari letu, tumpe na nyumba. Yesu alikuwa anatwambia jinsi ya kuonyesha uvumilivu na huruma kwa kiwango cha juu sana wakati tunapokabiliana na makosa madogo madogo na changamoto za kawaida za kushughulika na watu wenye ubinafsi. Hatazamii twende “maili mia zaidi”, anatazamia twende “maili moja zaidi”. Anataka tuwe wema kuliko watu wabinafsi wanavyotazamia, na tusiwe wachoyo na fedha zetu, tukitoa kwa ukarimu na kukopesha. Waandishi na Mafarisayo hawakufika hata nusu ya kiwango hicho. Vipi wewe – haki yako inazidi yao katika eneo hili?

Siwezi kuacha kuuliza hivi: Mbona wengi wanaojiita Wakristo wanakwazwa kirahisi mno? Mbona wanakasirishwa upesi na vikwazo ambavyo ni vidogo mara kumi kuliko kupigwa kofi shavuni? Je, watu hao wameokoka?

Kuwapenda Jirani Zetu

Mwisho Yesu akataja amri nyingine moja iliyotolewa na Mungu ambayo waandishi na Mafarisayo walikuwa wameibadilisha ili kulingana na mioyo yao yenye chuki.

“Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Umpende jirani yako’ na ‘Umchukie adui yako’. Lakini mimi nawaambia, ‘Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni. Maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi, ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu’.” (Mathayo 5:43-48).

Katika Agano la Kale, Mungu alikuwa amesema hivi: “Mpende jirani yako” (Walawi 19:18), lakini waandishi na Mafarisayo, kwa mawazo yao tu, wakawa wamefikiri kwamba, kama Mungu alitaka wawapende jirani zao, basi pia alimaanisha wawachukie adui zao. Ukawa wajibu wao mtakatifu. Lakini, kulingana na Yesu, Mungu hakumaanisha hivyo, na wala hakusema hivyo.

Baadaye Yesu angefundisha katika hadithi ya Msamaria Mwema kwamba tunapaswa kumhesabu kila mtu kuwa ni jirani yetu. Mungu anataka sisi tumpende kila mtu, pamoja na adui zetu. Hicho ndicho kiwango cha Mungu kwa watoto Wake, ambacho Yeye Mwenyewe anakifuata. Yeye hutuma mvua na jua kwa ajili ya kukuza mazao, si kwa watu wema tu, bali hata kwa waovu. Tunapaswa kufuata mfano Wake, tukionyesha wema kwa watu hata wasiostahili. Tukifanya hivyo, tunaonyesha kwamba sisi ni “wana wa Baba [yetu] aliye mbinguni” (Mathayo 5:45). Watu waliozaliwa upya kweli kweli hutenda kama Baba yao.

Upendo ambao Mungu anatazamia tuwaonyeshe adui zetu si hisia au kukubaliana na uovu. Mungu hatulazimishi tuwe na hisia za joto zisizoeleweka kuhusu wanaotupinga. Hatuambii tuseme kisichokuwa kweli, kwamba adui zetu ni watu wazuri kweli. Lakini anatutazamia tuwapende na kuchukua hatua za makusudi kuonyesha hilo, haidhuru basi iwe ni kwa kuwasalimu vizuri na kuwaombea.

Vipi Wewe?

Mpaka hapa unatambua kwamba waandishi na Mafarisayo hawakuwa wenye haki hata kidogo. Walikuwa na aina fulani ya haki ya nje, lakini, sawa tu na wengi wanaojiita Wakristo, walikuwa wenye chuki, tamaa mbaya, wabinafsi, wenye kulipiza kisasi, wasio na huruma, wachoyo, na wadanganyifu wenye kubadili Maandiko. Lakini, kulingana na Yesu, waamini wa kweli wanaonyeshwa kuwa wapole, wenye njaa ya haki, wenye rehema, wasafi moyoni, wapatanishi na wanaoudhiwa au kuteswa. Basi, sehemu hii ya Mahubiri ya Mlimani inatakiwa ifanye mambo mawili: Aidha ikujaze uhakika kwamba kweli wewe umezaliwa mara ya pili, au ikujaze hofu kwa sababu unatambua kwamba huna tofauti na wale waliohukumiwa na kulaumiwa na Yesu. Kama uko katika fungu la kwanza, wewe kama wengine wote hapo tambua kwamba bado una nafasi ya kufanya maboresho. Lakini, ukamilifu ndilo lengo lako kwa sababu ndilo lengo la Mungu kwa ajili yako, kama alivyosema Yesu (ona Mathayo 5:48; ona pia Wafilipi 3:12-14).

Kama uko kwenye lile fungu la pili, unaweza kutubu na kuwa mtumwa wa Yesu kwa kumwamini. Mara moja utajisikia ukihamishwa na Mungu na kuingizwa katika fungu lile la kwanza kwa neema Yake!

 

“Mkristo” Ambaye Hajajitoa

SURA YA NNE

 

Hivi karibuni mfuasi kijana wa Ukomunisti alimwandikia mchumba wake barua ya kuvunja uchumba, baada ya kufunguliwa kutoka gerezani. Aliandika hivi:

“Sisi Wakomunisti tunakufa sana. Sisi ndiyo hupigwa risasi au kunyongwa au kudhihakiwa au kufukuzwa kazi na kufanyiwa maudhi mengi tu ili maisha yetu yasiwe mazuri. Asilimia fulani yetu huuawa au kufungwa. Tunaishi katika umaskini kabisa. Kila senti tunayopata ambayo ni zaidi ya mahitaji tuliyo nayo tunatakiwa kuitoa kwa chama. Sisi Wakomunisti hatuna muda wala fedha kwa ajili ya kwenda sinema sana, au kwenye matamasha ya muziki, au kula nyama, au kukaa nyumba nzuri, au magari mapya. Tunaitwa waliobobea. Sisi tumebobea katika ukomunisti. Maisha yetu yanatawaliwa na jambo moja kubwa: Kuufanya ulimwengu mzima kuwa wa Kikomunisti. Sisi tuna mtazamo katika maisha ambao hakuna kiasi chochote cha fedha kinachoweza kuununua. Tuna jambo tunalopigania, tuna kusudi dhahiri maishani mwetu. Tunaweka makusudi yetu na nia zetu kwenye nafasi ya pili maana nafasi ya kwanza ni kuteka ulimwengu. Basi, japo maisha yetu binafsi yanaonekana kuwa magumu au ubinafsi wetu unaonekana kuteseka kwa sababu ya kujiweka nafasi ya pili chini ya chama, tunafidiwa sana kwa wazo kwamba kila mmoja wetu kwa njia yake ndogo tu anachangia kuleta kitu kipya na cha kweli na kilicho bora kwa ajili ya mwanadamu.

Kuna kitu kimoja tu ambacho nina shauku nacho sana maishani, nacho ni Ukomunisti. Ni maisha yangu, ndiyo biashara yangu, ndiyo dini yangu, ndiyo kazi yangu, ndiyo mpenzi wangu, ndiyo mke wangu, ndiyo pumzi yangu na chakula changu. Ninautumikia mchana na kuota juu yake usiku. Ukomunisti umenishika sana, na nguvu yake inazidi badala ya kupungua kadiri muda unavyopita. Basi, siwezi kuingia kwenye urafiki, wala kujiingiza kwenye mapenzi wala mazungumzo bila ya kuvihusisha hivyo na hiki kitu changu ambacho ndicho kinasukuma maisha yangu na kuyapa nguvu. Ninawatazama watu, vitabu, hoja na matendo kulingana na jinsi vyote hivyo vinavyoathiri Ukomunisti, na jinsi wao wanavyoutazama. Tayari nimekwisha fungwa kwa ajili ya msimamo wangu, na kama ni lazima, niko tayari kupigwa risasi kwa ajili hiyo hiyo.”

Japo amedanganywa na kupotoshwa, huyu mfuasi kijana wa Ukomunisti ana kitu ambacho wengi wanaojiita Wakristo hawana: kujitoa. Tunaweza kutikisa vichwa kwa kumhurumia kwamba ameamini kitu potofu, lakini imani yake imethibitishwa kuwa ya kweli kwa matendo yake. Hatuwezi kusema hivyo kuhusu wote wanaodai kwamba ni wafuasi wa Kristo.

Imani ya kweli daima hujidhihirisha kwa matendo. Kuna mlingano usiotenganishwa kati ya imani na tabia au mwenendo. Kama alivyoandika Martin Luther katika utangulizi wa kitabu chake cha kufafanua Waraka kwa Warumi, “Kweli kweli haiwezekani kutenganisha matendo na imani, kama ambavyo haiwezekani kutenganisha joto na mwanga kutoka katika moto.”

Utajuaje kwamba mtu anaamini unachomwambia? Utajua kama atatenda kama anayekuamini. Ukimwambia kwamba kuna mdudu hatari anayempandia mguuni, naye acheke tu na kuendelea kuzungumza nawe, jua kwamba hakuamini. Vivyo hivyo mtu anayemwamini Yesu hutenda kulingana na imani yake. Imani yake inaonyeshwa kwa kutii kwake.

Japo wengi wanaokiri kwamba ni Wakristo hudai kwamba wanamwamini Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, inaonekana kutokana na matendo yao kwamba hawaamini hata kidogo. Juu ya hao Paulo aliandika hivi: “Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana …” (Tito 1:16).

Yesu, Afisa Mkuu Mtendaji

Hebu fikiri kwamba unafanya kazi kwenye kampuni kubwa sana. Siku moja ukiwa kazini, mtu aliyevalia vizuri sana na ambaye hujawahi kumwona anaingia kwa mlango wa pembeni. Anakuja mezani pako na kusema, “Isaka, mimi ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hili. Tengeneza vizuri meza yako mara moja!” Utafanyaje? Ukweli ni kwamba itategemeana na kuamini kwako au kutokuamini kwamba yeye ndiye Afisa Mkuu Mtendaji kama alivyosema. Ni hivi: Afisa Mkuu Mtendaji ndiye mwenye mamlaka makubwa kuliko mwingine yeyote katika shirika. Yeye ndiye ambaye usingependa achukizwe na wewe. Kwa hiyo, ikiwa unaamini alichosema, mara moja utamtii. Usipomtii ni kwamba huamini yeye ndiye Afisa Mkuu Mtendaji.

Bila shaka unaelewa mfano huo. Kumwamini Yesu husababisha kujitoa kwake. Tunaokolewa kwa kumwamini Yesu, lakini imani yetu lazima iwe imani tiifu, la sivyo si imani. Hicho ndicho kinachosemwa mara mbili na Paulo katika waraka wake kwa Warumi, kwamba ni “utii utokanao na imani” (ona Warumi 1:5; 16:26). Lengo kuu la huduma yake yote lilikuwa ni kusababisha “utii wa imani” kwa watu wote wa Mataifa (ona Warumi 1:5).

Mtu anaweza kusema hivi: “Mfano wako si sawa kwa sababu Yesu si Afisa Mkuu Mtendaji wa kuogopwa.”

Hoja hiyo inaonyesha kiini cha tatizo tulilo nalo. Ikiwa mfano huo si sawa, ni kwenye ukweli kwamba Yesu ni zaidi ya Afisa Mkuu Mtendaji. Yeye ndiye muumbaji wa watu wote, ndiye hakimu wa walio hai na waliokufa; Yeye ana jina kuu lipitalo majina yote.

Lakini, katika mawazo ya wengi wanaojiita Wakristo, Yesu ni Mwokozi tu, siyo Bwana. Yeye ni jirani rafiki, si Kichwa cha Kanisa. Yeye ana upendo wote lakini hana mamlaka yote mbinguni na duniani. Yeye ni “ndugu mpendwa”, si Mfalme wa wafalme. Ni muungwana, lakini si ambaye mbele Zake kila goti litapigwa. Ni mzuri lakini si Mungu. Kibaya ni hiki: Yesu wa aina hiyo hayupo, na wale wanaodhani hivyo ni waabudu sanamu wabaya mno – wamemtengeneza mungu anayelingana na mawazo yao.

Mtume Yakobo anasema tena na tena juu ya kutodanganywa kuhusu imani isiyokuwa na matendo yanayotokana na kutii. Anasema hivi:

Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu… Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake dini yake mtu huyo haifai … Ndugu zangu, yafaa nini mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? (Yakobo 1:22, 26; 2:14 – Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).

Yakobo ameweka hoja yake wazi kabisa na kwa uzuri kabisa. Imani pasipo matendo haiwezi kutuokoa. Tunachokiamini hudhirishwa kwa maneno yetu na matendo yetu. Tena, inawezekana kabisa kujidanganya nafsini mwetu katika jambo hili na kuwa na dini isiyo na faida.

Yakobo anaendelea na kusema hivi:

Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?… Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake, si kwa imani peke yake…. Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa (Yakobo 2:18-20, 24, 26 — Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).

Yakobo anaonyesha kwamba hata mapepo wana imani kiasi fulani, na imani yao huonyeshwa kwa matendo – wanatetemeka kwa hofu. Lakini, ni wangapi wanaojiita waamini wanao-onyesha imani ndogo kuliko hata ya mapepo, kwa maana ya kwamba hawaonyeshi kumwogopa Mungu?

Yesu Alitaka Wasioamini Waamini Kwa Kutii

Ona pia kwamba Yakobo anamhimiza yeyote athibitishe imani yake bila ya matendo (ona Yakobo 2:18). Matendo hayawezi kutenganishwa na imani ya kweli. Hiyo ndiyo sababu imani ya kweli ya kuokoa huanza na toba kila mara. Na hiyo ndiyo sababu kila mara Yesu alipowaita watu waokolewe aliwataka wajitoe kabisa na kutii. Yesu aliwaita watu waingie kwenye imani tiifu, na kwa wengi waliokuwa wanaitenganisha imani na matendo, Yesu aliwakwaza maana hakusema chochote kuhusu imani wakati alipowaita watu kuokoka. Wafuasi Wake wa kweli wangeonyesha imani yao kwa matendo yao.

Cha kushangaza ni kwamba, mwito wa Yesu kwamba watu wajitoe kabisa mara nyingi hupuuzwa na watu wanaojiita Wakristo. Au kama wanakubali, wanajaribu kufafanua kwamba ni mwito wa kuingia katika mahusiano ya ndani zaidi, tena kwa wale ambao wamekwisha pokea neema ya Mungu tayari, sio wale ambao hawajaokoka. Lakini inasikitisha kwamba, wengi katika wale “waamini” wanaodai kwamba mwito wa Yesu kujitoa ni kwa ajili yao na si kwa wasioamini hawasikilizi mwito Wake kwa jinsi wanavyotafsiri. Wao wanafikiri kwamba wana uchaguzi wa kutotii mwito huo, na kwa kawaida hawafanyi hivyo.

Hatua Za Kwanza Au Kuingia Ndani Zaidi?

Hebu tutafakari mwaliko mmoja wa wokovu ambao Yesu aliutoa, unaotafsiriwa kwa makosa mara nyingi na kudhaniwa na wengi wanaokiri Ukristo kwamba ni mwito wa kuingia katika kutembea na Mungu kwa undani zaidi. Mwaliko wenyewe ni huu:

“Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, ‘Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake? Maana kila mtu atakayenionea haya mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu’.” (Marko 8:34-38)

Je, huo ni mwaliko wa wokovu unaotolewa kwa wasioamini au ni mwaliko wa kuingia katika mahusiano ya undani zaidi unaotolewa kwa waamini? Tukisoma kwa ukweli, jibu ni wazi kabisa.

Kwanza: Ona kwamba watu waliokuwa wanaambiwa maneno hayo na Yesu ni “mkutano” pamoja na wanafunzi Wake (ms. 34). Basi, “mkutano” hawakuwa wanafunzi Wake. Wao “waliitwa” Naye ili kusikiliza kitu alichokuwa anataka kusema. Yesu alikuwa anamtaka kila mmoja – wafuasi Wake, na waliokuwa wanatafuta kumjua – waelewe ukweli aliokuwa anataka kufundisha. Ona pia kwamba alipoanza kufundisha alianza kwa kusema, “Mtu yeyote…” (ms. 34 — Maneno mepesi ni ili kutilia mkazo). Yaani, maneno Yake ni kwa yeyote na kila mmoja.

Tunapoendelea kusoma inakuwa wazi zaidi kwamba Yesu alikuwa anazungumza na nani. Maneno Yake hasa yalikuwa yanaelekezwa kwa kila mtu aliyetamani “kumfuata” Yeye, “kuiponya nafsi yake” badala ya “kupata hasara ya nafsi yake” na kuwa miongoni mwa wale ambao Yeye hatawaonea aibu wakati “atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”. Maneno hayo yote yanaonyesha kwamba Yesu alikuwa anaeleza juu ya watu waliokuwa na shauku ya kuokoka. Je, ni sawa kwetu kufikiri kwamba kuna mtu anayetaka kwenda mbinguni ambaye hataki “kumfuata” Yesu na “kuiponya nafsi yake”? Je, ni sawa kwetu kuamini kwamba wapo waamini wa kweli watakaopata “hasara ya nafsi” zao, na wenye kumwonea Yesu na maneno Yake aibu, na ambao Yesu Mwenyewe atawaonea aibu atakaporudi? Basi, ni dhahiri kwamba Yesu alikuwa anazungumza juu ya wokovu wa milele.

Ona kwamba kila sentensi katika zile nne zilizo katika fungu hili lenye sentensi tano inasema kweli muhimu kwa kuanza na maneno “Kwa kuwa”. Ni kwamba kila moja inasaidia kufafanua zaidi ile iliyopita. Hakuna sentensi katika fungu hili inayopaswa kufafanuliwa pasipo kutazama jinsi hizo nyingine zinavyoipa mwanga. Hebu tuangalie maneno ya Yesu sentensi kwa sentensi kwa mtazamo huo.

Sentensi Ya Kwanza

“Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate” Marko 8:34).

Ona tena hapa kwamba maneno ya Yesu yalikuwa yanaelekezwa kwa yeyote aliyetaka kumfuata, yeyote aliyetaka kuwa mfuasi Wake. Huu ndiyo uhusiano wa pekee ambao Yesu anautoa mwanzoni kabisa.

Wengi wanatamani kuwa rafiki bila kuwa wafuasi Wake, lakini hakuna uchaguzi aina hiyo. Yesu hakumhesabu yeyote kuwa rafiki Yake kama hakumtii. “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo” (Yohana 15:14).

Wengi wangependa kuwa ndugu Zake bila kuwa wafuasi Wake. Lakini hapo tena Yesu hakutoa nafasi kama hiyo. Hakuna aliyemhesabu kuwa ndugu Yake kama hakuwa mtii. “Yeyote atendaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu …” (Mathayo 12:58 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Wengi wanapenda kujiunga na Yesu mbinguni bila ya kuwa wafuasi Wake, lakini Yesu aliweka wazi kwamba jambo hilo haliwezi kutokea. Ni wale watiifu tu ndiyo wanaokwenda mbinguni. “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni” (Mathayo 7:21).

Katika sentensi yetu tunayoitazama, Yesu aliwajulisha wale waliotaka kumfuata kwamba wasingeweza kufanya hivyo bila ya kujikana wenyewe. Lazima wawe tayari kuweka shauku zao pembeni, na kuzitia chini ya mamlaka ya mapenzi Yake. Kujikana na kunyenyekea ndicho kiini katika kumfuata Yesu.

Lakini, Yesu anategemea kujikana mpaka wapi? Je, alikuwa anazungumzia juu ya kuacha kula vitu fulani tu wakati wa Pasaka? Katika hiyo sentensi ya kwanza, Yesu alitumia maneno yaliyofanya isiwe vigumu kuelewa anachosema. “Ajitwike msalaba wake.” Pengine si Yeye aliyeanzisha kusema hivyo – labda ilikuwa lugha ya kawaida katika siku Zake. Je, nini maana yake?

Katika siku za Yesu, watu waliojitwika misalaba walikuwa wale waliohukumiwa kufa. Hicho hakikuwa kitu ambacho mtu alipenda kufanya, kwa sababu kilikuwa cha mwisho ambacho angefanya. Wakati mhalifu alipobeba msalaba wake, aliinua kile kipande cha mbao ambacho baada ya muda mfupi angetundikwa juu yake ii afe kifo kibaya, cha taratibu. Ulikuwa ni wakati wa kutisha, wa kukabiliana na kitu kisichoepukika.

Kwa hiyo maneno: “mtu ajitwike msalaba wake” yanafanana na mtu kueleza juu ya kitu ambacho kwa kawaida kisingefanyika. Huo ni mfano wa kujikana kwa hali ya juu sana, kufanya kitu ambacho mtu alikuwa hataki kufanya. Kama ulikuwa msemo wa kawaida katika siku za Yesu, basi tunaweza kufikiri kwamba akina baba walikuwa wanawaambia watoto wao wa kiume wasiopenda kabisa: “Mwanangu! Unajua ni wajibu wako kuchimba choo wakati kimejaa. Sasa, jitwike msalaba wako na uendelee na kazi.” Au wake za watu wakiwaambia waume zao waliokunja uso, “Mume wangu! Najua hupendi kusikia hiki, lakini leo kodi zetu zinatakiwa na serikali ya Kirumi, na tunayo ile fedha inayotakiwa na yule mtoza ushuru tapeli. Hatuna uchaguzi katika jambo hili. Si ujitwike msalaba wako na uende kwenye ofisi yake asubuhi hii mkamalize mambo?”

Sentensi Ya Pili

Sentensi ya pili anayotamka Yesu inafanya maana ya ile ya kwanza kuwa dhahiri zaidi. “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha” (Marko 8:35).

Hapa tena ona kwamba sentensi inaanza kwa neno “kwa kuwa”, lenye kuiunganisha na ile ya kwanza, na kuifafanua zaidi. Hapa Yesu anatofautisha watu wawili, wale wale waliokuwa wametajwa katika sentensi ya kwanza – yule ambaye angekuwa tayari kujikana na kujitwika msalaba wake ili kumfuata, na yule ambaye asingekuwa tayari kufanya hivyo. Yule ambaye asingekuwa tayari kujikana anataka kuokoa nafsi yake, lakini ataipoteza. Yule ambaye angekuwa tayari kujikana atapoteza nafsi yake lakini mwishoni anaiokoa.

Kweli, Yesu hakuwa anazungumza juu ya mtu mmoja kupoteza au kuokoa maisha yake kimwili. Wafuasi Wake wengi walipoteza maisha yao kimwili haraka sana, kwa sababu walimfuata. Walikufa kwa ajili ya imani yao. Tena, sentensi zinazofuata katika fungu hili zinaonyesha kwamba mawazo ya Yesu yalikuwa kwenye mambo ya milele – faida na hasara za milele.

Mtu anayetajwa katika sentensi ya kwanza ambaye asingejikana ni yule yule anayetajwa katika sentensi ya pili ambaye alitaka kuyaokoa maisha yake. Basi, tunaweza kufikia hitimisho kwamba “kuokoa nafsi” maana yake “kuokoa mipango ya mtu kwa ajili ya maisha yake.” Hii inadhihirika zaidi wakati tunapotazama yule mtu anayelinganishwa katika kisa hicho, ambaye “anapoteza nafsi yake kwa ajili ya Kristo na Injili”. Ni huyo anayejikana mwenyewe, anayejitwika msalaba wake na kuachana na mipango yake binafsi, na kuanza kuishi kwa ajili ya kusudi la kuendeleza mipango ya Kristo na kueneza Injili. Huyo ndiye atakaye”okoa nafsi yake” mwisho wa siku, wakati ambapo yule mwingine ataipoteza. Anayetafuta kumpendeza Kristo badala ya kujipendeza mwenyewe atajikuta mbinguni akiwa na furaha, huku yule anayeendelea kujipendeza mwenyewe atajikuta jehanamu akiwa na huzuni, na huko kupoteza kila nafasi ya uhuru wa kufuata mambo yake mwenyewe maishani.

Sentensi Ya 3 Na Ya 4

Sasa tugeukie sentensi ya tatu na ya nne. “Kwa kuwa, itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Au mtu atoe nini badala ya nafsi yake?” (Marko 8:36, 37). Katika sentensi hizi, huyo mtu ambaye hatajikana anawekwa bayana. Ndiye anayetamani kuyaokoa maisha yake, lakini ndiye anayeyapoteza mwishoni. Sasa anazungumzwa kwamba ni mwenye kutaka kufuata kile kitolewacho na dunia na ambaye mwishoni “anapata hasara ya nafsi yake”. Yesu anaonyesha hasara ya mtu wa aina hiyo kwa kufananisha thamani ya dunia nzima na thamani ya hiyo roho moja. Ni kwamba hakuna mlinganisho. Mtu anaweza kupata vitu vyote ambavyo dunia inatoa, lakini, kama matokeo ya mwisho wa maisha yake ni kuwa jehanamu milele, amefanya kosa kubwa sana sana.

Kutokana na sentensi hizo mbili tunapata kuona sababu zinazowavuta watu wasijikane na kuwa wafuasi wa Kristo. Ni ile shauku waliyo nayo ya kujitosheleza, itolewayo na dunia. Wakisukumwa na kujipenda wenyewe, wale wanaokataa kumfuata Kristo wanatafuta starehe za dhambi, ambazo wafuasi wa Kristo wa kweli huziepuka kwa sababu ya kumpenda na kumtii Yeye. Wale wenye nia ya “kupata kila kinachowezekana kwa juhudi zote” hufukuzia mali, mamlaka na sifa, wakati ambapo wale wafuasi wa Kristo wa kweli hutafuta kwanza ufalme Wake na haki Yake. Mali yoyote, mamlaka au sifa vinavyopatikana nao huhesabiwa kama fursa ya uwakili kutoka kwa Mungu, na hutumiwa kwa ajili ya utukufu Wake bila ubinafsi wowote.

Sentensi Ya Tano

Hatimaye tunafikia sentensi ya tano katika fungu tunalotazama. Ona tena jinsi ilivyounganishwa na zile nyingine kwa maneno yale ya kwanza – Kwa maana. “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu” (Marko 8:38).

Hapa tena, anayehusika ni yule ambaye hakujikana mwenyewe. Badala yake, alitaka kufuata mpango wake mwenyewe, akifukuzia vile vitolewavyo na dunia, na ambaye alipoteza maisha yake na mwishowe kupata hasara ya nafsi yake. Sasa anaonyeshwa kwamba ni mtu mwenye kumwonea aibu Kristo na maneno Yake. Aibu yake inatokana na kutokuamini kwake. Kama kweli aliamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, asingemwonea Yeye wala maneno Yake aibu. Lakini ni mmoja kati ya “kizazi cha uzinzi na dhambi” na Yesu atamwonea aibu wakati atakaporudi. Hapa ni wazi kwamba Yesu hakuwa anazungumza juu ya mtu ambaye ameokoka.

Hitimisho ni nini? Ni hili: Fungu hili zima haliwezi kuhesabiwa kuwa mwito wa kuingia katika maisha ya kujitoa zaidi, unaotolewa kwa wale ambao tayari wanakwenda mbinguni. Ni onyesho la wazi kuhusu njia ya wokovu kwa kuwalinganisha wale waliookoka kweli na wale ambao bado. Hakuna hata mara moja ambapo Yesu anataja juu ya imani au kuamini, japo sababu nzima ya mtu kukataa kujikana mwenyewe na kuendelea kufuata vishawishi vya dunia ni uasi wa dhambi dhidi ya Kristo. Na hiyo ni kwa sababu hamwamini Kristo. Tunda la kutokuamini ni kutokutii. Yesu hakuwa anatangaza wokovu upatikanao kwa matendo bali wokovu ambao matokeo yake ni matendo, utokanao na imani ya dhati. Basi, hakuna “Mkristo ambaye hajajitoa kikamilifu” kulingana na tafsiri Yake.

Ubatizo Kama Wanavyofanya Nepali

Mwito wa kuokoka ni mwito wa kujitoa kabisa kwa Kristo. Katika mataifa mengi duniani ambako mateso ni kawaida, jambo hilo linaeleweka vizuri sana na waamini wapya. Wao wanajua kwamba kumfuata Kristo kuna gharama ya kulipa.

Sundar Thapa, Mkristo wa KiNepali ambaye ameanzisha makanisa zaidi ya mia moja katika taifa lake la KiBuddha, alinishirikisha maswali nane ambayo anamwuliza kila mwamini mpya kabla ya kumbatiza. Ni haya:

Je, uko tayari kulazimika kuondoka nyumbani kwenu na kuwaacha wazazi wako?

Je, uko tayari kupoteza haki yako ya kurithi mali ya baba yako?

Je, uko tayari kupoteza kazi yako kama watu wakijua kwamba wewe ni Mkristo?

Je, uko tayari kwenda gerezani?

Je, uko tayari kupigwa na kuteswa na polisi?

Je, uko tayari kufa kwa ajili ya Kristo ikibidi?

Je, uko tayari kuwaambia wengine habari za Yesu?

Je, uko tayari kuleta zaka yako yote na sadaka katika nyumba ya Bwana?

Kama huyo mwamini mpya anajibu ndiyo kwa yote nane, basi lazima atie sahihi karatasi yenye tamko la majibu yake. Ndipo baada ya hapo anabatizwa. Je, ni wangapi kati yetu ambao wangehesabiwa kuwa wameokoka wakiwa Nepal? Au swali muhimu zaidi: Ni wangapi kati yetu watakaohesabiwa kuwa ni Wakristo tutakaposimama mbele za Yesu?

“Waamini” Wasiokuwa Wanafunzi

Pengine mfano mzuri sana wa tafsiri isiyo sahihi ya maneno ya Yesu kuhusu wokovu na kudhaniwa kwamba ni mwito kwa watu “kutembea kwa karibu zaidi Naye” ni yale makundi yanayoundwa siku hizi na wanatheolojia wa kisasa. Wanasema kwamba kuna waamini Wakristo na wanafunzi. Watu wengi sana kanisani wanaamini kwamba mtu anaweza kuwa mwamini wa Kristo anayekwenda mbinguni bila ya kuwa mwanafunzi Wake. Kiwango cha kujitoa ambacho Yesu alitaka kwa mtu kuhesabiwa kuwa mfuasi wake ni cha juu sana kiasi cha kwamba wengi wanaojiita Wakristo lazima wakiri haraka kwamba hawawezi kukifikia. Lakini, hakuna shida maana katika akili zao hatua ya uanafunzi ni ya hiari. Kwa kuwa hawaelewi asili ya imani yenye kuokoa, wao wanaamua kwamba kufanyika mwanafunzi si sawa na kuokoka, kwa sababu ipo gharama ya kuwa mwanafunzi, ila wokovu ni bure.

Lakini kuelewa hivyo ni makosa makubwa. Uchunguzi wa kweli wa Agano Jipya unadhihirisha kwamba wanafunzi si waamini waliojitoa zaidi – wao ni waamini wa kweli tu. Katika kanisa la kwanza havikuwepo vikundi hivyo vya kisasa – “waaminio” na “wanafunzi”. Kila aliyemwamini Yesu alikuwa mwanafunzi Wake. Ukweli ni huu: “Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia” (Matendo 11:26 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Kumwamini Yesu ni kumfuata kwa utii, na ndivyo ilivyo mpaka leo. Wokovu kweli ni zawadi ipatikanayo pasipo kuifanyia kazi, lakini ni zawadi inayopokelewa kwa kuwa na imani hai tu. Kule kujitoa kutokanako na imani kama hiyo si kazi; bali ni kitu kinachothibitisha imani hiyo. Neema inayotusamehe pia inatubadilisha.

Masharti Ya Yesu Kuhusu Uanafunzi

Hebu tutazame masharti ambayo Yesu aliorodhesha kwa mtu kuwa mwanafunzi Wake huku tukitazama kama Maandiko yanafundisha ikiwa waamini wote wa kweli ni wanafunzi.

Tunasoma katika Luka 14:25 kwamba “makundi makubwa” yalimfuata Yesu. Lakini Yeye hakuridhika. Makundi makubwa ya mashabiki wakati mambo ni mazuri hayakumgusa. Alitaka kujitoa kwa moyo wote, bila ya kubakiza chochote. Alitazamia kupendwa na kuaminika kwa hali ya juu kabisa. Basi akawaambia hivi:

“Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Luka 14;26).

Hakuna mfasiri wa Maandiko mwenye akili timamu atakayesema kwamba Yesu alimaanisha mtu lazima awachukie kweli wale anaowapenda sana maishani mwake ili kuwa mfuasi Wake. Ni dhahiri kwamba Yesu alikuwa anatumia lugha ya mfano. Bila shaka alichokuwa anamaanisha ni kwamba upendo wetu kwa tunaowapenda uonekane kama chuki unapolinganishwa na upendo wetu Kwake Yeye. Alimaanisha kwamba Yeye ndiye awe wa kwanza katika kupendwa maishani mwetu. Wanafunzi Wake wanapaswa kumpenda Yeye zaidi sana kuliko mtu mwingine yeyote, na hata wao wenyewe.

Yesu akaendelea na kusema hivi: “Mtu yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Luka 14:27).

Hapa tena si kwamba maneno Yake yachukuliwe kama yalivyo. Hatazamii wanafunzi Wake kubeba misalaba ya mbao kila waendapo. Kuubeba msalaba wa mtu lazima iwe ni ishara ya kitu fulani, na vyovyote vile, nani atafikia mahali pa kudhani kwamba Yesu alikuwa anazungumzia kitu kizuri cha kupendeza au rahisi? Sasa sana alikuwa anazungumzia kujitoa kwa kujikana.

Ona pia kwamba hili sharti la pili la mtu kuubeba msalaba wake ni sawa na lile ambalo Yesu aliwataka wote waliotaka kumfuata wafanye, kama tulivyoona katika mafunzo yetu mapema katika sura hii, kutoka Marko 8:34 hadi 38. Yesu katika fungu hilo bila shaka alikuwa anataja masharti ya wokovu, akionyesha ushahidi dhahiri kwamba masharti ya kuokoka na kuwa mfuasi ni sawa – ni yale yale.

Alipoendelea na fundisho Lake juu ya uanafunzi, ndipo alipowashauri wasikilizaji Wake kuhesabu gharama kabla ya kuanza kuwa wafuasi Wake. Anasema hivi:

“Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.’ Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali” (Luka 14:28-32).

Nani awezaye kupinga kwa usahihi kwamba hakuna gharama ya kuwa mwanafunzi wa Kristo kutokana na maneno hayo?

Akamalizia hivi: “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu” (Luka 14:33). Ili kuwa mwanafunzi wa Yesu hatuna budi kuacha umiliki wa vitu vyetu vyote, avimiliki Yeye. Tunafanyika mawakili tu wa vitu vile ambavyo vimekuwa Vyake kuanzia hapo, na mali yetu inatumiwa kwa makusudi Yake. Vinginevyo, sisi si wanafunzi Wake.

Ni wazi Yesu alitaka kuonyesha kwamba kuwa mwanafunzi Wake ni kujitoa kwenye gharama kubwa. Lazima Yeye awe wa kwanza katika maisha yetu, nasi lazima tumpende kuliko maisha yetu, watu tunaowapenda na mali zozote.

Sharti Lingine

Wakati mwingine tena Yesu alieleza maana ya kuwa mwanafunzi Wake. Yohana anataarifu kwamba wakati Yesu alipokuwa anazungumza Hekaluni,

Wengi walimwamini. Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, ‘Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru’.” (Yohana 8:30-32)

Ona kwamba Yohana mara mbili anatuambia kwamba maneno ya Yesu katika 8:31-32 yalitolewa kwa waliokuwa wanamwamini. Kwa hao waamini wapya, Yesu hakuwaambia hivi: “Huko baadaye mtahitaji kufikiri kujitoa kabisa kama wanafunzi.” Hapana. Yeye alisema nao moja kwa moja kama wanafunzi. Kwa Yesu, kumwamini Yeye ilikuwa ni sawa na kuwa mwanafunzi.

Vile vile angalia kwamba Yesu hakuwahakikishia mara moja hao waamini kwamba wameokoka kama inavyofanyika leo. Badala yake, Yeye aliwapa changamoto wajihoji ikiwa imani yao ilikuwa ya kweli. Je, walikuwa wanafunzi Wake kweli kweli? Ingefanyika hivyo kama wangedumu katika neno Lake.

Kudumu katika neno la Yesu maana yake ni kukaa ndani yake, kupafanya kuwa nyumbani kwako au makao yako. Huonyesha shauku ya kutaka kujua na kulitii neno Lake, kama tu alivyosema: “Mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru” (Yohana 8:32 — Maneno mepesi ni ili kutilia mkazo). Yesu hasa alikuwa anazungumza juu ya uhuru kutokana na dhambi (ona Yohana 8:34-36). Hili tena linatwambia kwamba wanafunzi wa kweli wa Yesu, wale ambao wamemwamini Yeye kweli kweli na kuzaliwa mara ya pili, wanaonekana kwa utakatifu wao unaozidi kukua.

Ubatizo Wa Wanafunzi

Katika Agizo Kuu lipatikanalo katika mistari ya mwisho ya Injili ya Mathayo, Yesu alitumia neno mwanafunzi kwa njia isiyoleta mashaka yoyote kuhusu maana yake. Alisema hivi: “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:19, 20 – Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).

Cha kwanza tunachoona hapa ni kwamba Yesu anataka wanafunzi, naye anawataka hao wabatizwe. Lakini tunajua pia kwamba Yesu na waandishi wa Agano Jipya wanakubaliana kwamba kila anayemwamini Yesu anatakiwa kubatizwa mara tu anapokiri imani yake kwa Kristo. Hii inaonyesha tena kwamba waamini wote wa kweli ni wanafunzi. Yesu hakuwa anasema katika Agizo Lake Kuu kwamba tusiwabatize wale wanaomwamini Kristo, bali kwamba tuwabatize wale wote wanaochukua hatua ya kuwa wanafunzi waliojitoa kikamilifu.

Kutokana na kusoma juu ya Agizo Kuu, ni wazi pia kwamba Yesu alimhesabu mtu aliyekuwa anataka kujifunza maagizo Yake yote na kuyashika kuwa ndiye mwanafunzi (Mathayo 28:20). Ni wazi kwamba kujifunza ni kitu kinachoendelea, kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye anakuwa mtii mara moja katika kila kitu. Lakini kila mwanafunzi wa kweli anakubali kuwa chini ya Kristo, anakubali kujitia katika kujifunza na kufanya mapenzi Yake, na kwa njia hiyo anakuwa mwamini wa kweli kwa sababu waamini wote wa kweli ndiyo wanafunzi.

Ushuhuda Wa Yohana

Ushahidi mwingine kwamba waamini na wanafunzi ni kitu kimoja unapatikana katika Injili ya Yohana, na waraka wake wa kwanza. Hebu linganisha mistari ifuatayo:

“Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi> wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:34, 35 – Maneno mepesi kwa ajili ya kutilia mkazo).

Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti (1Yohana 3:14).

Upendo usio na ubinafsi kwa ndugu ndiyo unaonyesha wanafunzi wa Kristo wa kweli, na pia unawaonyesha wote waliopita kutoka mautini kwenda uzimani, yaani, wale ambao wamezaliwa mara ya pili. Sababu rahisi ni kwamba, wanafunzi wa Kristo ni wale tu ambao wamezaliwa mara ya pili.

Matawi Yadumuyo Katika Mzabibu

Mwaliko mmoja wa mwisho kuhusu wokovu ambao mara nyingi hutafsiriwa kwamba ni mwito wa kuingia katika “undani wa mwenendo” unapatikana katika Yohana 15. Hapa tena Yesu anafafanua maana ya kuwa mwanafunzi Wake. Anasema hivi:

“Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu” (Yohana 15:1-8 – Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).

Mahubiri mengi sana yamehubiriwa kwa Wakristo waamini kutoka mistari hii, yakiwashauri “kusogea karibu na Yesu” na kukaa ndani Yake ili waweze kuzaa matunda mengi! Lakini, Yesu hataki tufikiri kwamba kukaa ndani Yake ni kitu ambacho waamini waendao mbinguni wanahitaji kuamua kuwa nacho au hapana. Kukaa ndani Yake ni sawa na kuokoka – kama maneno ya Yesu yanavyoweka bayana kabisa: “Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea” (Yohana 15:6). Wale wasiokaa ndani ya Kristo wamelaaniwa. Wale wanaokaa ndani ya Kristo huzaa matunda, wakijithibitisha kwamba ni wanafunzi Wake kama Yesu alivyosema (Yohana 15:8). Hapa tena tunaona kwamba watu waliookoka kweli ni wanafunzi wanaozaa matunda.

Mizabibu inaweza kuzaliwa kwenye tawi ambalo limeunganika na mzabibu tu. Tawi hupokea uzima kutoka kwa mzabibu, ambacho ndicho muhimu kwa ajili ya kuzaa matunda. Huo ni mfano unaofaa kabisa wa mahusiano yetu na Kristo. Tunapomwamini Kristo, tunafanyika tawi lililo hai, lenye kuzaa matunda ndani Yake. Sawa na jinsi ambavyo maji ya uzima yanavyopita katika mzabibu na kupeleka uhai kwa tawi ili liweze kuzaa matunda, ndivyo na Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu alivyo chanzo cha matunda ya mwamini.

Je, ni matunda ya aina gani yanayozalishwa kwa nguvu za Roho Mtakatifu? Bila shaka Roho Mtakatifu anazaa tunda la utakatifu. Orodha ya Paulo ya tunda la Roho inayopatikana katika sura ya tano ya Wagalatia inaanza kwa tunda la upendo, ambalo, kama tulivyokwisha ona hapo nyuma, ndiyo alama ya wanafunzi wa kweli wa Yesu. Orodha hiyo inaendelea kwa kutaja tunda la furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (ona Wgalatia 5:22). Hayo ndiyo Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu anayozalisha, na hayo ndiyo alama ya kila mwamini wa kweli kwa kiasi fulani. Kwa mfano: Tunasoma kwamba wanafunzi wa kwanza mara zote “walijaa furaha na Roho Mtakatifu” (Matendo 13:52).

Matunda huiva na kukomaa, na ndivyo ilivyo hata kwa tunda la Roho. Wakristo wasiokomaa mara nyingi wana matunda ambayo bado ni mabichi. Lakini, kama Roho anakaa ndani ya mtu (na ndivyo ilivyo kwa kila aaminiye kweli – Warumi 8:9), haiwezekani Yeye Roho asizae matunda Yake.

Vipi Kuhusu Tawi Lisilozaa Katika Kristo?

Lakini, Yesu si alizungumzia kuhusu uwezekano wa tawi “ndani Yake” lisilozaa matunda? Ndiyo. Ila, tamko Lake lazima litafsiriwe katika maelezo Yake kuhusu mzabibu na matawi. Ona kwanza kwamba tawi “ndani Yake” lisilo na matunda “linaondolewa” (Yohana 15:2). Maana yake ni kwamba hilo tawi lililokuwa kwenye mzabibu halipo tena. Kilichotokea kwa tawi hilo baada ya “kuondolewa” ni kitu cha kufikiri. Lakini, baada ya tawi hilo “kuondolewa” na kutokuwepo tena, bila shaka haliwi “linalokaa kwenye mzabibu.” Basi, ni kitu gani kinachotokea kwa matawi yasiyokaa katika mabibu? Yesu alisema hivi katika mistari ya mbele kidogo: “Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea” (Yohana 15:6).

Inabidi tuwe makini sana tunapofasiri mfano wa aina yoyote. Mfano ni mlinganisho wa vitu viwili ambavyo havifanani kimsingi, japo vina mambo kidogo yanayofanana. Ninapomwambia mke wangu kwamba macho yake ni kama vidimbwi vya maji, maana yake ni kwamba yana kina, ni meusi na yenye kuvutia. Lakini hapo ndipo mwisho wa kufanana. Sina maana kwamba samaki huogelea ndani yake au kwamba bata maji hutua hapo au kwamba yanaganda wakati kuna baridi!

Na mifano ya Yesu ni vivyo hivyo. Tunaweza kutafuta kwa makosa maana ya kiroho katika maelezo ambayo yamekwisha kwa habari ya kufanana kwake. Kwa mfano: Siwezi kutumia mfano wa Yesu kuhusu “mzabibu na matawi” ili kuthibitisha kwamba Wakristo wanazaa matunda zaidi wakati wa miezi ya joto, kama ambavyo ni kweli kwa mizabibu. Hapo ni kuongezea mambo yasiyofaa katika mfano.

Vivyo hivyo siwezi kufikia uamuzi kwamba Yesu alikuwa anajaribu kusema kwamba mwamini wa kweli ndani Yake anaweza asizae matunda kabisa, hasa tunapotambua kwamba hoja kuu ya mfano Wake huo inakwenda kinyume na wazo hilo. Hitimisho linalofaa basi ni kwamba lile tawi lisilozaa lililokuwa “ndani Yake” linamwakilisha mwamini anayerudi nyuma na kuanguka (linganisha na Luka 8:12, 13). Anafanyika mtu asiye na matunda na mwishowe anakatiliwa mbali kutoka kwa Kristo. Licha ya kuwepo mawazo mengi kinyume cha hilo, Maandiko yanaonyesha kwamba ni kitu kinachowezekana. Tutajaribu kuthibitisha hicho katika sura nyingine huko mbele. Uwezekano mwingine wa pekee ni kwamba tunda hilo lisilozaa ni mfano wa mwamini bandia, anayedhani yuko ndani ya Kristo lakini kumbe amekufa na hapati nguvu za uzima kutoka Kwake, kama inavyo-onekana kwa kutokuwa na matunda. Lakini, Yesu hakufafanua matawi kuwa ni wale wanaokiri tu kwamba wamo ndani Yake na kumbe hawamo. Yeye alifafanua matawi kwamba ni wale walio ndani Yake.

Wale wazaao matunda wameahidiwa kusafishwa na Mungu Mwenyewe. Pengine Yesu alikuwa anazungumza juu ya kusafishwa kwa hali ya juu ambako hutokea wakati wa kuzaliwa upya, mtu anapoonyesha matunda yale ya mwanzo kabisa ya toba na imani. Au labda alikuwa anaeleza juu ya kuendelea kwa mpango wa utakaso ambao Mungu huutekeleza katika maisha ya kila mwamini anayekubaliana Naye (ona Wafilipi 2:13). Vyovyote vile, mfano wa Mungu kwamba ni mkulima (au mtunza mizabibu) unazungumzia juu Yake Yeye akikata kitu kisichompendeza katika maisha yetu. Chochote kinachozuia matunda yasizalishwe na Roho anayekaa ndani yetu kitakutana na makasi Yake ya kukatia.

Upinzani Mdogo

Mara nyingi swali hutokea kuhusu Yusufu wa Arimathea, ambaye Biblia inasema alikuwa “mwanafunzi wa siri” wa Yesu (ona Yohana 19:38). Je, anawezaje kusemekana ni mwanafunzi kama imani yake ilikuwa ya siri? Je, hayo hayapingani na yote niliyoandika juu ya hali ya kujitoa inayoonyeshwa na wanafunzi wa kweli?

Hebu nianze kwa kusema kwamba jambo hilo hunisumbua mara nyingi sana kwamba, baada ya kutoa andiko baada ya andiko lenye kuthibitisha kweli fulani, mtu atatafuta mstari mmoja mdogo, uliofichika, ambao unaonekana ni kana kwamba unapinga yote niliyofundisha. Kisha anautaja kwa kiburi, kana kwamba huo mstari mmoja tu unabatilisha ile mingine yote tuliyokwisha itazama. Hoja hii ya sasa ni mfano. Kila kitu nilichoandika juu ya gharama ya kujitoa kuhusu uanafunzi kimejengwa kwenye Maandiko. Nimesema kinachosemwa na Biblia. Kwa hiyo, swala la kuunganisha uanafunzi wa siri wa Yusufu wa Arimathaya na yale yote yaliyofundishwa na Yesu kuhusu gharama ya kujitoa ya uanafunzi wa kweli ni letu wote, si langu peke yangu.

Sasa tujibu hoja: Yusufu wa Arimathaya alimpenda Yesu sana. Kulingana na taarifa ya Biblia, alikuwa “mtu mwema na mwenye haki” (Luka 23:50). Lakini, kama mwanachama maarufu wa Baraza la Wazee wa Kiyahudi (Sanhedrin), alificha upendo wake “kwa kuwaogopa Wayahudi” (Yohana 19:38). Wayahudi aliowaogopa bila shaka walikuwa wale wanachama wengine wa Baraza la Wazee wa Kiyahudi.

Ni wazi kwamba Yusufu wa Arimathaya alijua kwamba yalikuwepo matokeo mabaya kwake kama angefunua jinsi alivyojisikia kuhusu Yesu. Inawezekana kwamba alichokuwa anaogopa ni kuondolewa kwenye Baraza lile, kitu ambacho kingempunguzia nafasi ya kuwashawishi vizuri kuhusu Kristo. Tunajifunza kutoka Luka 23:51 kwamba Yusufu “hakukubaliana” na “mipango” ya Baraza kuhusu kukamatwa, mashtaka na hukumu iliyotolewa kwa Yesu. Na baada ya kifo cha Yesu, alifanya kitu kilichoweka hatarini hadhi yake, maana tunaambiwa kwamba “akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu” (Marko 15:43). Kisha, yeye mwenyewe binafsi akautayarisha mwili wa Yesu na kuuzika katika kaburi lake mwenyewe. Hakika uwezekano wa kugunduliwa kwa mambo aliyofanya na Baraza ulikuwa mkubwa! Lakini baada ya kusulubiwa kwa Yesu, inaonekana hakujali tena kwamba wenzake katika Baraza wanafikiri nini.

Kujitoa kwa Yusufu kwa Kristo kilikuwa kitu wazi, na usiri wake kuhusu upendo wake ulikuwa ni wa muda tu. Zaidi ya hayo, inawezekana kuwa mwanafunzi halisi wa Kristo na kuogopa matokeo mabaya yanayoweza kutokana na jambo hilo. Yusufu wa Arimathaya alikuwa na matunda mengine katika maisha yake yaliyothibitisha kujitoa kwake kwa Kristo kuwa ni halisi.

Vipi Kuhusu Wakristo “Wa Kimwili”?

Kuna upinzani mwingine unaotolewa mara kwa mara. Siku hizi kuna wanaoitwa “Wakristo wa kimwili”. Wao ni kundi la kisasa la waamini wanaodaiwa kuwa wa kweli, ambao mara kwa mara wanakubaliana na mwili, na ambao matendo yao ya kimwili huwafanya kuwa kama wasiokuwa waamini. Japo “wamempokea Kristo”, hawaonyeshi kujitoa kwao Kwake. Wengi wao hawahudhurii hata kanisani, na wanafanya dhambi nyingi tu, lakini inasemekana wao ni salama katika neema ya Mungu, na wanakwenda mbinguni.

Je, hilo wazo kwamba kuna Wakristo wa kimwili lilitokea wapi? Chanzo chake ni tafsiri potofu inayoshikiliwa na wengi ya kile ambacho Paulo aliandika katika sura ya tatu ya Wakorintho wa Kwanza. Aliandika hivi:

“Lakini ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina; je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?” (1Wakor. 3:1-3)

Swali: Je, Paulo alikuwa anazungumza juu ya kundi fulani la Wakristo ambao hawana tofauti na wasioamini kwa sababu ya kufuata asili au tabia zao za kimwili? Wengi wanasema ndiyo, japo ni kinyume kabisa cha mafundisho mengi ya Agano Jipya. Wanadai hivi: “Paulo si aliwaambia Wakristo hao kwamba ‘mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu’ (3:3) na kuonyesha kwamba walikuwa wanatenda kama watu ambao hawajaamini?”

Jibu litapatikana katika kutazama kila kitu ambacho Paulo alisema kuhusu Wakorintho. Tukifanya hivyo, tutagundua kwamba “Wakorintho wa kimwili” kweli hawakuwa na tofauti na watu wasiookoka, kwa sababu imani yao halisi ilionekana kwa matendo mengi ya nje yaliyoonyesha upendo wao kwa Kristo. Naam: na kwa kuwa walikuwa na asili mbili – kama ilivyo kwa Wakristo wote – walikabiliana na ile vita kati ya Roho na mwili. Wengi wao kwa kuwa hawakuwa wamekomaa kiroho walifikia mahali pa kukubaliana na kuenenda katika asili yao ya kale (yaani, kuenenda katika mwili), na kutoenenda katika upendo kati yao. Walikuwa wanashindana juu ya waalimu waliokuwa wanawapenda na kuonyesha hali ya kupuuza Meza ya Bwana. Wengine walikuwa wanashtakiana mahakamani. Walihitaji kukua katika tunda la upendo, na Paulo aliandika mengi sana kuwasaidia katika jambo hilo.

Sababu ya msingi ya tatizo lao ni wao kutokujua kile ambacho Mungu alitazamia kutoka kwao. Kwa kuwa walikuwa watoto katika Kristo ambao Paulo alikuwa amewalisha tu maziwa ya Neno la Mungu badala ya nyama au chakula kigumu (3:2), maarifa yao (au walichojua) yalikuwa madogo na yenye mipaka. Ndiyo sababu Paulo aliwaandikia na kushughulikia makosa yao mbalimbali. Baada ya kuwaambia kile ambacho Mungu alitazamia kutoka kwao, aliwatazamia wafikie kiwango kinachotakiwa.

Wakorintho Wa Kiroho, Waliokuwa “Kimwili”

Nini baadhi ya kazi za Wakristo Wakorintho zilizowatamblisha kwamba wana imani ya kweli? Ni nini kilichowatofautisha na wasiokuwa Wakristo? Yafuatayo ni mambo yaliyodhihirishwa na Maandiko.

Kwanza: Wakati Paulo alipohubiri Injili mara ya kwanza huko Korintho, alifanikiwa sana. Mungu Mwenyewe alimwambia kwamba walikuwepo wengi huko Korintho ambao wangeokoka (tazama Matendo 18:0), na Paulo alikaa huko mwaka mmoja na nusu. Wengi “walikuwa wakiamini na kubatizwa” (Matendo 18:8). Ubatizo ndilo lilikuwa tendo lao la utii la kwanza kwa Kristo.

Paulo, akiwaelezea baadhi ya Wakristo Wakorintho anaandika kwamba zamani walikuwa wazinzi, waabudu sanamu, waasherati, walawiti, wezi, wenye kutamani, walevi na wadanganyifu (ona 1Wakor. 6:9-10). Lakini kwa sasa walikuwa wamesafishwa na kutakaswa; walikuwa wamebadilishwa. Hilo peke yake linavunjilia mbali hoja ya kijinga kwamba Wakorintho walikuwa hawana tofauti na wasioamini.

Tena, Paulo aliwafundisha Wakristo Wakorintho kwamba “msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi – mtu wa namna hii msikubali hata kula naye” (1Wakor. 5:11). Bila shaka Wakristo Wakorintho wenyewe hawakuwa na hatia ya kufanya hayo, maana kama ndivyo, Paulo alikuwa anawaambia wasishirikiane wao kwa wao, wala wasile pamoja!

Barua ya Paulo ya kwanza kwa Wakorintho ilikuwa ni jibu la barua aliyokuwa amepokea kutoka kwao juu ya maswala fulani. Walikuwa wameuliza kuhusu kilichokuwa sawa na kisichokuwa sawa, wakionyesha shauku yao wenyewe ya kutaka kutenda yaliyo sawa. Je, ilikuwa ni kosa kwa watu wasio na ndoa kuoana? Vipi kuhusu wale ambao waliwahi kuwa na ndoa? Vipi kuhusu kula nyama zilizokuwa zimetolewa sadaka kwa sanamu? Wengi katika Wakristo Wakorintho, kwa sababu ya kumpenda Kristo, walikataa kula nyama za aina hiyo wasije wakamchukiza Bwana – onyesho kwamba walikuwa na imani hai.

Paulo akawaandikia hivi katika 1Wakor. 11:2 – “Basi nawasifu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale mapokeo vile vile kama nilivyowatolea.” Je, hao ni watu wasio na tofauti yoyote na wasioamini?

Wakristo Wakorintho walishiriki Meza ya Bwana mara kwa mara (japo sivyo kama ilivyotakiwa), wakitii agizo la Yesu (ona 1Wakor. 11:20-22). Pia walikusanyika mara nyingi ili kuabudu Kikristo (ona 1Wakor. Sura ya 12 na 14), kitu ambacho wasioamini hawakufanya katika siku zile.

Walikuwa na shauku sana ya kupata karama za kiroho (ona 1Wakor. 14:12).

Ukweli kwamba barua zote mbili za Paulo kwa Wakorintho zimejaa mashauri kuhusu utakatifu huonyesha kwamba Paulo aliamini kwamba watajali alichoandika. Aliwaagiza wamtenge mtu mnafiki (ona 1Wakor. 5:13) na kufanya changizo kwa ajili ya Wakristo maskini waliokuwa Yerusalemu (ona 1Wakor. 16:1-4), kitu ambacho walikuwa wamekwisha anza kukifanya, tena kwa shauku kubwa (ona 2Wakor. 8:10; 9:1-2). Kwa njia hiyo, walionyesha upendo wao kwa ndugu, kile kile kitu ambacho Yesu alisema kingekuwa alama ya wanafunzi Wake wa kweli (Yohana 13:35).

Barua ya pili ya Paulo inaonyesha kwamba wengi wao – kama si wote – walikuwa wameitikia vizuri maagizo ya barua yake ya kwanza (ona 2Wakor. 7:6-12). Baada ya barua ya kwanza na kabla ya barua ya pili, Tito alisafiri kwenda Korintho na akarudi na taarifa nzuri sana juu ya utii wao (ona 2Wakor. 7:13-16). Wale watoto wachanga katika Kristo walikuwa wanakua. Ndiyo – yalikuwepo bado matatizo kidogo huko Korintho, na Paulo alipanga kuwatembelea ili kutengeneza yaliyobaki.

Hitimisho ni hili: Wakati Paulo alipoandika kwamba Wakristo Wakorintho walikuwa wanaenenda “kwa tabia ya kibinadamu” hakumaanisha kwamba hawakuwa tofauti na wasioamini kwa kila hali. Walikuwa wanatenda kama wasioamini kwa njia moja, lakini kwa njia nyingine nyingi walikuwa wanatenda kama wanafunzi wanaompenda Kristo sana.

Vipi Kuhusu Kazi Zitakazoteketea?

Hoja nyingine ambayo mara nyingi inatumiwa kuunga mkono wazo la kundi maalum la Wakristo wa kimwili hujengwa juu ya maneno ya Paulo katika 1Wakor. 3:12-15. Inakwenda hivi: Je, Paulo hakuwahakikishia Wakorintho katika maandiko hayo kwamba wangeokolewa hata kama kazi zao zote zingeteketea wakati wa hukumu? Je, hiyo haionyeshi kwamba mtu anaweza akawa hana matunda kabisa na bado awe ameokoka?

Mantiki ya maandiko hayo inadhihirisha kosa la hoja hiyo. NI wazi kwamba Paulo alikuwa anaandika juu ya thawabu ambazo watumishi binafsi watapokea au kupoteza, kwa sababu ya ubora wa kazi zao. Akifananisha kanisa na “jengo la Mungu” (3:9), na akitaja kwamba yeye aliuweka msingi “ambao ni Yesu Kristo” (3:11), Paulo aliandika kwamba kila mtumishi “aangalie jinsi anavyojenga juu ya msingi” (3:10). Inawezekana kabisa kujenga kwa makosa. Kisha, Paulo, kwa njia ya mfano, anataja vifaa vya aina sita vya ujenzi ambavyo vingeweza kutumiwa: “dhahabu, fedha, mawe ya thamani, miti, majani [na] manyasi” (3:12). Vile vitatu ni vya thamani kubwa sana, na haviwezi kuteketea au kuungua, ila vile vya mwisho vitatu si vya thamani kubwa na ni rahisi sana kuungua na kuteketea.

Kulingana na Paulo, aina ya vifaa vinavyotumiwa na mtumishi binafsi kujenga jengo la Mungu haviwezi kuonekana wakati huu. Lakini siku moja vitakuwa dhahiri kabisa, kwa sababu “kazi ya kila mmoja … itafunuliwa kwa moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu” (3:13). Kisha anaendelea hivi:

Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto” (1Wakor. 3:14-15).

Yamekuwepo majadiliano mengi kuhusu ni kazi zipi zinazoweza kuwa “dhahabu, fedha na mawe ya thamani,” na ni zipi zinazoweza kuwa “miti, majani na manyasi”. Hata hivyo ni kweli kabisa kwamba watumishi “wanaojenga” jengo la Mungu kwa kutumia matofali ambayo ni Wakristo bandia na sementi ya injili ya uongo watapata maandiko hayo kuwa yanayofaa sana wakati Bwana atakapopima kazi yao. Watu wengi wasiokuwa watakatifu ambao wamo kanisani sasa hivi mwishoni watajikuta katika moto wa jehanamu, na yule mtumishi “aliyewaleta kwa Kristo” au aliyewahakikishia kwamba wameokoka kwa kutangaza neema ya uongo atatambua kwamba juhudi zake zote hazikuwa kitu katika kujenga “hekalu la kweli la Mungu” (3:16). Alichojenga kitaungua, naye “atapata hasara” (3:15), na hatapokea thawabu yoyote. Lakini, yeye mwenyewe, kama ni mwamini wa kweli, “ataokolewa; lakini ni kama kwa moto” (3:15).

Ni dhahiri kwamba kusudi la Paulo katika maandiko haya halikuwa kuwahakikishia wale wanaoitwa “Wakristo wa kimwili” kwamba wanaweza kuwa bila matunda na bado wawe na uhakika wa wokovu wao. Yeye alikuwa anaandika juu ya thawabu ambazo watumishi watapokea au kupoteza kulingana na hali ya kazi yao, itakayofunuliwa wakati wa hukumu.

Ndiyo – Wakristo wa kweli wakati mwingine hutenda mambo ya kimwili. Kila wanapokubaliana na mwili ni sawa kusema kwamba wanatenda kama “watu wa tabia ya mwilini”. Lakini, hakuna kundi maalum la “Wakristo wa kimwili” katika mwili wa Kristo, ambao wanakwenda mbinguni lakini wanakubaliana kabisa na tabia na asili zao za kimwili. Paulo anasema hivi katika Warumi, kuhusu jambo hilo:

Kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao> ndio wana wa Mungu (Warumi 8:13, 14 – Maneno mepesi ni kutilia mkazo).

Tena, kama anavyowaandikia Wakristo Wagalatia: “Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake” (Wagalatia 5:24).

Je, Ungefanya Nini Kama …

Kuna kisa – pengine si cha kweli – ambacho kimesimuliwa juu ya kanisa dogo katika kijiji kilichojificha sana huko Marekani ya Kati. Jumapili moja asubuhi wakati ibada inakaribia kuanza, milango ya kanisa ilifunguka na wanaume wawili wakaingia. Hawakuwa wasafi sana, tena walikuwa wamevalia mavazi ya kijeshi na wameshika bunduki. Mabegani walikuwa wamefunga mikanda yenye kujaa risasi.

Hofu ikawapata washirika. Wapiganaji Wakomunisti walikuwa na tabia ya kuwaua Wakristo katika eneo hili. Je, wakati wao ulikuwa umefika?

Mmoja akadai kuwe kimya kisha akasema: “Ninyi Wakristo sikuzote mnazungumza kuhusu kwenda kumwona Mwokozi wenu, yule mnayemwita Mwana wa Mungu. Basi leo mmebahatika kwa sababu muda si mrefu ujao mtakwenda kujua ikiwa Mungu wenu kweli yupo! Haya! Jipangeni mistari kwenye kuta za kanisa!”

Haraka haraka washirika wakaondoka kwenye viti na kwenda kujipanga ukutani pande zote.

Akasema, “Sasa, kabla ya kuwaua, tungependa kuhakikisha kwamba ni waamini tu ndiyo watakufa. Yeyote hapa ambaye haamini kweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu atoke upesi akipitia hapa kwetu. Harakisha!”

Wengi hawakusita. Kwa dakika moja, nusu ya washirika wakawa wametoka.

Mtu wa mwisho alipotoka, milango ikafungwa. Mmoja wa wale askari akatazama kupitia dirishani na kuwaona wale waliotoka wakikimbia mbio kutoka eneo la kanisani. Kisha, alipoweka chini bunduki yake, alisema huku akitabasamu: “Ndugu zetu! Mtusamehe tafadhali. Tulitaka kumwabudu Bwana nanyi asubuhi ya leo, lakini tulitaka kuabudu na Wakristo wa kweli tu. Sasa hebu tumwabudu Bwana pamoja!” Ikawa ibada ya kipekee sana asubuhi hiyo!

Kisa hiki husimuliwa ili kuwalazimisha watu wanaokiri Ukristo wafikiri kitu ambacho wangefanya kama wangekuwepo asubuhi hiyo. Lakini, kuamini hadithi hii kwamba ni ya kweli inabidi tupuuze ukweli kwamba Wakristo wawili wenye bunduki walijifanya, wakatoa vitisho na wakamkana Kristo, ili waweze kumwabudu Mungu katikati ya waamini wa kweli! Je, kwa walichofanya, hawakumkana Kristo sawa na wale waliokimbia kutoka kanisani?

Basi, ningependa kuigeuza hadithi hiyo kidogo tu, hasa kwenye kumalizia. Ingawa kipengele changu pia sijawahi kukishuhudia, ndivyo matukio mengi yanayofanana na hicho kisa yalivyomalizika, mara nyingi sana.

Baada ya dakika moja, nusu ya washirika wakawa wametoka nje.

Mtu wa mwisho alipotoka, milango ikafungwa. Askari mmoja akatazama kwenye dirisha na kuona wale waliotoka wakikimbia kutoka eneo la kanisa. Kisha akiwa amekunja uso kikatili, aliwaelekezea wale wanafunzi wachache waliobaki bunduki yake na kusema: “Jitayarisheni kukutana na Mungu wenu.” Baada ya kusema hivyo, alianza kupiga risasi. Ikawa ibada ya ajabu sana kwao, mbele za Bwana wao!