Mchana anafanya kazi katika ofisi mojawapo huko mjini. Ni mfanyakazi mwenye bidii sana na amepanda cheo mara kwa mara. Kila mmoja anampenda. Ni mwaminifu, anapendeza kuwa naye. Ni baba mzuri mwenye watoto watatu, mtu ambaye usingedhani ana siri ya kutisha maishani mwake.
Usiku, kazi yake ni kuvizia nyumba za jirani, akijificha nyuma ya miti na kandoni mwa uzio. Anatafuta nyumba za wastani ambazo wakaaji wake ni wana-ndoa vijana, tena ambazo si za ghorofa, maana, vyumba vya kulala vitakuwa chini.
Ni Ijumaa nyingine, na usiku huu amerudi maeneo aliyozoea. Moyo wake unadunda kwa kasi anaposogelea nyumba fulani ambayo juma lililopita “alifanikiwa”. Watu waliofunga ndoa hivi karibuni walinunua jumba hilo pamoja na shamba lake, naye anatabasamu anapoona taa ikiwaka kwenye dirisha upande wa nyuma ya nyumba. Anasogea karibu akitumaini kusikia muziki laini, ambao unamwambia kwamba dirisha liko wazi usiku huo wa joto kali. Naam – ni muziki wa ala. Leo tena “atafanikiwa”. Anasogea taratibu mpaka anakaribia nyumba ile na kupiga hatua mpaka dirishani. Akili yake imejaa picha za mambo ambayo amekwisha kuyaona.
Mtu wa aina hiyo anajulikana kama “mwenye kupenda kuchungulia watu”. Anachofanya ni kosa. Wengi wetu tutakubali kwamba watu aina hiyo wanapaswa kuwa gerezani. Yeye amepotoka ndani, na kwa kweli si mtu tunayetazamia kumwona mbinguni. Hakuna Mkristo anayeweza kuwa na tabia kama hiyo. Hata Biblia inakubali, kama inavyosema:
Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, … aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi (Waefeso 5:5, 6 – Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).
Je, “wachunguliaji” ni wasafi au wachafu? Ni waadilifu au si waadilifu? Jibu ni dhahiri kabisa, tena, kulingana na Maandiko, hawana urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Watu waliozaliwa mara ya pili kweli kweli si wachunguliaji.
Picha Ya Pili:
Mchana anafanya kazi katika ofisi mojawapo huko mjini. Ni mfanyakazi mwenye bidii sana na amepanda cheo mara kwa mara. Kila mmoja anampenda. Ni mwaminifu, anapendeza kuwa naye na ni baba mzuri mwenye watoto watatu. Ni mshirika wa kanisa lenye kuamini Injili, naye anahudhuria kila Jumapili asubuhi na hata anafundisha darasa la Shule ya Jumapili mara mbili kwa mwezi. Mwaka jana alichaguliwa kuwa shemasi, naye yuko karibu sana na mchungaji na ni mtu anayeheshimika sana na washirika. Kwenye mlingoti wa redio wa gari lake ameweka kitambaa cheupe kuonyesha kwamba anapinga picha chafu zenye kuonyesha matendo ya kujamiiana. Nafsini mwake mambo ni mazuri.
Baada ya kazi ngumu za juma zima, anapenda kujipumzisha Ijumaa jioni. Kwa hiyo anapokwenda nyumbani, anapitia kwenye maktaba ya kuazima mikanda ya video. Kuna toleo jipya ambalo amesikia juu yake, naye anatumaini atapata nakala moja ya kukodisha akatazame. Anaikuta. Ni sinema nzuri, yenye wachezaji anaowapenda. Imewekwa alama kuonyesha kwamba si nzuri, naye anajua vizuri sana kwamba itakuwa imejaa matendo ya kujamiiana na matusi mengi.
Anapotazama ile picha ya juu, dhamiri yake inasema naye kwa muda mfupi. Lakini, amekwisha andaa utetezi wake: Atakaposema na waamini wenzake kanisani juu ya sinema hiyo, atalalamika sana jinsi ilivyojaa matendo ya kujamiiana pamoja na matusi, kama ifuatavyo:
“Loo! Inatia aibu sana kuona jinsi watengeneza sinema wanavyofikiri kwamba huo uchafu wote ni lazima uwepo, sivyo?”
Jibu: “Ndiyo! Kabisa! Ni aibu kweli kweli!”
Mara tu watoto wanapokwenda kulala, anaweka mkanda wake kwenye mashine na kuketi kwenye kiti na mkewe waitazame. Mama huyo hawezi kudhania jinsi mwenzake anavyotazamia kwa hamu kubwa kuona miili ya wale wanawake wacheza sinema watakaotokea humo, wakiwa hawajavaa nguo nyingi. Aliwasikia wenzake huko ofisini ambao hawajaokoka wakieleza jinsi ambavyo sinema hiyo inasisimua. Ni Ijumaa nyingine.
Kuwalinganisha Hao Wawili
Nini tofauti kati ya mtu wa kwanza na wa pili? Yule “mchunguliaji” alitazama watu hai wakikutana kimwili katika vyumba vya kulala. Huyu mwingine alitazama sinema ya watu wakikutana kimwili. Wa kwanza alikuwa anaona kidogo tu kwa kupitia dirisha lililofunguliwa nusu. Huyu wa pili aliona kila kitu waziwazi. “Mchunguliaji” aliwatazama watu wawili ambao walikuwa wamejitoa kila mmoja kwa mwingine maisha yao yote, wakifurahia upendo walio nao. Wangeshtuka sana kujua kwamba kuna mtu wa tatu katika jambo lao hilo. Huyu wa pili aliwatazama watu wawili wasiokuwa na ndoa ambao wamelipwa fedha nyingi sana ili wavue nguo na kukutana kimwili mbele ya watu mamilioni, tendo linalowafanya wao kuwa makahaba wanaolipwa fedha nyingi sana duniani. Tena, sehemu ya fedha aliyolipa kukodisha mkanda huo iliwaendea wao. Kwa maneno mengine ni hivi: Aliwalipa makahaba wapigwe picha wakikutana kimwili ili yeye astarehe.
Yule “mchunguliaji” alikuwa ni mwenye kwenda jehanamu. Huyu wa pili ni mfuasi wa Kristo, anayekwenda mbinguni.
Kweli ni hivyo? Si tumesoma sasa hivi tu kwamba hakuna mtu mwasherati au mchafu atakayerithi ufalme wa Mungu? Je, katika hao wawili, ni yupi aliye mchafu zaidi?
Kuna mambo mawili ya kutazama juu ya mtu wa pili, anayesemekana ni mfuasi wa Kristo: Kwa kukodisha mkanda wa picha chafu, alichangia biashara ya picha hizo, akipiga kura yake kwamba anaunga mkono sinema za aina hiyo zizidi kutengenezwa. Fedha yake itawapa watu wengine nafasi ya kutazama uchafu zaidi kama huo. Basi, amesaidia kuendeleza dhambi maishani mwa wengine. Yule “mchunguliaji” hakufanya hicho.
Pili ni kwamba, ile sinema ambayo yule “Mkristo” alilipia kuitazama ilikuwa imejaa matusi. Jina la Mungu lilitumiwa mara kwa mara kwa mzaha. Je, haishangazi kwamba mtu ambaye kila Jumapili anaomba kwamba jina la Mungu litakaswe na kutukuzwa atakuwa tayari kutoa fedha zake ili kustareheshwa na watu wanaolitukana na kulikufuru jina la Mungu tena na tena?
Sababu Wanafiki Kujifanya Watakat ifu
Kama yule mtu wa pili ni mchafu kuliko yule mchunguliaji asiyeokoka, mbona basi wengi wanaokiri kwamba ni Wakristo wanatenda kama yeye, wakizidisha ashiki za mwili kila wakati kwa kutazama uchafu wa picha kwamba ni njia ya kustarehe? Jibu ni kwamba, hawajaokoka kweli kweli.
Ukikubaliana nami kwamba yule mtu wa pili ni mchafu sawa tu na yule wa kwanza au hata zaidi, na unaamini kwamba watu aina hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu (kama inavyosema Biblia), basi lazima ukubaliane pia na uamuzi wangu. Lakini, mbona watu wengi wamedanganyika katika jambo hili?
Ni salama kudhani kwamba yule Mkristo wa kawaida anayetazama mara kwa mara sinema hizo mbaya hawezi kuvizia nyumba za jirani ili achungulie watu madirishani mwao. Ukweli ni kwamba yeye anamhesabu yule “mchunguliaji” wetu kuwa ni mtu mwenye matatizo. Kwa nini? Je, ni kwa sababu anampenda Mungu? Au ni kwa sababu ya utakatifu wake au usafi wa ndani? Hapana – hayo hayawezi kuwa ndiyo sababu – maana ingekuwa hivyo, angechukizwa pia na wazo la yeye mwenyewe kutazama sinema ya matendo ya kukutana kimwili kati ya watu ambao hawana ndoa.
Jinsi asivyokuwa na msimamo huonyesha kile kinachomfanya asivizie nyumba za watu usiku: ubinafsi tu. Akikamatwa kwenye kuchungulia anaweza kupatikana na madhara makubwa. Sifa yake itaharibika. Ataaibishwa mbele ya kanisa lake. Hata inawezekana akatupwa gerezani.
Lakini, amegundua njia ya kufanya hicho hicho kila mara, bila kujitia hatarini kama yule mchunguliaji. “Utakatifu” wake haukujengwa kwenye viwango vya Mungu bali vya dunia. Katika utamaduni wa kisasa ni kitu kinachokubalika kutazama mikanda ya video yenye picha za ovyo, kwa hiyo hana sababu ya kuwa na wasiwasi. Sifa yake haitaharibika. Mke wake hatamwacha, wala hatapoteza kazi yake. Hawezi kufungwa gerezani. Lakini, kama angekuwa mfuasi wa kweli wa Kristo, angetilia maanani sana maonyo mazito ya Yesu kuhusu matokeo mabaya ya tamaa. Alisema hivi:
“Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini’; lakini mimi nawaambia, ‘Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum’.” (Mathayo 5:27-30. Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).
Ni hivi: Yule mtu wa pili ana kitu cha kumpa wasiwasi ambacho ni kibaya kuliko kupoteza sifa yake au kazi yake – atambue asitambue – nacho ni kawaida yake ya kuamsha ashiki au tamaa itampeleka jehanamu milele. Lakini anapuuza au anajaribu kujitetea dhidi ya kile ambacho Kristo alifundisha waziwazi, akitegemea neema yenye kusamehe bila kumbadilisha, neema isiyokuwepo kabisa!
Wakati Uungwana Unapokuwa Uovu
Bado kuna la kusema juu ya mtu yule wa pili. Kawaida yake ya kutenda uchafu pamoja na maisha yake ya nje yenye kuonekana kuwa ya haki humfanya kuwa mnafiki. Mnafiki si mtu aliyechanganya mema na maovu – mnafiki ni mtu mwovu kabisa. Sababu ya kufunga kitambaa cheupe kwenye mlingoti wa redio wa gari lake haikuwa kuonyesha kwamba anapinga uchafu. Hili liko wazi kwa sababu yeye anatumia fedha zake mara kwa mara kutazama sinema chafu na kwa njia hiyo anachangia kuendelea kwa biashara hiyo, na kuunga mkono kutumiwa vibaya kwa wanawake na kuharibiwa kwa maadili ya watoto. Sababu ya yeye kufunga kitambaa cheupe kwenye mlingoti wa redio wa gari lake ni ili aonekane mwenye haki. Maisha yake mbele za watu ni kujifanya. Kinachomsukuma maishani si kumtii Mungu au huruma kwa ajili ya wale wanaoharibiwa na sinema za uchafu – msukumo wake ni ubinafsi – anataka wengine wamfikirie kwa kiwango cha juu. “Matendo mema” yote anayofanya yametiwa doa kwa ukweli huo. Yeye ni mnafiki, anayepinga uchafu mkubwa huku akiunga mkono uchafu mdogo.
Tabia yetu hufunuliwa kwa yale tunayofanya juma zima, si yale tunayofanya Jumapili asubuhi tu. Hufunuliwa zaidi kwa vitu “vidogo” na kwa yale tufanyayo tunapokuwa peke yetu. Chukua mfano wa dhambi ya kuiba, iliyotajwa katika zile Amri Kumi kwamba ni dhambi ambayo, mtu akiitenda, hakika atakwenda jehanamu (ona 1Wakor. 6:10).
Ni Wakristo wachache sana wanaothubutu kuvamia benki na kuiba kwa kutumia silaha. Lakini wengi wanadanganya mara nyingi tu kwa habari ya kodi zao, kwa kufanya hivyo wakiwaibia wananchi wote. Wengine wanawalipa wafanyakazi wao “chini ya meza” (yaani, bila ya mkataba wa kazi na marupu-rupu yote yanayotakiwa) au wanakubali kulipwa hivyo kama wafanyakazi, ili wasilipe kodi. Hapo tena ni kuibia wananchi wote. Wengi huiba vitu vidogo vidogo kutoka makazini mwao. Wakirudishiwa fedha zaidi dukani, wananyamaza nazo. Hao ni wezi. Basi, sababu za kutokuiba benki si kwamba hawajipendi au wanampenda Mungu maana wizi wao mdogo mdogo unaonyesha vinginevyo. Sababu hawaibi benki ni kwa kuwa wanaogopa watakamatwa. “Wema” wanao-onyesha wanaufanya kama ishara ya ubinafsi wao. Kama wangeweza kuiba benki bila kuhatarisha usalama wao na sifa zao na uhuru wao kama inavyokuwa kwa habari ya kodi, wangefanya hivyo. Lakini, ubinafsi ule ule unaowasukuma kuiba vitu vidogo vidogo ambavyo hakuna mtu atakayejua juu yake pia huwasukuma kuwa “wazuri” katika vitu vikubwa. Sifa yetu ya kweli hufunuliwa wakati tunapojaribiwa kufanya makosa kwa kuwa hakuna tishio la kuathirika waziwazi.
Kamera Ya Mungu Iliyofichika
Hebu fikiri kwamba wewe ni bosi mwenye mfanyakazi unayempenda sana. Anafika mapema kila siku, anachelewa kuondoka, anafanya kazi kwa bidii na anapendwa sana na wafanyakazi wengine.
Lakini siku moja unaamua kuweka kamera zilizofichika mahali pale unapofanyia kazi, na unasikitishwa kuona yule mfanyakazi wako umpendaye akiiba kitu cha shirika na kukificha nguoni mwake. Kisha anatoka nje, anatazama huku na kule na kukitia katika gari lake. Je, mawazo yako yatakuwa: “Aa! Sawa tu. Hata hivyo, yeye ni mfanyakazi mzuri sana. Ana ta tizo dogo tu. Ngoja nilipuuze” ?
Hapana. Ghafula, mtazamo wako kuhusu huyo mfanyakazi wako bora utabadilika. Tangu wakati huo, yale mazuri yake yote yanaanza kuonekana kwa mwanga mwingine. Sasa unaanza kujiuliza kinachomfanya afike mapema na kuchelewa kuondoka. Ni ili aweze kuibia shirika wakati watu wengi hawapo? Ni ili wewe umwone kuwa ni mzuri, uache kuwa na mashaka naye wakati vitu fulani vinapotoweka au kukosekana? Sasa kwa kuwa unajua tabia yake ya kweli, matendo yake mema yote yanaonekana kuwa ni uovu. Basi – hivyo ndivyo Mungu anavyomwona kila mnafiki. Hivyo ndivyo Mungu anavyomwona yule mtu wa pili katika visa vyetu. Kutokuwa na msimamo kwake hudhihirisha tabia yake halisi. Yeye si Mkristo mwenye tatizo dogo. Yeye ni mnafiki ambaye ni mwovu kabisa. Matendo yake mema hayaondoi tatizo lake dogo – badala yake, ni ufunuo wa kutisha kuhusu jinsi alivyo mwovu na mbinafsi.
Mtu ambaye amezaliwa kweli mara ya pili anaye Roho wa Mungu ndani yake naye huendelea kutakaswa kadiri anavyoshirikiana na Roho. Hataishi maisha ya aina mbili. Ndiyo – atajikwaa na wakati mwingine anaweza kutenda dhambi. Lakini hivyo sivyo alivyo kila wakati. Maisha yake kimsingi ni ya kumtii Mungu anayempenda kila wakati. Kama alivyoandika mtume Yohana: “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu” (1Yohana 3:9). Kuzaliwa mara ya pili ni mwanzo wa maisha mapya ya utakatifu. Na, kadiri yule Mkristo wa kweli anavyojifunza zaidi mapenzi ya Mungu, ndivyo anavyozidi kubadilishwa na kufanana zaidi kama Yesu (ona Warumi 12:2).
Kinyume chake – yule ambaye ameongoka tu kwa hali ya bandia atafanya mambo mengi nyumbani na nje ambayo hawezi kufanya akiwa kanisani au akiwa na Wakristo wengine. Kanuni zake za kiadili hazikujengwa juu ya anachosema Mungu bali juu ya kile dunia inachosema, na kanuni za kidunia ni zenye kushuka kila mara. Hii ndiyo sababu yule Mkristo bandia anafanya kwa kawaida vitu ambavyo vingewashangaza hata wasiokuwa Wakristo miaka kadhaa iliyopita. Mfano: Siku hizi, wengi katika watu wanaojiita Wakristo hawashtushwi na maneno machafu ya kufuru, laana na matusi, na hata maonyesho ya ubatili na fujo katika mikanda ya video au sinema – vitu ambavyo vingewashtua na kuwashangaza sana wasiokuwa Wakristo si si nyingi zilizopita. Hata baadhi ya viongozi maarufu Wakristo wanaotambulikana sana wanashauri sinema kama hizo zitazamwe, mradi kuna kipengele kidgo “cha ukombozi” kimaadili kama vile ujasiri, staha au kujitoa!
Wakristo wa kweli wanatiwa moyo wawe watakatifu kwa sababu wamezaliwa upya na Roho Mtakatifu, na kwa sababu wanampenda Mungu. Kwa upande wa pili, kinachowahamasisha Wakristo bandia kuwa waadilifu kama walivyo ni kujitakia mambo yao – ubinafsi tu – kile kile kinachowafanya wasiokuwa Wakristo kuwa waadilifu!
Makusudi Yasiyokuwa Matakatifu
Kwa nini wasiokuwa Wakristo hujizuia wasifanye dhambi fulani? Ni kwa sababu wanaogopa matokeo mabaya. Kanuni hii imethibitishwa tena na tena katika historia ya wanadamu nyakati ambapo vizuizi vile vya kiadili vya kawaida vinapokuwa vimeondolewa, kama vile sheria za serikali au maoni ya wengi. Wakati ukatili unapokubalika, ukatili ndiyo unaotawala. Mafungu ya mafuvu ya vichwa vya binadamu huko Kambodia, na matanuru yanayobomoka sasa ya kuchomea wanadamu katika makambi ya mateso ya KiNazi ni ushuhuda tosha kuhusu asili ya kweli ya mwanadamu ambaye hajazaliwa upya. Ni kitu gani kinachotokea wakati mauaji yanaporuhusiwa kisheria? Au wakati sheria ya Serikali au maoni ya wengi yanaposema ni sawa kuua Wayahudi au kurarua-rarua mimba changa zikiwa bado tumboni? Hakuna anayehitaji kufikiri jibu lake.
Ni watu wangapi wanaojiita Wakristo ambao wanahamasishwa kuwa watakatifu kwa hali ya chini na kuonyesha uadilifu japo kidogo, si kwa sababu wanampenda Mungu au wamezaliwa mara ya pili kwa njia ya Roho Mtakatifu, bali kwa sababu ya maoni yanayobadilika siku zote ya wengi, au sheria za nchi zinazorekebishwa kila leo, au kuogopa rika la wenzao wanaoshiriki pamoja kanisani? Mungu tu ndiye anayejua kwa uhakika jibu la maswali hayo. Lakini, kwa kujipima kweli kweli na kumaanisha, kila mmoja wetu anaweza kutambua ni kitu gani kinachomhamasisha kweli. Kama kila anayejiita Mkristo angefanya hivyo, wengi wangeshtushwa kwa kugundua kwamba wema wao wote kwa kweli ni uovu, unaohamasishwa na ubinafsi tu.
Je, yawezekana kweli kufanya mambo mazuri lakini yatokane na ubinafsi tu? Kabisa! Kama ambavyo tumekwisha ona, matendo “mema” mengi yanayofanywa na wasiokuwa Wakristo hutokana na ubinafsi. Fikiria maneno ya Paulo kuhusu jambo hili, anaposema hivi:
Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu (1Wakor. 13:3).
Yesu, Mfichua Wanafiki
Wengi wanaojiita Wakristo siku hizi wako kinyume kabisa na sinema chafu. Lakini, kusema tu kwamba si kitu kizuri hicho si kipimo cha wokovu wa kweli wa Kikristo. Kama mtu anahamasishwa na upendo kwa Mungu na kwa mwanadamu mwenzake katika kupinga kwake maovu hayo, basi matendo yake, mawazo na maneno vitalingana katika hilo. Atatenda maishani mwake mambo yenye kupinga dhambi hizo na zile nyingine zinazohusiana nazo. Tena, kama yule mtu wa pili katika visa vyetu angekuwa anapingana kweli na sinema chafu kwa sababu ya kuwajali waathirika wake au kwa sababu ya kupenda sheria ya Mungu, asingekuwa mtazamaji wa mikanda hiyo mara kwa mara. Mtazamo wake kuhusu uchafu wa aina zote ungelingana.
Hii kanuni ni kweli kwa habari ya dhambi zingine pia, licha ya hizo za uchafu kimwili. Kwa mfano: Ni wangapi katika wale wanaojiita Wakristo wenye kupinga kwa bidii biashara ya tumbaku, pombe na utoaji mimba, na hapo hapo wanaunga mkono na kufaidika na biashara hizo kwa kuwa wanachama wa mashirika ya uwekezaji ambayo fedha zao za akiba ya uzeeni zinawekwa?
Yesu alifunua unafiki wa aina hiyo uliokuwa miongoni mwa watu wa dini katika siku Zake, akionyesha kanuni isiyopitwa na wakati inayofanya kazi kwa kila anayejidhania anakwenda mbinguni. Hebu tuangalie tena maneno Yake yanayopatikana katika mahubiri kuhusu wokovu, yajulikanayo sana kama Mahubiri ya Mlimani. Hebu ona kama utaweza kupata maana iliyomo katika mafundisho Yake kwa wanaojiita Wakristo wa siku hizi ambao wanapinga sana sinema mbaya, lakini wanajihusisha katika uchafu wa aina zingine wa kukutana kimwili.
“Mmesikia kwamba imenenwa, ‘Usizini’; lakini mimi nawaambia, ‘Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum’.” (Mathayo 5:27-30).
Kwanza – Ona kwamba Yesu anawaonya watu fulani kuhusu jehanamu. Ukitazama mantiki, ni watu ambao hawafanyi uzinzi kimwili. Lakini, wanafanya uzinzi kimawazo, na Yesu anasema wasipotubu, wanakwenda jehanamu.
Andiko Na Moyo wa Sheria
Je, Yesu alikuwa anaongeza masharti mengine tena kwenye Amri ya Saba? Hapana! Alikuwa anaziba pengo lililokuwepo katika mawazo ya wanadamu na kudhihirisha maana halisi ya Mungu tangu alipotoa zile Amri Kumi. Ndani ya hiyo amri iliyokataza uzinzi kulikuwa na kizuizi cha tamaa pia. Ni hivi: Kama kukutana na mke wa jirani yako kimwili ni dhambi, basi hata kumvua nguo kwa mawazo ni dhambi pia. Mtu yeyote aliye wa haki na mwenye kufikiri angekiri kuwa ni hivyo. Lakini, wasikilizaji wa Kristo walikuwa kama wasikilizaji wengi wa siku hizi tu – wanatunza andiko la Sheria na kupuuza moyo wake. Kwa sauti wanapinga zile dhambi ambazo wao hawana hatia nazo, lakini wanatenda dhambi hizo hizo kwa njia nyingine. Mapenzi ya Mungu kwa habari ya usafi katika mahusiano yetu kimwili ni zaidi ya kujiepusha tu na uzinzi, uasherati na ulawiti. Yeye anatazamia kwamba tutakuwa wasafi mpaka katika mawazo yetu, kama ambavyo Yesu aliweka wazi sana, pamoja na midomo yetu. Kwa mfano: Paulo aliandika hivi:
Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe; wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru (Waefeso 5:3-4).
Tafsiri zingine za Biblia zinafafanua zaidi hizo dhambi za aibu, maneno ya upuzi na ubishi kuwa ni “mazungumzo machafu, maneno ya kipumbavu na vichekesho vya ovyo.” Mazungumzo machafu na vichekesho vya ovyo ni maneno ambayo yanaingiza mawazo ya uchafu wa mahusiano ya kimwili kwa njia ya kuchekesha au nzuri, na “maneno ya kipumbavu” yanaweza kuelezwa kuwa ni mazungumzo yaliyojaa habari za mahusiano kimwili kutoka kwa watu wanaoitwa na Biblia, wapumbavu. Hoja ya Paulo ni kwamba hakuna mfuasi wa Kristo anayetakiwa kuhusika katika uchafu wa mahusiano kimwili, pamoja na mazungumzo yasiyofaa. Je, unafikiri Paulo angewaambia nini Wakristo wanaojifurahisha siku hizi kwa kutazama sinema za televisheni zenye mambo ya kujamiiana? Je, angesemaje juu ya sinema nyingi ambazo zinatengenezwa leo na kuwekwa alama kwamba zinafaa kuangaliwa na wote?
Mafundisho Ya Kisasa Ya Uongo
Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya (wanaoitwa) waalimu wa Biblia wanatumia andiko la Waefeso kupinga mafundisho wanayoita “yasiyokuwa na usahihi” na “yenye kuleta hatia” kama haya ninayotoa mimi. Hoja yao iko hivi: “Bila shaka inawezekana kwa Wakristo wa kweli kutenda dhambi za uchafu wa kujamiiana. Vinginevyo, Paulo asingeshughulikia jambo hilo.”
Sisemi kwamba haiwezekani kwa Mkristo kuzini au kufanya uasherati. Inawezekana kwa sababu Wakristo ni watu wenye hiari ya kuamua. Mkristo wa kweli anaweza kutumbukia katika dhambi hizo. Lakini, kusudi la Paulo kuandika yaliyotajwa hapo nyuma si kuwahakikishia waliokuwa wanadumu katika dhambi hizo kwamba wameokoka kweli licha ya maisha yao. Hapana! Yeye aliandika kuwaonya Wakristo wakae mbali kabisa na dhambi hizo au hata kivuli chake, maana hizo zinaonyesha watu wanaokwenda jehanamu. Ndivyo anavyoendelea kusema katika mistari miwili inayofuata.
Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi (Waefeso 5:5-6).
Ndiyo, Mkristo anaweza kuingia katika jaribu la kufanya uchafu. Lakini wale wafanyao hivyo mara kwa mara wanajionyesha kuwa wachafu, na hivyo kujidhihirisha kwamba ni Wakristo bandia. Kwa sababu ya hali ya kutawala ya dhambi, hasa kuhusiana na tamaa za mwili, mfuasi wa Kristo mwenye hekima ataepuka na kupingana na wazo lolote, neno au hata tendo lenye kuhusiana na uchafu wa dhambi za kujamiiana. Pengine Mkristo mchanga sana hatajua viwango vya Mungu kuhusu usafi wa mahusiano kimwili, lakini atakaposoma Waefeso 5:3-5 hawezi tena kujitetea kwamba hajui chochote. Hiyo ndiyo sababu Paulo aliandika alivyoandika.
Maswala Mengine Yenye Utata
Katika kuzidisha utata na kupuuza maonyo dhahiri ya Maandiko, watu wengine huuliza hivi: “Matendo ya dhambi yanapimwaje? Kama nilizini mara moja tu mwaka huu na mara moja miaka mitatu iliyopita, je, mimi ni mzinzi ambaye ni Mkristo bandia? Au nilijikwaa tu mara mbili?”
Swali la kwanza la kuuliza ni hili: “Je, baada ya kutenda dhambi ulitubu na kumwambia Mungu akusamehe?” Kuna tofauti kubwa kati ya mtu anayefanya hivyo na asiyefanya hivyo. Kama Mkristo wa kweli alishindwa na jaribu na akazini, angejisikia hatia kubwa sana na kulia mbele za Mungu kuomba msamaha. Akifanya hivyo, Mungu atamsamehe.
Je, kabla ya kumwomba Mungu msamaha wokovu wake ulikuwa hatarini? Vipi kama asingeomba msamaha na akarudia tendo lake la dhambi? Je, afanye uzinzi mara ngapi ndipo ahesabiwe kuwa “atendaye uzinzi”? Majibu ya maswali haya yamejadiliwa kwa kina na kwa jazba sana. Sijifanyi kuwa na jibu sahihi. Lakini, kwa maelezo ya Maandiko, mtu anahitaji kuzini mara moja tu naye atakuwa mzinzi, anayestahili kufa. Hebu endelea kusoma yafuatayo: “Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa” (Walawi 20:10 – Maneno mepesi ni kwa ajili ya kutilia mkazo).
Mtu yeyote anayetaka kujua ni mara ngapi anaweza kuzini bila kutubu na bado aende mbinguni anastahili kuchunguza wokovu wake. Wale ambao wamezaliwa upya kweli kweli wanatamani kuwa watakatifu – mwili, nafsi na roho. Wao wanajitahidi kuwa wasafi kabisa katika wazo, neno na hata tendo.
Vile vile kuna wengine wanaopinga, katika juhudi zao za kufanya maonyo ya wazi kabisa ya Maandiko kuwa batili, kwa kusema hivi: “Mimi ningetaka kuwa huru kutokana na uchafu wa matendo ya kujamiiana, lakini nashindwa. Ninampenda Bwana, na kweli ningependa kuwa huru lakini imeshindikana.” Wanatazamia kwamba kinachoamua si kile wanachofanya bali kile wanachosema wanatamani.
Kwa maneno mengine, wanachosema ni kwamba kushikwa kwao na dhambi kuna nguvu zaidi kuliko Mungu, na kwamba wokovu Wake huleta msamaha ila si mabadiliko. Agano Jipya mara tena na tena linathibitisha kwamba wamwaminio Kristo wamewekwa huru kutokana na nguvu za dhambi (ona Warumi 6:6, 7, 17-18, 22). Maandiko pia yanashuhudia kwamba kuna ukombozi kamili kutoka dhambi fulani fulani mbaya sana, na kwamba ipo tofauti ya mwenendo inayowapata waamini wa kweli (ona 1Wakor. 6:11; 2Wakor. 5:17; Tito 2:11-14; 1Yohana 3:7-10).
Zaidi ya hayo, Mungu ametuahidi sisi kwamba hatatuacha tujaribiwe kupita uwezo wetu wa kustahimili, na kila wakati atatupa njia ya kutokea (ona 1Wakor. 10:13). Kutokana na kweli hiyo iliyo wazi na iliyojaa mema, kujitetea kwa mtu kwamba angependa kuacha dhambi lakini hawezi kunakosa nguvu. Mara nyingi nimegundua kwamba wale wanaosema wanataka uhuru kutokana na dhambi za uchafu wa mwili au zinazofanana na hizo hawako tayari kuondoa maishani mwao kile kinachowafanya wajikwae mara kwa mara – kama ni kutupilia mbali televisheni yao, au kufutilia mbali kupokea magazeti fulani, au kuepuka sehemu fulani za kufanyia shughuli, au kuvunja mahusiano yasiyokuwa sawa, au kujiondoa kwenye mtandao wa internet. Paulo aliandika hivi: “Wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake” (Warumi 13:14). Na Yesu alisema kwamba tukate na kutupa chochote kinachotufanya tukose. Wanaokataa kutii agizo hilo wazi kabisa la Yesu wanaonyesha kwamba Yeye si Bwana kwao hata kidogo. Hawataki kumtii hata kidogo.
Dhambi hupoteza nguvu zake tunapotubu kwa sababu hapo ndipo Mungu hutusamehe na kutukomboa. Lakini, kutubu maana yake kugeuka na kuacha dhambi zote zinazojulikana. Ni hali ya moyo na tendo la hiari yetu. Watu wanaotubu kweli kweli huonyesha toba yao kwa matendo yao (ona Luka 3:8; Matendo 26:20).
Kama unaamini kwamba wewe ni mtu uliyezaliwa mara ya pili ambaye huwezi kuacha kutenda uchafu au dhambi nyingine yoyote, pengine swali rahisi tu litakusaidia kugundua kujidanganya kwako. Je, ungeacha kutenda dhambi kama mtu angekupa dola za Kimarekani milioni kumi ili uache? Kama ungeweza, ni kwamba inawezekana; na kama inawezekana, unaweza; na kama unaweza, unapaswa kuweza! Shida si kwamba huwezi kuacha – ni kwamba hutaacha. Kwa nini uweze kufanya kitu kwa sababu ya fedha, na ushindwe kufanya kwa kumpenda Kristo?
Kwa kweli, hakuna njia ya kuepukana na majaribu yote, na hakuna Mkristo anayetakiwa kujidhania kuwa si wa kawaida kwa kuwa anajaribiwa, au anashindana na dhambi au anajisikia shauku nzuri tu ya kutaka mapenzi ya kimwili. Msemo huu utafafanua vizuri zaidi: “Huwezi kuwazuia ndege kuruka juu ya kichwa chako, lakini waweza kuwazuia kujenga kiota katika nywele zako.” Tukiona tumekubali kufanya kitu tunachojua ni makosa, hapo tuwe na wasiwasi.
Kila Mkristo anapaswa kujitahidi ili kufikia ukamilifu katika usafi wa mahusiano ya kimwili, katika mwili, mdomo na akili zake. Uzinzi, uasherati, ulawiti, kutazama aina yoyote ya picha au sinema mbaya (hata kama ni matangazo tu au maonyesho mafupi ya “mambo ya kitandani” katika sinema zinazosemekana ni “nzuri”), vichekesho “vichafu”, kuwaza mambo ya mahusiano kimwili, na kusoma au kusikiliza chochote kinacho-onyesha mahusiano ya kimwili yasiyofaa kwa kusudi la starehe, yote ni makosa mbele za Mungu. Tukidai kwamba tunajikwaa kila mara pasipo kuondoa hicho kikwazo kama Yesu alivyoagiza, tunajidanganya wenyewe.